KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Sunday, December 14, 2014

SIMBA YAINYAMAZISHA YANGA



SIMBA jana iliendeleza ubabe wake kwa watani wao wa jadi Yanga, baada ya kuwachapa mabao 2-0 katika mechi ya Nani Mtani Jembe iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Hii ni mara ya pili kwa Simba kuishinda Yanga katika mechi hiyo, inayoandaliwa kila mwaka na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), kupitia bia yake ya Kilimanjaro. Katika mechi ya mwaka jana, Simba iliichapa Yanga mabao 3-1.

Yanga ililianza pambano hilo kwa kasi na kufanya mashambulizi kadhaa kwenye lango la Simba huku ikipata nafasi nzuri za kufunga, lakini umaliziaji mbovu wa washambuliaji wake, Simon Msuva, Emerson na Sherman ulikuwa kikwazo.

Kadri mchezo ulivyokuwa ukisonga mbele, wachezaji wa Simba walianza kutulia na kucheza kwa uelewano na hatimaye Awadh Juma kuiandikia bao la kwanza dakika ya 30 baada ya Kipa Dida wa Yanga kutema shuti la Emmanuel Okwi.

Zikiwa zimesalia dakika nne kuwa mapumziko, Elias Maguri aliiandikia Simba bao la pili baada ya mpira uliorushwa na Nassoro Masoud kumkuta akiwa katikati ya mabeki wa Yanga, akaupiga kichwa, ukagonga mwamba wa pembeni wa goli na kumrudia, ambapo aliutumbukiza kimiani. Timu hizo zilikwenda mapumziko Simba ikiwa mbele kwa mabao 2-0.

Kipindi cha pili kilianza kwa timu zote kufanya mabadiliko kadhaa ya wachezaji kwa lengo la kuongeza nguvu, lakini hakuna iliyoweza kupata bao.

Kwa ushindi huo, Simba ilizawadiwa fedha taslim sh. milioni 15 kutoka TBL wakati Yanga iliambulia sh. milioni tano. Hundi za fedha hizo zilikabidhiwa kwa manahodha wa timu hizo, Haruna Niyonzima wa Yanga na Okwi wa Simba.


No comments:

Post a Comment