KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Sunday, June 7, 2015

STARS YATUA ETHIOPIA, YAJIFUA MARA MBILI



Kikosi cha timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) inayodhaminiwa na bia ya Kilimanjaro, leo kimeendelea na mazoezi asubuhi na jioni katika uwanja wa Benki ya Biashara ya Ethiopia kujiandaa na mchezo dhidi ya Misri.

Jana kikosi cha Stars kilifanya mazoezi majira ya saa 9 mchana katika uwanja wa Taifa wa Ethiopia (Addis Ababa) ambao pia unatumiwa na timu yao ya Taifa kwa mazoezi.

Taifa Stars ambayo imeweka kambi jijini Addis Ababa nchini Ethiopia inajiandaa na mchezo wa kuwania kufuzu kwa fainali za Mataifa Afrika (AFCON) mwaka 2017 dhidi ya timu ya taifa ya Misri.

Daktari wa Taifa Stars, Billy Haonga amesema hali ya hewa ya Addis Ababa ni nzuri kwa maandalizi ya mchezo dhidi ya Misri, kutokana na timu kufanya mazoezi katika ukanda wa juu (mwinuko kutoka usawa wa bahari) hali itakayopelekea wachezaji kuwa fit kwa ajili ya mchezo.

"Hali ya hewa ya Alexandria ni ya kawaida, hakuna baridi sana kutokana na kuzungukwa na bahari ya  Mediterania, hivyo kipindi cha wiki moja tutakachokuwa kambini hapa Addis Ababa tunatarajiwa vijana watakua vizuri kabisa kw aajili ya mchezo” Alisema Haonga”.

Wachezaji wote wa Taifa Stars waliopo kambini Addis Ababa wapo katika hali nzuri, kiafya, kifikra na morali ya juu kujiandaa na mchezo dhidi ya Mapaharao.

Wenyeji Chama cha Soka cha Ethiopia (EFF) wanaangalia uwezekano wa Taifa Stars kupata mchezo mmoja wa kirafiki wa kujipima nguvu kabla ya kuelekea nchini Misri.

Mchezo kati ya Misri na Tanzania unatarajiwa kuchezwa Juni 14, katika uwanja wa Borg El Arab jijini Alexandria, ikiwa ni mchezo wa kuwania kufuzu kwa fainali za Mataifa Afrika (AFCON) mwaka  2017.

Wachezaji walioko kwenye kikosi cha Stars ni  Deogratias Munish, Aishi Manula, Mwadini Ali, walinzi Shomari Kapombe, Oscar Joshua, Erasto Nyoni, Nadir Haroub, Aggrey Morris, Mwinyi Haji, Salum Mbonde na Juma Abdul.

Wengine ni Mwinyi Kazimoto, Abdi Banda, Salum Telela, Frank Domayo, Jonas Mkude, Said Ndemla, washambuliaji Saimon Msuva, John Bocco, Thomas Ulimwengu, Mbwana Samatta,Mrisho Ngasa na Juma Liuzio.

Msafara wa Taifa Stars utaongozwa na Wajumbe wa Kamati ya Utendaji, Vedastus Lufano na Geofrey Irick Nyange “Kaburu”.

Naye mjumbe wa kamati ya Utendaji  ya TFF Vedastus Lufano amesema timu inakwenda kuweka kambi Ethiopia kwa ajili ya kupambana katika mchezo dhidi ya Misri.

Kikosi kingine cha timu ya Taifa kitaondoka nchini siku ya jumamosi kuelekea nchini Rwanda kucheza mchezo wa kirafiki na timu ya taifa ya Rwanda katika kumbukumbu ya mauaji ya Kimbali.

Kocha Salum Mayanga ataondoka na kikosi cha wachezaji 18 kuelekea nchini Rwanda kwa ajili ya mchezo huo wa kirafiki, akisaidiwa na kocha Bakari Shime.

Wachezaji watakaondoka kwenda Rwanda ni Peter Manyika, Said Mohamed, Emmanuel Semwanda, Joram Mgeveke, Hassan Isihaka, Gadiel Michael, Hassan Dilunga, Rashid Mandawa, Atupele Green, Kelvin Friday, Hassan Kessy, Ibrahim Hajibu, Malimi Busungu, Mudathir Yahya, Deus Kaseke, Andre Vicent, Amri Kiemba na Mohamed Hussein.

No comments:

Post a Comment