MUTOMBO Lufungula 'Audax (kushoto), akiwa na Kasongo Mpinda 'Clayton' katika moja ya maonyesho ya Bana Maquiz.
NA PETER
ORWA
WIKI chache
kabla ya kifo chake, mwaka 2010, mwimbaji mahiri wa muziki wa dansi, Kasaloo
Kyanga, alieleza changamoto aliyokumbana nayo wakati anajiunga na bendi ya Maquiz
Original mwanzoni mwa miaka ya 1980, kwamba:“Nilikutana na ‘Predezshee saba’…
Nikasema hapa ‘taweza’ kweli? “
Ujumbe wake ni
kwamba, wakati huo anajiunga akiwa na umri wa miaka 24, alikutana na magwiji
saba waimbaji unaomjumuisha Mutombo Lufungula Audax, akishirikiana na wengine
kama vile Mbuya Makonga ‘Adios, Kasongo Mpinda ‘Clyton’ na Kikumbi Mwanza
Mpango au King Kiki.
Leo hii ‘Predeshee’
huyo, Mutombo Lufungula Audax, hayupo tena kwa wiki moja sasa na alizikwa katika nyumba ya milele wiki moja iliyopita,
tukio lililotetemesha anga ya muziki nchini… Ni pigo kubwa ambalo limeacha masikitiko!
Marehemu huyo
ambaye ndiye mwanahisa na muasisi aliyebaki katika bendi ya Maquiz Du Zaire,
kati ya wenzake tisa waliounda zaidi ya miaka 50 iliyopita, nyumbani kwao,
Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC), wakati huo ikiitwa taifa hilo Congo na
baadaye Zaire.
Muasisi mwingine
aliye hai, lakini aliondoa hisa zake mapema kabla ya bendi kufilisika ni mpiga
solo mahiri, Nguza Vikings, ambaye baadaye alijiunga na Sambulumaa, kisha
akaanzisha bendi yake ya Achigo, kabla ya kukutwa na matatizo yaliyompeleka gerezani
kwa maisha yote.
Baadhi ya
wanahisa wengine ni Ilunga Lubaba, Mwema
Mujanga,’ Chibangu Katai, Robert Otrish na Chinyama Chiyaza, aliyekuwa kiongozi
wa bendi.
Audax
alizikwa Jumapili mchana iliyopita katika makaburi ya Kinondoni, baada ya kutanguliwa
na shughuli ya heshima za mwisho zilizofanyika katika Hospitali ya Mwananyamala,
Dar es Salaam.
Ni kifo
kinachotia simanzi katika tasnia ya muziki wa dansi, kwani gwiji mwingine
ninayethubutu kumtaja aliongeza ushindani katika mchuano kati ya Maquiz na
wapinzani wao, Orchestra Safari Sound, Kabeya Badu (65), naye alifariki mwaka
jana na kuzikwa katika makaburi hayo hayo ya Kinondoni.
Katika
historia yake, marehemu Kabeya aliwahi kupitia Maquiz kabla ya kujiunga na OSS
na kisha wakati fulani bendi ya Tancut Almasi Orchestra.
Mwimbaji mkongwe,
Tshimanga Kalala Assosa, ana maelezo ya ziada kuhusiana na kifo cha Audax,
ambacho kilitokana na maradhi ya kupooza yaliyomsumbua sana kwa miaka mitano
iliyopita.
“Ameteseka
sana,”anatamka Assosa, huku akifafanua kwamba kifo hicho kilitokea nyumbani kwa
marehemu Kimara King’ong’o, alikokuwa akiugua na hafichi kumtambulisha kuwa ni mtu
wake wa karibu.
Watu hao
wamefahamiana kwa takriban maisha yao yote, tangu zama za miaka ya 1950, wakiwa
kijijini kwao, Kamina Nsobongo, katika jimbo la Katanga, wakati huo ikiitwa
Jamhuri ya Congo na baadae ikawa Zaire mwaka 1965.
“Hata mara
ya mwisho nilipoenda nyumbani Congo (DRC), mama yake alikuja
nyumbani,”anasimulia Assosa na kufafanua kwamba marehemu Audax ana dada
anayeishi nchini, anayeitwa Kaiba.
Anafafanua
uhusiano wake na Audax kuwa, licha ya kutoka kijiji kimoja, walisoma shule moja
na anamfahamu kwamba katika maisha yake yote, Audax alikuwa mpenzi na mchezaji
mahiri wa mpira wa miguu, lakini akazama zaidi katika muziki kulikomfanya aache
soka na masomo.
“Mama zetu
pia walikuwa wanafahamiana sana,” anasema Assosa na kuongeza “Mara ya mwisho
nilipoenda Congo (DRC), mama yake alikuja nyumbani.”
Assosa anajitambulisha
kuwa na umri mdogo kwa marehemu Audax kwa wastani wa miaka miwili na alikuwa anasoma
madarasa ya chini yake, lakini binafsi hakubobea katika soka. Mapenzi yake
binafsi yaliozama kwenye masomo na kuimba kanisani.
Kwa mujibu
wa John Kitime, mwanamuziki mwingine mkongwe aliyewahi kupigia gita la rhythm
na besi kwa bendi kama Vijana na Tancut, marehemu Audax alizaliwa tarehe 9 ya
mwezi Oktoba ya mwaka 1945..
Assosa
anasimulia kwa hatua kisa cha Audax na baadhi ya wenzake ambao ndio wakawa
wanamuziki waasisi wa Maquiz, kwamba
kijijini kwao Kamina kulizuka makundi mengi ya vijana wanaobobea katika muziki
na kuunda bendi ndogo ndogo kijijini.
Moja ya
kumbukumbu alio nao Assosa ni kwamba, wakati wa harakati za kuelekea uhuru wa
Congo, yeye na marehemu Audax walikuwa katika kundi la vijana waliioonekana
wanaimba vizuri na waliteuliwa kwenda nchini Ubelgiji kumuimbia Mfalme wa taifa
hilo lilokuwa likiwatala.
Wakati huo
Audax alishakuwa ametawaliwa na muziki na kuacha masomo tangu kipindi kirefu.
“Tuliporudi
na sisi wengine ndio ukawa mwisho wa shule na hawa (vijana wenzake wa kijijini
akiwemo Audax) ndio walitufanya shule ikawa basi… ndio watu waliotufanya
tuvunje kalamu,” anasema Assosa.
Anafafanua
kwamba, hali ya kuzingirwa na vijana wanamuziki kijijini, ndio kulimteka naye azame
katika muziki na kuacha shule akiwa miongoni mwa vijana ambao awali walipenda
mno masomo.
Mwanamuziki
huyo anawataja wakongwe wa muziki nchini anaotoka pamoja kijijini Kamina
Nsabongo, ni pamoja na Mbombo wa Mbomboka na marehemu Issa Nundu, ambao katika
nafasi tofauti waliwahi kupitia bendi kama Makassy, Super Matimila, OSS na
Maquiz.
Assosa
anawataja wengine waliokuwa Maquiz ni, Nguza Vikings, Mbuya Makonga Adios na
Chinyama Chiyaza na anaongeza kuwa Adios alikuwa mwanakwaya mwenzake katika
kanisa analolitaja la Mtakatifu Bavo, akiwa mpiga kinanada na yeye mwimbaji wa
sauti ya pili, aliyodumu nayo hadi sasa katika dansi.
Kundi hilo
lililounda Maquiz likiwa na bendi yao kijijini lilianza na mkakati wa kuvuka
mpaka kwenda Uganda mwaka 1963, jambo ambalo Assosa hakukubaliana nalo na akaamua
kurudi nyumbani kutoka mpakani mwa nchi na baadaye alielekea Kinshasa alikovuma
kimuziki baada ya muda mfupi.
Lile kundi
lilounda Maquiz, wakati huo likiwa na jina la Super Gaby, baada ya kukaa
Uganda, lilihamia Tanzania mwaka 1972, ambapo Nguza na Audax walikuwa wamebaki
huko na muda mfupi walikuja kujiunga na wezao nchini.
Ikumbukwe,
mwaka 1971 taifa la Uganda utawala wake ulipinduliwa na kuchukuliwa na Rais Iddi
Amin Dada.
Bendi hiyo
ilipewa jina la Maquiz Du Zaire mwaka 1973, huku wakijozolea umaarufu, wakipiga
muziki katika ukumbi wa Mikumi Tours
iliyopo eneo la TAZARA, lililomilikiwa
na aliyekuwa mfanyabiashara maarufu wa Dar es Salaam, Mzee Batenga
Hata hivyo
hawakudumu sana, kutokana na eneo la ukumbi huo kuchukuliwa kwa ajili ya ujenzi
wa miundombinu ya stesheni ya TAZARA na walipata mkataba mwingine wa kupiga
katika ukumbi wa Tours and Hunters, eneo la Ubungo. Ulikuwa unamilikiwa na Hugo
Kisima, ambaye baadaye alimiliki bendi
ya OSS na ukumbi wa Safari Resort.
Mwanamuziki
Kitime, anamsifu Audax kwamba alikuwa mtunzi mahiri na mwalimu wa muziki katika
bendi ya Maquiz, iliyopitia mitindo mbalimbali kama vile Kamanyola Bila jasho,
ulioasisiwa na Kingi Kiki mwaka 1973, Sendema na Zembwela.
Naye Assosa,
anamwagia sifa kwamba, mbali na kuwa mtunzi, alikuwa mahiri katika kuchangia
mawazo bora kwenye tungo za ndani ya bendi na hata muundo wa sauti, akitoa
mfano kuna wakati alitoka na kujiunga na bedi ya Legho, lakini Audax aliwashawishi
wakurugenzi wenziwe hadi wakamrudisha.
“Alikuwa mtu
wangu wa karibu na alinipenda sana. Waliniita na hata nikasikia ile wanasema
‘nyongo ilitumbukia’ nikarudi Maquiz,” anasema Assosa.
Kwa mujibu
wa Kitime, marehemu aliuhusudu sana utunzi wake wa kibao cha Mpenzi Luta,
ingawaje kuna mingine mingi aliozitunga
ikiwemo kibao ‘Nani Atanitetea.’
Wakati fulani,
Audax alitunga kibao Kisebengo, kilichobeba ujumbe wenye kijembe kwa mwezake kutoka
kijijini Kamina – Nguza Vikings, aliyeamua kuichukua hisa zake za Maquiz, katika
dakika za mwisho baada ya safari ndefu ya kuunda bendi na maisha ya pamoja
kimuziki.
Ikumbukwe,
kuna wakati bendi ya Maquiz Du Zaire ilifikia kilele cha mafanikio, ambapo
wakurugenzi wake wakiwemo, kina Audax mbali na kupiga muziki, waliunda kampuni
iliyoitwa OMACO.
Assosa
anasema, wakati wanaendeleza mafanikio ya muziki kupitia Maquiz, upenzi wa
Audax katika soka hakuwahi kukoma, na ncjini alikuwa shabiki mkubwa wa klabu ya
Yanga na hata ulipotokea mgawanyiko ukiozaa timu ya Pan African, alijiunga nayo
na kuwa na kadi ya uanachama.
Hata baada
ya kusambaratika, Audax kwa kushirikiana na wenzake kama vile Mwema Mujanga na
Adios waliasisi bendi ya Bana Maquiz, iliyokuwa na makao makuu katika baa ya
Savoy, eneo la Tabata na baadaye walimuongeza mwenzao, Assosa.
Hata hivyo, Assosa
ana simulizi ya simanzi kwamba kwa bahati mbaya bendi hiyo ilifilisika vyombo,
huku Adios akiwa ameshafariki. Katika mihangaiko Audax na Asosa walifanikiwa
kupata msaada wa vyombo kwa mkopo wa shilingi milioni nane, ambao
mfanyabiashara mmoja aliyetoa sharti la hisani wamlipe kidogo kidogo.
Assosa anasema,
tukio ambalo hatolisahau na ni la kumsikitisha, lililotokea miaka mitano iliyopita, kwamba siku ambayo aliahidiwa kukabidhiwa vyombo
na yeye akiwa katika mchakato wa kuvichukua, ni kwamba muda mfupi baadaye
alipigiwa simu ya kufahamishwa Audax amepatwa na kiharusi, yuko hospitalini
Muhimbili.
Anasema,
tangu wakati huo amekuwa mgonjwa na kamwe hakuwahi hata kuviona vyombo ambavyo
alishiriki katika mchakato wote wa kuvipata, jambo ambalo Assosa hafichi hisia
zake akisema ‘inamuuma sana.’
Ni historia
itayakayobaki kuwa ya kudumu, marehemu Audax ni nembo ya kudumu ya bendi ya Maquiz,
akiwa mwanahisa muasisi wa mwisho aliyekuwa amebaki.
MUNGU
AMBARIKI APUMZIKE KWA AMANI.