SIMBA imeendelea kujichimbia kileleni na kuwaacha kwa tofauti ya pointi tatu wapinzani wao Yanga wanaofukuzana nao katika msimamo wa ligi kuu, baada ya kuifumua Kagera Sugar mabao 3-1.
Katika mechi hiyo iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, vinara hao wa ligi wakiwa na pointi 40 kibindoni na Yanga pointi 37, walishinda kutokana na Kagera kushindwa kuonyesha upinzani kabisa huku ukosaji mabao ukitawala kwa pande zote.
Baada ya dakika 20 za kosa kosa, Simba walisahihisha makosa kwa kiungo mshambuliaji Patrick Mafisango kufunga bao la kwanza dakika 26 kutokana na kupiga shuti kali ambalo kipa wa Kagera Andrew Ntalla, alishindwa kuliona.
Mafisango alifunga goli hilo kutokana na pasi maridadi ya Juma Nyoso aliyewahi mpira wa adhabu na kumpasia kiungo huyo.
Baada ya bao hilo timu hizo ziliendelea kushambuliana kwa zamu na Kagera hawakucheza kwa kasi kama Simba na walipoteza muda mwingi wakati wa kurusha mipira.
Walinzi Nassoro Masoud 'Cholo' na Amir Maftah walipandisha vyema mashambulizi kwa upande wa Simba iliyowapa wakati mgumu Kagera ambao walikuwa wanawategemea Shija Mkina anayecheza kwa wakata miwa hao kwa mkopo kutoka Msimbazi na Paulo Ngwai.
Katika dakika za mwanzo, wachezaji walikuwa wanateleza kutokana mvua iliyonyesha kabla ya kuanza mchezo huku Simba wakinusurika kufungwa dakika 10 na Mkina, ambaye alipiga mkwaju uliodakwa kwa umakini na kipa Juma Kaseja.
Mkina alipata nafasi hiyo kutokana na kazi nzuri iliyofanywa na Muganyizi Martin ya kuwachambua mabeki wa Simba na kutoa 'pande' hilo, huku shambulizi hilo likijibiwa na Emmanuel Okwi aliyewalamba chenga walinzi wa Kagera na kuachia shuti ambalo lilitoka nje na kuwa kona butu.
Yona Ndabila naye, alimchachafya Amir Maftah na kupata mwanya wa kupiga shuti ambalo lilitoka nje sentimita chache na lango la Simba. Said Dilunga pia shuti lake lilishindwa kulenga lango la Simba dakika tatu kabla mapumziko.
Kipindi cha pili Simba walionekana wana uchu wa kuendeleza ushindi kutoka na kuwashambulia Kagera, ambapo 50 kama Felix Sunzu angekuwa makini angeipatia timu hiyo bao kutokana na mpira wake wa kichwa kutoka nje licha ya kuwazidi kete vizuri mabeki kwa kuwahi mpira wa juu.
Dakika 54 Katende alijibu mapigo kwa kumpa pasi Ndabila, lakini naye alifuata nyayo za Sunzu kwa kukosa bao na Felix Themi alisawazisha makosa ya wachezaji hao ya kukosa ufundi wa kulenga milango kwa kufunga bao la kusawazisha kwa wageni hao.
Themi aliyeingia badala ya Mkina alifunga bao hilo dakika 57 kwa shuti kali lililomshinda Kaseja aliyeanza kupangua krosi ya Katende na kumkuta mfungaji.
Kagera baada ya kusawazisha bao hilo waliridhika na kuanza kujiangusha na kusababisha mwamuzi Ronald Swai kutoka Arusha kumuonya kwa mdomo kipa Ntalla kwa kupoteza muda. Mwamuzi Swai aliwapa Simba penalti kutokana na beki David Charles kumuangusha Shomari Kapombe katika kisanduku cha hatari na 'tuta' hilo lilifungwa na Mafisango dakika 90, huku uzembe ukiendelea kuwagharimu Kagera kwa Sunday Frank kunyang'anywa mpira na Sunzu aliyepiga krosi iliyomkuta Okwi aliyepiga chenga mabeki na kufunga bao la tatu dakika za majeruhi.
Simba: Juma Kaseja, Nassoro Masoud, Amir Maftah, Kelvin Yondan, Juma Nyoso, Jonas Mkude, Shomari Kapombe, Patrick Mafisango, Felix Sunzu, Haruna Moshi 'Boban' na Emmanuel Okwi.
Kagera: Andrew Ntalla, Muganyizi Martin, David Charles, Freeman Nesta, Sunday Frank, George Kavila, Shija Mkina/Felix Themi, Daud Jumanne,Said Dilunga/Mike Katende, Yona Ndabila na Paulo Ngwai.
No comments:
Post a Comment