KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Monday, February 29, 2016

KAPOMBE MCHEZAJI BORA WA LIGI KUU MWEZI JANUARY


Beki Shomari Kapombe wa timu ya Azam FC ameshinda tuzo ya mchezaji bora wa Ligi Kuu ya Vodacom kwa mwezi Januari 2016.

Katika mwezi huo uliokuwa na raundi tatu, Kapombe alicheza dakika zote 180 za mechi mbili za timu yake dhidi ya African Sports na Mgambo Shooting. Mechi ya tatu ya Azam FC katika raundi hiyo dhidi ya Tanzania Prisons ilikuwa kiporo, na ilichezwa Februari24, 2016.

Kapombe alifunga mabao yote mawili kwenye ushindi wa mabao 2-1 wa timu yake dhidi ya Mgambo Shooting. Pia alisaidia kupatikana bao la Azam kwenye mechi dhidi ya African Sports iliyomalizika kwa sare ya bao 1-1, na mara nyingi mashambulizi ya timu yake yalianzia upande wake.

Washindani wa Kapombe kwenye kinyang’anyiro hicho katika mwezi huo walikuwa mshambuliaji wa Tanzania Prisons ya Mbeya, Jeremiah Juma na beki wa Coastal Union ya Tanga, Miraji Adam.

Kwa kutwaa tuzo hiyo, Kapombe atazawadiwa kitita cha sh. 1,000,000 (milioni moja) na wadhamini wa Ligi hiyo Kampuni ya simu za mkononi ya Vodacom Tanzania Limited.

NAPE MGENI RASMI TAMASHA LA PASAKA


Na Mwandishi Wetu

WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye anatarajia kuwa mgeni rasmi kwenye Tamasha la Pasaka jijini Mwanza Machi 27.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Kamati ya maaandalizi ya tamasha hilo, Alex Msama, Waziri Nape amekubali kuwa mgeni rasmi katika tamasha hilo ambalo litaanzia Geita Machi 26 na kumalizia Kahama Machi 28.

Msama alisema kamati yake inaendelea na maandalizi ya kuelekea tamasha hilo ambalo litashirikisha waimbaji mbalimbali hapa nchini.

“Maandalizi kuelekea Tamasha la Pasaka yanaendelea vema, hivyo wakazi wa mikoa ya Kanda ya Ziwa wajiandae kupokea ujumbe wa neno la Mungu kupitia viongozi wa dini na waimbaji wa muziki wa Injili,” alisema Msama.

Msama alisema baadhi ya waimbaji  waliothibitisha kushiriki tamasha hilo ambao ni pamoja na Rose Muhando, Bonny Mwaitege, Upendo Nkone, Jesca BM Honore, Christopher Mwahangila, Joshua Mlelwa, Sifael Mwabuka, Jenipher Mgendi, Kwaya ya AIC Makongoro na Kwaya ya Wakorintho Wapili.

Aidha Msama alisema viingilio katika tamasha hilo ni shilingi 5000 kwa wakubwa na kwa watoto shilingi 2000.

SIMBA WAMPA TUZO IBRAHIM AJIB


Katika kuongeza morali na kuwazawadia wachezaji wanaofanya vizuri, Klabu ya Simba ilianzisha Tunzo ya Mchezaji Bora wa Mwezi kuanzia mwezi wa Septemba 2015.
Mshindi wa mwezi wa Disemba, 2015 ni Ibrahim Ajib ambapo amepata kura nyingi zaidi zilizopigwa na mashabiki na wapenzi wa Simba na soka wa Tanzania kwa ujumla kupitia simu za mkononi ambao pia wamejiunga na huduma ya Simba News.Akikabidhiwa tunzo pamoja na pesa taslim Tsh 500,000/= na Mkuu wa kitengo cha biashara na mipango kutoka EAG Group ambao ni washauri na watekelezaji wa Masoko na Biashara wa Simba, Richard Mvula, Ibrahim Ajib alisema “kila siku nimekuwa nikiendelea kujitahidi kufanya vizuri zaidi ili nami ifike siku niweze kukabidhiwa tunzo hii, kwakweli ni heshima kubwa sana kwangu, napenda kuchukua fursa hii kuupongeza uongozi mzima wa Simba kwa kuanzisha utaratibu huu, pia napenda kuwashukuru mahsbiki wangu ambao wamenipigia kura, wachezaji wenzangu kwenye kikosi cha Simba ambao kila siku tumekuwa tukishirikiana katika kazi yetu hii ya mpira, napenda kushukuru kwa sapoti kubwa ninayoipaa kutoka kwa familia yangu na mwisho napenda kumshukuru Allah kwa kuendelea kunibariki na neema zake kila siku”
Akimakabidhi tunzo hiyo Mkuu wa kitengo cha biashara na mipango kutoka EAG Group Richard Mvula alisema “kama mtakumbuka utaratibu huu ulianzishwa kwa ajili ya kuwapa motisha wachezaji wetu na sasa umekuwa ni utamaduni wetu katika kuwapongeza na kuonesha kuthamini jitihada zinazofanywa na wachezaji wetu katika kuutafuta ushindi wa msimu huu”
Napenda kuwakumbusha wanachama na wapenzi wa Simba kuendelea kuwapa sapoti wachezaji wetu kwani kwa sapoti yao ndio mafanikio ya timu yetu yanapopatikana, aliongeza Mkuu wa kitengo cha biashara na mipango kutoka EAG Group Richard Mvula
Akizungumza jinsi tunzo ya mchezaji bora itakavyoendeshwa, Mkurugenzi Mkuu wa EAG Group, Imani Kajula alisema “Wanachama na wapenzi wa Simba na wapenda michezo ndio watakao kuwa wanachagua mchezaji bora wa mwezi kwa kutuma jina la mchezaji wanayempendekeza kwenda kwenye namba 15460, Ni wale tu ambao wamejiunga na Simba News kupitia mtandao wa Voda na Tigo wataweza kupiga kura kuchagua mchezaji bora wa mwezi wa Simba”.
Tukumbuke kuwa unaweza kumchagua mchezaji bora wa mwezi ukiwa umejiunganisha na huduma ya Simba News kwa kutuma jina la mchezaji kwenda namba 15460. Zoezi la kumchagua mchezaji bora wa mwezi wa Januari, 2016 litaanza February 29 2016. Piga kura mara nyingi zaidi kuweza kumpata mchezaji wako bora wa Mwezi Januari, 2016.
Simba News ni huduma iliyoanzishwa na Simba ili kuwapa wapenzi wa Simba habari mbalimbali za Simba popote pale walipo ikiwemo matokeo, majina ya wachezaji wanaocheza mechi, usajili na habari nyingine za klabu ya Simba. Kujiunga na Simba News tuma neno Simba kwenda namba 15460 ni maalum kwa Tigo na Vodacom.

CHEKA ALIVYOMDUNDA MPINZANI WAKE KWA POINTI


Thursday, February 25, 2016

KAPUMZIKE KWA AMANI KASSIM MAPILI


 

Na Rashid Zahor

FANI ya muziki wa dansi nchini juzi ilipata pigo baada ya mwanamuziki mkongwe na nguli, Kassim Mapili, kufariki dunia akiwa usingizini.

Mapili, alifariki dunia usiku wa kuamkia juzi, nyumbani kwake Tabata Matumbi, ikiwa ni siku chache baada ya kushiriki kwenye mazishi ya mtangazaji wa Redio Tumaini, Fred Mosha, aliyezikwa Jumatatu iliyopita kwenye makaburi ya Kinondoni, Dar es Salaam.

Kifo cha Mapili kilijulikana baada ya majirani kutomuona kwa siku mbili nzima na kutia shaka, ndipo walipoamua kuvunja mlango wa chumba chake na kumkuta akiwa amelala kitandani, akiwa amekata roho.

Kwa mujibu wa ndugu wa marehemu, mazishi ya mwanamuziki huyo mkongwe na mahiri katika kupiga gita la solo na kuimba, yanatarajiwa kufanyika leo kwenye makaburi ya Kisutu, Dar es Salaam.

Kifo cha marehemu Mapili kimewagusa watu wengi, si wanamuziki na mashabiki wa fani hiyo pekee, bali hata wananchi wa kawaida. Alikuwa mcheshi na anayependa kujichanganya na watu mbalimbali. Lakini kikubwa zaidi alikuwa smati kwa mavazi na msafi kupindukia.

Mara nyingi marehemu Mapili alipenda kuvaa suti na kofia. Na kama hakuvaa suti, basi alipenda kuvaa suruali, shati na tai bila kuacha kofia. Huo ndio ulikuwa utamaduni wake.

Nilianza kufahamiana na marehemu Mapili mwanzoni mwa miaka ya 1990, nikiwa mwandishi wa habari wa kujitegemea katika magazeti ya Uhuru na Mzalendo, Kiongozi na pia Mwananchi na Majira wakati yalipoanzishwa.

Umaarufu na uhodari wake kimuziki ndio ulionifanya niandike makala hii iliyotoka kwenye gazeti la Kiongozi, toleo la pili la Julai, 1992.

                                             ALIKOTOKEA

Marehemu Mapili aliwahi kuziongoza bendi nyingi za muziki wa dansi hapa nchini, ikiwa ni pamoja na kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Chama cha Muziki wa Dansi Tanzania (CHAMUDATA), kilipoanzishwa, wadhifa ambao aliendelea nao hadi mwaka 1993, licha ya kuwepo kwa migogoro mingi ya kiuongozi.

Akiwa kiongozi wa chombo hicho kilichoanzishwa mwaka 1982, kwa madhumuni ya kutetea maslahi ya wanamuziki wa Tanzania, Mapili alifanya mengi. Ndiye aliyebuni mtindo wa kuzikutanisha bendi zaidi ya mbili (Top Ten Show) na kufanya onyesho kwa wakati mmoja. Pia ndiye aliyetoa wazo la kuundwa ka kundi la Tanzania All Stars.

Marehemu Mapili pia ndiye aliyefanya juhudi za kukutana na wanamuziki wenzao wa Kenya mwaka 1988, kwa lengo la kuzungumzia hakimiliki za wanamuziki wa Afrika Mashariki na pia kubadilishana mawazo na ujuzi.

                                  MUZIKI HAUKUMNUFAISHA KITU

Akizungumzia manufaa aliyoyapata kimuziki wakati huo, marehemu Mapili alikiri wazi kuwa muziki wa dansi haukumnufaisha chochote kwa kile alichodai kuwa, isingekuwa rahisi kwa mwanamuziki wa Tanzania kufaidika kutokana na kutokuwepo kwa sheria ya hakimiliki.

"Ingekuwepo sheria ya hakimiliki, bila shaka leo hii ningezungumza na wewe nikiwa kwenye jumba langu kubwa na pengine ningekuwa na magari lukuki ya kutembelea.

"Lakini maisha yetu wanamuziki wa Tanzania ni ya kusikitisha sana. Mwanamuziki anaweza kupiga muziki miaka hata 30, lakini asifaidike na chochote. Na hata anapokufa, wanawe hawana cha maana cha kurithi kutokana na jasho lake. Mfano mzuri ni wa marehemu Mbaraka Mwinshehe na Hemed Maneti,"alisema Mapili wakati huo akiwa nyumbani kwake Ilala, Dar es Salaam, huku akionekana kuwa na majonzi makubwa usoni.

Akielezea hali ya muziki ilivyokuwa wakati huo, marehemu Mapili alisema kiupigaji, muziki ulikuwa umepanda, lakini hakukuwa na maendeleo yaliyofikiwa katika hali za maisha ya wanamuziki kutokana na kutokuwepo kwa sheria ya hakimiliki.



Alisema kupanda kwa kiwango cha muziki wa dansi wakati huo, kulipaswa kwenda sambamba na kuinuka kwa hali za maisha ya wanamuziki. Alisema kilichopanda wakati huo kilikuwa ni kuibwa kwa nyimbo za wanamuziki na kuuzwa holela na maharamia wa muziki.

Mapili, ambaye alikuwa mstari wa mbele katika kutetea maslahi ya wanamuziki wa Tanzania, alisema kigezo cha nyimbo nzuri ni kuuzwa na kununuliwa kwa wingi.

Aidha, alisema nyimbo zote za wanamuziki wa Tanzania zilipokuwa zinapigwa nchini Kenya, zilikuwa na haki ya kulipwa na kwamba CHAMUDATA kwa wakati huo, ilifikia makubaliano na wenzao wa Kenya kwamba fedha hizo zilikuwepo, lakini ufuatiliaji wa vyombo vinavyohusika kiserikali ulikuwa mbovu.

                                           HALI YA MUZIKI

Akizungumzia tungo za wanamuziki wa Tanzania kimashairi, Mapili alisema hazikuwa zikivutia sana kama ilivyokuwa kwa wanamuziki wa miaka ya 60 hadi 80. Alilaumu mtindo wa bendi nyingi kutunga na kurekodi nyimbo nyingi kwa wakati mmoja, ambazo zilitungwa bila mpangilio wa kuvutia.



Kwa upande wa waimbaji na wapigaji wa ala za muziki wa enzi zake, marehemu Mapili alieleza kuvutiwa na watunzi na waimbaji mahiri wa zamani wa mkoani Morogoro, marehemu Salum Abdalla na marehemu Mbaraka Mwinshehe. Pia alieleza kuvutiwa na kiongozi wa bendi ya Shikamoo Jazz hadi sasa, Salum Zahor na bendi za Western Jazz, Tabora Jazz, Jamhuri Jazz na Atomic Jazz.

Alisema nyimbo zilizotungwa na kuimbwa na wanamuziki hao na bendi zao bado zinapendwa hadi sasa kutokana na ala kupangiliwa kwa ufundi wa hali ya juu na mashairi kuwa na mvuto wa aina yake.

Marehemu Mapili pia aliwalalamikia viongozi wa serikali waliokuwa wakisimamia maslahi ya wasanii kwa kutowapa kipaumbele, badala yake walikuwa wakipenda kuwatumia katika hafla mbalimbali za kitaifa na kuwalipa ujira kidogo.

Alisema matatizo ya wanamuziki yalikuwa yakieleweka wazi, lakini viongozi wa serikali walikuwa wakiyaafumbia macho. Vilevile alilaumu mtindo wa kuhamisha masuala yanayohusu utamaduni kutoka wizara moja hadi nyingine na hivyo kukwamisha juhudi zao za kutetea maslahi yao.

Mkongwe huyo wa muziki alisema maonyesho ya Top Ten yaliyokuwa yakiandaliwa na CHAMUDATA kwa kushirikiana na Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), yaliwavutia mashabiki wengi na kuleta ushindani uliosaidia kuinua kiwango cha muziki, lakini baada ya Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) kuingilia kati na kutaka wawe waandaaji, yalikufa kabisa.

Alisema tamaa ya viongozi wa BASATA ndiyo iliyosababisha hali hiyo, kwa kudhani kuwa kulikuwepo na manufaa fulani yaliyotokana na mashindano hayo.

                    ASHAURI MUZIKI WA ASILI UENZIWE

Ili kuinua kiwango cha muziki nchini wakati huo, marehemu Mapili alitoa mwito kwa wanamuziki wa Tanzania kupiga muziki wa kiasili na kuacha kupiga muziki wa kuiga kutoka nchi jirani, hasa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo.

"Kuna umuhimu hivi sasa kubadili mwelekeo wetu kimuziki na kufuata nyayo za wenzetu wa Tatunane na Tanzanites. Tujaribu kuuondoa muziki wetu kwenye ala za asili na kuuweka kwenye ala za kisasa. Hivi ndivyo wafanyavyo hata wenzetu wa mataifa mbalimbali hapa Afrika,"alisema.

Alitoa mfano wa baadhi ya nyimbo nyingi za asili zilizopigwa na bendi za Tanzania kuwa zinavutia, hivyo aliwashauri wanamuziki kuendeleza juhudi hizo, ikiwezekana kujifunza zaidi namna ya kutumia ala mbalimbali za kisasa za muziki ili waweze kwenda na wakati.

Marehemu Mapili pia alizishauri bendi za Kitanzania kutoajiri idadi kubwa ya wanamuziki, hali inayoweza kusababisha mishahara na marupurupu yao kuwa hayaridhishi. Alishauri bendi kuwa na idadi  ndogo ya wanamuziki ili ufanisi na maslahi ya wanamuziki yawe ya kuridhisha.

Aliwataja wanamuziki waliokuwa wakimvutia wakati huo kuwa ni Moshi William (sasa marehemu), Remmy Ongara (naye marehemu) na Hassan Bitchuka.

Alimsifu marehemu Moshi kuwa tungo zake zilikuwa zinagusa hisia, nyimbo za Remmy zilikuwa na hisia kali na mashairi ya matukio na kwamba sauti ya Bitchuka ina mvuto na iwezayo kumliwaza msikilizaji.

                                         ALIVYOANZA MUZIKI

Marehemu Mapili alizaliwa mwaka 1942 mkoani Lindi. Alisoma katika shule ya msingi ya Lionja Mission kuanzia 1949 hadi 1956, ambapo alikatisha masomo na kupelekwa kusoma masomo ya  Quraan.

Alianza kujishughulisha na muziki mwaka 1960, katika bendi ya White Jazz ya Lindi na mwaka uliofuata, alichukuliwa na marehemu Ahmad Omar kwenda Mtwara, alikojiunga na bendi ya Mtwara Jazz.

Mwaka 1963, alirejea tena Lindi na kujiunga na bendi ya Jamhuri, ambayo baadaye aliibadili jina na kuiita TANU Youth League. Baadhi ya wanamuziki aliokuwa nao katika bendi hiyo ni Athumani Manzi, Ali Bamtoto na Kaisi.

Mwaka 1965, alifuatwa na aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Kilwa wakati huo ili kwenda kufungua bendi ya muziki, ambayo aliita Lucky Star Jazz. Aliiongoza bendi hiyo kwa miezi michache kabla ya kuamua kuhamia Dar es Salaam baada ya kufuatwa na marehemu Ahmed Kipande wa Kilwa Jazz.

Huko alikutana na wanamuziki wengine nyota wa wakati huo kama vile Saidi Vinyama, Hassan Shabani, Juma Town, Athumani Omar, Kisi Rajabu, Abdu Baker na Juma Mrisho.

Baadhi ya nyimbo maarufu alizotunga wakati huo ni Kutyangatyanga mpunguti, Doli, Nililazwa jela na Kukurukakara mwatati.

Alikaa Kilwa Jazz kwa miezi michache kabla ya uongozi wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kumuomba kuanzisha bendi, ambayo aliiongoza kwa miezi michache na kuamua kubisha hodi Polisi Jazz, baada ya kufuatwa na Mzee Lawi Sijaona. Huko akateuliwa kuwa mwalimu wa muziki.

Mwaka 1969, alifuatana na bendi ya kwanza ya wanawake hapa nchini, Womes Jazz, ambayo alikuwa akiifundisha muziki, kwenda Kenya kushiriki kwenye sherehe za siku ya Kenyatta.

Baadhi ya wanamuziki aliokwenda nao Kenya ni pamoja na Mama Raheli, Kijakazi Mbegu, Mwanjaa Ramadhani, Siwema Mponji, Mwamvita Mwagoha, Rukia Hassan, Mary Kilima na mmoja aliyemtaja kwa jina la Josephina.

Akiwa katika bendi ya Polisi Jazz, Mapili aliweza kutunga nyimbo kadhaa zilizompatia umaarufu mkubwa. Baadhi ya nyimbo hizo ni Pongezi viongozi Tanzania, Kashma Kaligi, Josephina, Afrika tutaikomboa, Teddy, Dunia ni watu, Ulimi wa pilipili na Hongera Zimbabwe.

Aliiacha bendi ya Polisi mwaka 1980, akiwa na cheo cha sajenti na kujiunga na Tanzania Stars, ambayo ilikuwa ikipiga zaidi nyimbo za kuiga. Baadaye aliishauri kubadili mwelekeo na kuanza kupiga nyimbo zao wenyewe. Ndipo alipoibuka na tungo kama vile Mawazo, Jamila, Chiriku, Sanura mtoto wa Ilala, Safari sio kifo na Tuzo gani nimpe mke wangu.

Aliamua kustaafu muziki mwaka 1987 na kujikita zaidi katika kuisimamia CHAMUDATA, akiwa bado mwenyekiti. Akiwa kiongozi wa chama hicho,alitunga wimbo wa kuomboleza kifo cha Rais wa kwanza wa Msumbiji, marehemu Samora Machel, aliyefariki dunia mwaka 1986, akishirikiana na marehemu Marijani Rajabu.

Vilevile alishiriki katika kuunda kundi la Tanzania All Stars, lililorekodi nyimbo nne, ambazo ni Kifo cha Samora, Miaka 10 ya CCM, Azimio la Arusha na Kuwajibika.

MPINZANI WA CHEKA AWASILI NA KUTEMA CHECHE

 


Bondia Mserbia anayeishi Uingereza, Geard Ajetovic (katikati) akiwa na Mkurugenzi wa Advanced Security, Juma Ndambile (kushoto) na Promota Jay Msangi (kulia) katika mkutano na  waandishi wa habari jana.  Ajetovic atapigana na Francis Cheka Jumamosi kwenye viwanja vya leaders club kuwania mkanda wa uzito wa Super Middle wa Mabara wa chama cha WBF


Bondia Mserbia anayeishi Uingereza, Geard Ajetovic (katikati) akizungumza na waandishi wa habari jana tayari kwa pambano lake la jumamosi dhidhi ya Franci Cheka. kushoto ni Mkurugenzi wa Advanced Security, Juma Ndambile na kulia ni promota Jay Msangi. Ajetovic atapigana na Francis Cheka Jumamosi kwenye viwanja vya leaders club kuwania mkanda wa uzito wa Super Middle wa Mabara wa chama cha WBF.
 Mkurugenzi wa Advanced Security, Juma Ndambile (katikati) akizungumza katika mkutano huo.

 Na Mwandishi wetu
Bondia Geard Ajetovic amewasili nchini na kumuita bondia nyota wa ngumi za kulipwa nchini ,Francis “SMG” Cheka kuwa ni ‘babu’ na hawezi kupigwa na bondia huyo pamoja na kupigana katika ardhi ya Tanzania.
Ajetovic alisema kuwa anamjua Cheka  kwani amemuona kwenye pambano lake dhidi ya Thomas Mashali na kusema kuwa ‘amekwisha’ na kamwe si bondia wa kupambana naye.
Alisema kuwa Cheka amepigwa na bondia ambaye si lolote wala chochote na atampiga kabla ya raundi ya tano katika pambano hilo la ubingwa wa Mabara la uzito wa Super Middle unaotambuliwa na chama cha WBF.
“Cheka ni babu, si bondia wa kiwango changu, nimemuona na hana chochote kwangu, siwezi kupoteza pambano hili, ni rahisi ndiyo maana nimewahi kufika siku moja kabla ya muda niliopanga kuja hapa,” alisema Ajetovic.
Mkurugenzi wa Kampuni ya  Advanced Security, Juma Ndambile aliwahakikishia mashabiki  wa ngumi za kulipwa nchini kuwa maandalizi ya pambano hilo yamekamilika bada ya ujio wa Ajetovic.
Ndambile alisema kuwa maofisa wa Chama cha WBF, ikiwa pamoja na Rais wake, Howard Goldberg na mwamuzi wa pambano hilo ambao watawasili leo.
“Kama nilivyosema hapo awali, dhamira kubwa ya kampuni ya Advanced Security in kuendeleza mchezo wa ngumi za kulipwa nchini hasa kwa mabondia kufaidika na vipaji vyao na si vinginevyo,”
“Ili kufikia lengo letu, Advanced Security imeamua kuwashirikisha mabondia chipukizi katika mapambano ya utangulizi. Mabondia hao chipukizi wanatarajia kutoa changamoto kwa mabondia maarufu ambao pia watashiriki katika pambano hilo,” alisema Ndambile.
Alisema kuwa wameandaa mabondia chipukizi ili kupamba siku hiyo. Alisema kuwa Mohamed Bakari atapambana na Cosmas Cheka katika pambano la uzito wa feather la raundi nane (8) huku Mohamed Matumla ataonyeshana kazi na Mustapha Dotto katika pambao la uzito wa Light la raundi nane pia.
Bondia mkongwe na maarufu nchini, Mada Maugo ataingia ulingoni kwa kupambana na bondia kutoka Mbeya, Baraka Mwakansope baadala ya bondia Abdallah “Dulla Mbabe” Pazi kama ilivyotangazwa awali.
Alisema kuwa pia siku hiyo, bondia wa kike, Lulu Kayage atazichapa na bondia nyota kutoka mkoa wa Mbeya, Mwamne Haji katika pambano la uzito wa fly lilillopangwa kuwa la raundi sita.

WACHEZAJI TWIGA STARS WATEMBELEA DUKA LA AIRTEL


Ofisa huduma kwa wateja wa Airtel , Juma Hassan akitoa maelezo ya jinsi ya kupata huduma mbalimbali za kisasa kwa timu ya taifa ya wanawake ya Twiga Stars walipotembelea duka la kisasa la Airtel Expo liliko Morocco jijini Dar es Salaam.
Wachezaji wa timu ya taifa ya wanawake ya Twiga Stars wakimfatilia kwa makini Ofisa wa huduma kwa wateja wa Airtel Bw Stephen Makongoro  wakati alipokuwa akitoa maelezo ya huduma na bidhaa mbalimbali zinazotolewa na kampuni ya simu za mkononi ya Airtel. Twiga Stars ilitembelea duka jipya la Airtel Expo lililopo jijini Dar es salaam.

Baadhi Wachezaji wa timu ya taifa ya wanawake ya Twiga Stars wakitumia vifaa mbalimbali pamoja na simu za kisasa zilizopo katika duka la Airtel Expo wakati timu hiyo ilipotembelea duka hilio Jana, akishuhudia ni Ofisa huduma kwa wateja wa Airtel , Boaz
 Kikosi kizima cha timu ya taifa ya wanawake ya Twiga Stars pamoja na uongozi wa timu hiyo na baadhi ya wafanyakazi wa Airtel wakiwa katika picha ya pamoja wakati timu hiyo ilipotembelea duka la kisasa la Airtel Expo lililopo Morocco jijini Dar Es Salaam.
 Ofisa Uhusiano wa Airtel Bi Jane Matinde (katikati) pamoja na Mkurugenzi wa kitengo cha huduma kwa wateja Adriana Lyamba (nyuma) wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wachezaji wa Twiga Stars ambao wametokana na matunda ya mpango wa kuinua soka la vijana chini ya miaka 17 wa  Airtel Rising Stars.

BASATA YATOA ONYO KWA WASANII


Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) linawataka wasanii wote kuwa makini na wakuzaji Sanaa (Mapromota) au baadhi ya wanaojiita wadau wa Sanaa ambao wamekuwa wakitumia njia za kiulaghai na utapeli katika kujipatia faida na manufaa kupitia mgongo wa Wasanii.

Baraza linatoa angalizo hili kufuatia kuwepo kwa ongezeko la matukio ya baadhi ya watu wanaojiita wadau wa Sanaa ambao wamekuwa wakiwadanganya wasanii na kuwalaghai kwa kuwaahidi fursa mbalimbali kama za maonesho ya ndani na nje ya nchi ambazo hata hivyo zimekuwa zikiishia katika kuwaletea wasanii matatizo kiuchumi na kijamii.

Aidha, watu hao wamekuwa wakitumia majina ya viongozi wa Serikali kuwatapaeli wasanii na kujipatia fedha isivyo halali.

BASATA linapenda kuwakumbusha wasanii kwamba kabla hawajaingia makubaliano yoyote na mtu, asasi au kampuni yoyote wawasiliane na wanasheria au watoe taarifa Ofisi za Utamaduni za wilaya au manispaa zilizo karibu nao ili kuhakikisha wanaepuka ulaghai na udanganyifu kutoka kwa watu hao wasio waaminifu.

Aidha, kwa wasanii walioko Dar es Salaam BASATA linawaelekeza kufika Ofisi zake zilizoko Ilala Sharif Shamba jijini Dar es Slaam ili wapate msaada wa kisheria na kujiridhisha kama makubaliano yao ni halali na ya uhakika.

Mwisho kabisa, BASATA linapenda kuwakumbusha wasanii kwa ujumla kwamba, tangu Januari Mosi mwaka 2013 tasbia za muziki na filamu ni rasmi hivyo Wasanii wote hawana budi kusajiliwa na Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) na wanafanya kazi kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na taratibu za uendeshaji wa kazi za Sanaa nchini.

Aidha, kila msanii anawajibika kuhakikisha anafanya kazi na mtu, watu, asasi au kampuni iliyo na vibali halali vya kuendesha shughuli za Sanaa na si vinginevyo.

Sanaa ni Kazi, Tuitunze, Kuikuza na Kuithamini

Godfrey L. Mngereza

Katibu Mtendaji – BASATA

YANGA YASONGA MBELE KOMBE LA SHIRIKISHO


YANGA jana ilisonga mbele katika michuano ya soka ya Kombe la Shirikisho (FA) baada ya kuilaza JKT Mlale mabao 2-1.

Katika mechi hiyo iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, timu hizo mbili zilikwenda  mapumziko zikiwa sare ya bao 1-1.

Kocha Hans van der Pluijm wa Yanga alilazimika kupangua kikosi kilichocheza jana kwa kuwapanga baadhi ya wachezaji wapya, wakiwemo Matheo Anthony, Paul Nonga na Saidi Juma 'Makapu' huku akimrejesha dimbani nahodha Nadir Haroub 'Cannavaro' aliyekuwa nje kwa miezi kadhaa kutokana na kuwa majeruhi.

Baada ya kosakosa kadhaa kwa kila upande, JKT Mlale kutoka Ruvuma, inayoshiriki michuano ya ligi daraja la kwanza, ilikuwa ya kwanza kupata bao dakika ya 21 lililofungwa na Mgandila Shaaban baada ya kupokea krosi  kutoka kwa Edward Songo.

Nonga aliifungia Yanga bao la kusawazisha dakika ya 42, akiunganisha wavuni krosi kutoka kwa Godfrey Mwashiua.

Mabadiliko yaliyofanywa na Yanga katika kipindi cha pili, yaliiwezesha kubadili sura ya mchezo dakika ya 58 kwa kufunga bao lililopachikwa kimiani na Thabani Kamusoko.

TFF, KTA KUBORESHA SOKA YA WANAWAKE


Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), kwa kushirikiana na Taasisi binafasi ya Karibu Tanzania Association (KTA) kwa pamoja wamezindua programu ya maendeleo ya soka kwa wanawake vijana ili kuhamasisha usawa wa kijinsia, uwezeshaji kijamii na kiuchumi kwa wanawake nchini itakayofadhiliwa na Shirika la Forum Syd kutoka nchini Sweden.

Uwekaji saini wa mkataba huo wa ushirikiano umefanywa na Katibu Mkuu wa TFF, Mwesigwa Selestine na Mia Mjengwa Bergdahl, Mratibu wa Programu hiyo kutoka taasisi ya Karibu Tanzania Sweden katika ofisi za TFF zilizopo Karume.

Programu hiyo ni ya aina yake ambayo haijapata kufanyika nchini inalenga kujenga mfumo utakaotumiwa nchi nzima katika kutoa elimu na mafunzo kwa soka la wanawake kwenye maeneo ya ufundi (makocha), waamuzi (refarii), uongozi na tiba kwenye michezo.

Pia itawezesha kuendeleza vipaji kwa wachezaji wanawake vijana na kuongeza hali ya kujitambua na kujiamini kwa walengwa. Lengo ni kuongeza idadi ya wachezaji wenye ubora na viwango kwa soka la wanawake vijana katika ngazi zote, hivyo kuifanya programu hii kuwa nyenzo katika kuwawezesha wanawake. 

Kwa kuanzia kozi 20 za soka la wanawake vijana kwenye Vyuo 20 vya maendeleo ya wananchi zitaanzishwa kwenye kanda saba.  Jumla ya wanawake vijana 600 ikiwamo 30 kutoka katika kila chuo cha Maendeleo ya Wananchi watashiriki.

Katika programu hii, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto wanashiriki kikamilifu kwa kuwezesha wanafunzi na miundo mbinu ya vyuo vya maendeleo ya wananchi vilivyo chini ya wizara hiyo kutumika katika kufanikisha programu hii.

Mafunzo yatatolewa sambamba na mafunzo mengine ya kawaida yanayotolewa kwenye Vyuo Vya Maendeleo ya Wananchi, kama vile maarifa ya jumla na mafunzo ya ufundi.

Friday, February 19, 2016

TIKETI ZA MECHI YA SIMBA, YANGA ZAANZA KUUZWA LEO


Tiketi za mchezo wa watani wa jadi wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania (VPL) kati ya Yanga SC dhidi ya Simba SC Jumamosi, Februari 20, 2016 zimeanza kuuzwa leo Ijumaa saa 2 asubuhi leo asubuhi katika vituo 10 mbalimbali vilivyopo jijini Dar es salaam.

Vituo vinavyotumika kuuza tiketi za mchezo huo ni ofisi za TFF – Karume, Buguruni Oilcom, Ubungo Oilcom, Uwanja wa Taifa Temeke, Mavuno House - Posta, Dar Live Mbagala, Breakpoint – Kinondoni, Kidongo Chekundu – Mnazi Mmmoja, Mwenge na Kivukoni Ferry.

Kiingilio cha juu cha mchezo huo ni shilingi Elfu Thelathini (30,000) kwa VIP A, Elfu Ishirini (20,000) VIP B & C, Elfu Kumi (10,000) kwa viti vya rangi ya machungwa (Orange), na Elfu Saba (7,000) kwa viti vya rangi ya bluu na kijani.

Milango ya Uwanja wa Taifa itafunguliwa kuanzia saa 5 kamili asubuhi, huku barabara ya Chang,ombe ikifungwa kuanzia asubuhi, na magari maalumu yenye stika maalumu ndiyo yatakayoruhushiwa kuingia eneo la uwanja wa Taifa kwa kupitia barabara ya Mandela na uwanja wa Uhuru.

Upande wa ulinzi, Jeshi la Polisi na vyombo vingine vya usalama watakuwepo kuhakikisha usalama wa wapenzi wa mpira watakaokuja kushuhudi mchezo huo, vitu kama silaha, vilevi, mabegi na vitu vyenye ncha havitaruhusiwa kuingia ndani ya uwanja.

Shirikisho linawaomba wapenzi, wadau na washabiki wa mpira wa miguu nchini kununua tiketi katika magari ya kuuzia tiketi katika vituo vilivyotajwa, ili kuondokana na tatizo la kuuziwa tiketi zisizo halali kwa mchezo huo.

Mchezo huo utachezeshwa na mwaamuzi Jonesia Rukyaa (Kagera), akisaidiwa na mwamuzi Josephat Bulali (Tanga), Samwel Mpenzu (Arusha) wote wakiwa wakiwa waaamuzi wenye beji za FIFA, mwamuzi wa akiba Elly Sasii (Dar) na Kamisaa wa mchezo huo atakua Khalid Bitebo (Mwanza).

LIGI KUU BARA KUENDELEA KESHO, SIMBA DIMBANI NA YANGA


Ligi Kuu ya Vodacom inatarajiwa kuendelea wikiendi hii mzunguko wa 20 kwa michezo nane kuchezwa katika viwanja mbalimbali huku Jumamosi michezo mitano ikichezwa kwa kila timu kusaka pointi tatu muhimu katika ligi hiyo.

Uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam, Yanga SC v Simba SC watakua wakichuana kusaka uongozi wa Ligi hiyo katika mchezo namba 153, huku Mgambo Shooting wakiwakaribisha Tanzania Prisons katika uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.

Wagonga Nyundo wa jiji la Mbeya, Mbeya City watawakaribisha Azam FC katika uwanja wa Sokoine mjini humi, mjini Shinyanga chama la wana Stand United watawakaribisha JKT Ruvu katika uwanja wa Kambarage, huku Toto Africans wakicheza dhidi ya Kagera Sugar katika uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.

Jumapili Ndanda FC watakua wenyeji wa African Sports uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara, Mwadui FC watakua wenyeji wa Coastal Union uwanja wa Mwadui Complex mkoani Shinyanga, huku wana lizombe Majimaji FC wakicheza dhidi ya Mtibwa Sugar katika uwanja wa Majimaji mjini Songea

Ligi Daraja la Pili (SDL) inatarajiwa kuendelea wikiendi hii katika mzunguko wa lala salama (raundi ya 9), kwa timu zote 24 kushuka dimbani pointi 3 muhimu katika msimamo ili kuweza kupanda ligi daraja la kwanza msimu ujao.

Jumamosi Kundi A, Green Warriors v Transit Camp (Mabatini), Singida United v Abajaro Tabora (Namfua), Mvuvumwa FC v Mirambo (Lake Tanganyika).

Kundi B, Jumapili Pamba FC v Madini FC (CCM Kirumba), AFC ARUSHA v Bulyanhulu (Sheikh Amri Abeid), huku Jumatatu Alliance School v JKT Rwamkoma (CCM Kirumba).

Jumamosi Kundi C, Cosmopolitan FC v Abajaro Dar (Karume), Jumapili Mshikamano FC v Kariakoo FC (Mabatini), Villa Squad v Changanyikeni (Karume).

Kundi D, Jumamosi African Wanderes v Mkamba Rangers (Wambi Mafinga), Jumapili Wenda FC v Sabasaba FC (Sokoine) huku Jumatatu The Mighty Elephant v Mbeya Warriors (Majimaji)

Thursday, February 18, 2016

KAMATI YA NIDHAMU KUAMUA HATMA YA TIMU ZINAZOTUHUMIWA KUPANGA MATOKEO


Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi ya Ligi (Kamati ya Saa 72) imekutana jana (Februari 16, 2016) kupitia taarifa za mechi mbili za Kundi C la Ligi Daraja la Kwanza ya StarTimes kati ya JKT Kanembwa na Geita Gold SC, na Polisi Tabora na JKT Oljoro ambapo Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) lilisimamisha matokeo yake hadi taarifa hizo zitakapopitiwa.

JKT Kanembwa ilifungwa mabao 8-0 na Geita Gold SC katika mechi iliyofanyika Uwanja wa Lake Tanganyika mjini Kigoma, wakati Polisi Tabora ilishinda mabao 7-0 dhidi ya JKT Oljoro kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora.

Baada ya kupitia taarifa hizo na vielelezo vingine, Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi imeonyesha mashaka kutokana na kuwepo viashiria vya upangaji wa matokeo (match fixing).

Kwa vile suala hilo linahusisha masuala ya kinidhamu, na kwa kuzingatia Ibara ya 50(1) na (11) ya Katiba ya TFF na Ibara ya 69 ya Kanuni za Nidhamu za TFF, Kamati ya Saa 72 imemuelekeza Katibu Mkuu wa TFF apeleke suala kwenye Kamati ya Nidhamu ya TFF kwa ajili ya uchunguzi na hatimaye kufanya uamuzi.

Tuesday, February 16, 2016

SAMATTA AANZA RASMI KUVAA UZI WA GENK YA UBELGIJI

MSHAMBULIAJI Mbwana Samatta (wa tatu kushoto) akipongezana na wachezaji wenzake wa Genk ya Ubelgiji baada ya kuibuka na ushindi katika moja ya mechi za ligi ya nchi hiyo
Hapa Samatta (kushoto) akikabiliana na mchezaji wa timu pinzani katika moja ya mechi za ligi hiyo

KUZIONA SIMBA NA YANGA BUKU SABA, PAMBANO KUCHEZESHWA NA MWANAMAMA


Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) leo limetangaza viingilio vya mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) Jumamosi kati ya watani wa jadi Simba SC dhidi ya Yanga SC utakaochezwa Uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam, huku kiingilio cha chini kikiwa ni Shilingi elfu saba tu (7,000).

Kiingilio cha juu cha mchezo huo kitakua shilingi Elfu Thelathini (30,000) kwa VIP A, Elfu Ishirini (20,000) VIP B & C, Elfu Kumi (10,000) kwa viti vya rangi ya machungwa (Orange), na Elfu Saba (7,000) kwa viti vya rangi ya bluu na kijani.

 Tiketi za mchezo huo zitaanza kuuzwa siku ya Ijumaa saa 2 kamili asubuhi katika vituo vya TFF (Karume), Buguruni Olicom, Ubungo Oilcom, Kidongo Chekundu (Mnazi Mmoja), Posta (Agip), Dar Live (Mbagala), Uwanja wa Taifa, Makumbusho Stand, Kivukoni Ferry.

Mchezo huo utachezeshwa na waamuzi wote wenye beji za FIFA, mwamuzi wa katikati Jonesia Rukyaa (Kagera), akisaidiwa na Josephat Bulali (Tanga), Samwel Mpenzu (Arusha), mwamuzi wa akiba Elly Sasii (Dar) huku Kamisaa wa mchezo huo akiwa Khalid Bitebo (Mwanza).

Ligi hiyo ya Vodacom itaendelea Jumamosi kwa michezo sita, Young Africans v Simba (Taifa), Mbeya City v Azam (Sokoine), Stand United v JKT Ruvu (Kambarage), Toto Africans v Kagera Sugar (CCM Kirumba), Mgambo Shooting v Tanzania Prisons (Mkwakwani) na Majimaji FC v Mtibwa Sugar (Majimaji).

Jumapili ligi hiyo itaendelea kwa michezo miwili, Mwadui FC v Coastal Union uwanja wa Mwadui Complex, huku Ndanda FC wakicheza dhidi ya African Sports uwanja wa Nagwanda Sijaon mjini Mtwara.

Monday, February 15, 2016

TFF YAIPONGEZA AFRICAN LYON KUREJEA LIGI KUU



Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limeipongeza timu ya African Lyon FC ya jijini Dar es salaam kwa kufanikiwa kupanda ligi kuu ya Vodacom (VPL) msimu ujao, baada ya kuwa vinara wa Kundi A katika ligi hiyo iliyomalizika jana.

African Lyon imeungana na timu ya Ruvu Shooting FC ya Mlandizi mkoa wa Pwani iliyokua timu ya kwanza kupanda ligi kuu wiki iliyopita kutoka kundi B.

TFF inaitakia kila la kheri Africa Lyon FC katika maandalizi ya msimu mpya wa Ligi Kuu ya Vodacom, kwa kujiandaa vizuri na mikiki mikiki ya VPL ambayo ina jumla ya timu 16 na kila klabu kucheza jumla ya michezo 30 kwa msimu nyumbani na ugenini.

TFF YASIKITISHWA KAZIMOTO KUMPIGA MWANAHABARI



Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limepokea kwa masikitiko taarifa ya kupigwa kwa mwandishi wa habari za michezo wa gazeti la Mwanaspoti nchini, Mwanahiba Richard na kiungo wa timu ya Simba SC Mwiny Kazimoto mjini Shinyanga.

Kufuatia kitendo hicho kilichotokea wakati wa mazoezi, TFF imesema tukio liliofanywa na mchezaji huyo ni kinyume na sheria, taratibu/kanuni zinazoendesha mpira wa miguu nchini, hivyo wanakilaani kitendo hicho kwa nguvu zote.

Kwa kuwa tukio lilitokea wakati wa mazoezi, mpaka sasa TFF bado haijapokea taarifa rasmi kuhusiana na suala hilo.

SIMBA HIYOOOOOOOO


MABAO mawili ya mshambuliaji Mganda, Hamisi Friday Kiiza yametosha kuipa Simba SC ushindi wa 2-1 dhidi ya wenyeji, Stand United katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara jioni ya leo Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga.
Kwa ushindi huo, Simba SC inapanda kileleni mwa Ligi Kuu kwa mara ya kwanza msimu huu, ikifikisha pointi 45, baada ya kucheza mechi 19, ikiwazidi kwa pointi mbili, mabingwa watetezi, Yanga SC ambao hata hivyo wana mchezo mmoja mkononi. 

Kiiza alifunga mabao yake katika dakika za 34 na 47, hivyo sasa anaongoza kwa kufunga Ligi Kuu akifikisha mabao 16 dhidi ya 14, ya mshambuliaji wa mahasimu, Yanga SC, Mrundi Amissi Tambwe.
Stand United ilipata bao lake la kufutia machozi dakika ya 90 kupitia kwa David Ossuman. Mechi nyingine za Ligi Kuu leo, African Sports imeifunga 1-0 Mgambo Uwanja wa Mkwakwani, Tanga wakati kocha Mmalawi, Kinnah Phiri ameanza na ushindi wa 5-1 dhidi ya Toto Africans Uwanja wa Sokoine, Mbeya.
Mabao ya MCC yamefungwa na Raphael Alfa kwa penalti dakika ya tano, baada kiungo mshambuliaji wa Mbeya City Ditrim Nchimbi kuchezewa vibaya kwenye boksi, Ramadhani Chombo 'Redondo' dakika ya 35, Haruna Moshi 'Boban', dakika ya 41 na 43 na Meshack Samueli dakika ya 79, wakati bao pekee la Toto lilifungwa na Japhet Mkala dakika ya 78.
Ndanda FC imeifunga 1-0 Majimaji Uwanja wa Nangwanda Sijaona.

BODI YA LIGI KUU YAKUNJUA MAKUCHA, YAMTOZA FAINI 500,000 KEVIN YONDANI, YANGA NAYO YALIMWA FAINI



Kikao cha Kamati ya Kusimamia na Kuendesha ligi (Kamati ya Masaa 72) kimekutana Jumatano katikati ya wiki kupitia taarifa na ripoti mbalimbali za michezo ya Ligi Kuu (VPL), na Ligi Daraja la Kwanza (FDL) zinazoendeea kutimua vumbi katika viwanja mbalimbali nchini.

Ligi Kuu ya Vodacom

Mchezaji Kelvin Yondani wa Yanga amefungiwa mechi tatu na kupigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) baada ya kumpiga usoni kwa box la dawa Dk. Mganga Kitambi wa Coastal Union wakati akitoa huduma kwa kipa wake katika mechi namba 121 kati ya timu hizo iliyofanyika Januari 30, 2016 kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.

Yondani alitenda kosa hilo baada ya kumuomba maji Daktari huyo, lakini akamnyima. Adhabu huyo imetolewa kwa kuzingatia Kanuni ya 37(3) ya Ligi Kuu Toleo la 2015 ambapo baada ya kutumia adhabu ya mechi hizo, hataruhusiwa kucheza hadi atakapokuwa amelipa faini hiyo.

Naye Dk. Kitambi anapelekwa kwenye Kamati ya Nidhamu kwa kitendo chake cha kumrudishia Yondani kwa kumpiga ngumi. Kitendo cha Daktari huyo ni kinyume cha Kanuni ya 41(2), na pia Kanuni ya 36 kuhusu mchezo wa kiungwana.

Klabu ya Yanga imepigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) kwa mujibu wa Kanuni ya 42(1) kutokana na washabiki wake kuwatupia chupa za maji wachezaji wa Coastal Union walipokuwa wakishangilia bao la pili.

Nayo klabu ya Coastal Union imepigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) kwa washabiki wake kuvamia uwanja baada ya filimbi ya mwisho, kitendo ambacho ni kinyume cha Kanuni ya 14(11) inayohusu taratibu za mchezo.

Mgambo Shooting imepigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) kwa kutumia chumba cha waandishi wa habari badala ya kile cha timu wakati wa mechi kati yao na Simba iliyochezwa Februari 3, 2016 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Adhabu hiyo imetolewa kwa uzingativu wa Kanuni ya 14(13) ya Ligi Kuu kuhusu taratibu za mchezo.

Kocha Ally Jangalu wa Coastal Union ameripotiwa kutoa matamashi ya kuidhalilisha TFF kwenye vyombo vya habari kuwa Refa wa mechi kati yao na Ndanda SC iliyochezwa mjini Tanga alikwenda na maelekezo ya kuhakikisha wapinzani wao wanashinda. Coastal Union ilifungwa bao 1-0 katika mechi hiyo iliyochezwa Februari 4, 2016. Suala lake linapelekwa Kamati ya Nidhamu.

Mchezaji Daud Jumanne amefungiwa mechi tatu na kupigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) baada ya kumkanyaga vidole kwa makusudi mchezaji wa Simba aliyekuwa akisubiri kupatiwa matibabu kwenye mechi kati ya timu hizo iliyofanyika Februari 7, 2016 kwenye Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga.

Adhabu hiyo imetolewa kwa mujibu wa Kanuni ya 37(3) ya Ligi Kuu Toleo la 2015. Pia kwa kuzingatia Kanuni ya 37(20), hauruhusiwi kucheza mechi inayofuata ya timu yake mpaka faini hiyo iwe imelipwa. Iwapo atacheza kabla ya kulipa faini hiyo, timu yake itapoteza mchezo husika.

Klabu ya Stand United imepigwa faini ya sh. 500,000 kwa kutoingia vyumbani wakati wa mapumziko katika mechi dhidi ya African Sports iliyochezwa Februari 6, 2016 kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga. Kitendo hicho ni kinyume na Kanuni ya 14(13) kuhusu taratibu za mchezo.

Kamishna wa mechi hiyo namba 140, Idelfonce Magali amepewa karipio kwa kutoripoti vizuri tukio hilo, wakati Refa Elly Sasii amepewa karipio kali kwa kutoripoti kabisa tukio hilo.

Ligi ya StarTimes

Wachezaji Ismail Nkulo, Said Juma, Idd Seleman na Edward Amos wa Polisi Dodoma wanapelekwa kwenye Kamati ya Nidhamu baada ya kumzonga, kumtolea lugha ya matusi ya nguoni na kutaka kumpiga Refa katika mechi ya Ligi ya StarTimes kati ya timu yao na African Lyon iliyofanyika Januari 30, 2016.

Kitendo hicho katika mechi hiyo iliyochezwa Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma ni kinyume cha Kanuni ya 37(7) ya Ligi Daraja la Kwanza kuhusu udhibiti wa wachezaji.

Kiongozi wa Friends Rangers, Heri Mzozo anapelekwa Kamati ya Nidhamu kwa kutoa lugha chafu kwa viongozi na waamuzi muda wote wa mchezo dhidi ya Ashanti United uliofanyika Januari 31, 2016 kwenye Uwanja wa Karume jijini Dar es Salaam. Vitendo vyake ni kiyume na Kanuni ya 41(2) ya Ligi Daraja la Kwanza kuhusu udhibiti wa viongozi.

Mwamuzi Msaidizi namba 2 kwenye mechi kati ya Kimondo na Ruvu Shooting, Idd Mikongoti wa Dar es Salaam ameripotiwa na Kamishna kuondoka na timu ya Ruvu Shooting kwa kupanda basi lao mara baada ya mchezo, kitendo ambacho ni kinyume na maadili ya uamuzi. Suala lake limepelekwa kwenye Kamati ya Waamuzi kwa ajili ya hatua stahiki dhidi yake.

Klabu ya Geita Gold imepigwa faini ya sh. 1,000,000 (milioni moja) na onyo kali kwa kukataa kuingia kwenye chumba cha wachezaj, na badala yake kutumia chumba kingine ambacho pia walijisadia haja ndogo wakati wa mechi dhidi ya Polisi Tabora iliyofanyika Januari 31, 2016 kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora.

Nayo Polisi Tabora imepigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) kutokana na kitendo cha mshabiki wake kupita pembezoni ya uwanja (running track) kwa kasi wakati mechi hiyo dhidi ya Geita Gold ikiendelea.

Pia klabu ya Polisi Tabora imepewa onyo kali kutokana kipa wa timu yake kuvaa jezi ambayo haikuwa na nembo (logo) ya Mdhamini wa Ligi Daraja la Kwanza wakati wa mechi hiyo.

Geita Gold imepewa ushindi wa pointi tatu na mabao matatu baada ya JKT Oljoro kugomea mchezo kati ya timu hizo uliofanyika Februari 6, 2016 kwenye Uwanja wa Nyankumbu Girls mkoani Geita. Timu hiyo iligomea mechi hiyo dakika 70 baada ya kufungwa bao la pili. Kitendo hicho ni kinyume cha Kanuni ya 29(1) ya Ligi Daraja la Kwanza.

Pia JKT Oljoro imepigwa faini ya sh. 1,000,000 (milioni moja) kutokana na kitendo hicho kwa kuzingatia Kanuni ya 29(4), wakati wachezaji wake Kapteni Shaibu Nayopa na Sunday Paul waliomvamia na kumpiga Refa wanapelekwa Kamati ya Nidhamu kwa ajili ya kuchukuliwa hatua stahiki.

Naye Kocha Msaidizi wa JKT Oljoro, Bunu Abdallah  ambaye alitolewa kwenye benchi la timu yake kwa kosa la kumtolea lugha chafu Mwamuzi Msaidizi namba 1 anapelekwa Kamati ya Nidhamu kwa ajili ya hatua stahiki.

NAIBU WAZIRI WA MICHEZO ATEMBELEA TFF



Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Annastazia Wambura  ametembela ofisi za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na kupata kujionea shughuli mbalimbali zinazondeshwa na shirikiso hilo.

Akiongea na viongozi na wachezaji wa timu ya Taifa ya Wanawake “Twiga Stars” waliopo kambini kujiandaa na mchezo wa kuwania kufuzu kwa Fainali za Mataifa Afrika kwa Wanawake dhidi ya Zimbambwe, Wambura amesema Serikali itashirikiana na TFF kuhakikisha timu inapata ushindi katika mchezo huo wa awali utakaochezwa Machi 4, 2016.

Wambura amewataka wachezaji wa Twiga Stars kuwa na nidhamu ndani na nje ya uwanja, kujituma na kuiipenda kazi yao hiyo ambayo kwa sasa ni ajira itakayoweza kuwasaidia kuendesha maisha yao.

Aidha Wambura amesema anaamini kuwa Twiga Stara bado wana nafasi ya kufanya vizuri katika mchezo unaowakbalili, na kuwaomba kupambana zaidi kuhakikisha inapanda na kushinda nafasi ya kwanza Afrika katika soka la wanawake.

Pia amesema wizara yake inashugulikia maombi ya TFF kuiomba wizara ya TAMISEMI ikasimishe mchezo wa mpira wa miguu katika mashindano ya UMITASHUMITA na UMISSETA yaweze kusimamiwa na TFF kwani wao ndio wenye utaalamu wa mchezo huu

TFF YATUMA RAMBIRAMBI KWA MWANAHABARI HAMISI DAMBAYA


Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limetuma salamu za rambirambi kwa familia ya mwandishi wa habari za michezo nchini Hamis Dambaya kufuatia kufiwa na mkewe, mwanae pamoja mama mkwe wake.

Katika salamu hizo, TFF imempa pole Dambaya kwa msibu huo mzito uliomfika na kusema kwa niaba ya familia ya mpira wa miguu nchini, Shirikisho liko pamoja nao katika kipindi hichi kigumu cha maombelzo ya misiba hiyo.

Mkewe Hamis Dambaya, mwanane na mama mkwe wake wamefariki katika ajali ya bus la Simba Mtoto iliyotokea leo asubuhi katikati ya eneo na Muheza na Hale wakati wakiwa safarini kuelekea jijini Dar es salaam wakitokea mkoani Tanga.

MALINZI AMPONGEZA RAIS MPYA WA KFF


Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi ametuma salamu za pongezi kwa Rais mpya wa Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini Kenya (FKF), Nick Mwendwa kwa kuchaguliwa kuliongoza shirikisho hilo.

Katika salamu hizo, Malinzi amempongeza Mwendwa kwa nafasi hiyo aliyopewa kuliongoza soka la nchini Kenya, na kuahidi TFF itaendelea kushirikiana nae katika maendeleo ya mpira wa miguu kwa ukanda huu wa Afrika Mashariki.

Nick Mwendwa alishinda nafasi hiyo jana katika uchaguzi uliofanyika jijini Nairobi kwa kupata alama 50 kati ya 77 za wapiga kura wote na kupata nafasi hiyo iliyokua inashikiliwa na Samwel Nyamweya aliyemaliza muda wake.

SERENGETI BOYS KUKIPIGA NA SHELISHELI MICHUANO YA AFRIKA


Shirikisho la Mpira wa Miguu Barani Afrika (CAF) limetoa ratiba ya kuwania kufuzu kwa Fainali za Mataifa Afrika kwa vijana wenye umri chini ya miaka 17 (U-17) zitakazofanyika nchini Madagascar mwakani kwa timu ya Taifa ya Tanzania (Serengeti Boys) kuanza na Shelisheli.

Katika ratiba hiyo iliyotolewa makao makuu ya CAF, Cairo Misri na nakala yake kutumwa kwa TFF, Tanzania imepangwa kucheza mchezo wa kwanza dhidi ya Shelisheli kati ya Juni 24,25,26 nchini na marudaino kuchezwa Julai 01,02,03 nchini Shelisheli.

Mshindi kati ya mchezo huo namba 15 na16 atacheza dhdi ya timu ya Taifa ya  Afrika Kusini katika hatua inayofuata ya 16 bora, na kisha baadae kupata timu 8 zitakazofuzu kwa fainali hizo zitakazofanyika nchini Madagascar mwakani.

Fainali za Kombe la Dunia (FIFA U17) kwa vijana wenye umri chini ya miaka 17 zitafanyika mwezi Septemba waka 2017 nchini India.

KOMBE LA SHIRIKISHO KUENDELEA KUTIMUA VUMBI FEB 26


Ratiba ya michuano ya Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) imetolewa leo, ambapo jumla ya timu 16 zinakutana katika hatua hiyo (16 bora) itakayoanza kutimua vumbi wikiendi ya Februari 26-1 Machi 2016 katika viwanja mbalimbali nchini.

Michuano hiyo iliyoshirikisha jumla ya timu 64 kutoka ngazi za Ligi Kuu, Ligi Daraja la Kwanza na Ligi Daraja la Pili, inaingia katika mzunguko wa nne huku kukiwa na timu kutoka katika ngazi zote za ligi za TFF nchini.

Ijumaa tarehe 26 Februari kutachezwa michezo miwili ambapo, Ndanda FC watawakaribisha JKT Ruvu katika uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara, huku Coastal Union wakiwa wenyeji wa wakata miwa wa Mtibwa Sugar katika uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.

Jumamosi, Februari 27, Mwadui FC watawakaribisha Rhino Rangers katika uwanja wa Mwadui Complex - Shinyanga, Jijini Mbeya Tanzania Prisons watacheza na mshindi kati ya Mbeya City/Wenda FC kwenye uwanja wa Sokoine jijini Mbeya.

Februari 28, michezo mitatu itachezwa, Simba SC watawakaribisha Singida United katika uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam, Panone FC watacheza dhidi ya Azam FC uwanja wa Ushirika mjini Moshi, huku Toto African wakicheza na wachimba madini wa Geita Gold katika uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.

Raundi hiyo itamalizika Machi 01, 2015 kwa mchezo mmoja kuchezwa ambapo Young Africans watawakaribisha JKT Mlale katika uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam.

Bingwa wa michuano ya Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) mwaka huu ataiwakilisha Tanzania kwenye Mashindano ya kombe la Shirikisho Barani Africa (CAF CC) mwakani 2017.

Monday, February 8, 2016

KAMUSOKO MCHEZAJI BORA WA LIGI KUU DESEMBA 2015




Mchezaji Thaban Kamusoko amechaguliwa kuwa mchezaji bora wa Ligi Kuu ya Vodacom kwa mwezi Disemba, 2015 baada ya kumshinda mchezaji mwenzake wa Yanga (Amissi Tambwe).

Kamusoko ameisaidia timu yake ya Yanga katika michezo iliyochezwa mwezi Disemba kwa kushiriki dakika zote katika michezo mitatu iliyochezwa mwezi wa Disemba.

Kwa kuchaguliwa kwake kuwa mchezaji bora wa wa mwezi Disemba, Kamusoko atakabidhiwa zawadi ya fedha taslimu shilingi milioni moja (1,000,000) kutoka kwa wadhamini wa ligi Kampuni ya simu za mkononi ya Vodacom.

SIMBA, YANGA ZAENDELEA KUMEREMETA LIGI KUU BARA



SIMBA na Yanga jana ziliendelea kuchanua katika michuano ya soka ya ligi kuu ya Tanzania Bara, baada ya kuibuka na ushindi dhidi ya Kagera Sugar na JKT Ruvu.

Wakati Simba iliichapa Kagera Sugar bao 1-0 kwenye Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga, watani wao Yanga walishusha kipigo cha mabao 4-0 dhidi ya JKT Ruvu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Pambano kati ya Simba na Kagera Sugar lilikuwa gumu na kali kutokana na kila timu kupania kushinda ili itoke uwanjani na pointi zote tatu.

Hata hivyo, mshambuliaji machachari Ibrahim Hajib ndiye aliyeiwezesha Simba kutoka uwanjani na ushindi baada ya kuifungia bao hilo la pekee na la ushindi.

Nayo Yanga ilijipatia mabao yake manne kupitia kwa Simon Msuva aliyefunga mawili, Haruna Niyonzima na Hamisi Tambwe.

Wakati huo huo, Azam jana ilirejea ligi kuu kwa kishindo kwa kupata ushindi kiduchu wa bao 1-0 dhidi ya Mwadui FC katika mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Azam Complex, ulioko Chamazi, Dar es Salaam.

Katika mechi zingine za ligi hiyo zilizochezwa Mbeya City ilitoka suluhu na Prisons Uwanja wa Sokoine, Mbeya, Ndanda FC ililazimishwa sare ya 1-1 na Mtibwa Sugar Uwanja wa Nangwanda Sijaona, Mtwara, Toto Africans ilishinda 2-1 dhidi ya Coastal Union Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza, Majimaji imeshinda 1-0 dhidi ya Mgambo JKT Uwanja wa Majimaji, Songea, wakati African Sports ilitoa sare ya 0-0 na Stand United Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.

Sunday, February 7, 2016

OCEAN VIEW KUZIDHAMINI MAFUNZO NA JKU


MENEJA wa hoteli za Zanzibar Ocean View Jacob Makundi (kulia), akimkabidhi Mkuu wa Idara ya Michezo wa Vyuo vya Mafunzo Khamis Ali Machenga, shilingi 5,000 zikiwa gharama za tiketi za mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kati ya klabu ya Mafunzo na AS Vita ya DRC itakayochezwa Februaei 13, 2016, ambazo zilikwishachapishwa na kuanza kuuzwa. Kampuni ya hoteli za Zanzibar Ocean View imeamua kubeba gharama hizo pamoja na za mechi ya JKU na Gaborone United ya Botswana kuwania Kombe la Shirikisho.

(Picha na Ameir Khalid).

Na Salum Vuai, ZANZIBAR
UONGOZI wa kampuni ya hoteli za Zanzibar Ocean View (ZGH), umeamua kubeba mzigo wa gharama za mechi za wawakilishi wa Zanzibar katika michuano ya klabu barani Afrika zitakazochezwa mwishoni mwa wiki ijayo.
Mechi hizo za kwanza za raundi ya awali, ni ile ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambapo Mafunzo wataikaribisha AS Vita kutoka Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, na JKU dhidi ya Gaborone United ya Botswana.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Februari 6, 2016 katika ukumbi wa Nyerere ulioko hoteli ya Zanzibar Ocean View mjini hapa, Meneja wa hoteli hizo Jacob Makundi, amesema hatua hiyo inalenga kuwafanya mashabiki wafike kwa wingi uwanjani siku ya mechi hizo.
Alifahamisha kuwa, tayari kampuni yake imezinunua tiketi elfu kumi (elfu tano kwa kila mechi) zilizobaki baada ya nyengine kuuzwa, kwa gharama ya shilingi elfu kumi, na zitagaiwa kwa mashabiki watakaofika uwanja wa Amaan siku za michezo hiyo bila malipo yoyote.
Makundi alifahamisha kuwa, kampuni yake pia itatoa fulana maalumu kwa wachezaji na viongozi wa klabu hizo, ambazo watavaa kabla ya mechi ya kwanza na watakaposafiri kwenda DRC na Botswana kwa ajili ya michezo ya marudiano.
Meneja huyo amezitaja gharama nyengine ambazo kampuni hiyo itazibeba, ni kutoa punguzo la asilimia 75 kwa waamuzi, makamisaa, viongozi na wachezaji wa timu za wageni kwa huduma ya malazi na chakula kwenye hoteli zake.
Ili kuwapa nguvu wachezaji wa Zanzibar, Makundi aliahidi kuwa kampuni hiyo itatoa zawadi ya shilingi milioni tano iwapo timu itashinda hapa nyumbani, na kuongeza kuwa ushindi huo utakuwa chachu kwao kufikiria motisha zaidi kwa mechi za ugenini.
“Kwa kuwa sisi ni wadau wakubwa wa michezo, tumeona iko haja ya kuwashajiisha wawakilishi wetu hawa ili wafanye vizuri na kuinua jina la Zanzibar katika soka la kimataifa na tunatoa wito kwa taasisi nyengine zijitokeze kuongeza nguvu,” alieleza.
Mapema, Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Michezo Zanzibar (BTMZ) Khamis Abdallah Said, aliushukuru uongozi wa kampuni hiyo, akisema unaonesha uzalendo kwa nchi katika kuunga mkono juhudi za kuendeleza michezo.
Naye Abdallah Juma Mohammed, aliyemuwakilisha Mkurugenzi wa kampuni hiyo yenye hoteli tano kubwa Unguja na Pemba Amani Ibrahim Makungu, alisema Zanzibar Ocean imeanza lakini mlango uko wazi kwa wengine kuzisaidia timu hizo na pia michezo mingine.
Akitoa shukuani kwa niaba ya timu zote mbuli, Mkuu wa Michezo katika Jeshi la Kujenga Taifa (JKU) Khamis Mohammed Suleiman, alisema ufadhili waliopata utawatia nguvu ya kuhakikisha wanaipeperusha vyema bendera ya Zanzibar kwenye michuano hiyo.
Jumamosi Februari 13, Mafunzo wataikaribisha AS Vita katika mechi ya Ligi ya Mabingwa, wakati siku inayofuata JKU watakuwa wenyeji wa Gaborone United kutika Botswana kuwania Kombe la Shirikuso.
Mechi zote hizo zitachezwa katika uwanja wa Amaan mjini Zanzibar kuanzia saa 10:00 jioni, na zile za marudiano zitapigwa wiki mbili baadae.

Friday, February 5, 2016

TFF YAONYA UPANGAJI MATOKEO KATIKA LIGI ZINAZOENDELEA


Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF) limewaonya viongozi wa vilabu, wachezaji, waamuzi na wasimamizi wa mchezo kutojihusisha na upangaji wa matokeo (Match fixing) katika michezo inayoendelea sasa katika ligi za ngazi mbalimbali za nchini.

TFF imejipanga na inasimamia vizuri michezo ya Ligi Kuu (VPL), Daraja la Kwanza (FDL), Daraja la Pili (SDL) na Azam Sports Federation Cup (ASFC) inayoendelea na yoyote atakayebainika kujihusisha na mchezo huo wa upangaji matokeo, hatua kali za kinidhamu zitachukuliwa.

Katika michezo yote inayoendelea TFF ina maofisa wake wanaofuatilia kwa ukaribu michezo hiyo, hivyo endapo kiongozi, mchezaji, msimamizi au mwamuzi atabainika kujihusisha na upangaji wa matokeo hatua kali zitachukuliwa .

TFF inawaomba viongozi, wachezaji, wasimamizi wa michezo na waamuzi kutojihusisha na mchezo huo wa upangaji wa matokeo kwani kufanya hivyo ni kukiuka katiba, sheria na kanuni zinaongoza mpira wa miguu nchini.

SIMBA, YANGA KUENDELEA KUTIMULIANA VUMBI LIGI KUU JUMAPILI


 Ligi Kuu ya Vodacoma Tanzania bara raundi ya 18 inatarajiwa kuendelea wikiendi hii kwa michezo nane kuchezwa katika viwanja mbalimbali nchini, Jumamosi ukichezwa mchezo mmoja na Jumapili kuchezwa kwa michezo saba.

Jumamosi ligi ya kuu ya Vodacom itaendelea kwa mchezo mmoja tu, ambapo katika uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga, African Sports watawakaribisha Stand United kutoka mkoani Shinyanga.

Michezo saba itachezwa siku ya Jumapili ambapo maafande wa JKT Ruvu watakuwa wenyeji wa Young Africans katika uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam, Mbeya City dhidi ya Tanzania Prisons uwanja wa Sokoine jijini Mbeya, na Ndanda FC watawakaribisha Mtibwa Sugar katika uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara.

Kagera Sugar watacheza dhidi ya Simba SC katika uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga, Azam FC watawakaribisha Mwadui FC uwanja wa Chamazi, Majimaji dhidi ya Mgambo uwanja wa Majimaji mjini Songea na Toto Africans watawakaribisha Coastal Union uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.

AFRICAN LYON, POLISI DAR DIMBANI WIKIENDI HII LIGI YA FDL


Ligi Daraja la Kwanza nchini (FDL) raundi ya 13 inatarajiwa kuendelea wikiendi hii kwa timu 24 [kucheza michezo 12 katika viwanja tofauti, huku kundi A na C kukiwa na ushindani mkali kwa kila timu kuwania kupanda ligi kuu ya Vodacom msimu ujao.

Kundi A, African Lyon watawakaribisha Polisi Dar katika uwanja wa Mabatini – Mlandizi, Ashanti United dhidi ya KMC uwanja wa Karume, huku Jumapili Kiluvya wakiwakaribisha Polisi Dodoma uwanja wa Mabatini – Mlandizi na Friends Rangers wakicheza na Mji Mkuu uwanja wa Karume jijini Dar es salaam.

Kesho Jumamosi, Kundi B Polisi Morogoro watacheza dhidi ya Njombe Mji uwanja wa Jamhuri, Morogoro, Kurugenzi FC dhidi ya JKT Mlale uwanja wa Wambi – Iringa, Burkinafaso dhidi ya Lipuli na Kimondo watawakaribisha Ruvu Shooting kwenye uwanja wa Vwawa – Mbozi.

Kundi C, Polisi Mara FC watawakaribisha Panone FC uwanja wa Karume mjini Musoma, Geita Gold watacheza dhidi ya JKT Oljoro uwanja wa Nyankumbu mjini Geita, JKT Kanembwa watakua wenyeji wa JKT Oljoro uwanja wa Lake Tanganyika mjini Kigoma, huku Rhino Rangers wakicheza dhidi ya Mbao FC uwanja wa Ali Hassani Mwinyi mjini Tabora.

LIGI YA SDL KUENDELEA WIKIENDI HII


Raundi ya saba ya Ligi Daraja la Pili nchini (SDL) inaendelea wikiendi hii kwa michezo 12 kuchezwa nchini, kwa timu 24 kusaka pointi kutoka makundi ya A,B,C na D kuwania nafasi nne za juu ili kuweza kupanda ligi daraja la kwanza msimu ujao.

Kundi A, Leo Ijumaa Abajalo Tabora watakua wenyeji wa Mvuvumwa uwanja wa Ali Hassan Mwinyi Tabora, Green Warriors dhidi ya Singida United uwanja wa Mabatin Mlandizi (jumatatu) na Mirambo FC watacheza dhidi ya Transit Camp siku ya jumatatu uwanja wa Ali Hassani Mwinyi mkoani Tabora.

Kundi B, Kesho Jumamosi AFC ya Arusha watakua wenyeji wa Alliance Schools uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Madini FC watacheza dhidi ya JKT Rwamkoma uwanja wa Mbulu, huku Bulyanhulu FC watawakaribsiha Pamba FC uwanja wa Kamabrage mjini Shinyanga.

Kundi C, Leo Ijumaa Abajalo Dar watacheza dhidi ya Mshikamano uwanja wa Karume jijini Dar es salaam, kesho Jumamosi Kariakoo FC watawakaribisha Changanyikeni katika uwanja wa Ilulu – Lindi, na Cosmopolitani watacheza dhidi ya Villa Squad siku ya jumatatu katika uwanja wa Karume jijini Dar es salaam.

Kundi D, Jumamosi Mighty Elephant watacheza dhidi ya Wenda FC uwanja wa Majimaji mjini Songea, Mbeya Warriors watawakaribisha Mkamba Rangers uwanja wa Sokoine jijini Mbeya, huku Jumapili Sabasaba FC wakicheza dhidi ya African Wanderers uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro.

Wednesday, February 3, 2016

SIMBA YAONGEZA DOZI LIGI KUU BARA


SIMBA SC imejiweka sawa kwenye mbio za ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara baada ya kuifunga Mgambo JKT mabao 5-1 jioni ya leo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Ushindi huo unaifanya Simba SC ifikishe pointi 39 baada ya kucheza mechi 17, sasa ikiwa inazidiwa pointi moja tu na mabingwa watetezi, Yanga SC walio kileleni, wakifuatiwa na Azam FC yenye pointi 39 pia.
Mshambuliaji Mganda, Hamisi Kiiza ‘Diego’ aliifungia Simba SC bao la kwanza dakika ya tano akimalizia krosi ya mshambuliaji Ibrahim Hajib.
Kiiza akakosa penalti dakika ya 14 iliyookolewa na kipa Mudathir Khamis, kufuatia Henry Chacha kuunawa mpira kwenye boksi.
Lakini Mwinyi Kazimoto akafunga bao la pili dakika ya 28 kwa shuti kali kutoka nje ya boksi baada ya kugongeana vizuri na Hajib.
Hajib akaenda kufunga mwenyewe bao la tatu dakika ya 42 baada ya kuwachambua mabeki watatu wa Mgambo na kipa wao Mudathir Khamis, kufuatia pasi ya Kazimoto.
Daniel Lyanga aliyetokea benchi kuchukua nafasi ya Hajib kipindi cha pili, aliifungia Simba SC bao la nne kwa shuti kali kutoka nje ya boksi baada ya pasi ya kiungo Said Ndemla.
Kiiza akahitimisha karamu ya mabao ya Simba SC kwa kufunga bao la tano dakika ya 82 akimalizia krosi ya Hassan Kessy, ambaye amecheza kwa kiwango cha juu leo.
Fuluzulu Maganga ‘akachafua gazeti’ kwa kuifungia Mgambo bao la kufutia machozi dakika ya 88 baada ya mabeki wa Simba SC kumuacha wakidhani ameotea.

CHANZO CHA HABARI: BLOGU YA BINZUBEIRY

YANGA YAWEKEWA NGUMU NA PRISONS, ZATOKA SARE 2-2



YANGA SC imezidi kupoteza matumaini ya kutetea ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara baada ya jioni ya leo kulazimishwa sare ya 2-2 na Prisons Uwanja wa Sokoine, Mbeya.
Matokeo hayo hayaiondoi kileleni Yanga SC ikifikisha pointi 40 baada ya kucheza mechi 17, mbele ya Azam FC na Simba SC wenye pointi 39 kila mmoja.
Lakini Azam FC wana viporo wawili, wakati Simba SC ndiyo wamecheza mechi 17 kama Yanga.
Yanga SC walikuwa wa kwanza kupata bao dakika ya 35 kupitia kwa mshambuliaji wake Mrundi, Amissi Tambwe aliyefunga kichwa akimalizia krosi ya kiungo Mnyarwanda, Haruna Niyonzima
Prisons wakasawazisha bao hilo kupitia kwa Jeremiah Juma Mgunda aliyefunga kwa kichwa pia dakika ya 40 akimalizia krosi ya Mohammed Mkopi.
Mkopi akaifungia Prisons bao la pili dakika ya 62 kwa kichwa pia akimalizia mpira wa adhabu uliopigwa na kiungo wa zamani wa Yanga SC, Juma Seif ‘Kijiko’.
Mfungaji bora wa Ligi Kuu msimu uliopita, Simon Msuva aliyetokea benchi kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Deus Kaseke aliisawazishia Yanga kwa penalti dakika ya 84 baada ya beki Meshak Suleiman kuunawa mpira kwenye boksi.

CHANZO CHA HABARI: BLOGU YA BINZUBEIRY

Tuesday, February 2, 2016

SIMBA, YANGA DIMBANI TENA KESHO LIGI KUU YA BARA



Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania bara mzunguko wa 17 unatarajiwa kuendelea kesho Jumatano kwa michezo sita kuchezwa katika viwanja mbalimbali, huku kila timu ikisaka pointi tatu muhimu kwenye msimamo wa ligi hiyo.

Kesho Jumatano, Simba SC watakua wenyeji wa maafande wa Mgambo Shooting kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam, JKT Ruvu watawakaribisha Mbeya City katika uwanja wa kumbukumu ya Karume Ilala, huku Mtibwa Sugar wakicheza dhidi ya Toto Africans katika uwanja wa Manungu – Turiani.

Jijini Mbeya, Tanzania Prisons watakua wenyeji wa vinara wa ligi hiyo Young Africans katika uwanja wa Sokoine, Wana kimanumanu African Sports watacheza dhidi ya Mwadui FC uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga, huku wakata miwa wa Kagera Sugar wakiwakaribisha Majimaji FC katika uwanja wa Kamabarage mjini Shinyanga.

Alhamisi ligi hiyo itaendelea kwa kuchezwa mchezo mmoja tu, Wagosi wa Kaya Coastal Union watawakaribisha Ndanda FC katika uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.

Michezo ya viporo ya Azam FC imepangiwa ratiba, mchezo dhidi ya Tanzania Prisons utachezwa Februari 24 uwanja wa Sokoine jijini Mbeya, huku mchezo dhidi ya Stand United ukichezwa Machi 16 katika uwanja wa Azam Complex.

TFF YAMPONGEZA JK


Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanznaia (TFF), Jamal Malinzi amempongeza Rais wa awamu ya nne Jakaya Kikwete kwa kukubali uteuzi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu barani Afrika (CAF) na GAVI utakaomfanya kuwa bingwa wa chanjo na balozi wa mradi wa Africa United Duniani.

“Familia ya mpira wa miguu inajua umuhimu wa chanjo na hasa katika maendeleo ya vipaji na wanamichezo kwa ujumla na jinisi chanjo inavyoweza kuwapa watoto siyo tu fursa ya maendeleo bali pia haki ya kuishi” ilisema sehemu ya barua hiyo iliyosainiwa na Rais wa TFF, Jamal Malinzi.

Katika barua hiyo, Malinzi ameelezea furaha ya TFF kuona kiongozi wa Tanzania akiongoza mapambano ya kuokoa afya na uhai wa kizazi cha sasa na kijacho katika Afrika na dunia kwa ujumla.

“TFF itaunga mkono juhudi zako ili kufanikisha malengo yaliyowekwa na ushirika wa chanjo” ilimalizia barua hiyo ambayo nakala yake imetumwa kwa Rais wa Caf, Issa Hayatou.

TFF: HATUNA VITA NA ZFA


Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF), limesema hakuna vita kati ya Shirikisho na Chama cha Soka Zanzibar (ZFA) bali mawasiliano yanaendelea kati ya TFF na vyombo husika kuhakikisha ZFA ambaye ni mwanachama mshiriki wa CAF anaendesha shughuli zake kwa mujibu wa taratibu.

Kanuni na taratibu za CAF ziko wazi kuhusu nani aongoze Chama cha Soka Zanzibar (ZFA) na anapatikana kwa utaratibu upi.

Kikubwa ni kuzuia ZFA isipate madhara ya kufungiwa na Chama Cha Mpira wa Miguu barani Afrika (CAF).