KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Monday, February 8, 2016

SIMBA, YANGA ZAENDELEA KUMEREMETA LIGI KUU BARA



SIMBA na Yanga jana ziliendelea kuchanua katika michuano ya soka ya ligi kuu ya Tanzania Bara, baada ya kuibuka na ushindi dhidi ya Kagera Sugar na JKT Ruvu.

Wakati Simba iliichapa Kagera Sugar bao 1-0 kwenye Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga, watani wao Yanga walishusha kipigo cha mabao 4-0 dhidi ya JKT Ruvu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Pambano kati ya Simba na Kagera Sugar lilikuwa gumu na kali kutokana na kila timu kupania kushinda ili itoke uwanjani na pointi zote tatu.

Hata hivyo, mshambuliaji machachari Ibrahim Hajib ndiye aliyeiwezesha Simba kutoka uwanjani na ushindi baada ya kuifungia bao hilo la pekee na la ushindi.

Nayo Yanga ilijipatia mabao yake manne kupitia kwa Simon Msuva aliyefunga mawili, Haruna Niyonzima na Hamisi Tambwe.

Wakati huo huo, Azam jana ilirejea ligi kuu kwa kishindo kwa kupata ushindi kiduchu wa bao 1-0 dhidi ya Mwadui FC katika mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Azam Complex, ulioko Chamazi, Dar es Salaam.

Katika mechi zingine za ligi hiyo zilizochezwa Mbeya City ilitoka suluhu na Prisons Uwanja wa Sokoine, Mbeya, Ndanda FC ililazimishwa sare ya 1-1 na Mtibwa Sugar Uwanja wa Nangwanda Sijaona, Mtwara, Toto Africans ilishinda 2-1 dhidi ya Coastal Union Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza, Majimaji imeshinda 1-0 dhidi ya Mgambo JKT Uwanja wa Majimaji, Songea, wakati African Sports ilitoa sare ya 0-0 na Stand United Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.

No comments:

Post a Comment