KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Friday, June 19, 2015

MNIGERIA WA STAND UNITED ATUA COASTAL UNION


MSHAMBULIAJI wa timu ya Stand United ya Shinyanga, Abasalim Chidiebele amesaini mkataba wa mwaka mmoja kuitumikia timu ya Coastal Union ya Tanga  msimu ujao wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania bara.
Chidiebele alitua mkoani Tanga jana kwa ajili ya kuingia makubaliana na uongozi wa timu ya Coastal Union ambapo utiliaji saini huo ulishuhudiwa na viongozi mbalimbali akiwemo Katibu wa Coastal Union, Kassim El Siagi, Meneja wa Coastal Union, Akida Machai na viongozi wengine.
Akizungumza mara baada ya kusaini, Chidiebele amesema kuwa amefurahi kusajiliwa na Coastal Union na kuhaidi kutumia uwezo wake aliokuwa nao kwa ajili ya kuipa mafanikio timu hiyo msimu ujao

“Nashukuru kusajiliwa Coastal Union kikubwa niwahaidi tu wapenzi, wanachama na mashabiki kutumia uwezo wangu katika kuipa mafanikio timu yetu, “amesema Mshambuliaji huyo ambaye ni tishio hapa nchini.
Kwa upande wake, Ofisa Habari wa Klabu ya Coastal Union, Oscar Assenga alisema kuwa msimu huu timu hiyo imedhamiria kufanya usajili wa nguvu utakaowawezesha kuhakikisha wanachukua ubingwa wa Ligi kuu soka Tanzania bara.
“Unajua usajili wetu sio wa kukurupuka hivyo lazima tuwe makini kwani hiyo ndio itakuwa njia pekee ya kuhakikisha tunatimiza mipango yetu ya kuchukua Ubingwa wa Ligi kuu msimu ujao “Alisema.
Hata hivyo aliwataka wapenzi mashabiki kuweka mshikamano wa pamoja ambao utatuwezesha kufanikisha malengo yao ya mwakani kushiriki kombe la shirikisho kwa kuanza kufanya vizuri katika michuano ya Ligi Kuu.

No comments:

Post a Comment