BAADHI ya viongozi wa klabu ya Yanga kwa kushirikiana na tawi moja la klabu hiyo la mjini Dar es Salaam wamepanga mipango ya kumng’oa Kocha Mkuu wa timu hiyo, Kostadin Papic.
Uchunguzi uliofanywa na Burudani umebaini kuwa, mipango hiyo ilianza kusukwa mwanzoni mwa wiki hii, ikiwa ni siku chache baada ya Yanga kutolewa na Zamalek ya Misri katika michuano ya klabu bingwa Afrika.
Kwa mujibu wa uchunguzi huo, utekelezaji wa mpango huo unatarajiwa kuanza keshokutwa, saa chache kabla ya mechi kati ya Yanga na Azam, inayotarajiwa kuchezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Viongozi hao wa Yanga wamepanga kuwashirikisha wanachama wa tawi hilo katika mpango huo kwa kuingia uwanjani na bango lenye maandishi ya kumtaka kocha huyo ajiuzulu.
Mpango huo wa viongozi wa Yanga umelenga kuonyesha hasira zao kwa Papic, ambaye anadaiwa kuwa hataki kupokea ushauri kutoka kwao katika masuala mengi ya msingi, hasa upangaji wa timu.
Viongozi hao pia wamekerwa na kitendo cha Papic kuondoka kambini mjini Cairo, Misri akiwa na wachezaji wawili na kutokomea mahali kusikojulikana.
Yanga ilikwenda Misri kupambana na Zamalek katika mechi ya marudiano ya michuano ya klabu bingwa Afrika, ambapo ilichapwa bao 1-0 na kutolewa kwa jumla ya mabao 2-1.
Hii si mara ya kwanza kwa viongozi wa Yanga kusuka mipango ya kumng’oa Papic. Waliwahi kufanya mipango hiyo mwanzoni mwa mwaka huu, lakini utekelezaji wake ulikwama kwa vile hawakuwa na pesa za kumlipa kwa ajili ya kukatisha mkataba wake.
Sababu zingine za viongozi hao kutaka kumng’oa kocha huyo ni kutokuelewana kwake na baadhi ya wachezaji, ambao amekuwa hawapi nafasi kwenye kikosi cha kwanza.
Wachezaji, ambao kocha huyo amekuwa haelewani na hivyo kutowapanga katika mechi muhimu ni Rashid Gumbo, Godfrey Taita, Chacha Marwa, Geofrey Bonny na Jerryson Tegete na hivyo kusababisha kuzuka kwa makundi mawili ya wachezaji.
Kuna habari kuwa, iwapo Papic atakubali kujiuzulu kutokana na shinikizo hilo la viongozi na wachezaji, huenda nafasi yake ikachukuliwa na Charles Kilinda, ambaye kwa sasa ni kocha wa JKT Ruvu.
No comments:
Post a Comment