KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Sunday, June 1, 2014

MANJI, SANGA WAONGEZEWA MWAKA MMOJA YANGA, MAXIMO ANUKIA KUWA KOCHA



Mkutano Mkuu wa marekebisho ya baadhi ya vipengele kwenye Katiba ya Yanga umefanyika na kumalizika salama na furaha kwenye Ukumbi wa Bwalo la Polisi -Oysterbay huku wanachama wakipitisha kipengele cha kuundwa kwa kamati ya maadili.

Mwenyekiti wa klabu ya Yanga SC Yusuf Manji amewaongoza wanachama hai wapatao 1,560 kupitisha kipengele hicho kipya kwa ajili ya maslahi na faida ya Wana Yanga kwani bila kufanya hivyo timu isingeweza kuruhusiwa kushiriki Ligi Kuu msimu ujao.

Aidha katika mkutano huo Manji amewatoa hofu wanachama kwa kuwaambia kuwa usajili unaendelea kufanyika na nafasi zilizobakia ni nne tu hivyo pindi utakapokamilika basi wataweka wazi kila kitu.

Kuhusu nafasi ya Kocha Mkuu Manji amesema Kamati ya Mashindano imemkabidhi mapendekezo yao na kwa sasa yupo kwenye mazungumzo na Marcio Maximo aliyewahi kuwa kocha mkuu wa timu ya Taifa Tanzania kuja kukinoa kikosi cha Jangwani.

Mwenyekiti wa Baraza la Wadhamini Mama Fatma Karume aliongoza kikao cha waachama kilichomuomba Bw Manji kuendelea na uongozi ambapo mwenyeikti alitoka nje na kamati yake ya utendaji na pindi waliporejea walikubali ombi hilo na kusema watafuata taratibu za kikatiba.

Mwisho kupitia mkutano mkuu wa leo wa wanachama umeazimia kuwaongezea muda wa mwaka mmoja Mwenyekiti Yusuf Manji pamoja na Makamu wake Clement Sanga ili waweze kukamilisha masuala ya katiba na kuweza kuandaa mkutano wa uchaguzi baada ya katiba kupitishwa na TFF

No comments:

Post a Comment