KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, December 8, 2010

NATAFUTA KAZI


MIMI NI MSICHANA MWENYE UMRI WA MIAKA 25, MKAZI WA ARUSHA, NATAFUTA KAZI YA NDANI KWENYE NYUMBA YOYOTE YA KIONGOZI WA SERIKALI AMA MFANYABIASHARA. KWA ALIYE TAYARI KUNIPATIA AJIRA, AWASILIANE NAMI KUPITIA NAMBA HII YA KAKA YANGU 0774-455808

Friday, December 3, 2010

Wacheza filamu wanaong'ara Bongo




STEVEN KANUMBA
Amedhihirisha kwamba ujuzi wa kuigiza haupatikani kwa kukaa kwenye darasa lenye kuta nne na kujifunza, bali ni kipaji cha kuzaliwa na ubunifu wa kila mara.
Ni msanii ghali ambaye 'hakodishiki' na watayarishaji filamu wa Bongo zaidi ya wafanyabiashara wenye asili ya kiasia, maarufu kama Wadosi. Kwa sasa, Kanumba ameamua kuwa mtayarishaji filamu na pia msanii kwa wakati mmoja na ni kipenzi cha mashabiki wengi wa fani hiyo katika nchi za Afrika Mashariki. Sura yake pekee inatosha kuuza filamu husika.

VICENT KIGOSI 'RAY'
Kwa mujibu wa watayarishaji wa filamu, Ray ndiye msanii ghali zaidi wa kiume nchini, ambaye anapendwa na mashabiki wengi ndiyo sababu katika filamu kumi bora nchini, huwa ameshiriki katika filamu saba. Ukizungumzia filamu za Tanzania kwa sasa, unamzungumzia Ray na kipaji chake kimempa thamani kubwa mbele ya jamii.

JACOB STEVEN 'JB'
Ni msanii mwenye vituko, ambaye ukimuona akiwa mtaani kwake Sinza jijini Dar es Salaam, huwezi kuamini kuwa ndiye staa unayemuona kwenye filamu kwa jinsi anavyojirahisisha.Amekamata sehemu kubwa ya soko na asilimia kubwa ya filamu alizocheza zinafanya vizuri sokoni. Hivi karibuni, JB aliwahi kutaka ajulikane kwa jina la Amitha Bachchan, mwigizaji nyota wa zamani wa Kihindo.
SINGLE MTAMBALIKE 'RICH'
Katika wasanii waliokaa miaka mingi kwenye tasnia hiyo, Rich ni mmojawapo kwani miaka ya nyuma aliwahi kutamba katika maigizo ya televisheni. Ni msanii mwenye staili ya aina yake, ambaye muda wowote ule unatamani kumuangalia kwenye filamu na maharamia wengi wamekuwa wakinufaika kwa kuuza kinyemela kazi zake na mastaa wengine.
MZEE CHILO
Babu ndiyo jina linalomtambulisha zaidi katika fani ya filamu. Anaweza akawa ndiye msanii mwenye umri mkubwa kuliko wote kwenye tasnia ya filamu nchini, lakini hakuwahi kuwaboa mashabiki. Amefiti kwenye sehemu nyingi alizoigiza na anathibitisha usemi kuwa 'Simba hazeeki maini' kwani amekuwa akifanya vitu, ambavyo hata vijana wa kisasa hawawezi kufanya wala kuiga.
MAHSEN AWADHI 'CHENI'
Hana haja ya kutambulishwa kwa mashabiki wa filamu nchini kwani ameifanya kazi hiyo miaka mingi na uzoefu wake unamsaidia kwani anafiti kila sehemu anayoigiza.
Anazo staili zake, ambazo zimekuwa zikisisimua mashabiki wake kila wanavyomuangalia kwenye runinga na ni ngumu kutamani filamu imalizike ndiyo maana soko lake litazidi kuwa juu siku zote.
TINO
Kwa mujibu wa watayarishaji wa filamu, msanii huyu ni miongoni mwa mastaa wa kiume wanaopendwa sana na mabinti ndiyo maana hupenda kumtumia zaidi kwenye filamu za mapenzi.
Kila anapocheza filamu, anatoka na staili mpya na unadhifu wake pamoja na utundu imeelezwa kuwa ni miongoni mwa vitu vinavyomfanya azidi kupendwa.
CLOUD
Si msanii ghali sana kwa mujibu wa watayarishaji wa filamu, lakini cha kushangaza ni kwamba, amefanya kazi nyingi kwa kiwango cha juu, ambacho wakati mwingine huwafunika hata waigizaji maarufu zaidi yake. Yumo miongoni mwa wasanii mahiri na wenye majina makubwa nchini kuanzia kwenye maigizo mpaka filamu.
CHUZI
Ana majukumu mengi katika tasnia hiyo kwani mbali na kuwa mwigizaji, anahusika kwa kiasi kikubwa katika kutengeneza filamu na tamthilia mbalimbali, ambazo zinafanya vizuri. Amejijenga vilivyo na anadhihirisha kipaji chake kwenye runinga.
HEMED NA MLELA YUSUF
Wanachosema baadhi ya watayarishaji wa filamu ni kwamba, wasanii hawa ni wepesi wa kuelewa ndio sababu wamekuwa wakipenda kufanyanao kazi katika filamu na kung'ara, ingawa hawako miaka mingi. Wanapewa nafasi kubwa ya kuzidi kung'ara kadri siku zinavyoendelea kwa vile wamepokelewa vizuri sokoni, ingawa imewahi kuvumishwa kuwa waligombana na baadaye wakasuluhishwa.
NURDIN MOHAMMED a.ka.Chekibudi
Hadhi yake kwa mashabiki imekuwa juu sana katika miezi ya hivi karibuni kutokana na kushiriki kucheza filamu nyingi, ambazo zimefanya vizuri na sura yake imetokea sana. Imefahamika rangi yake ndiyo inachengua mashabiki wa fani hiyo hasa wa kike.
BABA HAJI NA SAJUKI
Wana miaka kadhaa kwenye fani hiyo ya uigizaji na kila kukicha wamekuwa wakifanya mambo ambayo yamekuwa yakizidi kuwakuza na kuongeza thamani yao. Ingawa wanaweza wakawa si maarufu sana kwa mashabiki kama walivyo mastaa wengine, filamu nyingi walizoigiza zimefanya vizuri sokoni.
IRENE UWOYA
Hashikiki kwa gharama. Baadhi ya watayarishaji wa filamu wamemuelezea kuwa ni msanii wa kike anayependwa zaidi kwa sasa na ghali zaidi, ingawa yeye mwenyewe amekuwa mara kadhaa akikataa.Uzuri wake, umbo na kipaji ndivyo vitu vinavyombeba. Inadaiwa kuwa ni miongoni mwa wasanii, ambao hata akiigiza upuuzi, mashabiki lazima wanunue filamu yake bila kujali.
ROSE NDAUKA
Silaha yake kubwa ni ubunifu ingawa hata uzoefu umemsaidia na kwamba yupo katika orodha ya wasanii bora watano wa kike kwa sasa kwenye filamu za Tanzania.Hakuna anayemuangalia kwenye video akaacha kutabasamu. Anaigiza kwa hisia zinazoteka akili ya mtazamaji.
AUNT EZEKIEL
Uzuri wake pamoja na staili za mavazi vinambeba, lakini neno unaloweza kutumia kumuelezea ni kwamba ana kipaji cha ukweli. Utundu wake katika kuigiza umewatoa wengi machozi kama si kuwafanya wabadili staili ya maisha kutokana na funzo wanalopata. Imeelezwa kuwa hata kashfa zinazomuandama kila siku zimemjengea jina na kumuongezea mashabiki zaidi.
JACKLINE WOLPER
Ukweli unabaki palepale kwamba ni msanii, ambaye muda wowote utavutika kumuangalia yeye binafsi au filamu aliyoigiza kutokana na staili yake na urembo aliojaliwa. Awe anaigiza kama mpenzi au mke, anafanya vizuri kazi yake kuanzia mwanzo mpaka mwisho.
MONALISA
Tofauti yake na wenzake ni kwamba ana uzoefu mkubwa, ambao pengine katika wasanii wa umri wake wanaong'ara kwa sasa, hakuna wa kumfunika kwa hilo. Wadau wanadai kuwa ni mkali kwenye uigizaji mara mbili au tatu ya Uwoya na Aunt Ezekiel, lakini wao wamekuwa maarufu zaidi kutokana na haiba zao na kashfa za kila kukicha.
JOHARI
Zilipoanza kuvuma filamu, ndio alikuwa kama malkia na wasanii wengi wa kike wanaotamba kwa sasa wamejifunza mambo mengi kutoka kwake. Ni msanii mwenye mvuto, ambaye hawezi kufanana na wenzake kutokana na ubunifu wake na kufanya mambo kwa kiwango cha juu zaidi. Wadau wanadai alistahili kuwa tajiri mkubwa kwa sasa kutokana na kipaji chake.
RIHAMA ALLY
Ni msanii mwenye kipaji cha aina yake, ambacho hakuna mtayarishaji yeyote wa filamu anaweza kupuuzia au kuacha kukitumia. Sababu kubwa ya kutumika kwenye filamu nyingi ni kutokana na kuwapa mashabiki kile wanachohitaji na anajiamini mno ndio maana hakuwahi kufanya vibaya.
MAMA KAWELE
Ukiangalia filamu yake, hutabanduka kwenye kiti kwa jinsi alivyo na uwezo mkubwa wa kucheza na hisia zake na kukusisimua kwa kile atakachokuwa akiigiza.
FLORA MVUNGI
Hazuiliki ni mjanja balaa. Kuanzia watayarishaji wa filamu mpaka wasanii wenzake wanakubaliana na hilo bila ubishi, ndiyo maana amezidi kuwa juu siku zote. Kipaji chake kinafanya filamu ionekane kamili na ndio sababu kubwa ya kupendwa.
MAYA
Yamesemwa mengi, lakini hakuna anayeweza kuwa kama yeye wala kufanya anachokifanya kwenye filamu, ndio maana wasanii wakubwa kama Ray na Kanumba wanapenda kumtumia mara nyingi kwenye kazi zao. Anateka nyoyo za watazamaji na kuwaacha kwenye ulimwengu wa kufikirika.
THEA
Wanajaribu kumpambanisha na Rihama pamoja na Aunt Ezekiel, lakini mwisho wa siku anabaki kuwa juu na kuthibitisha kwamba uzoefu ni kitu muhimu katika kila jambo. Anajua anachokifanya na mashabiki wanamfanya thamani yake izidi kupanda.
LULU
Ni binti mdogo, ambaye amejipatia umaarufu wa haraka kwa muda mfupi kutokana na kipaji alichoonyesha kwenye filamu kadhaa alizofanya chini ya Ray, lakini hata mvuto wake unachanganya wengi. Alikumbwa na kashfa za hapa na pale katika miezi ya hivi karibuni ambazo ni kubwa kushinda umri wake na zimechangia kukuza jina lake na kufanya mashabiki wamfuatilie.
MAINDA
Ray amemkubali, ingawa imekuwa ikielezwa kuwa wana uhusiano wa kimapenzi, lakini msanii huyo wa kike ni kama ametekwa kabisa na Ray kwani katika filamu zake karibu zote yumo na amefanya vizuri na thamani yake ni kubwa.
JINI KABULA
Kabula, ambaye aliwahi kuwa na uhusiano na mwanamuziki Mr. Nice, kazi zake zimemfanya amekuwa maarufu na ni ngumu kumfunika. Ni msanii mwenye kipaji cha aina yake ambaye, orodha hii ya wasanii wanaotumika sana kwenye filamu haiwezi kutimia bila jina lake kuwepo.
NORA
Ukifanya tathmini ya haraka, unaweza kusema Nora na Johari wamefunikwa na vijana wanaowika kama Uwoya na Aunt Ezekiel, lakini kwa mujibu wa maelezo ya watayarishaji wa filamu, wasanii hao ni tofauti na kila mmoja ana thamani yake na bado anakubalika sokoni.

Thursday, December 2, 2010

Wacongo wa Yanga wakwama Dar

KLABU ya Yanga imesema, itawasajili wachezaji wake wapya, Itubu Imbem na Selenga Motitya kutoka Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo wakati wa msimu wa ligi wa 2011/12.
Habari za kuaminika kutoka ndani ya Yanga zimeeleza kuwa, klabu hiyo imeshindwa kuwasajili wachezaji hao wakati wa usajili wa dirisha dogo kutokana na kushindwa kupata vibali vya uhamisho wa kimataifa kutoka klabu yao.
Wachezaji hao wawili wanatoka timu ya AFC Leopards ya Kenya, Itubu akiwa anacheza nafasi ya ushambuliaji wakati Selenga ni mchezaji wa kiungo.
Chanzo cha habari kutoka ndani ya Yanga kimeeleza kuwa, wachezaji hao wawili waliletwa nchini na Makamu Mwenyekiti wa klabu hiyo, Davis Mosha kwa ajili ya usajili wa dirisha dogo.
“Tatizo ni kwamba wachezaji hao walikuja wakati zikiwa zimebaki siku chache kabla ya usajili wa dirisha dogo kufungwa, hivyo haikuwa rahisi kufanya mazungumzo na klabu yao na kuwapatia uhamisho wa kimataifa,”kilisema chanzo hicho.
Kiliongeza kuwa, kufuatia usajili wao kukwama, uongozi umepanga kuwasajili katika ligi ya msimu wa 2011/12 iwapo benchi la ufundi litaridhishwa na viwango vyao vya soka.
Mtoa habari huyo alisema, timu hiyo inatarajiwa kuanza mazoezi kesho kwenye uwanja wa shule ya kimataifa ya Tanganyika, Dar es Salaam ikiwa chini ya Kocha Kostadin Papic.
“Lengo letu ni kuwabakisha ili tuwasajili katika ligi ya msimu ujao, lakini kabla ya kufanya hivyo, lazima tuwajaribu na kuridhishwa na viwango vyao,”alisema.
Katika usajili huo wa dirisha dogo, Yanga imefanikiwa kuwasajili mshambuliaji Davis Mwape kutoka Zambia na Juma Sefu kutoka JKT Ruvu ya mkoani Pwani.
Mwape amesajiliwa kwa ajili ya kuziba pengo la Kenneth Asamoah kutoka Ghana, ambaye klabu ya Yanga imeshindwa kupata uhamisho wake wa kimataifa kutoka katika klabu aliyokuwa akiichezea nchini Serbia.
Katika hatua nyingine, uongozi wa Yanga umeshindwa kufikia makubaliano na klabu ya African Lyon kuhusu usajili wa mkopo wa kipa Ivan Knezevic kutoka Serbia.
Yanga ilipanga kumuuza kipa huyo Lyon ili ipate nafasi ya kusajili mchezaji mwingine kutoka nje ya nchi kwa vile tayari imeshafikisha wachezaji watano wanaohitajika kwa mujibu wa kanuni.
Mmoja wa viongozi wa Yanga alithibitisha jana kuwa, viongozi wa Lyon wamegoma kumnunua kipa huyo kwa mkopo kwa madai kuwa, hawamuhitaji.

KUMBE JK MKALI WA KUPIGA GITA!


RAIS Jakaya Kikwete akipiga gita wakati alipowaongoza wanafamilia, kumpongeza mkewe, Mama Salma Kikwete wakati wa sherehe ya kutimiza miaka 47 iliyofanyika Ikulu mjini Dar es Salaam jana. (Picha ya Ikulu).

SAM WA UKWELI: Namshukuru Mungu, sasa nimetimiza malengo yangu


KWA kipindi cha takriban miezi mitatu sasa, kibao cha ‘Sina raha’ cha msanii Salum Mohamed Salum, maarufu kwa jina la ‘Sam wa Ukweli’, kimekuwa kikishika chati kwenye vituo mbalimbali vya radio na televisheni nchini.
Kushika chati kwa kibao hicho kumetokana na mambo mawili makubwa. Kwanza ni mpangilio wa ala za muziki na sauti mwanana ya mwimbaji na pili ni ujumbe uliomo kwenye kibao hicho.
Ni kibao kinachozungumzia masuala ya mapenzi, ambapo kijana Sam wa Ukweli anasikika akimlalamikia mwanadada fulani kwa kumtesa kimapenzi kiasi cha kumfanya asiwe na raha.
Akizungumza na Burudani wiki hii, Sam alikiri kuwa, kibao hicho kimempatia umaarufu mkubwa nchini kutokana na kukubalika kwa mashabiki wengi wa muziki wa kizazi kipya.
Kibao hicho ndicho kilichobeba jina la albamu yake ya kwanza yenye jumla ya vibao kumi. Mbali na ‘Sina raha’, vibao vingine vilivyomo kwenye albamu hiyo ni ‘Hata kwetu wapo’, ‘Usiniache mchumba’, ‘Lifti’, ‘Utamu ulokela’, ‘Lonely’, ‘Huwezijua’, ‘Penzi la kushare’, ‘Tunda la msimu’ na ‘Sina raha remix’.
“Kwa kweli kibao hiki kimefanya vizuri sana sokoni kuliko nilivyotarajia. Ni kibao kilichoniweka kwenye chati ya juu. Nashukuru kwamba mashabiki hivi sasa wananikubali sana,”alisema Sam.
“Nawashukuru mashabiki kwa kunisapoti. Kwa kweli hivi sasa ukitaja majina ya wasanii watatu wa muziki wa kizazi kipya hapa nchini, jina langu haliwezi kukosekana,”aliongeza msanii huyo, asiyekuwa na makeke.
Sam alisema albamu hiyo iliyoanza kuuzwa Oktoba mwaka huu na ambayo aliirekodi kwenye studio za Imotion Records za mjini Dar es Salaam, imemwezesha kutimiza mahitaji yake mengi muhimu ya kimaisha.
“Nashukuru kwamba hivi sasa napata pesa ya ugali, siwezi kufa njaa. Nina uwezo wa kununua kila ninachokihitaji kwa mahitaji muhimu ya kibinadamu,”alisema.
Sam alisema anashukuru kwamba, mafanikio ya albamu yake hiyo sokoni yametimiza malengo aliyokuwa amejiwekea baada ya safari ndefu ya kiusanii, iliyokuwa na vikwazo vya kila aina.
Alivitaja baadhi ya vikwazo alivyokuwa akikabiliana kuwa ni pamoja na kukosekana kwa studio za kurekodi nyimbo mahali alikokuwa akiishi, Kiwangwa mjini Bagamoyo mkoani Pwani.
“Kwa kweli, vikwazo nilivyowahi kukumbana navyo kimuziki ni vingi na vya kukatisha tamaa, lakini nilipiga moyo konde na kuamua kupambana navyo, nikiamini kwamba ipo siku Mungu atajibu dua zangu,”alisema.
Kufuatia mafanikio aliyoyapata, Sam alisema kwa sasa anajiandaa kurekodi wimbo mpya pamoja na video yake, akiwashirikisha wasanii chipukizi wawili, Miundombinu na Sal B kwa lengo la kuibua vipaji vyao.
Msanii huyo alisema kwa sasa, wapo wasanii wengi chipukizi wenye vipaji hapa nchini, lakini tatizo kubwa linalowakabili ni uwezo mdogo wa kifedha kwa ajili ya kurekodi nyimbo zao.
Alisema gharama za kurekodi nyimbo studio pamoja na kutengeneza kanda za video ni kubwa na kuongeza kuwa, kwa wasanii wengi chipukizi si rahisi kumudu gharama hizo.
Sam amewashukuru maprodyuza wa muziki, waandishi wa habari na watangazaji wa vituo vya radio kwa kumpa sapoti na kuzipa nafasi kazi zao kusikika na kutambulika kwa mashabiki.
Ametoa wito kwa wasanii chipukizi kufanyakazi kwa kujituma na pia kuipenda kazi yao ili iweze kuleta ushindani katika soko la muziki na kuwavutia mashabiki.
Sam, ambaye anavutiwa na wasanii Ambwene Yesaya ‘AY’ na Judith Wambura ‘Lady JayDee’, alianza kujihusisha na muziki mwaka 2005 kwa kuimba nyimbo za kuiga za wanamuziki mbalimbali wa zamani kama vile marehemu Marijani Rajabu na za bendi ya Msondo Ngoma.
Kutokana na umahiri wake wa kuiga nyimbo hizo, baadhi ya jamaa zake walimshauri ajitose kwenye fani hiyo kikamilifu kwa kutunga na kuimba nyimbo zake mwenyewe.
Hata hivyo, hakuweza kurekodi nyimbo hizo hadi mwaka 2007 baada ya kukutana na prodyuza Kisaka, ambaye alimshirikisha kwenye tamasha la kusaka vipaji lililofanyika kwenye ukumbi wa Moment Park, Kiwalani Dar es Salaam. Katika tamasha hilo, Sam aliibuka mshindi.
Baada ya kushinda tamasha hilo, Sam aliingia mkataba na Prodyuza Sam kwa ajili ya kurekodi nyimbo zake kupitia lebo ya kampuni yake na hadi sasa yupo chini ya kampuni hiyo.

Z'bar yajiweka pabaya Kombe la Chalenji


TIMU ya soka ya Zanzibar, Zanzibar Heroes jana ilikwaa kisiki katika michuano ya Kombe la Chalenji baada ya kupokea kichapo cha bao 1-0 kutoka kwa Ivory Coast katika mechi ya kundi B iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Kipigo hicho kimeiweka Zanzibar Heroes kwenye nafasi ngumu ya kutinga robo fainali, ambapo sasa italazimika kushinda mechi yake ya mwisho dhidi ya Rwanda itakayochezwa kesho.
Pamoja na kupata kipigo hicho, Zanzibar Heroes inashika nafasi ya pili katika msimamo wa kundi hilo, ikiwa na pointi tatu sawa na Ivory Coast, lakini ipo mbele kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa.
Mshambuliaji Kipre Bolou ndiye aliyepeleka kilio kwa Zanzibar baada ya kuifungia Ivory Coast bao hilo pekee na la ushindi dakika ya 61. Alifunga bao hilo kwa shuti kali la umbali wa mita 30.
Katika pambano hilo, Ivory Coast ilionyesha kiwango cha juu cha soka, hasa kipindi cha kwanza kabla ya Zanzibar kushtuka dakika za mwisho, lakini washambuliaji wake walipoteza nafasi kadhaa za kufunga mabao.
Katika mechi nyingine ya kundi hilo iliyochezwa jana, Rwanda na Sudan zilishindwa kutambiana baada ya kutoka suluhu.
Pambano hilo halikuwa na msisimko mkali kutokana na timu zote mbili kushindwa kuonyesha soka ya kuvutia.

SHIBOLI, mshambuliaji mpya wa Simba mwenye ndoto za kufika mbali kimuziki

MSHAMBULIAJI nyota wa timu ya Zanzibar, Zanzibar Heroes, Ally Ahmed Shiboli ametamba kuwa, ataibuka mfungaji bora katika michuano ya mwaka huu ya Kombe la Chalenji inayoendelea kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Akizungumza na Burudani mjini Dar es Salaam wiki hii, Shiboli alisema amedhamiria kuibuka mfungaji bora wa michuano hiyo ili aweze kutimiza malengo aliyojiwekea kisoka.
Majigambo hayo ya Shiboli yamekuja siku chache baada ya kuifungia Zanzibar mabao mawili, ilipoibwaga Sudan mabao 2-0 katika mechi ya kundi B iliyochezwa kwenye uwanja huo.
“Nimedhamiria kumaliza mashindano haya nikiwa mfungaji bora. Ndoto yangu imeanza kukamilika kwani nimeweza kufunga mabao mawili peke yangu katika mechi moja,”alisema.
Mshambuliaji huyo aliyesajiliwa na klabu ya Simba katika usajili wa dirisha dogo akitokea KMKM ya Zanzibar alisema, amepania kuifungia bao Zanzibar katika kila mechi atakayocheza.
“Nimedhamiria kucheza kwa kujituma na kuifungia timu yangu mabao mengi zaidi ili tumalize mechi za kundi letu tukiwa wa kwanza,”alisema.
Shiboli alisema Zanzibar imeanza vyema michuano ya mwaka huu kutokana na maandalizi mazuri waliyoyafanya ikiwa ni pamoja na wachezaji kufuata vyema mafunzo ya Kocha Stewart Hall kutoka Uingereza.
Zanzibar ilitarajiwa kutupa karata yake ya pili jana kwa kumenyana na Ivory Coast, ambayo katika mechi yake ya kwanza, ilichapwa mabao 2-1 na Rwanda.
Akizungumzia usajili wake Simba, Shiboli alisema alikuwa na ndoto za kuichezea timu hiyo kwa kipindi kirefu, lakini hakuwa akifahamu angewezaje kufika huko.
Alisema aliposikia kwamba viongozi wa Simba, Yanga na Azam, zote za Dar es Salaam wanamtafuta, alifarijika kwa kutambua kwamba kiwango chake kimewakuna.
Shiboli aliwavutia viongozi wa klabu hizo tatu baada ya kuonyesha soka ya kiwango cha juu wakati Zanzibar Heroes ilipomenyana na Dar es Salaam All Stars katika mechi za kirafiki zilizochezwa Dar es Salaam na Zanzibar.
Awali, Mwenyekiti wa klabu ya Yanga, Llyord Nchunga aliwaambia waandishi wa habari mjini Dar es Salaam wiki iliyopita kuwa, walikuwa katika hatua za mwisho za kumsajili mchezaji huyo na kwamba mazungumzo kati yao yalikuwa yakienda vizuri.
Lakini siku chache baadaye, Makamu Mwenyekiti wa Simba, Geofrey Nyange ‘Kaburu’ alitoa taarifa kuwa, klabu hiyo imefanikiwa kumsajili Shiboli kwa mkataba wa miaka mitatu.
Shiboli anatarajiwa kuanza kuichezea Simba katika mzunguko wa pili wa ligi kuu ya Tanzania Bara, unaotarajiwa kuanza Januari 15 mwakani. Simba inaongoza ligi hiyo kwa tofauti ya pointi mbili kati yao na watani wao wa jadi Yanga.
Alipoulizwa kuhusu matarajio yake kwa Simba, Shiboli alisema hawezi kuwaahidi mengi mashabiki wa timu hiyo, lakini alisisitiza kuwa, atacheza kwa kujituma ili kuisaidia ifanye vizuri katika ligi hiyo.
“Ni vigumu kwa sasa kusema nitafanya nini Simba kwa sababu mimi ni mgeni na ligi kuu ya Tanzania Bara, lakini kwa vile lengo langu ni kupata mafanikio zaidi kisoka, nitafanya kila ninaloweza kuisaidia timu yangu mpya,”alisema.
Wakizungumzia usajili wa mchezaji huyo, baadhi ya wachezaji nyota wa Simba, akiwemo kipa Juma Kaseja walikiri kuwa, timu yao imepata mshambuliaji hatari na mwenye uwezo wa kuiletea mafanikio zaidi.
Kaseja alisema Shiboli ni mshambuliaji mwenye uwezo wa kufanya lolote kila anapofika karibu na lango la upinzani na pia ana uwezo mkubwa wa kufunga mabao kwa mashuti ya mbali.

Thursday, November 25, 2010

Yanga yagonga mwamba kwa Lyon

JARIBIO la klabu ya Yanga kumtoa kwa mkopo kipa Ivan Knezevic kwa ajili ya kupata nafasi ya kumuongeza mshambuliaji Davies Mwape, limegonga mwamba, kufuatia timu ya African Lyon kugoma kumsajili kipa huyo.

Mabingwa hao wa zamani wa ligi kuu ya Vodacom walipanga kumpeleka kwa mkopo kipa huyo African Lyon, lakini timu hiyo imesisitiza haimuhitaji mzungu huyo kutoka Serbia.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi katika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam juzi, mmiliki na meneja mkuu wa African Lyon, Rahim Kangezi alisema wanahitaji wachezaji wazawa zaidi.

“Sisi wenyewe tunatafuta wachezaji wa ndani ili wakifanya vizuri tuwauze, sasa kwa nini tumchukue kipa wa Yanga, ambaye ni mzungu?” Alihoji Kangezi.

Alisema hawana mpango na mchezaji yeyote wa kigeni na waliopo kwenye timu hiyo waking’ara, watawauza nje na ‘biashara’ hiyo inaanzia kwa wachezaji Mbwana Samatta na Hamis Thabiti, ambao wanapelekwa Benfica ya Ureno.

Alisema wachezaji hao walitarajiwa kuondoka jana nchini kwenda kufanya majaribio katika klabu hiyo, huku Jona Kajuna na beki Meshack Abel wakipelekwa Marekani kutafutiwa timu.

“Wachezaji wote wanne wanaondoka Jumatano (jana) na watakuwepo katika nchi hizo kufanya majaribio,” alisema Kangezi.

Kangezi pia alikanusha madai kuwa, Simba imemrejesha Meshack kwa maelezo kwamba, mchezaji huyo anakwenda nje kujaribu bahati yake na kamwe hawezi kukubali kurejea Msimbazi, ambako alikuwepo misimu miwili iliyopita kabla ya kuhamishwa Lyon kwa mkopo.

Wednesday, November 24, 2010

Dk. Nchimbi kuongoza michezo



RAIS Jakaya Kikwete amemteua Dk. Emmanuel Nchimbi kuwa Waziri wa Habari, Vijana na Michezo.

Kabla ya uteuzi huo, Dk. Nchimbi alikuwa Naibu Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa katika awamu ya kwanza ya serikali ya nne ya Rais Kikwete.

Dk. Nchimbi amechukua nafasi ya George Mkuchika, ambaye katika baraza jipya lililotangazwa jana, amehamishiwa katika Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa.

Katika uteuzi huo, Rais Kikwete pia amemteua Dk. Renella Mukangara kuwa Naibu Waziri wa Habari, Vijana na Michezo.

Dk. Renella amechukua nafasi ya Joel Bendera, ambaye alishindwa katika kura za maoni za uteuzi wa mbunge wa jimbo la Korogwe Vijijini.


Caption
VILIMA KWA VILIMA HAVIKUTANI, LAKINI BINADAMU HUKUTANA!
KOCHA wa makipa wa timu ya soka ya Taifa, Taifa Stars, Juma Pondamali (kulia) akisalimiana na wachezaji wenzake wa zamani wa timu hiyo, Athumani Juma 'Chama' (kushoto) na Mohamed Mwameja (katikati) wakati wa mazishi ya mwanasoka wa zamani nchini, Juma Mkambi yaliyofanyika Jumatatu iliyopita kwenye makaburi ya Kisutu, Dar es Salaam.

TMK Wanaume Family: Hakuna mchezo



KUNDI la muziki wa kizazi kipya la TMK Wanaume Family lipo mbioni kuachia singo ya ‘Hakuna mchezo’, ambayo ni sehemu ya maandalizi ya albamu yao ya tatu.

Kiongozi wa kundi hilo, Rashid Ziada 'KR' alisema mjini Dar es Salaam wiki hii kuwa, wimbo huo unatarajiwa kuanza kuchezwa mwezi ujao katika vituo mbalimbali vya radio nchini.

KR alisema kwa sasa wapo katika hatua za mwisho za kukamilisha kazi ya kurekodi singo hiyo, ambayo aliielezea kuwa, itakuwa moto wa kuotea mbali.

Alisema kundi lao lilikuwa kimya kwa muda ili kutoa nafasi kwa baadhi ya wasanii kutoa kazi zao katika mtindo huru (solo artist), ambapo baada ya kupita katika hatua hiyo, wanajiandaa kutayarisha albamu yao.

KR (33) alisema walimpisha Mheshimiwa Temba na Chege Chigunda kutoa nyimbo zao mpya na baada ya kukamilisha, imefika zamu ya kundi hilo kuendelea kupika nyimbo mpya.

TMK hadi sasa imetoa albamu mbili ambazo ni ‘Kazi ipo’ na ‘Ndio zetu'.

Katika hatua nyingine, KR amesema Aprili mwakani atazindua albamu yake nje ya kundi hilo. Amesema albamu hiyo itakuwa na nyimbo 10 na mpaka sasa ameshakamilisha nyimbo saba.

Q-Chilla avunja ukimya




BAADA ya ukimya wa muda mrefu, msanii nyota wa muziki wa kizazi kipya nchini, Abubakar Katwila amesema anatarajia kuibuka na albamu mpya hivi karibuni.

Akihojiwa katika kipindi cha Bongo Planet kilichorushwa hewani na kituo cha televisheni cha East Africa mwishoni mwa wiki iliyopita, msanii huyo alisema albamu hiyo itajulikana kwa jina la ‘Machoni’.

Abubakar, maarufu kwa jina la Q-Chilla alisema, amerekodi vibao vilivyomo kwenye albamu hiyo kwa kuwatumia watayarishaji tofauti wa muziki kwa lengo la kuvipa ladha tofauti.

Q-Chilla alisema ukimya wake wa muda mrefu ulitokana na mitihani mbalimbali iliyomkuta katika maisha yake, ambayo alikiri kwamba imempa fundisho kubwa.

“Najua watu wamesema mengi, unaweza kunichukulia vyovyote upendavyo, lakini mitihani ipo na kwangu ni changamoto, watu wasubiri vitu tofauti,”alisema.

Msanii huyo aliyewahi kung’ara kwa kibao chake cha ‘Aseme’ amekiri kuwa, ushindani katika muziki wa kizazi kipya hivi sasa umekuwa mkali, lakini hauwezi kufikia enzi zao.

Alisema wakati alipoanza kutamba katika muziki huo, ushindani ulikuwa mkali zaidi na kila wasanii walipopanda wasanii, vita ya kuwapa mashabiki burudani safi ilikuwa kubwa.

“Enzi zile kila nilipopanda stejini na kuimba, watu walikuwa wakilia. Ilikuwa ukipanda stejini na kumuona msanii huyu na yule, vita inakuwa kali,”alisema.

Akizungumzia hali ya muziki huo kwa sasa, Q-Chilla alisema ushindani upo, wasanii wanafanya vizuri na muziki unakua, lakini pia kuna aina fulani ya upendeleo kwa baadhi ya wasanii.

“Hii ndiyo sababu iliyonifanya nitulie na kuandika zaidi kwa sababu sipaswi kujiona nimebaki peke yangu, haipendezi, mtanichoka haraka,”alisema.

“Kukaa kwangu kimya kwa muda mrefu kumewafanya muwe na hamu na mimi, nahitajika,”aliongeza.

Hata hivyo, Q-Chilla alieleza wasiwasi wake kuwa, muziki wa sasa haudumu kwa muda mrefu kwa vile ni mwepesi na hauna ujumbe wa maana kwa jamii.

“Leo hii mimi nikisimama jukwaani na kuimba ‘Aseme’ na atokee msanii wa sasa aimbe wa kwake, bado mimi nitachukua kijiji changu,”alisema.

Kuliacha Kombe la Chalenji liondoke, itakuwa aibu nyingine kwa Tanzania

Kuliacha Kombe la Chalenji liondoke, itakuwa aibu nyingine kwa Tanzania
MICHUANO ya soka ya Kombe la Tusker Chalenji imepangwa kuanza mwishoni mwa wiki hii hadi Desemba 12 mwaka huu mjini Dar es Salaam, ikizishirikisha timu za mataifa tisa kutoka Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA).
Mbali na nchi hizo tisa wanachama wa baraza hilo, michuano hiyo pia itazishiriki nchi zingine tatu, ambazo zimealikwa. Nchi hizo ni Ivory Coast, Malawi na Zambia.
Kwa mujibu wa CECAFA, nchi wanachama wa baraza hilo zitakazoshiriki katika michuano ya mwaka huu, ambayo imepangwa katika makundi matatu tofauti ni wenyeji Tanzania Bara, Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Somalia, Zanzibar, Ethiopia na Sudan.
CECAFA imesema uamuzi wa kuzialika Ivory Coast, Malawi na Zambia umelenga kuongeza ushindani na pia kukuza soka katika nchi za ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, hasa ikizingatiwa kuwa, viwango vya nchi hizo vipo juu ikilinganishwa na nchi nyingi zinazounda baraza hilo.
Katibu Mkuu wa CECAFA, Nicholas Musonye alisema, kwa mara ya kwanza, michuano ya mwaka huu itadhaminiwa na Kampuni ya Bia ya Serengeti (SBL), ambayo itatoa zawadi za jumla ya dola za Marekani 60,000 kwa washindi watatu wa kwanza.
Mbali na kutoa zawadi kwa washindi, Musonye alisema SBL pia itazigharamia timu shiriki usafiri wa ndege wa kwenda na kurudi, chakula na malazi kwa muda wote wa mashindano. Kampuni hiyo itatumia dola 450,000 za Marekani kudhamini michuano hiyo.
Uamuzi wa SBL kudhamini michuano hiyo unastahili kupongezwa, hasa ikizingatiwa kuwa, utaongeza hamasa na ushindani kwa timu shiriki, huku kila moja ikipania kushinda ili ipate zawadi tatu za kwanza za pesa.
Lakini ili michuano hiyo iwe na msisimko na ushindani wa kweli, ni vyema CECAFA ihakikishe kuwa, waamuzi walioteuliwa kuchezesha mechi za michuano hiyo wanafuata na kuheshimu sheria zote 17, badala ya kuchezesha kwa upendeleo kwa lengo la kuzibeba baadhi ya timu.
Hii ni kwa sababu imekuwa ikitokea mara kwa mara, baadhi ya waamuzi wanaoteuliwa kuchezesha michuano hiyo, wamekuwa wakizibeba baadhi ya timu kwa lengo la kuzikomoa timu zingine na hivyo kuharibu kabisa maana nzima ya ushindani.
Lakini kikubwa nilichokilenga kwenye safu hii wiki hii ni kutoa changamoto kwa timu za Tanzania Bara na Zanzibar, kuutumia vyema uenyeji wa michuano hiyo kuhakikisha kombe hilo linabaki nyumbani.
Sababu na uwezo wa timu hizo kulibakisha kombe nyumbani zipo. Ni kwa sababu zinaundwa na wachezaji wengi wenye uzoefu wa michuano ya kimataifa na pia zitakiwa zikicheza kwenye uwanja wa nyumbani, mbele ya maelfu ya mashabiki wake.
Kuliruhusu kombe hilo liondoke nyumbani kama ilivyokuwa miaka kadhaa iliyopita ni aibu na fedheha kubwa kwa Taifa na hali hiyo itawavunja nguvu mashabiki wengi wa soka hapa nchini.
Itakuwa ni sawa na ilivyotokea kwa Simba mwaka 1993 wakati ilipofuzu kucheza fainali za Kombe la CAF, ambapo ilifanikiwa kutoka suluhu na Stella Abidjan ya Ivory Coast mjini Abidjan, lakini ikachapwa mabao 2-0 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Ilikuwa siku ya simanzi kubwa kwa mashabiki wa Simba na Watanzania kwa jumla.
Ikumbukwe kuwa, kwa mara ya mwisho, Tanzania Bara ilitwaa kombe hilo mwaka 1994 michuano hiyo ilipofanyika nchini Kenya wakati Zanzibar ililitwaa mwaka 1996 michuano hiyo ilipofanyika nchini Uganda.
Tangu wakati huo, Tanzania Bara na Zanzibar zimekuwa zikishiriki kwenye michuano hiyo kama wasindikizaji, na mbaya zaidi wakati mwingine zimekuwa zikitolewa hatua za awali.
Kwa kuzingatia rekodi hizo, wakati umefika kwa wawakilishi wetu hawa kuhakikisha kuwa, kombe hilo linabaki nchini, si tu kwa ajili ya kurejesha imani kwa mashabiki, bali pia kudhihirisha kuwa, kiwango chetu cha soka nchini kipo juu kama nchi zingine za ukanda huu wa Afrika Mashariki na Kati.
Lakini ili hayo yote yawezekane, timu hizo mbili zinapaswa kucheza kwa kujituma, ikiwa ni pamoja na wachezaji wake kufuata na kuheshimu mafunzo ya makocha wao badala ya kila mchezaji kucheza kwa kutumia kipaji chake.
Kauli ya Kocha Jan Poulsen wa Tanzania Bara kwamba ataitumia michuano hiyo kutengeneza kikosi imara cha Taifa Stars kwa ajili ya michuano ya kufuzu kucheza fainali za Afrika za mwaka 2012 haifai kupewa nafasi kwa sababu watanzania wanataka kuona kombe linabaki nyumbani na si kuitumia michuano hiyo kama mazoezi.
Ni wazi kuwa, iwapo Tanzania Bara na Zanzibar zitashiriki katika michuano hiyo zikiwa na dhamira ya dhati ya kutwaa ubingwa, lengo hilo litatimia kwa vile katika soka, lolote linawezekana. Cha muhimu ni wachezaji kucheza kwa kujituma huku wakiweka mbele utaifa.

Buriani 'Jenerali' Juma Mkambi

KIUNGO wa zamani wa kimataifa wa klabu ya Yanga na timu ya soka ya Taifa, Taifa Stars, Juma Mkambi amefariki dunia. Mkambi alifariki dunia Jumapili iliyopitwa na kuzikwa siku iliyofuata kwenye makaburi ya Kisutu, Dar es Salaam.
Mkambi (55), ambaye alikuwa maarufu kwa jina la Jenerali, alifariki kutokana na ugonjwa wa vidonda vya tumbo. Kabla ya mauti kumkumba, Mkambi alikuwa amelazwa kwenye hospitali ya Muhimbili, Dar es Salaam.
Mazishi ya mwanasoka huyo mkongwe yalihudhuriwa na wanamichezo mbalimbali maarufu nchini, wakiwemo wachezaji wa zamani wa klabu za Simba, Yanga na Taifa Stars.
Enzi za uhai wake, Mkambi alikuwa mchezaji mahiri wa idara ya kiungo, akiwa na uwezo wa kuiunganisha vyema idara ya ulinzi na kiungo na wakati huo huo kusaidia mashambulizi.
Marehemu Mkambi alikuwa mmoja wa wachezaji wa Taifa Stars walioshiriki kwa mara ya kwanza katika fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika za mwaka 1980 zilizofanyika nchini Nigeria. Katika fainali hizo, Taifa Stars ilifungwa mechi mbili na kuambulia sare mechi moja.
Baadhi ya wachezaji aliokuwa nao kwenye kikosi hicho mwaka huo niJuma Pondamali 'Mensah', Ahmed Amasha, Leodegar Tenga, Salim Amir, Jellah Mtagwa, Mohamed Adolf Rishard, Hussein Ngulungu, Thuweni Ally, Mohamed Salim, Omar Hussein, Leopard Tasso Mukebezi na Peter Tino.
Je, ni kwa nini Mkambi alipewa jina la Jenerali wakati hakuwa mwanajeshi?
Kilichotokea ni kwamba, gazeti moja la Kiingereza la Afrika Magharibi liliandika kuhusu michuano hiyo na kuchambua ubora wa timu zilizoshiriki.
Lilipoizungumzia Tanzania, lilisifu viwango vya wachezaji wa Taifa Stars. Katika moja ya sehemu za habari hiyo, gazeti hilo liliandika:"Generally, Juma Mkambi played so well in midfield," likiwa na maana: "Kwa jumla, Juma Mkambi alicheza vizuri sana katika sehemu ya kiungo."
Gazeti hilo liliposomwa hapa nyumbani, baadhi yetu tulidhani ile ‘Generally’ (kwa ujumla) ilimaanisha cheo cha kijeshi cha ‘General’ na kuanza kumwita Mkambi kwa kutanguliza cheo hicho, tukidhani mwandishi alimwita kwa cheo hicho kwenye makala yake.
Jina hilo liliendelea kutumika kwa Mkambi hadi alipostaafu kucheza soka na hadi mauti yalipomkuta, aliendelea kuitwa hivyo. Kiwango chake katika michuano hiyo kilivifanya vyombo vingi vya habari vimsifu na kwa kweli havikukosea.
Akizungumza nyumbani kwa marehemu Mkambi, aliyekuwa Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo katika serikali iliyopita, Joel Bendera alimwelezea mchezaji huyo kwamba alikuwa msikivu, aliyejituma na chachu ya hamasa kwa wenzake uwanjani.
Bendera alikuwa kocha msaidizi wa Taifa Stars iliposhiriki fainali za Mataifa ya Afrika za mwaka 1980, akiwa chini ya Slowmir Work kutoka Poland.
"Tutamkumbuka siku zote kwani alikuwa mmoja wa wachezaji viungo makini na zaidi nasema alikuwa akijituma sana uwanjani na si mtu wa kusukumwa ndani na nje ya uwanja,”alisema Bendera.
"Tulipokuwa Nigeria, alikuwa akichukia sana kupoteza mchezo, lakini ilikuwa haina jinsi, mchezo wa mpira kufungwa ni sehemu ya mchezo. Tumempoteza mtu muhimu na pia mshauri, maanake mpaka kifo chake, alikuwa mtu wa ushauri hasa jinsi gani tunaweza kujikwamua kwenye soka," aliongeza Bendera.
Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Leodegar Tenga, ambaye aliwahi kucheza na Tenga alisema: "Mkambi alitusaidia sana katika kiungo wakati tulipokuwa Lagos. Nasema hivyo kwa sababu hayo ndiyo mashindano yake makubwa ukiacha hizi Chalenji na mechi nyingine za ligi.”
"Alikuwa na nguvu, alikuwa na uwezo wa kumiliki mipira na alikuwa na mashuti makali. Nilifurahi sana wakati tukicheza pamoja kwani alikuwa akitulisha mipira na alikuwa mpiganaji mzuri uwanjani," alisema Tenga.
Kocha Mkuu wa timu ya taifa ya wanawake, Twiga Stars, Charles Boniface Mkwasa alisema kifo cha Mkambi kimemwacha kwenye simanzi kubwa kwa sababu alikuwa rafiki yake wa karibu.
Mbunge wa Kinondoni (CCM), Idd Azzan alisema bila kujali itikadi za klabu zao, alishirikiana vyema na marehemu Mkambi kuanzisha timu ya Tanzania Stars, ambayo iliwahi kuiwakilisha Tanzania katika michuano ya Kombe la CAF mwanzoni mwa miaka ya 1990.
Baadhi ya wachezaji walioshiriki kikamilifu katika maombolezo na mazishiri ya marehemu Mkambi ni pamoja na Jamhuri Kihwelo, Mohamed Mwameja, Mwanamtwa Kihwelo, Mohamed Hussein 'Mmachinga', Idd Selemani, Dua Said na Lawrence Mwalusako.
Wengine ni Shaaban Geva, Mtemi Ramadhani, Charles Boniface Mkwasa, Makumbi Juma, Kitwana Manara, Omar Gumbo, Athumani Iddi ‘Chama’ na makocha Salum Madadi, Sunday Kayuni na Eugen Mwasamaki.
Mkambi, ambaye ameacha mke na watoto kadhaa, aliianza kupata umaarufu kisoka mwishoni mwa miaka ya 1970 wakati akichezea timu ya Nyota ya Mtwara (sasa Bandari Mtwara), aliyoichezea kwa muda kabla ya kujiunga na Yanga mwaka 1982.
Alikuwa miongoni mwa wachezaji waliochezea Yanga kwa muda mrefu bila kuhamia klabu nyingine hadi alipostaafu soka mwanzoni mwa miaka ya 1990.
Kabla ya kifo chake, marehemu Mkambi alikuwa katika jopo la Kamati ya Ufundi ya Chama cha Soka Mkoa wa Pwani (COREFA) na ni mmoja wa washauri wa maendeleo ya soka ya vijana TFF.

Thursday, November 18, 2010

SENDOFF PARTY YA FURAHA OMARY





MWANDISHI wa habari wa magazeti ya Uhuru, Mzalendo na Burudani, Furaha Omary jana aliagwa rasmi na ndugu, jamaa na rafiki zake katika sherehe ya Sendoff Party iliyofanyika kwenye ukumbi wa PTA, Sabasaba mjini Dar es Salaam. Sherehe hiyo ilihudhuriwa na watu mbalimbali wakiwemo wafanyakazi wa Kampuni ya Uhuru, Publications Ltd, ambako Furaha anafanyakazi.

Sikinde yazuiwa kufanya maonyesho DDC Kariakoo

Kisa? Ukumbi wakodishwa kwa mmiliki mpya

BENDI ya muziki wa dansi ya Mlimani Park Orchestra ‘Sikinde’ imezuiwa kufanya maonyesho kwenye ukumbi wa DDC Kariakoo wa mjini Dar es Salaam.
Uamuzi huo umefikiwa na mmiliki mpya wa ukumbi huo, ….ambaye alishinda tenda ya kuuendesha baada ya Shirika la Uchumi na Maendeleo la Dar es Salaam (DDC) kuamua kuukodisha.
Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi mjini Dar es Salaam juzi, kiongozi wa bendi hiyo, Habibu Abbas ‘Jeff’ na Katibu, Hamisi Milambo walisema walitimuliwa kwenye ukumbi huo kuanzia wiki mbili zilizopita.
Kwa mujibu wa Jeff, awali mmiliki huyo aliwaita na kuwaeleza kwamba, atawaruhusu kuendelea na maonyesho yao ya kila Jumapili kwenye ukumbi huo kwa sababu lengo la kila upande ni kufanya biashara.
“Lakini tulishangaa kuona kuwa, baada ya siku moja alituita tena na kutueleza kuwa, hawezi kuturuhusu kufanya maonyesho hayo kama hatutamlipa sh. 200,000 kwa kila onyesho,”alisema.
“Tulishangazwa na uamuzi huo kwa sababu tangu mwanzo, uongozi wa DDC ulituruhusu kufanya maonyesho yetu bure kwenye ukumbi huo licha ya kwamba kwa sasa bendi inajiendesha kwa kujitegemea. Hatuelewi ni makubaliano gani yaliyofikiwa kati ya mmiliki huyo na uongozi wa DDC,”aliongeza.
Kwa upande wake, Milambo alisema wanahisi hiyo ni hujuma iliyoandaliwa na uongozi wa DDC baada ya kutokea hali ya kutokuelewana kati yao, baada ya baadhi ya wanamuziki wa bendi hiyo kufungua kesi ya kupinga kupunguzwa kazini.
“Tulimuomba mmiliki huyo atupunguzie malipo ya ukumbi kwa sababu uwezo wetu kwa sasa ni mdogo kwa sababu tunajiendesha wenyewe. Tulikuwa tayari kumlipa sh. 50,000 kila wiki, lakini aligoma katakata,”alisema.
Milambo alisema kilichowasikitisha zaidi ni kauli za dharau, ambazo zimekuwa zikitolewa na mmiliki huyo, ikiwa ni pamoja na kuwabeza kuwa hawawezi kumfanya lolote na kwamba hawana chao kwenye ukumbi huo.
Kwa mujibu wa Milambo, awali uongozi wa DDC pia ulitaka kuwatimua kufanya mazoezi kwenye ukumbi wa Mlimani kabla ya baadhi ya viongozi wa serikali kuingilia kati na kuuzuia kufanya hivyo.
Milambo na Jeff wameviomba vyombo vya serikali kuingia kati suala hilo ili kuinusuru bendi hiyo kongwe nchini kusambaratika kwa vile kutoweka kwake kutadhoofisha maendelezo ya muziki nchini.
“Bendi pekee kongwe zilizosalia hapa nchini hivi sasa ni Sikinde na Msondo Ngoma. Mojawapo ikitoweka, ni sawa na kusema utambulisho wa muziki wa Tanzania nao utatoweka,”alisema Jeff.
Juhudi za kumtafuta mmiliki mpya wa ukumbi huo pamoja na Meneja Mkuu wa DDC hazikuweza kufanikiwa kwa vile jana ilikuwa siku ya mapumziko kikazi.

Mambo Hadharani

RAPA na mpuliza trumphet wa bendi ya muziki wa dansi ya Msondo Ngoma, Roman Mng'ande 'Romario' akiselebuka na mmoja wa wacheza shoo wapya wa bendi hiyo wakati wa onyesho lililofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita kwenye ukumbi wa Max Bar, Ilala, Dar es Salaam.

Wednesday, November 17, 2010

MAMA RAHMA ASAIDIA BONANZA LA YATIMA


RAIS wa Kampuni ya RBP Oil & Industrial Technology Tanzania Ltd, Rahma Al Kharoos akimkabidhi kitita cha sh. milioni nne, Mkurugenzi wa Taasisi ya Popular Sports and Entertainment Tanzania, Osman Kazi kwa ajili ya kuandaa bonanza la watoto yatima, linalotarajiwa kufanyika Jumapili kwenye ufukwe wa Coco Beach mjini Dar es Salaam.

RAGE: Siondoki Simba ng'o


MWENYEKITI wa klabu ya Simba, Ismail Aden Rage amesema, kamwe hawezi kujiuzulu uongozi wa klabu hiyo kutokana na kuchaguliwa kwake kuwa mbunge wa Jimbo la Tabora Mjini kwa tiketi ya CCM.
Akihojiwa na kituo cha televisheni cha TBC 1 kutoka mjini Dodoma wiki hii, Rage alisema katiba ya Simba haimzuii kushika nyadhifa mbili kwa wakati mmoja.
Rage alisema, kwa mujibu wa katiba ya Simba, mwenyekiti asipokuwepo, makamu wake ndiye anayeshika majukumu yake ikiwa ni pamoja na kuendesha vikao vya uongozi na mikutano ya wanachama.
“Hivyo hata kama sintakuwepo Dar es Salaam kwa sababu ya shughuli za Bunge, hiyo haisababishi shughuli za klabu kushindwa kuendelea kwa sababu yupo makamu mwenyekiti,”alisema.
Akitoa mfano, Rage alisema wapo baadhi ya wabunge, ambao pia ni viongozi wa taasisi mbalimbali na wamekuwa wakitekeleza majukumu yao yote mawili bila ya kuwepo kwa mwingiliano ama athari yoyote.
Aliwataja baadhi ya wabunge hao kuwa ni pamoja na Kepteni mstaafu John Komba, ambaye ni mbunge wa Jimbo la Mbinga Magharibi kwa tiketi ya CCM na pia Mkurugenzi Mtendaji wa kikundi cha sanaa za maonyesho cha TOT Plus.
Hata hivyo, Rage alisema anatarajia kukutana na viongozi wenzake wa kamati ya utendaji ya Simba mwishoni mwa wiki hii ili kujadili suala hilo kabla ya kulitolea uamuzi wa mwisho.
Wakati huo huo, Rage alithibitisha kuwa, wamekata rufani kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kupinga adhabu iliyotolewa kwa kipa Juma Kaseja.
TFF ilitangaza kumfungia Kaseja kucheza mechi tatu na pia kumtoza faini ya sh. 500,000 kwa tuhuma za kukataa kumpa mkono Mkuu wa mkoa wa Mwanza, Abbas Kandoro, ambaye alikuwa mgeni rasmi wa mechi ya ligi kuu ya Tanzania Bara, kati ya Simba na Yanga, iliyochezwa Oktoba 16 mwaka huu.
Hata hivyo, TFF imekuwa ikijikanganya kuhusu adhabu hiyo baada ya gazeti moja la kila siku kuchapisha picha iliyomwonyesha Kaseja akipeana mkono na Kandoro wakati wa mechi hiyo.
Kaimu Katibu Mkuu wa TFF, Sunday Kayuni alikaririwa akisema kuwa, taarifa hiyo ilitolewa kimakosa kwa vile Kaseja hakugoma kupeana mkono na Kandoro bali wachezaji wa Yanga.

Uongozi Yanga wamtikisa Manji


UONGOZI wa klabu ya Yanga umeeleza kukerwa na kitendo cha mfadhili wao, Yusuf Manji kuwapigisha kura wachezaji wa timu hiyo kuhusu utendaji kazi wa viongozi na Kocha Kostadin Papic.
Habari za uhakika kutoka ndani ya klabu hiyo zimeeleza kuwa, kitendo cha Manji kuteta na wachezaji na kuwataka wamueleze utendaji kazi wa viongozi, hakikubaliki kwa vile kimelenga kuwadhalilisha.
Kwa mujibu wa habari hizo, tayari baadhi ya viongozi wameanza kuhoji uhalali wa Manji kuwataka wachezaji wafanye hivyo wakati wenye mamlaka hayo ni wanachama wa klabu hiyo.
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili umebaini kuwa, viongozi wa klabu hiyo walikutana wiki iliyopita kwa ajili ya kumjadili mfadhili huyo kuhusu kitendo chake hicho, lakini haikuweza kufahamika mara moja uamuzi waliofikia.
“Hatuwezi kuvumilia kumuona Manji akitudhalilisha kiasi hiki na hana uwezo wa kuwahoji wachezaji kuhusu utendaji wetu wa kazi. Yeye siye aliyetuchagua, yeye ni mfadhili tu, wenye jukumu hilo ni wanachama,”alisema mmoja wa viongozi wa juu wa klabu hiyo, ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini.
Kiongozi huyo pia alieleza kushangazwa kwao na kauli ya Manji kuwataka Makamu Mwenyekiti wa klabu hiyo, Davis Mosha na Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano, Seif Ahmed kutafuta kocha atakayechukua nafasi ya Papic na pia kumrejesha mshambuliaji Mrisho Ngasa aliyesajiliwa na Azam FC.
“Sisi tunadhani Manji sasa amefika mbali na kuna kitu anachotaka kifanyika ndani ya Yanga. Lakini sisi kama viongozi tunamuomba atuheshimu kwa sababu tumechaguliwa na wanachama kikatiba na ndiyo wenye uwezo wa kuhoji utendaji wetu wa kazi,”alisema.
Kiongozi huyo alisema kitendo cha Manji kuingilia kati jukumu hilo huenda kimelenga kuzusha mgogoro ndani ya klabu hiyo, ambao unaweza kuathiri mwenendo wa timu katika michuano ya ligi kuu ya Tanzania Bara, ambayo kwa sasa ipo kwenye mapumziko. Manji alikutana na wachezaji wote wa Yanga wiki mbili zilizopita katika ofisi za Kampuni ya Quality Group zilizopo kwenye barabara ya Nyerere, Jijini Dar es Salaam.
Katika kikao hicho, Manji aliwataka wachezaji wapige kura kuhusu uwezo wa Kocha Papic, utendaji wa viongozi wa klabu na mchango wa kila mchezaji kwa timu. Awali, utata ulikuwa umeigubika klabu hiyo kuhusu hatma ya Kocha Papic baada ya kuondoka nchini wiki mbili zilizopita na kurejea kwao Serbia kwa mapumziko.
Kocha huyo, ambaye mkataba wake wa kuinoa timu hiyo unatarajiwa kumalizika Aprili mwaka huu, alikuwa ameweka mgomo baridi wa kukinoa kikosi cha timu hiyo kutokana na kuchelewa kusaini mkataba mpya.
Mgomo huo aliufanya kabla ya mchezo kati ya Yanga na Toto African ya Mwanza, uliofanyika hivi karibuni katika Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro. Katika mechi hiyo, Yanga ilishinda mabao 2-0.

CECAFA yapania kupeleka timu Kombe la Dunia 2014


NAIROBI, Kenya
BARAZA la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) limezindua mkakati wa kutaka ipate mwakilishi katika fainali za Kombe la Dunia za mwaka 2014 zitakazofanyika nchini Brazil.
Mkakati huo ulizinduliwa mwanzoni mwa wiki hii mjini Nairobi nchini Kenya, yakiwa ni makubaliano ya pamoja kati ya CECAFA na Kampuni ya East African Breweries (EABL).
Katika kutekeleza mkakati huo, EABL imeamua kudhamini michuano ya soka ya Kombe la Chalenji, inayotarajiwa kufanyika nchini Tanzania kuanzia Novemba 27 hadi Desemba 12 mwaka huu.
Kampuni hiyo imepanga kutumia dola 450,000 za Marekani kwa ajili ya kudhamini michuano hiyo, itakayozishirikisha nchi 12, zikiwemo nchi tatu waalikwa za Ivory Coast, Malawi na Zambia.
CECAFA inataka nchi zilizo wanachama wake kutumia michuano hiyo kama sehemu ya maandalizi ya mashindano ya kuwania kufuzu kucheza fainali za Afrika za mwaka 2012 na pia fainali za Afrika kwa wachezaji wa ndani (CHAN) zitakazofanyika Machi mwakani nchini Sudan.
Nchi wanachama wa CECAFA zinazotarajiwa kushiriki katika michuano hiyo ni Tanzania Bara, Zanzibar, mabingwa watetezi Uganda, Kenya, Rwanda, Burundi, Ethiopia, Sudan na Somalia.
Akitangaza mkakati huo, Katibu Mkuu wa CECAFA, Nicholas Musonye alisema hawatarajii kurudia aibu ya kukosa fainali za mwaka huu za Kombe la Dunia zilizofanyika nchini Afrika Kusini.
“CECAFA ni kanda pekee ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) yenye mafanikio makubwa na tunapaswa kupata angalau nafasi moja kati ya tano zilizotengwa kwa bara la Afrika katika fainali zijazo za Kombe la Dunia,”alisema.
Musonye alisema baraza lake limepania kuutumia udhamini wa EABL kuyafanya mashindano ya mwaka huu ya Kombe la Chalenji yawe ya aina yake.
“Fedha tutakazozipata kutoka EABL zitapelekwa moja kwa moja kwa timu shiriki ili kuziwezesha zitoe ushindani mkali,” alisema.
Kwa mujibu wa Musonye, fedha hizo zitatumika kuzisafirisha timu kwenda Dar es Salaam, kuzipatia huduma za malazi na chakula pamoja na usafiri wa ndani.
Mshindi wa michuano hiyo atazawadiwa dola 30,000 za Marekani (sh. milioni 35), wa pili dola 20,000 (sh. milioni 25) na wa tatu dola 10,000 (sh.milioni 15)
“Soka katika ukanda wetu kwa sasa inapata sapoti kubwa, mashabiki wetu wana kiu kubwa ya kupata kiwango bora na kutokana na udhamini huu, tutaweza kuandaa mashindano ya kiwango cha juu na hivyo kukuza kiwango cha soka katika ukanda huu,”alisema Musonye.
Katika uzinduzi huo, Mkurugenzi Mtendaji wa EABL, Seni Adetu alimkabidhi Musonye kombe litakaloshindaniwa katika michuano hiyo. Kombe hilo litapitishwa katika nchi sita kabla ya kutua Dar es Salaam.
Adetu alisema udhamini wa mwaka huu wa Kombe la Chalenji ni sehemu ya mipango ya muda mrefu ya EABL kukuza soka katika nchi za ukanda wa Afrika Mashariki na Kati na kuhakikisha mojawapo ya nchi hizo inafuzu kucheza fainali za Kombe la Dunia za mwaka 2014.

SPUTANZA yaandaa tuzo ya mwanasoka bora

CHAMA cha Wanasoka wa Zamani nchini (SPUTANZA) kimesema kitaandaa tuzo maalumu kwa ajili ya mchezaji bora wa michuano ya ligi kuu ya Tanzania Bara msimu wa 2010-2011.
Katibu Mkuu wa SPUTANZA, Said George alisema wiki iliyopita mjini Dar es Salaam kuwa, chama chake kimeamua kujitosa kutoa tuzo hiyo kwa lengo la kuipa hadhi zaidi.
Saidi alisema, japokuwa zipo tuzo za wanamichezo bora zinazotolewa kila mwaka na Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo nchini (TASWA), wameona ni bora waitengenishe tuzo hiyo na za michezo mingine.
"Hatupingi kuwepo kwa tuzo za TASWA, isipokuwa tuzo ya mchezaji bora wa soka ina hadhi yake. Tunaanza kuitoa kwa mara ya kwanza ligi hii itakapomalizika na wachezaji ndio watakaopendekeza mshindi,"alisema.
Katibu Mkuu huyo wa SPUTANZA alisema, kwa kuanzia watatoa tuzo ya mchezaji bora wa mwaka, mshindi wa pili na wa tatu nakuwataka wahisani mbalimbali kujitokeza kudhamini tuzo hizo.
Wakati huo huo, SPUTANZA imelitaka Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kuvunja mara moja kamati ya kusimamia maadili na hadhi ya wachezaji kwa madai kuwa, imeshindwa kufanyakazi iliyokusudiwa,badala yake imeundwa kwa maslahi binafsi.
Saidi alisema kamati hiyo, ambayo inaongozwa na Wakili Alex Mgongolwa, ambaye ni mnazi mkubwa wa Yanga, imekumbwa na mgongano wa kimaslahi kwa watendaji wake kugubikwa na upenzi badala ya kutenda haki.
"Ni wazi kuwa, Yanga haikufuata taratibu wakati ikivunja mkataba na wachezaji wake wanne, na ni muda mrefu sasa sakata hili halijapatiwa ufumbuzi,”alisema Saidi.
“Na sasa ni usajili wa dirisha dogo, fursa ya wao kupata timu ya kuchezea ni finyu kwa vile uongozi wa Yanga haujawalipa madai yao wanayostahili, "aliongeza.
Alisema chama chake kimeiomba TFF kuzuia usajili wa nyongeza wa Yanga kwa ajili ya mzunguko wa pili wa ligi kuu hadi suala la wachezaji hao litakapopatiwa ufumbuzi.
Saidi alisema wachezaji hao wanne wa Yanga waliaochwa kwenye usajili wa msimu huu, walifuata taratibu zote katika kudai haki zao, lakini wamekuwa wakipigwa danadana isiyokuwa na mwisho.
Wachezaji, ambao Yanga imevunja mikataba yao bila kuwalipa haki zao ni Steven Malashi, John Njoroge, Wisdom Ndhlovu na Ally Msigwa. Mikataba ya wachezaji hao ilitakiwa kumalizika mwaka 2012.
Marashi anaidai Yanga sh. milioni 37.5, Ndhlovu anadai sh.milioni 82, Msigwa sh. milioni 89.7 na Njoroge sh. milioni 44.

NYOSHI: Hakuna bendi kama FM Academia



RAIS wa bendi ya muziki wa dansi ya FM Academia, ‘Wazee wa Ngwasuma’, Nyoshi El Saadat, ametamba kuwa, bendi yake ndiyo inayoongoza kwa kuwa na mashabiki wengi mikoani kuliko bendi zingine.
Akizungumza na Burudani mjini hapa wiki iliyopita, Nyoshi alisema, bendi nyingi maarufu nchini, zinapata mashabiki wengi zinapofanya maonyesho Jijini Dar es Salaam, lakini hali huwa tofauti zinapokwenda mikoani.
Nyoshi alitoa majigambo hayo wakati bendi hiyo ilipokuwa ikifanya onyesho la uzinduzi wa albamu yake mpya ya ‘Vuta nikuvute’, lililofanyika kwenye ukumbi wa Benjamin Mkapa.
Katika onyesho hilo lililohudhuriwa na mashabiki lukuki, bendi hiyo ilifanikiwa kukonga nyoyo zao kutokana na vibao vyao vipya 11 vilivyopigwa kwa mpangilio wa kuvutia.
“FM Academia kila tunapokwenda kwenye mkoa wowote hapa Tanzania, tunaongoza kwa kupata mashabiki wengi. Bendi zingine nyingi zinapata mashabiki zinapokuwa Dar es Salaam, zikitoka kwenda mikoani, hazipati kitu,”alisema Nyoshi.
Aliongeza kuwa, kinachoifanya bendi hiyo kuwa ‘matawi ya juu’ ni kudumu kwa muda mrefu, wasanii wake kufanyakazi kwa umoja, kuwa na nidhamu ndani na nje ya jukwaa na uwajibikaji wa pamoja.
Kwa mujibu wa Nyoshi, albamu hiyo ni bora na akiwa kiongozi, ameshiriki kutunga nyimbo mbili, ‘Jasmini’ na ‘Ushirikiano wa Tanzania na nchi jirani’.
Alizitaja baadhi ya nyimbo zingine zilizomo kwenye albamu hiyo kuwa ni ‘Shida yangu’ na ’Mgeni’, ambazo zimerekodiwa kwenye studio za Metro za mjini Dar es Salaam.
Baadhi ya mashabiki waliohudhuria onyesho hilo walikiri kuwa, bendi ya FM Academia inafahamu vyema kukidhi kiu ya mashabiki wake na wanamuziki wake wana nidhamu ya hali ya juu wanapokuwa stejini.

Kuigiza filamu nyingi ni kujimaliza-Monalisa


MWIGIZAJI filamu maarufu wa kike nchini, Yvonne Cherly amefichua kuwa, tabia ya kuigiza filamu nyingi kwa muda mfupi imechangia kushuka kwa hadhi ya fani hiyo.
Yvonne, maarufu kwa jina la Monalisa alisema mjini Dar es Salaam wiki iliyopita kuwa, tabia hiyo haiwajengei heshima wasanii wa fani hiyo bali inawamaliza.
"Lazima utafika wakati, wasanii wa aina hiyo watapotea kabisa. Mashabiki watawachoka haraka na hii ni hatari kwa vile itashusha thamani ya filamu zetu. Msanii anapaswa kufanya mambo kwa mpangilio na hii inaleta heshima, si kukurupuka tu,”alisema.
Monalisa, ambaye ni miongoni mwa wasanii waasisi wa fani hiyo hapa nchini alisema, si kazi rahisi kwa mwigizaji filamu kucheza filamu nyingi kwa muda mfupi na zikawa nzuri.
"Unakuta msanii ndani ya mwezi mmoja anaigiza filamu tano, mtu huyo mmoja kila sehemu unamuona anatokea yeye na uhusika unakuta ni uleule, huko ni kujimaliza,"alisema.
"Msanii unakuwa huna kitu kipya, huna ubunifu, ndio maana ukiangalia filamu nyingi za sasa, hazina jipya. Wasanii wanafanya mambo yaleyale kwa sababu mtu anakuwa hana muda wa kupumzika na akili kufikiria kitu kipya,”aliongeza.
"Kila muda anakuwa ‘bize’ na kukazana kuhakikisha anakamilisha kazi alizonazo. Matokeo yake analipua tu na watazamaji hawapati kitu, ambacho wanategemea, ndio maana mwisho wa siku thamani ya mtu inashuka,”alisisitiza.

'Banana hakuwahi kunikataza kujihusisha na muziki'


MSANII nyota wa kike wa muziki wa kizazi kipya nchini, Maunda Zorro amesema kamwe kaka yake, Banana Zorro hakuwahi kumkataza kujihusisha muziki katika maisha yake.
Badala yake, Maunda amesema alichokuwa akikifanya Banana ni kumuusia mara kwa mara kumaliza kwanza masomo yake kabla ya kujitosa kwenye muziki.
Akihojiwa katika kipindi cha Burudani ni Nyumbani cha TBC 1 mwishoni mwa wiki iliyopita, Maunda alisema Banana alimpa usia huo kwa sababu fani hiyo ilimuathiri kwa kumfanya ashindwe kuyapa kipaumbele masomo yake.
"Ukweli ni kwamba Banana hakuwahi kunikataza mimi nisijihusishe na muziki. Alichokuwa akiniusia ni kuweka mbele masomo kwanza kabla ya kujitosa kwenye muziki,"alisema.
"Alikuwa akiniambia, hakuna kwenda studio wala kurekodi wimbo, nitafanya hivyo baada ya kumaliza masomo,"aliongeza.
"Banana alifanya hivyo kwa sababu alishabaini tatizo la kuchanganya muziki na masomo kwa vile lilimkuta. Alipokuwa akisoma sekondari, muziki ulimuingia sana kwenye damu yake kiasi kwamba alishindwa kuyapa kipaumbele masomo. Hakutaka nami niingie kwenye mkumbo huo,"alisisitiza.
Kwa mujibu wa Maunda, kwa sasa Banana amekuwa mstari wa mbele kumpatia misaada ya aina mbalimbali kimuziki ili aweze kufanikisha ndoto yake ya kuwa mwanamuziki.

Amini aamua kutoka kivyake


MSANII chipukizi wa muziki wa kizazi kipya nchini, Amini kutoka kundi la THT amedokeza kuhusu mbinu anazotumia kimuziki ili kujiweka kwenye matawi ya juu.
Amini, ambaye kwa sasa anatamba kwa kibao chake cha ‘Unikimbie’, alisema mjini Dar es Salaam wiki hii kuwa, anazo nguzo kuu tatu, ambazo amekuwa akizitekeleza kwa lengo la kutimiza azma yake hiyo.
Msanii huyo anayechipukia alisema, amekuwa akitekeleza nguzo hizo kila anapokuwa kwenye maandalizi ya kutoa nyimbo mpya, ndiyo sababu zimekuwa zikiwavutia mashabiki wengi wa muziki huo.
"Kabla sijatunga wimbo wowote, ninakuwa makini katika kuhakikisha nimetuliza kichwa changu, kwani ninakuwa nimetenga muda muafaka wa kuifanyakazi hiyo ipasavyo," alisema Amini, ambaye ni miongoni mwa wasanii chipukizi wanaong'ara kwa sasa.
Aliitaja nguzo yake ya kwanza kuwa ni kukiamini kila anachokifikiria na kukifanyiakazi mara moja kwa kuandaa melodi nzuri kwa ajili ya kuwavutia mashabiki wake.
"Pia ninahakikisha nakuwa makini ninapoutengeneza wimbo wangu na baada ya kumaliza, ninarudia mwanzo mpaka mwisho kwa usahihi na baada ya hapo, ninahakikisha vibwagizo vya wimbo wangu vimekaa sawa," alisema Amini.
Aliitaja nguzo yake ya pili kuwa ni namna anavyoweza kuandaa maneno mazuri ya wimbo na kuongeza kuwa, huo ndio msingi bora wa kuzifanya nyimbo zake zikubalike na mashabiki.
Kwa mujibu wa Amini, nguzo yake ya tatu ni kuhakikisha anafuata misingi yote ya uimbaji na kuongeza kuwa, hilo ndilo lililomwezesha kufika alipo sasa.
"Nipo makini katika kufuata misingi ya uimbaji kwani ninajua namna ya kupanda na kushuka ninapotengeneza wimbo na ninahakikisha sitoki nje ya biti," alisisitiza.
Msanii huyo asiyekuwa na makeke alisema, ametoka mbali kimuziki na anazidi kukua taratibu na kujifunza mengi katika fani hiyo na hilo linamsaidia kujijenga vizuri.
Albamu ya pamoja aliyoifanya kwa kushirikiana na msanii Barnabas, ndiyo iliyomwezesha kuwa matawi ya juu na kwa sasa anajiandaa kupakua albamu ya peke yake, ambayo ameshaanza kuiandaa.
"Nilitoka na Barnabas kwa awamu ya kwanza kwa sababu kila mmoja alifahamika kwa nafasi yake, lakini hivi sasa nimeshaanza kuandaa albamu yangu mwenyewe,”alisema.
“Ninatumia muda mwingi hivi sasa katika kuandaa albamu yangu hii kwa sababu nataka iwe kwenye chati ya juu kimuziki. Nimepanga kuikamilisha albamu hii mwanzoni mwa mwaka 2011," alisema Amini.
Alizitaja baadhi ya nyimbo zake, zinazotarajiwa kuwemo kwenye albamu hiyo kuwa ni pamoja na 'Kumanya', 'Tumetoka mbali', 'Anavuruga', 'Subira', 'Mapenzi ya nani duniani' na 'Unikimbie'.

Wednesday, October 27, 2010

K-One, msanii mwenye ndoto ya kufika mbali kimuziki


WASWAHILI wana msemo usemao, ‘Avumaye baharini papa, kumbe wengi wapo’. Hivyo ndivyo ilivyojidhihirisha kwa msanii chipukizi wa muziki wa kizazi kipya, Karim Othman, maarufu kwa jina la K-One.
Japokuwa jina lake si maarufu miongoni mwa wasanii wa muziki wa kizazi kipya nchini, lakini umahiri wake wa kuimba na kutunga nyimbo zenye mashairi yenye mvuto umedhihirisha kwamba naye wamo.
K-One amedhihirisha ukali wake huo katika vibao vyake kadhaa, vikiwemo ‘Bila wewe’, ‘Sema baby’ , alivyowashirikisha wasanii nyota kama vile Ney wa Mitego na Pasha. Vibao hivyo viwili vimekuwa vikipigwa mara kwa mara kwenye vituo vya radio vya Times FM na Radio Uhuru.
Msanii huyo chipukizi amerekodi vibao hivyo katika studio za Brain Trust, zilizopo Temeke, Dar es Salaam kwa udhamini wa dada yake, ambaye hakupenda kumtaja jina.
Kwa mujibu wa K-One, amekuwa akipata sapoti kubwa ya kiusanii kutoka kwa familia yake, wakiwemo dada zake, ambao ndio wadhamini wake wakuu.
“Sio siri, naishukuru sana familia yangu, hasa bi mkubwa wangu (mama yangu) na dada zangu kwani wamekuwa wakinipa sapoti kubwa kiusanii. Japokuwa bado sijatoka kama ilivyo kwa wasanii wengine, lakini wamekuwa wakinipa moyo,”alisema msanii huyo.
Mbali na kurekodi vibao vyake, K-One pia amekuwa akishirikishwa kuimba viitikio katika nyimbo za wasanii mbalimbali maarufu wa muziki hao. Baadhi ya wasanii hao ni JB wa kundi la Mabaga Fresh na Mood Kibra.
Hivi sasa, K-One yupo katika hatua za mwisho za kukamilisha kibao chake kipya kinachokwenda kwa jina la ‘Valentine’. Amerekodi kibao hicho katika studio za Baucha Records.
Vibao vingine vilivyorekodiwa na msanii huyo, anayependa kutengeneza nywele zake kwa mtindo wa rasta ni ‘Kwa nini’, ‘Mpenzi sasa why’ na ‘Fau’. Amerekodi vibao hivyo kwenye studio za Brain Trust.
“Lengo langu ni kuwa na albamu moja ya nyimbo zangu zote. Naamini baada ya muda si mrefu, nitakuwa nimekamilisha albamu yenye nyimbo nane,”alisema msanii huyo.
Aliongeza kuwa, hadi sasa amekuwa akirekodi nyimbo zake kwa kutegemea msaada wa fedha kutoka kwa dada zake kwa vile bado hajapata wadhamini.
Ametoa mwito kwa wakuzaji wa vipaji vya wasanii nchini, kujitokeza kumsaidia kurekodi albamu yake na kusisitiza kuwa, hawatajutia uamuzi wao huo ama kupoteza fedha zao.
“Kipaji cha muziki ninacho na nimedhihirisha ukweli huo kupitia nyimbo zangu zilizofanikiwa kuzirekodi hadi sasa. Lakini ningependa kufika mbali zaidi, hivyo nawaomba mapromota wa muziki wa kizazi kipya wajitokeze kunidhamini,”alisema.
K-One alisema, muziki kwa sasa hapa nchini ni biashara na iwapo msanii atajiamini na kufanyakazi zake kwa umakini, ni rahisi kufaidi matunda ya jasho lake.
Kwa mujibu wa K-One, amepanga kukamilisha kazi ya kurekodi albamu yake kabla ya mwisho huu wa mwaka kumalizika. Alisema mambo yakienda vizuri, albamu yake hiyo itakuwa sokoni mwishoni mwa mwaka huu.
Je, ni kwa nini K-Onea aliamua kujitosa kwenye fani ya muziki wa kizazi kipya?
“Tangu nikiwa mdogo, nilipenda sana kushiriki katika maigizo na shughuli zozote zilizohusu mambo ya muziki. Ndipo nilipojigundua kwamba ninacho kipaji cha muziki kwani tangu nikiwa shule, niliweza kutunga mashairi ya wimbo,”alisema.
Kwa mujibu wa K-One, katika familia yake, hakuna ndugu yoyote aliyewahi kujihusisha na muziki huo. Ni yeye pekee, aliyejitosa kwenye fani hiyo baada ya kubaini kuwa, ana uwezo nayo.
“Lengo langu ni kuwaonyesha watanzania kwamba nina kipaji cha muziki. Pia nataka niutumie muziki kama ajira yangu kwa sababu ni biashara inayolipa,”alisema.
K-One ametoa wito kwa wasanii wa muziki wa kizazi kipya nchini, wapendane, kusaidiana na kuaminiana ili waweze kupiga hatua za juu zaidi kimaendeleo.
Alisema miongoni mwa sababu zinazochangia kuwakwamisha wasanii chipukizi wa muziki huo, ni kutokuwepo kwa umoja miongoni mwao, kuchukiana na kutosaidiana.
“Wasanii walio juu wanapaswa kukumbuka kuwa, kabla ya kufika huko waliko hivi sasa, nao walianzia chini, hivyo wasikwepe kuwasaidia wenzao wanaohitaji msaada kutoka kwao, hata kama wa kurekodi pamoja,”alisema.





Mwasiti kufyatua albamu mpya


BAADA ya ukimya wa muda mrefu, msanii Mwasiti Almasi ameibuka na kusema anatarajia kudondosha albamu yake mpya mara baada ya kumalizika kwa uchaguzi mkuu wa rais, wabunge na madiwani.
Akizungumza mjini Dar es Salaam wiki hii, Mwasiti alisema albamu yake hiyo itakuwa na vibao vinane, kikiwemo ‘Si kisa pombe’ alichokiimba kwa kumshirikisha rapa Quick Racka.
Albamu hiyo itakuwa ya pili kwa Mwasiti tangu alipoanza kung’ara katika muziki wa kizazi kipya, kutokana na tungo zake zenye mvuto na pia sauti maridhawa. Albamu yake ya kwanza inajulikana kwa jina la ‘Niambie’.
"Kwa sasa najiandaa kufyatua albamu yangu mpya ya pili, ambayo itakuwa na nyimbo nane na nimezirekodi kwenye studio tatu tofauti,” alisema mwanadada huyo.
Alizitaja studio alizorekodi vibao hivyo kuwa ni Ngoma Records, Fishcrab ya Lamar na Sound Crafters ya Enrico.
Licha ya maandalizi kuachia albamu hiyo kuendelea vyema, Mwasiti alisema hadi sasa bado hajaamua aiite jina gani kwa vile lengo lake ni kutafuta jina litakalowavuta mashabiki baada ya kuingia sokoni.
"Jina ndo bado naendelea kulitafuta, isipokuwa kila kitu kinaendelea vyema. Natumaini kila kitu kitakamilika mwezi ujao," alisema.
Mwanadada kutoka kundi la THT, alianza kutamba mara baada ya kuachia wimbo uliotamba wa 'Haooo' kabla ya kufyatua vibao vingine kama vile 'Niambie,' 'Huruma' na 'Nalivua pendo'.

Genevieve aendelea kuchemsha China

SANYA, China
MATUMAINI ya mrembo wa Tanzania, Genevieve Emmanuel kufanya vizuri katika shindano la kumsaka mrembo wa dunia mwaka huu, yamezidi kuota mbawa baada ya kuvurunda katika kinyang’anyiro cha kuwania mataji ya michezo na mitindo ya mavazi.
Katika kinyang’anyiro hicho, kilichowashirikisha warembo wote 119 wanaoshiriki kwenye shindano hilo, mrembo Lori Moore kutoka Ireland Kaskazini aliibuka mshindi wa taji la michezo wakati mrembo Mariann Birkedal kutoka Norway alitwaa taji la mitindo ya mavazi.
Mashindano ya kuwania mataji hayo pamoja na lile la vazi la ufukweni, hufanyika kabla ya fainali ya shindano hilo. Tayari Genevieve ameshachemsha katika taji la ufukweni, ambalo lilinyakuliwa na Yara Santiago kutoka Puerto Rico.
Washindi wa mataji hayo, wamefuzu moja kwa moja kuingia kwenye fainali ya shindano hilo, ambayo imepangwa kufanyika Oktoba 30 mwaka huu mjini Sanya.
Shindano la kuwania taji la michezo ndilo lililokuwa na mvuto wa aina yake kutokana na washiriki wote kuonyesha vipaji vyao katika michezo mbalimbali. Shindano hilo lilifanyika kwenye ufukwe wa hoteli ya Sheraton.
Mrembo Lori alishinda taji hilo baada ya kufanya vizuri na kutia fora katika michezo ya kuruka juu, mbio fupi na kuogelea. Alama alizozipata katika michezo hiyo ndizo zilizomwezesha kuibuka mshindi.
“Siwezi kuamini. Nimefuzu kuingia fainali,”alisema Lori, ambaye alizawadiwa medali.
Mshindi wa pili wa taji hilo alikuwa Marina Georgievo kutoka Slovakia wakati nafasi ya tatu ilinyakuliwa na Mariann wa Norway. Wote wawili pia walizawadiwa medali.
Katika kinyang’anyiro cha kuwania taji la mitindo ya mavazi, Mariann kutoka Norway aliibuka mshindi akifuatiwa na mrembo Irina Sharipova kutoka Russia na Alexandria Mills kutoka Marekani.
Katika kuwania taji hilo, washiriki walichuana kwa mavazi mbalimbali yaliyobuniwa na wabunifu maarufu wa mavazi wa China na kuwapa wakati mgumu majaji katika kuamua mshindi.
“Kwa kweli siwezi kuamini kwamba nimewashinda wasichana wengi na kuibuka mshindi wa taji hili,”alisema Mariann. “Ni heshima kubwa kwangu na bila shaka, nimefurahia kuingia fainali.”

Thursday, October 21, 2010

AZAM YAMKANA PHIRI


UONGOZI wa klabu ya Azam umesema, hauna mpango wa kumnyakua Kocha Mkuu wa Simba, Patrick Phiri katika mzunguko wa pili wa ligi kuu ya Tanzania.
Azam imesema, inauheshimu mkataba wa Phiri na Simba na kusisitiza kuwa, hauwezi kufanya mazungumzo na kocha huyo ama kufikiria kumwajiri wakati bado ana kibarua sehemu nyingine.
Msimamo huo wa Azam umekuja siku chache baada ya baadhi ya vyombo vya habari nchini kuripoti wiki hii kuwa, klabu hiyo imefanya mazungumzo na Phiri kwa lengo la kumwajiri.
Akizungumza kwa njia ya simu kutoka Turiani mjini Morogoro jana, Mratibu wa timu hiyo, Mohamed King alisema hakuna kiongozi yeyote wa klabu hiyo aliyewahi kukutana na kufanya mazungumzo na Phiri.
"Ninachoweza kusema ni kwamba, habari hizo ni za uzushi kwa sababu hazina ukweli wowote. Sisi kama Azam tunaheshimu mkataba kati ya Phiri na Simba,”alisema.
Mratibu huyo alisema, kwa sasa Azam itaendelea kuwa chini ya kocha wake mkuu, Itamar Amorin kutoka Brazil akisaidiwa na Habibu Kondo.
Baadhi ya vyombo vya habari viliripoti kuwa, Phiri huenda akajiunga na Azam siku chache zijazo baada ya kutokea hali ya kutokuelewana kati yake na viongozi wa Simba.
Hata hivyo, habari za uhakika kutoka ndani ya Simba zimeeleza kuwa, mkataba wa Phiri kuinoa timu hiyo unatarajiwa kumalizika mwishoni mwa mwezi ujao.
Naye Ofisa Habari wa Simba, Clifford Ndimbo amesema, taarifa za Phiri kwenda Azam sio za kweli kwa vile mkataba wa kocha huyo unatarajiwa kumalizika Januari mwakani.
"Phiri hawezi kuondoka Simba kwa sababu bado ana mkataba nahajawahi kuzungumza na viongozi wa Azam,"alisema Ndimbo alipozungumza kwa njia ya simu jana kutoka Mwanza.

BITEBO: Simba, Yanga zinashusha kiwango cha Stars

Na Mwandishi Wetu, Mwanza
MWANASOKA wa zamani wa timu ya Pamba ya Mwanza, Khalid Bitebo, amesema klabu za Simba na Yanga zimekuwa zikichangia kushuka kwa kiwango cha timu ya taifa, Taifa Stars.
Akizungumza mjini hapa mwishoni mwa wiki iliyopita, Bitebo alisema uamuzi wa klabu hizo kongwe nchini kusajili wachezaji wengi wa kigeni, ndio unaosababisha kiwango cha Taifa Stars kushuka.
Bitebo, ambaye enzi zake alikuwa maarufu kwa jina la Zembwela alisema, kuwepo kwa wachezaji wengi wageni katika klabu hizo kunawanyima nafasi wanasoka wazalendo kuonyesha vipaji vyao.
“Mimi siku zote huwa nasema, Simba na Yanga ndio mhimili wa soka ya Tanzania. Klabu hizi mbili ndizo zinazotoa wachezaji wengi wa Taifa Stars, hivyo zinaposajili wachezaji wengi wa kigeni, zinawanyima nafasi wanasoka wazalendo kuonyesha vipaji vyao,”alisema.
Aliongeza kuwa, japokuwa wanasoka wa kigeni wanasaidia kuleta ushindani katika ligi, lakini wingi wao ndani ya Simba na Yanga unashusha ari ya wanasoka wazalendo.
Mkongwe huyo wa soka alisema ni vyema viongozi wa Simba na Yanga wabadili mwelekeo kwa kutoa kipaumbele zaidi katika kusajili wachezaji wazalendo badala ya wageni.
Bitebo pia alieleza kushangazwa kwake na kiwango duni cha soka kilichoonyeshwa na timu za Simba na Yanga zilipomenyana katika mechi ya ligi kuu ya Tanzania Bara iliyochezwa mwishoni mwa wiki iliyopita.
Alisema kutokana na ukongwe wa timu hizo, uwezo zilionao kifedha na pia kuundwa na wanasoka wengi wageni, Simba na Yanga hazikupaswa kuonyesha kiwango duni.
Katika mechi hiyo iliyochezwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Yanga iliichapa Simba bao 1-0 na kuendeleza rekodi ya ushindi kwa watani wao hao.

MIMI NI YANGA DAMU!


HIVI ndivyo anavyoelekea kusema Kocha Mkuu wa Yanga, Kostadin Papic wakati alipokuwa akiingia kwenye Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza kabla ya timu hiyo kumenyana na Simba katika mechi ya ligi kuu ya Tanzania Bara. Yanga ilishinda bao 1-0.

SIMBA YAIPUMULIA YANGA

Na Mwandishi Wetu, Mwanza
SIMBA jana ilizunduka katika michuano ya soka ya ligi kuu ya Tanzania Bara baada ya kuicharaza AFC mabao 3-1 katika mechi iliyochezwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza.
Kwa matokeo hayo, Simba bado inashika nafasi ya pili katika msimamo wa ligi hiyo, ikiwa na pointi 18 baada ya kucheza mechi nane, nyuma ya vinara Yanga wanaoongoza kwa kuwa na pointi 19.
Yanga inaweza kuongeza tofauti ya pointi kati yake na Simba iwapo itaishinda JKT Ruvu leo katika mechi nyingine ya ligi hiyo, itakayochezwa kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro.
Simba ingeweza kuifunga AFC mabao mengi zaidi, hasa kipindi cha pili, lakini papara za washambuliaji wake, Emmanuel Okwi, Mussa Hassan ‘Mgosi’ na Patrick Ochan zilikuwa kikwazo.
Pambano hilo halikuwa na mvuto katika kipindi cha kwanza kutokana na timu zote kucheza soka ya kiwango cha chini na kushindwa kugongeana pasi za uhakika.
Iliwachukua Simba dakika tatu kuhesabu bao la kwanza lililofungwa na Hillary Echesa kwa mpira wa adhabu baada ya Emmanuel Okwi kuangushwa na beki mmoja wa AFC nje kidogo ya eneo la hatari.
Dakika tano baadaye, Jerry Santo aliiongezea Simba bao la pili baada ya kumalizia pasi maridhawa aliyotanguliziwa na Amri Kiemba.
AFC ilipata nafasi nzuri ya kufunga bao dakika ya 25 wakati Abdalla Juma alipofumua shuti kali la umbali wa mita 20, lakini kipa Juma Kaseja alilipangua na kuwa kona isiyokuwa na matunda.
Dakika ya 28, Ochan alitengenezewa pasi safi na Haruna Shamte na kubaki ana kwa ana na kipa Azizi Simon, lakini shuti lake lilitoka pembeni ya lango.
Okwi aliipotezea Simba nafasi nyingine nzuri ya kufunga bao dakika ya 33 baada ya kuwatoka mabeki wawili wa AFC, lakini shuti lake lilitoka nje.
AFC ilijibu mapigo dakika ya 45 baada ya Bakari Kigodeko kupewa pasi na kubaki uso kwa uso na kipa Kaseja wa Simba, lakini shuti lake lilitoka nje. Timu hizo zilikwenda mapumziko Simba ikiwa mbele kwa mabao 2-0.
Mchezo ulichangamka katika kipindi cha pili baada ya AFC kupata bao la kujifariji dakika ya 54. Bao hilo lilifungwa na mshambuliaji Jimmy Shoji baada ya kuunganisha wavuni kona iliyochongwa na Kigodeko.
Dakika 10 baadaye, Mgosi aliiongezea Simba bao la tatu, kufuatia kazi nzuri iliyofanywa na Okwi na Azizi Gilla waliogongeana pasi nzuri pembeni ya uwanja kabla ya kutoa pasi kwa mfungaji.
AFC ilipata pigo dakika ya 71 baada ya beki wake, Amri Msumi kutolewa nje kwa kadi nyekundu kwa kosa la kumchezea rafu mbaya Okwi. Awali, Msumi alikuwa ameonyeshwa kadi ya njano.
Pamoja na kucheza ikiwa pungufu, AFC ilipata nafasi mbili nzuri za kufunga mabao dakika ya 83 na 86, lakini zilipotezwa na Abdallah Juma na Shoji baada ya mashuti yao kuokolewa na kipa Kaseja.
Papara za Mgosi na Okwi ziliikosesha tena Simba bao dakika ya 90 baada ya kutokea piga nikupige kwenye lango la AFC. Shuti la kwanza la Mgosi lilimbabatiza kipa Azizi Simon wa AFC na lile la pili la Okwi lilitoka nje.
Simba: Juma Kaseja, Haruna Shamte, Juma Jabu, Kevin Yondani, Juma Nyoso, Hillary Echesa/ Mussa Mgosi, Jerry Santo, Amri Kiemba/Azizi Gilla, Rashid Gumbo, Patrick Ochani, Emmanuel Okwi.
AFC: Azizi Simon, Simon Mganga/Zahor Jairani, Andrew Carlos, Amri Msumi, Mohamed Upatu, Razaki Muhidin, Abdalla Juma, Kiworu Francis/Simon Nsajigwa, Juma Shoji, Bakari Kigodeko, Hilali Bigwa.

Genevieve aanza vibaya Miss World


SANYA, China
MREMBO wa Tanzania, Genevieve Emmanuel ameanza vibaya mashindano ya mwaka huu ya kuwania taji la dunia baada ya kutolewa mapema katika kinyang’anyiro cha vazi la ufukweni.
Genevieve hakuwa miongoni mwa warembo 40 waliovuka mchujo wa awali wa kuwania taji hilo. Alikuwa miongoni mwa warembo 79 waliotolewa mapema.
Taji hilo lilinyakuliwa na mrembo Yara Santiago kutoka Puerto Rico, ambaye sasa ataingia moja kwa moja katika hatua ya nusu fainali ya shindano hilo.
Katika shindano hilo lililofanyika juzi kwenye ufukwe wa mji wa Sanya, mrembo Alexandria Mills kutoka Marekani alishika nafasi ya pili akifuatiwa na Mariann Bincedal kutoka Norway.
Warembo 40 waliofuzu kuingia hatua ya nusu fainali ya shindani hilo walitoka katika nchi za Argentina, Australia, Bahamas, Barbados, Botswana, Bolivia, Bosnia & Herzegovina, Cape Verde, Cayman Islands, China PR, Jamhuri ya Czech, Ufaransa, French Polynesia, Ghana, Guadeloupe na Hong Kong China.
Wengine ni kutoka nchi za Hungary, India, Israel, Italia, Lithuania, Luxembourg, Martinique, Moldova, Mongolia, Uholanzi, New Zealand, Norway, Paraguay, Puerto Rico, Russia, St Lucia, Scotland, Sri Lanka, Thailand, Trinidad & Tobago, Uturuki, Ukraine, Marekani na Zimbabwe.
Kwa mujibu wa taratibu za shindano hilo, katika hatua za awali, washiriki huchuana katika kuwania taji la vazi la ufukweni, vipaji vya michezo na mrembo anayependeza kwenye picha (miss photogenic).
Fainali ya mashindano ya mwaka huu imepangwa kufanyika Oktoba 30, ambapo washiriki kutoka nchi 119 wanatarajiwa kupanda jukwaani kuwania taji hilo.
Katika mashindano hayo, bara la Afrika litawakilishwa na warembo kutoka nchi 18. Nchi hizo ni Angola, Botswana, Ivory Coast, Misri, Ethiopia, Ghana, Kenya, Lesotho na Malawi.
Zingine ni Mauritius, Namibia, Nigeria, Sierra Leone, Afrika Kusini, Uganda, Zambia, Zimbabwe na Tanzania.
Pamoja na kushindwa kufanya vizuri katika shindano la vazi la ufukweni, mrembo Emma Wareus kutoka Botswana ametajwa kuwa ni miongoni mwa wanaopewa nafasi kubwa ya kutwaa taji la dunia mwaka huu.
Shirika la Habari la OLBG limemwelezea Emma kuwa, ni mrembo mwenye sifa na vigezo vyote vinavyostahili kumfanya ashinde taji hilo, akifuatiwa na Kamilla Salgado kutoka Brazil na Laura Restrepo kutoka Colombia.
Emma amekuwa kivutio kikubwa tangu washiriki walipowasili mjini Sanya kutokana na uzuri wake wa sura na umbo na pia mambo mbalimbali, ambayo amekuwa akiyafanya.
Shirika hilo liliwataja warembo wengine wa Afrika wanaopewa nafasi ya kufanya vizuri kuwa ni Samantha Tshuma kutoka Zimbabwe, Ivaniltan Jones kutoka Angola na Zindaba Hanzala kutoka Zambia.

ROONEY: Bye bye Man Utd


LONDON, England
HATIMAYE Kocha Mkuu wa Manchester United, Sir Alex Ferguson amefichua kuwa, mshambuliaji Wayne Rooney anataka kuondoka katika klabu hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa juzi, Ferguson alikiri kuwa alipatwa na mshtuko na kukatishwa tamaa kusikia habari hizo, lakini alikanusha kuwepo na hali ya kutokuelewana kati yake na mchezaji huyo.
“Tumechanganyikiwa kama inavyoweza kutokea kwa yeyote, lakini hatuwezi kuelewa kwa nini anataka kuondoka,”alisema kocha huyo raia wa Scotland. Hata hivyo, Ferguson alisema milango ipo wazi kwa Rooney iwapo atabadili uamuzi wake huo. Rooney alishindwa kuichezea Manchester United jana katika mechi ya ligi ya mabingwa wa Ulaya dhidi ya Bursaspor kutokana na kuwa majeruhi.
Hatima ya Rooney kuendelea kuwepo Manchester United ilikuwa shakani, kufuatia kuwepo na habari kwamba aligoma kutia saini mkataba mpya wa kuichezea klabu hiyo. Mkataba wa sasa wa Rooney unatarajiwa kumalizika mwishoni mwa msimu wa 2011/12.
Akihojiwa na kituo cha televisheni cha MUTV kabla ya kuzungumza na waandishi wa habari juzi, Ferguson alisema Mtendaji Mkuu wa klabu hiyo, David Gill alimweleza kuhusu uamuzi huo wa Rooney kutosaini mkataba mpya.
“Nilikuwa ofisini Agosti 14 na David alinipigia simu kunieleza kwamba Rooney hatasaini mkataba mwingine,”alisema Ferguson.
“Miezi michache iliyopita alisema yupo kwenye klabu kubwa dunia na anataka kubaki hapa maisha yake yote. Hatuelewi nini kimebadili msimamo wa kijana huyu,”aliongeza.
Mara baada ya kupata taarifa hizo, Ferguson alisema aliomba kuzungumza na mchezaji huyo, ambaye alimuhakikishia kuhusu uamuzi wake huo.
Ferguson alisema amesikitishwa na uamuzi huo wa Rooney kwa sababu alifanya kila analoweza kumsaidia tangu alipojiunga na klabu hiyo mwaka 2004 akitokea Everton.
“Hatuna tulichokifanya zaidi ya kumsaidia tangu alipowasili katika klabu hii,”alisema Ferguson, ambaye bado hajakata tamaa ya kumzuia mchezaji huyo asiondoke.
Wakati huo huo, Rooney amewadokeza wachezaji wenzake wa Manchester United kuwa, huenda akafikiria kujiunga na mahasimu wao, Manchester City.
Rooney alielezea msimamo wake huo siku chache baada ya kuieleza Manchester United kwamba, hatarajii kuongeza mkataba mpya na klabu hiyo.
Tayari Manchester City imeshaonyesha dhamira ya kumsajili mchezaji huyo wakati wa usajili wa dirisha dogo Januari mwakani na ipo tayari kumlipa mshahara wa pauni 230,000 (sh. milioni 529) kwa wiki.
Iwapo Manchester City itafanikiwa kumsajili Rooney, atakuwa ndiye mchezaji ghali kuliko wote wanaocheza katika ligi kuu ya England hivi sasa.
Baadhi ya wachezaji wa Manchester United wamelieleza gazeti la Daily Mail kuwa, uamuzi wa Rooney kuondoka klabu hiyo unatokana na masuala ya pesa na si kutokuelewana kwake na Kocha Sir Alex Ferguson.
Mke wa mwanasoka huyo, Coleen ameshamweleza wazi mumewe kuwa, hawezi kwenda nje ya England, hasa katika kipindi hiki, ambacho dada yake, Rosie ni mgonjwa.
Msimamo huo wa Coleen umemfanya Rooney akubali kubaki England na kujiunga na moja kati ya klabu za Manchester City na Chelsea, ambazo ndizo pekee zenye uwezo wa kumlipa mshahara mnono na kumudu ada ya uhamisho.
Rooney amewaeleza wazi wachezaji wenzake kuwa, hatafikiria mara mbili kujiunga na Manchester City iwapo klabu hiyo itawasilisha maombi ya kumsajili kabla ya Januari mwakani.
Kwa mujibu wa sheria za Shirikisho la Soka la Dunia (FIFA), Rooney anaruhusiwa kulipa pauni milioni tano kwa ajili ya kuvunja mkataba wake, iwapo utakuwa umesalia mwaka mmoja kabla ya kumalizika.
Kipengele hicho ndicho kilichozua hofu kwa viongozi wa Manchester United, ambao wana wasiwasi kuwa, wasipomuuza Januari mwakani, huenda akavunja mkataba wake ama kuhama bila kulipiwa ada.
Kocha Mkuu wa Chelsea, Carlo Ancelotti alisema juzi kuwa, atafikiria kumsajili mshambuliaji huyo wakati Kocha Mkuu wa Manchester City, Roberto Mancini bado anafuatilia hatma ya mchezaji huyo katika klabu ya Manchester United.
“Kwa sasa, Chelsea haitarajii kumsajili Rooney kwa sababu bado ni mchezaji wa Manchester United na nafikiri bado wanaweza kumaliza tatizo lililojitokeza,”alisema Ancelotti.
“Kama Rooney atawekwa sokoni, si Chelsea pekee itakayotaka kumsajili, bali na klabu zingine kubwa duniani,”aliongeza.
Klabu nyingine iliyoonyesha nia ya kumsajili mshambuliaji huyo wa kimataifa wa England ni Real Madrid ya Hispania. Lakini kocha wake, Jose Mourinho alikuwa mwangalifu kuzungumzia suala hilo kwa hofu ya kumchefua Ferguson.
“Sifikirii iwapo atahama. Nafikiri kocha wake atamshawishi abaki,”aliongeza.
Mkurugenzi wa Real Madrid, Jorge Valdano alifichua juzi kuwa, anavutiwa na mchezaji huyo, lakini hana nafasi kwenye kikosi cha kwanza cha timu hiyo.
Real Madrid imekuwa ikihusishwa na mipango ya kumsajili Rooney tangu msimu uliopita, ambapo rais wake wa zamani, Ramon Calderano alidai mapema mwaka huu kuwa, mrithi wake, Florentino Perez naye anavutiwa na mchezaji huyo.
Valdano alilieleza gazeti la Telemadrid: "Navutiwa sana na Rooney, lakini swali la kujiuliza ni je, kama Rooney atakuja, nani tutamwondoa kwenye timu. Tunao wachezaji wazuri wa safu ya ushambuliaji, akina Ronaldo, Higuain, Ozil na Di Maria.”
Rais huyo wa zamani wa Real Madrid alisema pia kuwa, klabu hiyo ina hazina ya wachezaji wengi chipukizi, ambao wataifanya isiwe na tatizo la kusajili wachezaji nyota kutoka nje kwa kipindi cha miaka kumi ijayo.
Taarifa za Rooney kutaka kufuata nyayo za Carlos Tevez, aliyejiunga na Manchester City msimu uliopita akitokea Manchester United, huenda zikawashtua mashabiki wa klabu hiyo.
Uhusiano wa Rooney na Kocha Ferguson umekuwa mbovu tangu mchezaji huyo alipokumbwa na kashfa ya kufanya mapenzi na changudoa.
Kocha Ferguson amekuwa akimweka benchi Rooney katika mechi kadhaa za ligi kuu ya England huku akitoa taarifa kwamba, mchezaji huyo ni majeruhi.
Hata hivyo, Rooney amezikana taarifa hizo za Ferguson na kusisitiza kuwa, yupo fiti na hajawahi kuumia tangu msimu huu ulipoanza.
Tayari Manchester United imeshaeleza wazi kuwa, haina mpango wa kumuuza Rooney wakati wa dirisha dogo na imeziita taarifa hizo kuwa ni za uzushi.
Katika hatua nyingine, kiungo wa zamani wa Manchester United, Roy Keane amemwonya Rooney awe makini katika kufikia uamuzi wa kuihama klabu hiyo.
Keane alisema juzi kuwa, kutokuelewana kwa Rooney na Ferguson hakupaswi kuwa kigezo cha yeye kuhama kwa vile wachezaji na makocha kukorofishana mara kwa mara ni jambo la kawaida katika maisha ya soka.