KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, October 31, 2012

KUSHUHUDIA MISS TANZANIA SH. 100/-



WAKATI zikiwa zimesalia siku mbili kabla ya Redd’s Miss Tanzania 2012 kupatikana na kila mshiriki akibaki kujiuliza nani atatwaa taji hilo, kiingilio cha kushuhudia shindano hilo kimetajwa.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mkurugenzi wa Kampuni ya Lino walio waandaaji, Hashim Lundenga, alisema kiingilio kitakuwa Sh 100,00 huku kukiwa na burudani za kufa mtu.
Mshidi atajitwalia gari pamoja na fedha taslimu Sh milioni 8, katika kinyang’anyiro hicho kinachotarajiwa kufanyika kwenye ukumbi wa hoteli ya Blue Pearl uliopo jengo la Ubungo Plaza, Dar es Salaam keshokutwa.
Lundenga alisema warembo watano wamefanikiwa kuingia hatua ya 15 Bora ya Redd’s Miss Tanzania kutokana na kushinda katika mashindano madogo.
Warembo hao ni Lucy Stephano aliyeshinda Miss Photogenic, Mary Chizi aliyetwaa taji la Miss Sports Lady, Babylove Kalala aliyeshinda Miss Talent, Magdalena Roy aliyetwaa taji la Top Model na Miss Personality, Happiness Daniel.
Lundenga alisema, burudani siku hiyo itatolewa na msanii wa muziki wa kizazi kipya, Diamond Platinum, Winfrida Josephat ‘Rachel’ pamoja na yule wa ngoma za asili, Wanne Star.
“Tumekamilisha kila kitu, naamini atapatikana mrembo mkali zaidi ambaye atatuwakilisha vema katika mashindano ya dunia,” alisema.
Lundenga alisema, tayari tiketi zinauzwa katika vituo kadhaa ambavyo ni Regency Park Hotel, Rose Garden, Share Illusion, Mlimani City, City Sport Lounge, Giraffe Hotel, Ubungo Plaza na katika ofisi za Lino.
Shindano la Redds Miss Tanzania 2012 linadhaminiwa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), kupitia kinywaji cha Redds Original.



YANGA WANACHEEKA, SIMBA WAMENUNA


Mchezaji Simon Msuva (kushoto) wa Yanga akikabwa koo na beki wa Mgambo JKT wakati wa mechi ya ligi kuu ya Tanzania Bara iliyochezwa leo kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Yanga imeshinda mabao 3-0. (Picha kwa hisani ya BIN ZUBEIRY).

YANGA jana ilionyesha dhamira yake ya kuwapoka uongozi wa ligi kuu ya Tanzania Bara wapinzani wao wa jadi Simba baada ya kuicharaza Mgambo JKT mabao 3-0 katika mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Ushindi huo uliiwezesha Yanga kuwa na pointi sawa na Simba, lakini inazidiwa kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa na watani wao hao, ambao leo wamelazimishwa sare ya bao 1-1 na vibonde, Polisi Morogoro.
Mabao ya Yanga yalipachikwa wavuni na beki Nadir Haroub 'Cannavaro, Didier Kavumbagu na Jerry Tegete.
Nayo Simba ilijikuta majaribuni baada ya Polisi Morogoro kuwa ya kwanza kupata bao kupitia kwaa mshambuliaji wake, Mokili Rambo.
Simba ilisawazisha kipindi cha pili kwa bao lililofungwa na kiungo wake mahiri, Amri Kiemba.

Tuesday, October 30, 2012

WABABE WA TWIGA STARS WACHEZEA KICHAPO AWC



Ethiopia ambayo iliinyima Tanzania (Twiga Stars) nafasi ya kucheza fainali za Afrika kwa Wanawake (AWC) zinazochezwa Equatorial Guinea imeanza vibaya fainali hizo baada ya kufungwa mabao 5-0 na Ivory Coast.
Mechi hiyo ya kundi B ilichezwa juzi usiku (Oktoba 29 mwaka huu) Uwanja wa Nkoantoma ulioko mjini Bata, ambapo mpaka mapumziko Ethiopia ilikuwa imeshalala kwa mabao 2-0. Kwa ushindi huo Ivory Coast inaongoza kundi hilo kwa tofauti ya mabao dhidi ya Nigeria.
Nigeria ambao ni mabingwa watetezi waliibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Cameroon katika mechi iliyotangulia kwenye uwanja huo. Katika fainali saba zilizopita za AWC, Nigeria imeibuka mabingwa mara tano.
Ethiopia ambayo iliitoa Twiga Stars katika raundi ya mwisho ya mechi za mchujo za AWC kwa kushinda Addis Ababa na Dar es Salaam itacheza mechi yake ya pili Novemba Mosi dhidi ya Nigeria ambayo kama ikipoteza itakuwa imetolewa kwenye fainali hizo.
Katika mechi za ufunguzi za kundi A wenyeji Equatorial Guinea (Nzalang Nacional) waliibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Afrika Kusini (Banyana Banyana) kwenye Uwanja wa Malabo. Bao la washindi lilifungwa dakika ya 33 kwa kichwa na Gloria Chinasa.
Nayo Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) licha ya kuwasili hapa siku ya mechi iliifunga Senegal bao 1-0 katika mechi nyingine ya kundi A. Bao la DRC lilifungwa dakika ya 74 kwa njia ya penalti na Lucie Nona.
Boniface Wambura
CAF Media Team, Malabo, Equatorial Guinea

UCHAGUZI DRFA DESEMBA 12



TFF imebadilisha tarehe ya kuanza kuchukua fomu kwa watu wanaotaka kugombea uongozi wa Chama cha Mpira wa Miguu cha Dar es salaam (DRFA) kwa lengo la kuhakikisha kuwa mchakato wa uchaguzi unafanyika kwa mujibu wa kanuni. Kamati ya Uchaguzi ya DRFA ilitangaza jana kuwa uchukuaji fomu ungeanza leo, lakini DRFA iliandikiwa barua jana kuelezwa kuwa mchakato huo sasa utaanza kesho na uchaguzi utafanyika Desemba 12, 2012.
Mchakato wa uchaguzi wa viongozi wa DRFA utakuwa kama ifuatavyo:
30/10/2012 Kamati ya Uchaguzi DRFA kutangaza uchaguzi na nafasi
zinazogombewa kwa mujibu wa katiba ya DRFA
31/10/2012 Kuanza kuchukua fomu za kugombea uongozi
04/11/2012 Mwisho wa kurudisha fomu ifikapo saa 10:00 alasiri
05-09/11/2012 Kamati ya Uchaguzi DRFA kupitia fomu za waombaji uongozi na kutangaza matokeo na kubandika kwenye mbao majina ya waombaji uongozi.
10-14/11/2012 Kutoa fursa ya pingamizi dhidi ya waombaji uongozi. Pingamizi ziwasilishwe kwa katibu wa Kamati ya Uchaguzi DRFA na
wawekaji pingamizi wazingatie Ibara ya 11 (2) ya Kanuni za
Uchaguzi za Wanachama wa TFF.
15-17/11/2012 Kujadili pingamizi, usaili na kutangaza matokeo ya usaili na
kuwajulisha kwa maandishi.
18-20/11/2012 Kukataa rufaa dhidi ya maamuzi ya Kamati ya Uchaguzi ya DRFA
21-25/11/2012 Rufaa kusikilizwa na Kamati ya Uchaguzi ya TFF na kutangaza matokeo ya rufaa (Kama hakuna rufaa, Kamati ya Uchaguzi ya
DRFA kutangaza majina ya wagombea na nafasi wanazogombea
na kuanza kampeni).
26/11/2012 Baada ya maamuzi ya Kamati ya Uchaguzi ya TFF, Kamati ya
Uchaguzi ya DRFA kutangaza majina ya wagombea na nafasi zao na kuanza kwa kampeni
12/12/2012 Uchaguzi

TFF: CHONDE CHONDE YANGA, MLIPENI NJOROGE



TFF inapenda tena kuihimiza klabu ya Yanga kumalizana na mchezaji wake wa zamani, John Njoroge Mwangi kabla ya Novemba 2, 2012 ili ijiepushe na adhabu kaili inayoweza kuchukuliwa na Shirikisho la Kimataifa la Vyama vya Mpira wa Miguu (FIFA). Kwa mujibu wa barua ya FIFA, iwapo Yanga haitakuwa imemlipa mchezaji huyo na kusiwepo na mawasiliano yoyote, shauri hilo litawasilishwa kwenye Kamati ya Nidhamu ya FIFA itakayokutana Novemba 14, 2012 kutathmini hukumu iliyotolewa mapema Januari mwaka huu.
Mchezo namba 10 wa Ligi Daraja la Kwanza (FDL) baina ya Morani na Polisi Tabora uliokuwa uchezwe Kiteto mjini Tabora Oktoba 31, 2012, sasa utachezwa Novemba 01, 2012 baada ya treni ambayo Morani walikuwa wakisafiria kutoka kupata matatizo njiani wakati wakitoka Kigoma ambako walicheza na Kanembo.
TFF inapenda kutoa ufafanuzi wa taarifa zilizotolewa na baadhi ya vyombo vya habari leo, likiwemo gazeti la Habari Leo na Daily News, vikimnukuu rais wa TFF, Leodegar Tenga akisema kuwa amewataka watu wanaotaka kugombea uongozi wa shirikisho watangaze nia ili wapate kujadiliwa. Waandishi walioandika habari hiyo hawakumnukuu vizuri Rais Tenga wakati akizungumzia masuala ya uchaguzi na hivyo kupotosha maana nzima ambayo Ndg. Tenga alitaka iwafikie wapenzi wa michezo na hasa mpira wa miguu. Rais Tenga alivitaka vyombo vya habari vianzishe mjadala utakaowashirikisha wapenzi wa mpira wa miguu ili waelezee wanatarajia nini katika miaka ijayo na hivyo kuwafanya viongozi watakaochaguliwa kufanya kazi kwa utashi wa maoni hayo ya wananchi. Tunaelewa kuwa Rais Tenga ni muumini wa kuheshimu katiba, sheria na kanuni na hivyo hawezi kutoa kauli ambayo inakiuka mchakato wa uchaguzi wa TFF kwa kuwataka wanaowania uongozi kutangaza nia sasa badala ya kusubiri muda wa kikanuni ufike. Ikumbukwe katika kikao chake na wahariri aliwahi kuulizwa swali kama hilo na akasema kuwa akijibu lolote atakuwa amekiuka kanuni za uchaguzi kwa kuwa itamaanisha anaanza kampeniu kabla ya muda. Ni vizuri waliohusika wakafanya masahihisho ili kuzuia habari zao kutafsiriwa tofauti na wadau wa mpira wa miguu na hivyo kuweka uwezekano wa kuvuruga mchakato wa uchaguzi.

POULSEN AMALIZA ZIARA ZENJI



Kocha mkuu wa timu ya taifa ya Tanzania, Kim Poulsen amerejea Dar es salaam baada ya kufanya ziara kwenye visiwa vya Pemba na Unguja ambako alishuhudia mechi sita za Ligi Kuu ya Grand Malta kuanzia Oktoba 19, 2012 hadi Oktoba 26, 2012 visiwani Zanzibar. Poulsen alishuhudia mechi baina ya Falcom na Bandari iliyoisha kwa Falcom kushinda kwa mabao 3-1 na pia mechi baina ya Duma na Bandari ambayo iliisha kwa Bandari kuibuka na ushindi wa mabao 2-0. Mechi hizo mbili zilifanyika kisiwani Pemba.

Poulsen pia alishuhudia mechi zilizofanyika kwenye Uwanja wa Amaan kisiwani Unguja ambako Mtendeni iliibwaga Chipukizi kwa mabao 2-1; Mundu na Jamhuri (0-1), KMKM na Zimani Moto (1-0); na Mafunzo dhidi ya Chuoni iliyoisha kwa Mafunzo kulala kwa mabao 3-0.
Poulsen amefurahishwa na ziara hiyo na kusema kuwa ni kitu kizuri kwake na kwa soka la Tanzania kwa ujumla. Poulsen alisema kuwa amefurahishwa na mapokezi aliyopata visiwani Zanzibar na kukishukuru Chama cha Mpira wa Miguu cha Zanzibar (ZFA) kwa ushirikiano mkubwa alioupata wakati wote akiwa Zanzibar.
Hata hivyo, Poulsen alisema hawezi kueleza kwa sasa kama ameona wachezaji anaoweza kuwaita kwenye kikosi cha Taifa Stars, lakini akasema amevutiwa na viwango vya wachezaji wengi.

KAMATI YA LIGI YAWAOMBA RADHI WANAHABARI



1. Kamati ya Ligi jana (Oktoba 29,2012) ilifanya kikao pamoja na klabu zinazoshiriki Ligi Kuu ya Vodacom kujadili mambo kadhaa, likiwemo tukio la Jumamosi iliyopita la kuzuia televisheni na radio kutangaza moja kwa moja michezo ya Ligi Kuu pamoja na wapiga picha za televisheni kuchukua picha kwa ajili ya kutumia kwenye habari. Kamati ilifanya mazungumzo na mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo (TASWA), Juma Pinto kuhusu msukosuko huo na kufikia muafaka katika masuala yafuatayo:

a- kwamba uamuzi wa kuzuia vituo vya redio na televisheni kutangaza moja kwa moja ulikuwa sahihi lakini una kasoro katika utekelezaji kwa kuwa hayakuwepo mawasiliano rasmi kwa vyombo vya habari na pia haukutoa muda wa kutosha kwa vyombo hivyo vya habari kufanya maandalizi kwa kadri ya utashi wa klabu za Ligi Kuu.
b- Kwamba Kamati ya Ligi haijakataza redio kutangaza moja kwa moja michezo ya Ligi Kuu, bali vituo vya redio ambavyo vinataka kutangaza moja kwa moja michezo ya Ligi Kuu vifanye hivyo bila ya kuweka matangazo ya wadhamini na kama matangazo hayo ya moja kwa moja yatadhaminiwa, basi vituo hivyo havina budi kuwasiliana kwa maandishi na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kwa maelekezo zaidi.
c- Kwamba vituo vya redio vitakavyotaka kutangaza moja kwa moja michezo ya Ligi Kuu, ni lazima zitamke mashindano hayo kuwa ni “Ligi Kuu ya Vodacom”.
d- Kwamba vituo vya televisheni vitakavyotaka kutangaza moja kwa michezo ya Ligi Kuu ya Vodacom, ni lazima viingie mkataba na TFF ambao utaaridhiwa na klabu husika. Kwa sasa, kituo cha televisheni cha Star TV hakitaruhusiwa kurusha matangazo ya moja kwa moja ya michezo hiyo hadi hapo mkataba utakaposainiwa na tunatumaini mkataba huo utasainiwa kabla ya mechi za kesho na hivyo kuwapa fursa wapenzi wa soka wa maeneo mbalimbali kuendelea kushuhudia Ligi Kuu ya Vodacom.
e- Kwamba vituo vya televisheni vitakavyotaka kuchukua picha kwa ajili ya habari zinaruhusiwa kufanya hivyo. Endapo kituo hicho kitaonyesha mchezo uliorekodiwa, hatua zitachukuliwa dhidi ya kituo hicho.
f- Kamati inaomba radhi kwa usumbufu uliosababishwa na uamuzi huo, lakini inazidi kusisitiza kuwa uamuzi huo ulifanywa kwa lengo zuri la kuendelea kutafuta vyanzo vya fedha vitakavyoziwezesha klabu kujimudu kiuchumi na kuifanya Ligi Kuu ya Vodacom iendeshwe kwa ubora zaidi.

AZAM YAMTIMUA BUNJAK, YAMREJESHA STEWART


KLABU ya Azam imetangaza kumtimua kocha wake, Boris Bunjak kutoka Serbia na kumrejesha kocha wa zamani, John Stewart Hall.
Uamuzi huo wa bodi ya wakurugenzi ya Azam, umekuja siku chache baada ya timu hiyo kuchapwa mabao 3-1 na Simba katika mechi ya ligi kuu ya Tanzania Bara iliyochezwa kwenye uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Taarifa iliyotolewa na Azam leo imesema kuwa, Bunjak ameondolewa kutokana na kushuka kwa kiwango cha timu hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Stewart anatarajiwa kurejea nchini Alhamisi kutoka Kenya, ambako alikuwa akiifundisha timu ya Sofapaka.

NSA JOB NJE KWA WIKI SITA




MSHAMBULIAJI nyota wa Coastal Union, Nsa  Job atakuwa nje ya uwanja kwa wiki sita kufuatia kuvunjika mguu wake wa kushoto.
Nsa alipatwa na maswaibu hayo mwishoni mwa wiki iliyopita wakati Coastal Union ilipomenyana na JKT Ruvu katika mechi ya ligi kuu ya Tanzania Bara iliyochezwa kwenye uwanja wa Chamazi, Dar es Salaam.
Kwa sasa, mshambuliaji huyo amefungwa plasta ngumu na atakosa mechi zote zilizosalia za raundi ya kwanza ya ligi hiyo.
Mkurugenzi wa Ufundi wa Coastal Union, Nassor Bin Slum amesema goti la mshambuliaji huyo liligeuka, lakini madaktari wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili walifanikiwa kulirejesha kwenye sehemu yake.
Kwa mujibu wa Bin Slum, mchezaji huyo anatarajiwa kupelekwa India kwa ajili ya matibabu zaidi ya mguu wake ili aweze kuendelea kucheza soka.

Saturday, October 27, 2012

SIMBA YAITOA NISHAI AZAM, YANGA YAPAA



SIMBA jana iling'ara katika michuano ya soka ya ligi kuu ya Tanzania Bara baada ya kuichapa Azam mabao 3-1 katika mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Mshambuliaji Emmanuel Okwi kutoka Uganda ndiye aliyeing'arisha Simba baada ya kuifungia mabao mawili kati ya matatu. Bao lingine lilifungwa na Felix Sunzu.
Azam ilikuwa ya kwanza kupata bao kupitia kwa mshambuliaji wake nyota, John Bocco, ambaye alishindwa kuendelea na mchezo baada ya kuumia dakika ya 20.
Ushindi huo uliiwezesha Simba kuendelea kuongoza ligi hiyo ikiwa na pointi 22 baada ya kucheza mechi 10, ikifuatiwa na Yanga yenye pointi 20 na Azam yenye pointi 18.
Yanga ilichupa nafasi ya pili baada ya jana kuichapa JKT Oljoro bao 1-0 katika mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid mjini Arusha.
Bao pekee na la ushindi la Yanga lilifungwa na beki wa kimataifa wa Rwanda, Mbuyu Twite.
Katika mechi zingine za ligi hiyo zilizochezwa jana, African Lyon ilitoka sare ya bao 1-1 na Kagera Sugar kwenye uwanja wa Chamazi, Dar es Salaam, Ruvu Shooting iliichapa Polisi Morogoro mabao 2-1 kwenye uwanja wa Mabatini, Mlandizi, Pwani.

Friday, October 26, 2012

IDD EL HAJJ NJEMA


Allaahu Akbar, Allaahu Akbar, Allaahu Akbar

Allaah is Great, Allaah is Great , Allaah is Great
Mwenyezi Mungu ni mkubwa, Mwenyezi Mungu ni mkubwa, Mwenyezi ni mkubwa

Laa ilaaha illaLlaah
there is no God, but Allaah
Hakuna Mola isipokuwa Allaah

Allaahu Akbar, Allaahu Akbar
Allaah is Great, Allaah is Great
Mwenyezi Mungu ni mkubwa, Mwenyezi ni mkubwa

Walillaahil Hamd
to Him belongs all Praise
Kwake ndiye anaestahiki kushukuriwa

Wednesday, October 24, 2012

YANGA RAHA TUPU



YANGA jana iliendelea kujiimarisha katika msimamo wa ligi kuu ya Tanzania Bara baada ya kuichapa Polisi Morogoro mabao 3-0 katika mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Matokeo hayo yameiwezesha Yanga kuendelea kushika nafasi ya tatu katika msimamo wa ligi hiyo, ikiwa na pointi 17 baada ya kucheza mechi tisa, nyuma ya Azam inayoshika nafasi ya pili kwa kuwa na pointi 18 na mabingwa watetezi Simba wanaoongoza kwa kuwa na pointi 19.
Iliwachukua Yanga dakika tano kuhesabu bao la kwanza lililofungwa na Simon Msuva baada ya kupokea pasi safi kutoka kwa Jerry Tegete.
Dakika moja baadaye, Didier Kavumbagu aliiongezea Yanga bao la pili kwa shuti kali baada ya kupokea pande kutoka kwa Athumani Iddi 'Chuji'.
Yanga nusura iongeze bao dakika ya 13 baada ya Tegete kuwatoka mabeki wawili wa Polisi, lakini shuti lake lilimbabatiza beki mmoja na kuwa kona, ambayo haikuzaa matunda.
Msuva angeweza kufunga bao dakika ya 21 baada ya kupokea pasi kutoka kwa Tegete, aliyewatoka mabeki wawili wa Polisi, lakini shuti lake lilidakwa na kipa Kondo Salum, aliyeingia dakika ya 19 kuchukua nafasi ya Kulwa Manji, aliyeumia.
Polisi ilifanya shambulizi kali langoni mwa Yanga dakika ya 25 wakati Nadir Haroub na Chuji walipotegeana kuokoa mpira, lakini shuti la Nicholas Jabipe lilitoka sentimita chache nje ya lango.
Vijana wa Polisi walifanya shambulizi lingine dakika ya 35 wakati Mokili Rambo alipomtoka Chuji na kufumua kiki kali, lakini ilitoka nje.
Mwamuzi Alex Mahagi kutoka Mwanza aliizawadia Yanga penalti dakika ya 37 baada ya Msuva kuvutwa jezi na beki John Bosco ndani ya eneo la hatari, lakini shuti la Haruna Niyonzima liligonga mwamba na kuokolewa na mabeki wa Polisi.
Polisi walipata nafasi nzuri za kufunga dakika ya 41 na 41, lakini shuti la Bantu Admini lilidakwa na kipa Ally Mustafa wakati lile la Malimi Busungu lilitoka nje ya lango. Timu hizo zilikwenda mapumziko Yanga ikiwa mbele kwa mabao 2-0.
Timu zote mbili zilikianza kipindi cha pili kwa kasi, lakini ni Yanga iliyopata nafasi nzuri ya kufunga dakika ya 51 wakati Tegete alipounganishwa kwa kichwa krosi kutoka kwa Niyonzima, lakini mpira ulitoka nje.
Hamisi Kiiza aliifungia Yanga bao la tatu dakika ya 58 kwa shuti kali la mguu wa kulia baada ya kupokea pasi kutoka kwa Luhende.
YANGA: Ally Mustapha, Shadrack Nsajigwa, Oscar Joshua, Nadir Haroub, Mbuyu Twite, Athumani Iddi, Simon Msuva, Haruna Niyonzima/ Nurdin Bakari, Jerry Tegete/ Hamisi Kiiza, Didier Kavumbagu, David Luhende.
POLISI: Manji Kulwa/ Kondo Salum, Nahodha Bakari, John Bosco, Noel Msakwa, Salmini Kisi, Hamisi Mamiwa, Bantu Admini, Paschal Maige, Mokili Rambo, Malimi Busungu, Nicholas Jabipe.
Wakati huo huo, Azam leo ilishindwa kutwaa uongozi wa ligi kuu ya Tanzania Bara baada ya kulazimishwa kutoka sare ya bao 1-1 na Ruvu Shooting katika mechi iliyochezwa kwenye uwanja wa Chamazi, Dar es Salaam.
Sare hiyo imeifanya Azam iendelee kushika nafasi ya pili katika msimamo wa ligi hiyo, ikiwa na pointi 18 baada ya kucheza mechi nane wakati Ruvu Shooting ni ya 10 ikiwa na pointi 10.
Katika mechi nyingine zilizochezwa leo, Coastal Union iliichapa African Lyon bao 1-0 kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga. Bao pekee na la ushindi la Coastal lilifungwa na Nsa Job dakika ya 47.
Nazo Mtibwa Sugar na Kagera Sugar zilishindwa kutambiana baada ya kutoka sare ya bao 1-1 katika mechi iliyopigwa kwenye uwanja wa Manungu uliopo Turiani mjini Morogoro.

WAAMUZI WALA RUSHWA KUCHUNGUZWA


CHAMA cha Waamuzi wa Soka Tanzania (FRAT), kimesema kinafanyia kazi tuhuma za waamuzi wake kupokea rushwa ili wachezeshe kwa upendeleo katika mechi za ligi kuu ya Tanzania Bara.
Mwenyekiti wa FRAT, Joan Minja alisema mjini Dar es Salaam jana kuwa, wamekuwa wakipokea tuhuma hizo mara kwa mara kutoka kwa wadau wa soka hivyo wameona ni vyema wazifanyie kazi ili kubaini ukweli.
Joan alisema tuhuma zozote zinazohusiana na rushwa ni nzito na zinapaswa kuchunguzwa kwanza ikiwa ni pamoja na kupatikana kwa uthibitisho kabla ya kutolewa uamuzi.
Alisema baada ya kuzifanyiakazi tuhuma hizo, wanatarajia kuwasilisha ripoti kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwa ajili ya maamuzi zaidi.
"Hatuwezi kutoa ripoti za uchunguzi wetu kwa vyombo vya habari, tutafanya hivyo kwa TFF kwa sababu ndicho chombo tunachofanyanacho kazi,"alisema mwenyekiti huyo mpya wa FRAT aliyechaguliwa hivi karibuni mjini Dodoma.
Timu kadhaa zinazoshiriki katika michuano ya ligi kuu, zimekuwa zikiwalalamikia baadhi ya waamuzi kwa madai kuwa, wamekuwa wakichezesha kwa upendeleo kutokana na kupewa rushwa.
Tayari kamati ya ligi imeshatangaza kuwasimamisha baadhi ya waamuzi na kuwaondoa kwenye ligi kwa madai ya kuvurunda katika baadhi ya mechi.
Mmoja wa waamuzi waliofungiwa ni Mathew Akrama kutoka Mwanza, aliyechezesha mechi ya ligi hiyo kati ya Simba na Yanga, iliyopigwa kwenye Oktoba 3 mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Timu hizo zilitoka sare ya bao 1-1.

MILOVAN AWATOSA BOBAN NA NYOSO




KOCHA Mkuu wa Simba, Milovan Cirkovic amesema hajutii kuwakosa beki Juma Nyoso na mshambuliaji Haruna Moshi 'Boban', ambao wamesimamishwa na uongozi kwa muda usiojulikana.
Kocha huyo kutoka Serbia ameelezea msimamo wake huo siku moja baada ya uongozi wa Simba kutangaza kuwasimamisha wachezaji hao kwa makosa ya utovu wa nidhamu.
Milovan alisema wachezaji hao wanastahili adhabu waliyopewa na uongozi kwa vile wamekithiri kwa utovu wa nidhamu na pia ni chanzo cha timu kufanya vibaya katika michuano ya ligi.
Kocha huyo alisema, licha ya wachezaji hao kuwa muhimu kwenye kikosi chake na kusimamishwa kwao ni pengo katika timu, suala la nidhamu ni la muhimu zaidi kuliko mchezaji binafsi.
"Boban na Nyoso ni wachezaji wazuri na wanapokosekana katika timu huwa inapwaya, lakini mambo wanayofanya hayawezi kuvumilika,"alisema.
Hata hivyo, Milovan alisema kikosi chake kinaundwa na wachezaji wengi wazuri, wakiwemo waliopandishwa daraja msimu huu, hivyo anaamini timu itaweza kufanya vizuri bila kuwepo kwao.
"Hata Ulaya wachezaji nyota wanapokosa nidhamu, husimamishwa lakini, wapo wengine ambao huchukua nafasi zao na timu ikafanya vizuri, hivyo kusimamishwa kwao kwa utovu wa nidhamu hata mimi naafiki," alisema Cirkovic.
Alisema kwa sasa, timu yake inaendelea na mazoezi ya kujiwinda na mchezo wao wa ligi kuu dhidi ya Azam utakaofanyika keshokutwa katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Mapema jana, Simba kupitia kwa ofisa wake wa habari, Ezekiel Kamwaga ilitangaza jana kuwa, imemsimamisha Boban kuichezea timu ya wakubwa kutokana na vitendo vyake vya utovu wa nidhamu na pia kutokuwa na heshima kwa mwajiri wake.
Kamwaga alisema uongozi umempa Boban siku 21 kutoa maelezo kuhusu makosa yake na iwapo atashindwa kufanya hivyo, klabu inaweza kumchukulia hatua kali zaidi za kinidhamu.
Ofisa huyo alisema, katika kipindi hicho cha siku 21, Boban atalipwa nusu ya mshahara wake wa kila mwezi na hatapata marupurupu yoyote yanayohusiana na timu ya wakubwa.
Akimzungumzia Nyoso, ofisa huyo alisema uongozi umemwagiza afanye mazoezi na kikosi cha timu ya pili ya Simba B hadi hapo atakapoimarisha kiwango chake cha uchezaji.
Alisema hatua hiyo imetokana na ripoti ya benchi la ufundi kuonyesha kuwa, mchezaji huyo amekuwa akifanya makosa mengi uwanjani yanayoigharimu timu, na ingawa amekuwa akipewa maelekezo na walimu, bado amekuwa akiyarudia mara kwa mara.
Kamwaga alisema, kutokana na kosa hilo, Nyoso atafanya mazoezi na wachezaji wa kikosi cha pili hadi walimu watakaporidhika kwamba amejirekebisha na yuko tayari kukitumikia kikosi cha wakubwa.
Aliongeza kuwa, katika muda wote huo atakaokuwa akifanya mazoezi na timu B, Nyoso atakuwa akipata mshahara wake wa kila mwezi kama kawaida na pia atapata marupurupu wanayopata wachezaji wa timu hiyo.

BOBAN, NYOSO WASIMAMISHWA SIMBA



SIMBA SPORTS CLUB
P.O.BOX 15318
TEL+255 222183330
FAX +255 222183330
MSIMBAZI/MCHIKICHI STREET
DAR ES SALAAM
TANZANIA
EMAIL simbasportsclub@yahoo.com
WEBSITE www.simba.co.tz
AFFILIATED TO TFF, DRFA and IDFA
24/10/2012
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
KLABU ya soka ya Simba inapenda kutoa taarifa zifuatazo kwenu siku ya leo.
1. Kuhusu Boban na Nyoso
Wachezaji wawili wa Simba, Haruna Moshi Shaaban (Boban) na Juma Said Halfan (Nyoso), wamesimamishwa kuitumikia timu ya wakubwa (senior) kwa sababu na nyakati tofauti.
Moshi amesimamishwa kuichezea timu ya wakubwa kutokana na vitendo vya utovu wa nidhamu na kutokuwa na heshima kwa mwajiri (timu). Klabu imempa Haruna muda wa siku 21 kutoa maelezo kuhusu makosa yake na iwapo atashindwa kutoa maelezo ya kuridhisha, klabu inaweza kumchukulia hatua zaidi.
Katika kipindi hicho (siku 21 kuanzia jana), Boban atapokea nusu ya mshahara wake wa kila mwezi na hatapata marupurupu yoyote yanayohusiana na timu ya wakubwa.
Kwa upande wa Nyoso, uongozi umemwagiza afanye mazoezi na kikosi cha timu ya pili (Simba B) hadi hapo atakapoimarisha kiwango chake cha uchezaji.
Hatua hii imetokana na ripoti ya benchi la ufundi iliyoonyesha kwamba mchezaji huyo amekuwa akifanya makosa mengi ya kiuchezaji yanayoigharimu na ingawa amekuwa akipewa maelekezo na walimu, bado amekuwa akirudia makosa yaleyale.
Kutokana na hilo, Nyoso atafanya mazoezi na wachezaji wa kikosi cha pili hadi walimu watakaporidhika kwamba amejirekebisha na yuko tayari kutumikia kikosi cha wakubwa.
Katika muda wake wote huo akifanya mazoezi na timu B, Nyoso atakuwa akipata mshahara wake wa kila mwezi kama kawaida na pia atapata marupurupu wanayopata wachezaji wa Simba B.

Emmanuel Okwi
Klabu ya Simba inaeleza kusikitishwa kwake na taarifa za vyombo vya habari vyenye lengo la kuuza magazeti pasipo kujali athari za habari zenyewe.
Kwa mfano, habari ya kwenye gazeti la CHAMPIONI la leo ina kichwa cha habari KATIBU MKUU AMFUKUZA OKWI SIMBA. Hata hivyo, kilichoandikwa ndani ya habari yenyewe kinamnukuu aliyewahi kuwa Katibu Mkuu kwenye miaka ya nyuma.
Gazeti hilo linafahamu kabisa kwamba Simba ina Katibu Mkuu mmoja tu kwa sasa na anaitwa Evodius Mtawala. Simba haijawahi kuwa na makatibu wakuu wawili kwa wakati mmoja.
CHAMPIONI linafahamu ukweli huu lakini kwa sababu inazozijua lenyewe, imeamua kuandika habari hiyo na kuweka kichwa cha habari cha namna hiyo pasipo kujali athari zake kwa wanachama wa Simba, Katibu Mkuu aliyepo madarakani kwa sasa na weledi wa fani ya uandishi wa habari
Kilichoandikwa kwenye habari hiyo ya CHAMPIONI ni maoni binafsi ya mwanachama wa Simba na kwa mujibu wa Katiba ya Tanzania, kila mtu ana uhuru wa kutoa maoni yake kuhusiana na jambo lolote ali mradi halivunji sheria za nchi.
Simba SC inarudia wito wake wa kuvitaka vyombo kubaki kwenye misingi ya kitaaluma na kuacha kuandika habari zilizotiwa chumvi na kuleta mitafuruku isiyo na sababu yoyote.

Kikosi
Simba inaendelea vizuri na mazoezi visiwani Zanzibar kujiandaa na mechi dhidi ya Azam itakayopigwa katika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam Jumamosi hii.
Hata hivyo, mchezaji Salim Kinje ameruhusiwa kuondoka kambini Zanzibar leo kutokana na kupata msiba wa baba yake mkubwa uliotokea Dar jana.
Uongozi, kwa namna ya kipekee kabisa, unatoa salamu za pole kwa familia ya Kinje kutokana na msiba huu.

Boniface Wambura
Kwa niaba yangu binafsi na klabu ya Simba, napenda kumpongeza Ofisa Habari wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Boniface Wambura, kwa kuteuliwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) kuwa miongoni mwa wasimamizi wa shirikisho hilo katika michuano ya Wanawake itakayofanyika nchini Guinea ya Ikweta (Equatorial Guinea).
Wambura ndiye Mtanzania pekee aliyeteuliwa na CAF kutumika kwenye michuano hiyo na jambo hilo ni la faraja kwa tasnia ya habari nchini ambako Wambura ametokea.
Imetolewa na
Ezekiel Kamwaga
Ofisa Habari
Simba SC







ABDALLA KIBADENI: WAAMUZI WANATUHARIBIA ULAJI


JINA la Abdalla 'King' Kibadeni si geni masikioni mwa mashabiki wa soka nchini. Ni mmoja wa wachezaji waliong'ara miaka ya 1970 akiwa na kikosi cha Simba na timu ya taifa, Taifa Stars. Kwa sasa Kibadeni ni Kocha Mkuu wa Kagera Sugar ya Bukoba. Katika makala hii ya ana kwa ana iliyoandikwa na ATHANAS KAZIGE  gazeti la Burudani, kocha huyo anazungumzia mambo mbali mbali kuhusu soka.

SWALI: Umekuwa kocha wa Kagera Sugar kwa kipindi kifupi, lakini umeiwezesha kupata mafanikio kwa kuifunga Yanga na kutoka sare na Simba katika mechi za ligi kuu ya Tanzania Bara. Unaweza kutueleza nini siri ya mafanikio yako?
JIBU: Kwanza kabisa napenda kumshukuru Mungu kwa kuniwezesha kufanyakazi yangu kwa mafanikio. Lakini ukweli ni kwamba mafanikio yetu katika ligi yametokana na mambo mengi. Kubwa ni wachezaji kucheza kwa kujituma na kufuata maelekezo ya mwalimu na pia kuwemo kwa umoja miongoni mwa wachezaji na viongozi.
SWALI: Ni tatizo lipi kubwa, ambalo hadi sasa mmekuwa mkikumbana nalo mara kwa mara katika michuano ya ligi kuu?
JIBU: Tatizo kubwa ni uamuzi mbovu. Kusema kweli uamuzi katika mechi za ligi kuu ya Tanzania Bara naweza kusema unatia kinyaa. Waamuzi wengi wamekuwa wakitoa maamuzi mabovu, iwe kwa makusudi kwa lengo la kuzibeba baadhi ya timu ama kutofahamu vyema sheria 17 za soka.
Japokuwa TFF (Shirikisho la Soka Tanzania) limeweka waangalizi katika mechi zote za ligi, sidhani kama hilo litasaidia kitu. Na kama waangalizi hao wataweza kufanyakazi yao kwa umakini, nina hakika waamuzi wengi watafungiwa kwa vile wamekuwa wakifanya vitendo vingi vya ajabu.
Kila kukicha, makocha wengi wa timu za ligi kuu wamekuwa wakiwalalamikia waamuzi. Na si kwamba wanalalamika hivyo kwa lengo la kulinda vibarua vyao, huo ndio ukweli wenyewe.
SWALI: Unapenda kutoa mwito gani kwa TFF na waamuzi kuhusu tatizo hilo?
JIBU: Nawaomba wawe makini na kazi yao na waepuke vishawishi vya kuzibeba baadhi ya timu zenye uwezo kipesa. Wakifanya hivyo si tu kwamba wanazididimiza timu zisizokuwa na uwezo, bali pia wanautia doa mchezo wa soka na kujiharibia wao wenyewe.
Kibaya zaidi, iwapo wataendelea na uchezeshaji wao huo mbovu, ipo siku tutashuhudia mauaji kwenye viwanja vya soka kwa sababu utafika wakati mashabiki watasema tumechoka kuonewa, watachukua sheria mikononi. Litakuwa jambo la hatari sana.
Naishauri TFF ichukue tahadhari mapema kabla ya kutokea matukio ya aina hiyo. Na kama haitakuwa makini, itakuwa ni ndoto kwa Tanzania kutoa waamuzi wa kuchezesha fainali za Afrika ama Kombe la Dunia.
SWALI: Unayaonaje maendeleo ya Kagera Sugar hadi sasa? Kuna uwezekano wowote kwa timu yako kutwaa ubingwa wa ligi ama kushika moja ya nafasi tatu za kwanza?
JIBU: Namshukuru Mungu kwamba timu inaendelea vizuri kwa sababu hatupo kwenye nafasi mbaya katika msimamo wa ligi. Tumeweza kuifunga Yanga nyumbani na kutoka sare na Simba ugenini. Haya ni matokeo mazuri kwetu.
Hadi sasa sina mkataba na Kagera Sugar, nafanyakazi kwa makubaliano maalumu ama naweza kusema bado nipo chini ya uangalizi kwa miezi sita. Iwapo timu itafanya vizuri, huenda uongozi ukanipa mkataba.
Moja ya malengo niliyojiwekea pamoja na wachezaji wangu ni kuhakikisha tunafanya vizuri katika mechi zetu zote za ligi na ikiwezekana tumalize msimu huu tukiwa katika moja ya nafasi tatu za kwanza.
SWALI: Je, umekuwa ukipata ushirikiano mzuri kutoka kwa msaidizi wako, Mrage Kabange na viongozi wa Kagera Sugar?
JIBU: Binafsi namshukuru sana Kabange, ambaye amekuwa akinipa ushirikiano mkubwa tangu nilipojiunga na timu hii. Pia nawashukuru wachezaji wote pamoja na viongozi kwa kunipa ushirikiano na kunifanya niifanye kazi yangu bila matatizo.
SWALI: Una maoni gani kuhusu uchaguzi mkuu ujao wa TFF?
JIBU: Umeniuliza swali zuri sana. Napenda kutumia fursa hii kuiomba kamati ya uchaguzi ya TFF kuwapima wagombea kwa mambo mbali mbali kabla ya kuwapitisha kuwania uongozi wa shirikisho hilo kwa sababu wengi hawana sifa na wamekuwa wakiwania uongozi kwa malengo yao binafsi, badala ya kuendeleza soka.
Na hili lifanyika kuanzia katika ngazi za wilaya na mikoa. Kusikuwepo nafasi ya kuwapitisha wagombea kwa sababu ya uwezo wao kifedha ama umaarufu wao. Wagombea wapitishwe kutokana na elimu zao, hasa za uongozi na uwezo wao.
Pengine ni vyema zingetolewa nafasi kwa watu waliowahi kucheza soka na kufika ngazi za juu kuwania uongozi katika ngazi zote zilizopo. Hawa angalau wanafahamu ABC ya soka kuliko wale, ambao hawajawahi kabisa kucheza mchezo huo.
SWALI: Unadhani tatizo hili la uongozi lipo kwenye vyama vya soka pekee?
JIBU: Hapana, tatizo hili lipo hata katika ngazi za klabu. Hata ukitazama klabu za Simba na Yanga, viongozi wake wengi sio watu wa mpira. Ni watu wanaotafuta umaarufu na kujinufaisha wao binafsi, ndio sababu matatizo katika klabu hizi hayaishi. Kila kukicha ni migogoro.
SWALI: Unatoa ushauri gani kwa serikali kuhusu maendeleo ya michezo nchini?
JIBU: Nawashauri viongozi wa serikali wahakikishe vyama vya kitaifa vya michezo vinatimiza malengo yake na viongozi wake wanaongoza kwa kufuata katiba. Hili litasaidia sana kuepusha migogoro

KUMBE TINO MPELELEZI

MCHEZA filamu machachari wa Tanzania, Hissan Muya 'Tino' ameibuka na movi mpya kali inayokwenda kwa jina la CID.
Akizungumza mjini Dar es Salaam wiki hii, Tino alisema filamu hiyo inahusu mambo ya upepelezi dhidi ya mtandao wa majambazi na wauaji.
Tino alisema filamu hiyo inatarajiwa kuzinduliwa rasmi kesho katika onyesho litakalofanyika kwenye ukumbi wa Business Park, ulioko Mikocheni, Dar es Salaam.
Alisema uzinduzi wa filamu hiyo utapambwa na burudani mbali mbali, zikiwemo muziki wa dansi na kizazi kipya.
Mcheza filamu huyo mwenye mvuto alisema, kwa sasa ameamua kuachana na filamu za mapenzi, badala yake atakuwa akicheza filamu za mapigano.
Alisema uamuzi wake huo umelenga kupiga hatua kubwa zaidi kimaendeleo katika fani hiyo baada ya kubaini kwamba, filamu za mapenzi hazina mvuto mkubwa kwa mashabiki.
Tino, ambaye amecheza filamu zaidi ya 20 alisema, mbali na filamu za mapigano, atakuwa akicheza filamu zenye mwelekeo wa kuielimisha jamii juu ya masuala mbali mbali.
"Kwa sasa watu wengi wamejikita kutengeneza na kucheza filamu za mapenzi na kusuahau mambo mengine muhimu yanayoigusa jamii, hasa ujambazi, magonjwa kama vile ukimwi na mengineyo,"alisema msanii huyo.
Aliitaja sababu nyingine iliyomfanya azitose filamu za mapenzi kuwa, ni baada ya kupata matatizo alipotengeneza filamu ya shoga.
Filamu hiyo ilikuwa ikielezea tabia ya ushoga katika jamii, lakini mamlaka zinazohusika ziliamua kuipiga marufuku kwa madai kwamba, ilikuwa inakiuka maadili ya kitanzania.
Hata hivyo, baada ya filamu hiyo kufanyiwa marekebisho, ilibadilishwa jina na kuitwa Shoga yangu. Tino hakufurahishwa na uamuzi huo kwa madai kuwa, ulipoteza maana halisi ya filamu hiyo.
“Filamu za mapenzi sasa kwangu basi, nataka kugeukia kwenye filamu za mapigano na zile zinazogusa maisha ya binadamu wa kawaida,” alisema Tino.
Tino amewashauri wasanii wengine kutojikita sana katika filamu za mapenzi kwa vile yapo matukio mengi yanayotokea katika jamii, ambayo yanapaswa kuandikiwa filamu.
Katika hatua nyingine, Tino ameanzisha shindano la Bongo Movie Star Search, linalotarajiwa kuanza hivi karibuni.
Tino amesema ameamua kuanzisha shindano hilo kwa lengo la kuibua na kuviendeleza vipaji vya vijana, hasa wanaoishi mikoani.
Alisema wazo la kuanzisha shindano hilo lilitoka kwa marehemu Steven Kanumba na walikuwa wamepanga kulifanyiakazi kwa pamoja kabla ya mauti kumkuta.

GUARDIOLA, CAPELLO WAMMWAGIA SIFA FALCAO


MADRID, Hispania
MSHAMBULIAJI Radomel Falcao wa klabu ya Atletico Madrid ya Hispania yupo njia panda baada ya klabu za Chelsea ya England na Real Madrid kumtolea udenda huku zikipigana vikumbo kuwania saini yake.
Mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Colombia kwa sasa ndiye tegemeo kubwa la Atletico Madrid, ambayo imeshatamka wazi kuwa haina kipingamizi cha kumuuza.
Atletico Madrid imesema itamuuza Falcao wakati wa usajili wa dirisha dogo Januari mwakani, iwapo klabu inayomtaka itakuwa tayari kulipa ada ya uhamisho ya pauni milioni 45.
Kwa upande wake, Falcao (26) ametoa masharti ya kupatiwa mkataba wa miaka minne na mshahara wa pauni milioni tano kwa mwaka baada ya kukatwa kodi.
Chelsea ndiyo inayopewa nafasi kubwa ya kumsajili Mcolombia huyo kutokana na ukweli kwamba, haitakuwa rahisi kwa Falcao kujiunga na Real Madrid, ambao ni wapinzani wakubwa wa Atletico Madrid.
Chelsea imekuwa na uhusiano mzuri na wawakilishi wa Falcao, akiwemo wakala maarufu, Jorge Mendes.
Hata hivyo, Mendes pia ndiye wakala wa Kocha Jose Mourinho wa Real Madrid na baadhi ya wachezaji nyota kama vile Cristiano Ronaldo.
Iwapo Falcao atasajiliwa na Chelsea, huenda ukawa mwisho wa mshambuliaji Fernando Torres, ambaye alisajiliwa na klabu hiyo msimu wa 2011 akitokea Liverpool, lakini ameshindwa kukidhi kiu ya mashabiki wa klabu hiyo.
Masharti mengine yaliyotolewa na Falcao ni kuhakikishiwa namba kwenye kikosi cha kwanza na Chelsea inaonekana wazi kuwa tayari kukidhi sharti hilo.
Chelsea ilimuhakikishia namba Torres kwenye kikosi chake cha kwanza, lakini kutokana na kushindwa kwake kuonyesha makeke yoyote, imeamua kutafuta nyota wengine wenye uzoefu zaidi.
Mbali na Falcao, wachezaji wengine wanaowaniwa na Chelsea kwa ajili ya kuiongezea nguvu ni Andre Schurrle wa klabu ya Bayer Leverkusen ya Ujerumani.
Chelsea ilianza kuvutiwa na Falcao baada ya kuifungia mabao matatu timu hiyo ilipomenyana na Atletico Madrid katika mechi ya fainali ya Kombe la Super iliyopigwa Agosti mwaka huu mjini Monaco, Ufaransa.
Falcao alisajiliwa na Atletico Madrid msimu wa 2011 akitokea Porto ya Ureno. Mcolombia huyo alimwaga wino katika klabu hiyo kwa ada ya uhamisho wa pauni milioni 35.
Kocha wa zamani wa Chelsea, Andre Villas-Boas alitaka kuondoka Porto akiwa na Falcao, lakini mmiliki wa klabu hiyo, Roman Abramovich alimwekea ngumu, akiamini kuwa Torres angeweza kurithi vyema mikoba ya Didier Drogba.
Atletico Madrid imeshatamka wazi kuwa, uamuzi wao wa kumuuza Falcao utaisaidia kutatua tatizo la kifedha, lakini imedokeza kuwa, huenda asiuzwe wakati wa dirisha dogo.
Mbali na Chelsea na Real Madrid, klabu zingine zilizoonyesha nia ya kumsajili Falcao ni matajiri wa Zenit St Petersburg na Anzhi Makhachkala wa Russia, ambao wapo tayari kulipa kitita kikubwa zaidi cha pesa.
Hata hivyo, Falcao imeonyesha nia ya kutaka kubaki Hispania ama kuhamia England na hivyo kutoa mwanya zaidi kwa Chelsea na Real Madrid kumnyakua.
Majina halisi ya mwanasoka huyo ni Radamel Falcao García Zárate. Alizaliwa Februar 10, 1986 katika mji wa Santa Marta nchini Colombia). Falcao pia ni maarufu kwa jina la El Tigre.
Falcao amekuwa akielezewa na wachambuzi wengi wa soka kuwa ni mmoja wa washambuliaji bora duniani kwa sasa, akiwa ameipiku rekodi ya Jurgen Klinsmann wa Ujerumani ya kufunga mabao 15 katika michuano ya ligi ya mabingwa wa Ulaya.
Mcolombia huyo pia alitoa mchango mkubwa kwa Porto ya Ureno ilipotwaa nafasi ya pili katika michuano ya Kombe la UEFA msimu wa 2010-11. Alikuwa mwanasoka bora wa tano duniani katika kura zilizopigwa na waandishi wa habari barani Ulaya.
Msimu huo huo, Falcao alishinda tuzo ya mpira wa dhahabu baada ya kuibuka mfungaji bora katika ligi ya Ureno, akiwa Mcolombia wa kwanza kunyakua tuzo hiyo.
Katika misimu mitatu iliyopita, aliyochezea klabu za Porto na Atletico Madrid, Falcao aliweka rekodi ya kufunga mabao zaidi ya 100. Pia aliiwezesha Real Madrid kuweka rekodi ya kushinda mechi 12 mfululizo za michuano ya ligi ya Ulaya.
Falcao amerithi kipaji cha baba yake, Radamel Garcia, ambaye alikuwa mmoja wa mabeki wa kutumainiwa nchini Colombia
Kocha Mkuu wa zamani wa Barcelona, Pep Cuardiola aliwahi kumwelezea Falcao kuwa ni mchezaji mwenye kipaji cha aina yake duniani na mwenye uwezo wa kufanya chochote uwanjani.
Kocha Fabio Capello pia amekuwa akimwelezea Falcao kuwa ni mchezaji mwenye kiwango sawa na Lionel Messi na Cristiano Ronaldo na pia kumwelezea kama mmoja wa washambuliaji bora duniani kwa sasa.
Alianza kung'ara kisoka akiwa katika klabu ya River Plate ya Argentina kabla ya kuhamia Porto msimu wa 2009-10, ambayo ilimsajili baada ya kumuuza Lisandro Lopez kwa klabu ya Plympic Lyon ya Ufaransa.
Alianza kuichezea timu ya taifa ya Colombia mwaka 2007 akiwa na umri wa miaka 21 na kuifungia bao katika mechi ya michuano ya Kombe la Kirin dhidi ya Montenegro kabla ya kuifungia bao lingine katika mechi dhidi ya Nigeria iliyochezwa mwaka 2008.

DEANGELIS GABRIEL BARBOSA, Mbrazil mwenye






Na Sophia Wakati, Tanga
KLABU ya Coastal Union ya mjini Tanga wiki iliyopita ilimtambulisha rasmi mshambuliaji wake mpya, Deangelis Gabriel Barbosa kutoka Brazil, ambaye anatarajiwa kuichezea katika michuano ya ligi kuu ya Tanzania Bara.
Barbosa (27) aliwasili mjini Tanga akiwa amefuatana na mkewe, Zaira Caroline na binti yao, Lara Barbosa na kupokewa kwa shangwe kubwa na mashabiki wa klabu hiyo yenye maskani yake barabara ya 12.
Kwa kumsajili Barbosa, anayecheza nafasi ya kiungo mkabaji, Coastal Union imeweka historia ya kuwa klabu ya kwanza ya Tanzania kumsajili mchezaji kutoka Brazil.
Barbosa amejiunga na Coastal Union akitokea klabu ya New Road ya Nepal aliyojiunga nayo mwaka 2010.
Kiungo huyo mkabaji pia amewahi kuzichezea klabu za Paham Footbal Club, Flamengo na Santa Cruz za Brazil na Churchill Brothers ya India.
Usajili wa mchezaji huyo umezua maswali mengi kutoka kwa mashabiki wa soka nchini. Wapo wanaohoji iwapo Mbrazil huyo ana kiwango kinachofanana na wachezaji kutoka nchi yake na wengine wanahoji iwapo Coastal Union itaweza kumlipa malipo anayotaka kulingana na mkataba wake.
Akimtambulisha mchezaji huyo kwa waandishi wa habari, Makamu Mwenyekiti wa Coastal Union, Steven Mnguto alisema wamefurahishwa na ujio wake kwa sababu wanaamini atatoa msaada mkubwa kwa timu hiyo.
Mnguto alisema kwa sasa wanashughulikia kibali chake cha kufanyakazi kutoka Idara ya Uhamiaji ili aanze kuichezea timu hiyo katika michuano ya ligi kuu ya Tanzania Bara, inayoendelea kwenye viwanja mbali mbali nchini.
Kwa mujibu wa Mnguto, Mbazil huyo ametia saini mkataba wa kuichezea Coastal Union kwa mwaka mmoja na anatarajiwa kuonekana uwanjani baada ya kupatiwa kibali hicho.
Mnguto alisema tayari mchezaji huyo ameshapata hati ya uhamisho wa kimataifa (ITC) kutoka kwa Chama cha Soka cha Nepal.
"Ujio wa Barbosa umekuja kwa wakati mwafaka kwa sababu tunahitaji sana mchezaji wa aina yake,"alisema.
Hata hivyo, Mnguto alikiri kuwa hawafahamu vyema uwezo wa Barbosa kisoka, lakini kutokana na wasifu wake kutoka kwa wakala aliyemleta nchini, wanaamini kuwa ni mchezaji mwenye uwezo mkubwa.
Akizungumza wakati wa utambulisho huo, Barbosa alisema amefurahi kuja kucheza soka Tanzania na Afrika kwa jumla na kuwataka mashabiki wa Coastal Union watarajie mambo mazuri kutoka kwake.
"Mimi na mke wangu hatukutarajia kupata mapokezo makubwa na mazuri kama haya. Ninachoahidi ni kwamba nitajitahidi kucheza kadri ya uwezo wangu ili kuisaidia timu yangu mpya,"alisema.
Mbrazil huyo alisema atarejesha shukurani zake kwa viongozi na mashabiki wa Coastal Union kwa kukipiga kwa uwezo wake wote ili timu hiyo iweze kufanya vizuri katika ligi kuu.
Hata hivyo, Barbosa alikiri kutoifahamu vyema Tanzania kisoka, lakini alisema hilo haliwezi kumpa matatizo kwa sababu mchezo huo unafanana kote duniani.
Barbosa alisema alianza kucheza soka nchini kwao Brazil katika Jiji la Paulo Alonso na kuitaja klabu yake ya kwanza kuwa ni Paham. Baadaye alijiunga na timu ya vijana ya Flamengo kabla ya kuhamia Santa Cruz zote za Brazil.
Mbrazil huyo alisema baadaye aliamua kwenda India, ambako alijiunga na klabu ya Churchill Brothers kabla ya kutua Nepal, ambako alijiunga na klabu ya New Road.
Kwa mujibu wa mtandao, majina halisi ya mchezaji huyo ni Deangelis Gabriel Galvão Barbosa da Silva. Alizaliwa Agosti 25, 1984. Ana uzito wa kilo 77 na anatumia zaidi mguu wa kulia.

COSSY AFANYA VITUKO SIKU YAKE YA KUZALIWA



LAGOS, Nigeria
MWANADADA Cossy Orjiakor mwishoni mwa wiki iliyopita alifanya kioja cha mwaka baada ya kuwakaribisha wageni aliowaalika kwenye hafla ya siku yake ya kuzaliwa kwa kucheza muziki kwa staili ya aina yake.
Mcheza filamu huyo, ambaye pia ni mwimbaji na mcheza shoo, aliandaa sherehe hiyo nyumbani kwake, nje kidogo ya mji wa Lagos na kuwaalika rafiki zake mbali mbali.
Wakati wageni hao walipoanza kuwasili nyumbani kwake, mwanadada huyo aliyekuwa amevaa nusu uchi, alikuwa akiwakaribisha kwa kucheza dansi kwa staili ya kumwaga lazi.
Baadhi ya wageni hao walionekana kufurahishwa na staili hiyo ya Cossy na kumtaka arudie kucheza mara kwa mara, lakini wengine walione aibu.
Hafla hiyo ilihudhuriwa na wacheza filamu wachache pamoja na waandishi wa habari wa vyombo mbali mbali.
Cossy si mwigizaji maarufu sana nchini Nigeria, lakini ni machachari kutokana na kuandamwa na kashfa mbali mbali kwenye vyombo vya habari.
Mwaka jana, Cossy aliamua kutengana na mpenzi wake baada ya kushindwa kumnunulia gari aina ya Range Rover Sport Jeep wakati wa sherehe yake ya kuzaliwa.
Baada ya kutengana na mpenzi wake huyo, Cossy aliamua kujitosa kimapenzi kwa mwanasoka, Abumere Ededuan.
Baadhi ya mashuhuda wameueleza mtandao wa nigeriafilms kwamba, Cossy na Abumere, ambaye kwa sasa ni wakala wa wachezaji, anayetambuliwa na Shirikisho la Soka la Dunia (FIFA), wamekuwa wakionekana sehemu mbali mbali za starehe pamoja.
Mashuhuda hao wamesema, mapenzi ya Cossy na mchezaji huyo wa zamani wa Nigeria, ni mwanana mithili ya watu waliojitosa kwa mara ya kwanza katika ulimwengu huo.

OMOTOLA: NOLLYWOOD SASA NI TISHIO KWA HOLLYWOOD




Achengua mashabiki katika uzinduzi wa filamu yake mpya ya Amina LONDON, Uingereza
MCHEZA filamu nyota wa kike wa Nigeria, Omotola Jalade amesema fani hiyo inaweza kupiga hatua kubwa zaidi kimaendeleo kuliko Marekani.
Omotola alisema hayo mwishoni mwa wiki iliyopita alipokuwa akihojiwa katika kipindi cha Focus on Africa kilichorushwa hewani na kituo cha televisheni cha BBC.
Mwanadada huyo mwenye sura na umbo lenye mvuto alisema, kwa sasa Wanigeria (Nollywood) wamepiga hatua kubwa katika fani ya filamu na wanakaribia kuwapiku Wamarekani (Hollywood).
Alisema hilo linatokana na kiwango cha filamu za Kinigeria kuwa juu na kukubalika na mashabiki wengi katika sehemu mbali mbali duniani.
Omotola alisema kwa sasa, filamu za Kinigeria zinaweza kuingia kwenye ushindani na zile za Hollywood.
Mwanadada huyo, ambaye ni mama wa watoto wanne, aliwekuwepo mjini London kwa ajili ya uzinduzi wa filamu yake mpya, inayojulikana kwa jina la Amina.
Uzinduzi wa filamu hiyo ulihudhuriwa na wasanii mbali mbali wa fani hiyo kutoka barani Afrika na Ulaya na kuwa na mvuto wa aina yake.
Mara baada ya kuteremka kwenye gari karibu na eneo la uzinduzi, Omotola alitembea kwenye zulia jekundu hadi ukumbini, ambako filamu hiyo ilionyeshwa kwa wageni mbali mbali.
Omotola alikuwa kivutio kikubwa kwa wageni hao kutokana na kuvalia gauni lenye thamani kubwa, lililonakshiwa kwa vitu mbali mbali vya kumeremeta na kumfanya aonekane kama vile malkia.
Baadhi ya mapaparazi waliohudhuria uzinduzi huo walikuwa wakihaha kupata picha za mwanadada huyo, ambaye hakuwa na hiyana zaidi ya kuwapa pozi za aina mbali mbali.
Omotola amecheza filamu hiyo akiwa mwigizaji mkuu. Filamu hiyo imemwezesha kushinda tuzo ya BEFFTA.

Tuesday, October 23, 2012

WAMBURA AULA CAF



Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linapenda kuwataarifu kuwa Ofisa Habari wake, Boniface Wambura ameteuliwa na SZhirikisho la Mpira wa Miguu la Afrika (CAF) kuwa mmoja wa maofisa watakaoshughulikia masuala ya habari wakati wa fainali za Mataifa ya Afrika kwa Wanawake zitakazofanyika nchini Equatorial Guinea.
Uteuzi huo umefanywa na Rais wa CAF, Issa Hayatou kwa ajili ya kufanikisha uendeshaji wa fainali hizo za Mataifa ya Afrika kwa Wanawake zilizopangwa kuanza Oktoba 28, 2012 na kumalizika Novemba 11, 2012.
Wambura atakuwa mmoja wa maofisa watatu watakaoshughulikia habari kwenye fainali hizo. Wengine ni ofisa kutoka makao makuu ya CAF, Mahmoud Garga na Arlindo Macedo kutoka Angola.
Wambura atakuwa ni Mtanzania pekee kwenye Kamati ya Maandalizi ya fainali hizo, kitu ambacho TFF inajivunia kutoa mwakilishi kwenye moja ya mashindanoi makubwa ya mpira wa miguu Tanzania.
Rais wa TFF, Leodegar Tenga ameelezea uteuzi huyo kuwa ni matokeo ya kazi nzuri ambayo Wambura amekuwa akiifanya tangu ajiunge na Shirikisho Januari mwaka 2011.
“Taarifa zake mbalimbali zimeifanya Tanzania iwe inang’ara CAF na hata FIFA kwa kuwa kwa sasa wanajua kila kinachoendelea kwenye soka la Tanzania,” alisema Rais Tenga na kumtakia Wambura kila la kheri kwenye kazi hiyo atakayoifanya kwa takriban siku 14.
Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah, akizungumza kwa niaba ya Sekretarieti, amemtakia Wambura kazi njema na kwamba awe kioo cha mabadiliko makubwa yanayoendelea kwenye soka la Tanzania.
Wambura alijiunga na TFF Januari, 2011 akiwa mmoja wa waajiriwa watatu wapya kwenye Shirikisho baada ya wsatendajiu wengine wawili kumaliza muda wao wa mikataba.
Wambura ni mwandishi wa habari mwandamizi ambaye ameshafanya kazi kwenye vyombo mbalimbali kuanzia kazi ya uandishi hadi Mhariri Mtendaji wa gazeti la Jambo Leo ambalo alikuwa akifanya kazi kabla ya kujiunga na TFF

AZAM KUTWAA UONGOZI WA LIGI KUU KESHO?



Michuano ya Ligi Kuu ya Vodacom kuwania ubingwa wa Tanzania Bara inaendelea kesho (Oktoba 24 mwaka huu) kwa mechi nne za raundi ya tisa huku Azam ikiusaka usukani wa ligi hiyo ikiwa mwenyeji wa Ruvu Shooting.
Mechi hiyo namba 60 ambayo kama Azam itashinda itafikisha pointi 20, hivyo kuwa kileleni mwa Ligi Kuu ya Vodacom itachezwa Uwanja wa Chamazi, Dar es Salaam. Viingilio katika mechi hiyo ni sh. 3,000 kwa sh. 10,000.
Yanga itawakaribisha Polisi Morogoro ambao ndiyo wa mwisho kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya Vodacom hivi sasa katika mchezo utakaofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kwa kiingilio cha sh. 5,000, sh. 8,000, sh. 15,000 na sh. 20,000.
Alex Mahagi kutoka Mwanza ndiye atakayepuliza filimbi kwenye mechi hiyo namba 62. Waamuzi wasaidizi ni Frank Komba na Michael Mkongwa, wote kutoka Iringa wakati mwamuzi msaidizi ni Oden Mbaga anayetambuliwa na Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) wa Dar es Salaam.
Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga utakuwa mwenyeji wa mechi kati ya African Lyon ya Dar es Salaam ambao ni wageni wa Coastal Union inayonolewa na Hemed Moroco. Nayo Mtibwa Sugar itaikaribisha Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Manungu ulioko kwenye mashamba ya miwa Turiani mkoani Morogoro.
MTIBWA SUGAR, JKT RUVU SASA KUCHEZA NOV 7
Mechi namba 79 ya Ligi Kuu ya Vodacom kati ya Mtibwa Sugar na JKT Ruvu iliyopangwa kuchezwa Novemba 3 mwaka huu Uwanja wa Manungu mkoani Morogoro, sasa itafanyika Novemba 7 mwaka huu.
Mabadiliko hayo yamefanyika kwa vile Novemba 4 mwaka huu, Mtibwa Sugar itacheza mechi namba 30 dhidi ya Simba kwenye Uwanja wa Jamhuri, mjini Morogoro. Mechi hiyo awali ilikuwa ichezwe Oktoba 3 mwaka huu lakini ikabadilishwa ili kutoa fursa kwa mechi za Super Week zilizooneshwa moja kwa moja na kituo cha televisheni cha Super Sport cha Afrika Kusini.
VITAMBULISHO FAINALI ZA AFCON 2013 MWISHO NOV 7
Waandishi wa Habari wanaotaka kuripoti fainali za mataifa ya Afrika (AFCON) zitakazofanyika mwakani nchini Afrika Kusini wanatakiwa kutuma maombi ya kupatiwa vitambulisho (Accreditation) kabla ya Novemba 7 mwaka huu.
Maombi hayo yatumwe Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) kupitia CAF Medial Channel inayopatikana katika mtandao wa Shirikisho hilo wa www.cafonline.com

SIMBA, MGAMBO JKT ZAINGIZA MIL 33/-



MCHEZO baina ya Simba Sports Club ya Jijini Dar es salaam na Mgambo Shooting uliofanyika katika uwanja wa Mkwakwani mjini Tanga umeingiza mapato ya jumla ya sh 33,303,000 kupitia viingilio vya watazamaji 5260 walioushuhudia mechi hiyo.
Meneja wa Uwanja wa Mkwakwani,Mbwana Msumari alitoa taarifa hiyo jana alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na mapato yaliyopatikana katika mchezo huo ambao matokeo yalikuwa sare ya kutofungana.
Alitoa mchanganuo kwa kusema kuwa, idadi ya watazamaji walioingia na kukaa katika jukwaa kuu ni 811 waliokata tiketi za sh 10,000 kwa kila mmoja zikakusanywa sh 8,110,000 huku jukwaa lijulikanalo kwa jina la Old Tanga ambalo ni maarufu kwa kukaliwa na mashabiki wa timu ya Coastal Union walikaa watazamaji 1474 waliolipa kiingilio cha sh. 7,000 kila mmoja na kupatikana sh 10,314,000.
Msumari alisema idadi ya watazamaji walioingia uwanjani hapo na kukaa Jukwaa maarufu kwa jina la Russia ilifikia 2975 waliolipa kiingilio cha sh 5,000 kwa kila mmoja zikapatikana jumla ya sh 14,875,000.
Alisema kupitia mapato hayo Simba na Mgambo Shooting kila moja ilipata kiasi cha sh 7,002,409.50 na shirikisho la soka nchini TFF liliweka kibindoni sh 1,068,164.16 huku mmiliki wa uwanja wa Mkwakwani ambaye ni chama cha Mapinduzi CCM ikipewa sh 3,560,547.20.
Kwa mapato hayo,Meneja huyo alisema imeonyesha kwamba timu ya Mgambo Shooting imekubalika na kufanikiwa kupata wapenzi wengi kutoka eneo lote la Mkoa wa Tanga.

LIGI DARAJA LA KWANZA KUANZA KESHO



Michuano ya Ligi Daraja la Kwanza (FDL) inaanza kutimua vumbi kesho (Oktoba 24 mwaka huu) kwenye viwanja mbalimbali nchini.
Kundi A kutakuwa na mechi tatu ambapo Burkina Faso itacheza na Mbeya City kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro wakati JKT Mlale itakuwa mwenyeji wa Small Kids kwenye Uwanja wa Majimaji, Songea.
Nayo Kurugenzi itaumana na Majimaji katika Uwanja wa Wambi ulioko Mufindi mkoani Iringa. Kundi hilo litamaliza raundi ya kwanza keshokutwa (Oktoba 25 mwaka huu) kwa mchezo kati ya Mkamba Rangers na Polisi Iringa utakaofanyika Uwanja wa Jamhuri, Morogoro.
Mechi za kundi B kwa kesho ni Ndanda dhidi ya Transit Camp katika Uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara na Villa Squad itakipiga na Moro United kwenye Uwanja wa Mabatini mjini Mlandizi. Oktoba 25 mwaka huu ni Green Warriors v Tessema (Mabatini, Mlandizi) na Polisi Dar v Ashanti United (Uwanja wa Chamazi).
Kundi C kesho (Oktoba 24 mwaka huu) ni Kanembwa FC v Polisi Dodoma (Uwanja wa Lake Tanganyika, Kigoma), Mwadui v Morani (Kambarage, Shinyanga), Pamba vs Polisi Mara (Kirumba, Mwanza) na Rhino Rangers vs Polisi Tabora (Ali Hassan Mwinyi, Tabora).

HASSANALI KUIWAKILISHA TANZANIA MAONYESHO YA MAVAZI AFRIKA KUSINI


Mbunifu maarufu wa mavazi kutoka Tanzania, Mustafa Hassanali ndiye Mtanzania pekee katika fani ya mitindo aliyepewa mualiko wa kushiriki katika maonyesho ya Wiki ya Mitindo Afrika chini ya African Fashion International (AFI) yatakayofanyika kwa siku nne kuanzia tarehe 24-28 Oktoba, 2012 katika ukumbi wa Melrose Arch, jijini Johannesburg, Afrika ya Kusini.
Mashindano hayo yanayodhaminiwa na kampuni ya kutengeneza Magari ya Mercedes-Benz yanatarajiwa kuwashirikisha wabunifu wa mavazi zaidi ya 35 kutoka sehemu mbalimbali barani Afrika, baadhi ya nchi hizo ni wenyeji Afrika ya Kusini, Ivory Coast, Morocco, Msumbiji, Cameroon, Rwanda, Angola, DRC, Nigeria, Ghana na Tanzania.
“Ni maonyesho ya pekee na yenye heshima yake barani Afrika na hata duniani kwa ujumla kwani wabunifu walioalikwa ni wazoefu na bora katika fani ya Mitindo barani Afrika. Hivyo mwaliko wangu si tu utaweza kutangaza kazi ni nazofanya bali pia utasaidia kutangaza nchi yetu ya Tanzania kupitia maonyesho haya” Alisema, Mustafa Hassanali.
“Watakapotaja jina langu pale katika maonyesho, hawatasema tu huyu ni Mustafa Hassanali, bali watasema huyu ni Mustafa Hassanali kutoka Tanzania, hivyo itakuwa ni mchango mkubwa kwa nchi yetu kuweza kuonyesha fursa zilizopo kupitia Ubunifu wa Mitindo. Nimejiandaa vizuri katika haya maonyesho, nataka kuonyesha nini Tanzania tunacho katika tasnia ya ubunifu kwa ulimwengu mzima ni imani yangu kufanya vizuri” aliongeza Hassanali.
AFI inaandaa mashindano haya ili kuweza kutangaza kazi za wabunifu wa mavazi kutoka barani Afrika katika soko la dunia kwani Afrika ina wabunifu wazuri na imara hivyo kujitokeza kwao katika maonyesho haya kutafungua milango zaidi katika soko la kimataifa na kuongeza fursa nyingi zitakazoinua uchumi wa bara hili kupitia sanaa ya ubunifu wa mitindo.
Licha ya kushiriki katika maonyesha haya, Mustafa Hassanali pia anawaomba Watanzania wote kwa ujumla kuweza kumpigia kura ya kuwa mwanamitindo bora barani Afrika kupitia tovuti ya www.awardnomination.afi.za.com na kuweza kuiletea sifa tasnia ya mitindo nchini Tanzania.
Huu ni mwaka wa tisa kwa Mustafa Hassanali kupata mwaliko wa kuonyesha ubunifu wake katika maonyesho haya. Ameshashiriki katika maonyesho zaidi ya nchi 16 katika miji 25 tofauti duniani, amekuwepo katika kilinge cha sanaa ya mitindo kwa muda mrefu hapa nchini, amechangia kwa kiasi kikubwa mabadiliko na maendeleo ya kazi za ubunifu wa mavazi hapa Tanzania.

Sunday, October 21, 2012

SIMBA KUNANI? YATOKA SARE TENA NA MGAMBO JKT

MABINGWA watetezi wa ligi kuu ya Tanzania Bara, Simba leo wameendelea kuchemsha baada ya kulazimishwa kutoka suluhu na Mgambo JKT katika mechi iliyochezwa kwenye Uwanja wa Mkwakwani mjini Tanga.
Licha ya kulazimishwa sare, Simba bado inaendelea kuongoza ligi hiyo kwa kuwa na pointi 19 baada ya kucheza mechi tisa, lakini inaweza kuenguliwa kileleni na Azam, iwapo itashinda mechi yake dhidi ya Ruvu Shooting Jumatano ijayo kwenye uwanja wa Chamazi, Dar es Salaam.
Katika mechi nyingine ya ligi hiyo iliyochezwa leo, JKT Ruvu ilitoka sare ya bao 1-1 na ndugu zao wa JKT Oljoro katika mechi iliyochezwa kwenye uwanja wa Chamazi wakati Prisons iliichapa Toto African bao 1-0 kwenye Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya.

SERENGETI BOYS YAINGIA KAMBINI



KIKOSI cha wachezaji 25 wa timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 17, Serengeti Boys kimeingia kambini leo mjini Dar es Salaam kujiandaa kwa mechi ya raundi ya mwisho ya michuano ya Afrika kwa vijana.
Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Boniface Wambura amesema leo kuwa, Serengeti Boys ambayo iko chini ya Kocha Mdenmark, Jakob Michelsen, itacheza mechi hiyo ya raundi ya tatu na mshindi kati ya Congo Brazzaville na Zimbabwe ambapo tayari Congo Brazzaville imefanikiwa kupata ushindi wa ugenini wa mabao 2-1. Mechi ya marudiano itachezwa jijini Brazzaville kati ya Oktoba 26-28 mwaka huu.
Katika mechi hiyo ya raundi ya tatu, Serengeti Boys itaanzia nyumbani katika mchezo utakaofanyika Novemba 17, mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, wakati mechi ya marudiano itachezwa wiki mbili baadaye.
Wambura amesema TFF ipo katika mikakati ya kuhakikisha Serengeti Boys inapata mechi mbili za kirafiki za kimataifa kabla ya kumvaa mshindi kati ya Congo Brazzaville na Zimbabwe. Fainali za Afrika kwa vijana wenye umri chini ya miaka 17 zitafanyika Machi mwakani nchini Morocco.
Tanzania imefuzu bila jasho hadi kufika hatua hiyo, baada ya wapinzani wake wa awali, Kenya na Misri kujitoa katika Raundi ya Kwanza na ya Pili.Kama Tanzania itafuzu kushiriki Fainali hizo za mwakani, itapoza machungu ya mwaka 2005 walipofuzu kucheza Fainali za Vijana wa umri huo kwa kuzitoa Rwanda, Zambia na Zimbabwe, lakini baadaye kwa sababu ya ‘kufoji’ umri wa Nurdin Bakari, ikaondolewa mashindanoni.
Zaidi ya Fainali za Mataifa ya Afrika 1980 na CHAN 2009, katika soka ya wanaume, Tanzania haijashiriki fainali nyingine zozote za Afrika tangu iingie kwenye soka ya kimataifa.

YANGA, RUVU SHOOTING ZAINGIZA MIL 47/-



MECHI ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, kati ya Yanga na Ruvu Shooting iliyochezwa jana kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na kumalizika kwa wenyeji Yanga kushinda mabao 3-2, imeingiza Sh. 47,615,000.
Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Boniface Wambura amesema leo kuwa, watazamaji 8,233 walikata tiketi kushuhudia mechi hiyo iliyochezwa kwa viingilio vya sh. 5,000, sh. 8,000, sh. 15,000, na sh. 20,000 huku kila klabu ikipata mgawo wa sh. 8,420,578.47 wakati Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) iliyolipwa ni sh. 7,263,305.08.
Amesema mgawo mwingine wa mapato hayo ni posho ya msimamizi wa kituo sh. 120,000, kamishna wa mechi sh. 203,000, waamuzi sh. 381,000, mwamuzi wa akiba sh. 70,000, usafi na ulinzi wa uwanja sh. 2,350,000 na Wachina (stadium technical support) sh. 2,000,000.
Gharama zingine ni umeme sh. 300,000, maandalizi ya uwanja (pitch preparation) sh. 400,000, ulinzi wa mechi sh. 3,500,000 wakati tiketi ni sh. 2,959,100.
Gharama za mchezo sh. 2,806,859.49, uwanja sh. 2,806,859.49, Kamati ya Ligi sh. 2,806,859.49, Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) sh. 1,684,115.69 na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) sh. 1,122,743.80.
Wakati huo huo, Wambura amesema Kamati ya Ligi ya TFF imeipa onyo kali African Lyon kutokana na washabiki wake kuweka bango lililoandikwa ‘We believe in 0777’ kwenye mechi yake dhidi ya Azam iliyochezwa Oktoba 6, mwaka huu Uwanja wa Chamazi, Dar es Salaam.
Amesema bango hilo ambalo si la mdhamini wa Ligi Kuu ya Vodacom halitakiwi kuonekana tena kwenye mechi ambazo African Lyon inacheza vinginevyo Kamati ya Ligi itachukua hatua kali dhidi ya timu hiyo.
Amesema Kamati ya Ligi imezikumbusha timu zote zinazoshiriki Ligi Kuu ya Vodacom kuzingatia kanuni zinazotawala ligi hiyo ili iweze kuendeshwa kwa ufanisi.


CHEKA SASA KUZIPIGA NA MJERUMANI



Mpambano unaosubiriwa kwa hamu kubwa na wadau wa ngumi nchini Tanzania na Ujerumani kati ya Francis Cheka na Benjamin Simon wa Ujerumani sasa utafanyika tarehe 18 November katika ukumbi wa Universal jijini Berlin nchini Ujerumani.
Awali mpambano huo ulikuwa ufanyike tarehe 17 November jijini Berlin, Ujerumani na tayari bondia Francis Cheka ameshasaini mkataba wa kukutana na mbabe huyo wa Ujerumani anayejulikana kwa jina la “Iron Ben” kwa ajili ya ukali wa makonde yanayowasulubu wapinzania wake.
Bondia Benjamin Simon ana rekodi ya mapambano 24 ambapo amepoteza pambano moja wakati bondia Francis Cheka ana rekodi ya mapambano 33 amepoteza mapambano 6.
Akimwandikia “Eva Rolle” wa kampuni ya “Primetime Event Management” ya Ujerumani ambaye ndiye promoter wa mpambano huo, mwenyekiti wa ubingwa wa IBF/USBA Lindsey Tucker alimfahamisha kuwa Rais wa IBF/USBA Daryl Peoples au yeye mwenyewe Lindsey Tucker watawasiliana na mama huyo kuhusu maofisa watakaosimamia mpambano huo.
Hii itakuwa mara ya kwanza kwa wababe hao kukutana kugombea mkanda wa IBF wa mabara (IBF I/C) na mpambano wao unategemnea kutoa ushindani mkubwa.
Mshindi katika mpambano huo ataingia moja kwa moja katika orodha ya mabondia 15 bora kwenye uzito wa Super Middle duniani.
Imetumwa na:
Onesmo Alfred McBride Ngowi
Rais
IBF Africa, Mashariki ya Kati, Ghuba ya Uarabu na Uajemi
(IBF Africa, Middle East, Arabian Gulf and Persian Gulf)

TANZANIA YAPATA MWAKILISHI MISS EAST AFRICA 2012


Mrembo atakaewakilisha Tanzania katika mashindano ya mwaka huu ya Miss East Africa ni Jocelyne Diana Maro (22)

Mrembo huyo alipatikana kufuatia mchakato ulioendeshwa na kamati maalum ya kuratibu zoezi hilo kwa zaidi ya miezi mitatu iliyopita na kuwashinda warembo wengine 148 waliojitokeza kutaka kuiwakilisha Tanzania katika mashindano ya Miss East Africa 2012
Jocelyne amehitimu shahada ya Business Economics mwezi wa saba mwaka huu katika chuo kikuu cha Keele University, Nchini Uingereza
Maandalizi ya mashindano hayo yanaendelea vizuri na yapo kwenye hatua za mwisho ikiwa ni pamoja na kukamilisha taratibu zote za BASATA ili kufanikisha mashindano hayo yatakayofanyika tarehe 07 December, 2012 katika ukumbi wa Mlimani City Jijini Dar es salaam
Mashindano ya Miss East Africa mwaka huu tayari yameanza kuvuta hisia za watu wengi barani Africa kufuatia kiwango cha juu cha warembo wanaowania taji hilo.
Nchi zilizothibitisha kushiriki mashindano hayo ni wenyeji Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi. Nchi zingin000e zilizoalikwa kushiriki ni pamoja na Ethiopia, Eritrea, Somalia, Djibouti, Southern Sudan, Malawi, pamoja na visiwa vya Seychelles, Madagascar, Reunion, Comoros, na Mauritius.
Mashindano ya Miss East Africa yanalenga kukuza ushirikiano na kutangaza utamaduni wa Afrika Mashariki, pamoja na kutangaza utalii wa Tanzania kama Nchi wenyeji wa mashindano hayo makubwa katika ukanda huu wa Afrika
Mashindano ya Miss East Africa yanamilikiwa na kuandaliwa na kampuni ya Rena Events Ltd ya jijini Dar es salaam,.

YANGA YAZIPUMULIA SIMBA NA AZAM




LICHA ya kuwa nyuma kwa mabao 2-0, Yanga jana ilizinduka na kuicharaza Ruvu Shooting mabao 3-2 katika mechi ya ligi kuu ya Tanzania Bara iliyopigwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Ushindi huo umeiwezesha Yanga kufikisha pointi 14 baada ya kucheza mechi nane na hivyo kuchupa hadi nafasi ya tatu katika msimamo wa ligi hiyo, ikiwa nyuma ya Simba na Azam.
Mashabiki wa Yanga walijikuta wakinyong'onyea dakika 10 za mwanzo za pambano hilo baada ya Ruvu Shooting kufunga mabao mawili ya haraka haraka kupitia kwa Seif Abdalla.
Yanga ilihesabu bao la kwanza kupitia kwa beki wake, Mbuyu Twite aliyefunga kwa mpira wa adhabu ya moja kwa moja uliowapita mabeki na kipa Benjamin Haule wa Ruvu Shooting na kujaa wavuni.
Jerry Tegete aliiongezea Yanga bao la pili dakika chache baadaye, akiunganisha wavuni mpira wa krosi uliopigwa na beki Juma Abdul. Timu hizo zilikwenda mapumziko zikiwa sare ya mabao 2-2.
Didier Kavumbagu ndiye aliyeifungia Yanga bao la tatu na la ushindi baada ya kutokea kizaazaa kwenye lango la Ruvu Shooting.
Katika mechi nyingine ya ligi hiyo iliyochezwa jana kwenye Uwanja wa Mkwakwani mjini Tanga, wenyeji Coastal Union waliendelea kujiimarisha nafasi za juu katika msimamo wa ligi hiyo baada ya kuibanjua Mtibwa Sugar mabao 3-1.

Friday, October 19, 2012

SIMBA YATANGAZA KIKOSI CHA KUIANGAMIZA MGAMBO JKT, CHAENDA TANGA LEO


Wachezaji 24 wa timu ya Simba wameondoka leo kwenda mjini Tanga tayari kwa mechi ya keshokutwa dhidi ya Mgambo Shooting katika Uwanja wa Mkwakwani.
Kikosi kamili kilichoondoka ni
MAKIPA
Juma Kaseja Juma, Wilbert Mweta William na Waziri Hamad Mwinyiamani
WALINZI
Nassor Said Masoud (Chollo), Amir Maftah Mrisho, Paulo George Ngalema, Koman Bili Keita, Pascal Ochieng Akullo, Hassan Hatibu Kondo.
VIUNGO
Jonas Mkude Gerrald, Ramadhani Chombo Redondo, Amri Kiemba Athumani, Abdallah Omar Seseme, Ramadhani Singano Yahya, Uhuru Selemani Mwambungu, Mrisho Khalfan Ngassa, Mwinyi Kazimoto Mwetula na Salim Abdallah Kinje.
WASHAMBULIAJI
Abdallah Juma, Daniel Akuffo, Felix Mumba Sunzu, Edward Christopher Shija, Haruna Athumani Chanongo na Emmanuel Arnold Okwi
WALIOBAKI
Haruna Moshi---------------Maumivu ya misuli
Haruna Shamte------------Goti
Kigi Makasi-----------------Goti
Shomari Kapombe---------------Enka
Juma Nyoso---------------- Kadi tatu za njano.

BAKHRESSA APIGWA CHINI DRFA

MAAMUZI KUHUSU RUFAA DHIDI YA MAAMUZI YA KAMATI ZA UCHAGUZI VYAMA VYA MPIRA WA MIGUU MKOA WA MBEYA (MREFA), MKOA WA SHINYANGA (SHIREFA) NA MKOA WA DAR ES SALAAA (DRFA).

19 OKTOBA 2012
1. Kwa mujibu wa Katiba ya TFF Ibara ya 49(1), Kanuni za Uchaguzi za wanachama wa TFF, Ibara ya 10(6), 12(1) na 26(2) na (3), Kamati ya Uchaguzi ya TFF katika vikao vyake vilivyofanyika tarehe 12 na 18 Oktoba 2012 ilijadili michakato ya chaguzi za vyama vya mpira wa miguu vya Mikoa ya Mbeya (MREFA), Shinyanga (SHIREFA) na Dar es Salaam (DRFA) na kutoa maamuzi kama ifuatavyo:
(a) Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Mbeya (MREFA)
(i) Rufaa ya Ndg. Charles Makwaza: Kamati ilijadili rufaa iliyowasilishwa na Ndg. Charles Makwaza dhidi ya Kamati ya Uchaguzi ya MREFA, iliyoomba Kamati ya Uchaguzi ya TFF kubatilisha uamuzi wa Kamati ya Uchaguzi ya MREFA kumpitisha Ndg. John Mwamwaja kugombea nafasi ya Mwenyekiti wa MREFA, kwamba hakutekeleza wajibu wa kikatiba wa kuitisha Mkutano Mkuu wa MREFA kwa muda wa miaka 3.
Baada ya kupitia maelezo ya warufani na warufaniwa, Kamati ya Uchaguzi ya TFF ilijiridhisha kuwa vielelezo na maelezo ya Ndg. Charles Makwaza yaliyowasilishwa mbele ya Kamati kwa kiwango kikubwa hayakuwa ya kweli. Kamati ya Uchaguzi ya TFF imeitupa rufaa hiyo.
(ii) Rufaa ya Ndg. Lusekelo E. Mwanjala: Kamati ilijadili rufaa iliyowasilishwa na Ndg. Lusekelo E. Mwanjala ikipinga maamuzi ya Kamati ya Uchaguzi ya MREFA kuliondoa jina lake kugombea nafasi ya Mwenyekiti wa MREFA, kwa kigezo cha kutokuwa na uzoefu wa uongozi wa mpira wa Miguu.
Kamati ilipitia vielelezo kuhusu rufaa na kujadili maelezo ya Mrufani na Mrufaniwa na ilijiridhisha kuwa Ndg. Mwanjala anakidhi kigezo cha uzoefu. Kamati inakubaliana na rufaa ya mrufaa dhidi ya maamuzi ya Kamati ya Uchaguzi ya MREFA na hivyo imemrejesha Ndg. Mwanjala kugombea nafasi ya Mwenyekiti wa MREFA.
(iii) Rufaa ya Ndg. Thadeo T. Kalua: Kamati ilijadili rufaa iliyowasilishwa mbele yake na Ndg. Kalua ikipinga maamuzi ya Kamati ya Uchaguzi ya MREFA kuliondoa jina lake kugombea nafasi ya Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa TFF, kwa kigezo cha kutokuwa Mkazi wa Mkoa wa Mbeya. Kamati ilipitia vielelezo kuhusu rufaa hii na kubaini kuwa Katiba ya MREFA iliyosajiliwa haina sharti hilo kwa waombaji uongozi. Kamati inakubaliana na maombi ya
(iv) mrufaa na inamrejesha Ndg. Thadeo Kalua kugombea nafasi ya Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa TFF.
(v) Uchaguzi wa MREFA utafanyika Jumamosi, tarehe 27 Oktoba 2012 kama ulivyopangwa.
(b) Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Shinyanga (SHIREFA).
(i) Rufaa ya Ndg. Ibrahim Magoma: Kamati ilijadili rufaa iliyowasilishwa na Ndg. Magoma ikipinga maamuzi ya Kamati ya Uchaguzi ya SHIREFA kuliondoa jina lake kugombea nafasi ya Katibu wa SHIREFA, kwa kigezo cha kuingilia Mchakato wa Uchaguzi kunyume na Kanuni za Uchaguzi za wanachama wa TFF na pia kutozingatia matakwa ya Kanuni hizo katika kujaza fomu za maombi ya uongozi wa SHIREFA.
Kamati ilipitia vielelezo kuhusu rufaa ya Ndg. Magoma na kujadili maelezo ya Mrufani na Mrufaniwa na ilijiridhisha kuwa Ndg. Magoma aliingilia mchakato wa uchaguzi wa SHIREFA kunyume na Kanuni za Uchaguzi za wanachama wa TFF akiwa Katibu Mkuu wa SHIREFA kwa kushiriki kuivunja Kamati ya Uchaguzi ya SHIREFA iliyokuwa ikendelea na mchakato wa uchaguzi wa SHIREFA. Kamati inakubaliana na uamuzi wa Kamati ya Uchaguzi ya SHIREFA wa kumwondoa Ndg. Magoma kugombea nafasi ya Katibu wa SHIREFA. Kamati ya Uchaguzi ya TFF imeitupa rufaa hiyo.
(ii) Uchaguzi wa SHIREFA umesogezwa Mbele kwa siku nne. Uchaguzi huo utafanyika Alhamisi, tarehe 25 Oktoba 2012, mjini Shinyanga.
(c) Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es salaam (DRFA).
Kamati ya Uchaguzi ya TFF ilijadili Mchakato wa Uchaguzi wa DRFA na rufaa dhidi ya maamuzi ya Kamati ya Uchaguzi ya DRFA na kuamua kama ifuatavyo:
(i) Marekebisho na usajili wa Katiba ya DRFA: Hoja ya rufaa iliwasilishwa na Ndg. Michael R. Wambura ilikihoji uhalali wa marekebisho na usajili wa Katiba ya DRFA, kwamba usajili wa Katiba ya DRFA si halali. Kamati ilibaini kuwa marekebisho ya Katiba hiyo yalifanyika kwa kufuata maagizo ya TFF na kwamba DRFA ilizingatia maagizo hayo. Kamati ya Uchaguzi ya TFF iliridhika kuwa Katiba ya DRFA imesajiliwa na Msajili wa vyama na vilabu vya michezo baada ya kuridhiwa na TFF, na hivyo, Kamati iliitupa hoja hiyo ya Mrufani kuhusu uhalali na usajili wa Katiba ya DRFA.
(ii) Kuundwa kwa Kamati ya Uchaguzi ya TFF : Hoja ya rufaa ya Ndg. Michael R. Wambura iliomba Kamati ya Uchaguzi ya TFF kutoa tamko kuwa Kamati ya Uchaguzi ya DRFA imeundwa bila kufuata Kanuni za Uchaguzi Ibara ya 3(2). Kamati iliridhika kuwa Kamati ya Uchaguzi ya DRFA iliteuliwa kabla ya marekebisho ya Kanuni za Uchaguzi za wanachama wa TFF hususan, Ibara ya 3(2), hivyo uteuzi wa wajumbe wa Kamati hiyo haukukiuka Kanuni za Uchaguzi. Kamati iliitupa rufaa hiyo.
(iii) Wapiga kura wa Mkutano Mkuu wa DRFA: Hoja za rufaa za Ndg. Michael R. Wambura na Ndg. Juma Jabir ziliomba kuyaondoa majina ya Ndg. Abeid Mziba, Ndg. Salehe Ndonga, Peter Muhinzi na Ndg. Daudi Kanuti katika orodha ya wapiga kura wa Mkutano Mkuu wa DRFA na uongozi wa wanachama wa DRFA, kwamba hawana sifa kwa mujibu wa Kanuni za Uchaguzi na Katiba za wanachama wa DRFA. Kamati ya Uchaguzi ya TFF haikupata vielelezo kuhusu hoja iliyowasisilishwa mbele ya Kamati na hivyo kuitupa hoja hiyo ya mrufani.
(iv) Rufaa dhidi ya Ndg. Mohamed Salim (Bakhressa) kugombea nafasi ya Mwenyekiti wa DRFA. Rufaa dhidi ya uamuzi wa Kamati ya Uchaguzi ya DRFA wa kumpitisha Ndg. Amin Mohamed Salim (Bakhressa) kugombea nafasi ya Mwenyekiti wa DRFA iliyowasilishwa na Ndg. Michael R. Wambura na Ndg. Juma Jabir iliomba jina la Ndg. Amin Mohamed Salim (Bakhressa) liondolewe katika orodha ya wagombea uongozi wa DRFA kwa nafasi ya Mwenyekiti, kwa kuwa hana elimu ya kiwango cha kidato cha nne na hivyo kutokidhi matakwa ya Katiba ya DRFA Ibara ya 29(2) inayotamka kwamba ‘Mtu yeyote anayegombea nafasi yoyote ya DRFA hana budi awe na kiwango cha elimu kisichopungua kidato cha nne (Academic Certificate of Ordinary Secondary Education).
Kamati ya Uchaguzi ya TFF ilipitia vielelezo kuhusu rufaa dhidi ya maamuzi ya Kamati ya Uchaguzi ya DRFA na kujadili maelezo ya Warufani, Kamati ya Uchaguzi ya DRFA na Ndg. Amin Mohamed Salim na ilijiridhisha kuwa Ndg. Amin Mohamed Salim (Bakhressa) hana elimu ya kiwango cha kidato cha nne na hivyo hakidhi matakwa ya Katiba ya DRFA Ibara 29(2). Kwa kutokidhi matakwa hayo ya katiba ya DRFA, Ndg. Amin Mohamed Salim (Bakhressa) hastahili kugombea nafasi ya Mwenyekiti wa DRFA. Kamati ya Uchaguzi ya TFF inakubaliana na maombi ya Warufaa.
(v) Rufaa kupinga kuenguliwa kugombea Uongozi DRFA: Ndg. Evans Elieza na Ndg. Juma Jabir waliwasilisha rufaa wakiomba Kamati ya Uchaguzi ya TFF kutengua uamuzi wa Kamati ya Uchaguzi ya DRFA wa kuwaengua kugombea uongozi kwa madai ya kugushi sahihi ya Katibu wa Chama cha Mpira wa Miguu Wilaya ya Kinondoni (KIFA). Katika vielelezo mbalimbali vilivyoletwa mbele ya Kamati na baada ya kuwahoji warufani, Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya DRFA, Katibu wa KIFA, Ndg. Seif Ally Mailo aliyeshuhudia maelezo ya fomu za waombaji uongozi DRFA na baadhi ya waombaji uongozi ambao kupitishwa kwao na Kamati ya Uchaguzi ya DRFA kulilalamikiwa, Kamati ilibaini kuwa kulikuwa na ukiukwaji mkubwa wa Kanuni na taratibu za uchaguzi zilizofanywa na Kamati ya Uchaguzi ya DRFA na pia ama KIFA au wagombea wenyewe. Kutokana na mkanganyiko, maelezo yenye utata kutoka kwa warufani na warufaniwa na maamuzi ya utata ya Kamati ya Uchaguzi ya DRFA yameufanya mchakato wa uchaguzi wa DRFA kupoteza hadhi ya uchaguzi unaozingatia Kanuni za Uchaguzi na misingi ya demokrasia na uwazi kama ilivyoainishwa kwenye Kanuni za Uchaguzi za TFF. Kamati ya Uchaguzi ya TFF ilijiridhisha kwamba:
· Kamati ya Uchaguzi ya DRFA iliwapitisha wagombea Ndg. Gungurugwa Tambaza, Ndg. Mohammed Bhinda, Ndg. Benny Kisaka na Ndg. Hamisi Ayoub Mpapai bila kuwa na vielelezo vinavyothibitisha kuwa wana kiwango cha elimu kisichopungua kidato cha nne (Academic Certificate of Ordinary Secondary Education).
· Hoja ya kughushi saini ya Katibu wa KIFA katika kushuhudia maelezo ya baadhi ya wombaji uongozi, ambayo ilitumiwa na Kamati ya Uchaguzi ya DRFA kuwaondoa kugombea uongozi waombaji uongozi watano (5) Ndg. Hamis Ambar, Ndg. Hamisi Kisiwa, Ndg. Andrew Tupa, Ndg. Evans Elieza na Ndg. Juma Jabir haikutumika kuwaondoa baadhi wagombea ingawa fomu za waombaji uongozi saba zilisainiwa na Ndg. Ndg. Seif Ally Mailo.
· Ndg. Seif Ally Mailo ambaye si mwajiriwa na si kiongozi wa KIFA hakuwa na mamlaka ya kushuhudia maelezo ya wagombea kwa mujibu wa Kanuni za Uchaguzi.
· Kulikuwa na hali ya kumficha Ndg. Seif Ally Mailo aliyesaini fomu za wagombea walioenguliwa kwa kigezo cha kughushi saini asifike kwenye kamati ya Uchaguzi ya TFF kutoa maelezo kuhusu ushiriki wake katika mchakato wa uchaguzi wa DRFA.
· Fomu za wagombea Ndg. Said H.Tully na Ndg. Shaffih Dauda zilizojadiliwa na Kamati ya Uchaguzi ya DRFA na hivyo kupitishwa na Kamati hiyo zilichezewa (tempered-with) kwa kunyofolewa baadhi ya kurasa na kuwekwa kurasa zenye maelezo na saini ambazo si za Ndg. Said H.Tully na Ndg. Shaffih Dauda. Wagombea hao ambao walikuwa wamepetishwa na Kamati ya Uchaguzi ya DRFA kwa maelezo kwamba fomu zao zilikuwa zimeshudiwa kwa sahihi halali ya Ndg. Ndg. Seif Ally Mailo walikana kwa maandishi na kutoa vielelezo vilivyothibitisha kwamba fomu zao zilichezewa na maelezo yaliyo kwenye kurasa zilizobadilishwa siyo wao walioyandika na kusaini.
· Kamati ya Uchaguzi ya DRFA iliwaondoa baadhi ya waombaji uongozi kwa maelezo kwamba maelezo kwenye fomu za wagombea hao hayakushuhudiwa na viongozi vyama wanachama wa DRFA wenye mamlaka ya kushuhudia maelezo ya waombaji uongozi lakini bila kuzingatia matakwa hayo ya kikanuni ikawapitisha kugombea Ndg. Muhsin S. Balhabou na Ndg. Benny Kisaka ambao maelezo ya kwenye fomu zao hayakushuhudiwa na kiongozi wa chama mwanachama yeyote wa DRFA.
· Kamati ya Uchaguzi ya DRFA inahusika kwa kiwango kikubwa katika ukiukwaji wa Kanuni na taratibu za uchaguzi na kutozingatia matakwa ya Katiba ya DRFA katika mchakato wa uchaguzi wa viongozi wa DRFA.
Kamati ya Uchaguzi ya TFF kwa kuzingatia Katiba ya TFF Ibara ya 49(1), Kanuni za Uchaguzi za wanachama wa TFF Ibara ya 10(6), 12(1) na 26(2) na (3):
(i) Imeifuta Kamati ya Uchaguzi ya DRFA. DRFA inaagizwa kuteuwa Kamati mpya ya Uchaguzi itakayoandaa na kutekeleza majukumu yake ikizingatia Kanuni za Uchaguzi za wanachama wa TFF na Katiba ya DRFA. Uteuzi wa Kamati mpya ya Uchaguzi ya DRFA ufanyike kabla ya tarehe 25 Oktoba 2012
(ii) Imefuta mchakato wa Uchaguzi wa DRFA. Mchakato wa uchaguzi utaanza upya tarehe 29 Oktoba 2012 na uchaguzi utafanyika tarehe 08 Desemba 2012. Wagombea wote waliokuwa wamelipia Fomu za maombi ya uongozi (Fomu Na. 1) wanaokidhi sifa za kugombea uongozi kwa mujibu wa Katiba ya DRFA na Kanuni za Uchaguzi za wanachama wa TFF wajaze upya Fomu Na.1 bila kutozwa ada kwa nafasi zinazoendana na zile walizokuwa wameomba kugombea.
Deogratias Lyatto
MWENYEKITI KAMATI YA UCHAGUZI TFF