KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, April 30, 2015

BURIANI MUTOMBO LUFUNGULA AUDAX, MZIZI WA MWISHO WA MAQUIZ ULIOKUWA UMEBAKIA


MUTOMBO Lufungula  'Audax (kushoto), akiwa na Kasongo Mpinda 'Clayton' katika moja ya maonyesho ya Bana Maquiz.

NA PETER ORWA

WIKI chache kabla ya kifo chake, mwaka 2010, mwimbaji mahiri wa muziki wa dansi, Kasaloo Kyanga, alieleza changamoto aliyokumbana nayo wakati anajiunga na bendi ya Maquiz Original mwanzoni mwa miaka ya 1980, kwamba:“Nilikutana na ‘Predezshee saba’… Nikasema hapa ‘taweza’ kweli? “

Ujumbe wake ni kwamba, wakati huo anajiunga akiwa na umri wa miaka 24, alikutana na magwiji saba waimbaji unaomjumuisha Mutombo Lufungula Audax, akishirikiana na wengine kama vile Mbuya Makonga ‘Adios, Kasongo Mpinda ‘Clyton’ na Kikumbi Mwanza Mpango au King Kiki.

Leo hii ‘Predeshee’ huyo, Mutombo Lufungula Audax, hayupo tena kwa wiki moja sasa na alizikwa  katika nyumba ya milele wiki moja iliyopita, tukio lililotetemesha anga ya muziki nchini… Ni pigo kubwa ambalo limeacha masikitiko!

Marehemu huyo ambaye ndiye mwanahisa na muasisi aliyebaki katika bendi ya Maquiz Du Zaire, kati ya wenzake tisa waliounda zaidi ya miaka 50 iliyopita, nyumbani kwao, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC), wakati huo ikiitwa taifa hilo Congo na baadaye Zaire.

Muasisi mwingine aliye hai, lakini aliondoa hisa zake mapema kabla ya bendi kufilisika ni mpiga solo mahiri, Nguza Vikings, ambaye baadaye alijiunga na Sambulumaa, kisha akaanzisha bendi yake ya Achigo, kabla ya kukutwa na matatizo yaliyompeleka gerezani kwa maisha yote.

Baadhi ya wanahisa wengine ni Ilunga  Lubaba, Mwema Mujanga,’ Chibangu Katai, Robert Otrish na Chinyama Chiyaza, aliyekuwa kiongozi wa bendi.

Audax alizikwa Jumapili mchana iliyopita katika makaburi ya Kinondoni, baada ya kutanguliwa na shughuli ya heshima za mwisho zilizofanyika katika Hospitali ya Mwananyamala, Dar es Salaam.

Ni kifo kinachotia simanzi katika tasnia ya muziki wa dansi, kwani gwiji mwingine ninayethubutu kumtaja aliongeza ushindani katika mchuano kati ya Maquiz na wapinzani wao, Orchestra Safari Sound, Kabeya Badu (65), naye alifariki mwaka jana na kuzikwa katika makaburi hayo hayo ya Kinondoni.

Katika historia yake, marehemu Kabeya aliwahi kupitia Maquiz kabla ya kujiunga na OSS na kisha wakati fulani bendi ya Tancut Almasi Orchestra. 

Mwimbaji mkongwe, Tshimanga Kalala Assosa, ana maelezo ya ziada kuhusiana na kifo cha Audax, ambacho kilitokana na maradhi ya kupooza yaliyomsumbua sana kwa miaka mitano iliyopita.

“Ameteseka sana,”anatamka Assosa, huku akifafanua kwamba kifo hicho kilitokea nyumbani kwa marehemu Kimara King’ong’o, alikokuwa akiugua na hafichi kumtambulisha kuwa ni mtu wake wa karibu.

Watu hao wamefahamiana kwa takriban maisha yao yote, tangu zama za miaka ya 1950, wakiwa kijijini kwao, Kamina Nsobongo, katika jimbo la Katanga, wakati huo ikiitwa Jamhuri ya Congo na baadae ikawa Zaire mwaka 1965.

“Hata mara ya mwisho nilipoenda nyumbani Congo (DRC), mama yake alikuja nyumbani,”anasimulia Assosa na kufafanua kwamba marehemu Audax ana dada anayeishi nchini, anayeitwa Kaiba.        

Anafafanua uhusiano wake na Audax kuwa, licha ya kutoka kijiji kimoja, walisoma shule moja na anamfahamu kwamba katika maisha yake yote, Audax alikuwa mpenzi na mchezaji mahiri wa mpira wa miguu, lakini akazama zaidi katika muziki kulikomfanya aache soka na masomo.

“Mama zetu pia walikuwa wanafahamiana sana,” anasema Assosa na kuongeza “Mara ya mwisho nilipoenda Congo (DRC), mama yake alikuja nyumbani.”

Assosa anajitambulisha kuwa na umri mdogo kwa marehemu Audax kwa wastani wa miaka miwili na alikuwa anasoma madarasa ya chini yake, lakini binafsi hakubobea katika soka. Mapenzi yake binafsi yaliozama kwenye masomo na kuimba kanisani.

Kwa mujibu wa John Kitime, mwanamuziki mwingine mkongwe aliyewahi kupigia gita la rhythm na besi kwa bendi kama Vijana na Tancut, marehemu Audax alizaliwa tarehe 9 ya mwezi Oktoba ya mwaka 1945..

Assosa anasimulia kwa hatua kisa cha Audax na baadhi ya wenzake ambao ndio wakawa wanamuziki  waasisi wa Maquiz, kwamba kijijini kwao Kamina kulizuka makundi mengi ya vijana wanaobobea katika muziki na kuunda bendi ndogo ndogo kijijini.

Moja ya kumbukumbu alio nao Assosa ni kwamba, wakati wa harakati za kuelekea uhuru wa Congo, yeye na marehemu Audax walikuwa katika kundi la vijana waliioonekana wanaimba vizuri na waliteuliwa kwenda nchini Ubelgiji kumuimbia Mfalme wa taifa hilo lilokuwa likiwatala.

Wakati huo Audax alishakuwa ametawaliwa na muziki na kuacha masomo tangu kipindi kirefu.

“Tuliporudi na sisi wengine ndio ukawa mwisho wa shule na hawa (vijana wenzake wa kijijini akiwemo Audax) ndio walitufanya shule ikawa basi… ndio watu waliotufanya tuvunje kalamu,” anasema Assosa.

Anafafanua kwamba, hali ya kuzingirwa na vijana wanamuziki kijijini, ndio kulimteka naye azame katika muziki na kuacha shule akiwa miongoni mwa vijana ambao awali walipenda mno masomo.   

Mwanamuziki huyo anawataja wakongwe wa muziki nchini anaotoka pamoja kijijini Kamina Nsabongo, ni pamoja na Mbombo wa Mbomboka na marehemu Issa Nundu, ambao katika nafasi tofauti waliwahi kupitia bendi kama Makassy, Super Matimila, OSS na Maquiz.

Assosa anawataja wengine waliokuwa Maquiz ni, Nguza Vikings, Mbuya Makonga Adios na Chinyama Chiyaza na anaongeza kuwa Adios alikuwa mwanakwaya mwenzake katika kanisa analolitaja la Mtakatifu Bavo, akiwa mpiga kinanada na yeye mwimbaji wa sauti ya pili, aliyodumu nayo hadi sasa katika dansi.

Kundi hilo lililounda Maquiz likiwa na bendi yao kijijini lilianza na mkakati wa kuvuka mpaka kwenda Uganda mwaka 1963, jambo ambalo Assosa hakukubaliana nalo na akaamua kurudi nyumbani kutoka mpakani mwa nchi na baadaye alielekea Kinshasa alikovuma kimuziki baada ya muda mfupi.

Lile kundi lilounda Maquiz, wakati huo likiwa na jina la Super Gaby, baada ya kukaa Uganda, lilihamia Tanzania mwaka 1972, ambapo Nguza na Audax walikuwa wamebaki huko na muda mfupi walikuja kujiunga na wezao nchini.

Ikumbukwe, mwaka 1971 taifa la Uganda utawala wake ulipinduliwa na kuchukuliwa na Rais Iddi Amin Dada.

Bendi hiyo ilipewa jina la Maquiz Du Zaire mwaka 1973, huku wakijozolea umaarufu, wakipiga muziki  katika ukumbi wa Mikumi Tours iliyopo eneo la TAZARA,  lililomilikiwa na aliyekuwa mfanyabiashara maarufu wa Dar es Salaam, Mzee Batenga

Hata hivyo hawakudumu sana, kutokana na eneo la ukumbi huo kuchukuliwa kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya stesheni ya TAZARA na walipata mkataba mwingine wa kupiga katika ukumbi wa Tours and Hunters, eneo la Ubungo. Ulikuwa unamilikiwa na Hugo Kisima, ambaye baadaye  alimiliki bendi ya OSS na ukumbi wa Safari Resort.

Mwanamuziki Kitime, anamsifu Audax kwamba alikuwa mtunzi mahiri na mwalimu wa muziki katika bendi ya Maquiz, iliyopitia mitindo mbalimbali kama vile Kamanyola Bila jasho, ulioasisiwa na Kingi Kiki mwaka 1973, Sendema na Zembwela.

Naye Assosa, anamwagia sifa kwamba, mbali na kuwa mtunzi, alikuwa mahiri katika kuchangia mawazo bora kwenye tungo za ndani ya bendi na hata muundo wa sauti, akitoa mfano kuna wakati alitoka na kujiunga na bedi ya Legho, lakini Audax aliwashawishi wakurugenzi wenziwe hadi wakamrudisha.

“Alikuwa mtu wangu wa karibu na alinipenda sana. Waliniita na hata nikasikia ile wanasema ‘nyongo ilitumbukia’ nikarudi Maquiz,” anasema Assosa. 

Kwa mujibu wa Kitime, marehemu aliuhusudu sana utunzi wake wa kibao cha Mpenzi Luta, ingawaje kuna mingine mingi aliozitunga  ikiwemo kibao ‘Nani Atanitetea.’

Wakati fulani, Audax alitunga kibao Kisebengo, kilichobeba ujumbe wenye kijembe kwa mwezake kutoka kijijini Kamina – Nguza Vikings, aliyeamua kuichukua hisa zake za Maquiz, katika dakika za mwisho baada ya safari ndefu ya kuunda bendi na maisha ya pamoja kimuziki.

Ikumbukwe, kuna wakati bendi ya Maquiz Du Zaire ilifikia kilele cha mafanikio, ambapo wakurugenzi wake wakiwemo, kina Audax mbali na kupiga muziki, waliunda kampuni iliyoitwa OMACO.

Assosa anasema, wakati wanaendeleza mafanikio ya muziki kupitia Maquiz, upenzi wa Audax katika soka hakuwahi kukoma, na ncjini alikuwa shabiki mkubwa wa klabu ya Yanga na hata ulipotokea mgawanyiko ukiozaa timu ya Pan African, alijiunga nayo na kuwa na kadi ya uanachama.

Hata baada ya kusambaratika, Audax kwa kushirikiana na wenzake kama vile Mwema Mujanga na Adios waliasisi bendi ya Bana Maquiz, iliyokuwa na makao makuu katika baa ya Savoy, eneo la Tabata na baadaye walimuongeza mwenzao, Assosa.

Hata hivyo, Assosa ana simulizi ya simanzi kwamba kwa bahati mbaya bendi hiyo ilifilisika vyombo, huku Adios akiwa ameshafariki. Katika mihangaiko Audax na Asosa walifanikiwa kupata msaada wa vyombo kwa mkopo wa shilingi milioni nane, ambao mfanyabiashara mmoja aliyetoa sharti la hisani wamlipe kidogo kidogo.

Assosa anasema, tukio ambalo hatolisahau na ni la kumsikitisha,   lililotokea miaka mitano iliyopita,  kwamba siku ambayo aliahidiwa kukabidhiwa vyombo na yeye akiwa katika mchakato wa kuvichukua, ni kwamba muda mfupi baadaye alipigiwa simu ya kufahamishwa Audax amepatwa na kiharusi, yuko hospitalini Muhimbili.

Anasema, tangu wakati huo amekuwa mgonjwa na kamwe hakuwahi hata kuviona vyombo ambavyo alishiriki katika mchakato wote wa kuvipata, jambo ambalo Assosa hafichi hisia zake akisema ‘inamuuma sana.’

Ni historia itayakayobaki kuwa ya kudumu, marehemu Audax ni nembo ya kudumu ya bendi ya Maquiz, akiwa mwanahisa muasisi wa mwisho aliyekuwa amebaki. 

MUNGU AMBARIKI APUMZIKE KWA AMANI.

Tuesday, April 28, 2015

SIMBA, AZAM ZATOZWA FAINI, WAAMUZI WAFUNGIWA
Ruvu Shooting imepigwa faini ya sh. 300,000 (laki tatu) kwa kuzingatia Kanuni ya 14(9) ya Ligi Kuu kwa kutoingia kwenye vyumba vya kubadilishia nguo (changing room) katika mechi namba 149 dhidi ya Kagera Sugar iliyochezwa Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga

Pia Ruvu Shooting imepigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) kwa kutoingia vyumbani wakati wa mapumziko kwenye mechi hiyo. Adhabu hiyo imetolewa kwa kuzingatia Kanuni ya 14(13) ya Ligi Kuu.

Stand United imepigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) baada ya washabiki wake kuwatupia chupa za maji wachezaji wa akiba wa timu ya Polisi Morogoro katika mechi iliyochezwa Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga. Adhabu hiyo imetolewa kwa mujibu wa Kanuni ya 42(1) ya Ligi Kuu.

Naye Meneja wa Polisi Morogoro, Manfred Luambano alitolewa kwenye benchi la Polisi Morogoro kwa kosa la kutoa lugha za kashfa kwa mwamuzi msaidizi namba moja Martin Mwalyanje. Suala lake linapelekwa kwenye Kamati ya Nidhamu ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kwa ajili ya hatua za kinidhamu.

Kipa wa Ndanda SC, Wilbert Mweta amefungiwa mechi tatu na kupigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) kwa kumkanyanga na kutaka kumpiga mwamuzi Eric Onoka kwenye mechi namba 155 dhidi ya Polisi Morogoro iliyochezwa Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro. Adhabu hiyo imetolewa kwa mujibu wa Kanuni ya 37(5) ya Ligi Kuu. Kabla ya kufanya kitendo hicho alikuwa ameonyeshwa kadi nyekundu.

Meneja wa Kagera Sugar, Mohamed Hussein anapelekwa kwenye Kamati ya Nidhamu ya TFF kwa kutoa lugha ya matusi kwa waamuzi na kutaka kumpiga mwamuzi msaidizi namba 2, Said Mnonga kwenye mechi namba 158 dhidi ya Azam FC iliyochezwa Uwanja wa Azam Compex jijini Dar es Salaam.

Naye Kipa Andrew Ntala wa Kagera Sugar amefungiwa mechi tatu na kupigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) kwa kuingia kwenye vyumba vya waamuzi na kuwatolea lugha ya matusi mazito ya nguoni baada ya mechi hiyo. Adhabu hiyo imetolewa kwa mujibu wa Kanuni ya 37(5)(c) ya Ligi Kuu.

Mwamuzi wa mechi kati ya Azam FC na Kagera Sugar, Stephen Makuka na mwamuzi msaidizi namba mbili Said Mnonga wameondolewa kwenye orodha za waamuzi wa Ligi Kuu na kufungiwa miezi 12 kwa kushindwa kumudu mchezo kwa uzembe. Adhabu hiyo imetolewa kwa kuzingatia Kanuni ya 38(1) ya Ligi Kuu.

Pia Kamishna wa mechi hiyo Bevin Kapufi amefungiwa mwaka mmoja kwa kutoa taarifa isiyo sahihi. Adhabu hiyo imetolewa kwa uzingativu wa Kanuni ya 39(1) ya Ligi Kuu.

Naye Kamishna wa mechi namba 159 kati ya Mbeya City na Simba, Joseph Mapunda amepewa onyo kutokana na ripoti yake kuwa na upungufu. Simba imepigwa faini ya sh. 300,000 (laki tatu) kwa kuzingatia Kanuni ya 14(9) ya Ligi Kuu kwa kutoingia kwenye vyumba vya kubadilishia nguo (changing room) katika mechi namba 159 dhidi ya Mbeya City iliyochezwa Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya.

Pia Simba imepigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) kwa kutoingia vyumbani wakati wa mapumziko kwenye mechi hiyo. Adhabu hiyo imetolewa kwa kuzingatia Kanuni ya 14(13) ya Ligi Kuu.

Mgambo Shooting imepigwa faini ya sh. 100,000 (laki moja) kwa kuchelewa kufika kwenye kikao cha kitaalamu cha maandalizi ya mechi (technical meeting) dhidi ya Ruvu Shooting. Mechi hiyo namba 161 ilichezwa Uwanja wa Mabatini mkoani Pwani, na adhabu hiyo imetolewa kwa mujibu wa Kanuni ya 14(2)(a) ya Ligi Kuu.

MALINZI AMPONGEZA MANJI


Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini TFF, Jamal Malinzi ametuma salamu za pongezi kwa Mwenyekiti wa klabu ya Young Africans, Yusuf Manji kufuatia timu yake kutwaa Ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom msimu wa 2014/2015.

Katika salamu zake za pongezi, Malinzi amesema kutwaa Ubingwa wa VPL ni jambo muhimu na sasa wanapaswa kuanza maaandalizi kwa ajili ya michuano ya kimataifa barani Afrika mwakani.

Klabu ya Young Africans imetwaa Ubingwa wa Ligi Kuu nchini kwa mara ya 25 (ishirini na tano) jana, baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 4-1 dhidi ya timu ya Polisi Morogoro katika uwanja wa Taifa huku ikiwa na michezo miwili mikononi kabla ya ligi kumalizika.

Waziri wa Habari, Vijana Utamuduni na Michezo, Dr. Fennela Mkangara anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika sherehe za kukabidhi Kombe la Ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Mei 6, 2015 katika mchezo kati ya Azam FC dhidi ya Young Africans.

YANGA BINGWA 2015


NA AMINA ATHUMAN

TIMU ya Yanga imetwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa 2014/2015 huku ikiendeleza wimbi la kugawa dozi kubwa baada ya jana kufumua Polisi Morogoro mabao 4-1.

Mchezo huo ulifanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, ambapo Amisi Tambwe aliendelea kuchana nyavu za timu mpinzani kwa jana kupachika mabao matatu.

Kwa matokeo hayo, Yanga imetwaa ubingwa huo na kuweka rekodi ya kutwaa taji hilo kwa mara ya 25 tangu kuanza kwa Ligi Kuu Tanzania Bara mwaka 1965.

Yanga ilichukua ubingwa kwa mara ya kwanza mwaka  1968, 1969,1970, 1971, 1972, 1974, 1981, 1983, 1985, 1987, 1989, 1991, 1992, 1993, 1996, 1997, 1998, 2002, 2005, 2006, 2007/08, 2008/09, 2010/11, 2012/13 na 2014/15.

Tambwe ndiye aliyekuwa shujaa wa mchezo huo kwa kutupia 'hat trick' kabla ya Simon Msuva kukamilisha karamu ya mabao kwa kupachika bao la nne.

Magwiji hao walianza kuandika bao la kwanza katika dakika ya  42 kupitia kwa Tambwe baada ya kuunganisha pasi ya Msuva kabla ya kuachia shuti kali lililojaa moja kwa moja wavuni.

Bao la pili lilipatikana dakika ya dakika ya 53 baada ya Tambwe kumalizia mpira uliopigwa na  Msuva na kumshinda kipa wa Polisi Morogoro Abdul Idad.

Tambwe aliendelea kuichachafya ngome ya Polis Moro, ambapo dakika ya  59 alipachika bao la tatu kabla ya  Msuva kukamilishabao la nne dakika ya 66 baada ya kumpiga chenga  Idad na kuachia shuti kali lililojaa moja kwa moja wavuni.

Polisi Moro ilipata bao la kufutia machozi dakika ya 83  kupitia kwa Nicolaus Kabipe baada ya kuachia shuti kali lililomshinda kipa wa Yanga Deogratius Munisi 'Dida'

Kutokana na matokeo hayo, Yanga imefikisha pointi 55 ambazo haziwezi kufikiwa na timu yeyote huku ikipakiza michezo miwili kibindoni.

Ushindi huo umeiwezesha Yanga kutangaza ubingwa na kuipiku Azam FC iliyokuwa ikishikilia kombe hilo msimu uliopita na kuipa nafasi ya kushiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika.

Katika mchezo huo, Yanga ilianza mchezo kwa kasi na dakika ya pili ilipata nafasi ya kupachika bao kupitia kwa Tambwe, lakini shuti lake lilitoka nje ya lango.

Yanga ilipata nafasi nyingine dakika ya nane kupitia kwa Kpah Sherman wakati Polisi Moro ilipata nafasi dakika ya 14, 27,33 na 72 kupitia kwa Suleiman Kassim na Bahanuzi lakini mipira yote ilitoka nje.

Yanga: Deogratius Munish, Juma Adbul, Oscar Joshua, Mbuyu Twite, Kelvin Yondan, Said Juma, Simon Msuva/Hussein Javus, Haruna Niyonzima, Amis Tambwe/Jerson Tegete, Mrisho Ngasa na Kpah Sherman.

Polisi Morogoro: Abdul Idad, Ally Teru, Hassan Mganga, Meshack Abel, Laban Kambole, Anafu Suleman, Adimin Bantu, Said Mkangu, Said Bahanuzi/Nicolaus Kibape, Suleman Kassim na James Ambrose/Mussa Mohamed.

Monday, April 27, 2015

MALINZI AFUNGUA KOZI YA WAKUFUNZI


Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini TFF, Jamal Malinzi leo amefungua kozi ya walimu wakufunzi wa mpira wa miguu chini inayofanyika katika uwanja wa Karume jijini Dar es salaam.

Malinzi amesema kozi hiyo ni muhimu kwa mustakabali wa soka la Tanzania, walimu wakufunzi watasaidia kuwafundisha walimu wengine wa mpira, ili kuweza kufundisha mpira kwa watoto wadogo ambao ndio hazina ya baadae.

Malengo ya TFF ni kuhakikisha timu ya vijana ya U17 inafuzu kwa fainali za Mataifa Afrika 2017 nchini Madagscar, na baadae kuwa na kikosi bora wakati tunapotarajia kuwa wenyeji wa fainali za U17 Afrika mwaka 2019 "alisema Malinzi".

TFF ina program mbili za kuwaandaa vijana wenye umri chini ya miaka 13, 15 kwa kuwaweka kambini na kucheza michezo ya kirafiki mikoani na kufanya ziara katika nchi za Malawi, Zambia, Zimbabwe, Bostwana na Afrika Kusini.

Aidha Malinzi amewaomba walimu wakufunzi kuwa karibu na makocha wa timu za Taifa, na kuwapa ushauri makocha hao ili kuweza kuwasaidia katika kuboresha vikosi vyao na maendeleo ya soka la Tanzania kwa ujumla.

Naye Rais wa CECAFA na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya CAF, Leodgar Tenga alimshukuru Malinzi kwa kuweza kufungua kozi hiyo ambayo inawakutansisha walimu wakufunzi wa mpira miguu kutoka sehemu mbalimbali nchini.

 Akiongea kwa niaba wa walimu wakufunzi, Dr. Mshindo Msolla alisema wanaishukuru TFF kwa kuandaa kozi na kuomba kuendelea kushirikishwa katika mipango mbalimbali ya soka nchini ikiwa ni pamoja na kutambulika kuanzia katika ngazi za juu mpaka katika maeneo waliyopo.

Kozi hiyoiliyoanza leo jumatatu itamalizika Mei 2 mwaka huu, inawajumuisha walimu 18, wenye leseni A, B na C za CAF kutoka mikoa mbalimbali Tanzania bara na Zanzibar.

Sunday, April 5, 2015

YANGA MBELE KWA MBELE


WAWAKILISHI wa Tanzania katika michuano ya soka ya Kombe la Shirikisho, Yanga wamefuzu hatua ya 16 bora licha ya kuchapwa bao 1-0 na Platnum ya Zimbabwe katika mechi iliyochezwa mjini Bulawayo.

Yanga imesonga mbele kwa ushindi wa jumla wa mabao 5-2, kufuatia kushinda mechi ya awali wiki mbili zilizopita mjini Dar es Salaam kwa mabao 5-1.

Kutokana na ushindi huo, Yanga sasa itakutana na mshindi wa mechi kati ya Etoile du Sahel ya Tunisia na Benfica ya Angola.

Platnum walilianza pambano hilo kwa kasi huku wakiwa na uchu mkubwa wa kushinda kwa idadi kubwa ya mabao ili waweze kusonga mbele. Platnum ilikuwa ikihitaji ushindi wa mabao 4-0 ili isonge mbele kwa faida ya bao la ugenini..

Bao pekee na la ushindi la Platnum lilifungwa na mshambuliaji wao hatari, Walter Musona dakika ya 29 kwa shuti la mguu wa kushoto, akiunganisha krosi kutoka pembeni ya uwanja.

Yanga ilitarajiwa kurejea nchini juzi usiku kwa ndege ya serikali, ambayo ndiyo iliyowapeleka Zimbabwe.

MALINZI AKUTANA NA MAKAMU WA RAIS WA FIFA


Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini TFF jana ijumaa ilipokea ugeni wa makamu wa Rais wa FIFA ambaye pia ni mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu nchini Jordan, HRH Prince Ali Bin Al Hussein.

Jioni, Prince Ali Bin Ali Hussein na ujumbe wake walifanya mazungumzo na Rais wa Shrikisho la Mpira wa Miguu nchini TFF Jamal Malinzi  katika hoteli ya Kilimanjaro Kempsinki (Hyatt) iliyopo jijini Dar es salaam.

Katika mazungumzo hayo, zaidi waligusia maeneo kadhaa ya ushirikiano kati ya TFF na Chama cha Mpirwa wa Miguu nchini Jordan (JFA), hasa katika maeneo ya maendeleo ya mpira wa vijana, makocha na waamuzi.

HRH Prince Ali Bin Al Hussein ambaye ni mgombea wa nafasi ya urais FIFA mwaka huu, ameondoka leo mchana kurudi nyumbani kwake Jordan.

TFF YATUMA SALAMU ZA RAMBIRAMBI SIMBA SC


Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini TFF Jamal Malinzi, ametuma salamu za rambi rambi kwa Rais wa klabu ya Simba SC, Evans Aveva kufuatia vifo vya mashabiki wa klabu hiyo, viliyotokea juzi katika ajali ya barabarani eneo la Makunganya mkoani Morogoro.

Katika salamu zake Rais Malinzi amesema, TFF imezipokea kwa masikitiko taarifa hizo za ajali na kwa niaba ya familia ya mpira wa miguu nchini, wanawapa pole wafiwa wote na mwenyezi Mungu awape nguvu majeruhi waweze kupata nafuu na kupona kwa uharaka zaidi.

Aidha Rais  Malinzi ameagiza michezo yote ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania itakayochezwa  wikiendi hii nchini, kusimama kwa dakika moja ili kuwakumbuka mashabiki waliopoteza maisha katika ajali hiyo.

Thursday, April 2, 2015

DIAMOND APEWA MIL. 14/- NA CRDBMWANAMUZIKI nyota nchini, Naseeb Abdul, maarufu kwa jina la Diamond, amepewa shilingi milioni 14 na benki ya CRDB kama fidia kwa ajili ya kujenga sehemu ya ukuta wa nyumba yake uliobomoka.

Ukuta wa nyumba ya Diamond, iliyoko Tegeta, Dar es Salaam, ulianguka wiki mbili zilizopita kutokana na kunyesha kwa mvua kubwa.

Akikabidhi fedha hizo kwa Diamond jana, Meneja Masoko wa Kampuni ya Bima ya UAP, ambayo ni wakala wa CRDB, Raymond Komanga, alisema Diamond amekatia bima mali zake zote, ikiwemo nyumba yake.

Alisema kutokana na sababu hiyo, wameamua kumlipa bima ya nyumba yake yenye thamani ya sh. milioni 14 kwa ajili ya kutengeneza ukuta uliobomoka.

Diamond aliishukuru CRDB kupitia wakala wake wa UAP, kwa kumpatia fedha hizo kwa kuwa yuko kwenye kipindi kigumu kifedha.

"Nipo kwenye kipindi kigumu mno, mama yangu ni mgonjwa, halafu nipo kwenye maandalizi ya kutengeneza na kutoa video zangu mpya na vyote hivyo vinahitaji fedha,"alisema.

BEKI SIMBA ATOWEKA


BEKI wa kushoto wa klabu ya Simba, Ramadhani Kessy, ameweka bayana kuwa kamwe hatarajii kurejea katika kikosi cha timu hiyo hadi atakapopewa nyumba ya kuishi.

Akizungumza kwa njia ya simu kutoka Morogoro, Kessy amesema hakwenda Shinyanga na timu hiyo hadi atakapotimiziwa mahitaji yake.

Simba iliondoka jana kwenda Shinyanga kwa ajili ya mchezo wake wa ligi kuu ya Tanzania Bara dhidi ya Kagera Sugar, utakaopigwa kesho kwenye Uwanja wa Kambarage.

Kessy alisema alipofuatwa na uongozi wa klabu hiyo kwa ajili ya kumsajili, walimpa ahadi ya kumtafutia nyumba ya kuishi, lakini hadi sasa wameshindwa kuitekeleza.

"Nimeamua kuondoka Simba na kurudi Morogoro kupumzika. Nitakuwa tayari kurejea Simba baada ya uongozi kutekeleza ahadi hiyo,"alisema.

Alisema tangu alipoamua kujiunga na Simba, amekuwa akiishi maisha ya kutangatanga na wakati mwingine kusaidiwa sehemu ya kulala na wachezaji wenzake.

"Nimekuwa nikijituma sana kila ninapoichezea Simba. Pia nimevumilia sana, lakini naona sithaminiwi. Kila meneja wangu akiwasiliana na viongozi kuhusu suala langu, wanakataa kupokea simu yake,"alilalamika Kessy.

Hata hivyo, Katibu Mkuu wa Simba, Steven Ally, alidai kuwa mchezaji  huyo ameachwa kwenye safari ya Shinyanga kutokana na kiwango chake kutomridhisha.

Steven alisema uongozi wa Simba uliahidi kumtafutia mchezaji huyo nyumba ya kuishi na si kumnunulia nyumba kama anavyodai.

TFF YAIOMBEA DUA YANGARAIS  wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania, (TFF), Jamal Malinzi, amewatakia kila la kheri wawakilishi pekee wa Tanzania kwenye Kombe la Shirikisho Barani Afrika, Young Africans, katika mchezo wa marudiano dhidi ya FC Platinum ya Zimbabwe, utakochezwa Jumamosi kwenye Uwanja wa Mandava ulioko mjini Bulawayo.

Malinzi amesema Young Africans hawapaswi kubweteka kwa ushindi walioupata awali wa mabao 5-1 na kwamba kikubwa wanapaswa kwenda kupambana kusaka ushindi ugenini ili kufuzu kwa hatua inayofuata ya timu 16.

Endapo Young Africans itafanikiwa kuwatoa FC Platinum, itaingia katika hatua ya 16 bora na itakutana na mshindi kati ya timu za Benifica de Luanda ya Angola au Etoile du Saleh ya Tunisia.

SIMBA, KAGERA SUGAR DIMBANI J'MOSILigi Kuu ya Vodacom inatarajiwa kendelea kutimua vumbi mwishoni mwa wiki katika viwanjasita nchini, kwa michezo minne. Michezo miwili itachezwa Jumamosi na michezo mingine miwili itachezwa siku ya Jumapili.

Siku ya Jumamosi, Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga, utawaka moto  wakati Kagera Sugar watakapomenyana na Simba SC.

Mjini Tanga, Coastal Union watawakaribisha maafande wa Jeshi la Magereza nchini, Tanzania Prisons kwenye Uwanja wa Mkwakwani.

Ndanda FC ya Mtwara watakuwa wenyeji wa wagonga nyundo, timu ya Mbeya City katika Uwanja wa Nagwanda Sijaona, wakati maafande wa Jeshi la Kujenga Taifa, Ruvu Shooting wakicheza na ndugu zao JKT Ruvu katika uwanja wa Mabatin ulioko Mlandizi.

Siku ya Jumapili, Stand United watawakaribisha wakata miwa kutoka Morogoro, Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Kambarage huku Mgambo Shooting wakiwa wenyeji wa timu ya Polisi Morogoro kwenye Uwanja wa Mkwakani jijini Tanga.

TWIGA STARS, ZAMBIA KURUDIANA APRILI 10


Timu ya Taifa ya Tanzania ya Wanawake (Twiga Stars), Aprili 10, mwaka huu, itashuka dimbani  Uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam kuwakarisbisha timu ya Taifa ya Wanawake ya Zambia (The She-Polopolo).

Twiga Stars inayonolewa na kocha mkuu Rogasian Kaijage iliingia kambini mwishoni mwa wiki na kikosi cha wachezaji 25 katika hostel za TFF zilizopo Karume, kujiandaa na mchezo huo ambao ni muhimu wa kuwania kufuzu kwa fainali za michezo ya Afrika mwaka huu.

Katika mchezo wa awali uliofanyika wiki mbili zilizopita jijini Lusaka Zambia, Twiga Stars iliibuka na ushindi wa mabao 4-2, mabao yaliyofungwa na Asha Rashid (2), Shelder Boniface (1) na Sophia Mwasikili (1).

Mshindi wa jumla katika mchezo huo atafuzu moja kwa moja kwa fainali za Michezo ya Afrika zitakazofanya nchini Congo - Brazzavile kuanzia Septemba 13 mwaka huu.