KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Monday, September 8, 2014

TFF YARUDISHA LIGI DARAJA LA PILI


Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) iliyokutana hivi karibuni imekubali mapendekezo ya Kamati ya Mashindano ya kurejesha michuano ya Ligi Daraja la Pili (SDL).

Lengo la kurejesha ligi hiyo ni kuongeza wigo wa mashindano kitaifa ambapo itasaidia kushirikisha kundi kubwa zaidi la wachezaji kwenye mashindano makini yanayozingatia viwango na vigezo ili kuwapa wachezaji maendeleo ya kiuchezaji ikiwemo kuendelezwa vipaji vyao kitaalamu.

Ligi hiyo yenye timu 24 itachezwa katika hatua ya makundi manne ya timu sita sita kwa mtindo wa nyumbani na ugenini ambapo mshindi wa kila kundi atapanda kucheza Ligi Daraja la Kwanza (FDL). Timu ya mwisho kila kundi itarudi kwenye ligi ya mkoa wake.

Hatua ya pili ni kutafuta bingwa wa SDL ambapo timu zilizoongoza makundi (nne) zitacheza kwa mtoano nyumbani na ugenini. Utakuwepo mchezo wa fainali ambapo mshindi atkuwa bingwa wa SDL msimu wa 2014/2015.

Timu zitakazocheza SDL kwa msimu huu ni zile zilizoshika nafasi ya pili hadi ya nane katika Ligi ya Mabingwa wa Mikoa (RCL) katika makundi yao msimu uliopita, na tatu zilizoshuka kutoka FDL msimu uliopita.

Kundi A litakuwa na timu za Milambo FC (Tabora), Mji Mkuu FC (Dodoma), Mpanda United (Mpanda), Mvuvumwa FC (Kigoma), Singida United (Singida) na Ujenzi (Rukwa). Kundi B ni Arusha FC (Arusha), Bulyanhulu FC (Shinyanga), Eleven Stars (Kagera), Mbao FC (Mwanza), Pamba FC (Mwanza) na Rwamukoma JKT (Mara).

Timu za kundi C ni Abajalo (Dar es Salaam), Kiluvya United (Pwani), Kariakoo FC (Lindi), Mshikamano FC (Dar es Salaam), Navy FC (Dar es Salaam) na Transit Camp (Dar es Salaam). Kundi D ni Magereza FC (Iringa), Mkamba Rangers (Morogoro), Njombe Mji (Njombe), Town Small Boys (Ruvuma), Volcano FC (Morogoro) na Wenda FC (Mbeya).

Ligi itachezwa kuanzia Novemba mwaka huu.

MBUNGE MTANDA KUFUNGA KOZI YA LESENI A
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Huduma za Jamii, Mheshimiwa Said Mtanda anatarajia kufunga kozi ya ukocha ya Leseni A ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) inayomalizika kesho (Septemba 7 mwaka huu).

Hafla hiyo ya ufungaji wa kozi hiyo iliyoshirikisha makocha 22 itafanyika saa 7 mchana kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, jijini Dar es Salaam.

Kozi hiyo ya siku tano iliyokuwa chini ya wakunzi wa CAF, Moatasim Mohamed Nasr kutoka Sudan na Sunday Kayuni wa Tanzania.

KOZI YA UKUFUNZI WA UTAWALA YA FIFA KUFANYIKA DESEMBA
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kwa kushirikiana na Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) wameandaa kozi ya ukufunzi wa utawala itakayofanyika Desemba mwaka huu.

Kozi hiyo itakayoendeshwa na wakufunzi kutoka FIFA itafanyika jijini Dar es Salaam kuanzia Desemba 1 hadi 5 mwaka huu, ambapo sifa ya chini ya elimu kwa wanaotaka kushiriki ni kidato cha nne.

Kwa wanaotaka kushiriki kozi hiyo wanatakiwa kutuma maombi yao kwa Katibu Mkuu wa TFF. Mwisho wa kupokea maombi hayo ni Septemba 12 mwaka huu ambapo wanatakiwa pia kuwasilisha nakala za vyeti vyao vya kitaaluma.

FDL KUCHEZWA MAKUNDI MAWILI
Ligi Daraja la Kwanza (FDL) msimu wa 2014/2015 itachezwa katika makundi mawili kwa mtindo wa nyumbani na ugenini kuanzia Oktoba 11 mwaka huu.

Kundi A lina timu za African Lyon, African Sports, Ashanti United, Friends Rangers, Kimondo SC, Kurugenzi Mafinga, Lipuli, Majimaji, Mlale JKT, Polisi Dar es Salaam, Tessema FC na Villa Squad.

Wakati kundi B lina timu za Burkina Faso, Geita Veterans SC, Green Warriors, Kanembwa JKT, Mwadui SC, Oljoro JKT, Panone FC, Polisi Dodoma, Polisi Mara, Polisi Tabora, Rhino Rangers na Toto Africans.

No comments:

Post a Comment