KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, March 29, 2012

Simba kutua Algeria Jumanne

KIKOSI cha wachezaji 20 na viongozi saba wa klabu ya Simba kinatarajiwa kuondoka nchini Jumatatu kwenda Algeria kwa ajili ya mechi ya marudiano ya michuano ya Kombe la Shirikisho dhidi ya ES Setif.
Ofisa Habari wa Simba, Ezekiel Kamwaga alisema mjini Dar es Salaam jana kuwa, timu hiyo itaondoka kwa ndege ya Shirika la Ndege la Egypt Air na kulala Misri siku moja.
Kamwaga alisema watalazimika kulala Misri kwa siku moja kwa ajili ya kubadili ndege itakayowapeleka Algeria. Alisema timu hiyo itaondoka Misri siku ya Jumanne.
Pambano hilo la marudiano kati ya Simba na ES Setif limepangwa kufanyika kati ya Aprili 6,7 na 8 katika mji wa Setif.
Kamwaga alisema wameamua kwenda Algeria mapema ili wachezaji waweze kuizoea hali ya hewa ya huko, ambayo kwa sasa ni baridi kali.
Simba inakwenda Algeria ikiwa kwenye mazingira mazuri ya kusonga mbele baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 katika mechi ya awali iliyochezwa wiki iliyopita mjini Dar es Salaam.
"Timu itakwenda Algeria ikiwa na wachezaji 20 na viongozi saba, lakini tunaamini idadi inaweza kuwa kubwa zaidi kwa sababu wapo wanachama na mashabiki wengi waliojitokeza kutaka kwenda kutushangilia,”alisema.
Taarifa zilizopatikana wiki hii kutoka katika mji wa Setif zimeeleza kuwa, baridi ya huko kwa sasa ni nyuzijoto 13 hadi 15.
Kamwaga alisema kwa sasa, timu inaendelea na mazoezi kwa ajili ya mechi yao ya ligi kuu dhidi ya African Lyon, itakayochezwa keshokutwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Alisema wachezaji wote wapo katika hali nzuri, isipokuwa beki Juma Jabu, ambaye anaendelea kupatiwa matibabu baada ya kuumia mguu.
"Jabu anaendelea vizuri, lakini sina hakika kama ataweza kwenda Algeria. Kulingana na taarifa ya daktari wa timu, nadhani ataanza mazoezi Jumatatu,” alisema Kamwaga.
Simba imeweka kambi kwenye hoteli ya Mbamba Beach iliyopo Kigamboni, Dar es Salaam.

Ommy Dimples apewa shavu na DJ Cleo

BAADA ya kutamba na kibao chake cha Nainai, msanii machachari wa muziki wa kizazi kipya nchini, Ommy Dimpoz ameamua kurekodi wimbo mwingine mpya.
Akizungumza na Burudani mjini Dar es Salaam wiki hii, Dimpoz alisema amerekodi wimbo huo kwa kushirikiana na msanii DJ Cleo wa Afrika Kusini.
Dimpoz alisema walirekodi wimbo huo kwenye studio za B Hits za Dar es Salaam wakati DJ Cleo alipofanya ziara ya kimuziki nchini.
Alisema tayari msanii huyo wa Afrika Kusini ameshaondoka na demo yenye wimbo huo kwa ajili ya kwenda kumalizia kazi ya kuurekodi nchini kwao.
“Nashukuru na nimefurahi sana kwamba nimepata bahati ya kurekodi wimbo na mmoja wa wasanii nyota wa muziki wa hip hop barani Afrika,”alisema Dimpoz.
“Nilichokifanya ni kumpatia demo yenye wimbo huo ili akamalizie kwao kazi ya kuingiza sauti na kuchanganya mipigo ili kuiongezea ubora na akishairejesha, wimbo utakuwa umekamilika,”aliongeza msanii huyo.
Dimpoz alisema wimbo huo utajulikana kwa jina la Tonight na ameurekodi katika miondoko ya soul. Alisema anatarajia wimbo huo utakuwa mkali zaidi ya Nainai.
Alisema ameamua kurekodi na DJ Cleo kwa sababu anataka kuwa msanii wa kimataifa na kuongeza kuwa, lengo lake lingine ni kuuza kazi zake barani Ulaya na Marekani.
Mbali na kuwa mwanamuziki, DJ Cleo ni mtayarishaji wa muziki, akiwa anamiliki studio yake binafsi nchini Afrika. Kwa sasa, mwanamuziki huyo anatamba kwa kibao chake cha Facebook.

CHIDI BENZI AMCHANACHANA AFANDE SELE

MSANII mkongwe wa muziki wa kizazi kipya nchini, Rashid Abdalla 'Chidi Benz' amemponda msanii mwenzake, Selemani Msindi 'Afande Sele' kwa madai kuwa, amepitwa na wakati.
Chidi amesema msanii huyo mwenye maskani yake mkoani Morogoro anapaswa kuchunga kauli zake kwa sababu baadhi ya matamshi yake yanaonyesha kuwa, upeo wake kiusanii ni mdogo.
Chidi alisema hayo wiki hii mjini Dar es Salaam, kufuatia Afande Sele kuuponda uamuzi wa msanii wake wa zamani, Dogo Dito kujiunga na kundi la La Familia.
Afande Sele ameufananisha uamuzi huo wa Dogo Dito kuwa ni sawa na mchezaji kuihama klabu ya Manchestern United na kujiunga na Wolves. La Familia ni kundi linaloongozwa na Chidi Benz.
"Mimi namshangaa sana Afande Sele kwa sababu ni mtu ninayemuheshimu na sikutarajia angeweza kusema maneno kama hayo," alisema.
"Kuifananisha La Familia na Wolves ni makosa makubwa sana kwa sababu kundi langu lipo mjini sio kama Watu Pori (kundi la Afande Sele), ambalo lipo Morogoro, kwa hiyo unapotoa mifano ya aina hii, unapaswa kuwa makini,"aliongeza.
Chidi alisema asingependa kuwa na malumbano na Afande Sele kwa sababu ameamua kubadilika kimaisha na hapendi kuendelea kuwa mtu wa vurugu kama ilivyokuwa miaka ya nyuma.
Alisema kwa sasa Dogo Dito yupo kundi la THT hivyo Afande Sele amefanya makosa kulilalamikia kundi lake na kuongeza kuwa, msanii anapotoka kundi moja kwenda lingine hapaswi kulaumiwa kwa sababu anatafuta maslahi mazuri zaidi.

COS B:Ali Kiba amerekodi wimbo wangu

MSANII chipukizi wa muziki wa kizazi kipya, Marius Rashid ameibuka na kudai kuwa, wimbo wake wa Single Boy umeibwa na msanii nyota wa muziki huo, Ali Kiba.
Akizungumza mjini Dar es Salaam wiki hii, msanii huyo ambaye ni maarufu zaidi kwa jina la Cos B alisema, aliutunga wimbo huo miezi mitano iliyopita.
Cos B alisema hakuwahi kuurekodi wimbo huo kwenye studio yoyote zaidi ya kumpatia Kiba kwa lengo la kumsaidia kuurekodi.
“Wakati nikihangaika kutafuta mfadhili ili anisaidie kuurekodi wimbo huo, nikakutana na Ali Kiba kwenye studio za G Records,”alisema Cos B.
“Baada ya kukutana naye, nilimuomba anisaidie nipate nafasi ya kurekodi kwenye studio hiyo, akaniomba nimwimbie kwanza wimbo wangu niliotaka kuurekodi,”aliongeza msanii huyo.
Cos B alisema baada ya kuuimba wimbo huo kwa mara ya kwanza, Kiba alitokea kuvutiwa nao na akamuomba auimbe kwa mara ya pili ili ausikilize tena.
“Wakati nikifanya hivyo, sikujua kwamba alikuwa akiurekodi wimbo huo maana alikuwa ameshika simu yake ya mkononi na kuibonyezabonyeza,”alisema.
Chipukizi huyo wa muziki wa kizazi kipya alisema, baada ya hapo Kiba alimpatia namba yake ya simu ili wawe wakiwasiliana, lakini kila alipokuwa akimpigia, hakuweza kumpata.
Alisema siku moja alipokuwa safarini kwenda nyumbani kwao Mpanda mkoani Rukwa, alishangaa kuusikia wimbo huo ukipigwa redioni ukiwa umeimbwa na Kiba.
“Kwa kweli nilishtuka na kushangaa sana kwa sababu haukuwa umebadilishwa sana mashairi yake. Ni yale yale ya kwangu na jina la wimbo ni lile lile la single boy,”alisema.
Cos B alisema kitendo cha Kiba kuurekodi wimbo wake bila ridhaa yake kimemshangaza kwa vile hawakuwa na makubaliano yoyote ya aina hiyo.
Amewataka mashabiki wa muziki wa kizazi kipya nchini kuuchukulia wimbo huo kuwa ni mali yake na kwamba Kiba alitumia hila kuuiba wakati alipomuomba amuimbie walipokutana kwenye studio za G Records.
Alipoulizwa kwa njia ya simu iwapo tuhuma hizo ni za kweli, Kiba aliomba kwanza apewe Cos B ili azungumze naye kabla ya kujibu swali hilo.
Alipobanwa zaidi na kuelezwa mazingira ya kuupata kwake wimbo huo kutoka kwa Cos B, Kiba alikana kumjua msanii huyo na kudai kuwa, hajawahi kuiba wimbo wake.
‘Huu wimbo ni wa kwangu na ingekuwa vizuri iwapo ningekutana na msanii huyo ili anieleze ni lini nilimwibia wimbo wake,’ alisema Kiba akionekana kuwa na hasira.

Nina uwezo wa kuimba aina zote za muziki-BI CHEKA

Ni Bi Kizee aliyejitosa kwenye bongo fleva
Anatamba kwa kibao chake cha Ni wewe

MSANII mkongwe wa muziki wa kizazi kipya nchini, Mwahija Cheka ‘Bi Cheka’ amesema ana uwezo wa kuimba aina zote za muziki, isipokuwa taarab.
Bi Cheka (55) amesema aliyebaini kipaji chake ni msanii Amani Temba wa kundi la TMK Wanaume Family, baada ya kukutana naye miaka mitatu iliyopita mjini Morogoro.
Mama huyo mwenye watoto na wajukuu kadhaa alisema hayo hivi karibuni alipokuwa akihojiwa katika kipindi cha Friday Night Live kilichorushwa hewani na kituo cha televisheni cha East Africa.
“Baada ya kukutana na Temba, nilikaa miaka mitatu bila kuwasiliana naye hadi nilipostukia naitwa Dar es Salaam kwa ajili ya kufanyiwa usaili,”alisema.
Bi Cheka alisema alifanyiwa usaili chini ya usimamizi wa kiongozi wa kundi la TMK Wanaume Family, Saidi Fela na siku hiyo hiyo alipelekwa studio kwa ajili ya kurekodi wimbo wake wa kwanza unaojulikana kwa jina la Ni wewe.
Bibi huyo amerekodi wimbo huo, unaozungumzia masuala ya mapenzi kwa kushirikiana na Temba.
“Nashukuru nilipokewa vizuri na ninapata ushirikiano mkubwa kutoka kwa wasanii wenzangu wa kituo cha kuendeleza vipaji cha Mkubwa na Wanawe,”alisema mama huyo.
“Kilichonipa moyo zaidi ni kuona kuwa mara baada ya kujaribiwa, wote walisema huyu bibi anajua kuimba, atatufaa, nikapewa nafasi, nikaonyesha vitu vyangu, ”aliongeza.
Bi Cheka alisema mara baada ya wimbo wake kuanza kuonekana kwenye luninga, baadhi ya wazee wenzake walionekana kumshangaa, lakini kwa sasa wameizoea hali hiyo.
“Kila nilipokuwa nikipita mitaani, walikuwa wakiitana na kuonyeshana yuleee, ndiye yeye, mara Tembaaa,”alisema mama huyo.
Pamoja na kuanza kupata umaarufu kimuziki, Bi Cheka alisema maisha yake hayajabadilika na kwamba ataendelea kubaki yule yule na kufanya yote aliyokuwa akiyafanya awali.
Bi Cheka alisema kwa sasa anajiandaa kutoa albamu, lakini haelewi ni lini itakamilika kwa vile hilo litategemea upatikanaji wa wadhamini kwa ajili ya kurekodi audio na video.
Akizungumzia ujio wa albamu ya bibi huyo, Fela alisema kwa sasa wanataka kumtambulisha kwanza kwa mashabiki ili nyimbo zake zijulikane.
Fela alisema wamepanga kumtambulisha Bi Cheka wakati wa sikukuu ya Pasaka katika onyesho litakalofanyika mkoani Morogoro. Alisema onyesho hilo litapambwa na wasanii mbalimbali nyota wa bongo fleva. Kiongozi huyo wa TMK Wanaume Family alisema maandalizi kwa ajili ya onyesho hilo litakalofanyika kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro, yamekamilika.
Alisema mbali na kibao chake cha Ni wewe, katika onyesho hilo, Bi Cheka atautambulisha wimbo wake mwingine mpya, lakini hakuwa tayari kutaja jina lake.
“Huu wimbo utapigwa kwa mara ya kwanza siku ya onyesho hilo, hatutaki kuutangaza hivi sasa kwa vile ni mapema kufanya hivyo. Tunataka kumtoa kiaina,”alisema.
Bi Cheka anavutiwa na wasanii wengi wa muziki wa kizazi kipya, lakini zaidi ni Diamond, Bob Junior, Ali Kiba na Dully Sykes. Kwa wasanii wa kike, alisema anavutiwa nao wote.

JULIO: Tutaizika Yanga Mkwakwani




WAKATI homa ya pambano la ligi kuu ya soka kati ya Yanga na Coastal Union ikiwa imeshaanza kupanda, Kocha Mkuu wa Wagosi wa Kaya, Jamhuri Kihwelu ‘Julio’ ametamba kuwa watawasambaratisha wapinzani wao katika mechi hiyo. Katika makala hii iliyoandikwa na Mwandishi Wetu ATHANAS KAZIGE, kocha huyo anaelezea mikakati yao katika mechi hiyo na mambo mengine kadhaa.

SWALI: Kikosi chako kinatarajiwa kushuka dimbani Jumamosi ijayo kucheza na Yanga katika mechi ya ligi kuu ya Tanzania Bara, itakayochezwa kwenye Uwanja wa Mkwakwani mjini Tanga. Hebu tueleze mmejiandaaje kwa ajili ya mechi hiyo.
JIBU: Kikosi changu kipo fiti na hakuna mchezaji yeyote, ambaye ni majeruhi. Tuna uhakika mkubwa wa kuchukua pointi zote tatu kutoka kwa Yanga kwa sababu nimerudi na mbinu mpya za soka kutoka Arabuni, ambako nilikwenda miezi michache iliyopita.
SWALI: Kwa nini unajiamini sana kwamba mtaishinda Yanga?
JIBU: Nasema hivyo kwa sababu kikosi changu kipo imara na ninataka Yanga waingie uwanjani na kikosi chao chote pamoja na viongozi wao wote, lakini lazima tutawafunga.
Vilevile nimeshazisoma mbinu zao zote, hivyo suala la kuifunga Yanga halina mjadala, uhakika wa kuifunga ni mkubwa sana, hata kama mwamuzi atakuwa mwenyekiti wao, Lloyd Nchunga.
Kwangu mimi ninachoweza kusema ni kwamba Yanga hawana jambo lolote jipya zaidi ya kupenda kulalamika na kudai wameonewa. Na hivyo ndivyo itakavyotokea siku ya mchezo.
SWALI: Unazungumziaje kuhusu kusitishwa kwa adhabu ya kufungiwa kwa wachezaji watano wa Yanga, ambao walifungiwa kwa kosa la kumpiga mwamuzi Israel Nkongo wakati wa mechi yao dhidi ya Azam?
JIBU: Kwa kweli hakuna uamuzi mbovu na uliowashangaza mashabiki wa soka nchini kama huu uliotolewa na Mwenyekiti wa Kamati ya Nidhamu na Usuluhishi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Alfred Tibaigana. Kila mtu alikuwa shahidi wa tukio la wachezaji wa Yanga kumpiga mwamuzi, sasa hili la kutaka vielelezo limetoka wapi? Namheshimu sana kama yangu Tibaigana, lakini kwa hili naweza kusema amekosea.
Kwa mtazamo wangu, mtindo huu utazidi kudidimiza soka ya Tanzania kwa sababu wachezaji wetu wengi, hasa wa Yanga hawana nidhamu. Hivyo unapositisha adhabu iliyotolewa kwao, unawafanya wengine nao waone kumbe kumpiga mwamuzi ni jambo la kawaida.Nadhani huu ni woga tu wa baadhi ya wajumbe waliopo kwenye kamati ya Tibaigana kuona Yanga ikipokea kipigo kutoka kwa Coastal Union.
Tumekerwa sana na uamuzi huu na tutakachokifanya ni kuifunga Yanga ikiwa na kikosi chake chote ili viongozi, wanachama na mashabiki wake wakose cha kusema.
SWALI: Mbona umekuwa mkali sana kuhusu jambo hili?
JIBU: Unajua umefika wakati lazima tuseme ukweli. Hivi kuna nani ambaye hakuona kupitia vituo mbalimbali vya luninga jinsi wachezaji wa Yanga walivyofanya uwanjani katika mechi yao na Azam?.
Kwa kweli nawahurumia sana viongozi wenye nia ya kweli ya kuleta maendeleo ya soka nchini kwa jinsi wanavyotolewa maneno ya kashfa kutokana na kutenda haki.
Kila kukicha baadhi ya wadau wa soka nchini wamekuwa wakitoa lugha chafu kwa Rais wa TFF, Leodegar Tenga na viongozi wengine, wakiwemo Sunday Kayuni na Sadi Kawemba, lakini wanawaonea. Hawa watu wamekuwa wakiheshimu sheria za soka, lakini watu wengine wanawaangusha kwa makusudi.
SWALI: Nadhani ulikuwepo uwanjani na kushuhudia Simba ikiichapa ES Setif ya Algeria mabao 2-0 katika mechi ya michuano ya Kombe la Shirikisho iliyochezwa mwishoni mwa wiki iliyopita mjini Dar es Salaam. Una maoni gani kuhusu mchezo huo?
JIBU: Nimefurahishwa sana na ushindi walioupata Simba kwa sababu ni ushindi wa watanzania wote. Binafsi nawatakia maandalizi mazuri katika mechi yao ya marudiano. Lakini inabidi waende Algeria kwa tahadhari kubwa huku wakiwa na dhamira ya kuibuka tena na ushindi.
Nimefurahi kusikia kwamba kabla ya kwenda Algeria, watapitia Misri na kufanya mazoezi kwa siku kadhaa kwa lengo la kuzoea hali ya hewa ya huko. Hili ni jambo zuri sana katika maandalizi.
SWALI: Una maoni gani kuhusu ujio wa makocha wa kigeni hapa nchini? Unadhani wamekuwa wakitoa mchango wowote katika kukuza soka yetu?
JIBU: Kusema ukweli sio makocha wote wa kizungu waliotusaidia kukuza soka yetu. Kiwango chetu bado kimedumaa na wakati mwingine huwa naona ni bora makocha wazalendo wangepewa nafasi kwa kupelekwa nje kusomea mafunzo ya ukocha.
Wapo makocha wengi wazalendo hapa nchini wenye uwezo wa kuibua vipaji vya vijana na kuwaendeleza, lakini hawapati nafasi hiyo. Hawa makocha wa kigeni wanachotazama ni mechi za ligi tu, hawafiki mikoani, ambako ndiko kwenye vipaji vingi zaidi.
Binafsi napenda kumfagilia kocha wa sasa wa timu za Taifa za Vijana, Kim Poulsen kwa kupenda kusikiliza ushauri wa makocha wazalendo. Ndiye kocha pekee mzungu, ambaye yupo karibu na makocha wazalendo.

Wacheza shoo watakaocheza nusu uchi kukiona cha moto

BARAZA la Sanaa la Taifa (BASATA) limesema bado linakerwa na tabia ya uvunjifu wa maadili katika sanaa za maonyesho, hasa unenguaji na kutaka hali hiyo ifike mwisho.
Katibu Mtendaji wa BASATA, Ghonche Materego alisema hayo mwishoni mwa wiki iliyopita mjini Dar es Salaam na kuongeza kuwa, ni lazima kuwe na mabadiliko dhidi ya uvunjifu wa maadili kwenye sekta ya sanaa, vinginevyo hatua zitaanza kuchukuliwa.
“Haya si mambo yanayofurahisha, ni lazima jamii ionyeshe ushirikiano kwa kupambana na udhalilishaji wa aina hii. Kuna mambo yasiyopaswa kufanyika hadharani na yanabaki kuwa ya ndani tu kwenye klabu za usiku na Casino, si vinginevyo” alisistiza Materego.
Aliongeza kuwa, si jambo la busara hata kidogo kwa maonyesho hayo ya sehemu maalum za ndani kuanza kufanywa hadharani kwani ni kinyume cha sheria na taratibu za nchi na ni udhalilishaji wa sekta ya sanaa hivyo aliwataka wasanii kujipanga ili kupambana na tatizo hilo.
“Mabadiliko lazima yafanywe. Vyama, mashirikisho na mitandao ya wasanii vianze mara moja kuangalia maadili kwenye maeneo yao. Hatua madhubuti zichukuliwe dhidi ya watakaoendelea kuvunja maadili kwenye sanaa” alisisitiza Materego.
Awali, Mwenyekiti wa Chama cha Muziki wa Dansi Tanzania (CHAMUDATA), Juma Ubao alisema kinachofanyika sasa kwenye unenguaji si muziki wa dansi bali ni aina fulani ya matukio ambayo ni maalum kwa ajili ya klabu za usiku.
“Unenguaji wa uchi usihusishwe hata kidodo na muziki wa dansi. Haya yanayofanyika sasa ni kuuchafua muziki huu. Ni lazima tuelewe haya si ya kuyavumilia kwenye muziki wetu” alisisitiza Ubao.
Alisema katika miaka ya nyuma, wanenguaji walikuwa wakivaa mavazi ya heshima na kufanya maonesho yaliyowavutia mashabiki wa rika zote, lakini kwa sasa hali ni tofauti kutokana na kuwepo kwa vikundi vinavyovaa uchi na kuanza kunengua hadharani.
Kwa upande wake, mtendaji kutoka asasi ya Binti Leo, inayojishughulisha na sanaa za majukwani, Betty Kazimbaya alisema, kinachofanyika sasa ni kudhalilisha sanaa na ukiukwaji wa maadili kupitia wasanii wanaolipwa pesa kiduchu hivyo kutaka hatua kali zichukuliwe.
“Kazi kubwa ya wasanii wa aina hii ni kusitiri mwili, inakuaje kuwe na vikundi havitumii mavazi haya kwa kazi hiyo?" Alihoji Kazimbaya

Shangwe ya ushindi Uhuru SC

BAADHI ya wachezaji wa timu ya netiboli ya Uhuru wakifurahia kikombe walichokitwaa kwa kushika nafasi ya pili katika bonanza la vyombo vya habari lililoandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo nchini (TASWA) na kufanyika mwishoni mwa wiki iliyopita kwenye ufukwe wa Msasani, Dar es Salaam. Kutoka kushoto ni Samira Kiango, Anna Nyangasa, Jane Mihanji na Lilian Timbuka. (Picha na Emmanuel Ndege).

Ligi Kuu Zenji yapata mdhamini mpya


Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
WIZARA ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo ya Zanzibar imesema, kuanzia sasa italivalia njuga tatizo la kukosekana kwa udhamini katika michezo visiwani Zanzibar.
Waziri wa wizara hiyo, Abdilah Jihad Hassan alisema hayo mwishoni mwa wiki iliyopita mjini hapa wakati wa mkutano wa wadau wa michezo na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharrif Hamad.
Alisema ukosefu wa udhamini katika michezo, umechangia kwa kiasi kikubwa kudorola kwa michezo na pia kushusha ari ya wachezaji.
Waziri Jihad amesema tayari ameshafanikiwa kuishawishi kampuni moja ili idhamini michuano ya ligi kuu ya Zanzibar msimu ujao, lakini hakuwa tayari kuitaja.
Alisema amelazimika kujitosa mwenyewe kutafuta mdhamini wa ligi hiyo baada ya kushauriwa mara kadhaa na viongozi wa Chama cha Soka cha Zanzibar (ZFA).
Jihad alisema kujitokeza kwa malumbano ya mara kwa mara kati ya viongozi wa ZFA na wadau wa michezo ni ishara ya kutaka yawepo mabadiliko katika uendeshaji na usimamizi wa soka.
Hata hivyo, aliwataka wadau wanaokikosoa chama hicho, kutoa maoni yenye mtazamo chanya badala ya kujenga chuki dhidi ya viongozi wake.
Alisema tayari tofauti zilizokuwepo kati ya ZFA na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) zimemalizwa na kwa sasa kumekuwepo na ushirikiano mkubwa kati ya vyama hivyo.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo, Ali Mwinyikai alisema, michezo katika karne hii ni fedha, hivyo ili kuwashawishi wadhamini kubeba gharama, ni lazima wanaobebwa wawe wakweli na wawazi na kuepuka ubabaishaji. Mwinyikai Kampuni ya Simu za Mkononi ya Zantel iliamua kujitoa kudhamini ligi kuu ya Zanzibar kutokana na ubabaishaji wa viongozi wa ZFA na pia kutokuwa wazi kuhusu mapato ya matumizi ya pesa za udhamini.
Alikumbusha kuwa, ZFA ndicho chama pekee kinachopata pesa nyingi kutoka serikali kuliko vyama vingine, hivyo viongozi wake wanapaswa kuwa makini katika matumizi ya pesa hizo.
ZFA imekuwa ikipewa ruzuku ya sh. milioni tano kila mwaka huku serikali ikitenga sh. milioni 100 kwa ajili ya kuihudumia timu ya Zanzibar.

SMZ yawashukia viongozi wa ZFA


Na Aboud Mahmoud, Zanzibar
MAKAMU wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharrif Hamad amekiri kuwa, Chama cha Soka cha Zanzibar (ZFA) kinakabiliwa na matatizo makubwa na kinahitaji kusaidiwa ili kibadilike.
Maalim Seif alisema hayo mwishoni mwa wiki iliyopita baada ya kukutana na wadau wa michezo katika mkutano uliofanyika kwenye hoteli ya Bwawani mjini hapa.
Makamu wa Kwanza wa Rais alisema matatizo yanayokikabili chama hicho si ya mtu mmoja, bali Wazanzibar wanaoguswa na kudorola kwa maendeleo ya michezo.
Hata hivyo, Maalim Seif alisema tatizo kubwa linalokikabili chama hicho ni upungufu uliomo kwenye katiba yake, ambayo haikidhi matakwa ya Wazanzibar na pia kwenda na wakati.
Alilitaka Baraza la Michezo la Zanzibar (BMTZ) kufanyakazi bega kwa bega na ZFA ili kuyafanyiakazi mapungufu yaliyomo kwenye katiba ya chama hicho kwa lengo la kuifanya iende na wakati. Maalim Seif aliwataka viongozi wa chama hicho kuacha kujenga chuki na watu wanaowakosoa kwa vile lengo la watu hao ni kuona mchezo wa soka unapiga hatua mbele kimaendeleo badala ya kurudi nyuma.
"Eleweni kuwa, anayekukosoa anakupenda, lakini asiyekupenda atakupa sifa tu hata kama ukifanya mabaya," alisema Maalim Seif.
Aliahidi kuyafanyiakazi maoni mbalimbali yaliyotolewa na wadau wa michezo katika mkutano huo na kusisitiza kuwa, lengo la serikali ni kuona hadhi ya michezo visiwani humo inarejea.
Katika mkutano huo, wadau mbalimbali wa michezo waliwalalamikia viongozi wa ZFA kwa kutokuwa na fikra na mtazamo mpya katika kuendeleza soka, badala yake wametawaliwa na ubinafsi na kuweka mbele zaidi maslahi yao.
Wadau hao pia waliwalalamikia viongozi wa chama hicho kwa kushindwa kuisimamia na kuilinda katiba ya chama chao, badala yake wamekuwa wakiendesha soka shaghalabaghala.

Ndoa ya Omotola yatimiza miaka 16


LAGOS, Nigeria
MCHEZA filamu nyota wa Nigeria, Omotola Jalade wiki iliyopita alisherehekea ndoa yake kutimiza miaka 16 na mumewe kepteni Matthew Jalade Ekeinde.
Omotola na kepteni Matthew walifunga ndoa Machi 23, 1996 na sherehe yao ya harusi ilifanyika ndani ya ndege aina ya Dash 7 iliyosafiri kutoka Lagos kwenda Benin siku ya Aprili 21, 2001.
Wanandoa hao wamefanikiwa kupata watoto wanne, wawili wa kike na wawili wa kiume. Watoto hao ni Princess, M.J, Meriaih na Michael Ekeinde.
Ndoa ya Omotola na mumewe imekuwa ikikumbwa na misukosuko mingi ikiwa ni pamoja na tuhuma za kuachana ama kutembea nje, lakini wote wawili wamekuwa ngangali kukabiliana nayo.
Omotola na mumewe walisherehekea siku hiyo kwa staili ya aina yake, ikiwa ni pamoja na kuwaalika ndugu na marafiki wachache kwa ajili ya chakula na vinywaji.
Akihojiwa na mtandao wa naijerules, Omotola alisema anamshukuru Mungu kwa kumwezesha ndoa yake kudumu kwa miaka 16 hadi sasa.
“Kwangu mimi, tulipokutana kwa mara ya kwanza, haikuwa suala la mapenzi. Lakini kwake, alisema ilikuwa ni mapenzi zaidi,”alisema Omotola.
Omotola alisema kabla ya kufunga ndoa, mumewe alimweleza kuwa, alikuwa akiomba dua usiku na mchana aweze kukutana na mwanamke wa aina yake.
“Kwa mujibu wa maelekezo yake, aliwasilisha majina ya wasichana aliowahi kuhusiana nao kimapenzi kwa wachungaji ili waweze kuyasalia na kubaini yupi alikuwa sahihi kwake,”alisema.
Omotola alisema yeye na mumewe hawapendi kuwa na marafiki wanaoweza kuyaathiri maisha yao. Alisema hakuna kati yao anayependa kujadiliana jambo mbele ya marafiki.
Mwanadada huyo alisema pia kuwa, mumewe hapendi kusoma habari za udaku na hakuna mtu anayeweza kumwonyesha habari zozote zilizochapishwa kwenye gazeti kuhusu yeye.
“Wakati picha za filamu ya ‘The Prostitutes’ (Malaya) zilipochapishwa gazetini, ilikuwa kama vile hivyo ndivyo nilivyofanya kwenye filamu hiyo. Ilikuwa ni siku mbaya kwangu. Tulizungumza kuhusu hilo. Ilikuwa kama ananipoza kwa sababu nilichanganyikiwa. Tukio hilo halikutuathiri kitu,”alisema.
Omotola alisema kamwe hajawahi kuwa na uhusiano wa kimapenzi na mcheza filamu yeyote wa Nigeria. Alisema amekuwa akipokea maombi ya aina hiyo kutoka kwa watu mbalimbali, lakini amekuwa akiwapuuzia.
Alisema hapendi kuwa adui wa watu kwa sababu ameolewa. Alisema wanaume wote waliowahi kumtongoza kwa sasa wamebaki kuwa rafiki zake wa kawaida na wanamuheshimu.
“Mume wangu hana tatizo na kazi yangu na kamwe hawezi kuwa hivyo. Ananiunga mkono. Ni shabiki wangu namba moja. Anapenda kutazama filamu zangu,”alisema.

Sunday, March 25, 2012

Simba yawaua Waalgeria

Kikosi cha Simba kilichoiua ES Setif ya Algeria

Hivi ndivyo ubao wa matangazo ulivyokuwa ukisomeka baada ya mchezo kumalizika

Baadhi ya vigogo wa serikali na michezo waliohudhuria mechi hiyo. Kutoka kushoto ni Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta, Waziri Mkuu mstaafu Fredrick Sumaye, mjumbe wa heshima wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF), Said Hamad El-Maamry, Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe na Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage.


Mshambuliaji Emmanuel Okwi (kulia) wa Simba akimtoka beki wa ES Setif ya Algeria


Makocha Milovan Cirkovic (kushoto) wa Simba akisalimiana na Alain Geiger wa ES Setif ya Algeria kabla ya timu hizo kumenyana jana.

Hekaheka kwenye lango la ES Setif ya Algeria katika pambano lao dhidi ya Simba


Machaku Salum wa Simba akimtoka beki wa ES Setif ya Algeria


SIMBA imeendelea kuwa kiboko ya timu za Waarabu, baada ya kuifunga timu ya Es Setif ya Algeria mabao 2-0 katika mechi ya raundi ya kwanza Kombe la Shirikisho iliyochezwa jana Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Mechi hiyo ilitawaliwa na kukosa mabao mengi kwa upande wa Simba, ambapo mshambuliaji Emmanuel Okwi, Felix Sunzu na Patrick Mafisango waliongoza mashuti yao kushindwa kulenga lango la wapinzani wao hao kutoka Afrika Kaskazini.
Dakika 43 Mafisango alishindwa kuunganisha wavuni pasi ndefu ya beki Kelvin Yondan aliyepanda kuongeza nguvu, ambapo mchezaji huyo alipiga shuti ambalo lilitoka nje, huku Okwi naye alirudia kosa hilo kwa kutoa nje mpira aliopewa pasi na Salum Machaku.
Timu hizo zilikwenda mapumziko zikiwa suluhu na wenyeji Simba walipata kona tatu wakiwa nyuma kwa kona moja dhidi ya Es Setif waliokuwa wanajihami muda mwingi wa mchezo.
Baada ya mashabiki wa Simba kuishia kushangilia 'gonga' za timu yao iliyokosa mabao mengi kipindi cha kwanza, raha yao ilikamilika dakika 72 baada ya Okwi kufunga bao la kwanza kwa shuti lililojaa wavuni kufuatia kuwababatiza mabeki wa Es Setif na kipa kuchanganywa na mwelekeo wa mpira huo.
Kuingia kwa bao hilo kuliongeza hamasa kwa Simba iliyokuwa na kila dalili ya ushindi kipindi cha pili kutokana na kulisakama lango la wapinzani wao kama nyuki.
Mchezo wa Es Setif kujihami hadi kipindi cha pili uliwafaidisha Simba ambao walicheza mpira nusu uwanja na kupata bao la pili dakika 79 lililowekwa wavuni na Haruna Moshi 'Boban' aliyewahi mpira uliopanguliwa na kipa Mohamed Benhamou, ambaye alitema mpira wa adhabu iliyopigwa vizuri na Machaku.
Adhabu hiyo ilitolewa na mwamuzi Hudu Munyemana kutoka Rwanda baada ya Okwi kuangushwa nje ya eneo la hatari na Machaku akapiga kiufundi na kumlazimu kipa huyo kupangua ndipo ulipomkuta Boban akauzamisha wavuni na kuibua shangwe kubwa kwa mashabiki wa klabu hiyo ya Msimbazi, huku upande wanaokaa mashabiki wa Yanga ukiwa kimya na baadhi yao kuondoka wakionyesha kutofurahi mahasimu wao kupata matokeo hayo.
Katika kipindi hicho, Es Setif walifanya mashambulizi machache likiwemo la dakika 49 Youcef Ghezzali kupiga shuti la mbali ambalo lilipaa katika lango la Simba na mchezaji huyo alikosa bao kipindi cha kwanza baada ya kupiga mpira uliodakwa na Juma Kaseja licha ya kubaki naye uso kwa uso.
Boban alijibu mapigo kwa kufumua kombora lililopanguliwa na kipa Benhamou na kuwa kona butu, naye Abderrahmane Hachoud alimjaribu Kaseja, lakini shuti lake lilitoka nje dakika 60. Pia, Sunzu alishindwa kuunganisha wavuni krosi ya Okwi aliyeongoza kwa kukosa mabao.
Wachezaji Racid Ferrahi, Akram Djanit wa Es Setif walionyeshwa kadi za njano na mwamuzi Munyemana kwa utovu wa nidhamu na wachezaji wa Simba hawakuonyeshwa kadi yoyote katika mechi hiyo ya raundi ya kwanza Kombe la Shirikisho. Simba iliyowahi kuweka historia ya kuzifunga timu za Arab Contractors na mabingwa Afrika mara tano klabu ya Zamalek, itakwenda Algeria kurudiana na Setif wiki mbili zijazo.
Simba: Juma Kaseja, Shomari Kapombe, Amir Maftah, Juma Nyoso, Kelvin Yondan, Patrick Mafisango/Gervas Kago, Salum Machaku, Mwinyi Kazimoto, Felix Sunzu /Jonas Kago, Haruna Moshi 'Boban' na Emmanuel Okwi.
Es Setif: Mohame Benhamou, Riadh Benchadi, Smain Diss, Farouk Belkaid/Akram Djanit, Mourad Delhoum, Mokhtar Benmoussa, Racid Ferrahi,Youcef Ghezzali, Youssef Sofiane/Mohamed Tiouli, Mokhtar Megueni na Abderrahmane Hachoud/Said Arroussi,

Thursday, March 22, 2012

MILOVAN: LAZIMA WAARABU WAFE



SWALI: Tumeona jinsi kikosi chako kilivyokuwa kikichoka, hasa kipindi cha pili katika baadhi ya michezo ya hivi karibuni ya ligi kuu ya Tanzania Bara. Unaweza kutueleza tatizo ni nini?
JIBU: Ni kweli tatizo hilo lipo, nimeligundua na tayari nimeshaanza kulifanyiakazi ili kuhakikisha tunafanya vizuri katika mechi zetu zilizosalia za ligi kuu na ya Kombe la Shirikisho.
Yapo mambo mengi yaliyochangia hali hiyo, lakini kikubwa ni kwamba baadhi ya wachezaji wangu wamerejea uwanjani hivi karibuni baada ya kuwa majeruhi kwa muda mrefu.
Wachezaji kama Amir Maftah na Juma Jabu kwa sasa ni majeruhi na wakianza mazoezi baada ya kupona, wanaanza taratibu, hivyo wakipewa nafasi ya kucheza, wanachoka haraka kwa vile hawajafanya mazoezi ya nguvu kwa muda mrefu.
Tatizo hili limekuwa likinichanganya sana kwa sababu limekuwa likiiathiri timu kwa muda mrefu. Tatizo lingine ni ukosefu wa stamina kwa baadhi ya wachezaji. Lakini hili si kubwa na linaweza kurekebishika.
SWALI: Simba inatarajiwa kucheza na ES Setif ya Algeria Machi 25 mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Je, umeshapata ripoti yoyote kuhusu wapinzani wenu?
JIBU: Kusema ukweli hadi sasa sijapata ripoti ya ES Setif, lakini tumefanikiwa kupata fununu kuhusu mbinu wanazotumia kimchezo katika mechi za nyumbani na ugenini. Wanatumia zaidi mfumo wa 4-5-1.
Nasi tumeshaanza kuutumia mfumo huu. Kama utakumbuka vizuri, tulicheza kwa kutumia mfumo huu katika mechi yetu dhidi ya Kagera Sugar na kushinda mabao 3-1. Pia tuliutumia katika mechi dhidi ya Toto African na kutoka nayo suluhu.
Lakini katika mechi yetu dhidi ya ES Setif hatutatumia mfumo huo muda wote wa mchezo. Tutaanza na mfumo wa 4-4-2 na baadaye kumalizia mfumo wa 4-5-1. Lengo letu ni kuwa na wachezaji wengi wa viungo ili kukabiliana na kasi ya mchezo na kucheza kwa kushambulia na kuzuia.
SWALI: Timu yako imekuwa ikipoteza nafasi nyingi za kufunga mabao kwenye michezo mbalimbali. Je umeshalifanyia kazi tatizo hilo kabla ya kucheza na ES Setif?
JIBU: Unajua tatizo la washambuliaji kushindwa kutumia vyema nafasi wanazopata kufunga mabao, halipo kwa Simba peke yake. Lipo kwenye timu nyingi, hata za Ulaya.
Hata hivyo, nimekuwa nikilifanyiakazi tatizo hilo mara kwa mara ili kuhakikisha timu yangu inaibuka na ushindi wa mabao mengi katika kila mechi zinazotukabili.
SWALI: Katika michuano ya ligi kuu msimu huu, tumeona baadhi ya timu zikiipania Simba? Unadhani ni kwa nini zinafanya hivyo?
JIBU: Simba ni timu kubwa na yenye rekodi nzuri katika ligi na michuano ya kimataifa. Vilevile katika michuano ya ligi kuu, kila timu imepania kutwaa ubingwa ikiwa ni pamoja na kuzishinda timu kongwe, hivyo ushindani wa aina hiyo lazima utokee.
Lakini kinachonisikitisha ni kwamba baadhi ya waamuzi wanaochezesha mechi za ligi wanashindwa kuheshimu sheria 17 za soka na wengine wanazikiuka kwa makusudi.
Wapo baadhi ya wachezaji wa timu pinzani, ambao wamekuwa wakiwaumiza wachezaji wangu kwa makusudi, lakini hakuna hatua zozote walizochukuliwa na waamuzi. Hali hii imechangia kwa kiasi kikubwa Simba kuwa na majeruhi wengi.
Uchezeshaji wa aina hii umekuwa ukizifanya baadhi ya klabu kuingia gharama kubwa za kuwatibu wachezaji wake na kuwakosa kwa muda mrefu kutokana na kuwa majeruhi.
Nadhani ni vyema waamuzi wawe makini katika kuwalinda baadhi ya wachezaji nyota, hasa wale wanaochezea timu ya taifa nap engine kutoa adhabu kali kwa wachezaji wenye tabia ya kucheza rafu za makusudi.
SWALI: Unawaeleza nini Watanzania kuhusu mechi yenu ya Jumapili na ES Setif ya Algeria?
JIBU: Nawaomba mashabiki wa soka wa Jiji la Dar es Salaam wajitokeze kwa wingi kushuhudia mechi hiyo kwa lengo la kuwaunga mkono wachezaji. Wakumbuke kwamba Simba ndio wawakilishi pekee wa Tanzania waliosalia katika michuano ya kimataifa, hivyo wanapaswa kuungwa mkono.
Pia nawaomba mashabiki wa Yanga waiunge mkono timu yetu badala ya kuizomea ama kuishangilia timu pinzani. Wanapaswa kuweka mbele uzalendo kwa nchi yao na kuacha ushabiki uliojaa chuki na uhasama usiokwisha.

Sitta mgeni rasmi bonanza la TASWA

WAZIRI wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki na mbunge wa Urambo Mashariki, Samuel Sitta anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika bonanza la vyombo vya habari.
Bonanza hilo limepangwa kufanyika keshokutwa kwenye ufukwe wa klabu ya Msasani, Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo nchini (TASWA), Juma Pinto alisema mjini Dar es Salaam jana kuwa, pamoja na mambo mengine, Sitta atakabidhi zawadi ya vikombe na medali kwa washindi.
Mbali na kukabidhi zawadi, Pinto alisema Waziri Sitta atapata fursa ya kuzungumza na washiriki wa bonanza hilo.
Kwa mujibu wa Pinto, bonanza hilo, ambalo huandaliwa kila mwaka na TASWA, litawashirikisha waandishi wa habari 1,500 kutoka vyombo mbalimbali vya habari nchini.
Pinto alisema lengo la bonanza hilo ni kuwaweka pamoja waandishi wote wa habari bila kujali ni wa siasa, michezo, uchumi, afya na mambo mengine pamoja na wafanyakazi wa idara zingine kwa ajili ya kubadilishana mawazo na kufurahi pamoja.
Alisema maandalizi ya bonanza hilo yapo hatua za mwisho, ambapo bendi ya FM Academia ‘Wazee wa Ngwasuma’ watatoa burudani kwa washiriki. Alisema bonanza hilo limepangwa kuanza saa tatu asubuhi hadi saa mbili usiku.
Pinto alisema burudani nyingine zitatolewa na wasanii wa muziki wa kizazi kipya, ambao watatangazwa leo, lengo likiwa kuwa na bonanza tofauti na miaka ya nyuma.
Amevitaka vyombo vya habari, ambavyo havijathibitisha ushiriki wake kwa njia ya maandishi, vifanye hivyo kama vilivyoagizwa kwenye barua zao za mialiko, vinginevyo ushiriki wao hautathaminika.

Martha Mlata, Kilahiro kuitoa 'Tulia miguuni mwa Yesu'

MBUNGE wa Viti Maalumu mkoa wa Singida, Martha Mlata, anatarajiwa kusindikiza uzinduzi wa albamu ya ‘Tulia miguuni kwa Yesu.
Martha, ambaye anatamba na nyimbo mbalimbali za injili, ataungana na wasanii wengine akiwemo Upendo Kilahiro kuitoa albamu hiyo ya nyota mwenzao Stella Joel.
Uzinduzi wa ‘Tulia miguuni mwa yesu’ unatarajiwa kufanyika Machi 25, mwaka huu, katika Ushirika wa KKKT Mabibo External.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Dar es Salaam, jana, Stella alisema albamu hiyo inasubiri kwa hamu kubwa na mashabiki wa muziki wa injili nchini.
Alisema mbali na Martha na Upendo, wasanii mbalimbali wa injili watashiriki kwenye uzinduzi wa albamu hiyo.
Stela aliwataja baadhi ya wasanii kuwa ni Addo November, John Shabani, Debora Saidi, Janeth Mrema, Victor Aron na Kwaya ya Joy Bringers.
Stella alisema maandalizi yote kwa ajili ya uzinduzi huo yamekamilika na kwamba, bado anaendelea na mazoezi makali ili kukonga nyoyo za mashabiki wake.
“Maandalizi yote yamekamilika na wasanii wanaendelea na mazoezi makali kwa ajili ya kukonga nyoyo za mashabiki wetu. Tulia miguuni kwa yesu ni albamu yenye ujumbe na mafundisho mengi, hivyo Mungu atuongoze salama wakati ufike,” alisema.
Stella alisema katika uzinduzi huo, mgeni rasmi atakuwa Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Dk. Didas Massaburi, ambaye ataongoza mamia kushuhudia uzinduzi huo na kwamba, hakutakuwa ni kiingilio.

Uhuru uso kwa uso na Jambo Leo

TIMU ya soka ya Uhuru leo inashuka dimbani kumenyana na Jambo Leo katika mechi ya robo fainali ya michuano ya Kombe la Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) itakayochezwa kwenye uwanja wa klabu ya Sigara, Chang’ombe, Dar es Salaam.
Pambano hilo ni miongoni mwa mechi mbili za robo fainali ya michuano hiyo zitakazochezwa leo. Katika mechi nyingine, NSSF itamenyana na mojawapo kati ya Tumaini, Mwananchi na Changamoto kwenye uwanja wa DUCE.
Uhuru ilifuzu kucheza robo fainali baada ya kutwaa uongozi wa kundi A wakati NSSF ilitwaa uongozi wa kundi B. Jambo Leo imeshika nafasi ya kwanza ya ‘best-looser’ wakati Mwanahalisi na Tumaini Media zilikuwa zikiwania nafasi ya pili ya ‘best-looser’.
Timu zingine zilizofuzu kucheza robo fainali ya michuano hiyo kwa upande wa soka ni Business Times, Habari Zanzibar na TBC. Timu nyingine ilitarajiwa kupatikana jana baada ya pambano kati ya Mwananchi na Changamoto.
Kwa upande wa netiboli, timu zilizofuzu kucheza robo fainali ni NSSF na IPP kutoka kundi A, Habari Zanzibar na Business Times kutoka kundi B na TBC na Uhuru kutoka kundi C.
Washindi wengine wawili watakaocheza hatua hiyo kama ‘best-loosers’ walitarajiwa kupatikana jana baada ya mechi kati ya Uhuru na Tumaini Media na kati ya NSSF na Mwananchi.
Akizungumzia pambano la leo, nahodha wa Uhuru, Mussa Hassan alijigamba kuwa, vijana wake wamejiandaa vyema kukabiliana na wapinzani wao.
Katika michuano ya mwaka jana, Jambo Leo iliitoa Uhuru katika mechi ya nusu fainali kwa ushindi wa bao 1-0.
Mussa alisema watalitumia pambano hilo kulipa kisasi kwa Jambo Leo na pia kujisafishia njia ya kufuzu kucheza fainali.

SINTA: Tujitambue, kujiamini na kujithamini


MSANII machachari wa filamu za kibongo, Christina Manongi ‘Sinta’ amewataka wasanii wa kike nchini kujitambua na kujithamini badala ya kuwa waoga wa kuonyesha vipaji vyao.
Sinta amesema iwapo msanii wa kike atashindwa kujitambua mapema, ni rahisi kwake kutumiwa kimapenzi na wanaume hata kama anacho kipaji cha fani anayoshiriki.
Msanii huyo, ambaye alikuwa kimya kwa muda mrefu, alisema hayo mwishoni mwa wiki iliyopita alipokuwa akihojiwa katika kipindi cha blogu yetu kilichorushwa hewani na kituo cha televisheni cha DTV.
“Msanii wa kike anapaswa kutambua kuwa, yeye ndiye baba na mama, akitaka kuwa kama Sinta, akiwa na moyo huo, atafanikiwa, vinginevyo utatongozwa na kutembea hovyo na wanaume,”alisema.
Sinta alisema binafsi alifanikiwa kujitosa kwenye fani ya filamu kutokana na uwezo na nguvu zake na kuongeza kuwa, kamwe hakuwahi kutumiwa na wanaume kwa jambo lolote.
Msanii huyo wa zamani wa kundi la sanaa la Kaole, alianza kujitosa kwenye fani ya filamu mwaka 2002, ambapo alishiriki kucheza filamu mbalimbali za kundi hilo.
Mbali na filamu, Sinta alishiriki kucheza tatmthilia kadhaa za kundi hilo zilizokuwa zikionyeshwa kupitia kituo cha televisheni cha ITV.
Sinta amekiri kuwa, japokuwa yamekuwepo mabadiliko makubwa katika fani hiyo hivi sasa, lakini zipo dosari nyingi, zikiwemo za baadhi ya wasanii kutokuwa na vipaji na uelewa wa fani hiyo.
Alisema baadhi ya wasanii wamejitosa kwenye fani ya filamu kutokana na kukosa la kufanya na wengine wanaiona fani hiyo kuwa ni nyepesi kuliko zingine.
“Hivi sasa kila mtu anataka kuwa mwigizaji. Ameshindwa kule, anataka uigizaji. Fani hii inataka kipaji zaidi, vingine vinafuata baadaye,”alisema.
Mwanadada huyo alisema anavutiwa zaidi na filamu za kiafrika, hasa za Kinigeria kwa sababu zinaelezea mazingira na hali halisi ya maisha ya kiafrika kuliko filamu za Hollywood.
Sinta alisema anamshukuru Mungu kwamba mpenzi wake wa sasa anamuelewa na kumwamini kwa kila kitu ndio sababu anaweza kufanya mambo yake bila kukumbana na vikwazo vyovyote.
“Nimekuwa nikipata mialiko mingi na wakati mwingine napata kazi za usiku, lakini kwa vile mpenzi wangu ni mwelewa, sipati matatizo,”alisema.
Alizitaja changamoto pekee, ambazo amekuwa akizipata katika maisha yake ya usanii kuwa ni kudharauliwa na baadhi ya watu bila ya kuwa na sababu za msingi.
Hata hivyo, alisema hakatishwi tamaa kutokana na dharau hizo kwa sababu anajiamini na siku zote humweka mbele Mungu na kusali kabla ya kufanya kitu chochote.
Kwa sasa, Sinta anajiandaa kuziingiza sokoni filamu zake mbili mpya. Alizitaja filamu hizo kuwa ni The return of J-LO na Sitaki demu.
Alisema filamu ya The return of J-LO inahusu mchezo wa soka na amewashirikisha wacheza soka kadhaa kama vile Emmanuel Okwi, Jerry Tegete na Amir Maftah.
Katika filamu ya Sitaki demu, amemshirikisha mpenzi wake wa zamani, msanii Juma Nature pamoja na wanasiasa Ridhiwani Kikwete na Zitto Kabwe.
Alisema filamu hizo ni tofauti na zile zilizozoeleka kwa sababu ameamua kutoka upya akiwa na vitu vipya. Alisema kama ni hadithi, nyingi zimeshatengenezewa filamu hivyo ni bora kutoka na mwonekano mpya.

DIAMOND: Sina demu, nipo singo



MSANII nyota wa muziki wa kizazi kipya, Naseeb Abdul ‘Diamond’ amesema kwa sasa yupo singo na kwamba hana papara ya kutafuta demu mwingine.
Diamond amesema ameamua kutulia kwa muda kwa sababu mapenzi hayapangwi, bali hutokea kimiujiza kama ilivyo kwa ajali ya aina yoyote.
Msanii huyo mwenye mvuto alisema hayo mwishoni mwa wiki iliyopita kupitia kipindi cha Friday Night Live kilichorushwa hewani kupitia kituo cha televisheni cha Channel Five.
Diamond alisema kwa kipindi kirefu sasa, amekuwa akikumbana na mikasa mingi inayohusu mapenzi, hivyo ameamua kutulia na kumuomba Mungu ampatie mpenzi mwema.
Msanii huyo alielezea msimamo wake huo, kufuatia hivi karibuni kutengana na mpenzi wake wa siku nyingi, Wema Sepetu.
Mbali na Wema, Diamond pia amekuwa akidaiwa kuwa na uhusiano wa kimapenzi na wasanii wengi nyota wakiwemo Jokate Mwegelo na Irene Uwoya.
“Kusema ule ukweli, kwa sasa sina mtu, nipo singo. Na siwezi kusema nitapata mpenzi mwingine hivi karibuni kwa sababu siku zote mapenzi huwa yanapangwa, hayaji kama ajali,”alisema msanii huyo, ambaye kwa sasa anatamba na kibao chake cha Mawazo.
Alipoulizwa kuhusu kitu gani asichokipenda katika maisha yake ya usanii, Diamond alisema hapendi kuwaudhi mashabiki wake kwa vile wao ndio wanaomwezesha kuwa kwenye chati ya juu kimuziki.
Alisema siku zote amekuwa akijitahidi kubuni vitu vipya kwa ajili ya kuwaburudisha mashabiki wake na kusisitiza kuwa, msanii asipokuwa mbunifu, ni rahisi mashabiki kumchoka.
Diamond amemmwagia sifa kedekede prodyuza mahiri wa video za muziki nchini, Adam Juma kwamba ndiye aliyewainua wasanii wengi wa muziki wa kizazi kipya.
“Siku moja nilikaa mahali na Adam Juma nikamwambia, ‘bradha ikitokea siku ukasema unaacha kazi hii ama ikatokea Mungu amekuchukua mapema, wasanii tutapata tabu sana,’” alisema Diamond.
“Unaweza kutengeneza nyimbo ya kawaida, lakini ikabebwa na video. Adam ni mkali mno katika kutengeneza video za muziki wa kizazi kipya. Na video ndizo zinazoufanya muziki uonekane kuwa bora,”aliongeza.
Ili kwenda na wakati, Diamond alisema kwa sasa, ameamua kuwa na mbunifu wake wa mavazi, ambaye amekuwa akimtengenezea mavazi ya aina tofauti.
Alisema wasanii wanapaswa kuwa na mwonekano maalumu badala ya kuvaa mavazi yanayoweza kuwafanya waonekane wasela ama wahuni.
“Msanii hapaswi kuvaa nguo za makabitini. Wapo wasanii wengine wenye pesa na uwezo mkubwa, lakini hawapendi kuvaa, lakini ukishakuwa mtu maarufu katika jamii, unapaswa kubadilika,”alisema.

Friday, March 16, 2012

UFUNGUZI KOMBE LA NSSF ULIVYOKUWA

Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudendia Kabaka (katikati) akimsikiliza kiongozi wa waamuzi, Winfrida Paul (kulia) wakati wa ufunguzi wa mashindano ya Kombe la NSSF. Kushoto kwa waziri ni Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Dk. Ramadhani Dau.

Mwenyekiti wa kamati ya mashindano ya Kombe la NSSF, Rashid Zahor (kushoto) akisalimiana na Meneja wa TBC, Chacha Maginga wakati wa ufunguzi wa mashindano hayo uliofanyika wiki iliyopita kwenye uwanja wa klabu ya Sigara, Chang'ombe, Dar es Salaam.



Mwenyekiti wa kamati ya mashindano ya Kombe la NSSF, Rashid Zahor akisalimiana na mchezaji wa timu ya netiboli yaMwananchi wakati wa ufunguzi wa mashindano hayo uliofanyika wiki iliyopita kwenye uwanja wa klabu ya Sigara, Chang'ombe, Dar es Salaam. (Picha zote na Emmanuel Ndege).

Wednesday, March 14, 2012

SINA HAMU NA LIGI KUU-NIYONZIMA

KIUNGO nyota wa klabu ya Yanga, Haruna Niyonzima amesema hana hamu na michuano ya soka ya ligi kuu ya Tanzania Bara kutokana na wachezaji wengi wa timu pinzani kupania kumuumiza.
Niyonzima amesema amebaini kuwa, baadhi ya wachezaji wa timu pinzani wamekuwa wakimchezea rafu kwa makusudi kwa lengo la kupunguza kasi yake.
Mwanasoka huyo wa kimataifa wa Rwanda alisema hayo mjini Dar es Salaam juzi kufuatia vurugu zilizotokea mwishoni mwa wiki iliyopita wakati Yanga ilipomenyana na Azam katika mechi ya ligi kuu iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa.
Katika mechi hiyo, ambapo Yanga ilichapwa mabao 3-1, Niyonzima alitolewa nje kwa kadi nyekundu na mwamuzi Israel Nkongo wa Dar es Salaam kwa kosa la kucheza rafu na kutoa lugha chafu.
Kufuatia Niyonzima kuonyeshwa kadi hiyo, baadhi ya wachezaji wa Yanga walipinga na kuanza kumzonga Nkongo kabla ya kumshushia kipigo kizito.
Kitendo hicho kilisababisha Nkongo amtoe nje kwa kadi nyekundu beki Nadir Haroub Cannavaro kwa kosa la kumpiga. Wachezaji wengine waliotuhumiwa kumpiga mwamuzi huyo ni Stephano Mwasika na kiungo Nurdin Bakari.
Tayari kamati ya mashindano ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) imeshatangaza kuwafungia wachezaji watano wa Yanga pamoja na kuwatoza faini kwa kosa la kumshambuliaji Mkongo.
Wachezaji waliofungiwa ni Cannavaro, Nurdin, Omega Seme na Jerryson Tegete, ambao wamefungiwa kwa kipindi cha kati ya miezi mitatu hadi sita na wengine mechi tatu.
Stephano Mwasika amefungiwa mwaka mmoja na kutozwa faini ya sh. milioni moja kwa kumpiga. Adhabu zote zimetolewa kwa mujibu wa Kanuni za Ligi Kuu. Kamati ya ligi imempongeza nahodha wa Yanga, Shadrack Nsajigwa na mshambuliaji wa timu hiyo Hamis Kiiza kwa kuwa mstari wa mbele kuzuia wenzao kumshambulia mwamuzi. Pia imempongeza kocha Kostadin Papic wa Yanga kwa kukemea vurugu zilizofanywa na wachezaji wake.
Niyonzima amewataka wachezaji wa Yanga kukubaliana na uamuzi huo wa TFF na kuendelea kucheza kwa bidii katika mechi zilizosalia za mzunguko wa pili ili timu hiyo iweze kutetea taji lake.
Alikiri kuwa ligi ya msimu huu ni ngumu kutokana na kila timu kupania kushinda ili ziweze kutwaa ubingwa na zingine kuepuka kuteremka daraja.

Wasanii wa Taruwa kazini



WASANII wa kikundi cha sanaa za maonyesho cha Taruwa wakionyesha umahiri wa kucheza ngoma wakati wa sherehe za ufunguzi wa michuano ya Kombe la Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) zilizofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita kwenye uwanja wa klabu ya Sigara, Chang'ombe, Dar es Salaam. Kulia ni msanii mwingine wa kundi hilo akionyesha ufundi wa kupuliza filimbi kwa kutumia pua. (Picha na Emmanuel Ndege).

INI EDO:Siogopi kupoteza uzuri kwa kuzaa



LAGOS, Nigeria
MCHEZA filamu wa kike anayeongoza kwa utajiri nchini Nigeria, Ini Edo amesema amepanga kuanza kuzaa hivi karibuni.
Ini amesema haogopi kuzaa kwa hofu kwamba atapoteza uzuri wa umbo lake na kuongeza kuwa, kwa mwanamke aliyeolewa, kuzaa ni jambo la lazima na kwamba anapenda kuwa na watoto
“Sihofuu kupoteza umbile langu kwa sababu ya kuzaa. Wakati utakapofika, nitaanza kuzaa. Napenda watoto. Siwezi kusubiri muda mrefu kupata watoto,”alisema mwanadada huyo mwenye umbo na sura yenye mvuto alipohojiwa na mtandao wa naijerules hivi karibuni.
Hata hivyo, Ini amesema kama ni uzuri, alikuwa nao alipokuwa kijana zaidi. Alisema aliziona baadhi ya picha zake alipokuwa mdogo na kuvutiwa nazo kiasi cha kumfanya aiamini kama ni yeye.
Ini alisema hana njia yoyote anayoifanya ili aonekane mrembo zaidi ya kufanyakazi zake kwa bidii, kula vizuri, kuiweka ngozi yake katika hali nzuri na kuwa mwenye furaha muda wote.
Mwanadada huyo alisema anamshukuru Mungu kwamba maisha yake ya ndoa yanakwenda vizuri na kuongeza kuwa, kwa sasa ameamua kuacha kuigiza nafasi, ambazo zinaweza kuitia doa ndoa yake.
Alisema kamwe hajawahi kuigiza filamu za ngono na hawezi kufanya kitu kama hicho katika maisha yake yote. Alisema anapenda zaidi kuigiza filamu zinazoelezea maisha halisi ya jamii kwa vile ndizo zinazokuwa na mvuto zaidi kwa jamii.
Alipoulizwa iwapo bado anaendelea kuvuta sigara, Ini alisema amekuwa akifanya hivyo katika baadhi ya filamu alizocheza, lakini kwa kawaida si mvutaji wa sigara.
Ini alisema skendo pekee iliyowahi kumchukiza katika maisha yake ni ile iliyoandikwa na baadhi ya vyombo vya habari, ikimuhusisha na uvutaji wa dawa za kulevya.
Mwanadada huyo mwenye macho ya mwito alikataa kutaja kiasi cha pesa, ambacho amekuwa akilipwa katika uigizaji wa filamu. Hata hivyo, alikiri kwamba amekuwa akilipwa fedha nyingi.
Ini alikiri kuwa si rahisi kumudu kuwa mke wa mtu na mwigizaji. Alisema anajitahidi kadri ya uwezo wake kumudu mambo hayo mawili na kwa kiasi fulani amefanikiwa.
“Nimekuwa nikipanga mapema ni lini niwe mahali fulani na lini nisiwe mahali hapo. Siweki vitu vingi kwenye sahani moja kwa wakati mmoja kwa sababu nikifanya hivyo, nitashindwa kufanya vitu vingine wakati ninapaswa kuvifanya. Bado nafanya kila kitu ambacho mwanamke anapaswa kukifanya. Kila ninapotoka kazini, nafanyakazi ya kupika nyumbani,”alisema.
Ini, ambaye ni msomi wa shahada ya sanaa alisema iwapo asingekuwa mwigizaji, angependa kuwa mwanasheria au mwanahabari.
Hata hivyo, Ini alisema upo uwezekano pia angeweza kufanyakazi nyingine yoyote ilimradi tu awe anaipenda.
“Mimi ni mtu makini katika kila jambo. Kila kitu ninachokiseti kukifanya katika akili yangu, kama ninakipenda, lazima nikifanye,”alisema.
Hivi karibuni, Ini alizindua filamu yake mpya ya I Will Take My Chances, ambayo Ini ameielezea kuwa, ana hakika itafanya vizuri sokoni na kupendwa na mashabiki.
Ini alisema ilimchukua miezi miwili kutengeneza filamu hiyo, mwezi mmoja kwa ajili ya mazoezi na mwezi mwingine kwa ajili ya kupiga picha za filamu hiyo.
Mwanadada huyo alisema licha ya kuolewa, hafikirii kustaafu kucheza filamu kwa sasa na kwamba hakuna kinachoweza kumfanya afikie uamuzi huo.
Alisema kwake, uigizaji wa filamu hautokani na kutafuta pesa, bali mapenzi kwa kazi hiyo.
Mumewe Ini kwa sasa anaishi nchini Marekani. Lakini mwanadada huyo amesisitiza kuwa, hilo si tatizo kwao kwa sababu wamekuwa wakikutana mara kwa mara.
Katika kujiweka safi kimwili, Ini amesema siku zote amekuwa akipenda kusafisha uso wake na kuuweka safi. Alisema anapokuwa hana kazi ama tukio lolote, hatumii vipodozi kutengeneza uso wake.

Simba yaipigia hesabu ES Setif

UONGOZI wa klabu ya Simba umesema umeanza kuchukua tahadhari kubwa kabla ya kupambana na ES Setif ya Algeria katika mechi ya raundi ya pili ya michuano ya Kombe la Shirikisho.
Makamu Mwenyekiti wa Simba, Geofrey Nyange ‘Kaburu’ alisema mjini Dar es Salaam jana kuwa, miongoni mwa tahadhari hizo ni pamoja na kuhakikisha kuwa, wachezaji wao nyota hawaumii kabla ya mechi hiyo.
Simba na ES Setif zinatarajiwa kumenyana Machi 25 mwaka huu katika mechi itakayopigwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na kurudiana wiki mbili baadaye mjini Algiers.
Kaburu alisema wamemwelekeza Kocha Mkuu wa timu hiyo, Milovan Cirkovic kupanga wachezaji kwa uangalifu ikiwa ni pamoja na kuwapumzisha baadhi ya nyota wao katika mechi za ligi kuu.
Alizitaja tahadhari nyingine walizochokua kuwa ni kuwaasa wachezaji wao kuepuka kucheza rafu za kizembe ili wasionyeshwe kadi nyekundu ama kufungiwa kucheza ligi.
Alisema wamepata funzo kubwa kutokana na vurugu zilizotokea wakati wa mechi ya ligi kuu kati ya Yanga na Azam, ambazo zilisababisha wachezaji watano wa timu hiyo ya Jangwani kufungiwa kucheza soka kwa nyakati tofauti.
Kaburu alikiri kuwa, mechi kati yao na ES Setif itakuwa ngumu kwa vile wapinzani wao ni wazoefu wa mashindano ya kimataifa na kikosi chao kinaundwa na wachezaji wengi nyota.
Alisema tayari wameshapata taarifa za kutosha kuhusu timu hiyo ya Algeria na wameshaanza kuzifanyiakazi kwa lengo la kuhakikisha wanaibuka na ushindi katika mechi hiyo.
Simba imepanga kucheza na ES Setif kuanzia saa tisa alasiri ili kuwachosha wapinzani wao, ambao hali ya hewa kwao ni baridi kali.
Tegemeo kubwa la Waalgeria ni nyota wake, Sofiene Zaaboub, ambaye ni raia wa Ufaransa, Kouamé Valentin kutoka Burkina Fasso, Youssef Sofiane na Akram Djahnit, ambao ni raia wa Algeria.

Yanga: Tumeonewa



Yasema hawana imani na Kaburu, Ndumbaro

Yalipishwa mil 5/- za viti vilivyovunjwa U/Taifa
Na Mwandishi Wetu
UONGOZI wa klabu ya Yanga umesema haukubaliani na adhabu zilizotolewa na Kamati ya Ligi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwa wachezaji watano wa timu hiyo.
Yanga imedai kuwa, adhabu hizo ni za kiuonevu na imewatupia lawama baadhi ya wajumbe wa kamati hiyo kwa madai kuwa ni wanachama wa Simba.
Akizungumza na Burudani mjini Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Yanga, Lloyd Nchunga alisema uamuzi wa TFF kuwafungia wachezaji hao haukubaliki.
Nchunga alisema waliitarajia kamati hiyo kutoa uamuzi wa kionevu kwa Yanga kwa sababu baadhi ya wajumbe, Geofrey Nyange na Damas Ndumbaro ni wanachama wa Simba.
Nyange, ambaye ni maarufu zaidi kwa jina la Kaburu ni makamu mwenyekiti wa klabu ya Simba wakati Ndumbaro ni makamu mwenyekiti wa kamati ya uchaguzi ya wekundu hao wa Msimbazi. “Sasa hapo unategemea nini? Ni wazi kwamba kamati ya TFF inapokuwa na viongozi kutoka Simba, haiwezi kutenda haki kwa Yanga,”alisema.
Nchunga alisema anaamini wajumbe hao walitoa mapendekezo ya kuwafungia wachezaji hao watano wa Yanga kwa lengo la kupunguza kasi yake ya kutetea ubingwa wa ligi kuu msimu huu.
Kamati ya ligi ya TFF inaongozwa na Wallace Karia, Said Mohamed kutoka Azam, ambaye ni makamu mwenyekiti. Wajumbe wengine ni Ndumbaro, ambaye ni mwanasheria na Yahya Ahmed kutoka Kagera Sugar.
Wajumbe wengine wanaounda kamati hiyo ni Meja Charles Mbuge kutoka JKT Ruvu, Steven Mnguto kutoka Coastal Union, Kaburu kutoka Simba, Seif Ahmed wa Yanga, ACP Ahmed Msangi kutoka Polisi Dar na Henry Kabera wa Majimaji.
Yanga imeelezea msimamo wake huo siku moja baada ya kamati ya ligi ya TFF kuwafungia wachezaji wake watano na kuwatoza faini kwa kosa la kumpiga mwamuzi Israel Nkongo.
Tukio hilo lilitokea mwishoni mwa wiki iliyopita wakati Yanga ilipomenyana na Azam katika mechi ya ligi kuu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Katika mechi hiyo, Yanga ilichapwa mabao 3-1.
Kamati hiyo imeitoza Yanga faini ya sh. 500,000 kutokana na mashabiki wake kufanya vurugu katika mechi namba 132 dhidi ya Azam na faini ya sh. 500,000 kufuatia wachezaji wake watatu kuonyeshwa kadi nyekundu katika mechi moja kwa kosa la kumpiga mwamuzi Nkongo.
Wachezaji wa Yanga waliokumbwa na adhabu hiyo ni Nadir Haroub ‘Cannavaro’, aliyefungiwa mechi sita za ligi na kutozwa faini ya sh. 500,000 na Jerryson Tegete, aliyefungiwa mechi sita na kutozwa faini ya sh. 500,000.
Wachezaji wengine ni Nurdin Bakari na Omega Seme waliofungiwa mechi tatu kila mmoja na kutozwa faini ya sh. 500,000 na Stephano Mwasika, aliyefungiwa mwaka mmoja na kutozwa faini ya sh. milioni moja.
Katika hatua nyingine, TFF imesema Yanga itapaswa kulipa sh. milioni tano kwa ajili ya kufidia gharama za kutengeneza viti 119 vilivyoharibiwa wakati wa mechi yake ya ligi dhidi ya Azam.
Ofisa Habari wa TFF, Boniface Wambura alisema mjini Dar es Salaam jana kuwa, wamepokea barua kutoka Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo kuhusu uharibifu huo kutokana na vurugu za mashabiki wa Yanga.
Wambura alisema kwa mujibu wa tathmini ya serikali, katika vurugu hizo, jumla ya viti 119 viliharibiwa na gharama za kuvitengeneza upya ni sh. milioni tano, ambazo serikali imeagiza zilipwe mara moja. “Kwa vile mashabiki wa Yanga ndiyo waliohusika na vurugu na uharibifu huo, gharama hizo zitabebwa na klabu hiyo ili serikali iweze kufanya ukarabati haraka,”alisema Wambura.

Wachezaji watano Yanga wafungiwa



Kamati ya Ligi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) iliyokutana Dar es Salaam jana (Machi 12 mwaka huu) imetoa adhabu kwa klabu mbalimbali na wachezaji sita wakiwemo watano wa Yanga.

Villa Squad imepigwa faini ya sh. 500,000 baada ya washabiki wake kufanya vurugu kwenye mechi namba 122 dhidi ya Azam iliyochezwa Februari 15 mwaka huu Uwanja wa Chamazi. Pia klabu hiyo imepigwa faini ya sh. 300,000 kwa kuchelewa uwanjani kwenye mechi namba 129 dhidi ya Mtibwa Sugar iliyochezwa Februari 19 mwaka huu Uwanja wa Manungu. Adhabu hiyo ni kwa mujibu wa Kanuni ya 8(13) ya ligi hiyo.

Nayo Yanga imepigwa faini ya sh. 500,000 kutokana na washabiki wake kufanya vurugu kwenye mechi namba 132 dhidi ya Azam iliyochezwa Machi 10 mwaka huu. Pia klabu hiyo imepigwa faini ya sh. 500,000 kwa mujibu wa Kanuni ya 25(d) baada ya kuoneshwa kadi kuanzia tano kwenye mechi hiyo.

Mchezaji Juma Mohamed wa Polisi Dodoma amefungiwa mechi tatu na kupigwa faini ya sh. 500,000 baada ya kuwashambulia watazamaji kwa chupa ya maji katika mchezo namba 114 kati ya timu yake na Villa Squad uliochezwa Februari 11 mwaka huu.

Nadir Haroub ‘Cannavaro’ wa Yanga amefungiwa mechi sita za Ligi Kuu na kupigwa faini ya sh. 500,000 baada ya kuoneshwa kadi nyekundu kwa kosa la kumshambulia mwamuzi Israel Nkongo kwenye mechi hiyo namba 132.

Wachezaji wengine wa Yanga walioadhibiwa kutokana na mechi hiyo ni Nurdin Bakari amefungiwa mechi tatu na faini ya sh. 500,000, Omega Seme amefungiwa mechi tatu na faini ya sh. 500,000, Jerryson Tegete amefungiwa miezi sita na faini ya sh. 500,000. Stephano Mwasika amefungiwa mwaka mmoja na faini ya sh. milioni moja kwa kumpiga mwamuzi Nkongo. Adhabu zote zimetolewa kwa mujibu wa Kanuni za Ligi Kuu.

Kamati ya Ligi imempongeza nahodha wa Yanga, Shadrack Nsajigwa na mshambuliaji wa timu hiyo Hamis Kiiza kwa kuwa mstari wa mbele kuzuia wenzao kumshambulia mwamuzi. Pia imempongeza kocha Kostadin Papic wa Yanga kwa kukemea vurugu zilizofanywa na wachezaji wake.

Pia Kamati ya Ligi imeiagiza Sekretarieti kutoa waraka kwa makamishna wote wa ligi juu ya utaratibu wa wageni rasmi wakati wa mechi za ligi.

Saturday, March 10, 2012

Waziri Kabaka awafagilia waamuzi kombe la NSSF




TBC hoi kwa Jambo Leo, Habari Z’bar yatoa onyo



WAZIRI wa Kazi na Ajira, Gaudencia Kabaka amewamwagia sifa waamuzi wa soka wa kituo cha Twalipo Academy kwa kuonyesha umahiri mkubwa katika uchezeshaji wa mchezo huo.
Gaudencia alitoa pongezi hizo jana wakati akifungua michuano ya soka na netiboli ya kuwania kombe la Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) kwenye viwanja vya klabu ya Sigara, Dar es Salaam.
Alisema uamuzi wa kituo cha Twalipo kuwapa mafunzo vijana hao ya kuchezesha soka tangu wakiwa mdogo, unastahili kupongezwa kwa vile wameanza kuandaliwa mapema kuwa waamuzi wa baadaye wa michuano mikubwa.
“Hawa vijana (waamuzi) peke yao ni burudani, ni vijana wadogo sana, lakini wanaifahamu vyema kazi yao, napongeza uamuzi wa kuwapa vijana hawa mafunzo ya uchezeshaji soka tangu wakiwa wadogo,”alisema.
Waziri Gaudencia alizitahadharisha timu shiriki katika michuano hiyo kuheshimu sheria za soka na kuepuka kutoa vitisho kwa waamuzi hao kwa sababu ya umri wao. Waamuzi hao kutoka Twalipo Academy wamekuwa wakitumika pia kuchezesha mechi za michuano ya Kombe la Uhai na Copa Cocacola.
Waziri huyo pia aliipongeza NSSF kwa kuendelea kuandaa michuano hiyo, ambayo hutoa fursa ya kuwakutanisha wafanyakazi wa vyombo vya habari nchini na pia kujenga afya zao kupitia michezo.
Viongozi wengine waliohudhuria ufunguzi wa mashindano hayo ni Naibu Waziri wa Kazi na Ajira, Makongoro Mahanga, Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Dk. Ramadhani Dau na maofisa mbalimbali wa shirika hilo.
Katika mechi za ufunguzi zilizochezwa jana, mabingwa watetezi Jambo Leo walianza vyema kuutetea ubingwa wao baada ya kuichapa TBC mabao 2-1.
Katika mechi za netiboli, IPP iliichapa Mwananchi mabao 16-12 wakati Habari Zanzibar iliinyuka bila huruma Global kwa kuitandika mabao 64-0.

Thursday, March 8, 2012

MAKABIDHIANO YA VIFAA VYA MICHEZO NSSF




Bingwa Kombe la NSSF kuzoa mil 3.5/-



MENEJA Kiongozi Idara ya Uhusiano na Huduma za Wateja wa Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), Eunice Chiume (kulia) akikabidhi jezi kwa mwakilishi wa timu ya soka ya Uhuru, Gule Mandago (kushoto) katika halfa iliyofanyika jana kwenye hoteli ya JB Belmont, Dar es Salaam. Wa pili kulia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya Kombe la NSSF, Rashid Zahor na wa pili kushoto ni mratibu wa mashindano hayo kutoka NSSF, Juma Kintu. (Picha na Emmanuel Ndege).
BINGWA wa mwaka huu wa michuano ya soka ya kombe la Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) atazawadiwa kitita cha sh. milioni 3.5 wakati bingwa wa netiboli atazawadiwa sh. milioni tatu.
Zawadi hizo zilitangazwa jana na Meneja Uhusiano wa NSSF, Eunice Chiume alipozungumza na waandishi wa habari kwenye hoteli ya JB Belmont mjini Dar es Salaam.
Eunice alisema mshindi wa pili wa mashindano hayo katika soka atazawadiwa sh. milioni tatu wakati mshindi wa tatu atazawadiwa sh. milioni 2.5.
Kwa mujibu wa Eunice, mshindi wa pili katika netiboli atazawadiwa sh. milioni mbili na wa tatu atazawadiwa sh. milioni moja.
Mbali na zawadi hizo, Eunice alisema kutakuwepo na zawadi maalumu ya sh. 300,000 kwa mwanasoka bora na mcheza netiboli bora.
Eunice alisema mashindano hayo yamepangwa kuanza kesho asubuhi kwenye viwanja vya klabu ya Sigara, Chang’ombe, Dar es Salaam na mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudencia Kabaka.
Katika mechi ya ufunguzi ya soka, mabingwa watetezi Jambo Leo watamenyana na TBC wakati katika netiboli, IPP itamenyana na Mwananchi.
Eunice alisema NSSF imepanga kutumia sh. milioni 150 kwa ajili ya kuandaa mashindano ya mwaka huu na fedha hizo zitatumika kwa zawadi za washindi, vifaa vya michezo, malipo ya viwanja, waamuzi na ulinzi.
Meneja Uhusiano huyo wa NSSF pia alikabidhi vifaa vya michezo kwa timu zote 18 zitakazoshiriki katika soka na timu 12 zitakazoshiriki kwenye netiboli.
Vifaa hivyo ni seti 20 za jezi, pea 20 za soksi, jozi 20 za viatu, shineguards 20 na mipira miwili kwa timu za soka na jezi 12, viatu 12, soksi pea 12, mipira miwili na beaps saba kwa timu za netiboli. Alisema lengo la NSSF kuandaa mashindano hayo ni kuwapa fursa wafanyakazi wa vyombo vya habari kufahamiana na pia kuimarisha afya zao kwa njia ya michezo.
Alizitaka timu shiriki kukubaliana na matokeo wakati wa mashindano hayo na kuepuka kutoa visingizio vya timu pinzani kuchezesha mamluki baada ya kutolewa.
Eunice alisema iwapo timu itakuwa na malalamiko kuhusu jambo lolote, inapaswa kuyawasilisha kwa kamati inayosimamia mashindano hayo badala ya kuiandika vibaya NSSF kupitia kwenye vyombo vyao vya habari.
Alisema katika mashindano hayo, timu za NSSF zitashiriki kama wenyeji, lakini hazitachukua pesa za zawadi iwapo zitashika nafasi tatu za kwanza.
Naye mratibu wa mashindano hayo, Juma Kintu alisema mwaka huu, wameamua kuwatumia waamuzi wa kituo cha Twalipo, ambao wamekuwa wakitumika kuchezesha mechi za kombe la Uhai na Copa Cocacola.

Wednesday, March 7, 2012

Kaburu: Tutaimudu ES Setif


UONGOZI wa klabu ya Simba umejigamba kuwa, hauna wasiwasi wa kupambana na ES Setif ya Algeria katika mechi ya raundi ya pili ya michuano ya Kombe la Shirikisho.
Makamu Mwenyekiti wa Simba, Geofrey Nyange ‘Kaburu’ alisema mjini Dar es Salaam juzi kuwa, wamepanga kujiandaa vyema kabla ya kumenyana na ES Setif.
Simba na ES Setif zinatarajiwa kuvaana Machi 25 mwaka huu katika mechi ya awali ya raundi ya pili itakayochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kabla ya kurudiana wiki mbili baadaye mjini Algiers.
Wekundu hao wa Msimbazi walifuzu kucheza raundi hiyo baada ya kuitoa Kiyovu ya Rwanda kwa jumla ya mabao 3-2.
“Taarifa tulizonazo ni kwamba wapinzani wetu, ES Setif ni wazuri, lakini nasi tutahakikisha tunajipanga vyema kukabiliana nayo,”alisema Kaburu.
Kaburu alisema kamati ya utendaji ya klabu hiyo imepanga kukutana mara baada ya mechi ya ligi kati ya Simba na Kagera Sugar, iliyotarajiwa kuchezwa jana kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Alisema katika kikao hicho, wajumbe watapeana majukumu kuhusu nini kifanyike na kisimamiwe na nani, ikiwa ni pamoja na kutafuta taarifa za wapinzani wao.
Makamu Mwenyekiti huyo wa Simba amewataka wanachama na mashabiki wa klabu hiyo kutoa ushirikiano wa kutosha kwa viongozi ili kufanikisha mipango hiyo.
Alisema lengo la Simba msimu huu ni kuhakikisha timu hiyo inafuzu kucheza ligi ya nane bora ya michuano hiyo kama ilivyokuwa mwaka 2003.

Mercy auza haki za filamu ya harusi yake

LAGOS, Nigeria
MWIGIZAJI machachari Mercy Johnson ameamua kufuata nyayo za Kim Kardasian kwa kuuza haki za picha za filamu za ndoa yake.
Mercy ameuza haki za filamu hiyo, My Wedding kwa Kampuni ya Great Star Production Ltd.
Filamu hiyo, ambayo ilikuwa izinduliwe Februari 17 mwaka huu, uzinduzi wake umeahirishwa hadi hapo baadaye.
Kuahirishwa kwa uzinduzi huo kumetokana na kampuni ya MJ na ile ya Great Star Production kushindwa kufikia makubaliano ya malipo.
Imedaiwa kuwa, tayari kampuni ya MJ, inayomilikiwa na Mercy, imeshalipwa malipo yote, lakini mwanadada huyo anataka kuhakikishiwa malipo mengine kwa mauzo ya baadaye ya filamu hiyo.

Segun Arinze apata mtoto wa pili

LAGOS, Nigeria
MCHEZA filamu mwenye umbile la miraba minne nchini Nigeria, Segun Arinze amepata mtoto wa pili.
Habari zilizoufikia mtandao wa nigeriafilms wiki hii umeeleza kuwa, mke wa Arinze, Julie alijifungua mtoto wa kike Machi 2 mwaka huu mjini Texas, Marekani.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, Julie alijifungua mtoto huyo saa tisa na nusu usiku.
Habari hizo zimeeleza kuwa, hali ya Julie na mtoto huyo inaendelea vizuri.
Juhudi za kumtafuta Arinze ili athibitishe habari hizo hazikuweza kufanikiwa kwa vile hakuwa akipokea simu yake ya mkononi.
Arinze ni rais wa chama cha waigizaji nchini Nigeria (AGN) na anatarajiwa kumaliza muda wake hivi karibuni.

Jim Iyke kuzindua albamu ya muziki



LAGOS, Nigeria
MCHEZA filamu mwenye makeke nchini Nigeria, Jim Iyke amekamilisha mipango ya kuzindua albamu yake mpya.
Jim alisema hivi karibuni mjini hapa kuwa, anatarajia kuzindua albamu hiyo baadaye mwezi huu.
Kwa mujibu wa Jim, uzinduzi wa albamu hiyo umepangwa kufanyika Machi 25 mwaka huu kwenye ukumbi wa klabu ya Aphrodisiac mjini Accra, Ghana.
Jim anakuwa mcheza filamu wa tano wa Nigeria kujihusisha na muziki. Wacheza filamu wengine wanaojihusisha na fani hiyo ni Genevieve Nnaji, Omotola Jalade, Desmond Elliot, Ramsey Nouah na Stella Damasus.
Hivi karibuni, Jim alirekodi vibao viwili akiwashirikisha wanamuziki nyota wan chi hiyo, 2Face Idibia na Puffy T. Vibao hivyo ni Who am I na Born to do this.

Namshukuru Mungu sina kashfa-Chioma




LAGOS, Nigeria
BAADA ya ukimya wa muda mrefu, mwigizaji nyota wa kike nchini Nigeria, Chioma Chukwuka amesema anamshukuru Mungu kwa kutoandamwa na kashfa tangu alipojitosa katika fani ya filamu.
Chioma ameueleza mtandao wa nigeriafilms wiki hii kuwa, bila ya Mwenyezi Mungu, asingeweza kupata mafanikio yoyote katika fani ya uigizaji filamu.
“Ni sala pekee kwa kila ninalotaka kulifanya ndizo zimenifanya nifike hapa nilipo,”alisema mwanadada huyo mwenye sura na umbo lenye mvuto.
“Lakini pia lazima niseme kwamba ni mapenzi ya Mungu. Kama siyo hivyo, kazi ngumu zinaweza kufanyika bila kutambulika,”aliongeza mwanadada huyo mwenye tabasamu la kukata na shoka.
Chioma amemshukuru Mungu kwa kumpa uwezo wa kufanyakazi kwa bidii na pia kumwezesha kupata mafanikio katika fani hiyo.
“Hakuna siri ya mafanikio haya kwa sababu kila unapomweka mbele Mungu katika kazi zako, lazima upate mafanikio katika jambo lolote, huwezi kukumbana na kikwazo,”alisisitiza.
Alipoulizwa ni kwa nini hajawahi kukumbwa na kashfa yoyote tofauti na waigizaji wengine wa kike wa Nollywood, Chioma alisema ni kwa sababu siku zote amekuwa akijichukulia kuwa mtu wa kawaida.
Chioma amesema kamwe katika maisha yake hapendi kujihusisha na mambo yasiyokuwa na maana na kwamba amekuwa akitumia muda wake mwingi kushughulikia masuala ya kifamilia.
“Kama usiponiona kwenye skrini ya sinema, basi ujue nipo na familia yangu nyumbani,”alisema.
Mwanadada huyo alisema siku zote binadamu anahitaji muongozo wa Mungu ili umsaidie kwenda katika njia iliyo sahihi katika kazi na maisha yake.

Osita: Sina papara ya kufunga ndoa




LAGOS, Nigeria
MCHEZA filamu machachari wa Nigeria, Osita Iheme amesema hana papara ya kufunga ndoa kwa sababu suala hilo linahitaji umakini mkubwa.
Osita, ambaye ni maarufu zaidi kwa jina la Ukwa ameueleza mtandao wa nigeriafilms wiki hii kuwa, kila kitu kinakwenda na wakati na kwamba muda wa kufunga ndoa utakapowadia, atafanya hivyo.
“Muda utakapofika, nitawapa taarifa na bila shaka mtapata mwaliko,”alisema mcheza filamu huyo mwenye umbo dogo.
Hivi karibuni, swahiba mkubwa wa mwigizaji huyo, Chinedu Ikedieze alifunga ndoa na Nneomwa kabla ya kwenda kutanua naye Arabuni na Marekani.
Osita ni mmoja wa wacheza filamu wanaoheshimika nchini Nigeria na hivi karibuni alitunukiwa tuzo ya hedhima ya MFR na Rais wa nchi hiyo, Jonathan Godluck.
Alisema anaona fahari kutunukiwa heshima hiyo na kuongeza kuwa, kamwe hawezi kuisahau siku aliyopata tuzo hiyo.
“Siku hiyo haitasahaulika maishani mwangu na naishukuru serikali kwa kutambua mchango wangu,”alisema.
Osita alisema tuzo hiyo imeonyesha jinsi serikali inavyofuatilia mchango wa wasanii wa fani hiyo katika kuleta maendeleo nchini humo kupitia filamu.
Mcheza filamu huyo mwenye mvuto kutokana na umbo na machachari yake, pia ameanzisha mradi maalumu kwa ajili ya kuendeleza utamaduni wa nchi hiyo katika shule za sekondari.