MSHAMBULIAJI nyota wa timu ya Zanzibar, Zanzibar Heroes, Ally Ahmed Shiboli ametamba kuwa, ataibuka mfungaji bora katika michuano ya mwaka huu ya Kombe la Chalenji inayoendelea kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Akizungumza na Burudani mjini Dar es Salaam wiki hii, Shiboli alisema amedhamiria kuibuka mfungaji bora wa michuano hiyo ili aweze kutimiza malengo aliyojiwekea kisoka.
Majigambo hayo ya Shiboli yamekuja siku chache baada ya kuifungia Zanzibar mabao mawili, ilipoibwaga Sudan mabao 2-0 katika mechi ya kundi B iliyochezwa kwenye uwanja huo.
“Nimedhamiria kumaliza mashindano haya nikiwa mfungaji bora. Ndoto yangu imeanza kukamilika kwani nimeweza kufunga mabao mawili peke yangu katika mechi moja,”alisema.
Mshambuliaji huyo aliyesajiliwa na klabu ya Simba katika usajili wa dirisha dogo akitokea KMKM ya Zanzibar alisema, amepania kuifungia bao Zanzibar katika kila mechi atakayocheza.
“Nimedhamiria kucheza kwa kujituma na kuifungia timu yangu mabao mengi zaidi ili tumalize mechi za kundi letu tukiwa wa kwanza,”alisema.
Shiboli alisema Zanzibar imeanza vyema michuano ya mwaka huu kutokana na maandalizi mazuri waliyoyafanya ikiwa ni pamoja na wachezaji kufuata vyema mafunzo ya Kocha Stewart Hall kutoka Uingereza.
Zanzibar ilitarajiwa kutupa karata yake ya pili jana kwa kumenyana na Ivory Coast, ambayo katika mechi yake ya kwanza, ilichapwa mabao 2-1 na Rwanda.
Akizungumzia usajili wake Simba, Shiboli alisema alikuwa na ndoto za kuichezea timu hiyo kwa kipindi kirefu, lakini hakuwa akifahamu angewezaje kufika huko.
Alisema aliposikia kwamba viongozi wa Simba, Yanga na Azam, zote za Dar es Salaam wanamtafuta, alifarijika kwa kutambua kwamba kiwango chake kimewakuna.
Shiboli aliwavutia viongozi wa klabu hizo tatu baada ya kuonyesha soka ya kiwango cha juu wakati Zanzibar Heroes ilipomenyana na Dar es Salaam All Stars katika mechi za kirafiki zilizochezwa Dar es Salaam na Zanzibar.
Awali, Mwenyekiti wa klabu ya Yanga, Llyord Nchunga aliwaambia waandishi wa habari mjini Dar es Salaam wiki iliyopita kuwa, walikuwa katika hatua za mwisho za kumsajili mchezaji huyo na kwamba mazungumzo kati yao yalikuwa yakienda vizuri.
Lakini siku chache baadaye, Makamu Mwenyekiti wa Simba, Geofrey Nyange ‘Kaburu’ alitoa taarifa kuwa, klabu hiyo imefanikiwa kumsajili Shiboli kwa mkataba wa miaka mitatu.
Shiboli anatarajiwa kuanza kuichezea Simba katika mzunguko wa pili wa ligi kuu ya Tanzania Bara, unaotarajiwa kuanza Januari 15 mwakani. Simba inaongoza ligi hiyo kwa tofauti ya pointi mbili kati yao na watani wao wa jadi Yanga.
Alipoulizwa kuhusu matarajio yake kwa Simba, Shiboli alisema hawezi kuwaahidi mengi mashabiki wa timu hiyo, lakini alisisitiza kuwa, atacheza kwa kujituma ili kuisaidia ifanye vizuri katika ligi hiyo.
“Ni vigumu kwa sasa kusema nitafanya nini Simba kwa sababu mimi ni mgeni na ligi kuu ya Tanzania Bara, lakini kwa vile lengo langu ni kupata mafanikio zaidi kisoka, nitafanya kila ninaloweza kuisaidia timu yangu mpya,”alisema.
Wakizungumzia usajili wa mchezaji huyo, baadhi ya wachezaji nyota wa Simba, akiwemo kipa Juma Kaseja walikiri kuwa, timu yao imepata mshambuliaji hatari na mwenye uwezo wa kuiletea mafanikio zaidi.
Kaseja alisema Shiboli ni mshambuliaji mwenye uwezo wa kufanya lolote kila anapofika karibu na lango la upinzani na pia ana uwezo mkubwa wa kufunga mabao kwa mashuti ya mbali.
No comments:
Post a Comment