KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Sunday, July 10, 2016

TUZO ZA LIGI KUU KUTOLEWA JULAI 17



Hafla ya kukabidhi tuzo mbalimbali za washindi wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kwa msimu wa 2015/2016 itafanyika Julai 17 mwaka huu.

Jumla ya tuzo 13 za Ligi hiyo inayodhaminiwa na kampuni ya mawasiliano ya Vodacom Tanzania zitatolewa katika hafla hiyo itakayofanyika jijini Dar es Salaam, na kuratibiwa na Kamati ya Tuzo ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).

Kamati hiyo inaundwa na waandishi wa habari za michezo, makocha, viongozi  (administrators) na wawakilishi kutoka kwa wadhamini (Vodacom na Azam Tv).

Tuzo hizo ni mabingwa, makamu bingwa, mshindi wa tatu, mshindi wa nne, timu yenye nidhamu, mfungaji bora, mchezaji bora wa Ligi, kipa bora, kocha bora, mchezaji bora chipukizi, mchezaji bora wa kigeni, goli bora la msimu na mwamuzi bora.

Waliopendekezwa (nominees) kuwania tuzo ya mchezaji bora wa Ligi ni Shiza Kichuya (Mtibwa Sugar), Juma Abdul (Yanga) na Mohamed Hussein (Simba) wakati kwa upande wa kipa bora ni Aishi Manula (Azam), Beno Kakolanya (Tanzania Prisons) na Deogratius Munishi (Yanga).

Kocha bora wapo Hans Van Pluijm (Yanga), Mecky Maxime (Mtibwa Sugar) na Salum Mayanga (Tanzania Prisons). Waliopendekezwa kuwania tuzo ya mchezaji bora chipukizi ni Farid Mussa (Azam), Mohamed Hussein (Simba), Mzamiru Yasin (Mtibwa Sugar) na Shiza Kichuya (Mtibwa Sugar).

Waliongia kwenye orodha ya tuzo ya mchezaji bora wa kigeni ni Donald Ngoma (Yanga), Thabani Kamusoko (Yanga) na Vincent Agban (Simba). Waamuzi bora katika kinyang'anyiro hicho ni Anthony Kayombo, Ngole Mwangole na Rajab Mrope.

Meneja Uhusiano wa Vodacom Tanzania, Matina Nkurlu amewapongeza wateule wote waliopendekezwa kuwania tuzo hizo. "Kama wadhamini tuna matumaini makubwa kuwa  msisimko wa ligi hii utazidi kuongezeka katika msimu ujao na kuzidi kuwapatia mashabiki wa soka wanaoifuatilia hapa nchini na nje ya nchi."

Alisema Vodacom itaendelea kudhamini ligi hiyo kubwa ya soka nchini  ili kutekeleza moja ya malengo yao ya kuibua na kuendeleza vipaji vya wachezaji nchini. Pia kuwawezesha wachezaji kujipatia ajira na kuboresha maisha yao kupitia sekta ya michezo bila kusahau kuwapatia burudani wateja wake na Watanzania wote kwa ujumla.

No comments:

Post a Comment