KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Sunday, November 2, 2014

DK. SHEIN AAHIDI KUINUA MICHEZO ZANZIBAR



RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar itahakikisha inaiendeleza sekta ya michezo sambamba na kuimarisha miundombinu yake ili Zanzibar iweze kurejesha hadhi yake katika sekta hiyo.

Dk. Shein aliyasema hayo, leo katika hotuba yake aliyoitoa kwenye sherehe za ushindi wa michezo mbali mbali ya Kikosi Maalum cha Kuzuia Magendo KMKM, zilizofanyika huko katika viwanja vya Maisara mjini Zanzibar ambazo pia,zimehudhuriwa na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad, viongozi mbali mbali wa serikali wanamichezo na wananchi.

Katika hotuba yake hiyo, Dk. Shein alisema kuwa katika kufanya hivyo, Serikali inapitia upya Sera ya Michezo ili iweze kufikia malengo ya Serikali katika kuinua sekta ya michezo hapa nchini.

Alisema kuwa wakati mchakato wa kuipitia upya Sera ya Michezo ukiendelea aliwahakikishia wananchi kuwa Serikali inaendelea na juhudi zake za kuimarisha miundombinu ya michezo ikiwemo ujenzi wa viwanja mbali mbali vya michezo Unguja na Pemba.

Dk. Shein alisema kuwa, lengo la Serikali ni kuhakikisha kuwa viwanja vitatu vya Kimataifa hapa Zanzibar vinaimarishwa ambapo hivi sasa tayari uwanja wa Amaan uliopo mjini Unguja uko tayari na kiwanja cha Gombani Pemba tayari kimeshajegwa ambacho ndani ya mwaka huu wa fedha uwanja huo utawekwa tatan katika eneo la kukimbilia.

Aidha, Dk. Shein alisema kuwa Serikali imeshafikia makubaliano na Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China ya ujenzi wa uwanja wa Mao-te-tung ili nao uweze kutumika sambamba na viwanja vya Amaan na Gombani huku akieleza azma ya kuviimarisha viwanja vyengine mbali mbali vya Unguja na Pemba kwa lengo la kuendeleza michezo pamoja na kutoa fursa nzuri kwa wananchi waweze kuendeleza michezo kwa ufanisi zaidi hapa Zanzibar

Dk. Shein alipendekeza kuongezwa kwa mashindano ya mpira wa miguu ili kuleta ushindani katika vilabu vya mpira vya hapa Zanzibar pamoja na kuvishirikisha vilabu vyengine kadhaa.

Alisema kuwa hatua hizo ni sehemu ya juhudi za Serikali za kuzijengea uwezo timu za Zanzibar ili ziweze kushiriki mashinadano ya ndani na nje ya nchi na kupata mafanikio na kusisitiza kuwa wakati umefika Zanzibar kuwa mshindani katika mashindano na kuchukua vikombe katika mashindano mbali mbali.

Dk. Shein alisema kuwa Zanzibar ina vipaji vya kutosha na wanamichezo wa kufanya vizuri wapo, kinachotakiwa ni maandalizi bora na kuondoa migogoro katika uongozi wa vilabu na vyama vya michezo hapa Zanzibar.

Kwa kusisitiza hilo, Dk. Shein alitoa mfano wa mgogoro wa Chama Cha Mpira wa Miguu Zanzibar (ZFA) katika uongozi uliopita ambapo ulisababisha wanamichezo wa timu ya Taifa ya Zanzibar walioshiriki katika mashindano ya 'Challange Cup' mwaka juzi kushindwa kuwakabidhi zawadi aliyowaandalia kutokana na migogoro kadhaa ndani ya chama hicho.

Alieleza kuwa iwapo mashirikiano mazuri yatakuwepo sekta ya michezo itapata mafanikio makubwa na kusisitiza kuwa Serikali itaendelea kuhakikisha kuwa malengo yake ya kukuza sekta ya michezo nchini yanafanikiwa.

Dk. Shein alisema kuwa michezo ni afya, ukakamavu, inajenga udugu na kuleta ushirikiano na kwa hivi sasa, michezo ni ajira kwa hivyo ni vyema wananchi wote wakashiriki katika michezo japo ya vilabu vya mazoezi ili kuimarisha afya zao.

Aidha, Dk. Shein alieleza kuridhishwa sana na mafanikio ya timu ya mpira wa miguu ya KMKM kwa kuwa mabingwa kwa misimu miwili mfululizo 2013-2014 na 2014-2015 pamoja na ushindi wa timu ya riadha pamoja na kupata ngao za hisani. "Naungana na nyinyi na wale wote wanaokupongezeni kwa mafanikio hayo", alisema Dk. Shein.

"Napenda kuwapongeza wanamichezo wa KMKM kwa kuchagua mbio hizi ambazo kwa kweli zinatukumbusha na sisi wengine enzi zetu katika michezo ya riadha hasa ya 'cross-country na field tract' tulishiriki vyema pamoja na mchezo huu wa kuvuta kamba ambapo mimi mwenyewe nilikuwa kocha", alisema Dk. Shein.

Alisema kuwa Uongozi wa Awamu ya Kwanza ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ulichukua jitihada za makusudi kujenga Uwanja wa Amaan uliofunguliwa mwaka 1970 na ule wa Gombani uliofunguliwa mnamo mwaka 1992 wakati wa uongozi wa Awamu ya Tano ambapo ujenzi wake ulianza katika uongozi wa Awamu ya Nne chini ya Marehemu Sheikh Idrisa Abdul Wakil.

Dk. Shein vile vile, alisisitiza haja ya kila timu hapa Zanzibar kuwa na Klabu yake na jengo lake na kuunga mkono azma ya klabu ya KMKM kutaka kujenga jengo maalum la ghorofa litakalokuwa na eneo la kufanyia mazoezi (GYM), ukumbi wa mikutano na maduka ya vifaa vya michezo.

Mapema Dk. Shein aliyapokea mashindano ya mbio za kilomita kumi katika viwanja hivyo vya Maisara yalioanzia huko Kibweni nje kidogo ya Mji wa Zanzibar, na kuwashirikisha wakimbiaji zaidi ya 200 ambapo mkimbiaji Philip Jacob Mambo kutoka Kikosi cha Mafunzo aliibuka mshindi wa kwanza na Mohamed Ramadhan kutoka KMKM ambae aliibuka mshindi wa Pili.

Kwa upande wa wanawake mshindi wa kwanza alikuwa Albina Edward kutoka KMKM na mshindi wa pili alikuwa Nuru Nasib kutoka Kambi ya Mtoni. Mashindano hayo pia, yalijumuisha Makundi maalum ambapo nafasi ya kwanza ilichukuliwa na mkimbiaji Ali Abdalla na mshindi wa pili alikuwa Amina Daudi Simba.

Naye Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Idara Maalum za SMZ Mhe. Haji Omar Kheir alitoa pongezi kwa Dk. Shein kwa kushirikiana pamoja na wanamichezo hao wa Kikosi cha KMKM katika sherehe zao hizo.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mkuu wa KMKM Komodoo Hassan Mussa alisema kuwa mbio za kilomita 10 ambazo zilishirikisha wanamichezo zaidi ya 200 zimefanyika kwa mara ya kwanza mwaka huu lakini zitafanyika kila mwaka katika siku itakayoteuliwa kuwa ya KMKM.

Katika risala yao nao wanamichezo wa KMKM walieleza mikakati inayochukiliwa katika kuendeleza michezo katika kikosi chao sambamba na kupongeza jinsi Serikali inavyowaunga mkono katika kufikia malengo waliyojiwekea

Sherehe hizo ziliambatana na burudani kutoka vikundi mbalimbali vya sanaa vikiwemo Diamond Morden Taarab, Kidumbaki kilichoongozwa na Msani Makame Faki maarufu sauti ya zege, ngoma ya Kibati kutoka kikundi cha sanaa cha JKU, JKU Morden Taarab ambacho kiliimba wimbo maalum kwa ajili ya sherehe hiyo.

Pia, mchezo wa kuvuta kamba ulifanyika katika sherehe hizo ambao uliwashirikisha maafisa wa KMKM wanaofanya kazi pamoja na Wastaafu ambapo Wastaafu walipata ushindi na kukabidhiwa zawadi na Rais zikiwemo fedha taslim zilizotolewa na wapenda michezo.

No comments:

Post a Comment