'
Sunday, November 12, 2017
UWANJA WA TAIFA RUKSA KUTUMIKA NOVEMBA 21
Matengenezo Uwanja Mkuu wa Taifa, Dar es Salaam, umekamilika na Mheshimiwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison George Mwakyembe, ameambiwa kuwa unaweza kuanza kutumika kuanzia Novemba 21, mwaka huu.
Kwa msingi, Waziri Dk. Mwakyembe ametoa maagizo ya kuandaliwa mchezo maalumu wikiendi ya Novemba 24, 25 au 26 kupata mchezo mmoja wa ufunguzi wa uwanja huo wenye uwezo wa kubeba takribani mashabiki walioketi 60,000 kwa wakati mmoja.
Akipokea ripoti hiyo kutoka kwa Alex – Mtaalamu kutoka Uingereza, Mheshimiwa Waziri Dk. Mwakyembe amesema: “Tuna changamoto kwenye matunzo na matengenezo. Sasa ili kukabiliana na changamoto hii, hatuna budi vijana sita waliofundishwa kazi na mtaalamu huyu, wakafanyiwa mpango wa ajira. Vijana hao wavumilie kwa sasa”
Mtaalamu huyo wa Uingereza, amesema kwamba wakati uwanja unatumika, ukarabati wa mara kwa mara utakuwa ukiendelea ili kuifanya hazina hiyo ya taifa kuendelea kuboreka kwa wakati wote.
Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Wallace Karia akizungumzia uboreshaji huo, alisema: “Ni vema wataalamu hao wakatumike pia kwenye viwanja vya mikoani. Huko wataviboresha na kuwafundisha wengine.”
DK. MWAKYEMBE ATEUA KAMATI YA AFCON U17 2019
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison George Mwakyembe leo Jumamosi Novemba 11, amezindua Kamati ya Maandalizi ya Mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa vijana wenye umri wa chini ya miaka 17 (AFCON U17) yakayofanyika Machi, 2019.
“Kama unavyofahamu, Tanzania ilipokea heshima ya kuandaa mashindano ya AFCON 2019 kwa vijana chini ya miaka 17 baada ya mashindano kama hayo kufanyika Libreville, Gabon mwezi Mei, mwaka huu.
“Ili kufanikisha maandalizi ya mashindano hayo ya Afrika nimezindua Kamati ya Maandalizi inayojumuisha viongozi wa Serikali na wadau mbalimbali wa Michezo kwa kuzingatia kanuni za Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (FIFA) na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF).
Kabla ya kuzindua kamati hiyo, Mhe. Waziri Mwakyembe alisema: “2019 tuna mtihani. Mtihani mkubwa. Na lazima tuufaulu. Tuna ugeni mkubwa ambao kamati itakuwa na kazi ya kufanya maandalizi haya kwa kazi ya kujitolea. Walioteuliwa ni watu wote wana rekodi na uzoefu mzuri kwenye masuala ya michezo.”
Uzinduzi wa kamati hiyo ulifanyika Ukumbi wa Watu Maalumu (VIP) katika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam ambako Mhe. Waziri Dk. Mwakyembe alikubali kuwa Mwenyekiti wa Kamati huku Makamu Mwenyekiti wake akiwa ni Rais wa Heshima wa TFF, Leodegar Chilla Tenga ilihali Mtendaji Mkuu atakuwa Dk. Henry Tandau.
Wajumbe ni Makamu Rais wa TFF, Michael Wambura na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda; Dk. Damas Ndumbaro ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Rufaa za Leseni za Klabu ya TFF; Dk. Francis Michael wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam – Kitivo cha Sheria; Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Mohammed Enterprises, Mohammed Dewji na Mkurugenzi Mtendaji wa Makampuni ya Said Salim Bakhressa, Abubakar Bakhressa.
Pia wamo Yussuph Singo Omari – Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo katika Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo; Ahmed Msafiri Mgoyi – Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya TFF; Khalid Abdallah – Mwenyekiti Kamati ya Maendeleo ya Vijana ya TFF kadhalika Dk. Hamis Kigwangalla – Waziri wa Maliasili na Utalii.
Wajumbe wengine ni Nassib Mmbagga – Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Temeke; Dar es Salaam; Angetile Osiah Mhariri Mwandamizi wa Magazeti ya Kampuni ya Mwananchi Communications; Dk. Allain Kijazi – Mkurugenzi Mkuu TANAPA; Dk. Dotto James – Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha na Mipango; Dk. A. P. Makakala – Kamishna Jenerali Idara ya Uhamiaji; Dk. Fredy Manongi – Mkurugenzi Mkuu Hifadhi ya Ngorongoro.
Wamo pia Lameck Nyambaya – Mjumbe Kamati ya Utendaji ya TFF; Mkurugenzi Mkuu wa PPF, William Erio; Kelvin Twissa – Ofisa Masoko Mkuu Sportpesa; Profesa Lawrence Museru – Mkurugenzi Mkuu Hospitali ya Taifa ya Muhimbili; Injinia Ladislaus Matindi – Mkurugenzi Mtendaji ATCL na Devotha Mdachi – Mkurugenzi Bodi ya Utalii Tanzania.
Pamoja na Wajumbe hao, wengine wanaoingia kwenye kwa nafasi zao katika Kamati hiyo ya maandalizi ni Rais wa TFF na Katibu Mkuu wa TFF
CHIRWA MCHEZAJI BORA WA MWEZI LIGI KUU
Mshambuliaji wa Young Africans ya Dar es Salaam, Obrey Chirwa amechaguliwa kuwa Mchezaji Bora wa Oktoba wa Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) msimu wa 2017/2018.
Chirwa raia wa Zambia alitwaa tuzo hiyo baada ya kuwashinda wenzake wawili, beki Erasto Nyoni wa Simba na mshambuliaji Ibrahim Ajibu pia wa Young Africans alioingia nao fainali katika uchambuzi uliofanywa na Kamati ya Tuzo za VPL zinazotolewa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kutokana na mapendekezo kutoka kwa makocha waliopo viwanja mbalimbali ambavyo ligi hiyo inachezwa msimu huu.
Mshambuliaji huyo alitoa mchango mkubwa kwa Young Africans mwezi huo ikipata pointi saba katika michezo mitatu iliyocheza na kupanda katika msimamo wa ligi kutoka nafasi ya sita iliyokuwepo mwezi Septemba hadi ya pili mwishoni mwa Oktoba.
Young Africans iliifunga Kagera Sugar mabao 2-1 Uwanja wa Kaitaba, Bukoba, ambapo Chirwa alifunga bao moja na kutoa pasi ya mwisho ya bao moja, pia Yanga iliifunga Stand United mabao 4-0 Uwanja wa Kambarage, Shinyanga, ambapo Chirwa alifunga bao moja na kutoa pasi ya mwisho ya bao moja.
Kiwango cha mchezaji huyo kilionekana pia katika mchezo wa watani wa jadi Yanga na Simba uliofanyika Oktoba 28, 2017 Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam na kumalizika kwa sare ya bao 1-1. Bao la Yanga lilifungwa na Chirwa, hivyo kwa mwezi huo alifanikiwa kuwa na kiwango cha juu katika kila mchezo ikiwa ni pamoja na kufunga.
Kwa upande wa Erasto naye alitoa mchango mkubwa kwa Simba uliowezesha timu hiyo kupata pointi nane katika michezo minne iliyocheza, akitoa pasi za mwisho za mabao nne, ambapo Simba ilishinda michezo miwili na kutoka sare miwili, huku Ajibu akitoa mchango mkubwa kwa Yanga ikiwa ni pamoja na kufunga mabao matatu na kutoa pasi ya mwisho ya bao moja.
Wachezaji wengine ambao tayari wameshinda Tuzo ya Mchezaji Bora wa mwezi wa VPL msimu huu ni mshambuliaji wa Simba, Emmanuel Okwi (Agosti), beki wa Singida United, Shafiq Batambuze (Septemba).
Kampuni ya Vodacom, ambao ndiyo wadhamini wa ligi hiyo ina utaratibu wa kuwazadiwa wachezaji bora wa kila mwezi, huku pia mwisho wa msimu kukiwa na tuzo mbalimbali zinazohusu ligi hiyo, ambapo msimu wa mwaka 2016/2017 kulikuwa tuzo 16 zilitolewa kwa washindi wa kada mbalimbali. Chirwa atazawadiwa Sh milioni moja kwa kuibuka Mchezaji Bora wa Oktoba.
TFF YAENDESHA MAFUNZO VYUONI SOKA YA UFUKWENI
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) litatoa mafunzo ya soka la ufukweni (Beach Soccer) kwa vyuo mbalimbali hapa nchini vilivyothibitisha kushiriki Ligi Maalumu ya soka la Ufukweni itakayoanza Novemba 18, 2017.
Kwa upande wa mafunzo ni kwamba yatafanyia siku tano kabla ya kuanza kwa ligi hiyo ambako itakuwa ni Novemba 13, mwaka hu. TFF imepanga kutoa mafunzo hayo kwa vyuo hivyo ili wauelewe zaidi mchezo huo pamoja na sheria zake.
Tumepeleka mchezo huo kwenye vyuo ili kutoa hamasa ya soka la ufukweni kuenea zaidi na kuweka hazina ya wachezaji wa timu ya taifa.
Mpaka sasa vyuo 14 tayari vimethibitisha kimaandishi kushiriki kwenye mafunzo hayo.
Vyuo vilivyothibitisha kushiriki ni Chuo cha Ardhi, Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE), Chuo Cha Ufundi (DIT), Chuo cha Usafirishaji (NIT), Chuo cha Elimu ya Tiba cha Kahiruki, Chuo cha Elimu ya Biashara cha Lisbon, Chuo cha Silva , Chuo UAUT, TIA, El-Maktoum collage Engineering, Magogoni, Chuo cha uandishi wa habari DSJ na TSJ.
Mafunzo hayo yatatanguliwa na tukio la kukutana na viongozi wa vyuo shiriki hapo Novemba 10, 2017.
Wakati huo huo kozi ya waamuzi wa Soka la Soka la Ufukweni imeanza leo Novemba 7, 2017 katika Makao Makuu ya TFF Karume, Dar es Salaam ambayo yanatarajiwa kumalizika Novemba 12, 2017.
TFF YASIMAMISHA MCHEZO WA FORODHANI v AMBASSODOR
Wakati mchezo wa TFF ikisimamisha mchezo wa Azam Sports Federation Cup kati ya Forodhani FC ya Mara na Ambassodor ya Kahama, Mchezo wa Bulyanhulu na Area C, sasa utafanyika kesho Jumatano Novemba 8, mwaka huu kwenye Uwanja wa Kambarage mkoani Shinyanga.
Mchezo kati ya Forodhani FC ya Mara na Ambassodor ya Kahama, umesimamishwa kusubiri uamuzi wa Kamati ya Mashindano baada ya Baruti ambayo imelete malalamiko kuhusu nafasi yake.
Mbali ya mchezo kati ya Bulyanhulu na Area C, mechi nyingine za kesho Jumatano, Novemba 8 zitakuwa ni kati ya Cosmopolitan na Abajalo kwenye Uwanja wa Mabatini mkoani Pwani wakati makumba Rangers watacheza na Green Warriors kwenye Uwanja wa Bandari, Dar es Salaam.
AFC ya Arusha itaikaribisha Nyanza FC kwenye Uwanja wa Ushirika; Boma Fc na African Sports watacheza kwenye Uwanja wa Ushirika; huku Motochini ikicheza na Ihefu wakati Stand Misuna watacheza na Madini ilihali Burkina FC itaialika Mbinga United kadhalika Mkamba Rangers itacheza na Makambako FC kwenye Uwanja wa Sabasaba.
35 WATEULIWA KUUNDA KILIMANJARO WARRIORS
Benchi la Ufundi la timu za taifa za vijana, limeita wachezaji 35 kwa ajili ya kambi yenye lengo la mchujo kutafuta kikosi imara cha timu ya taifa ya vijana wenye umri wa chini ya miaka 23 maarufu kwa jina la Kilimanjaro Warriors.
Kocha Msaidizi wa timu hizo, Oscar Mirambo alitangaza majina hayo leo Novemba 03, mwaka huu huku amesema: “Tunataka vijana wasiozidi 25 kwenye kikosi. Tutawapata kwenye kambi hii ya siku 10 inayoanza tarehe 5, mwezi huu wa 11.”
Kocha Msaidizi wa timu hizo, Oscar Mirambo alitangaza majina hayo leo Novemba 03, mwaka huu huku akisema: “Tunataka vijana wasiozidi 25 kwenye kikosi. Tutawapata kwenye kambi hii ya siku 10 inayoanza tarehe 5, mwezi huu wa 11.”
Wachezaji aliowaita ni makipa Metacha Mnata (Azam FC), Joseph Ilunda (JKT Ruvu), Liza Mwafwea (Tanzania Prisons).
Wengine ni Cleotas Sospter (Yanga); Idrissa Mohammed, Bakari Kijuji (Yanga), Joseph Prosper (Azam), Masoud Abdallah (Azam), William (Ruvu Shooting), Yussuph Mhilu (Yanga), Adam Salamba (Stand United), Omary Mponda (Ndanda) na Stanley Angeso (Stand United).
Pia wamo Eliud Ambokire (Mbeya City), Emmanuel Kakuti (Mbeya City), Medson Mwakatunde (Mbeya City), Daruweshi Shaliboko (Ashanti Unted), Abbas Kapombe (Azam/Ndanda), Ismail Aidan (Mtibwa Sugar), Salum Kihimbwa (Mtibwa Sugar), Hassan Mganga (Mtibwa Sugar) na Award Salum (Njombe Mji).
Wengine Awesu Ally (Mwadui), Salum Chuku (Singida United), Yahya Zayd (Azam), Emmanuel Martin (Yanga), Geofrey Mwashiuya (Yanga), Ayoub Masoud (Ndanda), Baraka Majogoro (Ndanda), Mohammed Habib (Miembeni), Yussuf Mlipili (Simba), Agathon Mapunda (Njombe Mji), Faisal Abdallah (JKU) na Yussuph Kagoma (Singida United).
TFF YATOA UFAFANUZI WA MALIPO MICHUANO YA ASFC
Wakati Michuano ya Kombe la Shirikisho la Azam yaani Azam Sports Federation Cup (ASFC), ikiwa imeanza jana Novemba 02, 2017 na kuendelea leo Ijumaa na kesho Jumamosi, Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), limetoa ufafanuzi wa malipo kwa hatua hii ya awali.
Kwa hatua za awali na hatua ya kwanza, TFF imetoa ufafanuzi kwamba kwa timu mwenyeji inalipwa shilingi lakini saba na elfu hamsini (Sh. 750,000) wakati timu ngeni inayosafiri hadi kituo cha mchezo inalipwa shilingi milioni mbili na lakini tano (Sh 2.5m). Fedha zote hizo, zinalipwa katika akaunti ya kila timu.
Lakini TFF imetoa ufafanuzi kwamba, kwa timu ambazo zinatoka katika kituo kimoja (mkoa mmoja) zote zitalipwa Sh 750,000 kama gharama sawa licha ya moja ya timu itakuwa mgeni na nyingine mwenyeji.
TFF imetoa ufafanuzi huo, baada ya kuibuka mjadala wa dhana ya uenyeji na ugeni licha ya kwamba timu shindani zinatoka kituo kimoja (mkoa mmoja). Timu hizo zielewe kwamba zitalipwa gharama inayofanana katika maandalizi.
Fedha zitaongezeka kwa timu ambayo inasonga mbele baada ya hatua ya awali na hatua ya kwanza.
Katika hatua nyingine, TFF inasubiri taarifa za Kamishna na Mwamuzi kuhusu vurugu zinazodaiwa kutokea huko Simiyu katika mchezo kati ya Usalama na Sahare All Stars uliofanyika Novemba 2, mwaka huu.
TFF imepanga mchezo kati ya Kisarawe United ya Pwani na Silabu ya Mtwara ufanyike kesho Novemba 4, mwkaa huu baada ya kuahirishwa Novemba 2, mwaka huu baada ya wachezaji wake kupata ajali maeneo ya Mchinga mkoani Lindi wakiwa safarini kwenda Pwani. Mechi inayofanyika leo Novemba 3, mwaka huu kati ya Buseresere ya Geita itayocheza na Isako ya Songwe.
Baada ya mechi hizo,itakuja Raundi ya Kwanza ya ASFC ambayo itachezwa ama Novemba 7, 8 au 9 ambako TFF imepanga kesho kutuma fedha zote za maandalizi ya timu husika ili kusiwe na kisingizio chochote cha kujiandaa.
Kaimu Katibu Mkuu wa TFF, Kidao Wilfred ameagiza Idara ya Fedha na Utawala ya TFF kulipa fedha kwa timu hizo haraka, lakini kwenye akaunti ya timu husika badala ya mwakilishi ye yote au kiongozi.
Timu ambayo haijafungua akaunti watakuta fedha hizo kwenye Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa (FA), lakini TFF ingependa kusisitiza kwa wadau hao kufufua akaunti au kufungua akaunti haraka.
Katika raundi hiyo ya kwanza Mashujaa ya Kigoma itacheza na Mshindi kati ya Buseresere ya Geita na Isako ya Songwe; wakati mechi nyingine zitakuwa Msange ya Tabora itacheza na Milambo pia ya Tabora ilihali Bulyanhulu ya Shinyanga itacheza na Area C ya Dodoma.
Kwa mujibu wa droo, Mji Mkuu FC ya Dodoma imeangukia kwa Nyundo ya Kigoma wakati Baruti FC ya Mara itacheza na Ambassodor ya Kahama, Shinyanga huku Eleven Stars ya Kagera ikipangwa kucheza na Ndovu ya Mwanza.
Changanyikeni ya Dar es Salaam itacheza na Reha FC pia ya Dar es Salaam wakati Mshindi kati ya Kisarawe United na Silabu ya Mtwara atacheza na Kariakoo ya Lindi huku Cosmopolitan ikicheza na Ajabalo wakati Makumba FC itapambana na Green Warriors ya Kinondoni wakati Namungo FC ya Lindi itachuana na Villa Squad ya Dar es Salaam huku Dar City ikicheza na Majimaji Rangers ua Nachingwea.
Michezo mingine ya hatua ya kwanza itakutanisha timu za Shupavu FC ya Morogoro na Sabasaba pia ya mjini humo wakati Motochini FC ya Katavi dhidi ya Ihefu FC ya Mbeya wakati The Mighty Elephant ya itacheza na Makanyagio ya Rukwa.
Timu ya Burkina FC ya Morogoro itacheza na Mbinga United ya Ruvuma wakati Makambako Heroes ya Njombe itacheza na Mkamba Rangers ya Morogoro wakati Real Moja Moja itapambana na African Wonderers – zote za Iringa. Boma FC ya Mbeya itacheza na African Sports ya Tanga.
Mechi nyingine za hatua hiyo itakuwa ni kati ya Pepsi ya Arusha ambayo itacheza na Kilimanjaro Heroes ya Kilimanjaro; huku Stand Misuna ya Singida itacheza na Madini FC ya Arusha ilihali AFC ya Arusha itacheza na Nyanza ya Manyara wakati New Generation itacheza na Mshindi kati ya Usamala FC na Sahale ya Tanga. Bodaboda FC itacheza na Kitayose ya Kilimanjaro.
Michuano hiyo ambayo Bingwa Mtetezi ni Simba SC ya Dar es Salaam, inashirikisha timu 91 msimu huu kwa mchanganuo wa timu 16 za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL); 24 za Ligi Daraja la Kwanza (FDL); 24 za Ligi Daraja la Pili (SDL) na 27 za Ligi ya Mabingwa wa Mkoa (RCL).
LIGI YA WANAWAKE KUANZA NOVEMBA 26
Ratiba ya Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania Bara inayotarajiwa kuanza Novemba 26, 2017, katika vituo viwili vya majiji ya Dar es Salaam na Arusha, imetangazwa.
Katika ratiba hiyo, Kundi A limepangwa kuwa katika Kituo cha Dar es Salaam ambako timu zake Simba Queens ya jijini Dar es Salaam iliyopanda daraja msimu huu, Mburahati Queens, JKT Queens, Evergreen zote za Dar es Salaam pamoja na timu za Fair Play ya Tanga na mabingwa watetezi – Mlandizi Queens.
Kundi B litakuwa na timu za Alliance ya Mwanza ambayo imepanda kutoka kituo cha Dodoma. Timu nyingine ni Marsh Academy pia ya Mwanza; Panama ya Iringa; Kigoma Sisterz ya Kigoma, Baobab ya Dodoma na Majengo Queens ya Singida.
Fungua dimba kwa Kituo cha Dar es Salaam, mabingwa watetezi wa taji hilo, Mlandizi Queens itacheza na JKT Queens katika mchezo utakaofanyika Uwanja wa Karume, Ilala jijini Dar es Salaam.
Katika kundi hilo la A, mechi nyingine zitakuwa siku inayofuata Novemba 27, mwaka huu kati ya Mburahati Queens na Evergreen saaa 8.00 mchana wakati Fair Play ya Tanga itacheza na Simba Queens saa 10.00 jioni.
Jijini Arusha, Panama ya Iringa itafungua dimba na Alliance Queens ya Mwanza huku siku ya pili Novemba 27, mwaka huu Baobab Queens itacheza na Marsh Academy saa 8.00 mchana wakati saa 10.00 jioni Majengo Queens itapambana na Sisterz ya Kigoma.
Timu hizo zitapambana katika vituo hadi Desemba 12, mwaka huu kabla ya kutoa jumla ya timu nane kwa maana ya nne kutoka kila kundi. Timu hizo nane zitapambana katika hatua ya Nane Bora ya Ligi hiyo kuelekea ubingwa. Ligi inatarajiwa kumalizika Machi 28, mwakani.
TANZANIA BARA YATHIBITISHA KUSHIRIKI CHALENJI ZOTE
Baada ya kupita miaka miwili bila kuchezwa kwa mashindano ya kuwania Kombe la Chalenji kwa nchi za Afrika Mashariki, michuano hiyo imerejea tena msimu huu na Tanzania imethibitisha kushiriki.
Nchi wanachama Tanzania Bara, Zanzibar, Uganda, Kenya, Burundi, Rwanda, Somalia, Sudan, Sudan Kusini, Eritrea na Ethiopia.
Kaimu Katibu Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Kidao Wilfred amethibitisha kikosi cha kwanza cha ‘Taifa Stars’ kushiriki na matarajio ya kufanya vema michuano hiyo itakayofanyika kuanzia Novemba 25, 2017 hadi Desemba 9, mwaka huu.
Kidao amesema kwamba uteuzi wa timu za kwanza kwa kila nchi mwanachama wa Baraza la Mpira wa Miguu la Afrika Mashariki ni makubaliano ya viongozi wa CECAFA waliokutana kwa pamoja huko Sudan, Septemba, mwaka huu.
Kutokana na makubaliano hayo ya kuita timu za kwanza, michuano hiyo itaathiri kidogot ratiba ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) kwa kuwa wachezaji wengi wanaounda kikosi hicho, wanatoka timu za VPL.
Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi (TPLB), Boniface Wambura amesema: “Tutakaa kama kamati na kuangalia siku ya Jumatano na Alhamisi baada ya michuano hiyo na kupanga ratiba ya mechi ambazo zitapanguliwa wakati wa michuano ya Chalenji.”
Mbali ya michuano hiyo, Tanzania imethibitisha kushiriki michuano ya Chalenji ya vijana wenye umri wa chini ya miaka 17 itakayofanyika Bujumbura nchini Burundi kuanzia Desemba 12, 2017 hadi Desemba 22, mwaka huu.
Kadhalika, Tanzania imethibitisha kushiriki michuano ya Chalenji kwa wanawake ikienda kutetea taji katika michuano itakayofanyika Rwanda mwezi Desemba, mwaka huu. Tarehe rasmi itatajwa baadaye.
CECAFA imeamua kurejesha hadhi yake kwani mara baada ya michuano ya Chalenji ya vijana huko Burundi, mwakani itakuwa ni zamu ya Tanzania ambako michuano hiyo inatarajiwa kuanza Agosti 11, 2018 hadi Agosti 25, mwakani.
Wakati huo huo Kidao amethibitisha Tanzania kuwa wenyeji wa mashindano ya Vijana ya Chalenji ya CECAFA/CAF kwa vijana chini ya miaka 17 mwakani na mashindano hayo yatatumika kama sehemu ya kufanya maandalizi Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa vijana wenye umri wa chini ya miaka 17 (AFCON – U17).
Michuano ya mwakani ina baraka za Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kwa sababu shirikisho hilo linataka kutumia michuano hiyo ya vijana ya Kanda mbalimbali za Afrika kupata timu saba katika michuano AFCON – U17 ya mwaka 2019.
Kanda hizo ni CECAFA (Afrika Mashariki), COSAFA (Nchi za Kusini mwa Afrika), WAFU – UFOA (Afrika Magharibi); UNAF (Afrika Kaskazini) na UNIFFAC (Afrika ya Kati).
Subscribe to:
Posts (Atom)