KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Sunday, February 7, 2016

OCEAN VIEW KUZIDHAMINI MAFUNZO NA JKU


MENEJA wa hoteli za Zanzibar Ocean View Jacob Makundi (kulia), akimkabidhi Mkuu wa Idara ya Michezo wa Vyuo vya Mafunzo Khamis Ali Machenga, shilingi 5,000 zikiwa gharama za tiketi za mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kati ya klabu ya Mafunzo na AS Vita ya DRC itakayochezwa Februaei 13, 2016, ambazo zilikwishachapishwa na kuanza kuuzwa. Kampuni ya hoteli za Zanzibar Ocean View imeamua kubeba gharama hizo pamoja na za mechi ya JKU na Gaborone United ya Botswana kuwania Kombe la Shirikisho.

(Picha na Ameir Khalid).

Na Salum Vuai, ZANZIBAR
UONGOZI wa kampuni ya hoteli za Zanzibar Ocean View (ZGH), umeamua kubeba mzigo wa gharama za mechi za wawakilishi wa Zanzibar katika michuano ya klabu barani Afrika zitakazochezwa mwishoni mwa wiki ijayo.
Mechi hizo za kwanza za raundi ya awali, ni ile ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambapo Mafunzo wataikaribisha AS Vita kutoka Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, na JKU dhidi ya Gaborone United ya Botswana.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Februari 6, 2016 katika ukumbi wa Nyerere ulioko hoteli ya Zanzibar Ocean View mjini hapa, Meneja wa hoteli hizo Jacob Makundi, amesema hatua hiyo inalenga kuwafanya mashabiki wafike kwa wingi uwanjani siku ya mechi hizo.
Alifahamisha kuwa, tayari kampuni yake imezinunua tiketi elfu kumi (elfu tano kwa kila mechi) zilizobaki baada ya nyengine kuuzwa, kwa gharama ya shilingi elfu kumi, na zitagaiwa kwa mashabiki watakaofika uwanja wa Amaan siku za michezo hiyo bila malipo yoyote.
Makundi alifahamisha kuwa, kampuni yake pia itatoa fulana maalumu kwa wachezaji na viongozi wa klabu hizo, ambazo watavaa kabla ya mechi ya kwanza na watakaposafiri kwenda DRC na Botswana kwa ajili ya michezo ya marudiano.
Meneja huyo amezitaja gharama nyengine ambazo kampuni hiyo itazibeba, ni kutoa punguzo la asilimia 75 kwa waamuzi, makamisaa, viongozi na wachezaji wa timu za wageni kwa huduma ya malazi na chakula kwenye hoteli zake.
Ili kuwapa nguvu wachezaji wa Zanzibar, Makundi aliahidi kuwa kampuni hiyo itatoa zawadi ya shilingi milioni tano iwapo timu itashinda hapa nyumbani, na kuongeza kuwa ushindi huo utakuwa chachu kwao kufikiria motisha zaidi kwa mechi za ugenini.
“Kwa kuwa sisi ni wadau wakubwa wa michezo, tumeona iko haja ya kuwashajiisha wawakilishi wetu hawa ili wafanye vizuri na kuinua jina la Zanzibar katika soka la kimataifa na tunatoa wito kwa taasisi nyengine zijitokeze kuongeza nguvu,” alieleza.
Mapema, Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Michezo Zanzibar (BTMZ) Khamis Abdallah Said, aliushukuru uongozi wa kampuni hiyo, akisema unaonesha uzalendo kwa nchi katika kuunga mkono juhudi za kuendeleza michezo.
Naye Abdallah Juma Mohammed, aliyemuwakilisha Mkurugenzi wa kampuni hiyo yenye hoteli tano kubwa Unguja na Pemba Amani Ibrahim Makungu, alisema Zanzibar Ocean imeanza lakini mlango uko wazi kwa wengine kuzisaidia timu hizo na pia michezo mingine.
Akitoa shukuani kwa niaba ya timu zote mbuli, Mkuu wa Michezo katika Jeshi la Kujenga Taifa (JKU) Khamis Mohammed Suleiman, alisema ufadhili waliopata utawatia nguvu ya kuhakikisha wanaipeperusha vyema bendera ya Zanzibar kwenye michuano hiyo.
Jumamosi Februari 13, Mafunzo wataikaribisha AS Vita katika mechi ya Ligi ya Mabingwa, wakati siku inayofuata JKU watakuwa wenyeji wa Gaborone United kutika Botswana kuwania Kombe la Shirikuso.
Mechi zote hizo zitachezwa katika uwanja wa Amaan mjini Zanzibar kuanzia saa 10:00 jioni, na zile za marudiano zitapigwa wiki mbili baadae.

No comments:

Post a Comment