KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, September 25, 2014

SSB KUDHAMINI TUZO ZA TASWA KWA MIL 10/-




TUZO za Wanamichezo Bora wa Tanzania zinazotolewa na Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA) zinatarajiwa kufanyika Desemba 12 mwaka huu, huku Kampuni ya Said Salim Bakhresa (SSB) Group Limited ikijitokeza kuwa mdhamini mshiriki wa tuzo hizo kwa kutoa Sh. Milioni 10.

Akizungumza na waandishi wa habari katika mgahawa wa City Sports Lounge, Dar es Salaam katika hafla ya kutangaza udhamini huo jana, Meneja Mkuu wa SSB Limited, Said Muhammad Said alisema wameamua kudhamini tuzo hizo kama hatua mojawapo ya kuinua michezo nchini.

Aliupongeza uongozi wa TASWA kwa juhudi kubwa inazofanya katika kuhamasisha michezo na kwamba wameona waunge mkono juhudi hizo kwa kutoa fedha hizo.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa TASWA, Juma Pinto alisema kampuni mbalimbali zimeonesha nia ya kudhamini tuzo hizo na watakuwa wanazitangaza kadri watakavyomalizana nazo.

“Tunaishuku sana Bakhressa kwa mchango huu mkubwa kwetu, pia tunaomba wadau tushirikiane kwa kila hali kuhakikisha tuzo zetu zinafanikiwa na tunaomba kampuni zaidi zijitokeze.

“Bajeti ya tuzo zetu ni Sh milioni 120, zipo kampuni zimeonesha nia ya kutusaidia, mwishoni mwa wiki hii au mwanzoni mwa wiki ijayo tutatangaza wadhamini wengine,” alisema Pinto.

Naye Katibu Mkuu wa TASWA, Amir Mhando alisema Kamati Maalum ya Tuzo hizo inaendelea na mchakato wake wa kupata wanamichezo hao na kwamba kadri watakavyokuwa wanapiga hatua watatoa taarifa kwa wanahabari.

Alisema maandalizi mengine yanaenda vizuri na wanaamini zitakuwa tuzo bora kuliko zote zilizowahi kufanywa na chama hicho katika miaka ya hivi karibuni.

Kwa miaka mitano iliyopita walioshinda Tuzo ya Mwanamichezo Bora wa TASWA walikuwa ni Samson Ramadhani (2006), Martin Sulle (2007), Mary Naali (2008), ambao wote ni wanariadha, wakati 2009 na 2010 alikuwa mcheza netiboli Mwanaidi Hassan na mwaka 2011 alikuwa beki Shomari Kapombe ambaye sherehe za kumkabidhi tuzo zilifanyika Juni mwaka 2012. Mwaka jana tuzo hizo hazikufanyika.

Wakati huohuo, Mhando alisema chama chake kinaendelea na mazungumzo na wadhamini mbalimbali kuhusiana na tamasha kwa ajili ya vyombo vya habari ‘Media Day Bonanza’ na kwamba mapema mwezi ujao suala hilo litakuwa limemalizika.

No comments:

Post a Comment