'
Thursday, March 1, 2012
Jabu, Ulimboka wapigwa chini Msimbazi
UONGOZI wa klabu ya Simba umeamua kuwaondoa kambini wachezaji wake wawili, Juma Jabu na Ulimboka Mwakingwe.
Ofisa Habari wa Simba, Ezekiel Kamwaga alisema mjini Dar es Salaam jana kuwa, wachezaji hao wameondolewa kambini kutokana na kuwa majeruhi.
Kamwaga alisema Jabu anasumbuliwa na maumivu ya kifundo cha mguu wakati Ulimboka bado anaendelea kutibiwa nyonga.
Ofisa huyo wa Simba alisema wachezaji wengine wanaendelea na mazoezi kwenye kambi yao iliyopo Mbamba Beach nje ya Jiji la Dar es Salaam kwa ajili ya kujiandaa na mchezo wao dhidi ya Kiyovu ya Rwanda.
Simba inatarajiwa kurudiana na Kiyovu mwishoni mwa wiki hii katika mechi ya michuano ya Kombe la Shirikisho itakayopigwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Katika mechi ya awali iliyopigwa wiki mbili zilizopita mjini Kigali, timu hizo zilitoka sare ya bao 1-1. Ili ifuzu kusonga mbele, Simba inahitaji ushindi wa idadi yoyote ya mabao.
Katika hatua nyingine, Kamwaga amesema kikosi cha Kiyovu kinatarajiwa kutua nchini leo jioni kwa ndege ya Shirika la Ndege la Rwanda.
Ofisa Habari wa Simba, Ezekiel Kamwaga alisema mjini Dar es Salaam jana kuwa, timu hiyo imepangiwa kukaa kwenye hoteli ya Wanyama iliyopo Sinza.
Kamwaga alisema Kiyovu inakuja nchini ikiwa na kikosi cha watu 25 wakiwemo wachezaji, viongozi na benchi la ufundi.
Alisema Simba haina wasiwasi na Kiyovu na kusisitiza kuwa, wamejipanga vyema kuhakikisha wanashinda mechi hiyo na kusonga mbele.
Wakati huo huo, uzinduzi wa kipindi cha Simba, ambacho kitakuwa kinarushwa hewani na kituo cha televisheni cha Clouds umepangwa kufanyika kesho.
Uzinduzi huo utafanyika kwenye ukumbi wa Cleopatra uliopo kwenye jengo la Quality Plaza lililopo barabara ya Nyerere mjini Dar es Salaam.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment