KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Saturday, November 8, 2014

YANGA, AZAM ZASHINDA LIGI KUU, MBEYA CITY HOI



MABAO mawili yaliyofungwa na mshambuliaji Simon Msuva jana yaliiwezesha Yanga kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Mgambo JKT katika mechi ya ligi kuu ya Tanzania Bara iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Msuva, ambaye aliingia uwanjani kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Haruna Niyonzima,alifunga mabao hayo dakika ya 73 na 88.

Kutokana na ushindi huo, Yanga sasa imefikisha pointi 13 baada ya kucheza mechi saba, ikiwa inakabana koo na Azam, inayoshika nafasi ya pili.

Azam ilitoka uwanjani kifua mbele baada ya kuichapa Coastal Union mabao 2-1 katika mechi iliyochezwa kwenye Uwanja wa Chamazi, Dar es Salaam.

Mabao ya Azam yalifungwa na beki Shomari Kapombe na mshambuliaji wa kimataifa wa Ivory Coast, Kipre Tchetche. Bao la Coastal Union lilifungwa na Rama Salim.

Timu ya soka ya Mbeya City jana ilipigwa mweleka wa bao 1-0 ba Stand United katika mechi ya ligi kuu ya Tanzania Bara iliyochezwa kwenye Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga.

Kipigo hicho ni cha tano kwa Mbeya City tangu ligi hiyo ilipoanza msimu huu, ambapo katika mechi saba ilizocheza, imeshinda moja na kutoka sare moja.

Katika mechi nyingine ya ligi hiyo iliyochezwa jana, Prisons ya Mbeya ilichezea kichapo cha bao 1-0 kutoka kwa maafande wa Polisi kwenye Uwanja wa Jamhuri Morogoro.

Pambano kati ya Mtibwa na Kagera Sugar lililochezwa kwenye uwanja wa Manungu mjini Turiani, lilivunjika kipindi cha pili kutokana na mvua kubwa kuanza kunyesha.

Hadi pambano hilo lilipovunjika, Mtibwa ilikuwa mbele kwa bao 1-0. Pambano hilo sasa litachezwa leo.

Katika mechi nyingine ya ligi hiyo itakayochezwa leo, Simba itashuka dimbani kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, kumenyana na Ruvu Shooting.

No comments:

Post a Comment