KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, April 2, 2015

BEKI SIMBA ATOWEKA


BEKI wa kushoto wa klabu ya Simba, Ramadhani Kessy, ameweka bayana kuwa kamwe hatarajii kurejea katika kikosi cha timu hiyo hadi atakapopewa nyumba ya kuishi.

Akizungumza kwa njia ya simu kutoka Morogoro, Kessy amesema hakwenda Shinyanga na timu hiyo hadi atakapotimiziwa mahitaji yake.

Simba iliondoka jana kwenda Shinyanga kwa ajili ya mchezo wake wa ligi kuu ya Tanzania Bara dhidi ya Kagera Sugar, utakaopigwa kesho kwenye Uwanja wa Kambarage.

Kessy alisema alipofuatwa na uongozi wa klabu hiyo kwa ajili ya kumsajili, walimpa ahadi ya kumtafutia nyumba ya kuishi, lakini hadi sasa wameshindwa kuitekeleza.

"Nimeamua kuondoka Simba na kurudi Morogoro kupumzika. Nitakuwa tayari kurejea Simba baada ya uongozi kutekeleza ahadi hiyo,"alisema.

Alisema tangu alipoamua kujiunga na Simba, amekuwa akiishi maisha ya kutangatanga na wakati mwingine kusaidiwa sehemu ya kulala na wachezaji wenzake.

"Nimekuwa nikijituma sana kila ninapoichezea Simba. Pia nimevumilia sana, lakini naona sithaminiwi. Kila meneja wangu akiwasiliana na viongozi kuhusu suala langu, wanakataa kupokea simu yake,"alilalamika Kessy.

Hata hivyo, Katibu Mkuu wa Simba, Steven Ally, alidai kuwa mchezaji  huyo ameachwa kwenye safari ya Shinyanga kutokana na kiwango chake kutomridhisha.

Steven alisema uongozi wa Simba uliahidi kumtafutia mchezaji huyo nyumba ya kuishi na si kumnunulia nyumba kama anavyodai.

No comments:

Post a Comment