KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Tuesday, April 28, 2015

YANGA BINGWA 2015


NA AMINA ATHUMAN

TIMU ya Yanga imetwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa 2014/2015 huku ikiendeleza wimbi la kugawa dozi kubwa baada ya jana kufumua Polisi Morogoro mabao 4-1.

Mchezo huo ulifanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, ambapo Amisi Tambwe aliendelea kuchana nyavu za timu mpinzani kwa jana kupachika mabao matatu.

Kwa matokeo hayo, Yanga imetwaa ubingwa huo na kuweka rekodi ya kutwaa taji hilo kwa mara ya 25 tangu kuanza kwa Ligi Kuu Tanzania Bara mwaka 1965.

Yanga ilichukua ubingwa kwa mara ya kwanza mwaka  1968, 1969,1970, 1971, 1972, 1974, 1981, 1983, 1985, 1987, 1989, 1991, 1992, 1993, 1996, 1997, 1998, 2002, 2005, 2006, 2007/08, 2008/09, 2010/11, 2012/13 na 2014/15.

Tambwe ndiye aliyekuwa shujaa wa mchezo huo kwa kutupia 'hat trick' kabla ya Simon Msuva kukamilisha karamu ya mabao kwa kupachika bao la nne.

Magwiji hao walianza kuandika bao la kwanza katika dakika ya  42 kupitia kwa Tambwe baada ya kuunganisha pasi ya Msuva kabla ya kuachia shuti kali lililojaa moja kwa moja wavuni.

Bao la pili lilipatikana dakika ya dakika ya 53 baada ya Tambwe kumalizia mpira uliopigwa na  Msuva na kumshinda kipa wa Polisi Morogoro Abdul Idad.

Tambwe aliendelea kuichachafya ngome ya Polis Moro, ambapo dakika ya  59 alipachika bao la tatu kabla ya  Msuva kukamilishabao la nne dakika ya 66 baada ya kumpiga chenga  Idad na kuachia shuti kali lililojaa moja kwa moja wavuni.

Polisi Moro ilipata bao la kufutia machozi dakika ya 83  kupitia kwa Nicolaus Kabipe baada ya kuachia shuti kali lililomshinda kipa wa Yanga Deogratius Munisi 'Dida'

Kutokana na matokeo hayo, Yanga imefikisha pointi 55 ambazo haziwezi kufikiwa na timu yeyote huku ikipakiza michezo miwili kibindoni.

Ushindi huo umeiwezesha Yanga kutangaza ubingwa na kuipiku Azam FC iliyokuwa ikishikilia kombe hilo msimu uliopita na kuipa nafasi ya kushiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika.

Katika mchezo huo, Yanga ilianza mchezo kwa kasi na dakika ya pili ilipata nafasi ya kupachika bao kupitia kwa Tambwe, lakini shuti lake lilitoka nje ya lango.

Yanga ilipata nafasi nyingine dakika ya nane kupitia kwa Kpah Sherman wakati Polisi Moro ilipata nafasi dakika ya 14, 27,33 na 72 kupitia kwa Suleiman Kassim na Bahanuzi lakini mipira yote ilitoka nje.

Yanga: Deogratius Munish, Juma Adbul, Oscar Joshua, Mbuyu Twite, Kelvin Yondan, Said Juma, Simon Msuva/Hussein Javus, Haruna Niyonzima, Amis Tambwe/Jerson Tegete, Mrisho Ngasa na Kpah Sherman.

Polisi Morogoro: Abdul Idad, Ally Teru, Hassan Mganga, Meshack Abel, Laban Kambole, Anafu Suleman, Adimin Bantu, Said Mkangu, Said Bahanuzi/Nicolaus Kibape, Suleman Kassim na James Ambrose/Mussa Mohamed.

No comments:

Post a Comment