KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, August 9, 2012

INI EDO AKIRI KUWA NA UJA UZITO

LAGOS, Nigeria
BAADA ya ukimya wa muda mrefu, hatimaye mcheza filamu tajiri wa kike nchini Nigeria, Ini Edo amethibitisha kuwa ni kweli ana uja uzito.
Ini amethibitisha ukweli huo katika mahojiano yaliyochapishwa hivi karibuni kati yake na gazeti la E 24-7 la Nigeria.
Uamuzi wa Ini kuthibitisha taarifa hizo, umekuja siku chache baada ya baadhi ya vyombo vya habari vya Nigeria kuripoti kuwa, yeye na Mercy Johnson ni waja wazito.
Vyombo hivyo vya habari pia viliripoti kuwa, Ini na Mercy wamepanga kujifungulia nchini Marekani, ambako ndiko waume zao wanakoishi.
Siku chache baada ya kuripotiwa kwa taarifa hizo, Ini alizikanusha kwa madai kuwa hazikuwa za kweli. Ini alifunga ndoa na Philip Ehiagwina mwaka 2008.
Kwa mujibu wa taarifa za mitandao, Ini na Mercy wanatarajiwa kujifungua hivi karibuni.
Ini na Mercy wanatarajiwa kwenda Marekani mara baada ya kukamilisha kazi ya kucheza filamu yao mpya, inayorekodiwa katika mji wa Asaba uliopo kwenye jimbo la Delta.
Mume wa Ini, Philip ni mfanya biashara anayeishi Marekani. Mercy na mumewe, Prince Odi Okoije walifunga ndoa Agosti 2011.

OMOTOLA AMPA TANO MUMEWE

LAGOS, Nigeria
WAKATI filamu yake mpya ya Last Flight to Abuja ikiwa inatamba, mcheza filamu nyota wa kike wa Nigeria, Omotola Jalade amesema anavutiwa na mumewe kutokana na uelewa wake juu ya masuala mbali mbali ya kimaisha.
Omotola alisema wiki hii mjini hapa kuwa, uelewa huo wa mumewe ndiyo ulioiwezesha ndoa yao kudumu kwa miaka 16 hadi sasa na pia kuzaa naye watoto wanne.
Mwanamama huyo mwenye umbo na sura yenye mvuto alisema, licha ya kuvumishiwa skendo mbali mbali, mumewe haonekani kukerwa kwa sababu anafahamu ukweli wa mambo juu yake.
“Nilivutiwa naye tangu tulipokutana kwa mara ya kwanza. Alionekana kunifahamu vyema kuliko nilivyokuwa nikijifahamu. Ni vigumu kuelezea,”alisema.
“Kama nisingefunga ndoa na yeye, nisingeweza kufunga ndoa na mtu mwingine yeyote,”aliongeza mwanadada huyo, ambaye mbali na kucheza filamu, pia ni mwanamuziki.
Omotola alisema amekuwa akizushiwa skendo mbali mbali kutokana na umaarufu wake kwenye fani ya filamu na muziki, lakini kamwe si za kweli.
Alisema yeye ni mtu anayejiheshimu na kamwe hawezi kuvunja utu wake ama kujishusha thamani kwa kufanya vitendo vinavyokiuka maadili ya ndoa.
“Ningekuwa nikijihisi uchungu kama mume wangu angekuwa akiyaweka moyoni mambo hayo na ningekuwa kwenye wakati mgumu. Lakini namshukuru Mungu kwamba huwa hayajali,”alisema Omotola.
Mwanadada huyo alisema alikutana na mumewe kwa mara ya kwanza siku chache baada ya kufiwa na baba yake mzazi na kwamba alipitia kwenye wakati mgumu.
Alisema katika kipindi hicho, alikuwa bado mdogo kiumri, lakini mumewe alikuwa akimpa moyo na kumfanya aweze kuhimili mambo mazito kwa haraka.

WACHEZA FILAMU WA NOLLYWOOD WALIZWA LONDON

LAGOS, Nigeria
WACHEZA filamu Segun Arinze na Justus Esiri wa Nigeria wiki iliyopita walikumbwa na mkasa baada ya kuporwa vitu vyao kadhaa kwenye hoteli moja mjini London, Uingereza.
Arinze na Esiri walikumbwa na mkasa huo wakati walipokuwa wamepanga kwenye hoteli ya Teavelodge iliyopo katika eneo la Surrey mjini London.
Kwa mujibu wa mtandao wa nigeriafilms, vyumba vya hoteli hiyo vina funguo tatu kila kimoja, moja ya mpangaji, ya meneja wa hoteli na nyingine ya mfanyakazi anayefanya usafi vyumbani.
Wacheza filamu hao walikuwepo London kwa mwezi mmoja katika ziara ya kuonyesha igizo la ‘The King must dance naked’ pamoja na maigizo mengine.
Imeelezwa kuwa, siku ya tukio, wacheza filamu hao walikuwa wamekwenda mazoezini na baada ya kurejea hotelini, waligundua kwamba vitu vyao vilikuwa vimepekuliwa.
“Baada ya kukagua mizigo yao, wakagundua kwamba baadhi ya vitu vyao vya thamani vimeibwa,” umeeleza mtandao huo.
Arinze aliripotiwa kupoteza Ipad wakati Justus alipoteza hati yake ya kusafiria, ikiwa na viza za kuingilia katika nchi kadhaa, nyaraka za safari, laptop pamoja na vitu vingine kadhaa vya thamani.
Kwa mujibu wa mtandao huo, tukio hilo liliripotiwa polisi, lakini hakuna mtu aliyekamatwa kuhusiana na wizi huo. Pia imeelezwa kuwa, hoteli hiyo haikuwa na kamera za CCTV kwa ajili ya kurekodi matukio ya aina hiyo.
Kufuatia wizi huo, ubalozi wa Nigeria nchini Uingereza ulimpatia Justus hati mpya ya kusafiria.
Wacheza filamu wengine waliokuwepo kwenye ziara hiyo ni Olu Jacobs, Joke Silva na Bimbo Akintola na walitarajiwa kurejea nchini Nigeria jana.

ELLIOT: Nilikuwa kipenzi cha mama yangu

LAGOS, Nigeria
MCHEZA filamu machachari wa Nigeria, Desmond Elliot amesema alijitokeza kuwa kipenzi cha mama yake baada ya kumpelekea pesa kutokana na ujira aliolipwa kwa kazi ya kucheza filamu.
Elliot ameueleza mtandao wa naijerules wiki hii kuwa, mama yake huyo aliona fahari kubwa kutokana na kazi yake hiyo na tangu wakati huo, akawa kipenzi chake kikubwa.
Msanii huyo mwenye sura yenye mvuto alisema, mama yake alipatwa na kiwewe cha furaha siku alipomuona kwa mara ya kwanza kwenye filamu ya Kinigeria.
"Alipokuwa hanioni katika filamu nilizoshiriki kuzicheza, alikuwa akilalamika sana kwa sababu siku zote nilikuwa nikitoka nyumbani asubuhi na kurudi usiku,"alisema.
"Kwa mara ya kwanza aliniona katika filamu ya Suitors, ambayo nilicheza sehemu ya muhusika wa kawaida. Alipatwa na kiwewe cha furaha," aliongeza msanii huyo.
Pamoja na kufurahishwa na kazi yake hiyo, Elliot alisema mama yake hakuwa mtu wa kudekeza watoto wake na kuongeza kuwa, kuna wakati aliwahi kumfikisha polisi.
"Baada ya kunifikisha polisi, alimweleza ofisa wa zamu kumsaidia kunifundisha nidhamu na kunipiga. Aliwahi kufanya hivyo mara mbili," alisema Elliot.
Elliot ni baba wa watoto wanne, akiwa amezaa mapacha mara mbili. Alisema wazazi wake hawana historia ya kuzaa watoto mapacha, lakini hilo lipo katika familia ya mkewe.
"Nilipopata mapacha kwa mara ya kwanza, nilifurahi na kumshukuru Mungu. Lakini mara ya pili, sikuwepo nchini, nilikuwa nje ya nchi. Mke wangu aliponipigia simu kunijulisha, sikuamini. Aliponiuliza kwa nini, nilimweleza sikutarajia," alisema.
Elliot alisema bado anahitaji kupata watoto wengine watatu zaidi. Alisema lengo lake ni kuwa na watoto saba.
Mcheza filamu huyo alisema amejipanga vyema kuhakikisha anawalea vyema watoto hao ikiwa ni pamoja na kuwapatia elimu nzuri kwa ajili ya maisha yao ya baadaye.
Elliot alisema anapenda sana watoto na kwamba baadhi ya wakati anapokuwa nyumbani, huwa akiwaogesha badala ya kazi hiyo kufanywa na mkewe.

SHARO MILIONEA: STAILI YANGU YA USHAROBARO NI YA PEKEE



MSANII nyota wa vichekesho na muziki wa kizazi kipya nchini, Hussein Mkiety amesema amebuni staili ya usharobaro kwa lengo la kujitofautisha na wasanii wengine.
Hussein, ambaye ni maarufu zaidi kwa jina la Sharo Milionea, alisema mjini Dar es Salaam wiki hii kuwa, ubunifu wake huo umemwezesha kupata mashabiki wengi katika fani zote mbili.
Alisema licha ya kuwepo kwa tabia ya watu wanaojikweza kwa muda mrefu, wakiwa maarufu kwa jina la ‘mabradha meni’, staili analiyoibuni ya watu wa aina hiyo imekuwa na mvuto zaidi.
Alivitaja vitu vingine alivyovibuni kwa lengo la kuupa mvuto ‘ubradha meni’ kuwa ni pamoja na uongeaji wake kwa kupinda mdomo, uvaaji, utembeaji, unyoaji nywele na kubandika plasta usoni.
“Staili ya mabradha meni asili yake hasa ni Wamarekani. Kila wakisema neno, lazima wamalizie kwa kusema ‘you know man’. Nami nimeiiga, lakini nimeongezea vionjo vingine zaidi,”alisema.
Hussein alisema alianza kujihusisha na uigizaji tangu akiwa shule ya sekondari na kwamba amewahi kucheza filamu moja na baadhi ya wasanii maarufu kama vile Masanja Mkandamizaji na McReagan wa kundi la Orijino Komedi.
Aliongeza kuwa, fani ya uchekeshaji ni asili yake tangu akiwa mdogo kutokana na kuwafurahisha vijana wenzake kila walipokuwa wakikutana kwa mazungumzo vijiweni kwa kubuni maneno yenye mvuto.
“Kila nilipokuwa nikikaa na kuzungumza na wenzangu, niliposema maneno fulani, walikuwa wakivutiwa nayo sana na kuniona mtu wa ajabu, yaani mchekeshaji,”alisema.
Hussein alisema aliamua kujitosa kwenye fani ya muziki baada ya kujibaini kwamba, anacho kipaji cha fani hiyo na hadi sasa amesharekodi nyimbo nne.
Alizitaja nyimbo hizo kuwa ni Tusigombane, Chuki bure aliomshirikisha Dully Sykes, Nawazamisha aliomshirikisha Nukta na Hawataki alioimba kwa kushirikiana na Kanali Top na Richard Mavoko.
Kwa mujibu wa Hussein, aliweza kurekodi nyimbo hizo kwa msaada mkubwa wa promota maarufu wa muziki nchini, Ustaadh Juma Namusoma, ambaye kwa sasa anamiliki kundi la Watanashati.
Hussein alisema kwa sasa ameshampata mdhamini, atakayekuwa akigharamia kurekodi nyimbo zake pamoja na kurekodi kanda za video, lakini hakuwa tayari kumtaja.
Alisema kwa kumtumia mdhamini huyo, ameanza kuandaa nyimbo zake mpya, ambazo atazirekodi kwa kushirikiana na msanii mwenzake nyota wa vichekesho, anayejulikana zaidi kwa jina la Kitale.
Alikiri kuwa, licha ya kurekodi nyimbo nne hadi sasa, bado hajaweza kupata mafanikio makubwa kimuziki kutokana na fani hiyo kukumbwa na vikwazo vingi.
Alisema mafanikio pekee aliyoyapata ni kujulikana na mashabiki wengi wa muziki na pia kupata marafiki wapya kila kukicha.
“Kwa sasa nitaendelea kurekodi wimbo mmoja mmoja hadi hapo mambo yatakapokuwa mazuri ndipo nitakaporekodi albamu,”alisema msanii huyo.
Alipoulizwa madai kuwa, amekuwa akipenda kujifagilia katika vichekesho anavyocheza pamoja na nyimbo zake, Hussein alisema huo ni uigizaji, lakini sivyo alivyo.
Hussein alikiri kuwa, miongoni mwa watu waliomwonyesha njia katika fani ya uigizaji ni msanii Kiwewe wa kundi la Ze Comedy. Lakini alikanusha madai kwamba, amewahi kuwa na uhusiano wa kimapenzi na mcheza filamu, Shilole.
“Shilole ni rafiki yangu na ni kama dada yangu. Vivyo hivyo kwa Mzee Majuto, namuheshimu nampenda na kumuheshimu kama baba yangu, ‘alisema.
Msanii huyo pia alikanusha madai kuwa, aliwahi kugombania jina la Sharobaro na msanii Bob Junior. Alisema jina la kiusanii analotumia ni Sharo Milionea na siyo Sharobaro.
Hussein amekiri kuwa, katika wimbo wa Ferouz wa Starehe gharama, alikubali kuvua nguo zake kwenye picha ya video baada ya kulipwa kitita cha sh. milioni moja na nusu, ambacho alikielezea kuwa kwake ni kikubwa.

'TUMIENI KISWAHILI KWENYE FILAMU ZENU'

SERIKALI imewataka wasanii wa filamu nchini kutumia lugha ya kiswahili kwenye filamu zao kwa lengo la kulinda na kutukuza utamaduni wa Mtanzania.
Mwito huo umetolewa na Mkurugenzi wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Profesa John Nkoma mwishoni mwa wiki iliyopita alipokuwa akifungua semina iliyoandaliwa na Shirikisho la Filamu Tanzania (TAFF) mjini Dar es Salaam.
Profesa Nkoma aliwapongeza wasanii wa fani hiyo kwa kuanzisha chombo chao, ambacho lengo lake kubwa ni kuwaunganisha, lakini aliwasihi kuiheshimu na kuitukuza lugha ya kiswahili kwenye filamu zao.
“Ukitazama filamu kutoka Bollywood, unaona kabisa utamaduni wao, lakini hata ndugu zetu wanigeria kupitia filamu zao, unaona utamaduni wao, lakini hapa kwetu, kuna watu wanawaiga wanigeria katika uzungumzaji wao,”alisema.
Mkurugenzi huyo wa TCRA alisema kuiga utamaduni wa kigeni si jambo zuri kwa sababu kunaweza kusababisha kazi za kitanzania zikapoteza mvuto.
Alisema ni vyema kwa wasanii wa filamu nchini kutengeneza kazi zao zikiwa na mwelekeo wa utamaduni wa mtanzania badala ya kuutangaza na kuutukuza utamaduni wa kigeni.
Profesa Nkoma alisema anapenda kuwaona wasanii wa filamu wa Tanzania wakipiga hatua kubwa kimaendeleo kama ilivyo kwa wasanii wa Nigeria.
“Kila jambo ukijipanga, linawezekana na kufanikiwa, hata sisi awali tuliposema tunataka kujenga jengo kubwa, ambalo ndimo mlimo leo hii mkifanyia mkutano huu, watu walibeza kwa kusema hatutaweza, lakini leo hii jengo limekamilika na linatumika,”alisema Prof. Nkomo.
Semina hiyo iliandaliwa na TAFF na kudhaminiwa na TCRA, ilifanyika kwa siku mbili na kuhudhuriwana wadau mbali mbali wa filamu. Wawezeshaji wa semina hiyo walitoka taasisi ya Tanzania Consultech International Limited wakati mtoa mada mkuu alikuwa Mkurugenzi wa Maendeleo ya Vijana kutoka Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Profesa Elisante Ole Gabriel.

WOLPER APIGA HESABU ZA MUZIKI

MCHEZA filamu machachari nchini, Jacqueline Wolper amesema anacho kipaji cha muziki, lakini bado hajaamua kujitosa kwenye fani hiyo.
Akizungumza mjini Dar es Salaam wiki hii, Jacqueline alisema wakati ukifika, huenda naye akaonyesha uwezo wake katika fani hiyo, inayoongoza kwa kuwa na mashabiki wengi nchini.
Jacqueline alisema tangu alipokuwa mdogo, aliweza kujitambua mapema kwamba anacho kipaji cha muziki, lakini hajaanza kukitumia, badala yake alijitosa kwenye filamu.
“Ukweli ni kwamba nina uwezo mkubwa sana katika fani ya muziki kuliko filamu,”alisema.
Kwa mujibu wa Jacqueline, filamu pekee, ambayo hadi sasa imemwezesha kupata malipo mazuri kuliko zingine kutokana na ushiriki wake ni Time After Time.
Alisema filamu hiyo iliyoandaliwa na Mussa Mtitu ni nzuri na ya aina yake kwa vile imeandaliwa kwa utaalam wa hali ya juu na kuhusisha matukio mengi ya mapigano.
“Napenda sana kucheza filamu za Mtitu kwa sababu ni za mapigano zaidi,”alisema.
Wakati huo huo, Jacqueline ametoa tahadhari kwa mashabiki wake kuhusu kujitokeza kwa mwanadada anayetumia jina lake kuomba fedha kwa watu mbali mbali.
Jacqueline amesema mwanamke huyo amekuwa akijitokeza mara kwa mara kwenye mitandao ya kijamii akijitambulisha kwa jina lake na kuomba misaada ya fedha.
“Huyu mtu ananijua vyema na kunifuatilia sana. Na wakati mwingine amekuwa akitumia jina la Jack Masawe, ambalo nilikuwa nikilitumia nilipokuwa shuleni,”alisema.
‘Nawaomba mashabiki wangu wajihadhari na mtu huyu kwa sababu ni tapeli,’ aliongeza.

KISIGA AIBUKIA MTIBWA SUGAR




KIUNGO wa zamani wa klabu ya Simba, Shaaban Kisiga amesajiliwa na Mtibwa Sugar ya Morogoro kwa ajili ya msimu ujao wa ligi kuu ya Tanzania Bara.
Mratibu wa Mtibwa Sugar, Jamal Bayser alisema mjini Dar es Salaam wiki hii kuwa, wameamua kumsajili Kisiga kwa lengo la kukiongezea nguvu kikosi cha timu hiyo.
Bayser alisema Kisiga ameshaanza mazoezi na timu hiyo na anatarajiwa kuanza kuichezea katika michuano ya BancABC Super 8 inayoendelea kutimua vumbi kwenye viwanja mbali mbali.
Mratibu huyo alikiri kuwa, kikosi chake kitapata upinzani mkali msimu ujao kutokana na timu nyingi kufanya maandalizi mazuri na kusajili wachezaji wengi nyota.
"Ni kweli kwamba tuna kazi ngumu na nzito msimu ujao kwa vile timu nyingi zimepania kuchukua ubingwa na sisi vivyo hivyo, kwa maana hiyo tutalazimika kupambana kufa na kupona,’ alisema.
Mbali na Kisiga, Mtibwa Sugar imemrejesha kipa wake wa zamani, Shabani Kado, ambaye msimu uliopita aliichezea Yanga na Machaku Salum, aliyekuwa akiichezea Simba.
Kwa sasa, Mtibwa Sugar inafundishwa na Kocha Mecky Maxime baada ya kutimuliwa kwa kocha wa zamani, Tom Olaba kutoka Kenya.

MSANII ANAPOMWAGA CHOZI

Msanii wa filamu Mohamed Nice 'Mtunisi' akilia kwa uchungu baada ya kukuta kazi feki zikiuzwa kwenye moja ya maduka ya mtaa wa Magila na Likoma, Kariakoo mjini Dar es Salaam juzi. (Na mpiga picha wetu)

Wednesday, August 8, 2012

MICHUANO YA BANCABC KUENDELEA LEO






Mechi za michuano ya BancABC SUP8R inayoshirikisha timu nane bora kutoka Tanzania Bara na Zanzibar zinaendelea kesho (Agosti9 mwaka huu) kwenye miji ya Dar es Salaam, Moshi, Mwanza na Zanzibar.

Mkurugenzi wa Mashindano wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Saad Kawemba na viongozi wa Chama cha Mpira wa Miguu Zanzibar (ZFA) chini ya Rais wao Amani Makungu walikutana leo mjini Zanzibar kuzungumzia maendeleo ya michuano hiyo. Viongozi wengine wa ZFA waliohudhuria kikao hicho ni Katibu Mkuu Kassim Haji Salum na wajumbe saba wa Kamati ya Utendaji.

Katika kundi A Jamhuri itacheza na Zimamoto kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar kuanzia saa 2 kamili usiku, wakati Simba itaparurana na Mtende kwenye Uwanja wa Ushirika, mjini Moshi. Mechi hiyo itaanza saa 10 kamili jioni.

Azam itakuwa mwenyeji wa Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Chamazi, Dar es Salaam wakati Uwanja wa CCM Kirumba, jijini Mwanza utakuwa mwenyeji wa mechi ya Polisi Morogoro na Super Falcon. Mechi hizo zote za kundi B zitaanza saa 10 kamili jioni.

Hatua hiyo ya makundi itamalizika Agosti 12 mwaka huu kwa mechi nne. Simba na Zimamoto zitaoneshana kazi Uwanja wa CCM Kirumba wakati Jamhuri na Mtende zitacheza kwenye Uwanja wa Chamazi, Dar es Salaam.

Mechi za kundi B zitakuwa kati ya Super Falcon na Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Amaan na Azam dhidi ya Polisi Morogoro kwenye Uwanja wa Ushirika.

NGASA, REDONDO, OKWI LAIVU SIMBA DAY

Mshambuliaji Emmanuel Okwi akipokea tuzo ya mwanasoka bora wa msimu wa 2011/12 kutoka kwa mmoja wa wadhamini wa klabu hiyo, Profesa Phillemon Sarungi.


Shomari Kapombe akipokea tuzo ya mchezaji mwenye nidhamu kutoka kwa Profesa Sarungi.




Klabu ya Simba leo imetoa tuzo kwa wanamichezo wake katika tamasha la kila mwaka la Simba Day lililofanyika kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.


Katika tuzo hizo, marehemu Patrick Mafisango alipewa tuzo ya heshima, Shomary Kapombe
alitwaa tuzo ya mchezaji mwenye nidhamu wakati Emmanuel Okwi alipewa tuzo ya
mchezaji bora wa klabu hiyo kwa msimu uliopita.


Watu wengine waliotwaa tuzo ni mwanachama wa siku nyingi wa klabu hiyo, Professa Philemon Sarungi, ambaye alipewa tuzo ya kuwa mtu aliyetoa mchango wa muda mrefu katika klabu hiyo, Haidari Abeid maarufu kama Muchacho alitwaa tuzo ya mchezaji wa bora wa Simba wa miaka ya 70's, Hamisi Kilomoni - mchezaji bora wa miaka ya 60 na Ally Sykes akapata tuzo ya heshima na udhamini.


Wakati wa tamasha hilo, washambuliaji Emmanuel Okwi, Mrisho Ngasa na Ramadhani Chombo Redondo walikuwa kivutio kikubwa kwa mashabiki wa Simba kutokana na kushangiliwa kwa mayowe mengi.

Tamasha hilo lilianza saa 9.15 alasiri kwa utambulisho wa wachezaji, ambapo Redondo aliyesajiliwa na Simba wiki hii akitokea Azam FC, alikuwa wa mwisho kutambulishwa kwa mashabiki na kushangiliwa kwa nguvu.

Okwi aliyewasili nchini juzi akitokea Uganda baada ya kufanyiwa majaribio katika klabu ya Red Bull Salzburg ya Austria, naye alishangiliwa kwa mayowe mengi kutokana na taarifa zilizokuwepo awali kwamba klabu ya Yanga ilikuwa ikimuwinda kwa udi na uvumba.

Baada ya utambulisho huo wa wachezaji, Simba ilitambulisha jezi zake mpya itakazotumia katika msimu ujao wa ligi kupitia kwenye luninga kubwa iliyopo kwenye uwanja huo. Jezi hizo zenye rangi nyekundu na nyeupe, zilikuwa na majina ya wachezaji wa timu hiyo.

Akizungumza wakati wa utambulisho huo, Kamwaga alisema jezi hizo zitaanza kuuzwa kwa mashabiki kwa utaratibu maalumu na aliwaonya mashabiki kuepuka kununua jezi feki.

Kamwaga alisema Simba itaanza kutumia jezi hizo katika mechi yake ya kuwania Ngao ya Hisani dhidi ya Azam, inayotarajiwa kuchezwa Agosti 25 mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Katika mwendelezo wa tamasha hilo, Simba ilichapwa mabao 3-1 na Nairobi City Stars katika mechi ya kirafiki ya kimataifa iliyochezwa kwenye uwanja huo.


Kufungwa huko kwa Simba kulitokana na kocha Milovan Cirkovick kubadilisha karibu kikosi kizima kilichoanza na kuingiza wachezaji wapya, ambao waliitoa City Stars ya Nairobi nyuma kwa 1-0 na kuipa ushindi wa 3-1.


Simba ilitangulia kupata bao kupitia kwa Felix Sunzu dakika ya 15, pasi ya Mwinyi Kazimot na ilikwenda kupumzika ikiwa mbele kwa bao hilo, lakini kipindi cha pili, kipa aliyempokea Juma Kaseja, Hamadi Waziri alitunguliwa mabao matatu katika dakika 57 na Duncan Owiti, dakika ya 64 na Bruno Okullu na dakika ya 79 na Boniphace Onyango.


Tuesday, August 7, 2012

AZAM YAMTAMBULISHA KOCHA WAKE MPYA



Makamu Mwenyekiti wa klabu ya Azam, Said Mohammed (kushoto), akimtambulisha kwa waandishi wa habari, kocha mpya wa timu hiyo, Boris Bunjak kutoka Serbia katika mkutano uliofanyika leo kwenye ofisi za Azam mjini Dar es Salaam. (Picha na Emmanuel Ndege wa blogu ya liwazozito)


TFF YASEMA REDONDO NI MCHEZAJI HURU

Kiungo Ramadhani Chombo Redondo amesema yeye ni mchezaji halali wa Simba kwa vile mkataba wake na Azam ulishamalizika tangu Juni mwaka huu.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Dar es Salaam jana, Redondo alisema ameamua kujiunga na Simba kwa vile kwa sasa yeye ni mchezaji huru.
Redondo amesajiliwa na Simba kwa kitita cha sh. milioni 30, ambapo tayari ameshalipwa sh. milioni 20 wakati sh. milioni 10 zingine atalipwa baadaye.
"Ninavyojua ni kwamba mkataba wangu na Azam ulishamalizika tangu Juni mwaka huu na sikuwa na mpango wa kuongeza mkataba mwingine,"alisema.
Kwa mujibu wa Redondo, baada ya uongozi wa Azam kumsimamisha kwa miezi minne mapema mwaka huu kwa tuhuma za utovu wa nidhamu, alielezwa kwamba ataongezewa mkataba iwapo ataonyesha mabadiliko kitabia na uwanjani.
"Lakini siku zimekuwa zikienda bila kuelezwa lolote na uongozi wa Azam hadi mkataba wangu umemalizika ndio sababu nimeamua kujiunga na Simba,"alisema.
Mwenyekiti wa Azam, Nassor Idrissa alisema jana kuwa, hawana taarifa kuhusu kusajiliwa kwa Redondo katika klabu ya Simba na kusisitiza kuwa, anachotambua ni kwamba bado ni mchezaji wao halali.
"Kama Simba walikuwa wanamtaka mchezaji huyo, walipaswa kufuata taratibu kama walivyofanya kwa Mrisho Ngasa,"alisema mwenyekiti huyo.
Hata hivyo, habari kutoka ndani ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) zimeeleza kuwa, ni kweli mkataba kati ya Azam na Redondo umemalizika na kwamba kwa sasa ni mchezaji huru.
Mmoja wa viongozi waandamizi wa TFF amesema leo kuwa, Simba haipaswi kulaumiwa kumsajili mchezaji huyo kwa vile yupo huru na Azam wameshindwa kumuongeza mkataba mwingine.
Makamu Mwenyekiti wa Simba, Geofrey Nyange Kaburu hakuwa tayari kuzungumzia suala hilo jana kwa madai kuwa, watalitolea maelezo wakati utakapofika.

OKWI ATUA DAR, ATULIZA PRESHA SIMBA

Mshambuliaji Emmanuel Okwi ameshusha presha ya mashabiki na wanachama wa klabu ya Simba baada ya kutua nchini leo akitokea nchini Uganda.
Okwi alitua kwenye uwanja wa ndege wa Dar es Saam leo jioni kwa ndege na Shirika la Ndege la Uganda na kupokewa na baadhi ya viongozi wa Simba, akiwemo Makamu Mwenyekiti, Geofrey Nyange Kaburu.
Kuwasili kwa Okwi kulishusha presha waliyokuwa nayo wana Msimbazi baada ya kuwepo na taarifa kwamba Yanga ilikuwa ikimuhitaji mchezaji huyo kwa udi na uvumba.
Baadhi ya vyombo vya habari viliripoti juzi kuwa, mjumbe wa kamati ya utendaji ya Yanga, Abdalla Bin Kleb alikwenda Uganda mwishoni mwa wiki iliyopita kwa lengo la kumshawishi Okwi ajiunge na timu hiyo.
Okwi alirejea Uganda wiki iliyopita akitokea nchini Austria, ambako alikwenda kufanya majaribio ya kucheza soka ya kulipwa katika klabu ya Red Bull Salzburg.
Imeelezwa kuwa mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Uganda amefuzu majaribio hayo na anatarajiwa kurejea huko wakati wowote.
Akizungumzia ujio wa mchezaji huyo, Kaburu alisema Okwi anatarajiwa kuichezea Simba katika mechi ya kirafiki ya kimataifa dhidi ya Nairobi City itakayochezwa kesho kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Kaburu alitoa onyo kwa viongozi wa Yanga kuacha kumfuatafuata mchezaji huyo kwa vile bado ana mkataba na Simba na ni kinyume cha sheria kufanya naye mazungumzo kabla ya kuwasiliana na uongozi.
Makamu Mwenyekiti huyo alisema kitendo cha viongozi wa Yanga kumfuatafuata Okwi ni sawa na kutapa tapa baada ya kupigwa bao katika vita ya kumsajili beki Mbuyi Twite kutoka APR ya Rwanda.
Mechi kati ya Simba na Nairobi City ni sehemu ya tamasha la Simba, ambalo litatumika kuwatambulisha wachezaji wapya wa klabu hiyo na pia kuwapa tuzo viongozi waliotoa michango mbali mbali kwa klabu hiyo.

Monday, August 6, 2012

YANGA YAPELEKA KOMBE BUNGENI

Waziri Mkuu Mizengo Pinda akiwa na wachezaji na viongozi wa klabu ya Yanga mara baada ya timu hiyo kuyambulishwa bungeni mjini Dodoma leo. Wengine pichani ni mdhamini mkuu wa klabu hiyo, Mama Fatuma Karume, mjumbe wa bodi ya udhamini, George Mkuchika na Kocha Mkuu, Tom Saintfielt.

MUETHIOPIA ASHINDA MBIO ZA MARATHONI ZA OLIMPIKI

Mwanariadha Tiki Galana wa Ethiopia leo ameibuka mshindi wa mbio za marathoni kwa wanawake katika michezo ya Olimpiki inayoendelea mjini London, Uingereza.

Tiki alishinda mbio hizo kwa kutumia saa 2:23:07, ikiwa ni rekodi ya Olimpiki, akifuatiwa na Priscah Jeptoo wa Kenya na Tatyana Petrova wa Russia.

USAIN BOLT AWEKA REKODI MPYA YA OLIMPIKI





Mwanariadha Usain Bolt leo amevunja rekodi yake ya Olimpiki na kuweka rekodi mpya baada ya kushinda mbio za mita 100 katika Michezo ya Olimpiki inayoendelea mjini London, Uingereza.

Bolt, ambaye ni raia wa Jamaica, alishinda mbio hizo na kupata medali ya dhahabu baada ya kukimbia kwa sekunde 9.63 akiipiku rekodi yake aliyoiweka miaka minne iliyopita mjini Beijing, China kwa sekunde 0.06.

SIMBA, YANGA, AZAM ZAFANYIANA UMAFIA, MSIMBAZI WAMSAJILI REDONDO KWA MIL 30/-

Klabu za Simba, Yanga na Azam sasa zimeamua kufanyiana vurugu kwa kuchukuliana wachezaji bila kufuata na kuheshimu taratibu za usajili.


Vurugu hizo zilianza jana baada ya kuwepo na taarifa kwamba, Simba imeamua kumsajili kiungo Ramadhani Chombo Redondo kutoka Azam wakati mchezaji huyo bado ana mkataba na klabu yake.


Habari kutoka ndani ya Simba zimeeleza kuwa, wameamua kumsajili Redondo baada ya mchezaji huyo kuwaeleza kuwa, mkataba wake na Azam umemalizika.

Redondo, ambaye aliondoka Simba takribani miaka 3 iliyopita, amesaini Simba kwa ada ya millioni 30. Kiungo huyo amepewa shilingi millioni 20, na millioni 10 zilizobaki atamaliziwa baadae.

Hata hivyo, kiongozi mmoja wa Azam amesema leo kuwa, mkataba wa Redondo kuichezea Azam unatarajiwa kumalizika Juni mwakani, hivyo Simba imecheza pata potea kumsajili mchezaji huyo.

Wakati Simba ikimsajili Redondo, watani wao wa jadi Yanga walibisha hodi katika Jiji la Kampala nchini Uganda wakisaka saini ya mshambuliaji Emmanuel Okwi wa wekundu hao wa Msimbazi.

Okwi alirejea Uganda wiki iliyopita akitokea Austria alikokwenda kufanya majaribio ya kucheza soka ya kulipwa na imeelezwa kwamba ameshafuzu majaribio hayo.

Mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Uganda alirejea kwao kwa ajili ya kupatiwa matibabu ya ugonjwa wa malaria alioupata Austria.

Habari za uhakika kutoka Yanga zimeeleza kuwa, mjumbe wake wa kamati ya utendaji, Abdala bin Kleb ndiye aliyetumwa nchini humo kushughulikia usajili wa Okwi.

Yanga imeamua kumuwinda Okwi baada ya kuzidiwa kete na Simba katika usajili wa beki Mbuyi Twite kutoka APR ya Rwanda. Yanga imesema lazima ilipe kisasi Simba kwa kumnyakua Okwi.

Mbali na Yanga, kuna habari pia kuwa, Azam nayo imetinga mjini Kampala, lengo lao kuu likiwa ni kumuwinda Okwi baada ya kupata taarifa kwamba, Simba imemsajili Redondo.

Je, nini utakuwa mwisho wa vurugu hizi? Tusubiri tuone.