KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Tuesday, November 11, 2014

MAMIA WAMZIKA AMIGOLAS, JK AMLILIA, WASANII WAANGUA VILIO MAKABURINI


RAIS Jakaya Kikwete amemtumia salamu za rambirambi Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Fenella Mukangara.

Rais Kikwete ametuma salamu hizo kuomboleza kifo cha mwanamuziki mwasisi wa bendi ya African Stars 'Twanga Pepeta', Hamisi Kayumbu 'Amigolas'.

Amigolas alifariki usiku wa kuamkia Jumapili saa 5:30 usiku katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), Dar es Salaam kwa ugonjwa wa moyo.

“Nimehuzunishwa na kusikitishwa na taarifa za kifo cha mwanamuziki Hamisi Kayumbu kilichotokea tarehe 9 Novemba, 2014 katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) alikokuwa amelazwa kwa matibabu ya ugonjwa wa moyo”, alisema Rais Kikwete katika Salamu zake.

Taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari na Ikulu jana, ilisema Rais Kikwete anatambua mchango mkubwa wa marehemu Amigolas, katika kuhamasisha maendeleo ya nchi yetu.

Taarifa hiyo ilisema Kayumbu alitoa mchango wake kupitia sanaa ya muziki kuwafikishia wananchi ujumbe muhimu wa masuala mbalimbali ya kijamii na kiuchumi.

Alisema Kayumbu alikuwa mfano unaofaa kuigwa na wasanii wengine nchini. Amigolas alikuwa kiongozi wa bendi mpya ya Ruvu Stars baada ya kuhama Twanga Pepeta.

“Kutokana na msiba huu, naomba upokee salamu zangu za rambirambi kwa kumpoteza mmoja wa wanamuziki mahiri hapa nchini, pia ziwafikie wanamuziki wengine kote nchini kwa kumpoteza mwenzao”, ilisema sehemu ya taarifa hiyo.

Aidha, Rais Kikwete amemwomba Dk. Fenella, kumfikishia salamu zake za pole kwa familia ya marehemu Kayumbu kwa kupotelewa na kiongozi na mhimili madhubuti.

Wakati huohuo, wasanii mbalimbali jana walishindwa kujizuia kuangusha vilio, baada ya mwili wa mwanamuziki mahiri marehemu Hamisi Kayumbu 'Amigolas' kuwasili nyumbani kwake Mburahati, Dar es Salaam.

Amigolas alifariki usiku wa kuamkia Jumapili saa 5:30 usiku katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), Dar es Salaam kwa ugonjwa wa moyo.

Mkurugenzi wa bendi ya Extra Bongo na mwimbaji hodari nchini, Ali Choki, alishindwa kuzungumza na vyombo vya habari kuhusu kifo cha Amigolas.

Choki na Amigolas, walifanya kazi kwa karibu na pia waanzilishi wa bendi ya African Stars 'Twanga Pepeta' mwaka 1997.

Hata hivyo, baadhi ya wasanii walitoa maoni yao kuhusu kifo cha Amigolas aliyekuwa na sauti nzito jukwaani.

Kiongozi wa Twanga Pepeta, Luiza Mbutu, alisema Amigolas alikuwa mtu muhimu katik tasnia ya muziki na ametoa mchango mkubwa kwa wasanii chipukizi.

Naye Saidi Mabera 'Dokta' wa Msondo Ngoma alisema alimfahamu, Amigolas, tangu mwaka 1986 alipokuwa mwimbaji wa bendi ya Bicco Stars.

"Nilimfahamu marehemu Amigolas tangu mwaka 1986 akiwa Bicco Stars, naomba wanamuziki tumuenzi kwa kudumisha muziki wa asili," alisema Mabera.

Ramadhani Athumani 'Dogo Rama' wa Twanga Pepeta alisema, Amigolas, alikuwa kiungo muhimu na mmoja wa wasanii walimsaidia kukuza kipaji chake cha kuimba.

Naye Stara Thomas, alisema alianza kufahamiana na Amigolas akiwa bado kinda katika muziki, hivyo ametoa rai kwa wadau kumuombea.

"Tunamshukuru Mungu kwa sababu kifo hakikwepeki, jambo la msingi ni kumuombea ingawa alikuwa bado anahitajika,"alisema msanii wa maigizo nchini Steven Mengele 'Steve Nyerere'.

Kwa upande wake Hassani Mussa 'Super Nyamwela' wa Extra Bongo, alisema hakutarajia kama nguli huyo angefariki kwa ugonjwa wa moyo na amemtaja Amigolas alikuwa mhimili wa Twanga Pepeta.

Marehemu Amigolas alizikwa jana alasiri katika makaburi ya Kisutu, Dar es Salaam na umati wa watu wakiwemo wasanii na watu mbalimbali maarufu.

No comments:

Post a Comment