KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, November 2, 2011

Tusker kudhamini Chalenji kwa mil. 823/-



Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), Nicholas Musonye (kulia), akipokea mfano wa hundi yenye thamani ya sh. milioni 823 kutoka kwa Mkurugenzi wa Kampuni ya Bia ya Serengeti (SBL), Richard Wells katika hafla iliyofanyika kwenye hoteli ya New Africa mjini Dar es salaam jana. Katikati ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya SBL, Jaji Mark Bomani.(Na mpiga picha wetu).


KAMPUNI ya Bia ya Serengeti (SBL) imetangaza kudhamini tena michuano ya mwaka huu ya Kombe la Chalenji, inayotarajiwa kufanyika mjini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mkuu wa SBL, Richard Wells alisema mjini Dar es Salaam jana kuwa, wamepanga kutumia sh. milioni 823 kwa ajili ya kudhamini michuano hiyo.
SBL ilitangaza udhamini huo kati yake na Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) kwenye hoteli ya New Africa mjini Dar es Salaam.
Richard alisema fedha hizo zitatumika kugharamia tiketi za ndege kwa msafara wote wa CECAFA, malazi, usafiri wa ndani, fedha za washindi na gharama zinginezo.
Mkurugenzi huyo alisema pia kuwa, fedha hizo zitatumika kuratibu waandishi wa habari na mahitaji mengine ya utawala.
Mashindano hayo, ambayo huendaliwa kila mwaka, yamepangwa kuanza Novemba 25 hadi Desemba 10 mwaka huu mjini Dar es Salaam.
Richard alisema udhamini huo ni mojawapo ya malengo yaliyowekwa na kampuni hiyo, yakiwa na nia ya kukuza na kuendeleza mchezo huo nchini.
Aliyataja malengo mengine ya SBL kuwa ni kukuza na kuinua vipaji vilivyopo mashariki na magharibi mwa Afrika.
“Udhamani huu unadhihirisha msimamo wa SBL kuwa kampuni inayowajibika kwa jamii inayoizunguka nchini na nchi jirani za kiafrika,”alisema.
“Tunajivunia kuwa wadhamini wakuu wa CECAFA na tunashukuru kupewa heshima hii na CECAFA pamoja na TFF,”aliongeza.
Mwenyekiti wa CECAFA, Leodegar Tenga aliishukuru SBL kwa udhamini huo na kuongeza kuwa, wana matumaini makubwa kwamba mashindano hayo yatafana.
Tenga alisema wamepanga kupeleka baadhi ya mechi za mashindano hayo mkoani Mwanza ili kuwapa burudani wakazi wa mikoa ya kanda ya Ziwa.
Hii ni mara ya pili mfululizo kwa SBL kudhamini mashindano hayo. Mwaka jana, ilitumia kiasi cha shilingi milioni 675, ambapo timu ya Tanzania Bara, ‘Kilimanjaro Stars’ iliiubuka mshindi.

No comments:

Post a Comment