KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, September 25, 2014

SIMBA YAPATA PIGO, IVO MAPUNDA AVUNJIKA KIDOLE, KUIKOSA YANGA OKTOBA 12


Zikiwa zimebakia wiki mbili kabla ya kukutana na mahasimu wao wa jadi, Simba imepata pigo kubwa katika timu kwa sababu kipa namba moja wa timu hiyo Ivo Mapunda amevunjika kidole mazoezini Zanzibar jana asubuhi na anatakiwa kuwa nje ya uwanja kwa wiki nane.


Hatoweza kusimama golini wakati tiu yake ikicheza na Yanga October 12 2014 ambapo daktari wa Simba SC Yassin Gembe amesema Ivo aliumia wakati anachupia mpira katika mazoezi ya asubuhi na kwa bahati mbaya mpira ukamgonga kwenye kidole kidogo cha mwisho mkono wa kulia.

Gembe amesema Ivo alitoka mazoezini baada ya tukio hilo na baadaye akapelekwa hospitali ya Mnazi Mmoja kisiwani humo ambako baada ya vipimo ikagundulika amevunjika sana.

“Si kuvunjika kwa mzaha, amevunjika sana na anatakiwa kupumzika kwa wiki nane, baada ya hapo aanze taratibu… ina maana makadirio ya kurudi tena uwanjani ni hadi baada ya miezi mitatu‘ – Gembe.

Kuumia kwa Ivo kunatoa nafasi kwa makipa chipukizi Hussein Sharrif ‘Cassilas’ na Peter Manyika kujibidiisha ili kuziba pengo lake ambapo sasa Ivo anafanya idadi ya wachezaji majeruhi ambao ni tegemeo Simba kufikia wanne baada ya Paul Kiongera anayetakiwa kuwa nje wiki sita, Haroun Chanongo na Issa Rashid ‘Baba Ubaya’.

NYOTA WATANO WA KIGENI SIMBA WAPIGWA MARUFUKU KUCHEZA LIGI KUU, HAWANA VIBALI VYA KUFANYAKAZI, HATARINI KUIKOSA YANGA OKTOBA 12




Mshambuliaji wa Simba raia wa Uganda, Emmanuel Okwi na wenzake wanne wanaweza kuwa wameiingiza klabu hiyo kwenye mgogoro mkubwa; hawana kibali cha kufanya kazi nchinilicha ya kutumiwa kwenye mechi za ufunguzi wa Ligi Kuu mwishoni mwa wiki.

Idara ya Uhamiaji ilisema jana kuwa Okwi, Joseph Owino, Pierre Kwizera, Amis Tambwe na Raphael Kiongera hawana kibali cha kufanya kazi nchini, ambacho ni moja ya masharti makubwa ya kupata leseni ya kusakata soka.

Mbali na wachezaji hao, kocha Patrick Phiri pia haruhusiwi kukaa kwenye benchi la ufundi kwa kuwa naye hana kibali cha kufanya kazi nchini.

Akizungumza na gazeti hili jana, naibu kamishna wa Uhamiaji ambaye pia ni msemaji wa Idara hiyo, Abbas Mussa Irovya alisema nyota hao wa kigeni wa Simba hawaruhusiwi kuingia uwanjani wala kufanya mazoezi mahali popote hapa nchini na watakapoonekana wakifanya kazi kuanzia leo, watakamatwa.

“Tayari idara imemuagiza Ofisa Uhamiaji wa Mkoa wa Dar es Salaam kuwakamata kuanzia kesho (leo) endapo wataonekana uwanjani aidha kwenye mechi au kwenye mazoezi na sheria itachukua mkondo wake,” alisema Irovya.

“Hatujapokea ombi lolote la klabu ya Simba kumuombea kibali mchezaji wala kocha wao wa kigeni ili afanye kazi hapa nchini na uwepo wao katika majukumu ya mazoezi au mechi ni kinyume cha sheria,” aliongeza msemaji huyo na kueleza kushangazwa na kitendo cha TFF kuwaachia waendelee kucheza wakati ikijua fika kuwa hawana kibali.

Okwi alikuwa na kibali cha kufanya kazi nchini alichoombewa na Yanga mwaka jana na baada ya kuidhinishwa Simba, klabu hiyo inatakiwa kumuombea kibali kipya.

“Tunamtambua Okwi kama muajiriwa wa klabu ya Yanga kwa kuwa ana kibali cha kufanya kazi hapa nchini chenye namba 1027397 kinachokwisha Machi 3, 2016 kilichoombwa na Yanga na siyo Simba alipo sasa,” alisema.

“Inachokifanya Simba ni kinyume cha sheria za nchi na za Idara ya Uhamiaji... kumwajiri mtu ambaye ana kibali cha kufanya kazi Yanga bila kutoa taarifa uhamiaji ni kukiuka taarifa za uhamiaji.”

Kwa mujibu wa kifungu cha 43 cha Kanuni za Ligi, mchezaji hawezi kupewa leseni ya kucheza soka nchini hadi atimize masharti mawili; kufanikiwa katika vipimo vya afya na kuwa na kibali cha kufanya kazi.

Alipoulizwa kuhusu suala hilo, kaimu katibu mkuu wa TFF, Boniface Wambura alijibu: “Wewe umeongea na Simba, wanasemaje?” na baadaye kumtaka mwandishi kuwasiliana na katibu mkuu wa TFF, Celestine Mwesigwa ambaye hakupatikana.

Kwa mujibu wa Irovya, Yanga ilishapeleka maombi ya vibali vya wachezaji wake kutoka Brazil, Genilson Santos ‘Jaja’ na Andrey Coutinho na makocha wao wawili kutoka nchi hiyo pia, Marcio Maximo na Leonardo Neiva na wako kwenye utaratibu wa kupata vibali hivyo

KATIBA MPYA KUWATAMBUA WASANII


 Msanii wa filamu nchini Tanzania maarufu kama Mzee Chilo akiwa katika picha ya pamoja na mjumbe wa Bunge Maalum la Katiba, Angellah Kairuki jana katika viwanja vya Bunge mjini Dodoma.
 Kiongozi wa msafara wa wasanii waliofika katika Bunge Maalumu la Katiba,Simon Mwakifwamba akiwa katika picha ya pamoja na mjumbe wa bunge hilo, Angellah Kairuki katika viwanja vya Bunge mjini Dodoma.
Baadhi ya Wasanii wakijadiliana jambo mara baada ya kutoka nje ya Bunge Maalumu la Katiba jana mjini Dodoma.
 Baadhi ya wasanii wakimsikiliza kwa makini Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo ambaye pia ni mjumbe wa Bunge Maalum la Katiba, Fenella Mukangara (wa pili toka kushoto) wakati alipokutana nao maeneo ya viwanja vya bunge hilo.
 Wasanii wakiendelea kumsikiliza Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo ambaye pia ni mjumbe wa Bunge Maalum la Katiba, Fenella Mukangara wakati alipokutana nao maeneo ya viwanja vya bunge hilo jana mjini Dodoma.
Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo ambaye pia ni mjumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, Fenella Mukangara akiwa katika picha ya pamoja na wasanii maeneo ya viwanja vya bunge hilo jana mjini Dodoma.


Na Happiness Mtweve, Dodoma

HATIMAYE Bunge Maalumu la Katiba, limeridhia mapendekezo ya kuboresha Rasimu kuhusu kuanzishwa kwa Ibara mpya inayohusu uhuru wa taaluma, ubunifu na ugunduzi.

Akiwasilisha Rasimu ya Katiba Mpya iliyopendekezwa na Bunge hilo mjini hapa jana, Mwenyekiti wa Kamati ya Uandishi, Andrew Chenge, alisema hayo ni moja ya mapendekezo kutoka makundi mbalimbali yaliyoridhiwa.

“Kamati ya Uandishi, imekubaliana na pendekezo hilo na imeanzisha Ibara mpya ya 48 A inayohusu uhuru wa taaluma, ubunifu na ugunduzi ili kutoa fursa ya mtu kujifunza, kufundisha, kutafiti na kueneza matumizi ya matokeo ya utafiti kulingana na kanuni za kitaaluma na za kiutafiti,” alisema Chenge.

Aidha, alisema serikali imepewa mamlaka ya kulinda hakimiliki za ugunduzi na ubunifu, ikiwa ni pamoja na haki za wabunifu na watafiti nchini kwa manufaa ya Taifa.

Mwenyekiti huyo pia alisema Kamati ya Uandishi imependekeza kuongezwa kwa aya mpya ya (f) inayoweka masharti kwa serikali kukuza na kuendeleza utafiti inayoeleza: “Mambo mengine yanayohusu ubunifu, ugunduzi na utafiti.”

Hatua hiyo ni mwanzo wa mafanikio kwa wasanii wa fani mbalimbali nchini, ambapo sasa wataweza kunufaika kutokana na kulindwa na kutambulika kwa kazi zao.

Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Singida, Martha Mlata, akizungumza nje ya ukumbi wa Bunge jana, alieleza kufurahishwa na Katiba Inayopendekezwa, kuwatambua wasanii kwa kuwa kilikuwa kilio chake cha muda mrefu ndani na nje ya Bunge.

Alisema kwa muda mrefu wasanii nchini wamekuwa wakipambana kufanya kazi kwa ajili ya kuinuka kiuchumi, lakini wamekuwa wakikwamishwa kutokana na kunyonywa, hivyo kutopata kile wanachostahili, jambo ambalo kwa sasa limeangaliwa kwa umakini.

"Nimefarijika mno kuwepo kwa mapendekezo ya kutambua wasanii na kazi zao za sanaa...ni muda mrefu sana nimekuwa nikililia hili kwa manufaa ya wasanii wote nchini. Nawaomba wasanii waungane kuhakikisha wanatetea na kuipigia kura katiba hii ili kuhakikisha inapita," alisema Martha, ambaye amekuwa mstari wa mbele kutetea haki za wasanii nchini.

SSB KUDHAMINI TUZO ZA TASWA KWA MIL 10/-




TUZO za Wanamichezo Bora wa Tanzania zinazotolewa na Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA) zinatarajiwa kufanyika Desemba 12 mwaka huu, huku Kampuni ya Said Salim Bakhresa (SSB) Group Limited ikijitokeza kuwa mdhamini mshiriki wa tuzo hizo kwa kutoa Sh. Milioni 10.

Akizungumza na waandishi wa habari katika mgahawa wa City Sports Lounge, Dar es Salaam katika hafla ya kutangaza udhamini huo jana, Meneja Mkuu wa SSB Limited, Said Muhammad Said alisema wameamua kudhamini tuzo hizo kama hatua mojawapo ya kuinua michezo nchini.

Aliupongeza uongozi wa TASWA kwa juhudi kubwa inazofanya katika kuhamasisha michezo na kwamba wameona waunge mkono juhudi hizo kwa kutoa fedha hizo.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa TASWA, Juma Pinto alisema kampuni mbalimbali zimeonesha nia ya kudhamini tuzo hizo na watakuwa wanazitangaza kadri watakavyomalizana nazo.

“Tunaishuku sana Bakhressa kwa mchango huu mkubwa kwetu, pia tunaomba wadau tushirikiane kwa kila hali kuhakikisha tuzo zetu zinafanikiwa na tunaomba kampuni zaidi zijitokeze.

“Bajeti ya tuzo zetu ni Sh milioni 120, zipo kampuni zimeonesha nia ya kutusaidia, mwishoni mwa wiki hii au mwanzoni mwa wiki ijayo tutatangaza wadhamini wengine,” alisema Pinto.

Naye Katibu Mkuu wa TASWA, Amir Mhando alisema Kamati Maalum ya Tuzo hizo inaendelea na mchakato wake wa kupata wanamichezo hao na kwamba kadri watakavyokuwa wanapiga hatua watatoa taarifa kwa wanahabari.

Alisema maandalizi mengine yanaenda vizuri na wanaamini zitakuwa tuzo bora kuliko zote zilizowahi kufanywa na chama hicho katika miaka ya hivi karibuni.

Kwa miaka mitano iliyopita walioshinda Tuzo ya Mwanamichezo Bora wa TASWA walikuwa ni Samson Ramadhani (2006), Martin Sulle (2007), Mary Naali (2008), ambao wote ni wanariadha, wakati 2009 na 2010 alikuwa mcheza netiboli Mwanaidi Hassan na mwaka 2011 alikuwa beki Shomari Kapombe ambaye sherehe za kumkabidhi tuzo zilifanyika Juni mwaka 2012. Mwaka jana tuzo hizo hazikufanyika.

Wakati huohuo, Mhando alisema chama chake kinaendelea na mazungumzo na wadhamini mbalimbali kuhusiana na tamasha kwa ajili ya vyombo vya habari ‘Media Day Bonanza’ na kwamba mapema mwezi ujao suala hilo litakuwa limemalizika.

Tuesday, September 23, 2014

MREMBO MWENYE KIPAJI ASAKWA MANYARA


Warembo 15 kati ya 30 wanaoshiriki shindano la Redds Miss Tanzania 2014
wakisindikizwa na mkali wa Bongo Fleva kutoka Jijini Dar es Salaam,
Tunda Man, wametoa burudani kali wakati wa shindano dogo la awali la
kumtafuta mrembo mwenye kipaji lililofanyika Babati Mkoani Manyara.  



WASANII WASISITIZWA MATUMIZI SAHIHI YA MITANDAO




 Afisa Habari wa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) Aristides Kwizela (Kulia) akisisitiza jambo kwa Wasanii (Hawako pichani) wakati wa Jukwaa la Sanaa lililofanyika mapema wiki kwenye Ukumbi wa Baraza hilo ulioko Ilala, Sharif Shamba jijini Dar es Salaam. Katikati ni mdau wa Sanaa, Henry Mdimu na Afisa Sanaa wa Baraza hilo, Augustino Makame.

WASANII nchini wamesisitizwa juu ya matumizi sahihi ya mitandao ya kijamii kwani waandaaji wa matamasha na matukio mbalimbali ya kisanaa sehemu mbalimbali duniani wamekuwa wakiitumia katika kuwapa kazi.

Akizungumza kwenye Jukwaa la Sanaa lililofanyika mapema wiki hii kwenye Ukumbi wa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) ulioko Ilala Sharif Shamba jijini Dar es Salaam, mdau wa Sanaa Henry Mdimu alisema kuwa ni jambo la kushangaza kuona wasanii wakitumia kurasa zao kuonesha mambo binafsi kama ya mapenzi na matusi wakati zinapaswa kutumika kwa ajili ya kazi zao za Sanaa na kuwasiliana na mashabiki wao.

Alisisitiza kwamba si kila kitu kinapaswa kuwekwa kwenye kurasa za kijamii za wasanii na kwamba lazima wasanii wajifunze kutenganisha maslahi au masuala yao binafsi dhidi ya yale ya wapenzi wao na kwamba Sanaa iko kwa ajili ya walaji na si wasanii pekee.

“Wasanii hawana budi kuelewa kuwa hawatengenezi sanaa au kurasa za mitandao ya kijamii kwa ajili yao. Wanaitengeneza ili kuwasiliana na mashabiki wao kuhusu kazi wazifanyazo na kutafuta fursa za masoko na kazi nje. Lazima waelewe mapromota wa kimataifa hutumia sana kurasa hizi katika kutoa fursa” alisisitiza Mdimu.

Aliongeza kwamba, msanii yeyote anayefanya kazi ya Sanaa kama kazi yake lazima afikirie kutumia mitandao hii ya kijamii kiweledi katika kujitangaza kwani kutokufanya hivyo ni bora kufanya kazi nyingine maana hiyo ndiyo njia kuu kwa sasa ya kujitangaza na kupata fursa za maonesho mbalimbali ya kimataifa kwa gharama nafuu.

Kwa upande wake Afisa Sanaa kutoka BASATA, Augustino Makame alisema kwamba Baraza limekuwa mstari wa mbele kusisitiza matumizi sahihi ya teknolojia za kupashana habari muiongoni mwa wasanii na kwamba sasa ni muda wa wasanii kuona umuhimu wa mitandao hii ya kijamii na kuitumia ipasavyo katika kukuza Sanaa zao.

TASWA KUTETA NA WANAHABARI KESHO



Habari mdau, naomba kukujulisha kuwa kesho Jumatano Septemba 24, 2014, saa tano kamili asubuhi, Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA), Juma Pinto, akiambatana na wadhamini washiriki wa Tuzo za Wanamichezo Bora Tanzania zinazoandaliwa na TASWA, watakuwa na mkutano na waandishi wa habari kwenye mgahawa wa City Sports Lounge, Posta, Dar es Salaam kutangaza udhamini huo.


Pia katika mkutano huo, masuala ya Media Day Bonanza 2014 na mambo yahusiyo mafunzo kwa waandishi wa habari za michezo nayo yatazungumzwa.

Naomba ukipata taarifa hii, mjulishe na mwenzako. Karibu sana.

Ahsante,
Katibu Mkuu TASWA
0713-415346

MAKONGORO AIPA CHANGAMOTO TaSUBA


Mgeni rasmi ambaye, pia ni Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki, Makongoro Nyerere (kushoto) akifuatilia maonyesho mbalimbali yaliyokua yakiendelea wakati wa uzinduzi wa Tamasha la 33 la Sanaa lililofanyika katika Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa) jana. Katikati ni Mtendaji Mkuu TaSUBa, Michael Kadinde na kulia ni Mkurugenzi Maendeleo ya Utamaduni, Prof. Hermas Mwansoko.


 Mgeni rasmi ambaye ni Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki,  Makongoro Nyerere akipiga ngoma kama ishara ya uzinduzi wa Tamasha la 33 la Sanaa lililofanyika katika Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa) jana.

 Makongoro (kulia) akipokea zawadi ya picha kutoka kwa Mwenyekiti wa Bodi ya TaSUBa,
Ghonche Materego wakati wa uzinduzi wa Tamasha la 33 la Sanaa lililofanyika katika Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa) jana. Picha hii imechorwa sura ya Makongoro na msanii aliyefahamika kwa jina la Sunday Richard Kamangu.
Makongoro (kushoto) akimpa mkono wa pongezi msanii Sunday Richard Kamangu baada ya kupokea zawadi ya picha iliyochorwa na msanii huyowakati wa uzinduzi wa Tamasha la 33 la Sanaa lililofanyika katika Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa) jana.
Katibu Mtendaji Bodi ya Filamu, Joyce Fisoo (kushoto) na Mkurugenzi Msaidizi Sanaa, Leah Kihimbi wakifuatilia matukio mbalimbali yaliyokuwa yanaendelea wakati wa uzinduzi wa Tamasha la 33 la Sanaa lililofanyika katika Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa) jana.

Wasanii kutoka Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo wakitoa burudani wakati wa uzinduzi wa Tamasha la 33 la Sanaa lililofanyika katika Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa) jana.

Baadhi ya watazamaji wakifurahia mambo yalivyokuwa wakati wa uzinduzi wa Tamasha la 33 la Sanaa lililofanyika katika Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa) jana. Picha zote na: Genofeva Matemu - MAELEZO

Benjamin Sawe, Bagamoyo

TAASISI ya Sanaa Bagamoyo imeaswa kuendelea kutoa mafunzo ya sanaa na utamaduni ambayo yatakidhi mahitaji ya soko kwa nchi za Afrika Mashariki.

Hayo yamesemwa na Makongoro Nyerere kwa niaba ya Spika wa Bunge la Afrika Mashariki, Margaret Ntantongo Zziwa katika Ufunguzi wa Tamasha la 33 la sanaa na utamaduni wa Mtanzania lililofanyika katika Taasisi hiyo mjini Bagamoyo jana

Makongoro alisema Sanaa na Utamaduni vinaweza kutumiwa kuelezea masuala yote yanayomuhusu binadamu na mazingira yake hususani suala zima la utaliii

Alisema ni wakati mwafaka kwa jamii kuondokana na dhana ya kuona watalii ni wale wa kutoka nje ya nchi na kusahau kuwa wale wa ndani ambao kwa idadi kubwa ni wengi wa kuwezesha Serikali kukusanya maduhuli ya kutosha.

Kwa upande wake, Kaimu Mtendaji Mkuu wa TaSUBa Bw. Michael Kadinde alisema sanaa hutumika kuelimisha jamii katika masuala mbalimbali ikiwa ni pamoja na Utawala Bora, kuhifadhi mazingira, madahara ya rushwa katika jamii, namna ya kujikinga na maambukizi ya virusi vya Ukimwi na aina nyingine nyingi za utoaji elimu katika jamii.

Alitolea mfano wa sanaa ya ngoma, nyimbo, hadidhi simulizi, majigambo, uchoraji na sanaa nyingine nyingi za makabila mbalimbali vinaeleza utamaduni wa Mtanzania hivyo huwa kitambulisho cha jamii.

Kadinde alisema sanaa huonya na kutaadhalisha jamii juu ya mambo mabaya yanayoweza kuleta madahara katika jamii ikiwa ni pamoja na kuendekeza rushwa, Vijana au jamii nzima kuwa na tabia zisizokuwa na heshima .

Aliomba Bodi ya Utalii ya Tanzania mahali palipo na vituo vya Utalii viwatumie wahitimu wa TaSUBa kuanzisha vikundi vya sanaa ili watangaze utalii wa nchi ili na kuongeza mapato ya nchi na jamii kwa ujumla

Alisema kutoa mafunzo ya Sanaa na Utamaduni kwa nchi za Afrika Mashariki kuna changamoto zake ikiwa ni pamoja na upanuzi wa miundombinu ili kukidhi mahitaji ya ufundishaji ambapo iliyopo haiwezi kubeba mzigo mzito wa kutoa mafunzo kwa wanafunzi wa nchi za Afrika Mashariki.

Tamasha la Sanaa Bagamoyo lilianzishwa mwaka 1982 ambapo mwaka huu kauli mbiu yake ni “Sanaa na Utamaduni katika kukuza utalii”.

Monday, September 22, 2014

LAVEDA; MWAKILISHI WA TANZANIA BIG BROTHER AFRICA 2014


Tanzania
Laveda
Age: 23

Bachelor of Arts & Social Sciences graduate Laveda was born in Dar Es Salaam. She’s single and describes herself as ‘eccentric, loving, caring, simple and fun’. Laveda is the eldest of three children and she has a younger brother and sister. She says her mom is her role model, because she has moulded her over the years and inspired her in different ways ‘through the struggles and joy of life’.

Laveda says her favourite foods are pasta and minced meat, and prawns. She loves to read John Grisham novels and enjoys the music of Shakira, D’Banj, Miriam Makeba, P.Square, Rihanna, Beyonce, Tiwo Savage, Yvonne Chaka Chaka and Brenda Fassie. She’s a mean entertainer herself, she plays the saxophone, sings, acts and dances and thinks she’d make a ‘potential’ presenter. Laveda’s favourite movies include The Notebook, Titanic and Avatar.

She entered Big Brother Hotshots to be a role model and act as a voice for Africa’s youth. Laveda says that viewers can expect ‘massive entertainment’ from her and that if she wins, she’ll give her mom some money, ‘surprise disadvantaged children’, travel and invest the rest.

LIEWIG ATEULIWA KUWA KOCHA WA VIJANA AZAM




MFARANSA Patrick Liewig anatarajiwa kuchukua nafasi ya Mhindi, Vivek Nagul aliyeachia ngazi katika akademi ya Azam FC ya Dar es Salaam.


Katibu wa Azam FC, Nassor Idrissa Mohamed ‘Father’ amesema kwamba klabu hiyo imefikia makubaliano na Liewig, ambaye kwa sasa yupo Ufaransa na atakuja nchini mara moja kusaini Mkataba.

Nassor amesema klabu inatarajia makubwa kutoka kwa Mfaransa huyo aliyewahi kufanya kazi ASEC Mimosas ya Ivory Coast kwa mafanikio.

Amesema Vivek aliomba kuachia ngazi baada ya kupata kazi Chennayin FC ya Ligi Kuu ya kwao India, ambako anakwenda kuwa chini ya kocha Mkuu, Mbrazil, Zico na wachezaji maarufu kama Robert Pires, Edgar Marcelieno na Migeul Herlin.

Vivek alijiunga na Azam FC mwaka 2011 na katika kipindi hicho cha miaka mitatu na ushei, pamoja na kuzalisha vipaji vingi, pia ameiwezesha Akademi kushinda Kombe la Uhai mara mbili na Rollinstone mara moja

“Tunamtakia kila la kheri na ataendelea kuwa kwenye kumbukumbu zetu baada ya kuipa akademi mafanikio makubwa sana. Kazalisha nyota wengi ambao wamejaa timu zote za Ligi Kuu,” amesema Father.

Nassor amewataja baadhi ya wachezaji hao kuwa ni
Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ wa Simba SC, Simon Msuva wa Yanga SC, wakati Azam A wapo
Manula Aishi, Gardiel Michael, Bryson Raphael, Mudathir Yahya, Kevin Friday, Farid Mussa Malik,
Joseph Kimwaga, Dizana issa na Mgaya Abdul.

KUHUSU LIEWIG;
Nassor amesema kwamba klabu imeridhishwa na falsafa ya ufundishaji ya Mfaransa huyo baada ya kumuona akifanya kazi Simba SC mwaka jana, hivyo kuamua kumchukua ahamishie mafanikio yake Chamazi.

Liewig ana Stashahada ya Juu ya ukocha na Shahada ya tatu ya ualimu wa soka ya vijana aliyotunukiwa na Mkurugenzi wa Ufundi wa Ufaransa, Gerard Houiller na amehudhuria pia kozi za ufundishaji mazoezi ya viungo Juni mwaka 1999 katika Chuo Kikuu cha Dijon.

Kwa upande wa uzoefu, Liewig alifanya kazi PSG kuanzia mwaka 1989 hadi 1999 kama Kocha Mkuu wa akademi na kuna wakati alikuwa akishirikishwa pia katika programu za timu A, ingawa majukumu yake zaidi yalikuwa ni kwa Under 20, Under 18 aliowawezesha kutwaa Kombe la French Junior Gambardella na Under 16.

Kuanzia mwaka 1989 hadi 1990: alikuwa Meneja Mkuu wa Tomislav IVIC, 1990 hadi 1991 alikuwa Msaidizi wa Henri Michel, 1991 hadi 1994 alikuwa Msaidizi wa Artur Jorge, 1994 hadi 1996 alikuwa Msaidizi wa Luis Fernandez, 1996 hadi 1998: alikuwa Msaidizi wa Ricardo Gomez, 1998 hadi 1999 alikuwa Msaidizi wa Alain Giresse.

Liewig pia alifundisha Al Wahda FC ya Abu Dhabi kuanzia 1999 hadi 2001, ambayo aliipa ubingwa wa Ligi Kuu ya nchi hiyo na Kombe la Ligi.

Januari mwaka 2003 alikuwa Msimamizi wa Chama cha Soka UAE katika fainali za Afrika za U20 nchini Burkina Faso.

Kuanzia mwaka 2004 hadi 2009 alikuwa Kocha wa ASEC Mimosas ya Ivory Coast aliyoipa mataji matatu ya Ligi Kuu ya nchini humo mfululizo, 2004, 2005 na 2006, Super Cup ya nchini humo 2005, 2007, 2008 na 2009 na akaiwezesha kufuzu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa mara tatu, mara moja akiifikisha Nusu Fainali.

Amekuwa Kocha bora wa Ivory Coast miaka mitatu mfululizo, 2004, 2005 na 2006 na tangu Septemba mwaka jana hadi Juni mwaka huu, alikuwa kocha wa Club Africain ya Tunisia.

Januari mwaka jana alitua Simba SC ambako alifanya kazi hadi mwishoni mwa msimu alipoondoka kwa sababu ya matatizo ya uongozi wa klabu hiyo

Sunday, September 21, 2014

SIMBA YABANWA MBAVU NA COASTAL UNION



TIMU kongwe ya soka ya Simba jana ilitolewa jasho na Coastal Union baada ya kulazimishwa kutoka nayo sare ya mabao 2-2 katika mechi ya ligi kuu ya Tanzania Bara iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.


Simba itabidi ijilaumu kwa kushindwa kutoka uwanjani na ushindi kwani ilikuwa mbele kwa mabao 2-0 hadi mapumziko, yaliyofungwa na Shaaban Kisiga na Amisi Tambwe.

Uzembe wa mabeki wa Simba uliiruhusu Coastal Union kupata bao la kwanza dakika ya 68 lililofungwa na Yayo Lutimba kabla ya Ramadhan Salim kusawazisha dakika ya 81.

Kutokana na matokeo ya mechi za mwanzo za ligi hiyo, timu pekee iliyoibuka na ushindi mnono wa mabao ni Ndanda FC ya Mtwara, ambayo iliicharaza Stand United ya Shinyanga mabao 4-1.

YANGA YAZIMWA NA MTIBWA LIGI KUU, AZAM YACHANUA, NDANDA YAANZA KWA KISHINDO



YANGA jana ilianza vibaya kampeni ya kuwania ubingwa wa michuano ya soka ya ligi kuu ya Tanzania Bara baada ya kuchapwa mabao 2-0 na Mtibwa Sugar.

Katika mechi hiyo iliyochezwa jana kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro, mshambuliaji Genilson Jaja aliikosesha Yanga bao baada ya kupoteza penalti katika kipindi cha kwanza.

Mtibwa ilipata bao la kuongoza dakika ya 15 kupitia kwa mshambuliaji wake, Mussa Hassan 'Mgosi' baada ya kupokea pasi kutoka kwa Shaaban Nditi.

Yanga ilipata penalti dakika ya 46 baada ya Mrisho Ngasa kumnawisha mpira beki Saidi Mbonde wa Mtibwa. Hata hivyo, shuti la jaja liliokolewa kwa mguu na kipa Saidi Mohamed kabla ya mabeki wake kuuondosha kwenye hatari.

Zikiwa zimesalia dakika tano pambano hilo kumalizika, jahazi la Yanga lilizidi kuzama baada ya Ali kuifungia Mtibwa bao la pili kutokana na kazi nzuri iliyofanywa na Nditi.

Wakati huo huo, mabingwa watetezi wa ligi kuu ya Tanzania Bara, Azam jana walianza vyema kutetea taji lao baada ya kuichapa Polisi Moro mabao 3-1 kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.

Mabao yaliyoiwezesha Azam kutoka uwanjani na ushindi huo mnene yalipachikwa wavuni na Didier Kavumbagu, aliyefunga mawili na Aggrey Morris.


Katika mechi zingine za ligi hiyo zilizochezwa juzi, Ndanda FC iliibamiza Stand United mabao 4-1, Mgambo JKT iliichapa Kagera Sugar bao 1-0, Ruvu Shooting ilipigwa mweleka wa mabao 2-0 na Prisons wakati Mbeya City ilitoka suluhu na JKT Ruvu.

YANGA YATAKIWA KUWASILISHA RASIMU YA KATIBA MPYA TFF



Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limeitaka klabu ya Yanga kuwasilisha rasimu ya Katiba waliyoipitisha, kwa kuzingatia kuwa Muhtasari wa kikao cha Mkutano Mkuu wao wa Juni 1 mwaka huu umeainisha baadhi ya marekebisho waliyofanya kwa tulivyowaelekeza.

Yanga wanatakiwa kuwasilisha rasimu hiyo kabla ya Oktoba 5 mwaka huu. Ikiwa itakubaliwa na TFF, itapelekwa kwa Msajili wa Klabu na Vyama vya Michezo ili waweze kufanya uchaguzi wa viongozi wao.

KATIBU MKUU COASTAL UNION KITANZINI


Katibu Mkuu wa Coastal Union, Kassim El Siagi atafikishwa kwenye Kamati ya Maadili ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kwa kushinikiza mkutano wa wanachama wa klabu hiyo ufanyike bila kuandaliwa na Kamati ya Utendaji.

Pia El Siagi alitumia vyombo vya habari kuishambulia TFF ambayo haikutambua uamuzi wa mkutano huo ulioelezwa kumdumaza Makamu Mwenyekiti wa klabu hiyo Steven Mnguto.

TFF ilimtuma Mkurugenzi wake Msaidizi wa Sheria na Uanachama kufanya uchunguzi wa mgogoro uliokuwa unaendelea katika klabu hiyo.

Baada ya kupokea taarifa ya uchunguzi huo, TFF imebaini kuwa Mwenyekiti na Mweka Hazina wa klabu hiyo walishajiuzulu, hivyo uitishwe uchaguzi haraka na kujaza nafasi hizo na nyingine zilizo wazi.

Pia wajumbe wa Kamati ya Utendaji ya Coastal Union, Salim Amir na Albert Peter wameonywa kwa kushiriki katika mkutano ambao wanajua haukuandaliwa na Kamati ya Utendaji.

Vilevile uchunguzi wa TFF umebaini kuwa ushiriki wa Salim Bawazir na Akida Machai kwenye vikao vya Kamati ya Utendaji ya Coastal Union si halali kwa vile wajumbe wa kamati hiyo wanachaguliwa na Mkutano Mkuu na si kuteuliwa na Mwenyekiti.

Kwa vile kutakuwa na uchaguzi wa kujaza nafasi ambazo zipo wazi, uchaguzi huo utasimamiwa na Kamati ya Uchaguzi ya Coastal Union kwa kushirikiana na Kamati ya Uchaguzi ya TFF, na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Tanga na Coastal Union watafanya uhakiki wa reja ya wanachama.

TFF KUCHUNGUZA TUHUMA DHIDI YA TAIFA STARS



Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limepokea kwa masikitiko makubwa taarifa zilizoandikwa kwenye baadhi ya Vyombo vya Habari zikielezea tuhuma za hujuma kwa timu ya Taifa (Taifa Stars) katika mechi za kufuzu mashindano ya AFCON.

TFF pamoja na kutokuwa na uthibitisho wa tuhuma hizi nzito haliwezi kuzikalia kimya. Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania litateua jopo la kuchunguza tuhuma hizi.

Wanafamilia wa mpira wa miguu Tanzania (Members of TFF Family) watakaohitajika kuhojiwa na jopo hilo kwa mujibu wa Ibara ya 37 ya Kanuni za Maadili za TFF watalazimika kutoa ushirikiano. Atakayeshindwa kutoa ushirikiano atachukuliwa hatua za kimaadili.

Pia wadau wa mpira wa miguu ambao sio wanafamilia wa TFF, watakaoitwa na jopo hili wanaombwa watoe ushirikiano kwa nia ya kujenga mpira wetu.

Monday, September 15, 2014

KAMATI YA SHERIA YAPITISHA USAJILI LIGI KUU




Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji imepitisha usajili wa wachezaji wa klabu za Ligi Kuu na Ligi Daraja la Kwanza huku wenye kasoro ndogondogo klabu zao zikitakiwa kuziondoa ili waweze kupatia leseni za kucheza ligi msimu huu wa 2014/2015.

Kasoro hizo ni kufikia makubaliano na klabu ambazo wachezaji husika wametoka, kuwafanyia uhamisho (transfer) na kulipa ada za uhamisho. Kamati vilevile ilibaini wachezaji wengi hawakufanyiwa uhamisho kama kanuni za ligi hizo zinavyoelekeza.

Hivyo, klabu ambazo hazitakuwa zimeondoa kasoro hizo kwa wachezaji wao leseni zao zitazuiliwa mpaka watakapokuwa wamekamilisha kila kitu. Ni wachezaji wenye leseni tu ndiyo watakaoruhusiwa kucheza mechi za ligi.

Klabu za African Lyon, African Sports, Ashanti United, Coastal Union, Kiluvya United, Majimaji, Mji Mkuu, Polisi Dodoma, Polisi Morogoro, Red Coast na Stand United ziliwawekea pingamizi wachezaji mbalimbali kwa kutofanyiwa uhamisho.

Kuhusu Ike Bright Obina wa Nigeria aliyewekewa pingamizi na African Lyon dhidi ya Coastal Union, Kamati imezitaka klabu hizo kufikia makubaliano, na zikishindwa mchezaji huyo atabaki African Lyon.

Kamati vilevile ilijadili malalamiko ya Kocha wa zamani wa Simba, Zdravko Logarusic dhidi ya klabu hiyo, na kuzipa pande hizo mbili siku 14 kufikia muafaka juu ya malalamiko hayo, na zikishindwa ndipo zirejee tena mbele ya Kamati.

Logarusic aliyewakilishwa na mwanasheria wake Dickson Sanga anailalamikia klabu hiyo kwa kuvunja mkataba kinyume cha taratibu, hivyo kutaka Simba imlipe dola 6,000 kwa kuvunja mkataba, na pia kulipa dola 50,000 ikiwa ni fidia maalumu ya madhara yaliyotokana na uvunjwaji huo.

Sunday, September 14, 2014

YANGA YAIUA AZAM, YATWAA NGAO YA JAMII, JAJA ATUPIA MBILI




Jaja...Jaja....Jaja. Okwi wa nini tena, hatumuhitaji.

Hayo ni maneno ya wapenzi wa soka walioshuhudia mchezo wa leo kati ya Young Africans dhidi ya Azam FC baada ya mbrazil huyo kuonyesha kazi ya mshambuliaji uwanjani.


Mshambuliaji wa kimataifa kutoka nchini Brazil Geilson Santos "Jaja" leo amewaonyesha wapenzi wa soka nchini nini kazi yake uwanjani baada ya kuisadia Young Africans kuibuka na ushindi wa mabao 3-0 huku yeye akikwamisha mabao mawili safi mchezo uliofanyika katika dimba la Uwanja wa Taifa jijni Dar es salaam.

Young Africans ambayo ilikua ikicheza mchezo wa Ngao ya Jamii mbele ya mashabiki wake zaidi ya elfu thelathini waliofurika kuwapa morali wachezaji, walitulia na kucheza soka tangu mwanzo wa mchezo mpaka mwisho.

Kocha Mbrazil alianza na mfumo wa 4-5-1 walinzi Juma Abdul Oscar Joshua, Kelvin Yondani na Nadri Haroub "Canavvaro", mbele yao wakicheza viungo wa Ulinzi Mbuyu Twite na Said Juma "Makapu" wakisaidiwa na Haruna Niyonzima, Mrisho Ngasa na mbrazil Jaja akianza mshambuliaji peke yake.

Kipindi cha kwanza kilianza kwa kasi kwa timu zote kusaka bao la mapema, mipira mirefu ya Mbuyu Twite kwa Mrisho Ngasa haikuwa na madhara sana langoni mwa timu ya Azam katika dakika 10 za mwanzo.

Kiungo Said Juma "Makapu" alikosa nafasi ya kuipatia Young Africans bao la kwanza dakika ya 10 baada ya mpira wa kona uliopigwa na Niyonzima, huku Nizar Khalfani pia akikosa kuifungia pia timu yake bao baada ya shuti la faulo alilopiga kutoka mita chache pembeni mwa lango la Azam.

Young Africans iliendelea kulishambulia lango la Azam FC kupitia kwa washambuliaji wake Geilson Santos "Jaja" Mrisho Ngasa na Nizar Khalfani lakini kutoku makini kulipelekea timu zote kwenda mapumziko zikiwa sare ya kutofungana.

Kipindi cha pili Young Africans ilianza kwa kufanya mabadiliko ambapo kocha aliwaingiza Hassan Dilunga na Saimon Msuva waliochukua nafasi za Said Juma na Nizar Khalfani hali iliyopelekea kikosi cha mbrazil Maximo kutawala eneo la kiungo.

Dakika ya 58 Geilson Santos "Jaja" aliwainua vitini mashabiki, wapenzi na wanachama wa klabu ya Young Africans baada ya kuipatia timu yake bao la kwanza katikati ya walinzi wawili wa Azam FC akiitumia vizuri pasi ya Saimon Msuva.

Geilson Santos "Jaja" dakika ya 66 ya mchezo aliwainua tena vitini washabiki, wapenzi na wanachama baada ya kufunga bao la pili kwa ufundi wa hali juu, baada ya kupenyezewa pasi nzuri na Mrisho Ngasa na Jaja kuukota kwa hatua moja na kisha kumchambua mlinda mlango wa Azam FC Mwandini Ali kwa kuunyanyua kwa ufundi na kuamsha shangwe na nderemo uwanjani.

Huku wapenzi wa soka wakidhania mpira umemalizika, Saimon Msuva alimaliza ndoto za timu ya timu ya Azam kutwaa Ngao ya Jamii baada ya kuipatia timu yake bao la tatu na ushindi na kuifanya Young Africans kuchukua Ngao ya Jamii kwa mara ya nne tangu kuanzishwa kwake huku Simba wakiwa wamechukua mara mbili na Mtibwa Sugar mara moja.

Mpaka dakika 90 za mchezo zinamalizika, Young Africans 3 - 0 Azam FC.

Mara baada ya mchezo huo kocha mkuu wa Young Africans mbrazili Marcio Maximo alisema anawashukuru wachezaji wake kwa kucheza kwa kufuata maelekezo yake hali iliyoplekea kucheza soka safi la kuburudisha linaloambatana na ushindi.

Aidha Maximo alisema baada ya ushindi wa leo maandalizi ya mchezo dhidi ya Mtibwa Sugar yataanza siku ya jumanne ambapo kwa kesho ametoa mapumziko kwa wachezaji wote pamoja na benchi la Ufundi.

Mwisho Maximo amewapongeza vingozi, waachezaji na washabiki wa Young Africans kwa sapoti wanayoitoa kwa timu na kuomba wajitokeze kwa wingi pia mjin Morogoro mwishoni mwa wiki katika mchezo dhidi ya Mtibwa Sugar.

Young Africans: 1. Deo Munish "Dida", 2. Juma Abdul, 3.Oscar Joshua, 4. Nadir Haroub "Cananavao" (C), 5.Kelvin Yondani, 6.Mbuyu Twite, 7.Said Juma "Makapu"/Hassan Dilunga, 8.Haruna Niyonzima/Hamis Kizza, 9.Geilson Santos "Jaja"/Hussein Javu, 10.Mrisho Ngasa/Omega Seme, 11.Nizar Khalfani/Saimon Msuva/

Azam FC: 1.Mwadini Ali, 2.Shomari Kapombe, 3.Erasto Nyoni/Gadiel Michael, 4.David Mwantika, 5.Agrrey Morrsi, 6.Kipre Balou, 7.Himid Mao/Kelvin Friday, 8.Salum Abubakar, 9.Didier Kavumbag, 10.Kipre Tchetche/Ismail Diara, 11.Leonel st.Pres/Khamis Mcha

WAREMBO 30 WA MISS TANZANIA 2014 WAINGIA KAMBINI

Wanyange 30 watakaowania taji la Redd's Miss Tanzania 2014, wameingia kambini leo kwenye hoteli ya JB Belmint iliyoko katikati ya Jiji la Dar es Salaam kwa ajili ya kujiandaa kwa shindano hilo.


Warembo hao waliwasili kwenye hoteli hiyo kwa nyakati tofauti, kuanzia saa 12 jioni na kupokewa na waandaaji wa shindano hilo.



YANGA, AZAM KAZI IPO LEO NGAO YA JAMII



PAZIA la Ligi Kuu ya Tanzania Bara litafunguliwa leo kwa mchezo wa kuwania Ngao ya Jamii kati ya mabingwa wa msimu uliopita, Azam na washindi wa pili, Yanga utakaopigwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia saa 10 jioni.

Yanga itaingia uwanjani huku ikiwa na kumbukumbu ya ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Azam katika mechi ya kuwania Ngao ya Jamii msimu uliopita. Bao hilo la pekee lilifungwa na Salum Telela.

Kocha Mkuu wa Yanga, Marcio Maximo, ambaye atakuwa akiongoza Yanga kwa mara ya kwanza katika ligi, amesema vijana wake wote wapo katika hali nzuri, jambo linalompa wigo mpana wa kuchagua nani amtumie katika mchezo huo.

Mpaka sasa Maximo ameiongoza Yanga katika michezo minne ya kirafiki, akifanikiwa kushinda michezo yote, ambapo aliibuka na ushindi 1-0 (Chipukizi FC), 2-0 (Shagani FC), 2-0 (KMKM) na 1-0 (Thika United) kutoka nchini Kenya.

Katika mazoezi ya mwisho yaliyofanyika jana asubuhi katika uwanja wa shule ya Sekondari Loyola, mchezaji pekee ambaye hakuweza kufanya mazoezi ni Jerson Tegete, anayesumbuliwa na nyonga wakati Andrey Coutinho alifanya mazoezi mepesi chini ya usimamizi wa daktari wa timu, Suphian Juma.

Jumla ya wachezaji 26 wa Yanga wameendelea kuwepo kambini kujiandaa na mchezo huo katika Hoteli ya Tansoma iliyoko eneo la Gerezani, Kariakoo, Dar es Salaal.

Wachezaji hao ni walinda mlango: Juma Kaseja, Ally Mustafa "Barthez" na Deo Munish "Dida"
Walinzi wa Pembeni: Juma Abdul, Salum Telela, Oscar Joshua, Edward Charles na Amos Abel
Walinzi wa kati: Kelvin Yondani, Rajab Zahir, Pato Ngonyani na Nadir Haroub "Cannavaro"
Viungo: Mbuyu Twite, Hassan Dilunga, Omega Seme, Hamis Thabit, Nizar Khalfani, Haruna Niyonzima na Said Juma "Makapu"
Washambuliaji: Saimon Msuva, Mrisho Ngasa, Huseesin Javu, Said Bahauzi, Andrey Coutinho, Geilson Santana "Jaja" na Hamis Kizza "Diego"

Wakati huo huo, Kocha Mkuu wa Azam, Joseph Marius Omog amesema kikosi chake kipo tayari kwa mchezo wa leo wa Ngao ya Jamii dhidi ya Yanga SC.

Omog amesema japokuwa atamkosa nahodha wake, John Raphael Bocco ‘Adebayor’, lakini anaamini wachezaji waliobaki wana uwezo wa kuiwezesha Azam FC kutwaa Ngao ya Jamii kwa mara ya kwanza.

“Tuko tayari, vijana wapo katika hali nzuri kuelekea mchezo huo muhimu wa mwanzo wa msimu. Nitamkosa nahodha John (Bocco), lakini nina imani kubwa na wachezaji waliopo,”amesema Mcameroon huyo.

Bocco anasumbuliwa na maumivu ya nyama aliyoyapata katika mchezo wa robo fainali ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame mwezi uliopita mjini Kigali, Rwanda.

Akiwazungumzia wapinzani wao, Omog amesema anaiheshimu Yanga SC ni timu kongwe na yenye historia katika soka ya Tanzania na anatarajia mchezo utakuwa mgumu, lakini wamejiandaa kikamilifu kushinda.

Tayari TFF ilishatangaza viingilio vya mchezo huo kuwa ni Tshs 30,000 (VIP A) Tshs 20,000 (VIP B & C) Tshs 10,000 (Rangi ya Chungwa) na Tshs 5,000 (Bluu & Kijani).

SIMBA YABANWA MBAVU NA NDANDA FC

SIMBA imeendelea kwenda mwendo wa kusuasua katika mechi zake za kujiandaa kwa michuano ya ligi kuu ya Tanzania Bara baada ya juzi kulazimishwa kutoka suluhu na Ndanda FC.

Katika mechi hiyo ya kirafiki iliyochezwa kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara, vijana wa Ndanda waliwabana vyema wapinzani wao katika vipindi vyote viwili.

Sare hiyo imekuja siku chache baada ya Simba kuchapwa bao 1-0 na URA ya Uganda katika mechi ya kirafiki ya kimataifa iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Kama ilivyokuwa katika mechi dhidi ya URA, mshambuliaji Emmanuel Okwi alishindwa kuonyesha makeke yake kutokana na kubanwa vyema na mabeki wa Ndanda. Okwi aliingia kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Abdalla Seseme.