KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, June 12, 2014

WAMBURA KIDUME, AIBWAGA KAMATI YA UCHAGUZI SIMBA


MGOMBEA wa nafasi ya rais katika uchaguzi mkuu wa klabu ya Simba, Michael Wambura amepitishwa kuwania nafasi hiyo katika uchaguzi mkuu ujao.

Wambura aliondolewa katika mbio hizo na Kamati ya Uchaguzi ya Simba chini ya Mwenyekiti, Damas Ndumbaro kwa madai ya kukosa sifa.

Kamati ya Rufani ya Uchaguzi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), jana ilimtangaza Wambura kuwa mgombea halali wa nafasi hiyo katika uchaguzi mkuu wa Simba, uliopangwa kufanyika Juni 29 mwaka huu.

Kufuatia kupitishwa kuwania nafasi hiyo, Wambura sasa atachuana vikali na mpinzani wake wa karibu, Evans Aveva.

Wambura alifutiwa uanachama wa Simba katika kikao cha Kamati ya Utendaji ya klabu hiyo, kilichofanyika Mei 5, 2010 kwa madai ya kuipeleka klabu hiyo mahakamani katika kesi namba 100/2010.

Inadaiwa Wambura alikiuka katiba ya Simba Ibara za 11 (1), (e), (2) 12 (3) na 55 kwa kosa la kupeleka masuala ya michezo mahakamani.

Mwenyekiti wa Kamati ya Rufani ya Uchaguzi ya TFF, Julius Lugaziya, alisema Wambura amerejeshwa kwa kuwa Kamati ya Utendaji ya Simba ilishindwa kulinda katiba ya klabu hiyo.

Alisema tangu asimamishwe, amekuwa akifanya shughuli za Simba bila kuzuiwa na kulipa ada ya uanachama, kushiriki mikutano ya wanachama na ya dharula kwa kipindi chote.

"Sharti la msingi la katiba kuwa ni mwanachama halali tu ndiye anaruhusiwa kushiriki kwenye mikutano,"alisema.

"Uongozi au mwanachama wa Simba kwa mujibu wa katiba ana uwezo wa kuhoji mahudhurio ya mwanachama asiye na haki ya kushiriki, lakini kwa Wambura haikuwa hivyo,"alisema.

Alisema endapo chombo au kikao chochote kinafanya uamuzi na baadhi ya wajumbe wasiopaswa kushiriki na kutoa uamuzi, uamuzi uliopitishwa unakosa nguvu za kisheria.

"Kama hivyo ndivyo, je vikao vilivyoandaa katiba ya Simba na kuipitisha, ambavyo Wambura alishiriki, vina athari gani kuhusu uhalali wa katiba ya Simba?" Alihoji

Alisema hata vikao vilivyoteua kamati ya uchaguzi, ambavyo Wambura alishiriki, nayo itakuwa batili.

No comments:

Post a Comment