'
Wednesday, March 7, 2012
Kipingu apigiwa debe TFF
BAADHI ya watendaji wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na wajumbe wa mkutano kuu wa shirikisho hilo wameamua kumpigia debe Idd Kipingu ili awanie nafasi ya urais wa taasisi hiyo.
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili kwa wiki kadhaa umebaini kuwa, Kipingu anapigiwa debe kuchukua nafasi ya rais wa sasa wa shirikisho hilo, Leodeger Tenga kutokana na uwezo wake kiungozi.
Kipingu aliwahi kuwa mwenyekiti wa kamati ya muda ya kilichokuwa Chama cha Soka nchini (FAT) na pia mwenyekiti wa zamani wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT).
Kwa mujibu wa uchunguzi, Kipingu anapigiwa debe kuchukua nafasi hiyo iwapo makamu wa kwanza wa rais wa zamani wa TFF, Crescentius Magori atakataa kugombea wadhifa huo.
Baadhi ya watendaji wa TFF wamemwelezea Kipingu kuwa ni kiongozi mwadilifu na ndiye pekee mwenye sifa za kumrithi Tenga katika wadhifa huo.
Uchaguzi mkuu wa TFF umepangwa kufanyika mwanzoni mwa mwaka 2013 baada ya uongozi wa sasa chini ya Tenga kumaliza muda wake Desemba mwaka huu.
Tayari Tenga ameshatangaza kuwa hatawania tena nafasi hiyo katika uchaguzi huo, lakini ataendelea kuwa Rais wa Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA).
Wadau wengine wa soka waliotajwa kuizengea nafasi hiyo ni pamoja na katibu mkuu wa zamani wa Yanga, Jamal Malinzi na Makamu wa Kwanza wa Rais wa sasa wa TFF, Athumani Nyamlani.
Inadaiwa kuwa, tayari Nyamlani na Malinzi wameshaanza kufanya kampeni za kuwania wadhifa huo kwa kutembelea katika mikoa mbalimbali nchini kwa lengo la kuwashawishi wapiga kura.
Juhudi za kumtafuta Kipingu ili aeleze iwapo anakubaliana na maombi ya wadau kumtaka agombee wadhifa huo, hazikuweza kufanikiwa kwa vile siku nzima ya jana hakupatikana kupitia simu yake ya mkononi.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment