KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Sunday, June 8, 2014

TFF YATUMA RAMBIRAMBI MSIBA WA MWANAKATWE

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limepokea kwa masikitiko kifo cha aliyekuwa Katibu Mkuu wake (wakati huo ikiitwa FAT), Kanali mstaafu Ali Hassan Mwanakatwe kilichotokea leo asubuhi (Juni 7 mwaka huu) katika Hospitali Kuu ya Jeshi (GMH) Lugalo jijini Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa binti wa marehemu, Sophia, baba yake alianguka bafuni nyumbani kwake Mbezi Beach ambapo alikimbizwa katika Hospitali ya Lugalo ambapo ndipo umauti ulipomfika wakati madaktari wakimpatia matibabu.

Kanali Mwanakatwe alichaguliwa kuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Mpira wa Miguu Tanzania (FAT) katika uchaguzi uliofanyika mwaka 1993 mjini Kibaha mkoani Pwani.

Baada ya kuondoka FAT, aligombea nafasi ya Katibu Mkuu wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) na kufanikiwa kushinda katika uchaguzi uliofanyika mwaka 1997.

Msiba huo ni mkubwa katika fani ya mpira wa miguu nchini na Afrika kwa ujumla kwani, Kanali Mwanakatwen enzi za uhai wake alitoa mchango mkubwa akiwa kiongozi, na mkufunzi wa utawala wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF). Pia aliwahi kuwa Kamishna wa CAF.

TFF tunatoa pole kwa familia ya marehemu Kanali Mwanakatwe, DRFA, na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na kuwataka kuwa na subira na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu cha msiba huo mzito.
Taratibu za mazishi zinaendelea kufanywa na familia yake nyumbani kwake Mbezi Beach karibu na hoteli ya Giraffe wakati ndugu wakisubiriwa kutoka mikoani. TFF tunasubiri taratibu hizo ili tujipange jinsi ya kushiriki katika msiba huo.
Sisi sote ni waja wake Mola. Hakika kwake tutarejea.

No comments:

Post a Comment