KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Sunday, September 21, 2014

KATIBU MKUU COASTAL UNION KITANZINI


Katibu Mkuu wa Coastal Union, Kassim El Siagi atafikishwa kwenye Kamati ya Maadili ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kwa kushinikiza mkutano wa wanachama wa klabu hiyo ufanyike bila kuandaliwa na Kamati ya Utendaji.

Pia El Siagi alitumia vyombo vya habari kuishambulia TFF ambayo haikutambua uamuzi wa mkutano huo ulioelezwa kumdumaza Makamu Mwenyekiti wa klabu hiyo Steven Mnguto.

TFF ilimtuma Mkurugenzi wake Msaidizi wa Sheria na Uanachama kufanya uchunguzi wa mgogoro uliokuwa unaendelea katika klabu hiyo.

Baada ya kupokea taarifa ya uchunguzi huo, TFF imebaini kuwa Mwenyekiti na Mweka Hazina wa klabu hiyo walishajiuzulu, hivyo uitishwe uchaguzi haraka na kujaza nafasi hizo na nyingine zilizo wazi.

Pia wajumbe wa Kamati ya Utendaji ya Coastal Union, Salim Amir na Albert Peter wameonywa kwa kushiriki katika mkutano ambao wanajua haukuandaliwa na Kamati ya Utendaji.

Vilevile uchunguzi wa TFF umebaini kuwa ushiriki wa Salim Bawazir na Akida Machai kwenye vikao vya Kamati ya Utendaji ya Coastal Union si halali kwa vile wajumbe wa kamati hiyo wanachaguliwa na Mkutano Mkuu na si kuteuliwa na Mwenyekiti.

Kwa vile kutakuwa na uchaguzi wa kujaza nafasi ambazo zipo wazi, uchaguzi huo utasimamiwa na Kamati ya Uchaguzi ya Coastal Union kwa kushirikiana na Kamati ya Uchaguzi ya TFF, na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Tanga na Coastal Union watafanya uhakiki wa reja ya wanachama.

No comments:

Post a Comment