KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, November 2, 2016

YANGA MAJANGA, YAPIGWA 2-1 NA MBEYA CITY



MABINGWA watetezi wa ligi kuu ya soka ya Tanzania Bara, Yanga leo wamekwaa kisiki mbele ya Mbeya City baada ya kukubali kipigo cha mabao 2-1 katika mechi iliyochezwa kwenye Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya.

Katika mechi hiyo iliyokuwa na ushindani mkali, Mbeya City iliyokuwa ikishangiliwa kwa nguvu na mashabiki wake, ilikwenda mapumziko ikiwa mbele kwa mabao hayo 2-1.

Matokeo hayo yameiwezesha Mbeya City kufikisha pointi 19 baada ya kucheza mechi 14 wakati Yanga inaendelea kushika nafasi ya pili ikiwa na pointi 27 baada ya kucheza mechi 13.

Mbeya City ilikuwa ya kwanza kupata bao dakika ya sita lililofungwa na Hassan Mwasapili kwa shuti la mbali la mpira wa adhabu lililotinga moja kwa moja wavuni na kumwacha kipa Dida wa Yanga akigaagaa.

Bao la pili la Mbeya City lilifungwa na Kenny Ally dakika ya 36 kwa shuti la mbali baada ya kupokea pasi fupi ya mpira wa adhabu kutoka kwa Haruna Shamte.

Wachezaji wa Yanga walililalamikia bao hilo na kumzonga mwamuzi Rajab Mrope kutoka Ruvuma kwa madai kuwa halikuwa halali. Baada ya kujadiliana na wasaizidi wake, mwamuzi huyo aliashiria kwamba lilikuwa bao halali.

Bao la kujifariji la Yanga lilifungwa na mshambuliaji wa kimataifa wa Zimbabwe, Donald Ngoma dakika ya 45.

Katika kipindi cha pili, Mbeya City ilicheza zaidi mchezo wa kujihami na kuwapa usumbufu mkubwa washambuliaji wa Yanga kujaribu kutafuta bao la kusawazisha.


No comments:

Post a Comment