KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Saturday, June 28, 2014

SMALL BOYS, MSHIKAMANO, PACHOTO ZAPIGWA FAINI





Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) zimezipiga faini ya kati ya sh. 300,000 na sh. 500,000 klabu za Mshikamano FC, Pachoto Shooting Stars, Town Small Boys na Kiluvya United kutokana na makosa mbalimbali ikiwemo viongozi, wachezaji na washabiki kufanya vurugu kwenye mechi za Ligi ya Mabingwa wa Mikoa (RCL) iliyomalizika hivi karibuni.

Uamuzi huo umefanywa na Kamati ya Mashindano ya TFF iliyokutana juzi (Juni 23 mwaka huu) jijini Dar es Salaam kupitia masuala mbalimbali ikiwemo taarifa za mechi, na malalamiko kutoka kwa baadhi ya timu zilizoshiriki RCL iliyochezwa katika vituo vya Mbeya, Morogoro na Shinyanga.

Town Small Boys ya Ruvuma imepigwa faini ya sh. 500,000 kwa mujibu wa kanuni ya 37(13) ya Kanuni ya RCL kutokana na udanganyifu kwa kumtumia mchezaji Agaton Mapunda ambaye hakustahili ingawa usajili wake ulithibitishwa na TFF, kwa kutokuwepo pingamizi kutoka klabu yoyote katika kipindi cha pingamizi.

Licha ya usajili wake kuthibitishwa na TFF, Kamati ilibaini mchezaji huyo hakutoka ndani ya Mkoa wa Ruvuma kama kanuni za RCL zinavyoelekeza. Hata hivyo, matokeo ya mechi hiyo dhidi ya Njombe Mji iliyomalizika kwa bao 1-1 yanabaki kama yalivyo kwa mujibu wa kanuni ya Kanuni ya 52 (3 na 4) na 31(11) ya RCL kwa kuwa mchezaji Mapunda alithibitishwa na TFF (qualified player).

Vilevile mchezaji huyo amepigwa faini ya sh. 200,000 kwa mujibu wa kanuni za 48(4) na 31(11) za RCL. Nayo malalamiko ya Njombe Mji dhidi ya mchezaji David Noel Makakala kuwa ndiye aliyecheza mechi hiyo badala ya Carlos Mapunda yametupwa kwa kukosa vielelezo na ushahidi wa kuthibitisha hilo.

Kiluvya United FC ya Pwani imepigwa faini ya sh. 300,000 kwa mujibu wa kanuni ya 37(1) kutokana na vurugu za washabiki wake kwenye mechi namba 46 dhidi ya Abajalo iliyochezwa mjini Morogoro.

Pachoto Shooting Stars ya Mtwara na Mshikamano FC ya Dar es Salaam zimepigwa faini ya sh. 500,000 kila moja kwa kufanya vurugu kubwa kwenye mechi yao namba 100 iliyovunjika mjini Morogoro. Pia Mshikamano FC wamepewa pointi tatu na mabao matatu kwa mujibu wa kanuni ya 23(1na5) na 22(d).

Wachezaji na viongozi wa Pachoto Shooting na wachezaji wa Mshikamano FC waliofanya vurugu na kupigana, suala lao linapelekwa kwenye Kamati ya Nidhamu ya TFF kwa uamuzi na hatua za kinidhamu.

Nayo Tanzanite ya Manyara imefungiwa kucheza mashindano yote rasmi kwa msimu mmoja, na kuteremishwa daraja hadi ligi ya wilaya mara itakapomaliza kifungo chake kwa mujibu wa kanuni ya 21(3)(a), 37(14) na 22(a). Tanzanite iliadhibiwa kwa mujibu wa kanuni ya 23(1,5 na 6) baada ya kumpiga mwamuzi kwenye mechi dhidi ya AFC na baadaye kugomea mchezo. Ilishindwa kulipa faini na kujitoa mashindanoni kwa kuondoka kituoni.

Wachezaji wanaotuhumiwa kumpiga mwamuzi mpaka kumjeruhi suala lao litapelekwa kwenye Kamati ya Nidhamu ya TFF.

Kamati imetupa malalamiko ya African Sports ya Tanga dhidi ya Abajalo ya Dar es Salaam, Ujenzi FC ya Rukwa dhidi ya AFC, Panone FC ya Kilimanjaro dhidi ya Volcano FC ya Morogoro, na Mvuvumwa FC ya Kigoma dhidi ya Mbao FC ya Mwanza kwa kukosa vielelezo na ushahidi.

Pia malalamiko ya Mvuvumwa FC dhidi ya Geita Veterans ya Geita juu ya kuwachezesha Ibrahim Alphonce, Zamoyoni Magoma na John Mtobesya kwa kuwa hawakusajiliwa yametupwa kwa vile wachezaji hao ni halali, isipokuwa orodha ya wachezaji wa Geita Veterans FC iliyotolewa kwa ajili ya pingamizi ilikuwa na upungufu kiuchapaji ambapo wachezaji sita hawakuorodheshwa.

Nao makamishna Edward Hiza na Jimmy Lengwe waliokuwa kituo cha Morogoro wamepewa onyo kutokana na ripoti zao kuwa na upungufu.

Vilevile Kamati ya Mashindano imezitangaza rasmi timu za African Sports, Geita Veterans na Panone FC kupanda kucheza Ligi Daraja la Kwanza (FDL) msimu wa 2014/2015.

No comments:

Post a Comment