KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Tuesday, November 15, 2016

AZAM KUKIONGEZEA NGUVU KIKOSI CHAKE



UONGOZI wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, kwa kushirikiana na benchi la ufundi la timu hiyo hivi sasa upo kwenye mchakato wa kukiongezea nguvu kikosi hicho.

Hatua hiyo imekuja ikiwa ni nia ya dhati kabisa ya Azam FC kutaka kufanya vizuri zaidi kwenye mzunguko wa pili wa ligi, Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) na michuano ya Kimataifa inayokuja kuanzia mwezi ujao na mwakani (Kombe la Kagame na lile la Shirikisho Afrika).

Mabingwa hao wa Ngao ya Jamii mwaka huu, tayari wamemaliza mzunguko wa kwanza wa ligi wakiwa kwenye nafasi ya tatu kwenye msimamo wakijikusanyia jumla ya pointi 25, wakizidiwa pointi 10 na kinara Simba aliyejizolea 35.

Akizungumza na mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz juzi Kocha Msaidizi wa Azam FC, Yeray Romero, alisema kuwa kuelekea mzunguko wa pili wa ligi wanatarajia kuangalia mapungufu ya kikosi hicho kabla ya kuingiza sura mpya kwenye usajili ya dirisha dogo kwa ajili ya kuinyanyua timu na kufika kwenye nafasi nzuri zaidi.

“Wakati wachezaji wapya wanaingia pia tunatarajia kuwaangalia wachezaji ambao tunadhani kwa sasa kikosini hawawezi kuisaidia timu, ambao ndio watawapisha wachezaji hao, lengo la yote haya ni kuweza kuipeleka mbele zaidi timu zaidi ya hapa ilipo,” alisema.

Katika hatua nyingine, Romero aliwapongeza wachezaji kwa kazi waliyoweza kuifanya mpaka sasa huku wao kama benchi la ufundi wakiahidi kufanya kazi nzuri zaidi kwa asilimia 100 katika kuirekebisha zaidi timu na kuziba mapungufu yaliyopo.

Matarajio yamefikiwa?   

“Kiufupi matarajio hayakuwepo ya kumaliza nafasi ya tatu kwenye mzunguko wa kwanza, hatukuwa tumepanga kufika nafasi hiyo lakini mazingira tuliyokuwa nayo yametufanya kumaliza hapo, licha ya yote hii ni nafasi nzuri kwetu na tunachoangalia kwenye raundi ijayo ni kufika nafasi pili na ya kwanza,” alisema.

Kauli kwa mashabiki Azam FC

Kocha huyo wa zamani wa timu za CF Reale Juventud Laguna na CD Tenerife zote za Hispania, aliwashukuru mashabiki wa Azam FC kwa sapoti kubwa wanayoendelea kutoa kwenye mechi zao licha ya kupitia wakati mgumu kwenye baadhi ya mechi.

“Kwa kweli nachukua fursa hii kuwapongeza mashabiki wa Azam FC, kwa yote yaliyotokea wao wamekuwa pamoja nasi, timu inapofanya vibaya wapo na inapofanya vizuri wapo na ambacho tunaweza kuwaahidi ni mashabiki wetu ni kwamba waendelee kuwa na imani na timu yao kwa sababu nafasi tuliyofikia hivi sasa si mbaya sana, lakini ingawaje si kama ndio tuliyokuwa tumepanga kufika.

“Hivyo tunategemea raundi ya pili itakapoanza kwa nguvu ambazo tutaziingiza kikosini basi wakiwa wanaendelea kutusapoti kama mwanzo naamini ya kuwa mashabiki watajikuta kwamba hawakukosea kuichagua Azam FC kwa sababu matokeo yatakuwa ni mazuri kwa timu kuweza kupata ushindi,” alimalizia mtaalamu huyo.

Azam FC kuendelea kujifua

Wakati huo huo, mara baada ya kikosi cha Azam FC kurejea jana jioni jijini Dar es Salaam kikitokea mkoani Shinyanga kilipocheza na Mwadui, taarifa ni kuwa wachezaji wa timu hiyo wataendelea na mazoezi kama kawaida jioni ya leo.

Kwa mujibu wa programu ya benchi la ufundi chini ya Kocha Mkuu, Zeben Hernandez, mara baada ya mazoezi ya leo, kikosi hicho kinatarajia kucheza mchezo wa kirafiki kesho Jumamosi kabla ya kupumzika Jumapili na Jumatatu kitacheza mchezo mwingine wa kujipima ubavu.

Tathimini ya mzunguko wa kwanza

Azam FC inayodhaminiwa na kinywaji safi ya Azam Cola kinachochangamsha mwili na kuburudisha koo na Benki bora nchini kwa usalama wa fedha zako ya NMB, imefanikiwa kucheza jumla ya mechi 15 kwenye mzunguko wa kwanza wa ligi ikifanikiwa kushinda jumla ya mechi saba, sare nne na kupoteza nne ikiwa imekunja kibindoni pointi 25.

Takwimu pia zinaonyesha kuwa, Azam FC imeshinda robo tatu ya mechi zake ilizocheza ugenini, ikiibuka na ushindi mara tano kati ya mechi nane za ugenini, ikifungwa tatu, kati ya mechi saba ilizokuwa mwenyeji imefanikiwa kuibuka kidedea mara mbili, sare nne na kuteleza mechi moja.

Hivyo takwimu hizo zinaeleza kuwa Azam FC imefanikiwa kupata alama 15 kwenye viwanja vya ugenini kati ya 24 ilizotakiwa kuvuna, ambapo imepoteza jumla ya pointi tisa ugenini.

Mabingwa hao wamevuna jumla ya pointi 10 kati ya 21 katika uwanja wa nyumbani, ikiwa imeacha uwanjani jumla ya pointi 11, nane katika uwanja wake wa Azam Complex kutokana na sare nne ilizotoa ndani ya dimba hilo na tatu ikiziacha ndani ya Uwanja wa Uhuru kufuatia kupoteza bao 1-0 dhidi ya Simba ambayo inaongoza ligi ikiwa na pointi 35 pungufu ya pointi 10 na mabingwa hao.

Rekodi ya ufungaji wa mabao zinaonyesha kuwa mpaka sasa kikosi hicho kimefunga 21, ukiwa ni wastani wa bao 1.4 kwenye kila mchezo katika mechi 15 ilizocheza huku pia ikiruhusu nyavu zake kutikiswa mara 14 (yaani wastani wa kufungwa bao 1.0 kwenye kila mchezo iliocheza).

Nahodha John Bocco ‘Adebayor’, ndiye ameonekana kinara wa kutupia mabao msimu huu ndani ya Azam FC mpaka sasa akitupia sita akizidiwa mabao matatu na Shiza Kichuya wa Simba aliyekuwa kileleni kwa mabao tisa, wengine wanaomzidi ni Rashid Mandawa (Mtibwa Sugar), Simon Msuva, Amissi Tambwe (Yanga), ambao wote wamefunga saba kila mmoja.

Bocco pia yupo kileleni kwenye utengenezaji wa mabao akiwa ametoa pasi za mwisho nne, akifuatiwa kwa ukaribu na Khamis Mcha aliyechangia matatu ambaye pia ametupia wavuni matatu, huku Shaaban Idd aliyeweka kambani matatu naye akipika mawili.

Mpaka raundi ya kwanza inamalizika mchezaji wa Azam FC aliyecheza mechi nyingi kuliko mwingine yoyote ni kipa namba moja, aliyecheza 14 sawa na dakika 1,260 kati ya 1,350, alizotakiwa kucheza hadi ligi inafikia katikati na hii ni baada ya kupumzishwa mechi moja wakati kikosi hicho kikikabiliana Mbao, mchezo ulioisha kwa Azam FC kuteleza kwa kufungwa mabao 2-1.

No comments:

Post a Comment