KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, February 3, 2016

SIMBA YAONGEZA DOZI LIGI KUU BARA


SIMBA SC imejiweka sawa kwenye mbio za ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara baada ya kuifunga Mgambo JKT mabao 5-1 jioni ya leo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Ushindi huo unaifanya Simba SC ifikishe pointi 39 baada ya kucheza mechi 17, sasa ikiwa inazidiwa pointi moja tu na mabingwa watetezi, Yanga SC walio kileleni, wakifuatiwa na Azam FC yenye pointi 39 pia.
Mshambuliaji Mganda, Hamisi Kiiza ‘Diego’ aliifungia Simba SC bao la kwanza dakika ya tano akimalizia krosi ya mshambuliaji Ibrahim Hajib.
Kiiza akakosa penalti dakika ya 14 iliyookolewa na kipa Mudathir Khamis, kufuatia Henry Chacha kuunawa mpira kwenye boksi.
Lakini Mwinyi Kazimoto akafunga bao la pili dakika ya 28 kwa shuti kali kutoka nje ya boksi baada ya kugongeana vizuri na Hajib.
Hajib akaenda kufunga mwenyewe bao la tatu dakika ya 42 baada ya kuwachambua mabeki watatu wa Mgambo na kipa wao Mudathir Khamis, kufuatia pasi ya Kazimoto.
Daniel Lyanga aliyetokea benchi kuchukua nafasi ya Hajib kipindi cha pili, aliifungia Simba SC bao la nne kwa shuti kali kutoka nje ya boksi baada ya pasi ya kiungo Said Ndemla.
Kiiza akahitimisha karamu ya mabao ya Simba SC kwa kufunga bao la tano dakika ya 82 akimalizia krosi ya Hassan Kessy, ambaye amecheza kwa kiwango cha juu leo.
Fuluzulu Maganga ‘akachafua gazeti’ kwa kuifungia Mgambo bao la kufutia machozi dakika ya 88 baada ya mabeki wa Simba SC kumuacha wakidhani ameotea.

CHANZO CHA HABARI: BLOGU YA BINZUBEIRY

No comments:

Post a Comment