KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Tuesday, November 1, 2011

KAMATI YA KUSIMAMIA LIGI KUU

Uamuzi wa kutenganisha usimamizi wa Ligi Kuu na mashindano mengine haukufanyika siku za karibuni. Ulifanyika mwaka 2006 wakati Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) wakati ule ilipoamua kuwa hatua zichukuliwe kuboresha Ligi Kuu nchini na kupanga utaratibu mzuri wa kuisimamia peke yake.
TFF iliomba msaada wa kitaalamu kutoka FIFA ambayo ilikubali kutusaidia kwa kutujumuisha miongoni mwa wanachama wake watakaofaidika na Mpango Maalum wa Kuboresha Ligi Kuu za nchi wanachama wa FIFA. Tanzania ilikuwa miongini mwa nchi nane (8) za mwanzo kufaidika na mpango huo.
Semina ya kwanza ya FIFA juu ya uboreshaji wa Ligi Kuu iliyojumuisha viongozi wa klabu za Ligi Kuu ilifanyika mwaka 2007. Semina ile ilisisitiza haja ya kujenga msingi imara wa kuwa na Ligi Kuu bora.
Pamoja na mambo makubaliano yalifikiwa kuwa na Ligi ya Daraja la Kwanza ambayo itatoa fursa kwa timu kujitayarisha kwa ushindani endapo zitafanikiwa kuingia Ligi Kuu. Semina ya pili ya FIFA ilifanyika mwaka 2009 mjini Bagamoyo na ya tatu ilifanyika mjini Dar es Salaam mwaka 2010 mjini Dar es Salaam.
Semina hizi zilizaa makubaliano maalum, yanayofahamika kama ‘Maazimio ya Bagamoyo’ yanayozitaka timu za Ligi Kuu kutekeleza hatua kwa hatua masuala kadhaa muhimu kwa kuboresha utendaji wake na kujenga msingi wa kuendeleza kiwango cha mpira katika klabu. Hii ni pamoja na kuwa na watendaji wa kuajiriwa, timu za watoto, viwanja vya kuchezea, kufanya ukaguzi wa hesabu zao na kadhalika.
Katika semina hizi suala la usimamizi wa Ligi Kuu lilijadiliwa na kukubaliana kuwa waangalifu wa utaratibu tutakaoutumia. Msuguano wa uongozi baina ya kampuni zinazoongoza ligi na vyama vya soka nchini Afrika Kusini, Kenya na Uganda zilitufanya kuamua kuwa tusijiingize katika utaratibu wa kuwa na kampuni kama chombo cha kusimamia Ligi Kuu nchini bila ya kufanya utafiti wa kina.
Hivyo tukaiomba tena FIFA itusaidie Semina kwa ajili ya utaratibu utakaofaa, ikiwa na kuuagalia utaratibu unaotumika nchini Ujerumani (The Bundesliga Model) pamoja na miundo mengine ili tuafikiane juu ya utatibu unaofaa. Ipo haja pia ya kuangalia utaratibu unaotumiwa na nchi nyingine barani Afrika kama Ghana, Ivory Coast, Algeria, Tunisia, Misri na hata Sudan ambazo zina klabu zinazofanya vizuri katika mashindano ya Afrika.
Lakini tuliafikiana kuwa wakati tukifanya utafiti huo hadi kuafikiana, ni vyema tukaanza kuisimamia Ligi Kuu yetu bila kuichanganya na mashindano mengine haraka iwezekanavyo. Tukaamua tuanze kwa kuunda Kamati ya Ligi Kuu itakayojumuisha kwa kiasi kikubwa wawakilishi wa klabu za Ligi hiyo na kuipa majukumu yote ya usimamizi.
Kabla ya kutekeleza uamuzi huu, Kamati ya Utendaji iliomba na kupata ridhaa ya Mkutano Mkuu wa TFF wa 2010, kwa mujibu wa Katiba ya TFF. Hatimaye, majina ya wajumbe wa Kamati na majukumu ya Kamati kupitishwa na Kamati ya Utendaji katika kikao chake cha tarehe 27 Oktoba 2011.
Kwa maneno mengine, hatua iliyochukuliwa wiki iliyopita ni utelelezaji wa maagizo ya Mkutano Mkuu. Majina ya wajumbe wa Kamati na Majukumu yake yameambatanishwa. Ukiangalia majina ya wajumbe wa Kamati, utaona kuwa wote wametokana kwa namna moja au nyingine na klabu za Ligi Kuu na wanauelewa mkubwa sana wa mahitaji na matakwa ya klabu za Ligi Kuu na mchezo wa mpira kwa jumla.
Pia wapo wawakilishi wa klabu za Daraja la Kwanza kwa ajili ya kutoa michango juu ya mahitaji na matakwa ya klabu hizo. Kamati imepewa majukumu yote ambayo chombo chochote kile kitakachoamuliwa hapo baadae kitapewa. Kamati imepewa miaka miwili kutekeleza majukumu yake. Kipindi hiki kinachukuliwa kuwa cha mpito kuelekea mfumo/utaratibu muafaka wa kuisimamia Ligi Kuu.
Nimekuwa nikifuatilia mjadala huu kwa karibu sana kutokana na umuhimu wa suala hili kwa maendeleo ya mpira wetu. Mara nyingi imekuwa ikiwekwa kana kwamba upo uwezekano wa Ligi Kuu kuendeshwa nje ya mamlaka ya TFF.
Ni vyema wadau na wapenzi wa mpira wakafahamu kuwa kwa mujibu wa Ibara ya 18 ya Katiba ya FIFA, mashindano yote au kikundi chochote cha mpira wa miguu katika nchi wanachama wa FIFA, lazima yafanywe chini ya kivuli na uangalizi wa chama mwanachama. Kwa hiyo bni vyema ikahamika kuwa chombo chochote kile tutakachokubaliana kusimamia Ligi Kuu lazime kiwe chini ya uangalizi wa TFF.
Ningependa kuwahakikisha wadau wa mpira nchini kuwa TFF itafanya kila linalowezekana kusaidia mchakato utakaotupatia chombo muafaka cha kusimamia Ligi Kuu nchini kwa faida ya mchezo wa mpira nchini.
Tuhakikisha tunakuwa na utaratibu utakaoondoa uwezekano wa msunguano wa aina yoyote kati ya chombo hicho na vingine vya TFF na kuwa utafaidisha si tu timu za Ligi Kuu na Daraja la Kwanza bali mchezo wa mpira kwa jumla.
Ni matumaini makubwa kuwa wajumbe tuliowachagua watafanya kazi waliyopewa kwa ufanisi mkubwa na watatimiza majukumu waliyopewa. Ni matarajio yangu pia kuwa wadau wa mpira watatoa ushirikiano kufanikisha azma hii muhimu kwa maendeleo ya mpira wa miguu nchini.
Leodegar C Tenga
RAIS TFF

KAZI ZA KAMATI YA KUSIMAMIA LIGI KUU
1. Kuthibitisha ratiba
2. Kuthibitisha makamishna wa mechi (match commissioners)
3. Kupitia orodha ya waamuzi
4. Kusimamia na kufuatilia utekelezaji wa majukumu ya Azimio la Bagamoyo
5. Kuhakikisha Kanuni za Ligi zinatekelezwa (Ligi Kuu na Ligi Daraja la Kwanza)
6. Kusimamia na kufuatilia Ligi Kuu na Ligi Daraja la Kwanza
7. Kuthibitisha adhabu kwa makosa ya kikanuni ambayo hayakatiwi rufani
8. Kuandaa bajeti ya Ligi Kuu na Ligi Daraja la Kwanza
9. Kufuatilia/kusimamia fedha za Ligi Kuu na Ligi Daraja la Kwanza
10. Kuandaa semina kwa ajili ya klabu
11. Kuitangaza (Marketing) Ligi Kuu
12. Kupendekeza njia muafaka kuelekea chombo muafaka cha Kusimamia Ligi
13. Kupendekeza marekebisho kwenye Kanuni

WAJUMBE WA KAMATI YA LIGI

1. Wallace Karia- Mjumbe wa Kamati ya Utendaji (TFF- Club)- Mwenyekiti
2. Said Mohamed- Azam - M/Mwenyekiti
3. Damas Ndumbaro- Mwanasheria - Mjumbe
4. Yahya Ahmed- Kagera Sugar - Mjumbe
5. Maj. Charles Mbuge- JKT Ruvu Stars - Mjumbe
6. Steven Mnguto- Coastal Union - Mjumbe
7. Geoffrey Nyange- Simba - Mjumbe
8. Seif Ahmed- Yanga - Mjumbe
9. ACP Ahmed Msangi- Polisi Dar - Mjumbe
10. Henry Kabera- Majimaji - Mjumbe

Leodegar C Tenga
RAIS TFF

No comments:

Post a Comment