KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Monday, October 20, 2014

MREMBO NYANDA ZA JUU KUSIKI AFUNGUKA, APONDA USHINDI WA SITTI , ADAI ULIPANGWA MAPEMA


MARIA Itala, mama mzazi wa Maureen (kushoto) akiwa na binti yake.


Na Michael Katona, Njombe

MSICHANA Maureen Godfrey, ambaye ni mrembo wa Nyanda za Juu Kusini, akitokea Mkoa wa Njombe, amefunguka na kudai kuwa ni vigumu kwa warembo kutoka kanda hiyo kuweza kufika hatua ya fainali kwenye shindano la Mrembo wa Tanzania.

Akizungumza baada ya kushindwa kufanya vyema kwenye mashindano ya kumsaka Miss Tanzania, yaliyofanyika Oktoba 11, mwaka huu, jijini Dar es Salaam, Maureen alisema wakati akiwa anashiriki shindano la 'Miss Nyanda za Juu' mkoani Iringa, aliambiwa na mmoja wa majaji, ambaye anatoka ndani ya Kamati ya Miss Tanzania, kwamba ni ndoto kwa warembo kutoka mikoa ya kusini kuweza kushinda taji hilo.

“Hakuna warembo wazuri na wenye sifa kutoka kanda hiyo, hivyo si rahisi kwa mikoa ya Nyanda za Juu Kusini kuweza kutoa mrembo atakayeweza kutwaa taji hilo,” alisema Maureen akimnukuu jaji huyo (jina tunalo).

Mrembo huyo alisema kwa jinsi ambavyo ameona mashindano ya mwaka huu yalivyoendeshwa na Sitti Mtemvu kuvishwa taji la Miss Tanzania, haoni sababu kwa warembo wengine watakaotaka kushiriki mashindano hayo kwenye kanda ya Nyanda za Juu Kusini kuungana na warembo wengine katika kambi ya Miss Tanzania mwakani.

“Kwa warembo wengine ambao watataka kuja kushiriki kwenye kanda ya Nyanda za Juu Kusini, siwashauri washiriki mashindano haya. Niliwahi kumuuliza jaji mmoja ni kwa nini Nyanda za Juu Kusini mtu akijitihadi sana, anaishia 15 bora? Alinijibu kwa sababu huko kwenu hamna warembo wazuri, na alidai eti wasichana wazuri wako Mwanza, Dar es Salaam na Arusha,” alisema Maureen.

Maureen, ambaye hakuingia hatua ya 15 bora kwenye mashindano ya mwaka huu, yaliyowashirikisha warembo 30 kutoka nchi nzima, alisema warembo wenzake wanaotoka mikoani wamekuwa hawapewi nafasi kama warembo wengine wanaotoka kwenye mikoa ya Dar es Salaam, Arusha na Mwanza.

“Nilipotangazwa kuwa mshindi wa urembo wa mkoa wa Njombe na Nyanda za Juu Kusini, wapo baadhi waliniona ni mshamba na nisiyekuwa na sifa za kuuwakilisha mkoa kama mrembo, wengine walidai sisi warembo tunaotokea huku Nyanda za Juu Kusini eti tunatokea porini, hatujui lolote,” alisema Maureen.

Mrembo huyo alida wakati akiwa kwenye kambi ya Miss Tanzania, vipaumbele walikuwa wakipewa zaidi warembo kutoka Kanda ya Dar es Salaam, Arusha na Mwanza.

“Mambo mengi nilikuwa naona, wanapewa vipaumbele warembo wanaotoka Arusha, Mwanza, Shinyanga na Dar es Salaam, tena kwa kila kitu, hasa katika suala la mahojiano kwa kila mshiriki, tuliambiwa tutafanyiwa (interview) mara tatu ili tuonekane kwenye luninga, lakini nilimuuliza muongozaji filamu, inakuwaje mtu mmoja anakuwa ni yeye tu anayerekodiwa huku wengine hatupigwi picha za video?

“Muongozaji wa picha alikuwa anamchukua mtu mmoja pekee yake kwa kuanzia mguuni mpaka kichwani, lakini wengine tulikuwa hatupewi nafasi hiyo. Nilimuuliza mbona wengine hatuchukuliwi kama huyo, akasema wengine siyo lazima kuchukuliwa.

Kama mnasema picha si lazima, basi mngekuwa mnachukua warembo kumi tu ndiyo wanaotakiwa waonekane, kuliko kufanya ubaguzi wa picha na mahojiano kwa warembo wengine, ili hali wakiwa na matumaini ya kufanyiwa interview, lakini imekuwa ni tofauti,” alilalamika mrembo huyo.

Mwakilishi huyo kutoka mkoani Njombe pia aliyakosoa mashindano hayo kwa waandaji kuwanyima warembo wengine nafasi ya kujitambulisha jukwaani, kama ambavyo miaka mingine imekuwa ikifanyika,badala yake ilitumika njia ya kurekodiwa na kurushwa katika luninga kwa kila mshiriki kuonyeshwa anakotoka na vitu ambavyo anapendelea kufanya katika jamii.

“Tulipokuwa tunatoka Moshi kwenda KIA (uwanja wa ndege wa Kilimanjaro), nilihoji ni kwa vipi hatufanyiwi mahojiano sisi baadhi ya warembo huku wengine tayari wamefanyiwa zaidi ya mara tatu. Lakini picha ambayo nilipigwa mimi ni ile ya kujitambulisha unauwakilisha mkoa gani,” alisema mrembo huyo.

Alipoulizwa kama anakubaliana na uamuzi wa majaji kumtangaza Sitti, alisema hakustahili kabisa kuwa mshindi na tayari kulikuwa na dalili za upendeleo za kumtangaza mshindi huyo.

“Huyu dada hakustahili kuwa mshindi wa taji hili la Miss Tanzania, labda pengine alistahili kuwa mshindi wa kawaida kati ya warembo watano bora, mimi napinga yeye kuwa mshindi, kwa sababu tangu awali dalili za upendelo zilishafanyika na alikuwa amepangwa,” alisema Maureen.

"Jambo la kushangaza ni kwa vipi kila mara, mrembo huyo apite katika kila hatua na hata zaidi muda mwingi kamera zilikuwa zikimuonyesha yeye, hii si sawa, matokeo yalipotoka wapo watu waliangua kilio na wengine walipoteza fahamu kwa mshituko mkubwa, ambao hawakuutarajia,” alisema.

Aliwashauri waandaaji a Miss Tanzania, chini ya Mkurugenzi wa Lino International Agency, Hashim Lundenga, kuepuka lawama hivi sasa ni bora mashindano hayo yakawa yanafanyika katika miji mingine kuliko miaka yote kufanyika Dar es Salaam pekee.

“Rai yangu ni kwa waandaaji hawa wadogo kwamba wasikatishwe tamaa na haya yaliyotendeka katika shindano hili, lakini pia haki haikutendeka kwa washiriki wengine waliokwenda kushindana. Kama Nyanda za Juu Kusini imeonekana hawana warembo wazuri, nashauri mashindano ya urembo yatakayofanyika kwenye kanda hiyo, yaishie hapo hapo na si kupelekwa kwenye shindano la Miss Tanzania,” alisema Maureen.

"Ni vyema mshindi atakayeshindanishwa kutoka kwenye kanda, apewe zawadi sawa na zile zinazotolewa kwa Miss Tanzania. Hakuna maana ya sisi warembo tunaotoka mikoani, kushirikishwa kwenye fainali hizo. Tumekuwa tunaonekana sisi ni washamba na hatuna sifa zinazostahili,” alilalamika.

Tayari ushindi wa Sitti umeshaanza kulalamikiwa na wadau wa mashindano hayo, ambapo inadaiwa kuwa, ameghushi umri wake.

Sitti katika fomu za kujiandikisha kuingia katika mashindano hayo, alijaza ana umri wa miaka 18,

wakati umri wake halisi unadaiwa kuwa ni miaka 25. Sifa za mshiriki wa Miss Tanzania anatakiwa awe na umri wa miaka 18 hadi 23, awe raia wa Tanzania, awe hajaolewa, awe na ufahamu wa kutosha kujieleza, awe hajazaa na asiwe mwanafunzi wa shule ya msingi au sekondari.

Kwa upande wake, Maria Itala, ambaye ni mama mzazi wa Maureen, ambaye alikwenda kushuhudia fainali hizo jijini Dar es Salaam, akizungumza kwa niaba ya wazazi wenzake, alionya kwamba endapo waandaaji hawatakuwa makini, mashindano hayo yatapoteza sifa zake na jamii kuyachukulia kuwa ya kihuni.

“Kufanya mashindano ya kikanda zaidi bila kwenda Taifa, kutasaidia sana washiriki hususan wazazi wanaowakilishwa na watoto wao kwenye fainali hizo, wasipate hasara kubwa kama ambavyo mimi mzazi wa Maureen nilivyopata,” alisema Itala.

Aliishauri Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, kuangalia uwezekano wa kuyasimamia ili kuepuka utata, ambao umekuwa ukijitokeza mara kwa mara, ikiwemo harufu ya rushwa na upendeleo.

“Mashindano haya ni ya kitaifa, ambapo baadaye mwakilishi anapeperusha bendera ya Tanzania kwenye taji la dunia, ni vyema yakadhaminiwa na serikali yenyewe. Rushwa hivi sasa ni kubwa sana kwenye mashindano haya, ni vyema serikali ikachukua jukumu la kudhamini Miss Tanzania, kama ambavyo wanavyofanya nchi za Nigeria, Ghana na nyinginezo, ndiyo maana wenzetu wanapata wawakilishi wanaofanya vizuri kwenye shindano la dunia,” alisema.

“Endapo serikali itayachukua, kwanza itaingiza pato kubwa na vilevile itakuwa inagharamia kila kitu, lakini si kama hivi sasa, wenzetu wanatushangaa, iweje mpaka kwenye mashindano makubwa kama hayo, mzazi aendelee kutoa gharama kubwa za kuchangia maandalizi ya mshiriki? Hapana, hili siyo sahihi, mtoto anapata manyanyaso na kubaguliwa, kweli mzazi unaweza kuugua,” alisema Itala.

Alidai tangu mtoto wake ashiriki kwenye kambi hiyo ya Miss Tanzania, jambo kubwa ambalo amejifunza ni kuona baadhi ya wazazi wenzake wanashindwa uwezo wa kifedha kwenye maandalizi hayo, na hasa kwa baadhi ya warembo wanaotoka katika mikoa hiyo mipya kwa sababu hawafahamiki na hivyo warembo wanaopewa nafasi kubwa ni wale wanaotoka katika kanda fulani.

“Ni vigumu kwa mrembo anayetoka katika hii mikoa mipya kuweza kushinda. Kwanza hajulikani, mashindano ya sasa yanaonekana kuegemea zaidi kwenye kanda fulani, sikubaliani na waandaaji kujikita zaidi kutangaza vivutio vya kanda ya kaskazini, kwani hata nyanda za juu kusini inapaswa kupewa nafasi ya kutangazwa zaidi, pia zipo fursa,” alisema.

Itala pia alitoa tahadhari kwa waandaaji kuachana na kasumba ya upendeleo inayoanza kuonekana hivi sasa kwa mashabiki kutengeneza vipeperushi vya ushabiki kwa mrembo ambaye wanaona atashinda.

“Mtizamo wangu kwa sasa, mashindano haya yameanza kuingizwa na siasa, watu wanakuja na mabango, wengi tumeona wamekuja na vipeperushi vinavyoonyesha tayari mrembo fulani atakuwa mshindi, na hatimaye akawa mshindi, hiyo tayari ni siasa, hatufanyi mashindano ya urembo yakaingizwa siasa,” alisema.

MAUREEN Godfrey, mrembo wa mkoa wa Njombe na Nyanda za Juu Kusini

No comments:

Post a Comment