KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Saturday, June 28, 2014

RAY C ASIMULIA KILICHOMSIBU, AWATOA CHOZI WANANCHI




NA SOLOMON MWANSELE.

REHEMA Chalamila maarufu zaidi kama Ray C, siyo jina geni kwa wapenzi wa muziki wa Kizazi kipya nchini, maarufu zaidi Bongo fleva.Ni mmoja wa wasanii walioufikisha muziki huu hapa ulipo leo.

Ray C ni alianza kupata umaarufu, na mafanikio lukuki akiwa na umri mdogo wa miaka 17, na kuweza kutingisha vilivyo, akianzia kazi ya utangazaji katika kituo cha radio ya East Afrika, mnamo mwaka 1999, na mwaka mmoja baadaye alijiunga na radio Clouds.

Mwaka huo huo wa 2000, alianza kujihusisha na muziki wa kizazi kipya na kuweza kuliteka vilivyo soko huku mashabiki wake wakimuongezea jina lingine la kwa kuanza kumuita ‘Kiuno bila mfupa’ kutokana na unenguaji wake mahiri jukwaani.

Ray C aliweza kuutangaza vyema muziki wa Bongo Fleva, katika nchi za Marekani, Dubai ,Sweden, China, Uganda, Kenya, Afrika ya Kusini, Uingereza, Oman, Australia, Norway, Msumbiji, India na Nigeria.

Kutokana na mafanikio yake hayo katika fani hizo, za utangazaji na muziki wa Bongo Fleva, Ray C aliweza aliweza kujenga nyumba nzuri na kubwa, akiwa na umri huo mdogo na baadaye kununua magari, na vile vile kufanikiwa kufungua maduka makubwa jijini Dar es Salaam.

Lakini ghafla ujana uliompaisha na kumpeleka juu, ukamgeuza kichwa chini miguu juu, hali iliyopelekea nuru na nyota yake iliyokuwa inawaka kufifia, ambapo Ray C akawa haonekani tena, kiasi cha kufikia hatua baadhi ya watu kumzushia kuwa amefariki dunia.

Hivi karibuni Ray C alitoa ushuhuda mzito, na uliovuta hisia za mamia ya watu waliohudhuria maadhimisho ya Siku ya Kupiga vita matumizi ya dawa za kulevya Duniani, ambayo kitaifa yalifanyika katika viwanja vya Ruanda Nzovwe jijini Mbeya.

Mgeni rasmi katika maadhimisho hayo alikuwa ni Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk.Mohammed Gharib Bilal.Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uratibu, Sera na Bunge), William Lukuvi, pia alihudhuria.

Ray C anasema mara baada ya kujiingiza, katika matumizi ya dawa za kulevya uwezo wake wa kufanya muziki ulitoweka, na akajikuta anaanza taratibu katabia ka kuuza vitu vyake kimoja baada ya kingine.

“Nilianza kwa kuuza vitu vidogo vidogo, baadaye nikauza gari zangu, nyumba na maduka yote nikayafilisi.Nikaanza kuwa mtu wa kujificha, huku nikiendelea kudhoofika, ilifika wakati nililazimika kutembea nikiwa nimevaa ‘kininja’.

Mungu wangu!Nilikuwa nimenasa kwenye mdomo wa Mamba, dawa za kulevya zilikuwa zinanimaliza, na nilipokuja kushtuka nilikuwa nimenasa.Maisha yangu yakawa si starehe tena bali ni mateso na aibu” anasema Ray C.

Anaongeza, alipokuwa katika uteja alikwenda mbali zaidi ya kuuza vitu vyake vya thamani, na roho inamuuma sana anapokumbuka siku, alipomshikia kisu mama yake mzazi ili kumlazimisha ampe fedha ili akanunue dawa za kulevya.

Akiongea huku akishikwa na uchungu mkubwa, na machozi kumtoka akiwa jukwaani akionekana kujutia matendo yake, Ray C anasema roho inamuuma sana anapokumbuka siku alimnyonga mkono mama yake na kumpokonya simu.

“Ninapokumbuka haya roho huwa inaniuma, kuliko hata kupoteza vitu vyangu vya thamani.Namshukuru mama alitambua kuwa sikuwa mimi, hivyo hakunikatia tamaa aliendelea kunihangaikia na kufanya maombi sana” anasema Ray C huku akijifuta machozi.

Anaongeza kwa kumuomba msamaha mama yake mzazi, kwa mateso aliyompa na kumshukuru mama yake huku akimuombea kwa Mungu, azidi kumbariki na kuwaomba wazazi wote nchini kuiga mfano huo kwa kuwasaidia vijana wao.

Ray C anasema anakumbuka alivyofukuzwa kama mbwa, kwa muuza dawa za kulevya kwa sababu alikuwa hana fedha, na anaumia sana anapokumbuka siku alizokuwa analala kwenye boksi, kwani hakuweza kurudi nyumbani akiwa ana ‘arosto’, yaani bila kuvuta unga.

Anasema kwa sababu ya kukosa dawa za kulevya, kutokana na kutokuwa na fedha alilazimika kulala kwenye boksi, akisubiria labda itatokea ‘kampani’yaani rafiki, ili imnunulie dawa apone anasema yalikuwa ni mateso ya ajabu, ambayo hayana mfano.

Msanii huyu wa muziki wa Bongo Fleva, anaongeza kuwa mateso na dharau alizozipata hazikuwa za peke yake, kwani familia yake pia ilikuwa katika dimbwi la mateso, familia yote iliumwa ambapo mama yake alilia sana na kuhangaika.

Anamnukuu mama yake mzazi:”Mwanangu nini hiki…umerogwa na nani mwanangu?Eeeh Mungu nisaidie”.Kilikuwa ndio kilio cha mama kila wakati.

Anaongeza mtu aliyekuwa anategemewa na familia, alikuwa anatoweka taratibu na sasa akawa mzigo mkubwa kwa familia.Alikuwa anaumia sana na kutaka kuacha matumizi ya dawa za kulevya, lakini alikuwa amenasa kwenye meno makali ya Mamba, na hakuwa na ujanja.

“Mama alihangaika sana na ndugu zangu pia walikosa raha.Mama alikuwa ni mtu wa kwenda kwenye maombi kila wakati.Alikuwa na fedha lakini naye uchumi wake uliporomoka, na kutoweka kwa sababu yangu” anasema Ray C huku akijifuta machozi.

Anasema hatimaye Mungu, alimuinua Rais Jakaya Kikwete, ambaye alijitolea kumsaidia kwa kumpa matibabu, na kwa sababu hata yeye mwenyewe, alikuwa na dhamira ya dhati ya kuacha dawa za kulevya, kwake ilikuwa ni jambo rahisi kuachana na dawa hizo.

Anaongeza kuwa anatumia fursa hiyo, kwa mara nyingine kumshukuru mwenyezi Mungu kwa kumpa fursa nyingine ya kuwa Ray C, lakini siyo yule wa zamani bali kuwa mwenye akili na mitazamo mipya kabisa ya maisha, na ambaye watanzania na Taifa litanufaika naye.

Anasema kwa namna ya kipekee, na kwa mara nyingine anamshukuru Rais Kikwete, kwa kumsaidia na kumuomba Mungu azidi kumbariki.Anamuahidi kwa kumsaidia yeye wengi watapona, na anajua hiyo ndio ilikuwa dhamira yake (Rais Kikwete), ili awe mfano ili wengi waokoke na janga hilo la matumizi ya dawa za kulevya.
“Naamini Mungu alikuwa na mpango na mimi, hivyo ni lazima nimtumikie kwa njia hii” anasema Ray C.

Anabainisha kilichomuingiza kwenye matumizi ya dawa za kulevya, ilikuwa ni marafiki wabaya na mahusiano mabaya ya kimapenzi, ambapo kupitia mtu aliyempenda na kumuamini sana, katika mazingira ambayo hayakuwa wazi, alijikuta amenasa kwenye matumizi ya dawa hizo.

Anaongeza, alipokuwa katika tatizo hilo alijifunza mambo matatu, ambayo anayataja kuwa ni sio watu wote wanaotumia dawa za kulevya, wameingia huko wakijielewa.

Pili, kuna unyanyapaa mkubwa wanaofanyiwa waathirika wa dawa za kulevya, kutoka kwa jamii na vyombo vya dola, na kwa asilimia kubwa unyanyapaa huo unatokana na uelewa mdogo, juu ya hali halisi ya tatizo.

Tatu, alijifunza kuwa watu kuendelea kutumia dawa hizo, na nyingi hatarishi wanazokuwa nazo hakutokani na wao kupenda, bali mateso makali ambayo mtu anayapata anapokosa dawa hizo, na kuwa anayajua mateso mazito waliyonayo, tofauti na jamii inavyofikiri.

Ray C anasema kutokana na Mungu kumsaidia, kwa kumtumia Rais Kikwete, na jinsi yeye mwenyewe anavyoguswa na tatizo hilo, shukrani yake ni kwa Rais kufanya juhudi za kuielimisha jamii juu ya athari za dawa za kulevya, na pia kuwasaidia waliokwisha kuingia watoke huko na ambao hawajaingia wasithubutu.

“Kwa kufanikisha hilo, nimeamua kuanzisha asasi inayoitwa Ray C Foundation, asasi hii ina lengo la kufanya uelimishaji mkubwa kwa jamii, kupitia makundi yake mbalimbali pamoja na kusaidia walioathirika, warudi kuwa watu wa kawaida” anasema Ray C.

Kupitia asasi yake hiyo, tayari wameanza kampeni ya shule kwa shule wakitembelea baadhi ya shule za sekondari jijini Dar es Salaam, ambapo wana lengo la kuzitembelea shule zote za sekondari katika mikoa yote ya Tanzania, hasa ile iliyoathirika zaidi na dawa za kulevya.

Anasema, vile vile wameanza kutembelea vijana watumiaji wa dawa za kulevya kwenye maskini zao, na kuwaelimisha waache na katika kipindi cha miezi miwili tu ya kampeni hiyo, vijana 25 wameamua kuacha na wanapata matibabu ya Methadone.

Ray C anaongeza kwa miezi kumi sasa, amekuwa akizungumza kupitia vyombo mbalimbali vya habari, juu ya uwezekano wa kuacha dawa za kulevya kwa watumiaji, na wasio watumiaji kujiweka mbali na dawa hizo.

Anabainisha hilo limechangia ongezeko la watu, wanaotaka kuacha na kupata matibabu na kuwa utekelezaji wa malengo hayo kupitia Ray C Foundation, umepokelewa kwa shauku kubwa na watanzania, lakini anakumbana na changamoto ya uwezeshaji.

Anamuomba Makamu wa Rais Dk.Bilal, serikali, watu binafsi, na taasisi mbalimbali kuiunga mkono Ray C Foundation, ili iweze kutekeleza mikakati na malengo iliyonayo, kwani Taifa linaangamia na hali ni mbaya sana.

“Kwa namna ya pekee, pia natumia nafasi hii kuiomba serikali, kufanya uwekezaji mkubwa katika huduma ya matibabu kwa waathirika wa dawa za kulevya, kwa kufungua huduma hiyo katika hospitali za wilaya na za Rufani nchini” anasema Ray C.

Anaongeza hilo ni kutokana na idadi kubwa ya watu wanaopata ufahamu, na kuamua kuacha matumizi ya dawa za kulevya, inakuwa kwa kasi kubwa kutokana na kampeni wanazoendelea kuzifanya

No comments:

Post a Comment