'
Wednesday, June 10, 2015
TFF YAVUNJA MKATABA WA SIMBA NA MESSI
SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF), limevunja mkataba kati ya klabu ya Simba na mshambuliaji, Ramadhani Singano (Messi).
Kutokana na kuvunjwa kwa mkataba huo, Simba imetakiwa kuanza upya mazungumzo na mchezaji huyo, kama ina lengo la kutaka kumsajili msimu ujao kwa vile mkataba wa miaka mitatu walionao Simba, hautambuliki tena TFF.
Hatua hiyo imekuja baada ya TFF kubaini kuwa, kuna mkanganyiko katika mkataba alionao Messi na ule uliokuwa ukishikiliwa na viongozi wa Simba.
Mgogoro kati ya Messi na Simba, ulianza baada ya Messi kudai mkataba wake wa miaka miwili, umemalizika msimu uliopita huku Simba ikidai kuwa mchezaji huyo bado ana mkataba wa mwaka mmoja, utakaomalizika mwakani.
Akizungumza mjini Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa TFF, Celestine Mwesigwa, alisema mkataba wa mchezaji huyo na Simba, umegundulika una matatizo ndio maana wamefikia uamuzi wa kuuvunja.
"Kama Simba inataka kumsajili tena Messi, inachotakiwa kufanya ni kuzungumza naye upya,"alisema.
"Tumegundua kuna matatizo makubwa, siwezi kusema nani ameghushi mkataba kwa kuwa haya tayari ni makubaliano tuliyoafikiana kwa sasa. Mkataba wa miaka mitatu walionao Simba hatuutambui hivyo tunauvunja rasmi na tunaiagiza Simba ianze upya mazungumzo na Messi,"alisisitiza.
Mwesigwa alizitaka klabu za soka nchini, kuhakikisha zinatekeleza haki za wachezaji katika mikataba wanaoingia nao ili kuepusha migogoro.
Aidha, alitoa mwito kwa wachezaji wa Tanzania kuhakikisha wanatambua haki zao katika mikataba kwa kuisoma na kuielewa kabla ya kutia saini ili kujua nini wanachotakiwa kufanyiwa na klabu zinazowasajili.
Kwa upande wake, Messi alisema hana mpango wa kuichezea Simba msimu ujao kwa vile ameshahakikishiwa na TFF kwamba hawautambui mkataba wa miaka mitatu wa klabu hiyo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment