KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, November 12, 2014

SIMBA YAMNYEMELEA MSUVA, MKUDE ALAMBA MILIONI 40, AMWAGA WINO MIAKA MIWILI



KIUNGO Jonas Mkude (katikati) akitia saini mkataba wa kuichezea Simba mbele ya Rais wa klabu hiyo, Evans Aveva (kulia) na Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili, Zacharia Hanspope
MWENYEKITI wa klabu ya Simba, Evans Aveva (kushoto) akimpongeza Mkude baada ya kutia saini mkataba mpya na klabu hiyo.

KLABU ya Simba imetuma maombi kwa mahasimu wao Yanga, kutaka kuzungumza na mchezaji wao wa kiungo, Simon Msuva.

Simba imetuma salamu kwa mchezaji huyo wa timu ya taifa, Taifa Stars, ikitaka kumsajili katika usajili wa dirisha dogo.

Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), limetangaza kuwa, msimu wa usajili wa dirisha dogo utaanza rasmi keshokutwa hadi Desemba 15, mwaka huu.

Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia Hanspope, alisema jana kuwa, barua ya maombi kwa Yanga ilitumwa juzi.

Hanspope alisema Simba inataka kufuata kanuni za usajili, hivyo imeamua kutuma maombi hayo kwa kuhofia kuvunja sheria.

"Unapotaka kufanya mazungumzo na mchezaji, ambaye bado hajamaliza mkataba na klabu yake, unatakiwa kwanza kuiomba klabu ndipo uzungumze naye,"alisema.

Alisema Msuva ni mchezaji mzuri, ambaye ataisaidia Simba, hivyo watahakikisha anavaa uzi wa klabu hiyo mwakani.

Hanspope alisema ana imani uongozi wa Yanga utaijibu barua hiyo ili waanze kufanya mazungumzo na Msuva, ambaye kwa sasa ni kipenzi kikubwa cha mashabiki wa klabu hiyo ya Jangwani.

Licha ya kuwa tegemeo kubwa la Yanga katika kufunga mabao, Msuva amekuwa akikosa namba ya kudumu kwenye kikosi cha kwanza kutokana na kuanzia benchi.
Wiki iliyopita, Msuva aliifungia Yanga mabao yote mawili ilipoibwaga Mgambo JKT mabao 2-0 katika mechi ya ligi kuu ya Tanzania Bara, iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Alifunga mabao hayo kipindi cha pili akitokea benchi.
Hivi karibuni, mchezaji huyo alikarriwa akilalamikia kitendo cha Kocha Mkuu wa timu hiyo, Marcio Maximo kumwanzisha benchi wakati kiwango chake kipo juu.
Wakati huo huo, kiungo nyota wa Simba, Jonas Mkude, ameongeza mkataba wa kuichezea klabu hiyo kwa miaka miwili.
Mkude alimwaga wino Simba jana mbele ya Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili, Zacharia Hanspope, baada ya kupewa kitita cha shilingi milioni 40.
Kiungo huyo mkabaji amekubali kubaki Simba baada ya kuahidiwa kulipwa shilingi milioni 60. Fedha zingine zilizobaki atalipwa baadaye.

No comments:

Post a Comment