KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, November 30, 2011

Masikini Mercy Johnson





LAGOS, Nigeria
NI vigumu kuamini, lakini habari za uhakika kutoka vyanzo mbalimbali ndivyo zinavyosema. Kwamba jicho la kulia la mwigizaji nyota wa filamu nchini Nigeria, Mercy Johnson limeharibika.
Kwa mujibu wa vyanzo hivyo vya habari, Mercy aliumia jicho lake hilo hivi karibuni wakati akiwa kwenye eneo la kuchezea filamu huko Asaba katika Jimbo la Delta.
Vyanzo hivyo vimesema mrembo huyo alipatwa na maumivu hayo baada ya kutokea ugomvi kati yake na mwigizaji mwenzake, ambaye jina lake halikuweza kufahamika mara moja.
Taarifa zinasema familia ya mcheza filamu huyo, aliyefunga ndoa hivi karibuni, imekuwa ikihaha ili kuhakikisha anafanyiwa operesheni ya kurekebisha jicho lake mjini London, Uingereza.
Kuumia kwa Mercy kumeelezwa kuwa, kumemtia majonzi makubwa kiasi cha kumfanya asiwe na raha huku akiwaza nini la kufanya ili aweze kurejea katika hali ya kawaida.
Gazeti la Sun la Nigeria lilijaribu kuwasiliana na Mercy mara kadhaa ili kupata ukweli wa tukio hilo, lakini simu yake imekuwa ikiita kwa muda mrefu bila kupokelewa.
Filamu aliyokuwa akicheza Mercy imeandaliwa na Kampuni ya Magic Movies, imeandikwa na Micheal Jaja na kuongozwa na Jaja.

Hatimaye Aki afunga ndoa


LAGOS, Nigeria
HATIMAYE msanii nyota wa filamu wa Nigeria, Chinedu Ikedieze amefunga ndoa na mchumba wake wa muda mrefu, Nneoma Hope Nwajah.
Harusi hiyo ya kimila ilifanyika Jumamosi iliyopita kwenye kanisa katoliki la St. Theresa lililopo Obolo, Isiala Mbano, Jimbo la Imo.
Miongoni mwa watu maarufu waliohudhuria harusi hiyo ni pamoja na wacheza filamu nyota nchini humo, Segun Arinze, Uche Jombo, Oby Edozien na Ejike Asiegbu.
Watu wengine maarufu waliohudhuria harusi hiyo ni Gavana wa jimbo la Abia na mkewe pamoja na swahiba mkubwa wa Aki, Osita Iheme ‘Ukwa’.
Katika harusi hiyo, Aki alikuwa kivutio kikubwa kwa wageni waalikwa kutokana na kuvaa kofia na miwani myeusi pamoja na kushika fimbo kubwa ya kutembelea.
Maharusi hao wawili walioanza kuchumbiana miaka mitatu iliyopita, walitunzwa fedha nyingi na wageni waalikwa na muda wote walionekana kujawa na furaha kubwa.
Sherehe nyingine ya harusi hiyo imepangwa kufanyika Desemba 10 mwaka huu mjini Lagos.

Msondo, Sikinde uso kwa uso Krismas


BENDI kongwe za muziki wa dansi nchini, Msondo Ngoma na Mlimani Park Orchestra zimepanga kufanya onyesho la pamoja Desemba 25 mwaka huu kwenye viwanja vya klabu ya Sigara, Chang’ombe, Dar es Salaam.
Wakizungumza na Burudani kwa nyakati tofauti mjini Dar es Salaam juzi, viongozi wa bendi hizo walisema, onyesho hilo litadhaminiwa na Kampuni ya Konyagi.
Meneja wa Msondo Ngoma, Saidi Kibiriti alisema lengo la onyesho hilo ni kuimarisha umoja na ushirikiano kati ya wanamuziki wa bendi hizo kongwe nchini.
Kibiriti alisema bendi zote mbili zimekubaliana kuporomosha nyimbo mchanganyiko, zikiwemo za miaka 50 iliyopita na za sasa kwa lengo la kuwapa mashabiki burudani yenye vionjo na ladha tofauti.
“Hili si pambano la kutafuta nani mkali kati yetu, tunawaomba mashabiki waelewe hivyo, ni onyesho na kujenga na kuimarisha mshikamano kati ya wanamuziki wetu,”alisema.
Kwa upande wake, Katibu wa Mlimani Park, Hamisi Milambo alisema, maandalizi kwa ajili ya onyesho hilo yameshaanza na yanaendelea vizuri.
Milambo alisisitiza kuwa, lengo la bendi hizo si kupambana ili kumtafuta nani mkali kati yao, bali ni kuwapa mashabiki burudani kabambe ya muziki.
Hii itakuwa ni mara ya pili kwa Msondo na Mlimani Park kufanya onyesho la pamoja mwaka huu. Zilikutana kwa mara ya kwanza Juni mwaka huu katika onyesho lililofanyika kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee, Dar es Salaam.
Onyesho hilo lilifanyika siku chache baada ya mwimbaji machachari nchini, Shabani Dede kuihama Mlimani Park na kujiunga na Msondo Ngoma.

JB: Tumeweza, tunasonga mbele



MSANII mkongwe wa fani ya filamu nchini, Jacob Steven amesema, maendeleo ya fani hiyo kwa sasa ni makubwa ikilinganishwa na miaka iliyopita.
Akihojiwa na kituo cha redio cha Clouds FM cha mjini Dar es Salaam wiki hii, Jacob alisema wakati fani hiyo ilipoanza, wasanii walikuwa wachache na walishindwa kunufaika nayo.
Msanii huyo, ambaye ni maarufu zaidi kwa jina la JB alisema, kadri miaka inavyosonga mbele, wasanii wamekuwa wakiongezeka na pia yamejitokeza mabadiliko makubwa katika utayarishaji wa filamu.
JB alisema hali hiyo imekuwa ikiwafanya wasanii nao waanze kunufaika na vipaji vyao kutokana na soko la filamu kuwa kubwa.
“Maendeleo wakati ule yalikuwa madogo kwa sababu ilikuwa ndio kwanza tunaanza. Wasanii wengi wa wakati ule hivi sasa hawapo,”alisema.
Aliwataja wasanii waanzilishi wa fani hiyo, iliyoanza kujipatia umaarufu miaka ya 1900 na ambao kwa sasa wamejiweka kando kuwa ni Bishanga, Aisha, Waridi na Mama Bishanga.
“Nina hakika katika miaka michache ijayo, ushindani katika fani ya filamu utakuwa mkubwa zaidi kwa sababu wasanii watazidi kuongezeka,”alisema.
Alisema katika miaka ya hivi karibuni, kumejitokeza wasanii wengi wa mitindo ya mavazi, urembo na wasomi wa kada mbalimbali, ambao wamezidi kuzinadhifisha filamu za kibongo na kuzifanya ziwe na mwonekano wa kimataifa.
“Kwa sasa tunao wasomi kutoka vyuo vikuu mbalimbali pamoja na Taasisi ya sanaa Bagamoyo. Kujitokeza kwao kwa wingi kunadhihirisha wazi kuwa, fani ya filamu hivi sasa inakubalika,”alisema.
Mbali na ongezeko la wasanii, JB alisema teknolojia inayotumika sasa katika kutengeneza filamu nayo ni ya juu zaidi na hivyo kuufanya ushindani uwe mkali.

Twenty Percent, Man Walter sasa ni chui na paka




HUWEZI kuamini. Pia unaweza kuita ni mchezo wa kuigiza ama filamu ya mauzauza. Ni kwa sababu kilichotokea, hakuna aliyekitarajia.
Ni kwamba mshindi wa tuzo tano za muziki za Kilimanjaro mwaka jana, Abbas Kinzasa 'Twenty Percent' na prodyuza wake, John Shariza, maarufu kwa jina la Man Walter hivi sasa hawaelewani. Ni sawa na chui na paka.
Unajua kisa ni nini?
Hakuna kingine zaidi ya mkwanja. Ndivyo inavyokuwa miaka yote utakaposikia msanii na prodyuza wake wamekorofishana. Sababu kubwa huwa ni kudhulumiana malipo.
Hivyo ndivyo ilivyotokea kwa Twenty Percent na Man Walter, ambao hivi karibuni walitoleana lugha kali, kila mmoja akimshutumu mwenzake kwamba ndiye chanzo cha kutokuelewana kwao.
Akihojiwa na kituo cha Radio One Stereo mwishoni mwa wiki iliyopita, Man Walter, ambaye ndiye mmiliki wa studio ya Combination Sound alisema, chanzo cha kutokuelewana huko ni ugomvi uliotokea kati yao kabla ya kuanza kwa onyesho lililofanyika mjini Morogoro.
Prodyuza huyo alisema, aliamua kuandaa onyesho hilo kwa ajili ya kumpongeza Twenty Percent na pia kuwashukuru mashabiki kwa kumpigia kura nyingi.
Alisema kabla ya kuanza kwa onyesho hilo, alifuatwa na Twenty Percent na kumtaka ampe malipo yake mapema. Alisema alipompa kwa mara ya kwanza, msanii huyo alikataa kupokea kiasi cha pesa alicholipwa kwa madai kuwa ni kidogo.
“Akaomba akabidhiwe malipo hayo mbele ya polisi, pia akakataa kupokea. Baadaye nikwamwita Afande Sele na kumkabidhi malipo hayo mbele yake, ndipo akakubali kupokea,”alisema Man Walter bila ya kufafanua kiwango hicho cha pesa.
Kwa mujibu wa Man Walter, licha ya kupokea malipo hayo, msanii huyo alitoa lugha kali kwake, akimshutumu na kumwita tapeli, aliyetumia kipaji chake kujinufaisha kimaisha.
Aliongeza kuwa, msanii huyo pia aliapa mbele za watu kwamba, hatorekodi tena nyimbo zake kwenye studio yake na wala asitarajie kufanyanaye kazi zingine.
“Kwa kweli maneno aliyoyatamka kwangu sikuyatarajia kabisa. Hata mashabiki waliofika ukumbini kushuhudia onyesho hilo walilalamika sana na kutoka nje,”alisema Man Walter.
Prodyuza huyo alisema, kilichomsikitisha zaidi ni kumsikia msanii huyo akiapa kwamba, atamfanyia kitu mbaya. Alisema alichokifanya si haki hata kidogo.
“Mimi ndiye niliyemtoa na kumpatia umaarufu kimuziki. Kutokana na makubaliano tuliyokuwa nayo, hakupaswa kurekodi nyimbo mpya kwa prodyuza mwingine. Alipaswa kunipa angalau nyimbo mbili,”alilalamika.
Kwa upande wake, Twenty Percent alisema si kweli kwamba haelewani na Man Walter, isipokuwa amerekodi nyimbo zake mpya kwenye studio zingine kwa lengo la kuzipa ladha tofauti.
“Sina ugomvi wowote na Man Walter, isipokuwa watu walipotuona tukibadilishana maneno makali, wakachukulia kwamba ugomvi wetu ni mkubwa,”alisema.
Msanii huyo alisema yeye na Man Walter ni marafiki wakubwa, iwe kikazi ama wanapokuwa mtaani wanapoishi na amekuwa akimchukulia kama kaka yake.
Alisema sababu kubwa iliyomfanya aamue kurekodi nyimbo zake mpya kwenye studio zingine ni kutokana na Man Walter kutingwa na kazi nyingi.
“Haya ni mabadiliko ya kawaida kimuziki. Nilichokifanya ni kubadili ladha ya muziki wangu ili nitoke kivingine badala ya vile nilivyozoeleka,”alisema.
“Man Walter ni kama kaka yangu. Tunapokuwa mtaani, yeye ndiye anayenipa mawazo mbalimbali kuhusu maisha, hatuna ugomvi, tupo pamoja,”alisisitiza.

MAVITUZ YA TWANGA PEPETA LONDON





MWIMBAJI wa bendi ya muziki wa dansi ya Twanga Pepeta International, Hamisi Amigolas akicheza huku akiwa amembeba mcheza shoo wa bendi hiyo, Tina Mjapan wakati wa onyesho lililofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita mjini London, Uingereza.Juu ni mcheza shoo huyo akifanya mavituz. (Picha kwa hisani ya blogu ya Freddy Macha)

Chondechonde mwacheni Vengu-Seki


UONGOZI wa kundi la Orijino Komedi umevitaka vyombo vya habari nchini kuacha kumfuatilia msanii wake, Joseph Shamba ‘Vengu’ aliyelazwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Dar es Salaam.
Mbali na kuviasa vyombo vya habari, kundi hilo pia limewaomba mashabiki wake kuacha kumsumbua msanii hiyo kwa kulazimisha kuingia kwenye chumba alimolazwa hospitalini hapo.
Kiongozi wa kundi hilo, Sekione David alisema mjini Dar es Salaam juzi kuwa, madaktari wanaomtibu Vengu wameshauri asibughudhiwe na watu.
“Madaktari na familia yake hawataki jambo hili liwe wazi kwa kila mtu, ugonjwa ni siri ya mgonjwa na madaktari kwa manufaa ya hospitali,”alisema Sekione, ambaye ni maarufu zaidi kwa jina la Seki.
Kiongozi huyo wa Orijino Komedi alisema, binafsi haruhusiwi kutoa taarifa zinazomhusu msanii huyo kutokana na kuzuiwa kufanya hivyo na madaktari.
“Hizi ni taratibu walizoweka madaktari na ndugu zake, hatuwezi kwenda kinyume ya hapo,”alisisitiza Seki.
Vengu amelazwa Muhimbili kwa zaidi ya miezi miwili huku ugonjwa wake ukifanywa kuwa siri kubwa. Kuna habari kuwa, msanii huyo anasumbuliwa na kichwa.
Kufuatia kulazwa hospitalini hapo kwa muda mrefu, baadhi ya vyombo vya habari vimekuwa vikitoa taarifa tofauti kuhusu ugonjwa unaomsumbua msanii huyo.
Katika kipindi cha Orijino Komedi wiki iliyopita, msanii maarufu kwa jina la Masanja alisikika akisema kwa masikitiko kwamba, hali ya Vengu bado haijatengemaa.
“Jamani jamani, Vengu anaumwa. Masikini jembe langu, linaumwa,”alisema.
Masanja alisema hayo, kufuatia mashabiki wengi wa kipindi hicho kuwapigia simu wakitaka kujua maendeleo ya afya ya msanii huyo.
Kutokana na kuthamini mchango wa msanii mwenzao, Masanja alisema wataendelea kutumia kazi zake zilizopita ili kuwaliwaza mashabiki wao.

Shakur aipiga jeki Uhuru SC



MFANYABIASHARA Shakur Sanya ameipatia klabu ya michezo ya Uhuru vifaa vya michezo kwa ajili ya timu yake ya soka.
Shakur, ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Mipango, Uchumi na Fedha ya CCM Kata ya Jangwani, alikabidhi vifaa hivyo juzi kwa Katibu wa klabu ya Uhuru, Rashid Zahor.
Vifaa vilivyotolewa na Shakur kwa klabu ya Uhuru ni seti moja ya jezi na mipira mitatu, vyote vikiwa na thamani ya sh. 500,000.
Hafla ya kukabidhi vifaa hivyo, ambayo ilifanyika kwenye ofisi za Shakur, mtaa wa Mafia, Dar es Salaam, pia ilihudhuriwa na nahodha wa timu ya soka ya Uhuru, Mussa Hassan.
Akizungumza wakati wa kukabidhi vifaa hivyo, Shakur alisema ameamua kutoa msaada huo kwa lengo la kuiimarisha timu ya Uhuru.
“Msaada huu pia ni utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi, ambayo inasisitiza umuhimu wa kuibua vipaji vya michezo na kuviendeleza,”alisema.
Shakur alisema msaada huo ni wa mwanzo kwake kwa Uhuru, lakini hautakuwa wa mwisho, hivyo ameahidi kuendelea kuisaidia kila itakapohitaji msaada kutoka kwake.
“Ninayo taarifa kwamba timu yenu imekuwa ikisafiri mara kwa mara mikoani kucheza mechi za kirafiki na hivi karibuni mnatarajia kwenda Arusha, nitajitahidi katika siku zijazo kuendelea kuwasaidia,”alisema.
Kwa upande wake, Zahor alimshukuru Shakur kwa kuwapatia msaada huo wa vifaa vya michezo na kuahidi kuwa, watautumia kwa malengo yaliyokusudiwa.
Alisema msaada huo umekuja wakati mwafaka kwa timu yake kwa vile wamepanga kucheza mechi kadhaa za kirafiki kwa ajili ya kujiandaa na michuano ya Kombe la NSSF.
Uhuru ilitwaa kombe hilo mara mbili mfululizo mwaka 2007 na 2008 na mwaka 2009 ilishika nafasi ya pili wakati mwaka jana ilishika nafasi ya tatu. Timu ya netiboli nayo ilitwaa kombe hilo mwaka 2007.
Klabu ya michezo ya Uhuru pia imewahi kutwaa ubingwa wa jumla wa bonanza la vyombo vya habari mwaka 2010 na 2009.
Klabu ya Uhuru inaundwa na wafanyakazi wa Kampuni ya Uhuru Publications Ltd, wachapishaji wa magazeti ya Uhuru, Mzalendo na Burudani, kituo cha Radio cha Uhuru FM na ofisi ndogo ya CCM.

Friday, November 25, 2011

Asante Kotoko kutua Dar Des 9



TIMU ya soka ya Kumasi Asante kotoko ya Ghana inatarajiwa kuwasili nchini Desemba 9 tayari kucheza mchezo mmoja wa kirafiki dhidi ya kombaini ya timu za Yanga na Simba siku ya Desemba 11 kwenye uwanja wa Taifa. Mchezo huo ni sehemu ya kukamilisha maadhimisho ya sherehe za miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania na maandalizi yake yamekwisha kamilika kwa mujibu wa mwenyekiti mtendaji wa kampuni ya Future Century Limited, Helen Masanja. Masanja alisema kuwa timu hiyo itafikia Zanzibar na baadaye kuja jijini Dar es Salaam kwenye hotel ya Lamada tayari kwa mchezo huo ambao umedhaminiwa na PPF, Kenya Airways, Vanedrick Tanzania Limited, Lamada Hotel na Vanne Fashion Tabata. Alisema kuwa wanatarajia kuwa na burudani ya aina yake kwani tayari kombaini ya timu ya Yanga na Simba itaundwa na wachezaji nyota wanaocheza Ligi Kuu ya Tanzania Bara msimu huu. Aliongeza kuwa makocha wawili, mkongwe, Abdallah “King Mputa” Kibaden na Fred “ Minziro” Felix ndiyo watakuwa wakuu wa benchi la ufundi la timu hiyo ambayo itaundwa na wachezaji 20 watakaotangazwa hapo baadaye. Wengine katika benchi la ufundi na meneja, Boniface Pawasa na daktari wa timu, Juma Sufiani. Alifafanua kuwa uteuzi wa timu hiyo hautajali uraia wa wachezaji hivyo kama wachezaji kutoka nchi za nje ambao wanachezea timu hizo watateuliwa, basi watacheza mchezo huo.Masanja alisema kuwa Yanga na Simba zimekubaliana na kuweka historia kwa mara ya kwanza tangu timu hizo zitengane mwaka 1935. Alisema kuwa historia inaonyesha kuwa timu hizo zilikuwa pamoja kuanzia mwa 1922. Mwenyekiti wa Yanga Lyod Nchunga alisema kuwa mechi hiyo itaondoa tofauti iliyopo baina ya mashabiki wa Simba na wale wa Yanga hasa zinapotokea timu hizo zinacheza mechi za kimataifa ambapo imekuwa ni kawaida mashabiki wa timu hizo kushangilia timu pinzania. Wakati Nchunga akisema hayo, Katibu Mkuu wa Simba, Evodius Mtawala alisema kuwa muungano huo utaleta tija kwa timu hizo ambapo mashabiki wa Simba na Yanga siku hiyo watakuwa kitu kimoja kwa ajili ya kuishangilia timu yao tofauti na ilivyokuwa miaka ya nyuma.Alisema kuwa huu ndiyo mwanzo wa kuanza kushirikiana katika mechi za kimataifa na kuwataka mashabiki kufika kwa wingi na kutoa sapoti kubwa kwao

Tenga awa balozi wa malaria



Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania, Leodegar Tenga ambaye pia ni Rais wa CECAFA, akipokea tuzo baada ya kutangazwa kuwa Balozi wa United Against Malaria Tanzania na mmoja wa viongozi wa taasisi ya Johns Hopkins nchini, Anna McMartney (kushoto) katika hafla ya kuyakaribisha mashindano ya Tusker Challenge Cup yanaliyoanza kutimua vumbi jijini Dar es Salaam jana. Hafla hiyo iliyoandaliwa na United Against Malaria ilifanyika jana jijini humo.

KANIKI, JOHN WILLIAM WAPATA TIMU SWEDEN





Wachezaji wawili wa kitanzania, Joseph Kaniki (Golota) na William John wamefanikiwa kujiunga na timu ya ligi daraja la pili KonyaSpor (KIF) nchini Sweden, baada ya kufanikiwa kupita katika majaribio( Trials). Majaribio hayo yalijumuisha wachezaji zaidi ya thelathini ambapo wachezaji watano walichaguliwa kujiunga na klabu hiyo ya ligi daraja la pili KonyaSpor (KIF)

DIAMOND AIPUA ALBAMU MPYA



Nyimbo yangu mpya inaitwa Mawazo, nimerekodi studio za AM RECORD, producer Maneke, inapatikana katika albam yangu mpya ya inayoitwa LALA SALAMA, album ina nyimbo kumi ambazo ni

1) Moyo Wangu

2) lala salama

3) Chanda chema

4) Nimpende nani

5) najua

6) Mawazo

7) Kwanini

8) Gongolamboto

9) Natamani

10)Kizaizai

FAINALI KOMBE LA UHAI YASOGEZWA



Mechi ya fainali ya michuano ya soka ya vijana wenye umri chini ya miaka 20 ya Kombe la Uhai (Uhai Cup) kwa klabu za Ligi Kuu sasa itachezwa kesho (Novemba 26 mwaka huu) saa 3.00 asubuhi kwenye Uwanja wa Karume.

Awali fainali hiyo kati ya Simba, ambayo iliingia hatua hiyo kwa kuitandika Toto Africans mabao 4-1 na Azam, iliyofuzu kwa kuizamisha Serengeti Boys (timu ya Taifa ya vijana chini ya miaka 17) mabao 3-0, ilikuwa ichezwe leo (Novemba 25 mwaka huu) saa 9.00 kwenye uwanja huo.

Mabadiliko hayo yamefanyika ili kutoa nafasi kwa mashabiki kushuhudia mechi za michuano ya Kombe la Chalenji inayoanza leo (Novemba 25 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Taifa.

Kila siku kwenye michuano ya Chalenji zinachezwa mechi mbili; ya kwanza saa 8.00 mchana na nyingine saa 10.00 jioni.

Michuano ya Kombe la Uhai inadhaminiwa na Kampuni ya S.S. Bakhresa kupitia maji Uhai ambapo bingwa atapata sh. milioni 1.5, mshindi wa pili sh. milioni moja wakati wa tatu atapata sh. 500,000.

Mbali ya fedha hizo, bingwa atapata medali za dhahabu, makamu bingwa medali za fedha na mshindi wa tatu medali za shaba. Mchezaji bora sh. 400,000, mfungaji bora (sh. 300,000), kipa bora (sh. 300,000) na timu yenye nidhamu sh. 300,000.

VIINGILIO MICHUANO YA KOMBE LA CHALENJI

Viingilio kwa mechi za hatua ya makundi kwa michuano ya Kombe la Chalenji inayoanza leo (Novemba 25 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam vitakuwa kama ifuatavyo;

Kwa viti vya rangi ya bluu na kijani ambavyo ni zaidi ya 30,000, kiingilio kitakuwa sh. 1,000 wakati viti vya rangi ya chungwa ambavyo ni zaidi ya 10,000 kiingilio kitakuwa sh. 3,000. VIP C na B ambayo jumla ya viti vyake ni 8,000 kiingilio kitakuwa sh. 5,000 wakati VIP A yenye viti 700 kiingilio ni sh. 10,000.

Tenga achaguliwa tena kuongoza CECAFA



TENGA ACHAGULIWA TENA CECAFA

Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Leodegar Tenga amechaguliwa tena kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati (CECAFA).

Tenga amechaguliwa leo (Novemba 24 mwaka huu) bila kupingwa baada ya mpinzani wake Fadoul Hussein wa Djibouti kutotokea kwenye uchaguzi.

Kutokana na hali hiyo, mjumbe kutoka Uganda alitoa hoja ya Tenga kupitishwa bila kupingwa, hoja ambayo iliungwa mkono na Kenya, Tanzania, Uganda, Sudan, Zanzibar, Ethiopia, Burundi na Eritrea.

Jumla ya nchi wanachama zilizopiga kura katika uchaguzi uliofanyika hoteli ya New Africa ni kumi na moja, na kila moja ilikuwa na kura moja tu.

Kwa upande wa nafasi nne za wajumbe wa Kamati ya Utendaji kulikuwa na wagombea wanane. Waliopita katika raundi ya kwanza na kura zao kwenye mabano ni Abdiqani Saeed Arab wa Somalia (8), Tariq Atta Salih wa Sudan (8) na Raoul Gisanura wa Rwanda (8). Wengine katika raundi ya kwanza na kura walizopata kwenye mabano ni Sahilu Wolde wa Ethiopia (4), Justus Mugisha wa Uganda (4), Tesfaye Gebreyesus wa Eritrea (4), Hafidh Ali Tahir wa Zanzibar (2) naAbubakar Nkejimana wa Burundi (3).

Mjumbe aliyefanikiwa kushinda katika raundi ya pili na kuingia kwenye Kamati ya Utendaji ni Wolde wa Ethiopia aliyepata kura tano dhidi ya nne za Mugisha na mbili za Gebreyesus. Mwenyekiti anakaa madarakani kwa miaka minne wakati wajumbe wa Kamati ya Utendaji wanachaguliwa kila baada ya miaka miwili.

ZIMBABWE YAZIBA NAFASI YA NAMIBI

Timu ya Taifa ya Zimbabwe (Might Warriors) imeteuliwa na CECAFA kushiriki michuano ya Kombe la Chalenji inayoanza Novemba 25 mwaka huu jijini Dar es Salaam kuziba nafasi ya Namibia iliyojitoa. Zimbabwe itawasili Novemba 26 mwaka huu jijini Dar es Salaam na itakuwa kundi A pamoja na timu za Tanzania Bara, Rwanda na Djibouti.

KIKOSI CHA KILIMANJARO STARS

Kocha Mkuu wa timu ya Tanzania Bara (Kilimanjaro Stars), Charles Boniface Mkwasa ametaja kikosi cha mwisho cha wachezaji 20 kwa ajili ya michuano hiyo inayoanza kesho.

Wachezaji waliobaki kati ya 28 waliokuwa wameitwa awali ni Juma Kaseja (Simba), Shabani Kado (Yanga), Shomari Kapombe (Simba), Godfrey Taita (Yanga), Juma Jabu (Simba), Ibrahim Mwaipopo (Azam) ,Juma Nyoso (Simba), Said Murad (Azam), Erasto Nyoni (Azam) na Shabani Nditi (Mtibwa Sugar), Nurdin Bakari (Yanga), Haruna Moshi (Simba) na Mwinyi Kazimoto (Simba).

Wengine ni Said Maulid (Angola), Musa Mgosi (DC Motema Pembe, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo-DRC), Mrisho Ngassa (Azam), Ramadhan Chombo (Azam), Thomas Ulimwengu (TP Mazembe, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo- DRC), Mbwana Samata (TP Mazembe, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo- DRC) na Rashid Yusuf (Coastal Union).

Kilimanjaro Stars itacheza mechi yake ya kwanza Novembe 26 mwaka huu dhidi ya Rwanda.

Wednesday, November 23, 2011

GOFU KUSAIDIA WAGONJWA WA MACHO



Benki ya NIC Tanzania kwa kushirikiana na klabu ya Lions ya Dar es Salaam, imejitokeza kudhamini mashindano ya mchezo ya gofu kwa lengo la kusaidia watu wenye matatizo ya macho. Katika mashindano hayo, benki hiyo imetoa jumla ya dola za Kimarekani 2,000 (sawa na sh. milioni 3.5 za Tanzania) kwa lengo la kuinua afya za wananchi, hasa wanaosumbuliwa na matatizo ya macho.Pichani, Mkurugenzi na Mtendaji Mkuu wa NIC Tanzania, James Muchiri (kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na Meneja Mikopo wa benki hiyo, Regina Mwengi, Prisalla Karobia na David Muthungu kabla ya kuanza kwa michuano hiyo iliyofanyika juzi kwenye viwanja vya Gymkhana, Dar es Salaam.

Ferej alalamikia ukiukwaji wa katiba ZFA


VURUGU zinazotokea mara kwa mara katika Chama cha Soka cha Zanzibar (ZFA) ni matokeo ya kukiukwa kwa katiba na kanuni za kuendesha mchezo huo.
Hayo yamesemwa na Rais wa ZFA, Ali Ferej Tamim wakati wa mkutano mkuu wa dharula wa chama hicho uliofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita mjini hapa.
Mbali na kujadili masuala mbalimbali, mkutano huo uliitishwa kwa lengo la kufanya marekebisho ya katiba ya chama hicho.
Ferej alitoa kauli hiyo baada ya baadhi ya wajumbe wa kamati ya utendaji ya chama hicho kutoka Pemba, kulalamika kuwa, kimekuwa kikitoa maamuzi mengi bila ya kufuata katiba.
Wajumbe hao walilalamikia uamuzi wa ZFA wa kuirejesha Malindi katika ligi kuu bila kufuata taratibu ama kuishirikisha kamati ya utendaji ya chama hicho katika kutoa maamuzi.
Akijibu malalamiko hayo, Ferej alisema katika soka, hakuna kitu kinachoitwa makubaliano, kinachotakiwa ni kufuatwa kwa katiba na kanuni katika kutoa maamuzi.
Ferej alisema ni kweli kwamba yeye ni mwanachama wa klabu ya Malindi, lakini hawezi kutoa maamuzi kwa lengo la kuibeba.
Rais huyo wa ZFA alisema tatizo kubwa linaloikabili soka ya Zanzibar ni ukiukwaji wa kanuni na kusisitiza kuwa, iwapo halitapatiwa ufumbuzi, litakwamisha maendeleo ya mchezo huo.
Alisema yapo baadhi ya mambo, ambayo klabu zinaweza kukubaliana kama vile mfumo wa mgawo wa mapato, lakini si uendeshaji wa ligi.
“Katika hili, ni kweli kwamba kanuni zimevunjwa na timu zilizoshuka daraja, zimeonewa,”alisema rais huyo wa ZFA, ambaye ameichezea Malindi kwa miaka 11 na pia kuiongoza kwa kipindi kama hicho.

Kambi ya Misri yaipa jeuri Zanzibar Heroes


TIMU ya soka ya Zanzibar, Zanzibar Heroes imerejea nchini juzi kutoka Misri, ilikokwenda kuweka kambi kwa ajili ya kujiandaa na michuano ya Kombe la Chalenji.
Ofisa Habari wa Chama cha Soka cha Zanzibar (ZFA), Munir Zakaria alisema mjini hapa juzi kuwa, timu hiyo iliweka kambi Misri kwa wiki mbili.
Mbali ya kuweka kambi, Munir alisema timu hiyo ilicheza mechi tatu za kirafiki dhidi ya timu za Misri, ambapo ilishinda mechi moja na kufungwa mechi tatu.
Munir alisema timu hiyo ilipata ushindi wake wa pekee dhidi ya timu ya taifa ya vijana wa chini ya miaka 17 ya Misri. Katika mechi hiyo, Zanzibar Heroes ilishinda mabao 3-2.
Zanzibar Heroes ilikwenda Misri ikiwa chini ya Kocha Hemed Morocco, ambaye ndiye atakayeiongoza katika michuano ya Kombe la Chalenji, inayotarajiwa kuanza kesho.
Akizungumzia kambi hiyo, Munir alisema ilikwenda vizuri na kwamba mechi nne za kirafiki walizocheza, zimewaweka wachezaji katika hali nzuri kwa ajili ya Kombe la Chalenji.
Alisema kikosi hicho kwa sasa kipo fiti kwa ajili ya michuano hiyo na kuongeza kuwa, wachezaji wana ari kubwa ya kuibuka na ushindi.
Wakati huo huo, Munir amesema hatma ya Kocha John Stewart kutoka Uingereza kwa sasa ipo mikononi mwa ZFA.
Stewart, ambaye pia ni Kocha Mkuu wa Azam FC, alishindwa kujiunga na Zanzibar Heroes ilipokuwa Misri kwa madai kuwa, hati yake ya kusafiria ilikuwa imejaa.
Hata hivyo, utetezi wake huo umepingwa na baadhi ya viongozi wa chama hicho kwa madai kuwa, alifahamu mapema kuhusu safari hiyo.
Licha ya kuifundisha Azam, inayoshiriki michuano ya ligi kuu ya Tanzania Bara, Stewart pia ana mkataba wa kuifundisha Zanzibar Heroes wakati wa michuano mbalimbali.

SMG afurahia kuitwa Kilimanjaro Stars

MSHAMBULIAJI Saidi Maulid ‘SMG’ anayecheza soka ya kulipwa nchini Angola, amesema amefurahia kuitwa kwenye kikosi cha Tanzania Bara, Kilimanjaro Stars kitakachoshiriki katika michuano ya mwaka huu ya Kombe la Chalenji.
SMG alisema hayo mjini Dar es Salaam juzi, alipokuwa akizungumzia kuitwa kwake kwenye kikosi hicho baada ya kuachwa kwa zaidi ya miaka mitano.
Alisema kwa mchezaji yeyote wa kulipwa anayecheza nje ya nchi yake, huwa ni fahari kubwa kwake kuitwa kwenye timu ya taifa kwa sababu kunaonyesha anavyothaminiwa.
Mshambuliaji huyo wa zamani wa klabu za Simba na Yanga alisema, amekuwa akiisubiri nafasi hiyo kwa muda mrefu na baada ya kuipata amepania kuonyesha uwezo wake.
Hata hivyo, SMG alisema kufanya vizuri kwa Kilimanjaro Stars katika michuano hiyo kutategemea ushirikiano wa wachezaji uwanjani na kutiwa moyo na mashabiki.
Alisema wao kama wachezaji, watajitahidi kucheza kadri ya uwezo wao, lakini wanahitaji sapoti kubwa kutoka kwa mashabiki.
SMG aliichezea Taifa Stars mwanzoni mwa miaka ya 2000 ilipokuwa chini ya makocha wazalendo na baadaye Marcio Maximo kutoka Brazil, lakini alitemwa baada ya kwenda Angola.
Awali, SMG hakuwemo kwenye kikosi hicho, lakini makocha Charles Boniface Mkwasa na Jamhuri Kihwelu walilazimika kumwita baada ya kuumia kwa John Bocco.
Mkataba wa mshambuliaji huyo kucheza Angola unatarajiwa kumalizika Desemba 2012.

Mwaikimba amwaga wino Azam FC


MSHAMBULIAJI Gaudence Mwaikimba wa Moro United amejiunga rasmi na Azam FC kwa ajili ya mzunguko wa pili wa michuano ya ligi kuu ya Tanzania Bara.
Ofisa Habari wa Azam, Jafari Iddi alisema mjini Dar es Salaam juzi kuwa, tayari mshambuliaji huyo ameshatia saini mkataba wa kuichezea timu hiyo.
Jafari alisema wameamua kumsajili Mwaikimba kwa lengo la kuziba pengo la mshambuliaji wao kutoka Ghana, ambaye ameachwa kutokana na kiwango chake kushuka.
Msemaji huyo wa Azam alisema, Mwaikimba anatarajiwa kuanza mazoezi na timu hiyo mara baada ya kumalizika kwa michuano ya Kombe la Chalenji.
Alisema wanaamini, Mwaikimba atashirikiana vyema na mshambuliaji John Bocco na Mrisho Ngassa kuunda safi kali ya ushambuliaji.
Kwa mujibu wa Jafari, lengo la timu yake ni kuhakikisha kuwa, wanamaliza msimu huu wa ligi wakiwa mabingwa ama kushika nafasi ya pili ili waweze kushiriki michuano ya kimataifa mwakani.
Kwa sasa, Mwaikimba yumo kwenye kikosi cha Tanzania Bara, Kilimanjaro Stars kitakachoshiriki michuano ya Kombe la Chalenji, inayotarajiwa kuanza kesho mjini Dar es Salaam.
Mwaikimba alianza kujipatia umaarufu alipokuwa akichezea Ashanti kabla ya kuchukuliwa na Yanga na baadaye kuhamia Kagera Sugar ya Bukoba.
Mchezaji huyo alikuwemo kwenye kikosi cha timu ya Taifa, Taifa Stars kilipokuwa chini ya Kocha Marcio Maximo kutoka Brazil kabla ya kutemwa kwa madai ya kiwango chake kushuka.

Tenga ni kusuka au kunyoa leo


UCHAGUZI mkuu wa Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) umepangwa kufanyika leo kwenye hoteli ya JB Belmont mjini Dar es Salaam.
Katika uchaguzi huo, mwenyekiti wa sasa wa CECAFA, Leodegar Tenga atakuwa akitetea nafasi hiyo dhidi ya Fadoul Hussein wa Djibouti.
Kwa sasa, Fadoul ni makamu mwenyekiti wa baraza hilo, lakini ameamua kuwania wadhifa wa juu kwa kumpinga bosi wake.
Uamuzi wa Fadoul kugombea nafasi hiyo, unamweka Tenga kwenye wakati mgumu kwa vile atalazimika kutegemea zaidi kura za nchi jirani ya Tanzania.
Kutokana na mazingira yalivyo, Fadoul atategemea zaidi kura kutoka Djibouti, Eritrea, Somalia na Sudan wakati kura za Tenga huenda zikatoka katika nchi za Tanzania Bara, Zanzibar, Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi.
Hata hivyo, Tenga ndiye anayepewa nafasi kubwa ya kushinda wadhifa huo kutokana na kuungwa na nchi nyingi zilizo wanachama wa baraza hilo, akiwemo Katibu Mkuu, Nicholas Musonye.
Uchunguzi wa Burudani umebaini kuwa, nchi nyingi zinamuunga mkono Tenga kutokana na utendaji wake mzuri wa kazi, uwazi na pia ushirikiano na viongozi wenzake.
Tenga ndiye aliyeiwezesha CECAFA kupata udhamini wa michuano ya Kombe la Chalenji kutoka Kampuni ya Bia ya Serengeti (SBL) kwa miaka miwili mfululizo na kuhudhuriwa na mashabiki wengi zaidi kuliko nchi zingine.
Musonye alikaririwa hivi karibuni akisema kuwa, baraza lake linafurahia zaidi michuano hiyo kufanyika hapa nchini kutokana na kuwepo kwa udhamini mzuri na pia idadi kubwa ya mashabiki wanaofika uwanjani.
Mbali na uchaguzi wa mwenyekiti, pia watachaguliwa wajumbe wanne wa kamati ya utendaji. Wanaogombea nafasi hizo ni wajumbe wanane.
Wagombea hao ni Abdiqani Saeed Arab (Somalia), Tariq Atta Salih (Sudan), Justus Mugisha (Uganda), Tesfaye Gebreyesus (Eritrea), Hafidh Ali Tahir (Zanzibar), Sahilu Wolde (Ethiopia), Raoul Gisanura (Rwanda) na Abubakar Nkejimana (Burundi).

Simba yafanya kweli



WACHEZAJI Bukaba Bundara (kulia) wa Toto African na Abdalla Seseme wa Simba wakiwania mpira timu hizo zilipomenyana jana katika mechi ya nusu fainali ya michuano ya soka ya Kombe la Uhai kwa timu za vijana wa chini ya miaka 20 iliyochezwa kwenye Uwanja wa Karume, Dar es Salaam. Simba ilishinda mabao 4-1.


TIMU ya soka ya Simba jana ilifuzu kucheza fainali ya michuano ya Kombe la Uhai baada ya kuichapa Toto African mabao 4-1.
Katika mechi hiyo ya robo fainali, iliyochezwa kwenye uwanja wa Karume, Dar es Salaam, Simba ilikwenda mapumziko ikiwa mbele kwa mabao 3-0.
Kutokana na ushindi huo, Simba sasa itacheza fainali keshokutwa kwa kumenyana na mshindi wa mechi nyingine ya nusu fainali kati ya Azam na Serengeti Boys, iliyotarajiwa kuchezwa jana jioni.
Iliwachukua Simba dakika 25 kuhesabu bao la kwanza lililofungwa na mshambuliaji Edward Christopher baada ya kufanyika shambulizi kali kwenye goli la Toto.
Rama Singano aliifungia Simba bao la pili dakika ya 40 kabla ya Abdalla Seseme kuongeza la tatu dakika mbili zilizofuata.
Simba ilitawala zaidi kipindi cha kwanza cha mchezo huo, huku wachezaji wake wakipeana gonga safi na kuliweka lango la Toto kwenye msukosuko mkubwa.
Toto ilizinduka kipindi cha pili na kufanikiwa kupata bao la kujifariji dakika ya 51 lililofungwa na Iddi Mobi.
Matumaini ya Toto kusawazisha yalizimwa na Haroun Athumani, aliyeiongezea Simba bao la nne dakika ya 78 na kuamsha shamrashamra kutoka kwa mashabiki wa timu hiyo.
Bingwa wa michuano hiyo atazawadiwa kitita cha sh. milioni 1.5 wakati mshindi wa pili atapata sh. milioni moja na wa tatu sh. 500,000.
Mchezaji bora wa michuano hiyo atazawaduwa sh. 400,000, mfungaji bora sh. 300,000), kipa bora sh. 300,000 na timu yenye nidhamu sh. 300,000.

NEYMAR: Nataka kuweka historia duniani





RIO DE JANEIRO, Brazil
WAKATI alipokuwa akikatiza mitaani miaka kadhaa iliyopita,Neymar da Silva Santos Junior hakuwa mtu maarufu. Alionekana mtu wa kawaida, sawa na watoto wengine wa Kibrazil, nchi iliyobarikiwa kuwa na vijana wengi wenye vipaji vya kusakata kabumbu.
Lakini hali imekuwa tofauti miaka ya hivi karibuni, ambapo umaarufu wake kisoka umemfanya awe akizingirwa na kundi la watu kila anapopita mitaani, huku wengine wakimtaka atie saini vitabu vyao vya kumbukumbu na wengine kumuomba wapige naye picha ya pamoja.
Neymar (19) ni mchezaji mwenye kipaji cha aina yake kisoka, akiwa anafananishwa na Ronaldinho Gaucho, Robinho au Lionel Messi. Na kuna watu wanaobashiria kwamba, anaweza kuwa sawa na Pele kiuchezaji.
Chipukizi huyo amekuwa tegemeo kubwa la klabu yake ya Santos ya Brazil na pia timu ya taifa ya nchi hiyo. Uwezo wake kisoka ulizivutia klabu kadhaa kubwa za Ulaya kama vile Real Madrid ya Hispania na Chelsea ya England, lakini zote ziligonga mwamba kumsajili.
Kila anapokwenda, Neymar hufuatwa na kundi kubwa la wapiga picha. Iwe ni katika mji wa Santos, London na New York, hali huwa hivyo hivyo. Amekuwa shujaa kwa vijana wengi wa kiume na mvulana mwenye mvuto kwa wasichana, hasa kutokana na staili ya utengenezaji wa nywele zake.
Neymar anakumbuka miaka si mingi iliyopita, alipokuwa akitoka nyumbani kwenda kununua ice-cream, hakuwa akismamishwa na watu njiani. Lakini gharama za umaarufu zimeshayabadili maisha yake na kumfanya aonekane lulu machoni mwa mashabiki wa soka.
“Haya ndiyo maisha niliyoyachagua,”alisema Neymar alipohojiwa na mtandao wa FIFA hivi karibuni. “Sikuchagua niishi hivi, nilimuomba Mungu. Nilichokitaka ni kucheza soka na kuwa mwenye mafanikio na nipate umaarufu. Nimepata kila nilichokuwa nikikihitaji na nitakuwa mpumbavu kulalamikia chochote kwa sasa.”
“Siwezi kukaa mahali na kufikiria kwamba siwezi kutoka nje kwenda kununua ice-cream,”aliongeza. “Ninakwenda popote na kuishi maisha yangu ya kawaida, nasaini vitabu vya kumbukumbu vya mashabiki, napiga nao picha na hata kutolewa lugha za dhihaka kwa sababu hii ni sehemu ya maisha ya soka. Mwisho wa siku mimi ni binadamu wa kawaida.”
Licha ya kujifunza kuishi maisha hayo na ya matumaini tangu akiwa mdogo na pia kutawala kwenye vyombo vya habari mara kwa mara, ukweli unabaki palepale kwamba, Neymar bado ni kijana, aliyejawa na aibu na asiyeelewa maana ya mafanikio aliyoyafikia hivi sasa.
“Kusema ukweli, haya ni mambo mapya kwangu, kuwaona watu wote hawa wakishangilia kwa kutaja jina langu na kunitaka niseme ‘Hi’ ama kuwatolea tabasamu. Lakini tayari nimeshaanza kuzoea hali hii. Binafsi nilikuwa nikiwashabikia baadhi ya wachezaji nyota na kujawa na hofu wanapokatiza mbele yangu. Na sasa imekuwa zamu yangu na ninapata heshima kubwa kwa mashabiki,”alisema nyota huyo.
Neymar, ambaye mashabiki wa soka nchini Brazil wamempachika jina la Neymarzetes, amekuwa na wakati mgumu kwa mabeki wa timu pinzani, ambao wamekuwa wakifanya kila wanaloweza kumzuia uwanjani.
“Unamtoka mchezaji mmoja, hatua inayofuata unaangushwa chini. Unamtoka mchezaji mwingine, kinachofuatia unaangushwa tena chini. Na kigumu zaidi ni kwamba, kuna ukabaji wa mtu kwa mtu,”alisema.
Kupatiwa kwake nafasi ya kuichezea timu ya taifa ya Brazil kumemwezesha nyota huyo kujifunza mengi kuhusu mabeki kutoka sehemu mbalimbali duniani, elimu ambayo anakiri imemsaidia katika mambo mengi.
“Kucheza dhidi ya wachezaji waliopo Ulaya, kumenisaidia mambo mengi. Ukabaji wao ni mgumu, lakini ni tofauti,”alisema nyota huyo.
Neymar amemwelezea mshambuliaji wa kimataifa wa Argentina, Lionel Messi kuwa tayari ameshaweka historia na kupata mafanikio makubwa kisoka. Alisema binafsi ndio kwanza anaanza kuonyesha cheche zake na anakabiliwa na changamoto nyingi ili aweze kufikia mafanikio hayo.
Neymar, ambaye hivi karibuni alitia saini mkataba mpya wa kuichezea Santos hadi mwaka 2014, alisema anaamini michuano ya kuwania klabu bingwa ya dunia itakayofanyika mwezi ujao Japan, itamwongezea ujuzi zaidi kisoka.
Chipukizi huyu anavutiwa zaidi na klabu ya Barcelona ya Hispania. Anaielezea timu hii kuwa, inastahili tuzo zote ilizonyakua kwa vile soka yake ni ya kiwango cha juu na yenye mvuto wa aina yake.
Iwapo timu ya Santos na Barcelona zitakutana katika michuano hiyo, itakuwa ni burudani babu kubwa kwa mashabiki kwa vile itakuwa ni nafasi nzuri kwa Neymar na Messi kuonyesha uwezo wao.
Neymar na Messi ni miongoni mwa wachezaji 23 walioteuliwa kuwania tuzo ya mfungaji bora wa FIFA wa mwaka 2011.
“Siku zote nimekuwa nikisema kwamba, bado nina mambo mengi ya kujifunza. Messi ni mchezaji, ambaye tayari ameshaweka historia na atapata mafanikio mengi zaidi. Mimi ndio kwanza naanza na ninapaswa kufanya mengi ili niweze kufikia mafanikio yake,”alisema.
Neymar amesema amepania kujiweka fiti zaidi ili abaki kwenye kiwango cha juu na pia kuiwezesha nchi yake kufanya vizuri kimataifa.
“Nataka kuweka historia na Brazil mwaka 2014 na kuliweka jina langu kwenye kumbukumbu ya soka duniani,”alisema.
Neymar alijiunga na Santos mwaka 2003 na kuanza kupata namba kwenye kikosi cha kwanza miaka sita baadaye, akiwa na umri wa miaka 17.
Aprili 15, 2010 aliifungia Santos mabao sita katika ushindi wa mabao 8-1 dhidi ya Guarani katika mechi ya raundi ya pili ya michuano ya Kombe la Brazil. Aliifungia Santos mabao 16 katika mechi 19 za michuano hiyo na kuiwezesha kutwaa ubingwa.
Juni 2010, Santos ilikataa maombi ya kumuuza mshambuliaji huyo kwa klabu za West Ham, Manchester United, Chelsea, AC Milan, Inter Milan, Real Madrid na Juventus.
WASIFU

JINA: Neymar da Silva Santos Junior

ALIZALIWA: Februari 5, 1992

UMRI: Miaka 19

ALIKOZALIWA: Mogi das Cruzes, Sao Paulo, Brazil

UREFU: 1.74 m (futi 5 na inchi 9)

NAFASI: Mshambuliaji

KLABU: Santos

NAMBA YA JEZI: 11

TIMU ya TAIFA:

2009: Brazil U-17

2010: Brazil

2011: Brazil U-20

Ati Ukwa ajigeuza demu!





LAGOS, Nigeria
MSANII machachari wa filamu za vichekesho nchini Nigeria, Osita Iheme hivi karibuni alitoa kali baada ya kuonekana hadharani akiwa amevaa kike.
Osita, ambaye ni maarufu zaidi kwa jina la Ukwa, alitinga vivazi hivyo kwa nyakati mbili tofauti huku akiwa amesuka nywele zake.
Mbali na kusuka nywele zake kwa mtindo wa rasta, Ukwa pia alikuwa amepaka rangi ya mdomo na nyusi zake kuzikoleza rangi nyeusi. Alikuwa na mwonekano wa kike hasa.
“Osita amekuwa msichana!” Baadhi ya watu waliomwona walisikika wakisema.
Hali hiyo ilisababisha watu wengi iwapo Ukwa ameamua kufanya hivyo kwa makusudi ama alikuwa katika matayarisho ya kutengeneza filamu mpya.
Licha ya watu wengi kumshangaa, Ukwa alionekana kutojali huki akiendelea na mambo yake kama vile hakukuwa na jambo lililomshangaza.
Hata hivyo, baadhi ya watu waliohojiwa walisema wana hamu kubwa ya kuiona filamu hiyo mpya ya Ukwa, wakiamini itakuwa na vichekesho na vituko vya kuvunja mbavu.

Mr. Ibu, mkewe wapata mtoto


LAGOS, Nigeria
MCHEZA filamu mwenye vituko nchini Nigeria, John Okafor amefanikiwa kupata mtoto wa kike baada ya mkewe kujifungua.
Okafor, maarufu zaidi kwa jina la Mr. Ibu, amepokea taarifa hizo kwa furaha kubwa, ikiwa ni pamoja na kuandaa hafla fupi ya kumpongeza mkewe kwa kujifungia salama.
Habari kutoka kwa watu wa karibu na mcheza filamu huyo zimeeleza kuwa, mkewe, Stella Maris alijifungua siku chache zilizopita.
Kwa mujibu wa habari hizo, watu mbalimbali wamemtumia Mr. Ibu na mkewe salamu za pongezi na kuwatakia maisha mema na marefu.
Mr. Ibu ni mmoja wa wacheza filamu maarufu wa Nollywood, akiwa anavutia zaidi kuchezesha filamu za vichekesho.
Alianza kujipatia umaarufu kupitia filamu ya Mr. Ibu aliyocheza kwa kushirikiana na Osita Iheme (Aki) mwaka 2004.

Hakuna kama Genevieve


LAGOS, Nigeria
KATIKA maisha yake ya usanii, Genevieve Nnaji ameshindwa kupata mafanikio katika fani moja pekee. Ni pale alipojaribu kujitosa kwenye muziki.
Hata hivyo, albamu ya Genevieve ilimpatia kiasi kikubwa cha pesa. Ni kwa sababu, mmiliki wa studio aliyorekodi albamu yake alimlipa fedha nzuri kwa ajili ya kazi hiyo.
Hiyo ni sehemu ndogo ya vikwazo, ambavyo mwanadada huyo mwenye sura na umbo lenye mvuto amewahi kukumbana navyo.
Zaidi ya hapo, ni mtiririko wa matukio yenye mafanikio, si Nigeria pekee, bali katika bara zima la Afrika na sehemu zingine mbalimbali duniani.
Katika kipindi cha miaka sita iliyopita, hakuna mwigizaji filamu aliyeweza kupata mafanikio na kushinda tuzo nyingi kama Genevieve.
Msichana huyo, aliyekuwa akihisiwa kuwa na uhusiano wa kimapenzi na mwanamuziki D’Banj ameshinda tuzo zote alizoshiriki kuziwania na kuiwakilisha Nollywood sehemu mbalimbali duniani.
Genevieve pia amepata utajiri mkubwa kutokana na fani ya filamu na kuwa mwigizaji pekee wa kike anayelipwa fedha nyingi kwa kazi hiyo.
Hivi karibuni, Genevieve alikuwa miongoni mwa wacheza filamu nyota wa Nigeria waliopewa tuzo maalumu na Rais Goodluck Jonathan. Wengine walikuwa Olu Jacobs, Kanayo Kanayo, Amaka Igwe, Stephanie Okereke na Osita Iheme.
Mara baada ya kupokea tuzo hiyo, Genevieve alisema ameamua kuitoa kwa mashabiki wake, ambao bila wao, asingeweza kupata mafanikio aliyonayo sasa.
“Tuzo hii ni kwa wale wote walioniunga mkono miaka yote hii na kusema ndio kwa kila jambo. Wapo waliosema hapana, lakini namshukuru Mungu,”alisema.

AKI: Nampenda sana mchumba wangu




Asimulia walivyokutana, kupendana na kuamua wafunge ndoa
LAGOS, Nigeria
HATIMAYE mcheza filamu machachari wa Nigeria, Chinedu Ikedieze ameelezea jinsi alivyokutana na mchumba wake, Nneoma Hope Nwajah na kufikia uamuzi wa kufunga ndoa.
Chinedu, maarufu kwa jina la Aki na Nneoma, wanatarajia kufunga ndoa ya kimila keshokutwa katika kanisa Katoliki la St Theresa lililopo Obolo, Isiala Mbano katika jimbo la Imo.
Aki alisema mjini hapa wiki iliyopita kuwa, alianza kuwa na uhusiano na binti huyo miaka mitatu iliyopita baada ya kukutana naye mjini Lagos.
“Nilikutana naye Lagos na mara moja tukajikuta tukipendana. Ndiye pekee ninayempenda katika maisha yangu. Hakuna kingine kinachoweza kututenganisha zaidi ya kifo,”alisema msanii huyo. Aki, ambaye alianza kujipatia umaarufu mwaka 2003, alipocheza filamu ya Aki na Ukwa, akishirikiana na rafiki yake Osita Iheme, alisema mchumba wake huyo ni mweledi wa mambo mengi.
Alipoulizwa mchumba wake huyo alisema nini kuhusu kile anachovutiwa nacho kwake, Aki alisema: “Alisema nimekuwa mtu mzima, mwelewa, mwenye busara na upendo.”
Je, ni watoto wangapi, ambao Aki angependa kuzaa na mkewe?
“Hawatazidi watatu bila kujali jinsia zao,”alisema Aki, ambaye amecheza filamu nyingi zaidi kwa kushiriki na Osita.
Aki alisema pia kuwa, anampenda mkewe mtarajiwa kwa sababu ya umbo lake zuri alilopewa na Mungu.
Kwa sasa, Nneoma anakadiriwa kuwa na umri wa miaka 20, sura yake ni jalili na ni mcha Mungu wa ukweli.
Imeelezwa kuwa, ‘bestiman’ wa Aki katika ndoa hiyo atakuwa swahiba wake, Osita.
Aki anaamini uamuzi wake wa kufunga ndoa na Nneoma utamwingiza katika ulimwengu mpya kwa vile mwonekane wake utakuwa tofauti na wa sasa.
Kabla ya kukutana na Nneoma, Aki alimchumbia mwanadada Nkechi kutoka Jimbo la Delta, ambaye ni mfanyakazi wa benki, lakini hawakuweza kufunga ndoa.
Mcheza filamu huyo milionea wa Nigeria, pia aliwahi kuwa na uhusiano wa kimapenzi na mwanamke mwingine, lakini ulivunjika mapema zaidi.
Magavana watatu ni miongoni mwa watu mashuhuri walioalikwa kuhudhuria harusi ya Aki na Nneoma. Magavana hao ni Chifu T.A Orji wa Abia, Rochas Okorocha wa Imo na Peter Obi wa Anambra.
Kuna habari kuwa, sherehe za ndoa hiyo pia huenda zikahudhuriwa na Rais wa Nigeria, Goodluck Jonathan na mkewe.

Msechu arekodi na Kidumu


BAADA ya kung’ara katika shindano la mwaka huu la Tusker All Stars, msanii machachari wa muziki wa kizazi kipya nchini, Peter Msechu ameibuka na kibao kisemacho Relax.
Msechu amerekodi kibao hicho kwa kushirikiana na msanii machachari kutoka nchini Rwanda, Kidumu.
Akizungumza mjini Dar es Salaam wiki hii, Msechu alisema amefurahi sana kupata nafasi ya kurekodi na Kidumu kwa vile ni ndoto aliyokuwa nayo kwa miaka mingi.
Msechu alisema alikuwa na ndoto ya kurekodi na Kidumu kwa miaka mingi, lakini hakuweza kufanikiwa kwa vile alikuwa bado msanii mchanga.
Alisema katika maisha yake kiusanii, amepitia misukosuko mingi, ikiwa ni pamoja na kutembea kwa miguu umbali mrefu kuwatafuta wasanii maarufu ili wamsaidie katika kurekodi nyimbo zake.
“Ninachoweza kusema ni kwamba, hatimaye zile ndoto nilizokuwa nazo kwa miaka mingi, sasa zimeanza kutimia,”alisema.
Mbali na kurekodi na Kidumu, Msechu pia amepata nafasi ya kurekodi wimbo wake wa Unaniumiza kwa kushirikiana na kiongozi wa Akudo Impact, Christian Bella.
Vibao vingine vilivyomjengea umaarufu mkubwa Msechu ni pamoja na Hasira hasara na Poleni.
00000

Suma Lee azusha kasheshe



WIMBO mpya wa ‘Hakunaga’ uliopigwa na msanii nyota wa muziki wa kizazi kipya nchini, Ismail Sadiki umezua kasheshe baada ya Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) kutishia kuufungia.
Wimbo huo uliotokea kupendwa na mashabiki wengi nchini, umekuwa ukishika chati za juu kwenye vituo mbalimbali vya radio na televisheni kutokana na ujumbe na mpangilio wa ala.
Hata hivyo, lugha iliyotumiwa na Ismail, maarufu zaidi kwa jina la Suma Lee, imeonekana kuikera BASATA kwa vile Kiswahili kilichotumika sio fasaha.
Katibu Mkuu wa BASATA, Gonche Materego alisema mjini Dar es Salaam wiki hii kuwa, kwa sasa bado hawajafikia uamuzi wa kuufungia wimbo huo, lakini bado wanaujadili.
“Tunachokifanya kwa sasa ni majadiliano makubwa kuhusu nyimbo nyingi za wasanii wa Tanzania, ambazo tungo zake zinaharibu lugha ya Kiswahili,”alisema.
Akitoa mfano, Materego alisema wimbo wa Hakunaga ndio uliozua majadiliano makali kwa sababu Kiswahili kilichotumiwa na Suma Lee sio sahihi.
“Kusema ukweli, wimbo huu ulizungumzwa sana na hata watu wengine wa kawaida, ambao hawafanyikazi na BASATA walisema kwamba, unapotosha Kiswahili,”alisema Materego.
“Na kwa vile wasanii ni walimu wakuu wa Kiswahili, ni rahisi sana kwa watu wa kawaida kutumia lugha za wasanii wakidhani kuwa ni sahihi wakati sio kweli,”aliongeza.
“Wenzetu wa Baraza la Kiswahili wameona kuna haja ya kukaa na kujadiliana kuhusiana na tatizo la Kiswahili kuharibiwa kwenye nyimbo za wasanii. Tutakutana na wasanii tusikie wanachokisema na wananchi pia wasikie ili tupate michango mizuri zaidi,”alisisitiza.
Alipoulizwa kuhusu msimamo huo wa BASATA, Suma Lee alisema hawezi kuzungumza chochote kwa sasa kwa sababu baraza hilo halijawahi kumwita na kumueleza lolote.
“Nimekuwa nikisikia taarifa hizi kupitia kwenye vyombo vya habari, hivyo siwezi kuzungumza lolote hadi BASATA itakapowasiliana na mimi,”alisema.
Hata hivyo, Suma Lee alieleza kuridhishwa kwake na mapokezi ya mashabiki katika wimbo wake huo, ambao utakuwemo kwenye albamu yake mpya, aliyoipa jina la ‘Hesabu za Mapenzi’. Albamu hiyo itakuwa na nyimbo 15.

Thursday, November 17, 2011

Polisi Dom yawataka nyota saba wa Simba

KLABU ya Polisi Dodoma imeuandikia barua uongozi wa klabu ya Simba ikitaka kuwasajili wachezaji saba wa timu hiyo pamoja na aliyekuwa kocha msaidizi wa timu hiyo, Amri Said.
Wachezaji hao ni Shija Mkina, Amri Kiemba, Haruna Shamte, Salum Kanoni na wachezaji wa timu ya vijana wa chini ya miaka 20, Haruna Athumani na Edward Christopher.
Habari kutoka ndani ya Simba zimeeleza kuwa, Polisi Dodoma imeomba kuwasajili wachezaji hao katika dirisha dogo la usajili linaloendelea hivi sasa.
Mtoa habari huyo alisema, uongozi wa Polisi Dodoma umevutiwa na viwango vya wachezaji hao na kusema iwapo watafanikiwa kuwasajili, wataiimarisha timu yao.
Kuhusu Amri Said, uongozi wa Polisi umesema wanamuhitaji kocha huyo ili kulisaidia benchi la ufundi la timu hiyo kwa kuwa ana uwezo mkubwa katika masuala ya uongozi.
"Tulimuona Amri Said wakati ule akiwa kocha msaidizi na uwezo wake tunaukubali na tunaamini kuwa, akija katika timu yetu, tutapata mafanikio,“ alisema.
Kufuatia barua hiyo, uongozi wa Simba umesema unatarajia kulifikisha ombi hilo kwa kamati ya Utendaji kabla ya kutoa ridhaa ya kuwaachia wachezaji hao.

Kili Stars kukata utepe na Amavubi

MABINGWA watetezi, timu ya soka ya Tanzania Bara, Kilimanjaro Stars imepangwa kufungua dimba la michuano ya Kombe la Chalenji kwa kumenyana na Rwanda, Amavubi.
Ratiba ya michuano hiyo, iliyotolewa jana na Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) inaonyesha kuwa, mechi hiyo itapigwa kuanzia saa 10 jioni kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
CECAFA imesema, mechi za michuano hiyo sasa zitachezwa kwenye uwanja mmoja pekee wa Taifa, baada ya mkoa wa Mwanza kushindwa kutimiza masharti ya kuwa mwenyeji wa mechi zingine.
Kwa mujibu wa CECAFA, kwa siku zitachezwa mechi mbili, isipokuwa siku ya uzinduzi, ambapo itachezwa mechi moja pekee.
Ratiba inaonyesha kuwa, Novemba 25 mwaka huu, Burundi itamenyana na Somalia kuanzia saa 8 mchana) kabla ya Uganda kukipiga na Zanzibar kuanzia saa 10 jioni.
Wakati huo huo, CECAFA imesema Eritrea imejitoa kwenye michuano ya mwaka huu, kufuatia wachezaji wake wengi kutoka wanapokwenda kucheza ugenini.
Mwaka jana, wachezaji zaidi ya 11 wa timu ya Red Sea ya Eritrea walitoroka kwenye kambi ya timu hiyo siku chache kabla ya kuondoka nchini na kuomba hifadhi ya ukimbizi.
Hata hivyo, maombi ya wachezaji hao yalikataliwa kutokana na kutokidhi vigezo vinavyotakuwa na kurejeshwa kwao.
Kufuatia kujitoa kwa Eritrea, CECAFA imesema, nafasi yake sasa imechukuliwa na Namibia, ambayo itacheza kama timu mwalikwa pamoja na Malawi.
Namibia sasa ipo kwenye kundi A pamoja na mabingwa watetezi, Kilimanjaro Stars, Rwanda na Djibouti.
Michuano ya mwaka huu imedhaminiwa tena na Kampuni ya Bia ya Serengeti.
Katika hatua nyingine, Kocha Mkuu wa Kilimanjaro Stars, Charles Boniface Mkwasa leo anatarajiwa kutangaza kikosi cha timu hiyo kitakachoshiriki kwenye michuano ya Kombe la Chalenji.
Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Boniface Wambura alisema jana kuwa, Mkwasa atatangaza kikosi hicho katika mkutano wake na waandishi wa habari utakaofanyika saa sita mchana kwenye ofisi za shirikisho hilo.

Malindi yashushwa rasmi daraja

TIMU ya soka ya Malindi imeshushwa kutoka daraja la kwanza hadi la pili katika Wilaya ya Mjini, kufuatia kushindwa kutekeleza masharti ya mahakama.
Malindi ilikuwa imefungua kesi kupinga kanuni iliyotumika kuiteremsha daraja, kufuatia matokeo ya ligi ndogo iliyochezwa kwa mkondo mmoja mwanzoni mwa mwaka huu.
Katika kusikiliza kesi hiyo, mahakama iliitaka Malindi kuifutaili irejeshwe daraja la kwanza, lakini kwa masharti ya kukamilisha taratibu zote za kuwemo katika ligi.
Msemaji wa Chama cha Soka cha Zanzibar (ZFA), Hafidh Ali Tahir alisema, Malindi imeshindwa kutimiza masharti iliyopewa, ambapo ilitakiwa kufanya hivyo ndani ya wiki moja.
Baadhi ya masharti iliyopewa ni kufanya usajili wa wachezaji, kulipa ada ya mashindano na pia kujisajili kwa mrajisi wa vyama vya michezo.
Awali, Miembeni United ilikubali kuuza nafasi yake ili kuishawishi Malindi iondoe kesi iliyokuwa imeifungua mahakamani.
Tahir alisema baada ya Malindi kuwasilisha shauri lake katika Mahakama ya mkoa ya Vuga, ambayo ilitoa amri ya kusitisha ligi kuu, uongozi wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo, ulikutana na uongozi wa Malindi na ZFA, kutafuta namna ya kuimaliza kadhia hiyo nje ya mahakama.
Kufuatia kikao hicho, ambacho pia kilimjumuisha Mkurugenzi wa Miembeni, Amani Ibrahim Makungu, kiongozi huyo alikubali kuipa Malindi nafasi ya kucheza ligi kuu na timu yake icheze daraja la kwanza, kwa lengo la kufuta aibu ya kuzipeleka kesi za soka mahakamani.
“Baada ya yote hayo, ikiwa ni pamoja na kupewa nafasi ya upendeleo, Malindi imeshindwa kutimiza masharti iliyopewa, kwa hiyo ZFA inatoa tamko kuwa, timu hiyo imeteremshwa daraja la pili wilaya ya Mjini”, alifafanua.
Katika hatua nyingine, Tahir amesema kwa sasa, ZFA inajipanga kuanza ligi kuu na kwamba, taratibu zote zitapangwa katika mkutano wa kamati ya utendaji unaotarajiwa kufanyika leo kisiwani Pemba.
Kuhusu udhamini, alisema kumejitokeza taasisi iliyojitolea kutoa sare za waamuzi, kuwasafirisha pamoja na mahitaji yao mengine. Hata hivyo, alisema ni mapema kuitaja kwa vile bado inaendelea kujipanga.
Hata hivyo, alisema licha ya kuharibika kwa meli ya Sea gull na kuzuiwa, bado chama chake hakijapokea barua ya kujiondoa kwa kampuni hiyo katika udhamini wake wa ligi kuu, na kwamba makubaliano yao yapo pale pale.

Wednesday, November 16, 2011

ZFA yajitetea hati za wachezaji kuzuiwa

CHAMA cha Soka Zanzibar (ZFA) kimesema, kuzuiwa kwa hati za kusafiria za wachezaji wa Zanzibar Heroes walioko katika timu ya Taifa Stars, kulilenga kuepusha usumbufu wakati wa mechi ya kufuzu fainali za Kombe la Dunia dhidi ya Chad.
Msemaji wa ZFA, Hafidh Ali Tahir alisema hayo juzi mjini hapa alipokuwa akijibu maswali kutoka kwa waandishi wa habari katika hoteli ya Bwawani.
Tahir alisema katika mashindano ya kimataifa, hati za kusafiria za wachezaji ndizo zinazotambuliwa kama leseni, hivyo ni lazima ziwasilishwe wakati wa mechi maalumu kama za Kombe la Dunia.
Awali, mmoja wa viongozi wa ZFA, aliyefuatana na timu ya Zanzibar nchini Misri, alikaririwa akililaumu Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwa kitendo cha kuzizuia hati hizo huku viza za safari zikiwa hazijapatikana.
Akitoa ufafanuzi, Tahir alisema kwa kutambua umuhimu wa Taifa Stars, ZFA haikuona sababu ya kuwang’ang’ania wanandinga wake wa Zanzibar kwenda Misri mapema.
Alisema wachezaji hao waliondoka nchini jana kwenda Misri baada ya kumalizika kwa mchezo wa marudiano kati ya Taifa Stars na Chad uliochezwa juzi mjini Dar es Salaam.
Tahir alisema ZFA imetuma vivuli vya hati zao za kusafiria kwa TFF, ambayo ilizigongesha viza na kwamba zilishashughulikiwa na ofisa wake mmoja, aliyepelekwa huko.
Alipoulizwa kuhusu Kocha Mkuu wa Zanzibar Heroes, Stewart Hall, ambaye alikwama kusafiri timu hiyo ilipoondoka nchini Novemba 10 mwaka huu, msemaji huyo alisema, anatarajiwa kuondoka wakati wowote.
Tahir alisema hati ya kusafiria ya kocha huyo ilikuwa na makosa sehemu ya kugonga viza hivyo anatarajiwa kutumia hati ya muda.
Zanzibar Heroes imeweka kambi Misri kwa ajili ya kujiandaa na michuano ya Kombe la Chalenji, itakayoanza Novemba 25 mwaka huu katika miji ya Mwanza na Dar es Salaam.

JIM IYKE MATATANI


LAGOS, Nigeria
MCHEZA filamu nyota wa Nigeria, Jim Iyke amefikishwa mahakamani kwa tuhuma za kutapeli Naira milioni 15 za Nigeria.
Jim alifikishwa mahakamani mjini Abuja wiki iliyopita kwa tuhuma za kumtateli Habiba Abubakar.
Kabla ya Jim kufunguliwa kesi hiyo, Habiba aliwasilisha malalamiko kwa Kamanda wa Polisi wa Abuja, Agosti 8 mwaka huu, akimtaka kuchunguza tuhuma hizo.
Katika kesi hiyo, Jim anatuhumiwa kumtapeli Habiba kiasi hicho cha pesa, kupitia kampuni yake ya Untamed Records Ltd.
Imedaiwa kuwa, mara baada ya Jim kulipwa pesa hizo, aliziingiza kwenye akaunti yake binafsi na kufanya manunuzi ya vitu vya thamani sehemu mbalimbali duniani. Mlalamikaji alidai kuwa, kila alipokuwa akidai pesa hizo, mtuhumiwa alimtishia kumpiga na kumuua.
Jim alikanusha tuhuma hizo na kupewa dhamana ya Naira 500,000 na wadhamini wawili.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Desemba 9 mwaka huu itakapotajwa tena mahakamani.

Yvonne Nelson anusurika kufa


KUMASI, Ghana
MCHEZA filamu na mwanamitindo mwenye mvuto wa Ghana, Yvonne Nelson amenusurika kufa baada ya kula chakula chenye sumu.
Tukio hilo lilitokea Ijumaa iliyopita usiku, saa chache kabla ya Yvonne kupanda ndege kwenda Paris, Ufaransa.
Chanzo cha habari kimeeleza kuwa, Yvonne alikuwa akijiandaa kwenda Paris kusherehekea siku yake ya kuzaliwa, akiwa na rafiki zake.
“Ilikuwa saa 6.30 usiku Ijumaa, alikimbizwa hospitali kwa ajili ya kupata tiba. Alielezwa kwamba, alikula chakula chenye sumu,”kilisema chanzo hicho.
Akithibitisha tukio hilo, Yvonne alisema kupitia simu yake ya mkononi kwamba, anamshukuru Mungu kwa kuyanusuru maisha yake.
“Moja ya zawadi za kuzaliwa kwangu ilikuwa sindano. Mungu awajalie kila la heri,”alisema.
Kwa sasa, Yvonne yupo mjini Paris akishiriki katika kazi za miradi mbalimbali.
Mbali na kucheza filamu, Yvonne ni mmoja wa wanamitindo maarufu nchini Ghana, akishiriki kuonyesha mavazi ya wabunifu mbalimbali wa kimataifa.

IRENE: Sijawahi kufikiria kuolewa na AY


MSANII machachari wa filamu nchini, Irene Uwoya amesema kamwe hajawahi kufikiria kufunga ndoa na msanii nyota wa muziki wa kizazi kipya, Ambwene Yesaya.
Irene alisema hayo mwishoni mwa wiki iliyopita, alipokuwa akihojiwa na mtangazaji Salama Jabir katika kipindi kipya cha sanaa kilichorushwa hewani na kituo cha televisheni cha East Africa.
Alisema yeye na msanii huyo, maarufu kwa jina la AY, walikuwa na urafiki wa kawaida kutokana na ukaribu wa mama zao.
“Mimi na AY ni marafiki tu wa kawaida kutokana na urafiki waliokuwa nao mama zetu na kamwe hatukuwahi kufikiria kufunga ndoa,”alisema.
Irene alisema pia kuwa, kamwe hajawahi kunywa pombe na kulewa tilalila, japokuwa ni mnywaji mzuri.
Alisema siku zote anapokunywa pombe, amekuwa mwangalifu kuhakikisha kuwa, anapofikisha idadi fulani ya chupa, haendelei zaidi.
“Ndio sababu sijawahi kulewa tilalila, ndivyo kichwa changu kilivyo,”alisema.
“Hata nilipojifungua kwa operesheni, shindano ya ganzi haikufanyakazi sawa sawa, nilikuwa na fahamu zangu. Sielewi ni kwa nini,”aliongeza.
Irene alisema burudani yake kubwa kila anapokuwa nyumbani ni kutazama filamu, zikiwemo alizozitunga na kushiriki kucheza.
Alisema licha ya kuendelea na fani hiyo, amekuwa akiipa kipaumbele kikubwa familia yake, hasa malezi kwa mtoto wake, Krishna.

MAJUTO: Vichekesho vimenipa manufaa kimaisha


KWA watazamaji wa kipindi cha Comedy Show, kinachoonyeshwa kila siku za Alhamisi usiku, kupitia kituo cha televisheni cha Channel Ten, jina la King Majuto sio geni kwao.
Ni mmoja wa wasanii wakongwe wa maigizo na vichekesho nchini, lakini akiwa bado na kipaji cha hali ya juu katika kutunga vichekesho vinavyoonyeshwa kupitia katika kipindi hicho.
Umahiri wa Majuto katika fani hiyo haukuanza miaka ya hivi karibuni kama watu wengi wanavyofikiria. Safari ya Majuto ni ndefu, ikiwa ni pamoja na kukutana na vikwazo vingi vilivyomkatisha tamaa na kumfanya ajiweke pembeni ya fani hiyo.
Kama fani ya maigizo na vichekesho ingekuwa ikiwatajirisha wasanii wa fani hiyo, basi Majuto angekuwa bonge la milionea. Kabla ya kuanzishwa kwa vituo vya televisheni na wasanii kupata fursa ya kurekodi kanda za video, Alikuwa ametunga zaidi ya maigizo 1,000, lakini hakuna chochote cha maana alichoambulia.
Jina lake kamili ni Amri Athumani. Alipewa jina la King Majuto kutokana na umahiri wake katika fani hiyo na pia kumudu vyema kucheza nafasi alizokuwa akijipangia.
Majuto amepitia makundi mengi ya sanaa za maonyesho kama vile DDC Kibisa, Wazazi Dancing Troup na mengineyo kadhaa akiwa na Mzee Pembe, Mzee Uzegeni, Tomato na wengineo.
Akiwa ndani ya vikundi hivyo, alishirikiana navyo kuonyesha maigizo kwenye kumbi mbalimbali za burudani za mjini Dar es Salaam kama vile DDC Kariakoo, DDC Magomeni Kondoa, Super Mini, Temeke, Diluxe Bar na zinginezo.
Hata hivyo, kutokana na fani hiyo kutokuwa na manufaa makubwa kwa wasanii wake, Majuto aliamua kujiweka kando na kurejea nyumbani kwake Tanga kwa ajili ya kuangalia shughuli zingine za kufanya.
Kuanzishwa kwa vituo vingi vya televisheni nchini pamoja na wasanii wa fani hiyo kupata fursa ya kutengeneza kanda za video za vichekesho, ndiko kulikompa fursa Majuto ya kurejesha makali yake na pia kuanza kunufaika na fani hiyo.
Hadi sasa, Majuto ametengeneza kanda nyingi za vichekesho kupitia Kampuni ya Al-Riyami ya mjini Dar es Salaam. Baadhi ya kanda hizo ni pamoja na Inye, ambayo imepigwa marufuku kutokana na kukiuka maadili ya kitanzania.
Nyingine ni Ngoma kubwa, In the Court, Inye Plus na zinginezo, ambazo zimetokea kuwakuna mashabiki wengi wa fani hiyo kutokana na kujaa vichekesho vya kuvunja mbavu.
Akizungumza na Burudani mjini Tanga hivi karibuni, Majuto alisema anamshukuru Mungu kwamba fani hiyo kwa sasa imeyainua maisha yake, tofauti na miaka iliyopita.
Majuto alisema japokuwa sanaa ya maigizo na vichekesho imeanza kumlipa uzeeni, anamshukuru Mungu kwa kuweza kunufaika na kipaji chake kuliko angekufa masikini.
“Pamoja na misukosuoko yote niliyoipata kupitia sanaa ya vichekesho, namshukuru Mungu kwamba nimefanikiwa kujenga nyumba ya kuishi na pia ninamiliki magari mawili,”alisema.
Licha ya kukabiliwa na vikwazo vingi katika sanaa hiyo, Majuto alisema kamwe hakufikiria kuiacha kwa sababu ya umri wake kuwa mkubwa.
Majuto alisema anamshukuru Mungu kwamba pamoja na umri alionao, ana uwezo wa kuigiza nafasi zote, ikiwa ni pamoja na ya kijana wa kawaida, muhuni, mvuta unga na mzee.
Alisema anawashangaa watu wanaofikiria kwamba, atastaafu kazi hiyo hivi karibuni kutokana na uzee. Alisema watu hao wanasahau kwamba, hiyo ndiyo kazi aliyopangiwa na Mungu katika maisha yake.
“Nawashangaa, wanadhani nitaacha kuigiza leo au kesho, eti kwa sababu umri wangu mkubwa, mbona kwenye mashindano mbalimbali nawafunika,"alisema Majuto.
Msanii huyo mkongwe alisema, ameshiriki kwenye mashindano mengi ya vichekesho na kuibuka na ushindi, lakini kamwe hajawahi kupewa zawadi zilizoahidiwa na waandaaji.
Kutokana na kutapeliiwa huko, Majuto amesema kamwe hatarajii kushiriki tena katika mashindano ya aina hiyo kwa sababu amebaini kuwa, waandaaji huyaandaa kwa lengo la kuwatumia kujinufaisha.
King Majuto anao watoto na wajukuu kadhaa, lakini hapendi kutaja idadi yao. Alisema hayo ni mambo yanayohusu maisha yake binafsi.

MANARA: Tumepiga hatua kubwa kimaendeleo ya soka

Kitwana Manara (kushoto) akiwa na Peter Tino katika moja ya hafla zilizoandaliwa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).


KAMA kuna mwanasoka aliyewahi kuweka rekodi ya pekee na ya aina yake hapa nchini, si mwingine zaidi ya mkongwe Kitwana Manara.
Manara ndiye mchezaji pekee aliyeweza kucheza nafasi ya kipa kwenye kikosi cha timu ya taifa, Taifa Stars na nafasi ya mshambuliaji kwenye klabu yake ya Yanga.
Mkongwe huyo pia ndiye mchezaji pekee aliyeweka rekodi ya kucheza soka kwa miaka mingi kuliko mchezaji mwingine yeyote Tanzania. Alianza kucheza soka mwaka 1960 na kutundika daruga zake ukutani mwaka 1980.
Manara alianza kuvaa jezi za Taifa Stars mwaka 1961 akitokea klabu ya Cosmo ya Dar es Salaam. Alistaafu kuichezea timu hiyo mwaka 1975 akiwa klabu ya Yanga.
Alikuwa miongoni mwa wachezaji wa Yanga walioiwezesha timu hiyo kuwa ya kwanza nchini kufuzu kucheza robo fainali ya michuano ya klabu bingwa Afrika mara mbili, 1969 na 1970.
Katika hatua zote hizo mbili, Yanga ilitolewa na Asante Kotoko ya Ghana, ambapo katika robo fainali ya mwaka 1969, iliondoshwa kwa njia ya kura ya shilingi baada ya matokeo ya jumla kuwa sare ya bao 1-1.
Katika robo fainali ya pili mwaka 1970, Yanga ilikutana tena na Asante Kotoko, ambapo katika mechi ya awali, zilitoka sare ya bao 1-1 na katika mechi ya marudiano, hazikufungana.
Mshindi wa pambano hilo ilibidi apatikane katika muda wa nyongeza, lakini kutokana na giza kutanda uwanjani, mechi ilivunjika dakika ya 19 na hivyo kuhamishiwa kwenye uwanja huru wa mjini Addis Ababa, Ethiopia.
Katika mechi hiyo ya tatu, Yanga ilikubali kipigo cha mabao 2-0 kutoka kwa Asante Kotoko na kutolewa kwenye hatua hiyo. Kikosi cha Yanga wakati huo kilikuwa chini ya Victor Stanculescu kutoka Romania.
Manara pia alikuwa miongoni mwa wachezaji walioiwezesha Taifa Stars kufuzu kucheza michezo ya All Africa Games mwaka 1973 na kutinga nusu fainali, ambapo ilitolewa na Algeria baada ya kuchapwa mabao 2-1.
“Kwa kweli kama ni rekodi ya mwanasoka aliyecheza soka kwa miaka mingi hapa nchini na kwa nafasi mbili tofauti, hakuna anayeweza kuifikia rekodi yangu,”alisema. “Mimi nilianza kuichezea timu ya taifa kuanzia kwenye michuano ya Gossage hadi ilipobadilishwa jina na kuitwa Chalenji.”
Akizungumza na Uhuru hivi karibuni kuhusu mafanikio ya soka katika miaka ya 50 ya Uhuru, Manara alisema Tanzania imepiga hatua kubwa na kupata mafanikio ya kuridhisha.
Akitoa mfano, Manara alisema japokuwa kiwango cha uchezaji soka miaka ya nyuma kilikuwa juu ikilinganishwa na hivi sasa, kuwepo kwa vifaa vingi vya michezo na viwanja vya kisasa vya kuchezea mchezo huo ni miongoni mwa mafanikio makubwa yaliyopatikana.
Alisema miaka ya nyuma, vifaa vya michezo vilikuwa vichache na viwanja vilivyotumika kuchezea mchezo huo vilikuwa vya kawaida.
“Hivi sasa, timu yetu ya taifa imepata udhamini mkubwa, wachezaji wanalipwa vizuri, klabu zinamiliki viwanja vyao vya kuchezea soka, haya yote kwangu mimi ni mafanikio makubwa,”alisema.
Manara pia alieleza kufurahishwa kwake kuona Taifa Stars ikipata maandalizi kama ilivyo kwa baadhi ya nchi za mataifa ya Ulaya huku ikipatiwa huduma zote muhimu na wachezaji kulipwa vizuri.
Alisema miaka ya nyuma, ilikuwa vigumu kwa mashabiki kujitokeza kwa wingi kuishangilia timu hiyo kila ilipocheza ama kuhamasika na kuvaa fulana zenye rangi ya bendera ya taifa.
Manara alisema pia kuwa, soka inayochezwa hivi sasa ni ya kasi ikilinganishwa na miaka ya nyuma, lakini baadhi ya vitu vinavyofanywa na wanasoka maarufu duniani kama vile Lionel Messi wa Barcelona ya Hispania si vigeni kwa Tanzania.
Aliwataja baadhi ya wanasoka wa zamani waliokuwa na uwezo wa kucheza na mpira wanavyotaka, kupiga chenga na kupangua idadi kubwa ya mabeki kwa wakati mmoja kuwa ni pamoja na Mbwana Abushiri, Emily Kondo, Arthur Mambeta, Sunday Manara na Abdalla Kibadeni.
Alisema uwezo wa wanasoka hao haukuweza kutambulika kimataifa kutokana na kutokuwepo kwa vyombo vingi vya habari kwa ajili ya kuwatangaza. Alisema vyombo vilivyokuwepo wakati huo kama vile magazeti, vilikuwa vichache na teknolojia ya televisheni haikuwepo.
Manara alisema Tanzania ni nchi pekee kwa nchi za ukanda wa Afrika Mashariki iliyoweza kutoa wanasoka wengi nyota, ikilinganishwa na nchi za Kenya na Uganda.
Akizungumzia uongozi wa soka nchini, Manara alisema viongozi wa zamani wa klabu hawakuwa na elimu kubwa, lakini waliweza kubuni vitu vingi na kuziletea mafanikio makubwa klabu zao.
Akitoa mfano, alisema viongozi wa Yanga waliweza kununua nyumba mtaa wa Mafia kwa sh. milioni 11 kutokana na mapato ya sh. milioni 20 katika mechi kati yao na Abaluya ya Kenya na siku hiyo wachezaji hawakulipwa hata nauli.
“Hivyo utaona kuwa, uongozi wa zamani ulikuwa wa kujitolea zaidi na viongozi walihakikisha kila mchezaji anatafutiwa kazi na walicheza kwa moyo kwa sababu walikuwa wanachama wa klabu wanazochezea hivyo ilikuwa vigumu kuzihujumu,”alisema.
Alisema viongozi wa sasa wa klabu wana elimu kubwa, lakini wanakosa ubunifu na mashabiki wa klabu kongwe za Simba na Yanga wamekosa imani kwa viongozi wao, hasa timu zao zinapofungwa katika mechi muhimu.
Mkongwe huyo alisema ubunifu wa viongozi wa zamani ulianza kutoweka miaka ya 1976, ambapo klabu za Simba zilianza kutawaliwa na migogoro mingi, iliyosababisha zigawanyike.
Alisema migogoro hiyo ndiyo iliyosababisha klabu ya Yanga kugawanyika na kuzaliwa Pan African na ile ya Simba nayo kugawanyika na kuzaliwa Nyota Nyekundu.
Manara alisema migogoro ya mara kwa mara ndani ya klabu hizo, ilichangia kwa kiasi kikubwa kudumaza maendeleo ya soka na timu ya taifa kwa vile Simba na Yanga ndizo zinazotoa mchango mkubwa kwenye timu ya taifa.
“Asikudanganye mtu, mafanikio ya Taifa Stars yanapaswa kuanzia klabuni. Kukiwa na migogoro kwenye klabu hizo mbili, timu yetu ya taifa nayo itakuwa mbovu,”alisema.
Manara ameupongeza uongozi wa sasa wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwa kuleta mageuzi makubwa katika mchezo huo, ikiwa ni pamoja na kurejesha nidhamu kwa viongozi na kuleta utendaji mzuri.
“Kwa kweli mabadiliko katika uongozi wa chama cha soka yameonekana. Zamani pale uwanja wa Karume kulikuwa na jengo dogo tu kwa ajili ya ofisi za chama, lakini hivi sasa kuna ghorofa na uwanja wa kisasa wa mazoezi. Haya ni mafanikio makubwa,”alisema.
“Serikali nayo imejitahidi sana kutuletea makocha wa kigeni kwa ajili ya timu ya taifa na wachezaji wamekuwa wakihamasika kuichezea. Haya nayo ni mafanikio makubwa,”aliongeza.
Manara alimmwagia sifa kemkem Rais wa TFF, Leodegar Tenga kuwa ni kiongoni pekee aliyeleta mageuzi makubwa katika uongozi wa soka nchini na pia kuleta heshima kwa chama hicho.
Alisema nidhamu ndani ya shirikisho hilo imekuwa kubwa na kamati zimeachwa zifanyekazi zake kwa uhuru mkubwa bila ya kuingiliwa.
“Kwa kweli hajatokea kiongozi aliyeleta amani na utulivu katika chama cha soka kama Tenga. Waswahili wanasema, mnyonge mnyongeni, lakini haki yake mpeni. Tenga anastahili pongezi,”alisema.
Hata hivyo, Manara alisema wapo viongozi wengine wa chama hicho waliofanya vizuri huko nyuma, lakini hakuna anayeweza kufikia rekodi ya Tenga.
Manara amelitaka shirikisho hilo kufanya jitihada zaidi liwe na uwanja wake wa kuchezea soka kwa ajili ya kuongeza mapato yake, tofauti na ilivyo sasa, ambapo linategemea zaidi mgawo wa mechi za ligi kuu na za kimataifa.
Pia ameiomba serikali ifikirie kupunguza kodi kwenye vifaa vya michezo ili vijana wengi zaidi waweze kumudu kuvinunua na hivyo kuongeza hamasa kwao ya kushiriki katika mchezo huo.
Manara pia ametoa mwito kwa viongozi wa klabu na vyama vya soka, wawe wabunifu wa vyanzo vya mapato na uendeshaji wa mchezo huo kisasa zaidi badala ya kuweka mbele maslahi yao binafsi.
“Nawaomba wanasoka wetu nao, waone thamani ya kucheza soka kwa sababu hivi sasa mpira ni ajira na mchezaji anaweza kulipwa mamilioni ya shilingi kwa ajili ya usajili pekee,”alisema.
“Kama mchezaji unaweza kulipwa hata milioni 60 kwa msimu, unapaswa kuuheshimu mpira katika maisha yako kwa sababu ndiyo ajira yako,”aliongeza.
Amewataka viongozi wa klabu kuzithamini timu za vijana kwa vile ndizo chimbuko la wanasoka. Alisema timu hizo zinapaswa kupewa huduma zote muhimu kama ilivyo kwa timu za wakubwa ikiwa ni pamoja na kuzipatia usafiri wa uhakika.
Manara alianza kucheza soka katika timu za mitaani za Sambwisi, Young Boys, Cosmo, TPC ya Arusha, Feisal na baadaye Yanga na Pan African. Alistaafu rasmi kucheza soka mwaka 1983 akiwa Yanga, ambayo katika miaka miwili ya mwisho, aliifundisha akiwa kocha mchezaji.

Wednesday, November 9, 2011

TZ Bara kundi moja na Rwanda, Ethiopia

Katibu Mkuu wa Baraza la Vyama vya Michezo Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), Nicholas Musonye (kulia) akitangaza timu zitakazoshiriki katika michuano ya mwaka huu ya Kombe la Chalenji, alipozungumza na waandishi wa habari mjini Dar es Salaam jana. Wa pili kulia ni Rais wa baraza hilo, Leodegar Tenga, Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Kampuni ya Bia ya Serengeti (SBL), Teddy Mapunda na Meneja wa bia ya Tusker, Ritha Chaki. (Na mpiga picha wetu)


MALAWI ndio timu pekee kutoka nje ya ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, iliyoalikwa kushiriki katika michuano ya mwaka huu ya Kombe la Chalenji.
Katibu Mkuu wa Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), Nicholas Musonye alisema mjini Dar es Salaam jana kuwa, timu 12 zinatarajiwa kushiriki katika michuano hiyo.
Musonye alisema michuano hiyo imepangwa kuanza Novemba 25 na kumalizika Desemba 10 mwaka huu katika miji ya Mwanza na Dar es Salaam.
“Tumeialika timu hii makusudi kwa lengo la kusisimua maendeleo ya soka katika ukanda huu. Ni matumaini yetu kuwa, timu hii italeta changamoto katika michuano hii na kuifanya iwe na ushindani mkubwa,”alisema.
Kwa mujibu wa Musonye, timu hizo 12 zimepangwa katika makundi matatu yenye timu nne kila moja. Aliyataja makundi hayo kuwa ni A litakalokuwa na timu za Tanzania Bara, Rwanda, Ethiopia na Djibouti.
Kundi B litakuwa na timu za Uganda, Burundi, Somalia na Zanzibar wakati kundi C litakuwa na timu za Sudan, Kenya, Malawi na Eritrea.
Katibu Mkuu huyo wa CECAFA alisema, ratiba kamili ya michuano hiyo itatangazwa keshokutwa.
Musonye alisema lengo la CECAFA ni kuona kiwango cha soka katika nchi za ukanda huu kinapanda na mojawapo ya timu zake, inafuzu kucheza fainali za Kombe la Dunia za 2014.
Michuano ya mwaka huu imedhaminiwa na Kampuni ya Bia ya Serengeti (SBL) kupitia bia yake ya Tusker. Kampuni hiyo itatumia sh. milioni 823 kudhamini michuano hiyo.
Naye Meneja wa bia ya Tusker, Rita Mlaki aliwataka watanzania kujitokeza kwa wingi wakati wa michuano hiyo kuishangilia Tanzania Bara na Zanzibar ili ziweze kufanya vizuri.

Taifa Stars kukipiga na Chad kesho

TIMU ya soka ya Taifa, Taifa Stars inashuka dimbani kesho mjini N’Djamena kumenyana na timu ya Taifa ya Chad katika mechi ya kuwania kufuzu kucheza fainali za Kombe la Dunia za 2014.
Taifa Stars iliondoka nchini jana saa tisa alasiri kwa ndege ya Shirika la Kenya Airways, ikiwa na msafara wa watu 40, wakiongozwa na mjumbe wa kamati ya utendaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Eliud Mvella.
Msafara wa timu hiyo ulitarajiwa kuwasili N’Djamena saa 1.15 usiku kwa saa za Chad, sawa na saa 3.15 usiku kwa saa za Tanzania.
Katika msafara huo, wamo wachezaji 21 waliokuwepo kambini kwa ajili ya kujiandaa na pambano hilo, sita kutoka benchi la ufundi wakiongozwa na Kocha Jan Poulsen na wajumbe wawili kutoka Baraza la Michezo la Taifa (BMT).
Taifa Stars iliagwa juzi saa moja usiku kwa kukabidhiwa bendera ya Taifa na Mwenyekiti wa BMT, Dioniz Malinzi. Hafla hiyo ilifanyika kwenye hoteli ya New Africa, Dar es Salaam.
Katika hafla hiyo, Malinzi aliwataka wachezaji hao kucheza kufa na kupona ili waweze kushinda mchezo huo na kuahidi kuwalipia gharama za matibabu wale watakaoumia.
Akiwasilisha salamu zake kwa wachezaji hao kupitia njia ya video, Waziri Mkuu Mizengo Pinda alisema ushindi ni muhimu ili kusherehekea vyema miaka 50 na uhuru.
Pinda aliwazawadia wachezaji hao sh. milioni 10 kwa aili ya kuwaongezea ari ili waweze kushinda pambano hilo.
Timu hiyo inaundwa na makipa Juma Kaseja (Simba) na Mwadini Ally (Azam). Mabeki ni Aggrey Morris (Azam), Juma Nyoso (Simba), Idrissa Rajab (Sofapaka, Kenya), Erasto Nyoni (Azam), Godfrey Taita (Yanga) na Juma Jabu (Simba). Viungo ni Henry Joseph (Kongsvinger IL, Norway), Nurdin Bakari (Yanga), Shabani Nditi (Mtibwa Sugar), Abdi Kassim (DT Long An, Vietnam), Ramadhan Chombo (Azam) na Shomari Kapombe (Simba). Washambuliaji ni Nizar Khalfan (Vancouver Whitecaps, Canada), Mrisho Ngassa (Azam), Mbwana Samata (TP Mazembe, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo- DRC), Athuman Machupa (Vasalund IF, Sweden), Hussein Javu (Mtibwa Sugar) na Thomas Ulimwengu (TP Mazembe, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo- DRC).
Taifa Stars inatarajiwa kurejea nchini Novemba 13 saa 7.25 mchana kwa ndege ya Shirika la Ethiopia na kwenda moja kwa moja kambini kujiandaa kwa mchezo wa marudiano utakaopigwa Novemba 15 mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.