KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, September 11, 2014

YANGA, AZAM KUWAKOSA COUTINHO NA BOCCO J'PILI


TIMU za soka za Yanga na Azam, huenda zikaingia dimbani Jumapili bila ya baadhi ya wachezaji wake nyota.

Yanga na Azam zinatarajiwa kushuka dimbani Jumapili katika mechi ya kuwania Ngao ya Jamii, itakayopigwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Habari kutoka ndani ya Yanga zimeeleza kuwa, timu hiyo itamkosa mshambuliaji wake mahiri, Andrey Coutinho, ambaye ni majeruhi.

Mbrazil huyo aliumia wakati Yanga ilipocheza mechi ya kirafiki juzi dhidi ya Polisi Dar es Salaam kwenye uwanja wa sekondari ya Loyola.

Mshambuliaji huyo alipatwa na maumivu hayo wakati alipokuwa akijaribu kupiga mpira na hivyo kushindwa kuendelea na mchezo. Timu hizo zilitoka suluhu.

Kwa mujibu wa habari za uhakika, Mbrazil huyo huenda akakaa nje ya uwanja kwa zaidi ya mwezi mmoja. Yanga itatoa taarifa rasmi leo baada ya mchezaji huyo kufanyiwa vipimo.

Coutinho amekuwa kivutio kikubwa kwa mashabiki wa Yanga kutokana na staili yake ya uchezaji, aliyoionyesha katika mechi kadhaa za kirafiki alizocheza hadi sasa.

Wakati huo huo, mshambuliaji nyota wa Azam, John Bocco naye ataikosa mechi hiyo kutokana na kusumbuliwa na maumivu ya misuli.

Habari kutoka ndani ya Azam zimeeleza kuwa, mshambuliaji huyo atakuwa nje ya uwanja kwa wiki tatu.
Meneja wa Azam FC, Jemadari Said, amesema Bocco aliyeumia kwenye michuano ya Kombe la Kagame mwezi uliopita mjini Kigali, Rwanda baada ya kufanyiwa vipimo, ametakiwa kupumzika ili kupona vizuri.
“Tunao majeruhi wawili, ambao hawatakuwepo kwenye programu ya mchezo wa Ngao ya Jamii, ambao ni beki Waziri Salum na nahodha wetu, John Bocco,”alisema Jemedari.

No comments:

Post a Comment