KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, November 2, 2011

Hatuna papara ya kurekodi nyimbo mpya-Omar Tego


KIONGOZI wa kikundi cha taarab cha Coast Modern cha mjini Dar es salaam, Omar Tego amesema hawana papara ya kurekodi nyimbo mpya kila mara kwa sababu wanafanyakazi zao kiuhakika.
Akizungumza mjini Dar es Salaam wiki hii, Tego alisema utaratibu wa kikundi chake ni kurekodi albamu moja kila mwaka ili kuwapa mashabiki burudani iliyokamilika.
Tego alisema nyimbo nyingi za taarab zimekuwa zikiisha utamu mapema kutokana na watunzi na waimbaji wake kurekodi kila baada ya muda mfupi.
“Wasanii wengi wa taarab wanapenda kuharakisha kurekodi nyimbo zao ndio sababu zinachuja mapema. Wimbo haujamaliza miezi minne, unatolewa mwingine. Huwezi kurekodi nyimbo nzuri katika mazingira haya,”alisema.
Tego, ambaye amekuwa akirekodi baadhi ya nyimbo zake kwa ushirikiano na dada yake, Maua Tego alisema, albamu yake ya Damu Nzito bado ipo kwenye chati kwa sababu vibao vilivyomo ndani yake viliandaliwa kiuhakika.
Alisema licha ya albamu hiyo kurekodiwa mwaka mmoja uliopita, hadi sasa mashabiki bado wanazipenda nyimbo zake kwa sababu alitumia akili nyingi katika kuzitengeneza.
Alisema kwa sasa, kikundi chake kinajiandaa kurekodi albamu mpya, itakayojulikana kwa jina la Mapenzi.Com, ambayo inatarajiwa kuingia sokoni mwishoni mwa mwaka huu.
“Unapotaka kutoa kitu kipya, unatakiwa uhakikishe kwamba kinakuwa moto kwa sababu ushindani hivi sasa ni mkubwa kutokana na vikundi vya taarab kuwa vingi,”alisema.
Tego alisema pia kuwa, kikundi chake hupendelea zaidi kufanya maonyesho kwenye kumbi za uswahilini na mikoani kwa lengo la kuwapa burudani mashabiki wengi zaidi.
Kwa mujibu wa Tego, kikundi hicho kilitarajiwa kuondoka Dar es Salaam mwanzoni mwa mwezi huu kwenda Lindi kwa ziara ndefu ya kimuziki.
Alisema ziara hiyo inatarajiwa kuwafikisha katika miji ya Newala, Masasi, Luangwa na Kilwa. Alisema wakati wa sikukuu ya Idd El Hajj, kikundi hicho kitafanya onyesho Kilwa.
Amewataka wasanii wa taarab nchini kuacha tabia ya kurekodi nyimbo zao kwa kulipua, badala yake washushe tungo za uhakika ili waweze kuwapa mashabiki wao burudani iliyokamilika.
Naye Maua alisema lengo lake ni kuendelea kuimba nyimbo zinazofikisha ujumbe kwa jamii, ndio sababu nyimbo zake za Gubu la wifi na Kukupenda isiwe tabu bado zipo kwenye chati.
“Napenda kuwaambia mashabiki wangu kwamba sijalala, nitaendelea kuwepo na kazi zangu ni za uhakika, sikurupuki kutoa nyimbo mpya,”alisema.

No comments:

Post a Comment