KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, July 28, 2011

Mariam, nyota mpya ya taarab Five Stars
KIKUNDI cha taarab cha Five Stars cha mjini Dar es Salaam, hivi sasa kinasukwa upya baada ya kuondokewa na wasanii wake 13 katika ajali ya gari, iliyotolewa miezi michache iliyopita mkoani Morogoro.
Kwa sasa, uongozi wa kundi hilo upo kwenye hatua za mwisho za kuliunda upya kundi hilo, ambalo uzinduzi wake umepangwa kufanyika kesho kwenye hoteli ya Travertine, Magomeni, Dar es Salaam.
Katika kulisuka upya kundi hilo, tayari wameshapatikana waimbaji na wapiga ala kutoka vikundi mblaimbali, ambao wapo kwenye mazoezi makali kwa ajili ya kujiandaa kwa uzinduzi huo.
Miongoni mwa waimbaji wapya, wanaotarajiwa kuling’arisha kundi hilo ni pamoja na Mariam Mohamed, mshindi wa shindano la Bongo Star Search (BSS) mwaka jana.
Akizungumza na Burudani mjini Dar es Salaam wiki hii, Mariam alisema ameamua kuelekeza nguvu zake katika muziki huo kutokana na uwezo mkubwa alionao kiuimbaji.
Mariam anaamini kuwa, kwa sasa soko la muziki huo ni kubwa, ikilinganishwa na miziki mingine na kuongeza kuwa, iwapo atakuwa makini katika kazi yake, anaweza kufika mbali.
Mwanadada huyo mwenye mtoto mmoja, amejaaliwa kuwa na sauti yenye mvuto na inayoliwaza. Pia ni mahiri katika kutibwirika awapo stejini na sifa hizo ni miongoni mwa zilizomwezesha kuibuka mshindi wa shindano la BSS mwaka jana.
Mariam alisema tangu akiwa mdogo, alikuwa mpenzi mkubwa wa muziki huo na kwamba hawezi kuuacha kwa sababu upo kwenye damu yake.
Alisema uamuzi wake wa kujiunga na shindano la BSS ulilenga kuonyesha kipaji chake kwa vile alikuwa na imani kubwa kwamba, uwezo wa kuimba na kuvutia hadhira anao.
“Kwa kweli hakuna mtu aliyenishawishi kuupenda muziki huu. Hiki ni kipaji nilichorithi kutoka kwa marehemu babu yangu, ambaye alikuwa mwimbaji mashuhuri,”alisema.
Mariam alisema alianza kujifunza uimbaji kwa kuiga nyimbo za wasanii mbalimbali maarufu wa muziki huo hapa nchini na kuendelea kuonyesha kipaji chake alipokuwa akisoma shule ya msingi ya Kigogo Luhanga, Dar es Salaam.
Mwanadada huyo mwenye mwili uliojaajaa na kujengeka vyema alisema, akiwa katika shule hiyo, alishiriki mashindano ya kuimba na mara zote alikuwa akiiongoza shule yake kushinda.
Alisema kutokana na kuvutiwa na kipaji chake, baadhi ya walimu wa shule hiyo walimshauri aendeleze kipaji chake cha uimbaji kwa vile alikuwa na uwezo mkubwa wa fani hiyo.
Kutokana na uwezo mdogo wa familia yake, Mariam hakubahatika kuendelea na masomo ya sekondari. Baada ya kumaliza shule ya msingi mwaka 2007, aliamua kujihusisha na kazi za kufuma vitambaa, ususi na kupamba maharusi.
Mbali ya kuwa na kipaji cha uimbaji, Mariam pia ni hodari katika ususi wa nywele za aina mbalimbali. Utaalamu wake huo umemwezesha kujipatia umaarufu mkubwa katika eneo analoishi.
“Kwa siku nilikuwa naweza kusuka hata vichwa kumi, wateja wangu walikuwa wakitoka sehemu mbalimbali, hadi nikafikia uamuzi wa kutaka kufungua saluni," alisema.
Alisema kazi hiyo alikuwa akiifanya nyumbani kwao na kwamba wateja wake walikuwa wakimfuata kutokana na kutokuwa na ofisi maalumu.
Kabla ya kushiriki katika shindano la BSS, Mariam alijiunga na kikundi cha taarab cha Kings chenye maskani yake Mburahati, Dar es Salaam, lakini hakubahatika kurekodi nacho wimbo wowote.
Mwanadada huyo mwenye macho ya mwito alisema, aliamua kuimba nyimbo za taarab wakati wa shindano la BSS kwa lengo la kuonyesha kipaji na uwezo wake katika fani hiyo.
Tangu alipojiunga na kundi la Five Stars, Mariam amesema amesharekodi nalo wimbo mmoja, unaojulikana kwa jina la ‘Ulaumiwe wewe nani’. Alisema wimbo huo utapigwa kwa mara ya kwanza wakati wa onyesho la uzinduzi litakalofanyika kesho.
Kwa mujibu wa Mariam, lengo lake kubwa ni kutumia uwezo wake wote kuhakikisha kuwa, kundi hilo lililoundwa upya, linapata mafanikio makubwa kimuziki.
Aliushukuru uongozi wa kundi hilo na wasanii wenzake kwa kumpa ushirikiano mkubwa, hali aliyosema imezidi kumwongezea ari ya kiuimbaji.
Mariam alisema anapenda kuishi maisha ya kawaida na kusisitiza kuwa, kamwe katika maisha yake, hafurahii kuitwa nyota. Chakula kikubwa anachokipenda ni ubwabwa na maharage.
Mariam ametoa mwito kwa serikali kuisimamia vyema sheria ya hatimiliki ili wasanii waweze kunufaika na vipaji vyao, badala ya ilivyo sasa, ambapo alisema wanaonufaika ni wajanja wachache.
Mwimbaji huyo, ambaye ni mwenyeji wa Kilwa Masoko mkoani Lindi, amewataka wasanii nchini kuwa na ushirikiano na kusaidiana ili iwe rahisi kwao katika kutekeleza majukumu yao.
Mariam alizaliwa mwaka 1990 katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dar es Salaam. Ni mtoto wa kwanza katika familia ya watoto wanne. Hajaolewa, lakini anaye mchumba na wanatarajia kufunga ndoa hivi karibuni.

CHRISS: Kava za filamu wizi mtupuMTUNZI, mtayarishaji na mwongozaji maarufu wa filamu na tamthilia nchini, Chrissant Mhengga amesema, utengenezaji wa kava nyingi za filamu umelenga kuwaibia mashabiki wa tasnia hiyo.
Akizungumza na Burudani mjini Dar es Salaam wiki hii, Mhengga alisema, kava nyingi zinazotengenezwa hapa nchini kwa ajili ya filamu, haziendani na maudhui ya filamu hizo.
Akitoa mfano, Mhengga alisema mara nyingi kava za filamu zinakuwa na urembo mwingi kwa ajili ya kuvutia wateja, lakini vikorombwezo vinavyowekwa havimo ndani ya filamu husika.
“Utakuta kwenye picha ya kava, muhusika ama wahusika wakuu wanaonekana wamevaa mavazi ya gharama, lakini ndani ya filamu hakuna sehemu yoyote wanayoonekana wakiwa wamevaa mavazi hayo,”alisema.
“Na wakati mwingine unaweza kuona picha ya kava ikionyesha macho ya mmoja wa wahusika yanawaka moto, lakini ukitazama filamu yenyewe, huwezi kukutana na tukio hilo,”aliongeza.
Mhengga alilaumu tabia ya baadhi ya watayarishaji wa filamu nchini, kutoa zaidi ya filamu kumi kwa mwaka na kuongeza kuwa, huo ni udanganyifu kwa mashabiki wa fani hiyo.
Alisema kuharakisha kutoa filamu kwa sababu ya pesa, kumechangia kuifanya tasnia hiyo ionekane kuwa ya kulipua kutokana na filamu nyingi kukosa ubora unaotakiwa.
Mhengga pia alilaumu tabia ya kuzipa filamu za kibongo majina ya Kiingereza kwa madai kuwa, kufanya hivyo ni kuishusha thamani lugha ya Kiswahili, ambayo alisema ina utajiri mkubwa wa misemo na nahau zenye mvuto.
“ Huu ni upungufu mkubwa katika filamu zetu kwa sababu lugha ya Kiswahili ina hazina ya maneno mengi na yenye ladha nzuri. Sasa kama wanazipa filamu majina ya kiingereza, kwa nini waweke tafsiri yake kwa Kiswahili kwenye mabano?” Alihoji.
Muongozaji huyo wa filamu pia aliwatupia lawama watayarishaji wengi wa filamu nchini kwa kupendelea zaidi hadithi za mapenzi, ambazo alisema sio utamaduni wa kiafrika.
Alisema filamu za mapenzi hazihusiani na maisha halisi ya Kitanzania kwa sababu huo ni utamaduni wa kizungu na kwamba zipo hadithi nyingi na nzuri zinazohusu mila na utamaduni wa kiafrika, ambazo zinafaa kutengenezewa filamu.
Mhengga alisema uzuri wa filamu unategemea zaidi uzito wa hadithi na mwongozo wake na kwamba, jamii ya Tanzania bado inahitaji zaidi kuelimishwa kuliko kuburudishwa.
Alisema ni kweli kwamba maendeleo ya fani ya filamu hivi sasa ni makubwa, lakini filamu nyingi hazina mvuto na mafunzo kwa jamii kutokana na kukosekana utaalamu katika kuziandaa.
“Kuna dada mmoja mtayarishaji wa filamu kule Kenya, alipohojiwa alisema, alitumia miezi minane kuandika mwongozo wa filamu yake, lakini akatumia wiki moja katika kupiga picha. Hii inaonyesha kuwa, hadithi na mwongozo ni mambo muhimu na ya kuzingatiwa sana katika utengenezaji wa filamu,”alisema.
Mtaalamu huyo wa mambo ya filamu alisema, filamu nyingi za kibongo zimeandaliwa kama tamthilia kwa vile ndani ya filamu moja, zinaweza kupatikana filamu zingine tatu au nne.
Mhengga, ambaye ni mwasisi wa kundi la sanaa la Kaole na mwalimu wa wasanii wengi maarufu nchini alisema, ni kweli kuwa baadhi ya wasanii wamekuwa wakilipwa fedha nyingi hivi sasa kutokana na fani hiyo, lakini bado kiwango wanachokipata ni kidogo.
Alisema iwapo kungekuwepo na usimamizi mzuri katika mauzo ya filamu na kazi hiyo ingekuwa ikifanyika kwa utaalamu wa hali ya juu, wasanii wangeweza kupata fedha nyingi zaidi na hivyo kunufaika na vipaji vyao.
“Hata kama utamlipa msanii shilingi milioni 10 kwa filamu moja, kutokana na maisha wanayoishi, bado pesa hizo haziwezi kutosheleza mahitaji yao kwa sababu wanapenda sana kutanua na kujionyesha,”alisema.
Mhengga ametoa mwito kwa wasanii wa maigizo, kupenda kujifunza zaidi kuhusu fani hiyo kwa kusoma mambo yanayohusu filamu kupitia kwenye mitandao na pia kuomba ushauri kutoka kwa waliowazidi utaalamu.
Kwa sasa, Mhengga yupo katika hatua za mwisho za kukamilisha filamu yake mpya ya ‘Hazina ya marehemu’ kabla ya kuibuka na filamu nyingine, itakayojulikana kwa jina la ‘Ndoa ya hayawani’.
Alisema ameamua kuziita filamu zake kwa majina ya Kiswahili ili mashabiki waweze kujua ndani yake kuna nini badala ya kuzipa majina ya Kiingereza, ambayo majina na maudhui yake huwa tofauti.

Sikinde yaipiga bao Msondo Ngoma


BENDI ya muziki wa dansi ya Mlimani Park Orchestra ‘Sikinde’ imewapiga bao mahasimu wao, Msondo Ngoma baada ya kumnyakua mwimbaji wao nyota, Shukuru Majaliwa.
Majaliwa, ambaye ni mwajiriwa wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), alitambulishwa rasmi kwa mashabiki wa Sikinde katika onyesho lililofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita kwenye ukumbi wa DDC Kariakoo, Dar es Salaam.
Akizungumza wakati wa utambulisho huo, Majaliwa alisema ameamua kujiunga na Sikinde kwa ridhaa yake mwenyewe na bila ya ushawishi wa mtu yeyote.
“Ninachoweza kusema ni kwamba, nilikuwa nimepotea njia kwenda Msondo, lakini sasa nipo nyumbani. Kuanzia leo mimi ni mwimbaji wa Sikinde,”alisema mwanamuziki huyo, aliyeshangiliwa kwa mayowe mengi na mashabiki wa bendi hiyo.
Aliongeza kuwa, kabla ya kujiunga na Sikinde, aliwaeleza viongozi wa bendi hiyo sababu za kuondoka kwake Msondo na kuongeza kuwa, walimwelewa ndio maana walimkubalia ombi lake.
Majaliwa alikuwa akifanyakazi Msondo Ngoma akiwa ‘deiwaka’ kutokana na kuwa mwajiriwa wa JWTZ. Pia ni mwanamuziki wa bendi ya jeshi hilo ya Mwenge Jazz.
Kufuatia uamuzi wake huo, Majaliwa pia atakuwa akifanyakazi Sikinde akiwa ‘deiwaka’. Ajira yake jeshini haimbani kufanyakazi katika bendi za uraiani.
Akizungumzia ujio wa mwanamuziki huyo, kiongozi mkuu wa Sikinde, Habibu Abbas ‘Jeff’ alisema, wameingia naye mkataba maalumu na kuongeza kuwa, tayari ameshaanza mazoezi na bendi hiyo tangu Jumanne iliyopita.
Jeff alisema mwimbaji huyo mwenye uwezo wa kuiga sauti ya marehemu Moshi William, anafanya mazoezi ya kuimba nyimbo mpya za bendi hiyo na pamoja na wimbo wake binafsi.
“Kusema ule ukweli, kwa muda mrefu tulikuwa tukihitaji mwanamuziki wa aina yake na sasa tumempata. Tutaamini atatusaidia sana katika kuinyayua juu zaidi bendi yetu,”alisema.
Jeff alisema kabla ya kuingia mkataba na Majaliwa, waliitisha kikao cha wanamuziki wote wa Sikinde na kuulizana iwapo atawafaa na wote kwa pamoja walimkubali.
Majaliwa anatarajiwa kuanza kuitumikia rasmi Sikinde leo katika onyesho lao la pamoja na Extra Bongo litakalofanyika kwenye ukumbi wa Mzalendo Pub, Kijitonyama, Dar es Salaam.

Tunataka ubingwa wa Afrika-TimbeKOCHA Mkuu wa timu ya soka ya Yanga, Sam Timbe ametamba kuwa, lengo lake msimu ujao ni kuiwezesha timu hiyo kutwaa ubingwa wa klabu za Afrika.
Timbe alitoa majigambo hayo jana wakati wa mazoezi ya timu hiyo yaliyofanyika asubuhi kwenye uwanja wa Kaunda uliopo Jangwani, Dar es Salaam.
Majigambo hayo ya Timbe yamekuja wiki kadhaa baada ya kuiwezesha timu hiyo kutwaa Kombe la Kagame baada ya kuichapa Simba bao 1-0 katika mechi ya fainali, iliyochezwa mapema mwezi huu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Kocha huyo alisema kwa sasa, hana haja ya kuhangaikia mataji ya Afrika Mashariki na Kati kwa vile ameyakinai, hivyo anataka kuweka rekodi mpya ya kutwaa ubingwa wa Afrika.
Timbe, ambaye ni raia kutoka Uganda alisema, tayari ameshatwaa Kombe la Kagame akiwa na klabu za Villa na Polisi za Uganda, Atraco ya Rwanda na sasa Yanga ya Tanzania Bara.
Alisema hakuna kocha anayeweza kufikia rekodi yake kwa sasa na kusisitiza kuwa, dhamira yake ni kuongeza mataji mengine zaidi akiwa Yanga.
“Nina uhakika wa kutwaa tena ubingwa wa Tanzania Bara msimu ujao nikiwa na Yanga na nashukuru kuona kwamba kikosi changu kimekamilika,”alisema kocha huyo.
Kocha huyo asiye na mbwembwe na makeke alisema, amepania kuhakikisha Yanga inafuzu kucheza hatua ya makundi ya ligi ya mabingwa wa Afrika mwakani na ikiwezekana kutwaa ubingwa.
“Taarifa nilizonazo ni kwamba, Yanga ilishawahi kucheza hatua hiyo mwanzoni mwa miaka ya 2000, hivyo lengo langu ni kwenda mbali zaidi, ikiwezekana kucheza nusu fainali na kutwaa ubingwa,”alisema.
Aliongeza kuwa, anafurahishwa na mazoezi ya timu yake yanayoendelea kwenye uwanja wa Jangwani kwa vile wachezaji wake wamekuwa wakiyafuata na kuyashika vyema maelekezo yake.
Kwa sasa, Yanga inajiandaa na mchezo wake wa kuwania Ngao ya Hisani dhidi ya mahasimu wao Simba, utakaopigwa Agosti 20 mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Awali, mechi hiyo ilikuwa ipigwe Agosti 17 kwenye uwanja huo, lakini umezogezwa mbele ili kutoa nafasi kwa wachezaji wa timu hiyo, kuichezea timu ya Taifa, Taifa Stars katika mechi ya kirafiki dhidi ya Palestina.
Wakati huo huo, wachezaji wa Yanga jana asubuhi walionekana kuyafurahia mazoezi waliyokuwa wakipewa na Kocha Mkuu wa timu hiyo, Sam Timbe kwenye uwanja wa Kaunda, Dar es Salaam.
Katika mazoezi hayo, wachezaji wa timu hiyo walikuwa wakibebana wawili wawili na kuruka viunzi kwa lengo la kujenga stamina kabla ya kucheza soka.

Yanga kujipima ubavu kwa Coastal Union

MABINGWA wa soka wa Tanzania Bara, Yanga wanatarajiwa kushuka dimbani Jumapili ijayo, kumenyana na Coastal Union katika mechi ya kirafiki itakayochezwa kwenye Uwanja wa Mkwakwani mjini Tanga.
Ofisa Habari wa Yanga, Louis Sendeu, alisema mjini Dar es Salaam jana kuwa, pambano hilo ni maalumu kwa ajili ya maandalizi ya ligi kuu ya Tanzania Bara.
Sendeu alisema, katika mechi hiyo, Kocha Sam Timbe atawatumia wachezaji wake wapya kadhaa waliosajiliwa kwa ajili ya msimu ujao wa ligi.
Mbali na kuwajaribu wachezaji hao wapya, Sendeu alisema kocha huyo pia atapima uwezo wa kikosi chake baada ya kufanya mazoezi kwa wiki mbili kwenye uwanja wa Kaunda uliopo Jangwani, Dar es Salaam,
“Hii ni nafasi nzuri kwa Kocha Timbe kuona ni kwa kiasi gani wachezaji wake wameweza kushika mafunzo aliyowapa hadi sasa na pia timu inavyoweza kucheza kwa ushirikiano,”alisema.
Wachezaji wapya wa Yanga wanaotarajiwa kushuka dimbani Jumapili ni pamoja na Kenneth Asamoah, Haruna Niyonzima, Shabani Kado, Hamisi Kiiza, Oscar Joshua, Idrisa Rashid, Godfrey Taita.
Kwa upande wa Coastal Union, mechi hiyo itakuwa ya pili ya kirafiki kwenye uwanja huo baada ya wiki iliyopita kuibuka na ushindi dhidi ya Azam FC.
Kwa sasa, Coastal Union ipo mjini Mombasa, nchini Kenya, ambako imekwenda kuweka kambi kwa ajili ya kujiandaa na ligi hiyo. Timu hiyo inanolewa na Kocha Hafidh Badru.

USAJILI WA WACHEZAJI ENGLAND

Manchester United
Waliosajiliwa:
Phil Jones (Blackburn)
Ashley Young (Aston Villa)
David De Gea (Athletico Madrid)
Waliouzwa:
John O'Shea (Sunderland)
Wes Brown (Sunderland)
Nicky Ajose (Peterborough)
Ryan Tunnicliffe (Peterborough)
Scott Wootton (Peterborough)
Joe Dudgeon (Hull City)
Bebe (Besiktas)
Ritchie De Laet (Norwich)
Conor Devlin (huru)
Owen Hargreaves (huru)
Edwin van der Sar (amestaafu)
Gary Neville (amestaafu)
Paul Scholes (amestaafu)

Arsenal
Waliosajiliwa:
Carl Jenkinson (Charlton)
Gervinho (Lille)
Waliouzwa:
Gael Clichy (Man City)
Denilson (Sao Paulo)
Mark Randall (Chesterfield)
Thomas Cruise (huru)
Roarie Deacon (huru)

Manchester City
Waliosajiliwa:
Gael Clichy (Arsenal)
Stefan Savic (Partizan)
Waliouzwa:
Jerome Boateng (Bayern Munich)
Patrick Vieira (huru)
Javier Garrido (huru)
Shaleum Logan (huru)
Scott Kay (huru)
Javan Vidal (huru)
James Poole (huru)
Andrew Tutte (huru)
David Gonzalez (Aberdeen)

Aston Villa
Waliosajiliwa:
Shay Given (Manchester City)
Waliouzwa:
Ashley Young (Manchester United)
Nigel Reo-Coker (huru)
John Carew (huru)
Moustapha Salifou (huru)
Robert Pires (huru)
Isaiah Osbourne (huru)
Harry Forrester (huru)
Arsenio Halfhuid (huru)
Durrell Berry (huru)
Ellis Deeney (huru)
Calum Flanagan (huru)
Brad Friedel (huru)

Blackburn Rovers
Waliosajiliwa:
Hakuna
Waliouzwa:
Phil Jones (Manchester United)
Benjani Mwarurawi (huru)
Jordan Bowen (huru)
Jason Brown (huru)
Zurab Khizanishvili (huru)
Michael Potts (huru)
Marceo Rigters (huru)
Frank Fielding (Derby County)

Bolton Wanderers
Waliosajiliwa:
Darren Pratley (Swansea)
Waliouzwa:
Ali Al Habsi (Wigan)
Johan Elmander (Galatasaray)
Jlloyd Samuel (huru)
Joey O'Brien (huru)
Tamir Cohen (huru)
Sam Sheridan (huru)
Maison McGeechan (huru)
Tom Eckersley (huru)

Chelsea
Waliosajiliwa:
Hakuna
Waliouzwa:
Michael Mancienne (Hamburg)
Jacopo Sala (Hamburg)
Jeffrey Bruma (Hamburg)
Michael Woods (huru)
Samuel Hutchinson (huru)
Carl Magnay (huru)
Jan Sebek (huru)
Danny Philliskirk (huru)

Everton
Waliosajiliwa:
Eric Dier (Sporting Lisbon)
Waliouzwa:
James Vaughan (Norwich)
Luke Dobie (Middlesbrough)
Hope Akpan (huru)
Iain Turner(huru)
Kieran Agard (huru)
Nathan Craig (huru)
Gerard Kinsella (huru)
Lee McArdle(huru)

Fulham
Waliosajiliwa:
John Arne Riise (AS Roma)
Dan Burn (Darlington)
Waliouzwa:
Kagisho Dikgacoi (Crystal Palace)
Diomansy Kamara (huru)
John Pantsil (huru)
Eddie Johnson (huru)
Matthew Saunders (huru)

Liverpool
Waliosajiliwa:
Jordan Henderson (Sunderland)
Charlie Adam (Blackpool)
Stewart Downing (Aston Villa)
Waliouzwa:
Jason Banton (huru)
Deale Chamberlain (huru)
Douglas Cooper (huru)
Sean Highdale (huru)
Steven Irwin (huru)
Nikola Saric (huru)

Newcastle
Waliosajiliwa:
Yohan Cabaye (Lille)
Demba Ba (West Ham)
Mehdi Abeid (Lens)
Sylvain Marveaux (Rennes)
Waliouzwa:
Kevin Nolan (West Ham)
Sol Campbell (huru)
Shefki Kuqi (huru)
Patrick McLaughlin (huru)

Norwich
Waliosajiliwa:
Ritchie De Laet (Manchester United)
Steve Morison (Millwall)
James Vaughan (Everton)
Elliott Bennett (Brighton)
Waliouzwa:
Jens Berthel Askou (huru)
Matt Gill (huru)
Sam Habergham (huru)

Queen Park Rangers
Waliosajiliwa:
Jay Bothroyd (Cardiff)
Kieron Dyer (West Ham)
Waliouzwa:
Lee Brown (huru)
Pascal Chimbonda (huru)
Elliott Cox (huru)
Gavin Mahon (huru)
Joe Oastler (huru)
Josh Parker (huru)
Romone Rose (huru)
Georgias Tofas (huru)

Stoke City
Waliosajiliwa:
Hakuna
Waliouzwa:
Abdoulaye Faye (West Ham)
Eidur Gudjohnsen (huru)
Ibrahima Sonko (huru)

Sunderland
Waliosajiliwa:
Connor Wickham (Ispwich Town)
Craig Gardner (Birmingham City)
Roarie Deacon (Arsenal)
Ji Dong-won (Chunnam Dragons)
Sebastian Larsson (Birmingham City)
Wes Brown (Man United)
John O'Shea (Man United)
Keiren Westwood (Coventry)
Waliouzwa:
Jordan Henderson (Liverpool)
Bolo Zenden (huru)
Michael Kay (huru)
Nathan Luscombe (huru)
Daniel Madden (huru)
Robert Weir (huru)
Nathan Wilson (huru)
Mvoto Jean-Yves (huru)

Swansea City
Waliosajiliwa:
Danny Graham (Watford)
Waliouzwa:
Dorus De Vries (Wolverhampton)
Darren Pratley (Bolton)

Tottenham Hotspurs
Waliosajiliwa:
Brad Friedel (Aston Villa)
Waliouzwa:
Jonathan Woodgate (huru)
Jamie O'Hara (Wolves)

West Bromwich
Waliosajiliwa:
Billy Jones (Preston)
Gareth McAuley (Ipswich)
Waliouzwa:
Borja Valero (Villarreal)
Giles Barnes (huru)
Abdoulaye Meite (huru)
Gianni Zuiverloon (huru)

Wigan Athletics
Waliosajiliwa:
Ali Al Habsi (Bolton)
Waliouzwa:
Jason Koumas (huru)
Steven Caldwell (huru)
Daniel De Ridder (huru)
Joseph Holt (huru)
Thomas Lambert (huru)
Thomas Oakes (huru)
Francis Pollitt (huru)
Abian Serrano Davila (huru)

Wolves
Waliosajiliwa:
Jamie O'Hara (Tottenham)
Dorus De Vries (Swansea)
Waliouzwa:
Adriano Basso (huru)
John Dunleavy (huru)
Marcus Hahnemann (huru)
David Jones (huru)
Nathan Rooney (huru)

MAMBO YA MSONDO TUACHIE WENYEWE!
REPA wa bendi ya muziki wa dansi ya Msondo Ngoma, Roman Mng’ande ‘Romario’ (kushoto) akitibwirika stejini sanjari na mcheza shoo wa bendi hiyo, Mama Vanesa katika onyesho lililofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita kwenye ukumbi wa DDC Kariakoo, Dar es Salaam. (Picha na Emmanuel Ndege).

FIVE STARS MPYA KUZALIWA KESHO

JOKHA Kassim

Mussa Kijoti

SAMIRA Rajabu
ZENA Mohamed


KIKUNDI cha taarab cha Five Stars kinatarajiwa kufanya onyesho la uzinduzi mpya, utakaofanyika kesho kwenye ukumbi wa hoteli ya Travertine, Magomeni, Dar es Salaam.
Kiongozi wa kikundi hicho, Ally J alisema mjini Dar es Salaam juzi kuwa, maandalizi yote kwa ajili ya onyesho hilo yamekamilika.
Five Stars inafanya uzinduzi huo, kufuatia kuundwa upya baada ya wasanii wake 14 kufariki katika ajali ya gari, iliyotokea mapema mwaka huu Mikumi mkoani Morogoro.
Ally J alisema katika uzinduzi huo, wasanii wao wote wapya watapanda jukwaani, ikiwa ni pamoja na kuimba vibao vyao vipya, vitakavyokuwemo kwenye albamu yao ya kwanza.
Alivitaja vibao hivyo kuwa ni Mwenye hila habebeki, Watu na tabia zao, Ulaumiwe wewe nani, Silipizi ubaya, First Lady na Sina gubu nina sababu.
Miongoni mwa wasanii wapya wanaotarajiwa kupanda jukwaani leo ni pamoja na Mussa Kijoti na Mariam Mohamed, ambaye ni mshindi wa shindano la Bongo Star Search mwaka jana.
Waimbaji wengine wanaotarajiwa kupamba onyesho hilo ni pamoja na Jokha Kassim, ambaye alikuwepo kwenye kundi hilo kabla ya kujiengua.
Ally J amewataka mashabiki kujitokeza kwa wingi kushuhudia onyesho hilo kwa vile wamewaandalia vitu vya uhakika, ambavyo vitalifanya kundi hilo lirejee kwenye chati.

KOVA MGENI RASMI MISS ILALA


KAMANDA wa Kanda Maalumu ya Polisi mkoa wa Dar es Salaam, Suleiman Kova anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika shindano la kumsaka mrembo wa kanda ya Ilala.
Mratibu wa shindano hilo, Jackson Kalikumtima alisema mjini Dar es Salaam jana kuwa, warembo 12 wanatarajiwa kupanda jukwaani kuwania taji hilo.
Kwa mujibu wa Kalikumtima, shindano hilo limepangwa kufanyika kesho kuanzia saa mbili usiku katika viwanja vya Mnazi Mmoja mjini Dar es Salaam.
Kalikumtima alisema washindi watatu wa kwanza wa shindano hilo, wanatarajiwa kuiwakilisha kanda ya Ilala katika shindano la kumsaka Miss Tanzania 2011 litakalofanyika Septemba mwaka huu.
Hii itakuwa mara ya kwanza kwa Kamanda Kova kuhudhuria mashindano ya urembo akiwa mgeni rasmi, tangu alipoteuliwa kushika wadhifa huo miaka michache iliyopita.
“Tunajivunia kuwa pamoja na kiongozi huyu kwa sababu ndiye mwenye dhamana ya usimamizi wa ulinzi na usalama katika Jiji la Dar es Salaam na pia warembo wanaoshiriki kwenye shindano hili walishiriki katika shughuli za kuhamasisha ulinzi anaousimamia,”alisema Kalikumtima.
Aliongeza kuwa, kuwepo kwa Kamanda Kova katika shindano hilo ni uthibitisho wa wazi wa kuwepo kwa ulinzi mkali na kuwataka watu wanaomiliki vyombo vya usafiri wasiwe na wasiwasi wa usalama wao.
Kalikumtima alisema mandhari ya uwanja huo itabadilishwa na kugeuzwa kuwa eneo la starehe na burudani na kwamba michoro ya viwanja hivyo imetengenezwa kwa kufananishwa na Taman Mini Indonesia Park iliyoko katika Jiji la Jakarta.
Alisema kiingilio cha juu katika shindano hilo kitakuwa sh. 60,000, ambapo watakaolipa fedha hizo, watapata huduma ya chakula cha jioni kwenye viwanja hivyo.
Kwa mara ya mwisho, mrembo wa Ilala, Angela Damas alishinda taji la Miss Tanzania mwaka 2002. Mwaka 2003, Ilala ilishika nafasi ya tatu kupitia mrembo wake, Nargis Mohamed wakati mwaka 2004, mrembo wake mwingine, Verdiana Kamugisha alishika nafasi ya pili.
Kalikumtima alisema shindano hilo limedhaminiwa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), Vodacom Tanzania, Paradise City Hotel, Syscorp Group, Channel Ten, Michuzi Blogspot, Paris Pub, Papazi Entertainment, Maisha Club, TV Sibuka, Sofia Production, Fabak Fashion na Clouds FM.

Tuesday, July 26, 2011

BLOGU YA LIWAZO ZITO YAPATA TUZO
Wapenzi wasomaji wa blogu hii ya Liwazozito, napenda kuchukua fursa hii kuwashukuru wale wote walioipendekeza ishiriki kwenye shindano la blogu bora za Bongo. Blogu hii ilishirikishwa katika vipengele vya Best Informative Sports na Best Enterpreneur. Japokuwa haikushinda tuzo yoyote kati ya tuzo hizo mbili, lakini imetunukiwa vyeti viwili vya ushiriki. Kwangu, kushinda tuzo ni jambo lingine, lakini kupendekezwa na wasomaji ishiriki kwenye tuzo hizo ni heshima kubwa. Nawashukuru waandaaji wa tuzo hizo na natumaini wataendelea kuziboresha zaidi ili kuondoa kasoro zilizojitokeza mwaka huu.


Thursday, July 21, 2011

Twanga Pepeta, Msondo kumchangia Gurumo


BENDI ya muziki wa dansi ya Twanga Pepeta International imeandaa onyesho la pamoja kati yake na Msondo Ngoma kwa ajili ya kumchangia kiongozi wake, Muhidin Gurumo.
Mkurugenzi wa Kampuni ya African Stars Entertainment (ASET), inayomiliki Twanga Pepeta, Asha Baraka alisema juzi kuwa, onyesho hilo litafanyika keshokutwa kwenye ukumbi wa Mango Garden, Kinondoni, Dar es Salaam.
Asha alisema lengo la onyesho hilo ni kuchangisha fedha kwa ajili ya matibabu ya Gurumo, ambaye hali ya afya yake si nzuri, kufuatia kuugua na kulazwa mara mbili kwenye Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
Kiongozi huyo wa Twanga Pepeta alisema wameamua kuandaa onyesho hilo kutokana na kutambua na kuthamini mchango wa Gurumo katika kuendeleza muziki wa dansi nchini.
“Tumeamua kwamba, mapato yote yatakayopatikana katika onyesho hilo yatakwenda kwa Mzee Gurumo kwa ajili ya kugharamia matibabu yake,”alisema.
Kwa mujibu wa Asha, wakati wa onyesho hilo, mshindi wa taji la Kimwana wa Twanga Pepeta 2011, Mary Khamis ataonyesha umahiri wake wa kucheza miondoko ya bendi hiyo.
Mbali na kumchangia Gurumo, Asha alisema bendi yake pia italitumia onyesho hilo kutangaza albamu yake mpya, inayotarajiwa kuzinduliwa baadaye mwaka huu.
Baadhi ya nyimbo zilizomo kwenye albamu hiyo ni pamoja na Kauli, Kiapo cha mapenzi, Umenivika umaskini, Mtoto wa mwisho, Dunia daraja na Penzi na shemeji.
Asha amewataka mashabiki wa muziki wa jiji la Dar es Salaam kujitokeza kwa wingi kwenye onyesho hilo ili kumuenzi mwanamuziki huyo mkongwe.

Cannavaro: Nakwenda El-Merreikh


BEKI mahiri wa timu ya soka ya Yanga, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ amethibitisha kupata nafasi ya kwenda kucheza soka ya kulipwa katika klabu ya El Merreikh ya Sudan.
Akizungumza na Burudani wiki hii, akiwa nyumbani kwake mjini hapa kwa ajili ya mapumziko, Cannavaro alisema amefurahi kupata nafasi hiyo kwa vile ni fursa nzuri ya kuonyesha uwezo wake.
Cannavaro alisema pia kuwa, kupata kwake nafasi hiyo pia kutasaidia kuitangaza Zanzibar kisoka na hivyo kutoa nafasi kwa wachezaji wengine wa visiwa hivyo kuitwa nje.
Beki huyo, ambaye pia huichezea timu ya Zanzibar na ile ya Taifa, Taifa Stars alisema, anatarajia kuondoka nchini Desemba mwaka huu kwenda Sudan kwa ajili ya kuanza kuitumikia El- Merreikh.
Kwa mujibu wa Cannavaro, tayari ameshaingia mkataba wa kuichezea timu hiyo kwa miaka miwili na amepata baraka zote kutoka kwa uongozi wa Yanga.
“Kwa kweli nimefarijika sana kupata nafasi hii na ninaamini nitatumia uwezo wangu wote kuitangaza Zanzibar na Tanzania kisoka ili wachezaji wengine nao waweze kupata nafasi hiyo,”alisema.
Cannavaro ameushukuru uongozi wa Yanga kwa kumkubalia kwenda kucheza soka ya kulipwa katika klabu hiyo ya Sudan na kuongeza kuwa, anaamini hatoacha pengo katika klabu hiyo.
Uongozi wa El-Merreikh ulivutiwa na kiwango cha beki huyo wakati wa michuano ya Kombe la Kagame, iliyomalizika hivi karibuni kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Katika michuano hiyo iliyodumu kwa wiki mbili, Yanga ilitwaa ubingwa baada ya kuichapa Simba bao 1-0 katika mechi ya fainali. Katika mechi za robo na nusu fainali, ilizitoa Red Sea ya Eritrea na St George ya Ethiopia kwa njia ya penalti.

MWASITI: Udhalilishaji kwa wasanii wa kike ukomeshwe


MCHEZA filamu na mpambaji maarufu wa waigizaji nchini, Mwasiti Mohamed amesema, baadhi ya watayarishaji wa sinema wa kiume wamekuwa na tabia ya kuwadhalilisha wasanii wa kike.
Mwasiti, maarufu kwa jina la Shishi amesema, watayarishaji hao wamekuwa wakitumia udhaifu wa wasanii wa kike kuwalazimisha kufanyanao mapenzi ili wawapatie nafasi kwenye filamu zao.
“Sio siri, udhalilishaji kwa wasanii wa kike ni mkubwa kwa sababu baadhi ya watayarishaji wa filamu wamekuwa wakiutumia umaarufu wao kuwalazimisha wasanii hao kufanyanao mapenzi,”alisema Mwasiti alipozungumza na Burudani mjini Dar es Salaam wiki hii.
Mwasiti alisema si jambo baya kwa wasanii kuwa na uhusiano wa kimapenzi, lakini ni vyema wafikie uamuzi huo kwa hiari bila ya kuwepo kwa kishawishi chochote.
Alisema inapotokea msanii wa kiume anamtaka msanii wa kike, anapaswa kumweleza jambo hilo bayana na muhusika akubali badala ya kumlazimisha.
Akizungumzia maendeleo ya fani hiyo nchini hivi sasa, Mwasiti alisema yanaridhisha, isipokuwa kikwazo kikubwa ni uwezo mdogo wa wasanii na watayarishaji wa filamu.
Alisema utengenezaji wa filamu unahitaji gharama kubwa ya pesa, ambazo watanzania wengi hawana na ndio sababu baadhi ya filamu zinakosa mvuto na uhalisia.
“Ukitaka kuandaa filamu inayoelezea ama kuonyesha matukio halisi ya ndani ya mahabusu na jela za Tanzania, huwezi kupata nafasi hiyo kutoka serikalini,”alisema.
“Vilevile si rahisi kwa watayarishaji wa filamu kupata nafasi ya kutumia mahakama zetu kutengeneza filamu, ama kutumia matukio ya nyumba kuungua na magari kugongana kwa sababu gharama zake ni kubwa,”aliongeza,
Mwasiti alisema binafsi ameandaa filamu inayoelezea mtiririko wa matukio hayo, lakini anashindwa kuitengeneza kwa sababu ya uwezo mdogo wa kifedha.
Alisema katika nchi zilizoendelea katika tasnia hiyo barani Afrika, zikiwemo Nigeria, Afrika Kusini, Ghana na zinginezo, utengenezaji wa filamu za aina hiyo ni rahisi kwa sababu wanao uwezo mkubwa kifedha.
“Wenzetu bajeti zao za kutengeneza filamu ni kubwa, wana uwezo wa kujenga nyumba za muda na kutumia hata magari halisi kutengeneza ajali, lakini sisi hatuwezi,”alisema.
Kwa mujibu wa Mwasiti, hata utumiaji wa silaha katika kutengeneza filamu za Kibongo ni mgumu kwa sababu si rahisi kupata silaha halisi kama vile bunduki na bastola na zinapotumika huwa ni za plastiki, hivyo kukosa uhalisia.
Alilitaja tatizo lingine linaloikumba fani hiyo kuwa ni ubinafsi wa baadhi ya watayarishaji wa filamu katika uteuzi wa washiriki, ambapo alidai kuwa, wengi hufanya upendeleo.
Alisema kwa sasa, wapo waigizaji wengi wazuri wa filamu nchini, lakini wanakosa nafasi ya kuonyesha vipaji vyao kutokana na uteuzi wa washiriki kutofanywa kwa umakini.
Mwasiti pia aliilaumu serikali kwa kupiga marufuku filamu ya shoga kuuzwa nchini kwa madai kuwa, inakiuka maadili ya Kitanzania. Alisema filamu hiyo ilikuwa ikielezea matukio halisi yanayotokea katika jamii za Kitanzania, hivyo ilipaswa kuachwa ili itoe funzo.
Alisema inashangaza kuona kuwa, katika baadhi ya filamu, washiriki wengi wa kike wamekuwa wakivaa mavazi nusu uchi na kukiuka maadili ya Kitanzania, lakini zimeachwa bila kuchukuliwa hatua yoyote.
“Zipo baadhi ya filamu zina kasoro nyingi. Utakuta wasanii wa kike wanavaa nusu uchi, wengine wanavaa nguo za kutokea usiku wanapoigiza majumbani na wengine wanaigiza wakiwa nyumbani, lakini aanavaa vimini. Haya yote hayapendi na yanaondoa uhalisia katika filamu,”alisema.
Mwasiti pia alilalamikia soko la filamu nchini kuwa kwa sasa ni gumu, hali inayosababisha wasanii waendelee kulipwa malipo kidogo huku wasambazaji wakifaidika zaidi kimapato.
Kwa sasa, Mwasiti amekamilisha kutengeneza filamu yake binafsi, inayojulikana kwa jina la ‘She is Mine’, akishirikiana na msanii mwenzake, Halima Yahya ‘Da Vina’. Filamu hiyo ipo katika hatua za mwisho na inatarajiwa kuingia sokoni wakati wowote.
Alisema filamu hiyo inaelezea juu ya matatizo mengi yanayowakumba binadamu katika maisha yao ya kila siku, sababu zake na jinsi ya kuyatatua.
Wasanii wengine walioshiriki kucheza filamu hiyo ni Halima, Ndumbago Misayo ‘Thea’ na Hashim Kambi.
Filamu zingine, ambazo Mwasiti ameshiriki kuzicheza ni Point of no return, Pretty Girl, iliyotayarishwa na Kampuni ya RJ, inayomilikiwa na Vicent Kigosi ‘Ray’ pamoja na Jirani na Safari, zilizotayarishwa na Rashid Mrutu.
Mwasiti, ambaye pia aliwahi kucheza tamthilia ya Martin, alisema anavutiwa zaidi na wasanii wanaomudu kuvaa uhusika katika filamu wanazocheza.
Mwanadada huyu aliyesomea utaalamu wa kupamba wasanii wa filamu na shughuli zingine, amewataka watayarishaji wa fani hiyo kuwatumia kwa lengo la kuzinafidhisha zaidi kazi zao na pia kuzipa uhalisia.

RAHA YA USHINDI

Mshindi wa taji la Redds Miss Temeke 2011, Husna Twalib akiwa ameshikilia kitita cha sh. milioni mbili alichozawadiwa juzi baada ya kuibuka mshindi wa taji hilo.

Ngasa aichachafya Man Utd

Mrisho Ngasa akipiga chini kwa hasira baada ya kukosa bao wakati alipoichezea Seattle Sounders ya Marekani katika mechi ya kirafiki dhidi ya Manchester United ya England

Mrisho Ngasa (kulia) akiwania mpira sambamba na beki Rio Ferdinand wa Manchester United

Mshambuliaji Mrisho Ngasa (kushoto) wa Seattle Sounders ya Marekani akichuana na beki Fabio Da Silva wa Manchester United ya England katika mechi ya kirafiki ya kimataifa iliyochezwa jana mjini Seattle. Ngasa aliichezea Seattle Sounders kwa majaribio. Katika mechi hiyo, Manchester United iliibuka na ushindi wa mabao 7-0.

Five Stars mpya yakamilikaMIEZI michache baada ya wasanii wake 13 kufariki katika ajali ya gari iliyotokea eneo la Mikumi mkoani Morogoro, uongozi wa kundi la muziki wa taarab la Jahazi upo kwenye hatua za mwisho za kuliunda upya.
Rais wa kundi hilo, Ally J alilieleza gazeti la Burudani juzi kuwa, uzinduzi wa kundi hilo jipya unatarajiwa kufanyika Julai 29 mwaka huu kwenye ukumbi wa hoteli ya Travertine, Magomeni, Dar es Salaam.
Ally alisema tayari wameshawapata wasanii wa kutosha wa muziki wa taarab na wameshaanza mazoezi kwa ajili ya kulifufua upya kundi hilo.
Alimtaja mmoja wa wasanii hao wapya kuwa ni mwimbaji, Mussa Ally ‘Kijoti’, ambaye ni kaka wa marehemu, Issa Kijoti, aliyefariki katika ajali hiyo.
Kwa mujibu wa Ally, waimbaji wengine wapya watakaounda kundi hilo ni pamoja na mshindi wa shindano la Bongo Star Search (BSS) mwaka jana, Mariam Mohamed na Isha Mzee.
Alisema katika uzinduzi huo, Mussa atakabidhiwa rasmi mikoba ya marehemu kaka yake, Issa na ataimba nyimbo zote zilizoachwa na ndugu yake huyo.
Ally alisema uzinduzi huo utasindikizwa na wasanii mbalimbali nyota wa muziki, akiwemo mwimbaji mkongwe, Mwanahawa Ally na makundi mengine ya taarab.
Amewataka mashabiki wa muziki huo, kujitokeza kwa wingi katika uzinduzi huo, ambao aliuelezea kuwa, utakuwa wa aina yake.

Isha Mashauzi afungashiwa virago Jahazi


UONGOZI wa kundi la muziki wa taarab la Jahazi umetangaza rasmi kumtimua mmoja wa waimbaji wake nyota, Isha Ramadhani ‘Mashauzi’.
Habari za uhakika kutoka ndani ya kundi hilo zimeeleza kuwa, Isha ametimuliwa kutokana na sababu mbalimbali, zikiwemo utovu wa nidhamu uliokithiri.
Uamuzi wa Jahazi kumtimua Isha umekuja miezi michache baada ya mwimbaji huyo pamoja na Leila Rashid kusimamishwa kwa tuhuma za kujiona bora kuliko wenzao.
Ilidaiwa wakati huo kuwa, Isha na Leila walikuwa na kawaida ya kuleta ‘mapozi’ wakati wa maonyesho ya kundi hilo na pia kufika mazoezini katika siku wanazopenda wenyewe.
Hata katika uzinduzi wa albamu ya saba ya kundi hilo, uliofanyika Mei mwaka huu kwenye ukumbi wa Travertine, Magomeni, Dar es Salaam, waimbaji hao wawili hawakuonekana jukwaani.
Chanzo cha habari kutoka ndani ya Jahazi kilieleza juzi kuwa, uamuzi wa kumfukuza Isha umefikiwa na uongozi kutokana na kushindwa kuonekana kwenye maonyesho ya kundi hilo kwa muda mrefu.
Kufuatia kushindwa kuonekana jukwaani kwa mwimbaji huyo, uongozi wa kundi hilo uliamua nyimbo zake ziimbwe na waimbaji wengine chipukizi, ambao wamekuwa kivutio kikubwa.
Kuna habari kuwa, tayari Isha ameshaamua kuanzisha kundi lake, akishirikiana na mama yake mzazi, Rukia Ramadhani.
Isha alijizolea umaarufu mkubwa kupitia kundi la Jahazi, linaloongozwa na Mzee Yussuf. Mwimbaji huyo mwenye makeke, aliwahi kurekodi albamu yake binafsi mwaka jana, iliyozidi kumpatia umaarufu, inayojulikana kwa jina la ‘Mama nipe radhi.’
“Ni kweli tumeamua kumtimua Isha Mashauzi kwenye kundi letu kwa sababu tumeshindwa kuvumilia vitendo vyake,” kilisema chanzo cha habari.
“Amekuwa haonekani kwenye maonyesho ya kundi letu, tukimuuliza, majibu yake yanakuwa ya jeuri, kwa ujumla amekuwa akionyesha vitendo vya utovu wa nidhamu,”kiliongeza.
Kwa mujibu wa mmoja wa viongozi wa kundi hilo, ambaye hakupenda jina lake litajwe gazetini kwa kuepuka malumbano kati yake na mwimbaji huyo, hawapo tayari kumpokea tena Isha kwenye kundi hilo.
"Kwa hatua aliyofikia, hatuwezi kumpokea tena Isha Ramadhani kwenye kundi hili. Tunashukuru Jahazi tuna waimbaji wazuri zaidi yake, aende tu, lakini ipo siku atalikumbuka kundi hili," alisema kiongozi huyo.
Hivi karibuni, Isha alikaririwa na gazeti hili akisema kuwa, bado yeye ni mwimbaji wa Jahazi na hawezi kuhama kwa madai kuwa, ana mapenzi makubwa na kundi hilo.
Uchunguzi uliofanywa na Burudani umebaini kuwa, kwa kipindi kirefu sasa, Isha amekuwa akifanya maonyesho kwa kujitegemea katika kumbi mbalimbali za burudani za mjini Dar es Salaam.
Katika hatua nyingine, kundi la Jahazi lipo katika hatua za mwisho za maandalizi ya uzinduzi wa albamu yake ya nane, inayotarajiwa kuzinduliwa baada ya mfungo wa mwezi wa Ramadhani.
Kiongozi wa kundi hilo, Mzee Yussuf alisema juzi kuwa, maandalizi kwa ajili ya uzinduzi wa albamu hiyo yamekamilika na itakuwa na nyimbo nne.
“Ninawahakikishia mashabiki wetu kwamba, albamu hii itakuwa bora kuliko zote zilizotangulia, hivyo wakae mkao wa kula kuisubiri,”alisema mtunzi na mwimbaji huyo mwenye kipaji.