KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Tuesday, November 25, 2014

PONDAMALI AMCHANACHANA KASEJA




KOCHA wa makipa wa Yanga, Juma Pondamali 'Mensah' amemtaka kipa nguli nchini, Juma Kaseja, kuacha kutafuta mchawi baada ya kukosa namba katika kikosi hicho.

Kauli ya Pondamali imekuja siku chache baada ya Kaseja kukaririwa na vyombo vya habari akidai kocha huyo ni chanzo cha kukosa namba Yanga.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Pondamali, alisema kuwa kipa huyo amekosa namba mbele ya Deogratius Munishi 'Dida' baada ya kiwango chake kuporomoka.

Alisema nahodha huyo wa zamani wa Simba alikosa namba baada ya kuzembea katika mazoezi, hivyo hana sababu ya kutafuta mchawi.

Pondamali, alisema mchezaji huyo anatakiwa kuondoka kwa amani Yanga kurejea katika klabu yake ya zamani Simba.

Simba imeanza mazungumza ya kumsajili Kaseja katika usajili wa dirisha dogo lililofunguliwa Novemba 20 hadi Desemba 20, mwaka huu.

Kipa huyo wa zamani aliyekuwa na mbwembwe uwanjani, alidokeza kuwa Kaseja, alianza kupoteza namba Yanga ilipokuwa chini ya kocha Hans van der Pluijm.

"Nashangaa sana kwanini nahusishwa na sakata hili wakati anayepanga timu ni kocha (Marcio) Maximo, yeye ndiye msimamizi mkuu wa mazoezi," alisema Pondamali.

Alisema muda mfupi baada ya Maximo kujiunga na Yanga kuchukua nafasi ya Pluijm, alitaka kufahamu sababu za kipa huyo kutokuwemo katika kikosi cha Taifa Stars.

Kocha huyo alisema msingi wa swali la Maximo, lilikuwa ni kutaka kujua kwanini Kaseja hachezi timu ya taifa kwa kuwa hadi anaondoka nchini kurejea Brazil alikuwa kipa namba moja.

Maximo, aliwasili nchini mwaka 2006 kuinoa Taifa Stars hadi 2010 ambapo mkataba wake ulimalizika kabla ya kurejea kuifundisha Yanga mapema mwaka huu.

Katika kipindi hicho Kaseja, aliwahi kuingia matatani na Maximo, baada ya Maximo kudai alishangilia mabao manne aliyofungwa hasimu wake, Ivo Mapunda kwenye moja ya mechi za kimataifa.

Maximo, alimuengua Kaseja katika kikosi cha kwanza na kumpa nafasi Ivo katika mechi za kimataifa za Taifa Stars.

Hivi karibuni mchezaji huyo ameibua mzozo na Yanga akidai alipwe sh. milioni 20 zilizobaki katika usajili ambazo Yanga ilitakiwa kumlipa Januari, mwaka huu.

Hata hivyo, Katibu Mkuu wa Yanga, Benno Njovu, amedai mchezaji huyo haidai Yanga fedha za usajili.

No comments:

Post a Comment