KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Friday, November 25, 2016

ISERE SORTS KUNOGESHA USIKU WA SIKINDE


MKURUGENZI wa duka la kuuza vifaa vya michezo la Isere Sports, Abbas Isere (kulia), akimkabidhi moja ya fulana 30, Mratibu wa onyesho la Usiku wa Sikinde, Rashid Zahor, kwa ajili onyesho hilo, litakalofanyika kesho katika ukumbi wa DDC Kariakoo, Dar es Salaam. (Picha na Jumanne Gude).

KAMPUNI ya Isere Sports, inayojihusisha na utengenezaji na usambazaji wa vifaa vya michezo, imejitokeza kulinogesha onyesho la 'Usiku wa Sikinde' kwa kutoa zawadi maalumu ya fulana.

Onyesho hilo, ambalo limelenga kuwakumbusha mashabiki nyimbo za zamani na mpya za bendi ya Mlimani Park Orchestra, linatarajiwa kufanyika Novemba 27, mwaka huu, kwenye ukumbi wa DDC Kariakoo, Dar es Salaam.

Mkurugenzi wa kampuni hiyo,  Abbas Isere, alikabidhi fulana hizo jana, kwa Mratibu wa onyesho hilo, Rashid Zahor, katika hafla iliyofanyika ofisini kwake mjini Dar es Salaam.

Abbas alisema ameamua kutoa zawadi hiyo ya fulana ili kuiunga mkono bendi hiyo katika jitihada zake za kukuza na kuinua muziki wa dansi nchini.

"Mimi nimeishi sana mitaa ya Kariakoo na ni miongoni mwa mashabiki wakubwa wa Sikinde, nilikuwa sikosekani kwenye kumbi, ambazo bendi hii ilikuwa ikitumbuiza, hivyo nimetoa fulana hizi kwa lengo la kuiunga mkono pamoja na nyinyi waratibu,"alisema.

Mbali na kutoa zawadi hiyo ya fulana, Abbas alisema atakuwa miongoni mwa mashabiki watakaohudhuria onyesho hilo, ambalo amebashiri kuwa litakuwa la aina yake kwa sababu litakuwa kwa ajili ya watu maalumu.

Akipokea fulana hizo, Zahor alimshukuru Abbas kwa msaada huo, ambao alisema utalifanya onyesho hilo liwe na mvuto wa aina yake kwa sababu baadhi zitatolewa kwa mashabiki.

Alisema wakati wa onyesho hilo, mashabiki watakaopendeza kwa mavazi, kucheza vizuri na kujibu vyema maswali yanayohusu Sikinde, watapatiwa zawadi hizo za fulana.

Baadhi ya nyimbo adimu zitakazopigwa kwenye onyesho hilo ni pamoja na Celina, Maudhi, Taraka rejea, Clara, Christina Bundala, Hiba, Barua kutoka kwa mama, Chenga ya mwili, Dua la kuku, Sitokubali kuwa mtumwa, Mtoto akililia wembe, Cenjesta na Epuka jambo lisilokuhusu.

Kiongozi wa bendi hiyo, Abdalla Hemba, aliwahakikishia mashabiki kwamba, watapata burudani murua na adimu, ambayo hawataisahau katika maisha yao.

No comments:

Post a Comment