WIMBI la wizi wa kazi za sanaa limezidi kushika kasi baada ya baadhi ya wafanyabiashara kuiingiza mjini bendi ya muziki wa dansi ya Mlimani Park Orchestra 'Sikinde' kwa kutengeneza DVD yenye albamu tatu za bendi hiyo.
DVD hiyo yenye nyimbo 20, ilianza kuuzwa wiki mbili zilizopita katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam huku viongozi wa bendi hiyo wakiwa hawana taarifa.
Uchunguzi uliofanywa na Burudani umebaini kuwa, DVD hiyo ni feki kwa vile haina nembo ya hakimiliki na ile ya Mamlaka ya Kodi ya Mapato (TRA), ambayo imepewa jukumu la kusimamia mauzo ya kazi za wasanii.
Nyimbo zilizomo kwenye DVD hiyo, ambayo gazeti hili linayo nakala yake, ni za tangu miaka ya 2000 wakati bendi hiyo ilipokuwa chini ya uongozi wa Bennovilla Anthony na Shabani Dede, ambao kwa sasa hawapo.
Wanamuziki wengine wa zamani wanaoonekana kwenye DVD hiyo ni pamoja na marehemu Tino Masinge, marehemu Charles John 'Ngosha' na marehemu Machaku Salum.
Kava la DVD hiyo limeandikwa East African Music- DDC Mlimani Park-Three Album na picha kubwa zinazoipamba ni ya wanamuziki Hassan Bitchuka na Abdalla Hemba. Picha ndogo ni za Dede na Hassan Kunyata wakiwa wamevaa fulana zenye nembo ya Konyagi.
Kinachodhihirisha kwamba toleo hilo ni la 'kufoji' ni kukosewa kwa majina ya baadhi ya nyimbo na wanamuziki. Kwa mfano, wimbo wa Huruma kwa wagonjwa, umeandikwa Huruma kwa wagonwa.
Jina la mwanamuziki Karama Regesu, ambaye ni mtunzi wa wimbo wa Supu Umeitia nazi, nalo limekosewa kwa kuandikwa Karama Resegu wakati jina la Bitchuka katika baadhi ya nyimbo limeandikwa Bitchika.
Nyuma ya DVD hiyo zinaonekana picha ndogo za Hussein Jumbe, Bennovilla, Bitchuka na Ramadhani Kinguti 'System' wakiwa wamevaa sare za zamani za bendi hiyo.
Nyimbo zilizomo kwenye albamu ya Huruma kwa wagonjwa kwenye DVD hiyo ni Teddy Mwana Zanzibar, Furaha, Mkataa pema (Bitchuka), Binamu na Amina (Dede).
Albamu ya Supu umeitia nazi inaundwa na nyimbo za King Fish, Fitina, Full Squad na Ni nani (Bitchuka), Heshima, Njiwa Manga (Hemba) na Upendo (Ramadhani Mapesa).
Nyimbo zilizomo kwenye albamu ya Maneno Maneno ni Tende Haluwa, Fumanizi (Dede), Kelele za Paka (Bitchuka), Mshenga (Ally Jamwaka) na SACCOS uliotungwa kwa pamoja na wanamuziki wote wa bendi hiyo.
Nyimbo nyingi zilizomo kwenye albamu hiyo zilirekodiwa chini ya usimamizi wa Kampuni ya GMC Wasanii Promoters yenye makao makuu yake mjini Dar es Salaam.
Alipoulizwa kuhusu uhalali wa DVD hiyo, Katibu wa Mlimani Park Orchestra, Hamisi Milambo, alisema wamepata taarifa hizo na wameshaanza kuzifanyia kazi.
Milambo alisema walifika katika moja ya maduka yanayouza DVD hizo kwa jumla, lililoko mtaa wa Magila, Kariakoo, Dar es Salaam na kuzikuta zikiuzwa bila idhini ya uongozi.
"Tumeshangazwa sana na mmiliki wa duka hilo kwa sababu hatuna mkataba naye wowote. Tutakachokifanya ni kuwasilisha malalamiko yetu katika Chama cha Hakimiliki Tanzania (COSOTA) ili achukuliwe hatua za kisheria,"alisema Milambo bila kutaja jina la mmiliki huyo.
Aliongeza kuwa, kisheria bendi ya Mlimani Park ndiyo yenye hakimiliki ya kazi zake zote, hivyo hairuhusiwi kwa mtu mwingine kutumia kazi hizo bila idhini ya uongozi.
Hata hivyo, mmoja wa wanamuziki waandamizi wa bendi hiyo, ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini, aliutupia lawama uongozi kwa kushindwa kusimamia kazi zao.
"Mimi moja kwa moja nautupia lawama uongozi kwa sababu kila tunapokamilisha kurekodi nyimbo mpya, huwa tunawaambia tutengeneze albamu, lakini hawafanyi hivyo. Matokeo yake wajanja wachache wanazikusanya na kutengeneza albamu kinyemela,"alisema.
Kwa mujibu wa mwanamuziki huyo, bendi hiyo imekuwa ikishindwa kuendesha vyema mambo yake kutokana na kukosekana kwa meneja wa bendi na uongozi uliopo madarakani hautaki kuajiri mtu mwenye sifa hiyo.
"Sikinde ni kama vile inaendeshwa bora liende. Tunaingia gharama kubwa kurekodi nyimbo zetu studio, lakini mwisho wa siku nyimbo zinaibwa na kuuzwa bila bendi kunufaika,"alisema.
Aliongeza kuwa, kwa mara ya mwisho waliingia mkataba wa kurekodi video zao kupitia Kampuni ya GMC wakati bendi ilipokuwa chini ya Shirika la Uchumi mkoa wa Dar es Salaam (DDC) na ndiyo iliyosimamia mauzo ya albamu yao ya mwisho, inayojulikana kwa jina la Maneno Maneno.
"Sasa kama zipo nyimbo kwenye DVD hiyo tulizorekodi na GMC, ni wazi kwamba nayo huenda imehusika, lakini sina hakika. Lakini kwa vyovyote vile, wapo baadhi yetu ndani ya bendi wamehusika,"alisisitiza.
Akizungumza kwa njia ya simu jana, mmoja wa wamiliki wa GMC, ambayo pia hujulikana kwa majina ya Mwananchi, Mamuu Store na Wasanii Promoters, alikana kuhusika kwao na kazi hiyo.
"Ni kweli tuliwahi kuwa na mkataba na DDC Mlimani Park miaka ya nyuma, lakini ulishamalizika hivyo hatuhusiki kwa lolote na kazi hiyo,"alisema mtu huyo, ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini.
No comments:
Post a Comment