'
Tuesday, December 30, 2014
SIMBA, MTIBWA KUFUNGUA DIMBA KOMBE LA MAPINDUZI KESHO
Na Salum Vuai, Zanzibar
SIMBA SC na Mtibwa Sugar, keshokutwa wanatarajiwa kukata utepe wa michuano ya Kombe la Mapinduzi 2015 uwanja wa Amaan, kuanzia saa 2:15 ukiwa mchezo wa kundi C.
Pambano hilo linatarajiwa kuwa la marudiano kufuatia timu hizo kufungana bao 1-1 katika mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara msimu huu.
Katibu wa Kamati ya Mashindano hayo Khamis Abdallah Said, alisema mchezo huo utatanguliwa na mwengine wa kundi hilo kati ya maafande wa Mafunzo na JKU utakaoanza saa 9:00 mchana.
Mechi za kundi A zitaanza kwa pambano kati ya Shaba na Polisi mnamo saa 11:00 jioni.
Khamis, ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Michezo Zanzibar (BTMZ), alisema mashindano hayo sasa yatashirikisha timu za Tanzania na Uganda pekee baada ya timu ya Ulinzi ya Kenya na Al Ahly ya Misri kushindwa kuthibitisha ushiriki wao.
Alifahamisha kuwa nafasi moja itajazwa na Sports Club Villa ya Uganda, na nyengine itatajwa baadae lakini itakuwa kutoka Zanzibar.
Ratiba hiyo inaonesha kuwa, Januari 2, mwakani mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara Azam FC, watatiana mikonini KCC ambao ndio wanaotetea taji hilo, zikiwa kundi B.
Mapema wakati wa alasiri, kutakuwa na mchezo mwengine wa kundi hilo, baina ya Mtende Rangers na mabingwa wa soka Zanzibar, KMKM.
Yanga SC ambao kwa miaka miwili iliyopita hawakushiriki mashindano hayo kwa sababu mbalimbali, wataanza resi za kuwania taji hilo Januari 3, dhidi ya Sports Club Villa ya Uganda katika mchezo wa kundi A.
Wakati wa saa 10:00 alasiri, kutakuwa na mechi ya kundi C kati ya wajenga uchumi wa Zanzibar JKU na wazalishaji sukari wa Morogoro, Mtibwa Sugar.
Kwa jumla, timu zinazoshiriki mashindano hayo zimepangwa katika makundi matatu, ambapo kundi A linajumuisha timu za SC Villa, Yanga SC, Polisi na Shaba.
Mabingwa wa kombe hilo KCC, Azam FC, KMKM na Mtende Rangers ziko kundi B, huku kundi C likiundwa na wekundu wa Msimbazi Simba SC, Mtibwa Sugar, JKU na Mafunzo.
Timu mbili za kwanza kutoka kila kundi zitafuzu hatua ya robo fainali, na timu mbili zitapatikana kutokana na washindwa waliofanya vizuri (Best Loosers).
Fainali ya ngarambe hizo imepangwa kupigwa Januari 13, 2015.
WAAMUZI 18 WAPATA BEJI ZA FIFA
Waamuzi 18 wa Tanzania wamepata beji za uamuzi za Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) kwa mwaka 2015.
Idadi hiyo ambayo ni rekodi kwa Tanzania inahusisha waamuzi saba wa kike. Waamuzi wa kati wa kike waliopata beji hizo ni pamoja na Jonesia Rukyaa Kabakama aliyechezesha mechi ya Nani Mtani Jembe kati ya Simba na Yanga. Wengine ni Florentina Zablon Chief na Sophia Ismail Mtongori.
Waamuzi wasaidizi wa kike waliopata beji hizo ni Dalila Jafari Mtwana, Grace Wamala, Hellen Joseph Mduma na Kudura Omary Maurice.
Kwa waamuzi wa kati wa kiume ni Israel Mujuni Nkongo, Martin Eliphas Sanya, Mfaume Ali Nassoro na Waziri Sheha Waziri. Waamuzi wasaidizi ni Alli Kinduli, Ferdinand Chacha, Frank John Komba, John Longino Kanyenye, Josephat Deu Bulali, Samuel Hudsin Mpenzu na Soud Iddi Lila.
AZAM, SIMBA, YANGA, MTIBWA KUCHEZA KOMBE LA MAPINDUZI
Timu za Azam, Mtibwa Sugar, Simba na Yanga zitashiriki michuano ya Kombe la Mapinduzi inayofanyika kisiwani Zanzibar kuanzia Januari 1 hadi 13 mwakani.
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limetoa ruhusa kwa timu hizo kucheza mashindano hayo baada ya kuhakikishiwa na Chama cha Mpira wa Miguu Zanzibar (ZFA) kuwa kesi iliyofunguliwa dhidi ya viongozi wake imeondolewa mahakamani.
Kutokana na timu hizo kushiriki Kombe la Mapinduzi, mechi zao za raundi ya tisa na kumi ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) zitachezwa katikati ya wiki baada ya kumaliza mechi zao za michuano hiyo.
Hivyo mechi za VPL ambazo hazitachezwa wikiendi hii ni kati ya Azam na Mtibwa Sugar, Mbeya City na Yanga, na ile kati ya Mgambo Shooting na Simba. Mechi za wikiendi ijayo zinazopisha michuano hiyo ni kati ya Kagera Sugar na Azam, Coastal Union na Yanga, Mbeya City na Simba, na Mtibwa Sugar na Tanzania Prisons.
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limetoa ruhusa kwa timu hizo kucheza mashindano hayo baada ya kuhakikishiwa na Chama cha Mpira wa Miguu Zanzibar (ZFA) kuwa kesi iliyofunguliwa dhidi ya viongozi wake imeondolewa mahakamani.
Kutokana na timu hizo kushiriki Kombe la Mapinduzi, mechi zao za raundi ya tisa na kumi ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) zitachezwa katikati ya wiki baada ya kumaliza mechi zao za michuano hiyo.
Hivyo mechi za VPL ambazo hazitachezwa wikiendi hii ni kati ya Azam na Mtibwa Sugar, Mbeya City na Yanga, na ile kati ya Mgambo Shooting na Simba. Mechi za wikiendi ijayo zinazopisha michuano hiyo ni kati ya Kagera Sugar na Azam, Coastal Union na Yanga, Mbeya City na Simba, na Mtibwa Sugar na Tanzania Prisons.
Monday, December 29, 2014
PHIRI AFUNGASHIWA VIRAGO SIMBA
KLABU ya Simba imeamua kumfungashia virago Kocha Mkuu wa timu hiyo, Patrick Phiri kutoka Zambia.
Habari kutoka ndani ya Simba zimeeleza jana kuwa, kocha huyo alitarajiwa kukabidhiwa rasmi barua ya kuvunja mkataba wake jana.
Kwa mujibu wa habari hizo, Simba imeamua kuvunja mkataba na Simba kutokana na mwenendo usioridhisha wa timu hiyo katika michuano ya ligi kuu ya Tanzania Bara.
Simba imemfungashia virago Phiri siku chache baada ya timu hiyo kuchapwa bao 1-0 na Kagera Sugar katika mechi ya ligi hiyo iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Awali, kocha huyo aliingoza Simba kuichapa Yanga mabao 2-0 katika mechi ya Nani Mtani Jembe iliyochezwa kwenye uwanja huo.
Phiri alikaririwa jana kwenye mitandao ya kijamii akithibitisha kutaarifiwa kuhusu kuvunjwa kwa mkataba wake.
Kocha huyo amesema ni suala la kawaida kumtokea kocha, hivyo hana kinyongo na uongozi wa klabu hiyo.
"Wamenitaarifu kuhusiana na kuachishwa kazi, hili si jambo jipya, ingawa niliona tungeweza kubadilisha mambo.
"Najua Simba wanataka kufanya vizuri, hivyo siwezi kumlaumu mtu na utaona mwendo wa timu yetu ulivyokuwa," alisema Phiri.
Phiri amesema anatarajia kurejea kwao baada ya kulipwa madai yake na uongozi wa Simba. Hakutaja kiasi anachoidai klabu hiyo kama mishahara na fidia ya kuvunjwa kwa mkataba.
YANGA MDOMONI MWA MBEYA CITY J'MOSI, SIMBA YAIFUATA MGAMBO SHOOTING
WAKATI raundi ya nane ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) ilikamilika Desemba 29 mwaka huu kwa mechi tatu, ligi hiyo itaingia raundi ya tisa Januari 3 mwakani kwa mechi tano.
Coastal Union itacheza na JKT Ruvu katika Uwanja wa Mkwakwani, Ruvu Shooting itaikaribisha Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Mabatini, Azam itakuwa mwenyeji wa Mtibwa Sugar katika Uwanja wa Azam Complex, Stand United itakuwa mgeni wa Polisi Morogoro kwenye Uwanja wa Jamhuri wakati Mbeya City na Yanga zitaoneshana kazi kwenye Uwanja wa Sokoine.
Ligi hiyo ambayo itachezwa mfululizo (non-stop) hadi itakapomalizika Mei 9 mwakani, itakamilisha raundi ya tisa Januari 4 mwakani kwa mechi kati ya Mgambo Shooting na Simba kwenye Uwanja wa Mkwakwani, na Tanzania Prisons itakayokuwa mwenyeji wa Ndanda kwenye Uwanja wa Sokoine.
Nayo mechi kati ya Mtibwa Sugar na Stand United ambayo jana ilivunjwa na mvua dakika ya 6 imemaliziwa leo ambapo timu hizo zimetoka sare ya bao 1-1.
Wakati huo huo, mechi ya ligi iliyochezwa jana usiku kwenye Uwanja wa Azam Complex imemalizika kwa wageni Ruvu Shooting kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya JKT Ruvu. Bao hilo lilifungwa kipindi cha kwanza kwa mkwaju wa penalti uliopigwa na Hamisi Kasanga.
MBAO FC YAKAMATA USUKANI SDL
Timu ya Mbao FC ya Mwanza imekamata uongozi wa Kundi B la michuano ya Ligi Daraja la Pili (SDL) baada ya jana (Desemba 27 mwaka huu) kuizamisha JKT Rwamkoma ya Mara mabao 2-1.
Kwa matokeo hayo katika mechi hiyo iliyochezwa Uwanja wa CCM Kirumba, Mbao FC imeitoa kileleni JKT Rwamkoma baada ya kufikisha pointi tisa kwa kushinda mechi zote tatu dhidi ya Arusha FC, Pamba na JKT Rwamkoma.
Mbao FC inafuatiwa na JKT Rwamkoma yenye pointi sita, Arusha FC pointi sita wakati Bulyanhulu na Pamba zikiwa za mwisho kwa pointi moja kila moja. Kundi hilo litakamilisha mzunguko wa kwanza Januari 3 mwakani kwa mechi kati ya JKT Rwamkoma na Arusha FC, na Bulyanhulu na Mbao FC.
Katika kundi A, Mji Mkuu (CDA) na Singida United ndizo zinazochuana kileleni kwa kufikisha pointi saba kila moja. Timu hizo zinafuatiwa na Milambo yenye pointi nne, Mvuvumwa FC yenye pointi moja wakati Ujenzi Rukwa ni ya mwisho ikiwa haina pointi.
Hata hivyo, Mvuvumwa FC na Milambo ziko nyuma kwa mechi moja. Mechi hiyo ya kukamilisha raundi ya tatu kati ya timu hizo itachezwa kesho (Desemba 29 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika mjini Kigoma.
Kiluvya United imeendelea kuchachafya kundi C baada ya kushinda mechi zote ne ilizocheza, hivyo kufikisha pointi 12. Inafuatiwa na Mshikamano yenye pointi saba huku Abajalo ikiwa katika nafasi ya tatu kwa pointi 6.
Nafasi ya nne inashikwa na Transit Camp yenye pointi nne, Cosmopolitan yenye pointi mbili ni ya tano wakati Kariakoo ambayo haina pointi ni ya mwisho. Hata hivyo, Cosmopolitan na Kariakoo zina mchezo mmoja mkononi.
Mechi zinazofuata za kundi hilo ni Januari 3 mwakani kati ya Kariakoo na Mshikamano na Mshikamano (Ilulu), Transit Camp na Abajalo (Mabatini), na Cosmopolitan na Kiluvya (Karume).
Kundi D, vinara bado ni Njombe Mji yenye pointi 12 ikifuatiwa na Wenda yenye pointi sita wakati Volcano FC iko nafasi ya tatu ikiwa na pointi tano. Mkamba Rangers ina pointi nne, Town Small Boys ina pointi moja wakati Magereza FC haina pointi.
Katika kundi hilo leo (Desemba 28 mwaka huu) kutakuwa na mechi kati ya Town Small Boys na Magereza itakayochezwa Uwanja wa Majimaji mjini Songea. Januari 3 mwakani kutakuwa na mechi kati ya Town Small Boys na Njombe Mji, Volcano FC na Magereza, na Wenda na Mkamba Rangers.
Sunday, December 28, 2014
YANGA, AZAM HAKUNA MBABE
TIMU za soka za Yanga na Azam jana zilishindwa kutambiana baada ya kutoka sare ya mabao 2-2 katika mechi ya ligi kuu ya Tanzania Bara iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Kutokana na matokeo hayo, timu hizo mbili sasa zimefikisha pointi 14 kila moja, lakini Yanga inashika nafasi ya pili kutokana na kuwa na idadi ya mabao mengi ya kufunga.
Mtibwa Sugar, ambayo juzi ilitoka sare ya bao 1-1 na Stand United kwenye uwanja wa Manungu ulioko Turiani mjini Morogoro, bado inaongoza ligi hiyo kwa kuwa na pointi 16.
Katika mechi hiyo iliyokuwa na ushindani mkali, Azam ilikuwa ya kwanza kupata bao dakika ya tano lililofungwa na Didier Kavumbagu kwa shuti kali baada ya mabeki wa Yanga kujichanganya.
Yanga ilisawazisha dakika mbili baadaye kwa bao lililofungwa na Amis Tambwe kwa shuti kali lililomshinda kipa Mwadini Ally wa Azam. Timu hizo zilikwenda mapumziko zikiwa sare ya bao 1-1.
Mshambuliaji machachari na mwenye kasi, Simon Msuva aliiongezea Yanga bao la pili dakika ya 52 baada ya kufumua shuti kali la umbali wa mita 30 lililotinga moja kwa moja wavuni.
Azam ilisawazisha dakika ya 65 kwa bao lililofungwa na John Boko baada ya kuunganisha wavuni kwa kichwa krosi iliyopigwa na Himidi Mao.
Friday, December 26, 2014
KOMBE LA TAIFA WANAWAKE KUANZA KESHO
Mashindano ya Taifa ya mpira wa miguu kwa wanawake (Taifa Cup Wanawake) yanazinduliwa rasmi Januari Mosi mwakani kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza kwa mechi kati ya wenyeji Mwanza na Mara.
Mechi hiyo itakayoonyeshwa moja kwa moja na televisheni ya Azam itachezwa kuanzia saa 10 jioni. Mashindano hayo yanayodhaminiwa na kampuni ya Proin yatachezwa kwa mtindo wa nyumbani na ugenini katika hatua ya kwanza.
Januari 10 mwakani ndipo zitachezwa mechi kwa mikoa yote ambapo Geita itakuwa mwenyeji wa Kagera (Uwanja wa Geita), Tabora vs Kigoma (Ali Hassan Mwinyi), Simiyu vs Shinyanga (Uwanja wa Simiyu), Arusha vs Manyara (Sheikh Kaluta Amri Abeid), na Kilimanjaro vs Tanga (Uwanja wa Ushirika).
Mechi nyingine ni Lindi itaikaribisha Mtwara kwenye Uwanja wa Ilulu, Ruvuma vs Njombe (Uwanja wa Majimaji), Mbeya vs Iringa (Uwanja wa Sokoine), Katavi vs Rukwa (Uwanja wa Katavi), Dodoma vs Singida (Uwanja wa Jamhuri) na Pwani itakuwa mwenyeji wa Morogoro katika Uwanja wa Mabatini.
Timu hizo zitarudiana Januari 13 mwakani, ambapo baada ya matokeo ya nyumbani na ugenini timu iliyoshinda ndiyo itakayoingia hatua inayofuata ambayo pia itashirikisha mikoa ya kisoka ya Ilala, Kinondoni na Temeke.
Hatua hiyo, mechi zake za kwanza zitachezwa Januari 17 mwakani wakati zile za marudiano zitafanyika Januari 21 mwakani.
Baada ya hapo, hatua itakayofuata ni robo fainali, nusu fainali na fainali ambayo ndiyo itakayotoa bingwa wa michuano hiyo inayofanyika kwa mara ya kwanza nchini.
Mdhamini atatoa jezi kwa timu zote zinazoshiriki kabla ya kuanza mashindano hayo.
SDL KUTIMUA VUMBI KRISMASI
Michuano ya Ligi Daraja la Pili (SDL) inayochezwa katika makundi manne tofauti inaingia raundi ya nne kesho (Desemba 25 mwaka huu) kwa mechi ya kundi C kati ya Kiluvya United na Abajalo itakayochezwa Uwanja wa Mabatini uliopo Mlandizi mkoani Pwani.
Mechi nyingine ya kundi hilo kati ya Mshikamano FC na Transit Camp yenyewe itachezwa keshokutwa (Desemba 26 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume jijini Dar es Salaam.
Kundi A litakuwa na mechi Jumamosi (Desemba 27 mwaka huu) ambayo itazikutanisha timu za Ujenzi Rukwa na Mji Mkuu (CDA) kwenye Uwanja wa Nelson Mandela mjini Sumbawanga. Desemba 28 mwaka huu ni kati ya Mvuvumwa FC na Milambo SC kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika mjini Kigoma.
Jumamosi (Desemba 27 mwaka huu) kundi B litakuwa na mechi kati ya Arusha FC na Pamba (Uwanja wa Sheikh Kaluta Amri Abeid jijini Arusha), na Mbao FC vs JKT Rwamkoma (Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza).
Kundi D siku ya Jumamosi hekaheka itakuwa kati ya Mkamba Rangers na Volcano (Uwanja CCM Mkamba), Njombe Mji vs Wenda FC (Uwanja wa Amani, Njombe) na Town Small Boys vs Magereza FC (Uwanja wa Majimaji, Songea).
Tuesday, December 23, 2014
JK AMPONGEZA DIAMOND KWA KUTWAA TUZO ZA AFRIKA
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. Jakaya Mrisho Kikwete amewapongeza mwanamuziki Nassib Abdul maarufu kwa jina la Diamond na Mshindi wa Shindano la Big Brother Africa, Idris Sultan kwa kuiletea sifa Tanzania kupitia sanaa.
Rais Kikwete ametoa Pongezi hizo alipokutana na Msanii Diamond Ikulu jijini Dar es salaam leo Jumanne Desemba 23, 2014 , ambapo Msanii huyo amemwonyesha tuzo tano alizoshinda baada ya kupambanishwa na wasanii wengine wa Afrika.
Pamoja na pongezi hizo kwa Diamond na Idris kwa kile alichosema wameitoa nchi kimasomaso, Rais Kikwete amewasihi wasanii hao kujihadhari na athari za umaarufu na utajiri katika umri mdogo,zikiwemo kujitumbukiza katika matumizi ya dawa za kulevya na ulevi.
Kikwete amewaasa kuwa ni muhimu kwa wasanii hao kutumia mapato wanayoyapata katika kazi zao za usanii kwa kujijenga kifamilia ikiwa ni pamoja na kujenga nyumba zao za kuishi na wanafamilia wanaowategemea pamoja kuwasaidia wasanii wenzao.
“Umaarufu katika sanaa yoyote ile ni wa kupita hivyo tumieni umaarufu mlio nao sasa kama fursa ya kujijenga kimaisha na sio kutumbukia katika kadhia za kidunia kama vile ulevi, ukorofi mbele ya jamii na mambo mengine yasiyofaa", aliwaasa Mhe. Rais.
Rais Kikwete pia alimpongeza Sultan kwa kuiletea Tanzania sifa na kumtakia mafanikio zaidi katika shughuli zake za baadaye. Rais Kikwete alisema kuwa Sultan hakuifedhehesha Tanzania kwa kutofanya mambo yaliyo kinyume na maadili ya Mwafrika alipokuwa katika jumba la Big Brother Africa.
Kwa upande wake,Diamond amemshukuru na kumpongeza Rais Kikwete kwa ushirikiano anaoutoa kwa wasanii hapa nchini, hali ambayo amesema ndiyo iliyowawezesha kupata mafanikio kitaifa na kimataifa.
Diamond pia amemuahidi Rais Kikwete kutekeleza yote aliyomuasa kuhusu kujiheshimu na kutolewa umaarufu alionao, na kwamba ataendelea kufanya kazi zake za usanii wa Muziki kwa juhudi zake zote kuitangaza nchi.
Msanii huyo pia amemweleza Rais Kikwete kuwa hivi karibuni atapokea tuzo nyingine ya sita kutoka huko Nigeria.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu – Dar es Salaam.
23 Desemba,2014
Saturday, December 20, 2014
MKUTANO MKUU WA TFF KUFANYIKA SINGIDA
Kamati ya Utendaji imejadili rasimu ya Kanuni za Leseni za Klabu (Club Licensing Regulations), na kuagiza Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ifanye marekebisho ya mwisho, kabla ya kanuni hizo kusainiwa na kuanza kutumika.
UANZISHAJI MFUKO WA MAENDELEO YA MPIRA WA MIGUU (FDF)Kamati ya Utendaji imepokea taarifa ya maendeleo ya mchakato wa uanzishwaji wa Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (Football Development Fund- FDF).
Imeipongeza Kamati ya Mfuko huo inayoongozwa na Rais wa zamani wa TFF, Leodegar Tenga, na kuitaka fanye jitihada za kukamilisha rasimu ya kanuni za uendeshaji mfuko huo.
Mbali ya Tenga, wajumbe wengine wa mfuko huo ni Ayoub Chamshama, Ephraim Mafuru, Frederick Mwakalebela, Tarimba Abbas na Zarina Madabida. Sekretarieti ya mfuko huo inaundwa na Henry Tandau ambaye ni Katibu, Wakili Emmanuel Muga na Boniface Wambura.
FDF ambao ni mfuko utakaokuwa unajitegemea utakuwa unashughulika na maendeleo ya mpira wa miguu kwa vijana, na nyanja nyingine za maendeleo kwa mchezo huo.
MKUTANO MKUU KUFANYIKA SINGIDA MACHI 14
Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imepanga Mkutano Mkuu wa Kawaida wa mwaka ufanyike Machi 14 na 15 mwakani mjini Singida.
MGOGORO NDANI YA ZFA
Kamati ya Utendaji imepokea kwa masikitiko taarifa za masuala ya mpira wa miguu Zanzibar kupelekwa mahakamani.
Kwa mujibu wa Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) kitendo hicho ni kinyume cha taratibu za uendeshaji mpira wa miguu ambazo zinakataza masuala ya mchezo huo kupelekwa katika mahakama za kawaida.
Kamati ya Utendaji inatoa rai kwa pande zote mbili zinazohusika na mgogoro huo kukaa kwenye meza ya mazungumzo ili kumaliza tofauti zao.
Kamati ya Utendaji imejitolea kutuma ujumbe wake Zanzibar ili ukutane na pande zinazohusika katika mgogoro huo.
Ni muhimu usuluhisho upatikane haraka ili tuweze kujua hatma ya washiriki wetu kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi.
TFF: BADO KUNA UPUNGUFU MATUMIZI YA TIKETI ZA ELEKTRONIKI
Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) iliyokutana jana (Desemba 19 mwaka huu) jijini Dar es Salaam, imezingatia upungufu uliopo katika utekelezaji wa matumizi ya tiketi za elektroniki.
Hivyo, Kamati hiyo imeiagiza Sekretarieti ya TFF kuwasiliana na benki ya CRDB inayoendesha mfumo huo wa matumizi ya tiketi za elektroniki kuhusu upungufu huo na kuhakikisha unafanyiwa kazi.
MAREKEBISHO YA KATIBA YA TFF
Kamati ya Utendaji ya TFF imerejea mazungumzo kati yake na ujumbe wa Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) uliokuwa nchini ukiongozwa na Meneja wa Vyama Wanachama wa FIFA, James Johnson.
Mazungumzo hayo kuhusu Katiba ya TFF yalifanyika Desemba 18 mwaka huu jijini Dar es Salaam.
Kamati ya Utendaji inasubiri rasimu ya Katiba hiyo kutoka FIFA ili iweze kufanya utaratibu wa kuwaarifu wanachama wake juu ya maudhui ya rasimu hiyo.
Shughuli ya FIFA kurekebisha katiba za nchi wanachama wake inaendelea duniani kote, na kwa Afrika kazi hiyo imekamilika katika nchi za Namibia, Zimbabwe na Malawi.
USHIRIKIANO KATI YA TFF NA SAFA
Kamati ya Utendaji imepitia na kupitisha makubaliano ya ushirikiano kati ya TFF na Chama cha Mpira wa Miguu Afrika Kusini (SAFA).
Makubaliano hayo ni ushirikiano katika nyanja za mpira wa miguu wa vijana, maendeleo ya waamuzi, ufundi, menejimenti ya matukio (event management) na utafutaji udhamini (sponsorship).
Tuesday, December 16, 2014
WACHEZAJI YANGA WAMLILIA MAXIMO
KOCHA wa Yanga, Mbrazil Marcio Maximo amewaaga rasmi leo asubuhi wachezaji wa timu hiyo kwenye mazoezi uwanja wa Sekondari ya Loyola huku akitarajia kuvuna zaidi ya Milioni 20 ndani ya klabu hiyo ikiwa ni mshahara wake wa dola 1200 na yupo kwenye harakati za kudai fidia ya kuvunjiwa mkataba na kuletwa mrithi wake kabla uongozi wa klabu hiyo haujamaliza nae.
Hata hivyo, tayari Maximo ameaga wachezaji wake kwenye mazoezi ya asubuhi leo ambapo mazoezi hayo yaligeuka shubiri baada ya Maximo kuwakusanya wachezaji wake na kuwambia kuwa kuanzia leo sio kocha wa timu hiyo tena na kuwatakia maisha mema ndani ya klabu hiyo ya Jangwani.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wachezaji wa klabu hiyo ambao pia hawajaridhishwa na uamuzi wa uongozi wa klabu hiyo kumuacha mshambuliaji Hamis Kiiza na kumsajili Amis Tambwe.
Mmoja wa wachezaji hao alisema "Ni kweli kocha ametuaga asubuhi daa! ndio hivyo tumesikitika lakini hatuna jinsi."
Naye mchezaji mwingine ambaye hakutaka jina lake litajwe alisema "Inaumiza sana jana (juzi) tumefanya nae mazoezi vizuri kabisa tena amechangamka kama kawaida kumbe nyuma kuna mambo yanaendelea, leo asubuhi tumeenda mazoezi kama kawaida tukijua tunafanya mazoezi matokeo yake anasema acheni kila kitu kaeni hapo nataka kuzungumza na nyinyi.
"Uwezi kuamini kidogo machozi yanitoke pale aliposema kuanzia leo yeye sio kocha wetu tena, dah inaumiza sana, mtu ambaye mmemzoea mnafanya nae kazi kuondoka, ndo hivyo wakubwa wemeshaamua bwana wenye timu yao.
Wakati huyo akisema hayo, mchezaji nguli wa timu hiyo yeye alisema "Hakuna mchezaji kwa kweli aliyependezwa na kitendo cha uongozi, yani kwenye mazoezi asubuhi ilikuwa kama msiba, 'mood' ya kufanya mazoezi iilisha kabisa, yani hakuna aliyekuwa na hamu ya kuendelea na mazoezi.
"Tumefanya kidogo mazoezi tukaondoka, ukiangalia ni sawa tumefungwa cha muhimu ilikuwa ni kukaa chini na kuzungumza na kuangalia cha kufanya, kama kuna mapungufu basi yafanyiwe kazi, mimi sijaona haja ya kumfukuza kocha hasa kipindi kama hichi."
Meneja wa timu hiyo Hafidhi Saleh alikiri Maximo kuaga wachezaji kabla ya mazoezi ya timu hiyo kuanza akiwapa moyo wajitume kwa kuwa ni wachezaji wazuri na timu ni nzuri na kuwataka kuongeza bidii ili wafike mbali.
"Kwa kweli inasikitisha hakuna mchezaji wala mtu aliyefurahia, kama yupo labda kimoyomoyo ila dah imetuumiza, ni mazoea cha muhimu tugange yajayo hayo mengine tuwaachie viongozi."alisema Saleh
Saleh alisema kuwa tayari kocha Hans van Der Pluijm ambaye amefikia kwenye hoteli ya Tansoma jana alikuwa kwenye mazungumzo na uongozi wa klabu hiyo ili aichukue nafasi ya mbrazil Marcio Maximo ambaye amekumbwa na kipunga cha kutimuliwa baada ya kunyukwa mabao 2-0 katika mechi ya mtani Jembe, akiwa ni kocha wa pili kutimuliwa Yanga baada ya matokeo ya mtani jembe mwaka jana alitimuliwa Ernie Brandts baada ya kunyukwa mabao 3-1 na nafasi yake kuchukuliwa na Pluijim ambaye nae hakukaa sana akaikacha timu hiyo baada ya kupata kibara nchini Saudi Arabia.
Wakati huo huo, uongozi wa Yanga umegwaya mchezaji Andry Countinouh kuvunja mkataba wake baada ya kuwa wangelazimika kuvunja kibubu cha Sh185 milioni ili kumlipa fidia ya mshahara wake ambao ni dola 2800 kwa mwezi.
Katika hatua nyingine, pamoja na Yanga kumfungashia virago Emerson De Oliveira Neves Roque imemuombea kibali cha usajili wa kimataifa (ITC) kutoka Bonsucesso Brasil kwenda Yanga.
Mkurugenzi wa mashindano ya TFF, Boniface Wambura alisema kuwa TFF haina taarifa za Yanga kumuacha mbrazili huyo
WANASOKA 15 KUTOKA NJE WAOMBEWA USAJILI DIRISHA DOGO
Usajili wa dirisho dogo msimu wa 2014/2015 umefungwa jana (Desemba 15 mwaka huu) huku wachezaji 15 kutoka nje wakiombewa Hati ya Uhamisho wa Kimataifa (ITC) kutoka nchi mbalimbali.
Wachezaji walioombewa ITC kwa timu za Ligi Kuu ni Abdulhalim Humoud kutoka Sofapaka ya Kenya kwenda Coastal Union, Brian Majwega kutoka KCC (Uganda) kwenda Azam, Castory Mumbara kutoka Three Star Club (Nepal) kwenda Polisi Mara, Charles Misheto kutoka SP Selbitiz (Ujerumani) kwenda Stand United na Chinedu Michael Nwankwoeze kutoka Nigeria kwenda Stand United.
Dan Serunkuma kutoka Gor Mahia (Kenya) kwenda Simba, Emerson De Oliveira Neves Roque kutoka Bonsucesso FC (Brasil) kwenda Yanga, Halidi Suleiman kutoka Flambeau (Burundi) kwenda Stand United na Juuko Murushid kutoka SC Victoria University (Uganda) kwenda Simba.
Kpah Sean Sherman kutoka Aries FC (Liberia) kwenda Yanga, Meshack Abel kutoka KCB (Kenya) kwenda Polisi Morogoro, Moussa Omar kutoka Flambeau (Burundi) kwenda Stand United, Nduwimana Michel kutoka Flambeau (Burundi) kwenda Stand United, Serge Pascal Wawa kutoka El Merreikh (Sudan) kwenda Azam na Simon Serunkuma kutoka Express FC (Uganda) kwenda Simba.
Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya TFF inatarajia kukutana hivi karibuni kwa ajili ya kupitia usajili wa wachezaji wote walioombewa katika dirisha dogo wakiwemo wale wa mkopo.
TFF YATUMA RAMBIRAMBI KIFO CHA KOCHA MSHINDO MADEGA
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limepokea kwa masikitiko taarifa za kifo cha Kocha Mshindo Madega kilichotokea leo (Desemba 16 mwaka huu) mjini Bukoba.
Mbali ya kuwahi kuwa mchezaji katika timu ya RTC Kagera, Kocha Madega aliwahi kufundisha timu za Kagera Stars, Mwadui na kombaini ya Copa Coca-Cola ya Mkoa wa Kagera.
Mchango wake katika mchezo wa mpira wa miguu tangu akiwa kocha na baadaye kocha utakumbukwa daima.
Tunatoa salama za rambirambi kwa familia ya marehemu, Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Kagera (KRFA), Chama cha Makocha wa Mpira wa Miguu Tanzania (TAFCA) Mkoa wa Kagera na klabu ya Bukoba Veterans na kuwataka kuwa na subira na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu cha msiba huo.
TFF itawakilishwa kwenye msiba huo na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Kagera (KRFA).
MICHUANO YA COPA COCA-COLA YAENDELEA KUTIMUA VUMBI
Michuano ya Copa Coca-Cola kwa vijana wenye umri chini ya miaka 15 ngazi ya Taifa inaendelea leo jioni (Desemba 16 mwaka huu) kwa mechi mbili zitakazochezwa jijini Dar es Salaam na mkoani Pwani.
Uwanja wa Nyumbu uliopo mkoani Pwani utazikutanisha timu za Mjini Magharibi na Dodoma katika mechi ya kundi B, wakati kundi C kutakuwa na mechi kati ya Arusha na Mwanza itakayochezwa Uwanja wa Tanganyika Packers uliopo Kawe jijini Dar es Salaam.
Wakati kesho (Desemba 17 mwaka huu) ikiwa ni mapumziko, michuano hiyo itaingia hatua ya robo fainali keshokutwa (Desemba 18 mwaka huu) kwenye viwanja hivyo hivyo.
SIMBA YAMNASA BEKI WA MTIBWA SUGAR
HASSAN Ramadhani (kulia) akimdhibiti mshambuliaji Mrisho Ngasa wa Yanga katika moja ya mechi za ligi kuu ya Tanzania Bara.
KLABU ya Simba imekamilisha dirisha dogo la usajili kwa kumsajili beki Hassan Ramadhani kutoka Mtibwa Sugar.
Usajili wa beki huyo unaifanya Simba iwe imesajili wachezaji wapya wanne katika usajili wa dirisha dogo. Wengine niDan Sserunkuma, Simon Ssenrukuma na Juuko Jurshid.
Makamu wa Rais wa simba, Godfrey Nyange 'Kaburu, amesema usajili wa Kessy umezingatia matakwa ya Kocha Mkuu wa timu hiyo, Mzambia Patrick Phiri.
Kaburu alisema kwa sasa wanaamini kuwa kikosi chao kimekamilika katika kila idara na kwamba wanayo nafasi kubwa ya kushika nafasi mbili za kwanza katika michuano ya ligi kuu ya Tanzania Bara.
Simba imewatema kiungo Pierre Kwizera na mshambuliaji Amis Tambwe, ambaye tayari amejiunga na klabu ya Yanga.
KLABU ya Simba imekamilisha dirisha dogo la usajili kwa kumsajili beki Hassan Ramadhani kutoka Mtibwa Sugar.
Usajili wa beki huyo unaifanya Simba iwe imesajili wachezaji wapya wanne katika usajili wa dirisha dogo. Wengine niDan Sserunkuma, Simon Ssenrukuma na Juuko Jurshid.
Makamu wa Rais wa simba, Godfrey Nyange 'Kaburu, amesema usajili wa Kessy umezingatia matakwa ya Kocha Mkuu wa timu hiyo, Mzambia Patrick Phiri.
Kaburu alisema kwa sasa wanaamini kuwa kikosi chao kimekamilika katika kila idara na kwamba wanayo nafasi kubwa ya kushika nafasi mbili za kwanza katika michuano ya ligi kuu ya Tanzania Bara.
Simba imewatema kiungo Pierre Kwizera na mshambuliaji Amis Tambwe, ambaye tayari amejiunga na klabu ya Yanga.
YANGA YAMTUPIA VIRAGO MAXIMO
KLABU ya Yanga imemtupia virago Kocha Mkuu wa timu hiyo, Mbrazil Marcio Maximo pamoja na mshambuliaji Emerson.
Uamuzi huo wa Yanga ulifikiwa katika kikao cha kamati ya utendaji ya klabu hiyo, kilichofanyika jana chini ya uongozi wa Mwenyekiti, Yussuf Manji.
Habari za uhakika kutoka ndani ya klabu hiyo zimeeleza kuwa, nafasi ya Emerson imechukuliwa na mshambuliaji Amis Tambwe kutoka Simba.
Kutimuliwa kwa Maximo na Emerson kumekuja siku chache baada ya Yanga kuchapwa mabao 2-0 na Simba katika mechi ya Nani Mtani Jembe iliyochezwa Jumamosi iliyopita kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Kutimuliwa kwa Emerson, ambaye alipokelewa kwa mbwembwe nyingi huku akitajwa kuwa kiungo mahiri mkabaji, kumeifanya Yanga isaliwe na wachezaji watano wa kigeni.
Mbali na Tambwe, wengine ni Haruna Niyonzima, Mbuyu Twite, Andrey Countinho na Mliberia, Sherman.
Sunday, December 14, 2014
SSENKURUMA, JUUKO WAMWAGA WINO SIMBA
Simon Sserunkuma akitia saini fomu za usajili za Simba baada ya klabu hiyo kukatisha mikataba ya wachezaji wake wawili wa kimataifa, wote raia wa Burundi, mshambuliaji Hamis Tambwe na Kiungo Pierre Kwizera, ikiwa ni siku moja tangu Simba kuifunga Yanga kwenye mchezo wa nani mtani Jembe.
Beki Juuko Murushid, akitia saini mkataba wa kuichezea Simba. Juuko aliichezea Simba dhidi ya Yanga katika Uwanja wa Taifa Jijini Dar-es-Salaam na kuonyesha uwezo mkubwa na kuisaidia Simba kupata ushindi wa mabao 2-0. Kwa usajili huo, Simba sasa inao wachezaji watano kutoka Uganda. Wachezaji hao ni George Owino, Emmanuel Okwi, Dan Sserunkuma, Saimon Sserunkuma na Juuko Murushid
SIMBA YAINYAMAZISHA YANGA
SIMBA jana iliendeleza ubabe wake kwa watani wao wa jadi Yanga, baada ya kuwachapa mabao 2-0 katika mechi ya Nani Mtani Jembe iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Hii ni mara ya pili kwa Simba kuishinda Yanga katika mechi hiyo, inayoandaliwa kila mwaka na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), kupitia bia yake ya Kilimanjaro. Katika mechi ya mwaka jana, Simba iliichapa Yanga mabao 3-1.
Yanga ililianza pambano hilo kwa kasi na kufanya mashambulizi kadhaa kwenye lango la Simba huku ikipata nafasi nzuri za kufunga, lakini umaliziaji mbovu wa washambuliaji wake, Simon Msuva, Emerson na Sherman ulikuwa kikwazo.
Kadri mchezo ulivyokuwa ukisonga mbele, wachezaji wa Simba walianza kutulia na kucheza kwa uelewano na hatimaye Awadh Juma kuiandikia bao la kwanza dakika ya 30 baada ya Kipa Dida wa Yanga kutema shuti la Emmanuel Okwi.
Zikiwa zimesalia dakika nne kuwa mapumziko, Elias Maguri aliiandikia Simba bao la pili baada ya mpira uliorushwa na Nassoro Masoud kumkuta akiwa katikati ya mabeki wa Yanga, akaupiga kichwa, ukagonga mwamba wa pembeni wa goli na kumrudia, ambapo aliutumbukiza kimiani. Timu hizo zilikwenda mapumziko Simba ikiwa mbele kwa mabao 2-0.
Kipindi cha pili kilianza kwa timu zote kufanya mabadiliko kadhaa ya wachezaji kwa lengo la kuongeza nguvu, lakini hakuna iliyoweza kupata bao.
Kwa ushindi huo, Simba ilizawadiwa fedha taslim sh. milioni 15 kutoka TBL wakati Yanga iliambulia sh. milioni tano. Hundi za fedha hizo zilikabidhiwa kwa manahodha wa timu hizo, Haruna Niyonzima wa Yanga na Okwi wa Simba.
Monday, December 8, 2014
SECOM WIRELESS YADHAMINI TUZO ZA TASWA
Meneja Biashara, ukuzaji na Masoko wa kampuni ya Selcom Wireless, Juma Mgori (Katikati) akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na udhamini wa Tuzo za wanamichezo bora za Chama cha waandishi wa habari za michezo nchini (Taswa). Kampuni hiyo imetoa udhamini wa Sh Milioni 30. Kushoto ni Gallus Runyeta ambaye ni Meneja Miradi wa kampuni hiyo na kulia ni Mwenyekiti wa Taswa, Juma Pinto.
TAIFA STARS YA MABORESHO KUKIPIGA NA BURUNDI LEO
Kikosi cha Taifa Stars Maboresho kimerejea Dar es Salaam kutoka Bulyanhulu mkoani Shinyanga ambapo kiliweka kambi kwa ajili ya mechi ya kimataifa dhidi ya Burundi itakayochezwa leo.
Timu hiyo ambayo jana asubuhi ilifanya mazoezi kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, ilitua Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) juzi kwa ndege ya Fastjet saa 12.30 jioni na kwenda moja kwa moja kambini hoteli ya Tansoma.
Nayo timu ya Taifa ya Burundi ilitua nchini jana saa 10 jioni kwa ndege ya RwandAir. Kikosi hicho kitafikia hoteli ya Tiffany Diamond kitakwenda moja kwa moja Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam ambapo kitafanya mazoezi kuanzia saa 11 jioni.
Kiingilio cha mechi kati ya Tanzania na Burundi itakayochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia saa 10 jioni kitakuwa sh. 3,000 kwa viti vya raungi ya chungwa, bluu na kijani wakati VIP B na C ni sh. 5,000 tu.
MICHUANO YA TAIFA YA KOMBE LA WANAWAKE KUANZA DESEMBA 28
Michuano ya Taifa ya mpira wa miguu kwa wanawake ya Proin Women Taifa Cup inaanza rasmi Desemba 28 mwaka huu kwa mechi ya ufunguzi kati ya timu za mikoa ya Mara na Mwanza itakayochezwa Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.
Kombaini za mpira wa miguu za mikoa yote ya Tanzania Bara zitashiriki mashindano hayo yatakayochezwa kwa raundi mbili mwanzoni, na baadaye hatua ya robo fainali hadi fainali.
Mashindano hayo yanayodhaminiwa na kampuni ya Proin Promotions Limited, kuanzia hatua ya robo fainali, mechi zote zitafanyika jijini Dar es Salaam.
Meneja Biashara wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania, Peter Simon Shankunkuli aliishukuru kampuni ya Proin ambao ni watengenezaji, wazalishaji na wasambazaji wa filamu za kitanzania kwa kuwezesha mashindano hayo kufanyika kwa mara ya kwanza.
Proin Promotions imekua ikivumbua vipaji mbalimbali vya uigizaji na sasa imeamua kujikita katika mpira wa miguu ili kuweza kuvumbua vipaji kwa wachezaji wa kike.
Shankunkuli alisema nafasi bado zipo kwa wadhamini watakaoguswa na mashindano hayo, kwa kuwasiliana na TFF au Proin Promotions Limited kwa maelezo zaidi.
Friday, December 5, 2014
JUMA NYOSO AJIUNGA NA MBEYA CITY
Mlinzi wa kati Juma Nyosso amejiunga na kikosi cha Mbeya City Fc kwa mkataba wa mwaka mmoja.
Akizungumza mara baada ya kuisaini mkataba huo kwenye ofisi za timu zilizopo jengo la Mkapa Hall jijini Mbeya, Nyoso aliyewahi kucheza kwenye timu za Ashanti United, Simba na Coastal Union, alisema amekubari kujiunga na City kwa mkataba wa mwaka mmoja kwa imani kuwa utatosha kuushawishi uongozi wa timu kumpa mkataba mrefu zaidi mara baada ya huu wa sasa.
“City ni timu nzuri na imekuwa hivyo toka ilipoanzishwa miaka minne iliyopita, matokeo yaliyoo sasa ni sehemu ya soka ambayo timu yoyote inaweza kuyapata, nimekubari kujiunga na timu kwa mkataba wa mwaka mmoja kwa sababu naamini uwezo wangu uwanjani utawashawishi viongozi kunipa mkataba mrefu zaidi pindi huu utakapo malizika na nina amini hili linawezekana kwa sababu nataka kukaa kwenye timu hii mpaka mpira wangu utakapoisha” alisema Nyosso
Akiendelea zaidi beki huyo aliyewahi pia kucheza kwenye kikosi cha timu ya Taifa ‘Taifa Stars’ alisema kuwa mafanikio iliyopata Mbeya City msimu uliopita yamekuwa sababu kubwa ya yeye kukubari kujiunga na City huku akiamini kuwa amekuja kuongeza nguvu kwenye timu bora ili kuhakikisha mafanikio ya msimu uliopita yanafanikiwa tena.
K wa upande wake Katibu Mkuu wa City Emmanuel Kimbe alimshukuru Nyosso kwa kukubari kujiunga na timu hii huku akiamini kuwa uzoefu alionao mchezaji huyo utasaidia kuimarisha safu ya ulinzi kwenye kikosi cha City.
“Tunamshukuru kukubari kujiunga nasi, imani yetu kubwa kwamba uzoefu alionao utasaidia kuimarisha safu yetu ya ulinzi, hasa ukizingatia matokeo tuliyopata katika michezo saba ya mwanzo wa Ligi hii” alisema Kimbe huku kauli yake hiyo ikiungwa mkono na Kocha Mkuu Juma Mwambusi.
Kwa sasa Nyosso tayari yuko na kikosi cha City kilichosafiri kwenda mjini Songea kwa ajiri ya michezo ya kirafiki.
SIMBA, YANGA KUKIPIGA DESEMBA 13 MECHI YA NANI MTANI JEMBE
Mechi ya Nani Mtani Jembe 2 kati ya Simba na Yanga zinazodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager itachezwa Jumamosi, Disemba 13, 2014 saa kumi kamili jioni kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Meneja Udhamini wa TBL, George Kavishe amesema kwamba “Tayari Simba na Yanga zimesaini makubaliano ya kucheza mechi ya Nani Mtani Jembe 2 (Nani Mtani Jembe 2 Match). Pambano hili ni zawadi ya kufungia mwaka kwa mashabiki na kila timu imetia saini makubaliano kwamba itachezesha kikosi cha kwanza ili kuwapa mashabiki burudani ya uhakika.”
Kavishe aliongeza kuwa mechi hii ni maalumu kwa ajili ya kuhitimisha kampeni ya Nani Mtani Jembe 2 ambayo imeendeshwa kwa zaidi ya miezi miwili ikiwapa fursa mashabiki wa timu hizi kuchangia timu zao kila wanapoburudika na bia ya Kilimanjaro Premium Lager.
Alisema Nani Mtani Jembe 2 inahusisha mashabiki wa klabu za Simba na Yanga ambapo zawadi ya shilingi milioni 100 itatolewa na kugawanywa ifuatavyo.
Shilingi Milioni 20 ni zawadi ya mechi ya Nani Mtani Jembe ambapo timu itakayoshinda itapata sh milioni 15 na timu itakayofungwa itapata shilingi milioni 5.
Kampeni hii inaendeshwa kwa njia ya sms ambapo mashabiki wanapiga kura kwa njia ya sms na shilingi milioni 80 zimegawanywa kati ya timu hizo mbili ambapo kila timu ilianza na shillingi milioni 40 kwenye benki maalumu mtandaoni.
Meneja wa Bia ya Kilimanjaro Premium Lager, Pamela Kikuli alisema mashabiki wa Simba na Yanga wanaweza kushiriki kwa kununua bia ya Kilimanjaro Premium Lager yenye ujazo wa mililita 500 ambapo mteja atabandua ganda la kizibo cha bia ya Kilimanjaro Premium Lager na kuona namba maalumu. Ataandika jina la timu yake (SIMBA au YANGA) ikifuatiwa na namba hiyo ya kwenye kizibo ambayo anatuma kwenda namba 15415 na kwa kufanya hivyo anakuwa amepunguza pesa taslimu shilingi 10,000 kutoka timu pinzani na kuichangia timu yake.
Kikuli pia alizikabidhi timu hizo jezi maalumu itakayovaliwa mahususi kwa ajili ya mechi hiyo na kuwahimiza mashabiki waendelee kuzipigia kura timu zao na kikubwa kuhakikisha wanafika uwanja wa taifa na kujionea wenyewe pambano hilo ambalo lazima mshindi apatikane.
Mkurugenzi wa Mashindano wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Boniface Wambura aliwakaribisha mashabiki na kuwaomba wajitokeze kwa wingi kwani hivi sasa timu hizo ziko kambini zikijiandaa na mtanage huo wa kukata na shoka unaotarajiwa kuwa na msisimko mkubwa.
Alitaja viingilio vya mechi hiyo kuwa ni shilingi 30,000 kwa VIP B, 20,000/= VIP C, 15,000/= kwa viti vya rangi ya chungwa kiingilio kitakuwa ni sh 15,000 huku viti vya bluu na kijani tiketi zikiuzwa kwa sh. 7,000/=.
Wambura alisema pambano hilo litakalosimamiwa na TFF litaanza saa kumi kamili na litachezwa kwa dakika 90 tu ambapo kama muda huo timu hizo hazitafungana basi mikwaju ya penati itapigwa ili mshindi apatikane.
Taji la Nani Mtani Jembe linashikiliwa na Simba ambao waliwafunga mahasimu wao 3-1 katika mechi iliyochezwa Disemba 21, 2013.
MANDAWA MCHEZAJI BORA WA LIGI KUU NOVEMBA
Mshambuliaji wa timu ya Kagera Sugar ya mkoani Kagera amechaguliwa kuwa mchezaji bora wa Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kwa mwezi Novemba mwaka huu ambapo atazawadiwa kitita cha sh. milioni moja.
Mandawa ambaye kwa mwezi huo alichuana kwa karibu na mshambuliaji Fulgence Maganda wa Mgambo Shooting ya Tanga na nahodha wa Simba, Joseph Owino atakabidhiwa zawadi yake na wadhamini wa ligi hiyo kampuni ya Vodacom.
Hafla ya kukabidhi zawadi hiyo inatarajiwa kufanyika wakati wa mechi ya raundi ya nane ya ligi hiyo kati ya Simba na Kagera Sugar itakayochezwa Desemba 26 mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
KOZI YA UKUFUNZI WA UTAWALA YA FIFA SASA MACHIShirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) limesogeza mbele kozi ya ukufunzi ya utawala wa mpira wa miguu iliyokuwa ifanyika Desemba mwaka huu jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa FIFA, kozi hiyo sasa itafanyika Machi mwakani katika tarehe itakayotangazwa baadaye.
TFF imepokea maombi ya zaidi ya washiriki 40 kwa ajili ya kozi hiyo itakayoshirikisha washiriki 30. Kutokana na maombi kuzidi idadi ya nafasi zilizopo, FIFA itafanya mchujo wa washiriki. MIKOA MITANO YATAKIWA KUWASILISHA USAJILI COPA 2014
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limeitaka mikoa mitano kuwasilisha usajili wa wachezaji wake kwa ajili ya mashindano ya Taifa ya Copa Coca-Cola 2014 kabla ya Desemba 5 mwaka huu.
Mikoa hiyo ambayo haijawasilisha usajili wake hadi sasa kwa ajili ya michuano hiyo inayoanza Desemba 13 mwaka huu jijini Dar es Salaam ni Arusha, Dodoma, Katavi, Kusini Pemba, Kusini Unguja, Mjini Magharibi na Simiyu.
Kwa mujibu wa Kamati ya Mashindano ya michuano hiyo, mkoa ambao hautawasilisha usajili wake kwa ajili ya uhakiki wa umri wa wachezaji utakaonza Desemba 10 mwaka huu utaondolewa katika fainali hizo zitakazomalizika Desemba 20 mwaka huu.
Wachezaji watakaobainika kuzidi umri hawataruhusiwa kushiriki katika michuano hiyo inayoshirikisha wachezaji wenye umri chini ya miaka 15. Kwa mujibu wa Kanuni ya 29 ya michuano kuhusu idadi ya wachezaji, kila timu inatakiwa kuwa na wachezaji wasiozidi 20 na wasiopungua 16.
Hivyo, kila timu inatakiwa kuhakikisha inakuwa na idadi hiyo ya wachezaji, kwani kikanuni wakipungua 16 itaondolewa kwenye mashindano.
Timu 16 kwa upande wa wavulana zitashiriki katika fainali hizo wakati kwa upande wa wasichana ni timu nane. Mikoa iliyoingiza timu za wasichana kwenye fainali hizo ni Arusha, Dodoma, Ilala, Kinondoni, Mbeya, Mwanza, Temeke na Zanzibar.
KIKOSI CHA MABORESHO TAIFA STARS CHAINGIA KAMBINI
Kikosi cha Taifa Stars Maboresho kimeingia kambini leo (Desemba 1 mwaka huu) Bulyanhulu mkoani Shinyanga kujiandaa kwa mechi ya kirafiki dhidi ya Burundi itakayochezwa Desemba 9 mwaka huu jijini Dar es Salaam.
Ikiwa chini ya Kocha Mart Nooij, Stars Maboresho itapiga kambi mkoani humo hadi Desemba 6 mwaka huu ambapo itarejea jijini Dar es Salaam tayari kwa ajili ya mechi hiyo itakayochezwa Uwanja wa Taifa.
Wachezaji walioingia kambini ni Abubakar Ally (Coastal Union), Abubakar Ally Mohamed (White Bird), Aishi Manula (Azam), Andrew Vicent (Mtibwa Sugar), Atupele Green (Kagera Sugar), Edward Charles (Yanga) na Emmanuel Semwanda (African Lyon).
Gadiel Michael (Azam), Hashim Magoma (Stand United), Hassan Banda (Simba), Hassan Mwasapili (Mbeya City), Joram Mgeveke (Simba), Kassim Mohamed Simbaulanga (African Lyon), Kelvin Friday (Azam) na Makarani Ally (Mtibwa Sugar).
Miraji Adam (Simba), Mohamed Hussein (Simba), Muzamir Ally (Mtibwa Sugar), Omari Nyenje (Ndanda), Pato Ngonyani (Yanga), Rashid Mandawa (Kagera Sugar), Said Hamisi (Simba), Salim Hassan Mbonde (Mtibwa Sugar) na Shiza Ramadhan (Mtibwa Sugar).
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linaishukuru kampuni ya kuchimba madini ya Acacia Mining PLC (zamani African Barrick Gold PLC) kwa kufadhili kambi ya Stars kupitia mgodi wa Bulyanhulu.
Wednesday, November 26, 2014
SAAD KAWEMBA MTENDAJI MKUU MPYA AZAM
KLABU bingwa ya Tanzania Bara, Azam FC imemuajiri Mkurugenzi wa zamani wa Mashindano wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Saad Kawemba kuwa Mtendaji wake Mkuu.
Mwenyekiti wa Azam FC, Sheikh Said Muhammad amemtambulisha rasmi leo Kawemba mbele ya wachezaji na viongozi, makao makuu ya klabu Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam, baada ya mazoezi ya asubuhi.
“Nafurahi kupata nafasi hii, ni fursa nyingine tena ya kupata uzoefu mwingine katika uongozi wa soka baada ya kufanya kazi kwa mafanikio TFF,”amesema Kawemba.
Bodi ya Ukurugenzi ya Azam FC imefikia hatua ya kuajiri Mtendaji Mkuu, ili kurahisisha uendeshaji ndani ya klabu kwa lengo la kutafuta ufanisi zaidi.
Kawemba amesema anatarajia kupata ushirikiano mzuri kutoka kwa Bodi, Menejimenti na wafanyakazi wote wa klabu hiyo bingwa Tanzania Bara. “Nimekuja hapa kusaidia kusukuma mbele gurudumu la maendeleo la Azam FC, natarajia ushirikiano wa wote,”amesema.
Tuesday, November 25, 2014
PONDAMALI AMCHANACHANA KASEJA
KOCHA wa makipa wa Yanga, Juma Pondamali 'Mensah' amemtaka kipa nguli nchini, Juma Kaseja, kuacha kutafuta mchawi baada ya kukosa namba katika kikosi hicho.
Kauli ya Pondamali imekuja siku chache baada ya Kaseja kukaririwa na vyombo vya habari akidai kocha huyo ni chanzo cha kukosa namba Yanga.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Pondamali, alisema kuwa kipa huyo amekosa namba mbele ya Deogratius Munishi 'Dida' baada ya kiwango chake kuporomoka.
Alisema nahodha huyo wa zamani wa Simba alikosa namba baada ya kuzembea katika mazoezi, hivyo hana sababu ya kutafuta mchawi.
Pondamali, alisema mchezaji huyo anatakiwa kuondoka kwa amani Yanga kurejea katika klabu yake ya zamani Simba.
Simba imeanza mazungumza ya kumsajili Kaseja katika usajili wa dirisha dogo lililofunguliwa Novemba 20 hadi Desemba 20, mwaka huu.
Kipa huyo wa zamani aliyekuwa na mbwembwe uwanjani, alidokeza kuwa Kaseja, alianza kupoteza namba Yanga ilipokuwa chini ya kocha Hans van der Pluijm.
"Nashangaa sana kwanini nahusishwa na sakata hili wakati anayepanga timu ni kocha (Marcio) Maximo, yeye ndiye msimamizi mkuu wa mazoezi," alisema Pondamali.
Alisema muda mfupi baada ya Maximo kujiunga na Yanga kuchukua nafasi ya Pluijm, alitaka kufahamu sababu za kipa huyo kutokuwemo katika kikosi cha Taifa Stars.
Kocha huyo alisema msingi wa swali la Maximo, lilikuwa ni kutaka kujua kwanini Kaseja hachezi timu ya taifa kwa kuwa hadi anaondoka nchini kurejea Brazil alikuwa kipa namba moja.
Maximo, aliwasili nchini mwaka 2006 kuinoa Taifa Stars hadi 2010 ambapo mkataba wake ulimalizika kabla ya kurejea kuifundisha Yanga mapema mwaka huu.
Katika kipindi hicho Kaseja, aliwahi kuingia matatani na Maximo, baada ya Maximo kudai alishangilia mabao manne aliyofungwa hasimu wake, Ivo Mapunda kwenye moja ya mechi za kimataifa.
Maximo, alimuengua Kaseja katika kikosi cha kwanza na kumpa nafasi Ivo katika mechi za kimataifa za Taifa Stars.
Hivi karibuni mchezaji huyo ameibua mzozo na Yanga akidai alipwe sh. milioni 20 zilizobaki katika usajili ambazo Yanga ilitakiwa kumlipa Januari, mwaka huu.
Hata hivyo, Katibu Mkuu wa Yanga, Benno Njovu, amedai mchezaji huyo haidai Yanga fedha za usajili.
KIEMBA: NIMEKUJA AZAM KUTAFUTA MAISHA
MSHAMBULIAJI wa zamani wa klabu ya Simba, Amri Kiemba, amesema kwenda kwake Azam ni kwa ajili ya kutafuta maisha yake kwani maisha popote sio sehemu moja.
Kiemba ameyasema hayo baada ya kusaini mkataba wa kuitumikia Azam na kudai kuwa ataitumikia kwa moyo mmoja timu hiyo.
Akizungumza na mwandishi wetu kiemba alisema, japokuwa ameichezea simba kwa muda mrefu lakini amepiti changamoto nyingi kama kuambiwa kiwango kimeshikaa mara mzee.
"Changamoto zipo lakini nimeyavumuila mengi ila kwa sasa nashukuru kwamba nimeenda sehemu salama na nitahakikisha kuwa nitaonyesha ujuzi wangu wote na kuitumikia vyema timu yangu mpya,"alisema
Alisema kuwa kila mtu yupo kwa ajili ya kutafuta maisha kwa hiyo ikitokea nafasi kama hiyo hainahaja kuicha ukizingatia kwamba azam pia ni timu bora na inawachezaji bora.
Kiemba alisema kuwa timu kubwa zinakuwa na changamoto nyingi mno hivyo uvumilivu na ujasiri ndio ulio mfikisha hapo alipo.
Aliwataka mashabiki wake wasiwe na wasiwasi na yeye kwani ataendelea na kasi yae ileile pia atakuzidisha ili kuhakikisha kila mechi anapangwa katika kikosi cha kwanza.
"Nitajitahidi kufanya mazoezi kwa bidii ili kuwahakikisha kuwa napata nafasi ya kwanza katika kikosi cha mwalimu,"alisema
KIIZA ATEMWA YANGA, NAFASI YAKE KUCHUKULIWA NA MZAMBIA
HATIMAYE Marcio Maximo, amekata mzizi wa fitina baada ya kumtema mshambuliaji wa kimataifa, Hamisi Kiiza katika kikosi hicho.
Mchezaji huyo wa kimataifa wa Uganda ametemwa na nafasi yake inatarajiwa kujazwa na Mzambia Jonas Sakuwaha.
Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), limetangaza dirisha dogo la usajili kuwa Novemba 20 hadi Desemba 20, mwaka huu.
Maximo, alitarajia kuwasili jana usiku kutoka Brazil alikokwenda kwa mapumziko baada ya michuano ya Ligi Kuu Tanzania Bara kusimama kwa muda.
Habari za ndani kutoka Yanga zilidokeza kuwa kocha huyo amemuondoa, Kiiza, katika usajili wake kwa ajili ya kujiwinda na ubingwa wa Tanzania Bara msimu huu.
Chanzo hicho cha uhakika kilisema, Sakuwaha, anatarajia kuwasili nchini wiki hii kufanya majaribio kabla ya kupewa mkataba endapo atamridhisha Maximo.
"Kocha ametoa maagizo kwa uongozi kumuengua (Hamisi) Kiiza na nafasi yake kujazwa na Mzambia wa TP Mazembe," alidokeza kigogo huyo.
Alisema ripoti ya Maximo ilitoa mapendekezo ya mchezaji huyo kutemwa kabla ya kuondoka nchini kwa mapumziko ya muda mfupi.
Sekuwaha, anatajwa kuwa mmoja wa washambuliaji hodari wa TP Mazembe, lakini Maximo, anataka kuona kipaji chake kwenye mazoezi kabla ya kumsajili.
Straika huyo anakuwa mchezaji wa pili wa kimataifa wa Yanga kuwania usajili katika dirisha dogo akiungana na Emerson De Oliveira Neves Rouqe kutoka Brazil.
Hivi karibuni Yanga ilisema Maximo anatarajia kuwasili nchini na siri nzito kuhusu mikakati yake ya usajili.
Sunday, November 23, 2014
JAJA AITOSA YANGA, YAMNASA MBRAZIL MWINGINE, KIUNGO MKABAJI EMERSON
Kiungo mkabaji raia wa Brazil Emerson De Oliveira Neves Rouqe anatarajiwa kuwasili siku ya jumanne mchana jijini Dar es salaam kwa ajili ya majaribio katika klabu ya Young Africans na endapo atafuzu moja kwa moja atajiunga na mabingwa mara 24 wa Ligi Kuu Tanzania bara.
Emerson mwenye umri wa miaka 24 ambaye kwa sasa anachezea timu ya Bonsucesso FC iliyopo ligi daraja la pili nchini kwao Brazil, msimu uliopita alikuwa akicheza soka la kulipwa nchini Poland katika timu ya Piotrkow Trybunalski FC iliyopo Ligi Daraja la pili nchini humo.
Ujio wa Emerson kuja kufanya majaribio nchini unakuja kufuatia mshambuliaji wa kimataifa kutoka nchini Brazil pia Geilson Santos "Jaja" kushindwa kurejea nchini baada ya kwenda kwao Brazil na kutoa taarifa kwamba hataweza kurejea tena nchini kutokana kukabiliwa na matatizo ya kifamilia.
Awali ilikua familia ya Jaja ije nchini katika kipindi cha mapumziko, lakini waliomba yeye Jaja ndio aende Brazil na mara baada ya kufika huko matatizo ya kifamilia aliyokutana nayo yamepelekea kushindwa kurejea nchini kuitumikia klabu yake na kuomba abakie kwao kwa ajili ya kutatua matatizo hayo.
Kuondoka kwa Jaja kunafanya klabu ya Young Africans kubakia na wachezaji wanne tu wa kimataifa ambao ni Mbuyu Twite, Haruna Niyonzima, Hamis Kizza na Andrey Coutinho hivyo endapo Emerson atafuzu atakua anakamilisha idadi ya wachezaji watano wa kimataifa
Endapo Emerson atafuzu majaribo pamoja na vipimo atajiunga na kikosi cha kocha mbrazil Marcio Maximo katika nafasi ya kiungo mkabaji ikiwa ni sehemu ya kuboresha timu kuelekea kwenye michezo ya Ligi Kuu ya Vodacom pamoja na mashindano ya kimataifa.
Aidha kikosi cha Young African baada ya kuwa mapumzikoni kwa takribani wiki mbili, kinatarajiwa kuanza mazoezi siku ya jumatatu katika Uwanja wa shule ya sekondari Loyola kujiandaa na mchezo wa Nani Mtani Jembe pamoja na mzunguko wa nane wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania bara.
Thursday, November 20, 2014
BURIANI SWAHIBA WANGU INNOCENT MUNYUKU
HAIKUWA rahisi kuamini, lakini ukweli ni kwamba mwandishi maarufu wa habari za michezo nchini, Innocent Munyuku, amefariki dunia.
Munyuku alifariki dunia jana alfajiri nyumbani kwake Kimara Kibo Dar es Salaam. Alifariki akiwa usingizini.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa familia yake, mwili wa marehemu Munyuku unatarajiwa kusafirishwa kesho kwenda Mazimbu mkoani Morogoro kwa ajili ya mazishi. Mazimbu ndiko anakoishi mama yake mzazi, ambaye ni mkufunzi katika Chuo Kikuu cha Mzumbe.
Taarifa za kifo cha Munyuku zilipokelewa kwa mshtuko mkubwa. Wafanyakazi wenzake wa Kampuni ya New Habari, inayochapisha magazeti ya Mtanzania, Rai, Dimba na Bingwa, hawakuamini masikio yao baada ya kupata taarifa hizo.
Wapo waliozungumza na kuchati naye kwa simu hadi saa nne usiku juzi. Pia aliposti ujumbe wa aina mbalimbali kwenye mtandao wa facebook, ukiwemo ujumbe unaohusu masuala ya dini ya kikristo. Katika ujumbe wake wa mwisho, aliandika 'Usiku mwema'.
Mmoja wa wafanyakazi wenzake, Jimmy Chika, ambaye ni Mhariri wa gazeti la Dimba, anasema alitumiwa ujumbe na Munyuku, akimueleza kwamba amepata fedha alizoomba ofisini hivyo mambo yake yalikuwa safi.
Karibu kila mmoja aliyezungumza ama kuchati na Munyuku juzi, alisimulia kile walichozungumza naye. Zilikuwa simulizi za kuhuzunisha na kusikitisha. Hakuna anayeweza kutabiri ni lini ataondoka hapa duniani. Ni siri kubwa, ambayo imefichwa na Mwenyezi Mungu.
Mwanahabari mkongwe Abubakar Liongo aliandika kwenye mtandao wa facebook jana akisema:
" Japo lazima sote siku tutaipa kisogo dunia hii ya manani, lakini hakika habari za kifo cha comrade Innocent Munyuku, zimenistua sana. Si zaidi ya wiki nikiwa Dodoma, tulikuwa tukichati kupitia FB,tukitaniana kama kawaida yetu. Hakika kifo hakina hodi.Munyuku au Gaitanoama, tulivyokuwa tukiitana, umeondoka mapema ndugu yangu kama walivyoondoka Conrade Dunstan (kiona mbali) na Dan Mwakiteleko (mullah) na kuiachia pengo tasnia ya habari.".
Mwani Nyangasa naye aliandoka: "Ni vigumu kuamini, naona shida kuzungumzia kwa kuwa ni kitu ambacho sikiamini. Eti leo kaka zangu Innocent Munyuku na Baraka Karashani hatunao, wamekufa siku moja. Juzi nilipata taarifa za kuumwa Baraka, jana nikaenda hospitali na dada yangu Grace Hoka kumuangalia, tulitokwa na machozi. Baraka hakuwa na hali nzuri, tukajipa moyo atapona na tukamfariji mkewe kuwa asife moyo, Baraka atakuwa na nguvu, nikaondoka, Leo asubuhi naamshwa na simu eti Innocent amefariki nilipigwa na butwaa."
Kwa upande wake, Charles Mateso, alisimulia jinsi alivyokwenda ofisini kwa Munyuku, akamkosa, wakakutana siku inayofuata, wakazungumza mambo mbalimbali na kupanga kuyatekeleza jana, lakini Mungu hakupenda. Amemchukua Munyuku.
Binafsi nilipata taarifa za kifo cha Munyuku kupitia kwa Grace Hoka, Mhariri wa gazeti la Bingwa. Alinipigia simu saa 1.30, asubuhi na kuzungumza maneno matatu. Alisema: "Kaka Zahor, Munyuku amefariki." Akakata simu huku akiangua kilio.
Sikuamini masikio yangu. Nikakaa na kutafakari kwa sekunde kadhaa. Baada ya muda, nikaamua kupiga namba ya simu ya Munyuku. Ilipokelewa na mwanamke mmoja, ambaye naye alitamka maneno machache. Alisema: "Mwenye simu hii amefariki."
Nikamuuliza: "Amefariki lini?"
Akasema: "Leo alfajiri."
Nikaendelea kumuuliza: "Wewe ni nani?"
Akajibu: "Mimi mpangaji mwenzake."
Baada ya maneno hayo, yule dada alikata simu. Nadhani alichoshwa kupokea simu kutoka kwa watu mbalimbali waliokuwa wakiulizia taarifa za kifo cha mwanahabari huyo.
Nilipata uthibitisho zaidi wa kifo cha Munyuku baada ya kuelezwa na baadhi ya wafanyakazi wenzake kwamba, maofisa wa New Habari walikwenda nyumbani kwake na kuukuta mwili wake ukiwa bado kitandani kama alivyokuwa amelala. Wakauchukua na kuupeleka hospitali, bila shaka kwa lengo la kutaka kujiridhisha kuhusu sababu za kifo chake.
Hivyo ndivyo taarifa za kifo cha Munyuku zilivyoanza kusambaa katika vyombo mbalimbali vya habari. Taarifa zilizopokelewa kwa majonzi makubwa na wanahabari wengi waliomfahamu, hasa kutokana na ucheshi na vituko vyake, achilia mbali utendaji wake mzuri wa kazi.
Nilianza kumfahamu Munyuku tangu mwanzoni mwa miaka ya 2000. Wakati huo alikuwa akiandikia magazeti mbalimbali. Alipenda kuniita kaka na mimi nilipenda kumwita 'kamanda'. Tuliitana hivyo kila tulipozungumza kwa simu au tulipokutana, hasa katika vikao vya nje ya kazi.
Nilianza kuwa naye karibu mwaka 2006, wakati yeye na swahiba wake mkubwa, Charles Mateso, walipoajiriwa na Kampuni ya Uhuru Publications Ltd, inayochapisha magazeti ya Uhuru, Mzalendo na Burudani. Kuajiriwa kwao kulilenga kuliendesha gazeti la Burudani.
Walifanyakazi pamoja kwa kipindi kisichopungua miaka miwili. Baada ya muda huo, wote wawili waliamua kuacha kazi kwa pamoja. Sababu za kufanya hivyo walizijua wenyewe.
Kwa uchapakazi, Munyuku alikuwa na sifa za aina yake. Hakutaka utani katika kazi. Na kila alipokuwa 'bize', hakupenda usumbufu kutoka kwa mtu yeyote. Akiona unamsumbua, atakwambia 'kamanda niache kwanza nimalize kazi, tutaongea baadae.'
Munyuku pia alikuwa mbunifu mzuri. Nakumbuka yeye na Mateso walifanikiwa kubadili sura ya gazeti la Burudani hadi likawa na mvuto wa aina yake. Walianzisha 'kolamu' nyingi zenye kusisimua na ambazo zinapendwa na vijana. Waliliweka gazeti hilo kwenye matawi ya juu.
Hatimaye Munyuku ametutoka. Ametangulia kwenda kule ambako, sisi viumbe wote wa Mwenyezi Mungu lazima tutakwenda. Maana yamenena maandiko matakatifu kwamba, 'Kila chenye roho, lazima kitaonja mauti.'
Buriani Innocent Munyuku. Tunamuomba Mwenyezi Mungu akupe mapumziko mema.
Wakati huo huo, habari zingine za kusikitisha zilizopatikana jana jioni zimeeleza kuwa, mwanahabari mwingine maarufu wa michezo, Baraka Karashani, amefariki dunia.
Baraka alifariki jana mchana kwenye hospitali ya Jeshi ya Lugalo, Dar es Salaam, alikokuwa amelazwa kwa siku kadhaa.
LIGI YA SDL KUANZA KUTIMUA VUMBI DESEMBA 6
Michuano ya Ligi Daraja la Pili (SDL) msimu huu iliyokuwa ianze kutimua vumbi Novemba 22 mwaka huu kwa mechi kumi katika viwanja vitano tofauti imesogezwa mbele hadi Desemba 6 mwaka huu.
Mechi hizo zimesogezwa ili kutoa fursa ya kukamilisha maandalizi mbalimbali ya ligi hiyo inayoshirikisha timu 24 kutoka mikoa mbalimbali ya Tanzania Bara.
Mikoa yenye timu katika ligi hiyo ni Arusha, Dar es Salaam, Dodoma, Iringa, Katavi, Kigoma, Lindi, Mara, Mbeya, Morogoro, Mwanza, Njombe, Pwani, Rukwa, Ruvuma, Shinyanga, Singida na Tabora.
MASHINDANO YA TAIFA U12 YASOGEZWA
Mashindano ya Taifa kwa vijana wenye umri chini ya miaka 12 yanayoshirikisha kombaini za mikoa yote ya Tanzania yatafanyika jijini Mwanza kuanzia Desemba 30 mwaka huu hadi Januari 5 mwakani.
Awali mashindano hayo yalipangwa kuanza Desemba 6 mwaka huu, lakini yamelazimika kuyasogeza ili kutoa fursa ya kukamilika kwa matengenezo ya viwanja vitatu ambayo vitatumika.
Kila timu ya mkoa inatakiwa kuwa na ujumbe wa watu 16, wakiwemo wachezaji 14 na makocha wawili katika mashindano hayo ya timu yenye wachezaji saba (7 aside).
Timu zinatakiwa kuwasili jijini Mwanza kuanzia Desemba 28 mwaka huu tayari kwa ajili ya uhakiki wa umri na taratibu nyingine za mashindano. Timu zote zitafikia katika shule ya Alliance (Alliance Schools).
Wachezaji wanaotakiwa kushiriki mashindano hayo ni wenye umri chini ya miaka 12, hivyo ni wale waliozaliwa kuanzia Januari 2003 na kuendelea.
TASWA YATUMA RAMBIRAMBI VIFO VYA MUNYUKU, KARASHANI
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limepokea kwa masikitiko vifo vya waandishi wa habari Innocent Munyuku na Baraka Karashani vilivyotokea jana (Novemba 19 mwaka huu) jijini Dar es Salaam.
Msiba huo ni mkubwa katika familia ya mpira wa miguu, na tasnia ya habari nchini kwa ujumla kutokana na mchango mkubwa waliotoa katika ustawi wa mpira wa miguu nchini kupitia kalamu zao.
Munyuku alikuwa mmoja wa waandishi waanzilishi wa gazeti la Mwanaspoti wakati Karashani kwa nyakati tofauti alifanya kazi katika vyombo mbalimbali vya habari ikiwemo kampuni ya New Habari 2006 akiripoti habari za mpira wa miguu.
Tunatoa pole kwa familia za marehemu, Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA), na kampuni ya New Habari 2006 na kuwataka kuwa na subira na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu cha msiba huo mzito.
Bwana alitoa, Bwana ametwaa. Jina lake lihimidiwe.
Msiba huo ni mkubwa katika familia ya mpira wa miguu, na tasnia ya habari nchini kwa ujumla kutokana na mchango mkubwa waliotoa katika ustawi wa mpira wa miguu nchini kupitia kalamu zao.
Munyuku alikuwa mmoja wa waandishi waanzilishi wa gazeti la Mwanaspoti wakati Karashani kwa nyakati tofauti alifanya kazi katika vyombo mbalimbali vya habari ikiwemo kampuni ya New Habari 2006 akiripoti habari za mpira wa miguu.
Tunatoa pole kwa familia za marehemu, Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA), na kampuni ya New Habari 2006 na kuwataka kuwa na subira na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu cha msiba huo mzito.
Bwana alitoa, Bwana ametwaa. Jina lake lihimidiwe.
Monday, November 17, 2014
TFF YAIPONGEZA SAFA
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limetoa pongezi kwa Chama cha Mpira wa Miguu Afrika Kusini (SAFA) kufuatia timu yake ya Taifa (Bafana Bafana) kufuzu kucheza fainali zijazo za AFCON nchini Equatorial Guinea.
Afrika Kusini iliifunga Sudan mabao 2-1, hivyo kufuzu kabla ya kukamilisha michezo yote. Bafana Bafana bado imebakiza mchezo mmoja katika hatua hiyo.
Wakati huo huo, TFF imeipeleka barua ya shukrani kwa Chama cha Mpira wa Miguu Afrika Kusini (SAFA) kwa kufanikisha kambi ya Taifa Stars nchini humo kabla ya kwenda kucheza Swaziland.
SAFA ilitoa viwanja vya mazoezi kwa Taifa Stars na usafiri wa basi la kisasa kutoka Johannesburg kwenda Swaziland na kurudi, hivyo kuokoa zaidi ya dola 15,000 ambazo TFF ingetumia kama ingegharamia yenyewe safari hiyo au kuweka kambi ya timu hiyo nyumbani.
Awali Benchi la Ufundi la Taifa Stars chini ya Kocha Mart Nooij lilipendekeza timu kufika Swaziland mapema au kuweka kambi nchini Afrika Kusini. SAFA ikajitolea kusaidia kambi hiyo.
Pia TFF inakanusha madai ya gazeti moja la kila siku lililodai kuwa wakaguzi wa Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) wamevamia/wamefanya ukaguzi wa siri kukagua fedha za udhamini wao kwa Taifa Stars.
Ukaguzi wa hesabu ni utaratibu wa kawaida wa kila robo ya mwaka wa fedha. TFF ndiyo huwaalika TBL kutuma wakaguzi wao ili kuhakiki vitabu vya fedha. Uhusiano kati ya TFF na TBL ni mzuri, na kila kinachofanyika ni kwa nia njema kwa makubaliano ya pande zote mbili.
NGASA AFUNGA NDOA NA LADHIA
MSHAMBULIAJI wa Taifa Stars na Yanga SC, Mrisho Ngassa mwishoni mwa wiki iliyopita alifunga ndoa ya pili na Ladhia Mngazija eneo la Tegeta jijini Dar es Salaam.
STARS YATOKA SARE NA SWAZILAND
TIMU ya soka ya Taifa, Taifa Stars jana ilitoka sare yabao 1-1 na Swaziland katika mechi ya kirafiki ya kimataifa iliyochezwa kwenye uwanja wa Somhlolo mjini Mbabane.
Katika mechi hiyo iliyokuwa kwenye kalenda ya Shirikisho la Soka Tanzania (FIFA), Swaziland ilikuwa ya kwanza kupata bao kipindi cha kwanza kabla ya Thomas Ulimwengu kuisawazishia Taifa Stars kipindi cha pili.
Taifa Stars ilifanikiwa kupata penalti dakika 10 za mwisho wakati beki mmoja wa Swaziland alipounawa mpira wa krosi uliopigwa na Oscar Joshua, lakini shuti la Ulimwengu lilitoka pembeni ya lango.
Thursday, November 13, 2014
KASEJA RUDI SIMBA- ZACHARIA HANSPOPE
KIPA nguli wa zamani wa Simba, ambaye kwa sasa yupo kikosi cha Yanga, Juma Kaseja, ameitwa kwenye timu yake hiyo ya zamani.
Simba imeamua kumuita Kaseja kutokana na kukosa namba kwenye kikosi cha kwanza cha Yanga, inayonolewa na Mbrazil, Marcio Maximo.
Klabu hiyo imetoa baraka kwa nahodha wake huyo wa zamani kurejea mtaa wa Msimbazi, endapo mambo yataendelea kuwa magumu kwake Yanga.
Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia Hanspope, alisema jana kuwa, Kaseja ni mtoto wa Msimbazi na alikwenda Yanga kutafuta maisha.
Hanspope alisema kipa huyo ana mapenzi makubwa na Simba, licha ya kuichezea Yanga katika vipindi viwili tofauti.
Kigogo huyo alisema Kaseja aliondoka Simba bila ya matatizo, hivyo anazo kila sababu za kurejea iwapo atapenda kufanya hivyo.
Alisema Simba ipo tayari kuzungumza na Kaseja kuhusu mpango huo, lakini mwenye uamuzi wa mwisho ni mchezaji mwenyewe.
"Kaseja ni kipa bora na Simba inatambua hilo, ana uwezo mkubwa wa kulinda lango. Kama anataka kurudi Simba, sisi hatuna tatizo wala pingamizi, hapa ni nyumbani kwake,"alisema.
Hivi karibuni, wakala wa kipa huyo, Abdulfatah Saleh, alitoa masharti kwa Maximo, akimtaka kumchezesha Kaseja kwenye kikosi cha kwanza, vinginevyo watavunja mkataba na Yanga.
Wednesday, November 12, 2014
SIMBA YAMNYEMELEA MSUVA, MKUDE ALAMBA MILIONI 40, AMWAGA WINO MIAKA MIWILI
KIUNGO Jonas Mkude (katikati) akitia saini mkataba wa kuichezea Simba mbele ya Rais wa klabu hiyo, Evans Aveva (kulia) na Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili, Zacharia Hanspope
MWENYEKITI wa klabu ya Simba, Evans Aveva (kushoto) akimpongeza Mkude baada ya kutia saini mkataba mpya na klabu hiyo.
KLABU ya Simba imetuma maombi kwa mahasimu wao Yanga, kutaka kuzungumza na mchezaji wao wa kiungo, Simon Msuva.
Simba imetuma salamu kwa mchezaji huyo wa timu ya taifa, Taifa Stars, ikitaka kumsajili katika usajili wa dirisha dogo.
Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), limetangaza kuwa, msimu wa usajili wa dirisha dogo utaanza rasmi keshokutwa hadi Desemba 15, mwaka huu.
Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia Hanspope, alisema jana kuwa, barua ya maombi kwa Yanga ilitumwa juzi.
Hanspope alisema Simba inataka kufuata kanuni za usajili, hivyo imeamua kutuma maombi hayo kwa kuhofia kuvunja sheria.
"Unapotaka kufanya mazungumzo na mchezaji, ambaye bado hajamaliza mkataba na klabu yake, unatakiwa kwanza kuiomba klabu ndipo uzungumze naye,"alisema.
Alisema Msuva ni mchezaji mzuri, ambaye ataisaidia Simba, hivyo watahakikisha anavaa uzi wa klabu hiyo mwakani.
Hanspope alisema ana imani uongozi wa Yanga utaijibu barua hiyo ili waanze kufanya mazungumzo na Msuva, ambaye kwa sasa ni kipenzi kikubwa cha mashabiki wa klabu hiyo ya Jangwani.
Licha ya kuwa tegemeo kubwa la Yanga katika kufunga mabao, Msuva amekuwa akikosa namba ya kudumu kwenye kikosi cha kwanza kutokana na kuanzia benchi.
Wiki iliyopita, Msuva aliifungia Yanga mabao yote mawili ilipoibwaga Mgambo JKT mabao 2-0 katika mechi ya ligi kuu ya Tanzania Bara, iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Alifunga mabao hayo kipindi cha pili akitokea benchi.
Hivi karibuni, mchezaji huyo alikarriwa akilalamikia kitendo cha Kocha Mkuu wa timu hiyo, Marcio Maximo kumwanzisha benchi wakati kiwango chake kipo juu.
Wakati huo huo, kiungo nyota wa Simba, Jonas Mkude, ameongeza mkataba wa kuichezea klabu hiyo kwa miaka miwili.
Mkude alimwaga wino Simba jana mbele ya Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili, Zacharia Hanspope, baada ya kupewa kitita cha shilingi milioni 40.
Kiungo huyo mkabaji amekubali kubaki Simba baada ya kuahidiwa kulipwa shilingi milioni 60. Fedha zingine zilizobaki atalipwa baadaye.
WAAMUZI 23 KUSHIRIKI SEMINA DAR
Waamuzi 23 wa daraja la kwanza wakiwemo wenye beji la Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) wameteuliwa kushiriki semina itakayofanyika Novemba 16 mwaka huu jijini Dar es Salaam.
Washiriki wa semina hiyo ambayo pia itakuwa na mtihani wa utimamu wa mwili (physical fitness test) wanatakiwa kuripoti Novemba 15 mwaka huu kwenye hosteli ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) iliyopo Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume.
Wakufunzi wa semina hiyo wanaotambuliwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) ni Riziki Majala na Soud Abdi.
Waamuzi watakaoshiriki semina hiyo ni Ahmed Juma Simba (Kagera), Arnold Bugado (Singida), Charles Peter Simon (Dodoma), Dalila Jafari Mtwana (Zanzibar), Ferdinand Chacha Baringenge (Mwanza), Florentina Zabron (Dodoma) na Frank John Komba (Pwani).
Grace Wamara (Kagera), Hellen Joseph Mduma (Dar es Salaam), Israel Mujuni Nkongo (Dar es Salaam), Issa Bilali Ali (Zanzibar), Issa Haji Vuai (Zanzibar), John Longido Kanyenye (Mbeya), Jonesia Rukyaa Kabakama (Kagera) na Josephat Deu Bulali (Tanga).
Kudra Omary (Tanga), Martin Eliphas Saanya (Morogoro), Mary Kapinga (Ruvuma), Mfaume Ali Nassoro (Zanzibar), Mgaza Ali Kinduli (Zanzibar), Samwel Hudson Mpenzu (Arusha), Soud Iddi Lila (Dar es Salaam) na Waziri Sheha Waziri (Zanzibar).
Subscribe to:
Posts (Atom)