KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, November 2, 2011

Simba yapata kocha mpya


KLABU ya Simba kesho inatarajiwa kumtangaza rasmi kocha mkuu mpya, atakayechukua nafasi ya kocha wa zamani, Moses Basena kutoka Uganda.
Habari kutoka ndani ya Simba zilieleza jana kuwa, kocha huyo atatangazwa baada ya uchambuzi utakaofanywa na kikao cha kamati ya utendaji.
Kwa mujibu wa habari hizo, makocha watatu wamependekezwa kurithi mikoba ya Basena, ambaye mkataba wake umesitishwa.
Hata hivyo, kocha anayepewa nafasi kubwa ni Cirkovic Milovan kutoka Serbia, ambaye aliwahi kuifundisha Simba mwaka juzi kabla ya kuondoka katika mazingira ya kutatanisha.
Makocha wengine wanaopewa nafasi hiyo, majina yao hayakuweza kupatikana, lakini imeelezwa kuwa, waliwahi kuzifundisha timu za Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini na Enyimba ya Nigeria.
Milovan anapewa nafasi kubwa ya kurejea Simba kutokana na kuungwa mkono na wajumbe wengi wa kamati ya utendaji.
Kocha huyo kutoka Serbia aliwahi kuifundisha Simba kwa miezi mitatu, akiziba pengo la Patrick Phiri kutoka Zambia, ambaye alichelewa kurejea nchini kutoka kwao Zambia, alikokwenda kwa mapumziko.
Simba imesitisha mkataba wa Basena, siku chache baada ya kuchapwa bao 1-0 na watani wao wa jadi Yanga, katika mechi ya mzunguko wa kwanza wa ligi kuu ya Tanzania Bara, iliyochezwa mwishoni mwa wiki iliyopita kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Kocha huyo alikuwa akilalamikiwa na baadhi ya wachezaji kwa madai kuwa, mfumo wake wa ufundishaji soka haueleweki.
Kwa sasa, Simba ipo chini ya mchezaji wa zamani wa timu hiyo, Selemani Matola huko Basena akiwa amerejea kwao Uganda kwa madai ya kuuguliwa na mama yake mzazi.
Mbali na kikao cha kesho kujadili ujio wa kocha mpya, pia kitajadili usajili wa nyongeza unaotarajiwa kuanza hivi karibuni. Kwa mujibu wa ratiba, usajili huo ulipaswa kuanza Novemba Mosi.

No comments:

Post a Comment